Reader Settings

SEHEMU YA 35. 

Ndani ya ofisi  hio alikuwepo  Sebestiani Wambe, Willium  Libeta  ambao wote walikuwa ni wakurugenzi wasaidizi , kulikuwepo Shabani Chacha Mkuu wa idara ya fedha , Robinson Chenga  wa idara ya Strategy, Nahida Mohamed  mkuu wa idara  ya Masoko na kuendelea. 

Kilichomfanya  Hamza kutabasamu ni mara baada ya kumuona mpenzi wake Eliza alievalia suti akiwa amekaa kwenye sofa pia . 

Eliza hakutaka kabisa kuonyesha kufahamina na Hamza wakiwa kazini  hivyo  aliishia kutoa tabasamu tu. 

“Huzijui sheria , huelewi kwamba ukiingia katika ofisi ya  Afisa mtendaji mkuu wa kampuni unapaswa kugonga mlango?”Aliongea Mzee Sebastiani akionyesha hajafurahi. 

Hamza alimpotezea na alitembea  mpaka kwenye  meza ya Regina  na kisha aliweka   yale matunda. 

“Huyu  ni msaidizi w angu , kama  kuna wa kumkaripia basi ni  kazi yangu hio”Aliongea Regina. 

“Mkurugenzi hiki ni kikao cha siri kinachohusisha viongozi wa juu wa kampuni , msaidizi kama huyu anapaswa kuondoka”Aliongea  Mzee Sebastiani.  

“Hata mimi sitaki kushiriki pia , hivyo naondoka”Aliongea Hamza , hata hivyo hakutaka kujichosha kuhudhuria kikao ambacho hakikuwa kikimuhusu. 

“Wewe Hamza kaa chini na usikilize kinachozungumziwa hapa kwa umakini”Aliongea  Regina. 

Kauli ile ilimshangaza Hamza  na hivyo hivyo kwa wengine walionekana kushangaa pia , isitoshe sio jambo la kawaida, ilionyesha ni dhahiri  Regina alikuwa akimwamini  Hamza , maana hata msaidizi  namba moja Linda hakuruhusiwa kuingia katika kikao hicho , sasa Hamza ambae ana siku chache ndani ya kampuni  alikuwa akizingatiwa hivyo. 

Upande wa Hamza  hata hakufurahi kukaa na kusikiliza , angefurahi pengine kungekuwa na posho lakini hamna , aliona ni  bora kwenda kuendelea kutafuta hela mtandaoni kutumia internet ya kampunni. 

Lakini kwasababu bosi ndio alisema , hivyo aliona  atii kauli yake na kusikiliza kinachozungumziwa. 

“Mkurugenzi , una mpango wowote wa kudili na hii dharula ya  kampuni ya Omega kupakuliwa  na Zena?”Aliuliza Chenga mkuu wa idara ya mikakati  na mbinu za ki uwekezaji kwa lugha ya kingereza. 

“Omega  has already officially signed a contract with the Zena Group today, this purchase is already comfirmed  and irrevocable”Aliongea Regina akimaanisha kwamba Omega tayari  rasmi imeweza kutia saini   ya kimkataba na kampuni ya Zena  na  ununuzi huo hauwezi kubatilishwa. 

Baada ya kauli hio Mzee Libeta na Willium  walijikuta wakiangaliana huku wakitoa tabasamu la furaha  la chini chini. 

“Kama ni hivyo kwanini umeitisha kikao hiki leo  hii?”Aliuliza Willium na Regina aliwaangalia hao wasaidizi wake kwa macho ya kichokozi kaba ya kujibu. 

“Nimeitisha kikao  hiki kuwatangazia kwamba kampuni yetu itakamilisha ununuzi wa kampuni nyingine haraka iwezekanavyo”  

“Nini!?, Ununuzi mwingine ,  unazungumzia kampuni gani , sidhani ukiitoa Omega kuna kampuni  nyingine  inayojihusisha na uhandisi wa programu endeshi na akili bandia inayoweza kukidhi vigezo vyetu  ndani ya   Dar es salaam au Tanzania nzima”Aliongea Mzee Wambe.  

“Makamu , unaweza kuwa sahihi , ndio maana nimefikia  makubaliano ya kuinunua  kampuni changa ya  Moro  technology  na baada ya  kikao cha wahisani pamoja na  cha bodi ya wakurugenzi 

kumalizika ununuzi       wetu        utakuwa umekamilika”Aliuongea Regina.  

Maneno  hayo  yalivyotamkwa , kila mmoja ndani ya ofisi ukiachana  na Eliza  walikuwa katika hali ya mshituko. 

“Unamaanisha Moro Technology, hii kampuni ilioanzishwa na chuo cha sayansi   Morogoro  na kuingia katika  orodha kumi ya kampuni changa  ndani ya bara la Afrika?, nakumbuka  chini ya  idara yangu tulifuatilia na mmiliki mkubwa wa hisa  ni raia wa Canada , Mkurugenzi ulianza mazungumzo ya ununuzi lini?”Aliuliza Chenga akiwa na mshangao. 

“Wiki moja iliopita , kazi ya  maongezi ya manunuzi ilisimamiwa na Eliza Mkuu wa idara ya mauzo  na Moro walikubali kutuuzia hisa asilimia sabini  hivyo tutachukua udhibiti na kuweka vipaumbele vyetu vya ki ufundi”  

“Kumbe ndio maana  Eliza  alisafiri kikazi , kumbe ilikuwa ni swala hili , ndio maana hata idara yetu haina uelewa juu  ya swala hili”Aliiogea.  

Hata Nahida  mkuu  wa idara ya masoko alikuwa katika mshangao pia  juu ya jambo hilo. 

“Ili kuepusha  makosa yasiotakiwa mimi na  Eliza tuliamua kulifanya jambo hili siri mpaka hatua za mwisho”Aliongea Regina.  

“Meneja Chenga  naomba uniwie radhi juu ya hili ,  sikuwataarifu kwasababu ni maagizo kutoka kwa mkurugenzi”Aliongea  Eliza.  

“Hapana Eliza  , huna haja ya kuomba msamaha , swala hili  lina mchango mkubwa kwa kampuni , yaani bila ya kufanya  makosa umeweza kukamilisha kazi kubwa hivi kwa kampuni , haha  kama ilivyotarajiwa  vijana  mnaupiga mwingi kiasi  cha kuwashinda wapinzani wenu”Aliongea  Chenga akiwa na furaha. 

“Nadhani  kwasababu  ni kampuni ambayo ilikuwa nje ya Dar ndio maana Mkurugenzi hakuiweka kama chaguo la kwanza , hivyo baada ya plan A kufeli akatumia plan B”  

Mzee Sebastian na mzee Willium mara baada ya kusikia hivyo walijikuta  paji za  nyuso zao zikitoa  jasho. 

“Ukweli ni kwamba sikuwa na mpango wowote wa kuinunua Omega , Plan A niliokuwa nayo ni kuinunua Moro Technology”Aliongea Regina.  

“Nini?”Kila mtu alishituka , Mzee Willum na Mzee Sebastiani walizidi kufubaa. 

“Kama ni hivyo Mkurugenzi kwanini ulitupatia kazi  

idara yetu kufanya mazungumzo na Omega?”Aliuliza  Chenga.  

“Kuna haja ya kuuliza  kila kitu kipo wazi,  Omega ilikuwa ni chambo kwa  kampuni ya Zena ili kuinunua huku  mpango mwingine ukipikwa?”Aliongea Hamza.  

Mara baada ya kuongea hivyo kila mtu  sasa ni kama alitoka usingizini , muonekano wao ulibadilika mara moja , wengine walikuwa wakishangaa wakati wengine walikuwa wakimwangalia Regina na hofu  katika macho yao. 

Hamza ambae alikuwa amesimama katika mlango aliinua macho yake na kumwangalia Regina na muonekano usioelezeka. 

“Huyu mwanamke   mbele yangu ni tofauti sana na  mwanamke wa jana aliekuwa akisindilia Doughnut”Aliwaza Hamza.  

“Zena wameinunua kampiuni ya Omega kwa kiasi cha  bilioni  nne  na sisi tumetumia milioni mia saba tu pekee kuinunua kampiuni ya  Moro  ili kutimiza malengo yetu , kingine  msingi wa kampuni ya Moro   ni mzuri sana  kuliko wa Omega  na ndani ya siku  zijazo Moro itapiga hatua kubwa mno”  

“Duuh , milioni mia saba tu ,  nadhani  huu unuuzi  una thamani kubwa  ya muda kuliko wa Omega , vipi hakukuwa na  mshindani?”  

“Mshindani mkubwa wa kampiuni yetu  ni Zena Group , sasa wamekamilisha malipo ya  bilioni nne kuinunua Omega , unadhani wanaweza kuleta ushindani  tena wa kujaribu kuinunua  na Moro , isitoshe kwa taarifa nilizonazo  wamefikia ukomo wa kuomba mkopo benki”Aliongea Regina.  

“Mkurugenzi mbinu yako ilikuwa ni kuwasukumiza Zena kwenye kona  kwa kuwaingiza kwenye mtego ili kujiondolea  vikwazo vya kulenga shabaha bila  tatizo”Aliongea Shabani kwa furaha kama zote.  

Upande wa Wakurugenzi wasaidizi  walikuwa wakitokwa na jasho sio kitoto , ilishakuwa wazi   hawakuwa wakiisaidia Zena bali walikuwa wakiiharibu. 

Ni sawa na kusema  wameomba kisu kwa ajili ya kumuua  Regina  lakini wakati huo huo Regina akawatumia wao na kisu chao kuua mtu mwingine. 

Regina mara baada ya kuona wazee hao walivyokuwa wakitokwa na jasho , tabasamu la kejeli lilimvaa , aliangalia muda kwenye saa ya ukutani na kisha alishika rimoti na kuwasha TV. 

“Taarifa ya  ununuzi kutoka Morogoro nadhani  ishaanza ,  mnaweza kuangalia kila mtu”Mara baada ya kuongea hivyo kila mtu aliekuwepo hapo ndani aligeuka  na kuangalia. 

Ilikuwa ni kweli mkurugenzi wa kampuni ya  Moro alikuwa akitaarifu waandishi wa habari juu ya maamuzi ya kampuni  yao kuuza hisa asilimia sabini kwenda   kwa mmiliki mwingine, huku habari ya kuaminika ni kwamba   kampuni ya

Dosam ndio imehusika na ununuzi wa hisa hizo.  “Haha CEO kazi nzuri , sisi wazee  hakika umejua kutuweka  gizani , huku ukitupiga chenga”Aliongea Mzee Chenga huku akiinua kidole gumba. 

“Natamani kuona  viongozi wa kampuni ya Zena watakavyojisikia baada ya kuona hii habari, nina uhakika Mzee Benjamini atatapika lita nne za damu haha..”Aliongea Nahida.  

Mzee Willima na Sebastian  waliona hali sio shwari , pumzi zao zilizidi kuwa nzito , walijua  kabisa  lawama zitaangushiwa kwao na kampuni ya Zena na moja kwa moja ingeonekana wao ndio wamecheza mchezo  mchafu. 

“Wewe mwanamke , tokea mwanzo ulikuwa ukitutumia kuvujisha taarifa  makusudi kabisa kwenda Zena  na kisha ukatugeuzia kibao”Aliongea Mzee Willium. 

“Una moyo wa kishetani sana..”Aliongea Mzee Sebastian na wota kwa pamoja walisimama. 

Wafanyakazi wengine wote walijikuta wakishangazwa na jambo hilo , ndio sasa wanaelewa  kwanini walikuwa wakipingana na Regina kuinunua kampuni  ya Omega katika kikao cha  bodi ya wakurugenzi kumbe wao ndio walikuwa wasaliti. 

Kwa  kitendo cha kuwaingiza Zena Chaka sio rahisi  kutoziepuka  lawama  na swala kama hilo haliwezi kupita kirahisi. 

“Boss   Wambe , Bosi Libeta, kwanini  mfanye hivi , inamaana ndio nyie mliovujisha nyaraka za kampuni?”Aliongea Mzee Chenga. 

“Nyamaza , unajua nini wewe , hii kampuni imeanzishwa  na kizazi chetu  cha watu wanaofanya kazi kwa bidii , taarifa kidogo  tu inataka kumtoa jasho huyu msichana”Aliongea Mzee Willium.  

Lakini Regina  alikuwa kauzu na hakuwa na  mabadiliko yoyote  ya kimuonekano  na aliishia kunyanyua bilauri  ya maji na kunywa kidogo. 

“Wakurugenzi wasaidizi , Mzee Sebastiani na Mzee Willium , nyie wote ni wazee  katika hii kampiuni  na niliwapa nafasi  kutokana na vyeo vyenu mkagoma , nikawawekea mtego mkaingia wenyewe  kwanini mnakasirika?”  

“Unaongea ujinga  ili hali unaujua ukweli , tokea ulivyochukua uongozi wa kampuni mpango wako ni kututoa sisi wazee na kuajiri vijana , huku ukiwa na uwezo wakufanya chochote utakavyo”  

“Hii ni kampuni  na sio sehemu ya kulelea wazee , kama huna uwezo wa kufanya kazi unaachia ngazi na kuwaachia nafasi wenye uwezo , acheni kuegamia  katika vigezo vyenu ambavyo vimepitwa na wakati”  

“Bullshit , wewe ni mwizi , usidhani hatujui unapanga pia kutupokonya hisa zetu , wewe ni mtoto wa mfanyakazi wa ndani  tu uliezaliwa nje ya ndoa”Aliongea kwa hasira.  

“ Unaruhusiwa kunifokea  na  kunitukana mimi mwenyewe ila sio mama yangu”Aliongea Regina.  

“Sina haja ya kuendelea kubaki ndani ya hii kampuni hata hivyo , nani asiejua ukweli , mama yako ni kahaba tu aliekuja  kujiuza kwa kujifanyisha  mfanyakazi wa ndani , wengine wanaweza wasijue ila sisi tunaojua historia yako tunaujua ukweli”  

Regina uvumilivu ulimshinda na palepale  aliinua glasi ya maji kutaka kumwagia Mzee Willium  lakini kaba ya kufanya hivyo  mtu   tayari ashajitokeza na  kumpiga mzee Willium ngumi ya  mdomo  na kusababisha meno mawili kuchomoka. 

“Hamza!!!?”  

Wote walimaka, ilikuwa sahihi kwa mzee huyo kupokea kibano lakini tatizo  pigo la Hamza lilikuwa la kuua mtu. 

Mzee Willium alijikuta akitoa kilio, nusu ya uso wake wote ulivimba  huku damu  nyingi ikimtoka , alikuwa katika maumivu makali kiasi kwamba machozi yalikuwa yakimtoka. “Wewe.. unathubutu vipi kunipiga?”  

“Mzee umeshindwa na msichana mdogo   tofauti ya kukubali kushindwa unamtukannia mama yake , watu kama nyinyi kwanini nisiwashushie kipigo”Aliongea Hamza na alimsimamisha Mzee huyo   na kisha alimlamba vibao viwili  kulia na kushoto na akapoteza fahamu palepale na kisha alimgeukia Mzee Sebastiani. 

Upande wa Mzee Sebastiani alikuwa   akitetemeka kwa woga  na aliishia kurudi nyuma kwa kujikokota. 

“Usije kunisogelea , napiga simu polisi”Aliongea.  

“Mkurugenzi muache apige simu polisi , kosa la kuvujisha nyaraka za kampuni, kuihujumu kampuni  na kuiba hela , yote haya ni makosa ya jinai , tunaweza kuwaacha polisi wawakamate tu”Aliongea Hamza   

Regina alijikuta akirudi katika hali ya kawaida baada ya mshituko  usio na kifani , hakutegemea  Hamza angechukua  maamuzi ya namna hio. 

“Kwanini umekuwa mkatili hivi , nimekuammbia mpige?”  

“Si ndio maana umenibakisha hapa ili  niwashughulikie , au unataka kusema umeniruhusu 

kubaki hapa kusikiliza mnachozungumzia?”Aliuongea Hamza.  

Regina alijikuta akinyamaza , ilikuwa ni kweli huo ndio mpango wake , alitegemea  kabisa Mzee Willium na Mzee Sebastiani wakiujua ukweli  lazima wapandwe na vichaa , hivyo alimfanya Hamza kubaki kuimarisha hali ya ki usalama, lakini tatizo Hamza amekuwa mkatili katika pigo lake mpaka kumng’oa mtu meno.  

“Hii sio namna  ya kitendo nilichotaka , ukimuumiza mtu hivi atakushitaki”  

“Hehe,Mkurugenzi unachotakiwa kufanya ni kunitafutia  Mwanasheria wa viwango  vya juu , linaweza kuwa kosa ila mwanasheria anaweza kuligeuza na kuwa  kitendo cha  kishujaa  cha kudumisha  haki , au Self defence”Aliongea Hamza. 

Regina   asingeweza kumfanya chochote , lakini mara baada ya kuona  namna ambavyo  alimkingia kifua  alijisikia vizuri. 

“Haina haja ya kuita polisi”Aliongea na kisha alisogea hadi kwenye meza yake na kuongea na  Linda kupitia simu. 

“Linda waambie mapokezi  wawaruhusu  polisi kupandisha wawachukue wahalifu”Baada ya kuongea hivyo aligeuka. 

“Nishakabidhi ushahidi , wanasheria wa kampuni na polisi watadili na hili”Aliongea Regina.  

Kila mtu aliekuwa hapo ndani alishangaa  kwa mara nyingine , kwahio  Regina alikuwa amepanga kila kitu , yaani tokea mwanzo  ilikuwa ni kama Mzee Willium na Sebastiani  wanasomewa hukumu.  

Hazikupita  hada dakika nyingi polisi waliweza kufika  na kumchukua Mzee Sebastiani na Mzee Willium na kuondoka nao , ilikuwa  sasa ni wazi hawatoweza kurudi tena kama wakurugenzi ndani ya kampuni. 

****** 

Muda huo huo katika eneo la Mbezi Beach , yalipo  makao makuu ya  kampuni ya Zena , ndani ya ofisi ya  mwenyekiti , Mzee Benjamini alijihisi ni kama vile ukichaa umemvaa. 

Alikuwa ameshikilia Golf club mkononi  na kwa hasira alianza kuponda ponda  vifaa vilivyokuwa vimewekwa ndani ya ofisi yake, ikiwemo tarakishi yenye thamni ya hela nyingi. 

“Baba , kuna  tukio kubwa limetokea”  

Mlango wa kuingilia ofisini ulifunguliwa  na alikuwa ni James aliekuwa akipiga kelele , ilionekana na yeye amekwisha kuziona habari za Dosam kuinunua Moro  Technology corp, James mara baada ya kuangalia mazingira ya ofisi ya baba yake alisita kupiga hatua kuingia zaidi. 

“Ushazipata habari tayari?”  

“Yule mwanamke  kahaba  Regina .. alikuwa akijua kila kitu kuhusu sisi , Wambe na Libeta  aliwapatia taarifa kuzileta kwetu ili  tuingie mkenge kwa kuinunua  Omega kwa pesa nyingi , ulikuwa ni mtego wake”Aliongea kwa hasira  huku akilegeza  tai. 

“Baba  kipi kifanyike sasa hivi , kwanini tusilifute dili letu na Omega”  

“Unaoingea upuuzi gani , mkataba tushasaini unadhani ni rahisi kuufuta , , tutashitakiwa , tutalipa fidia ya kuvunja mkataba  na  juu zaidi taswira yetu 

itaporomoka na kuzidi kumpa  ushindi Regina”Aliongea kwa hasira.  

“Basi tunaweza kuomba  mkopo benki kwa namna yoyote ile na kisha tunainunua  na hio Moro?”  

“Wewe mjinga nini ,  unadhani watu watafufikiriaje  tukinunua kampuni  mbili zinazofanana ,  unadhani ni rahisi kupata mkopo benki”Aliongea huku akitamani kumpiga James , alijiuliza kwanini  Regina ana akili nyingi kuliko mtoto wake ilihali wote wana umri mmoja. 

“Kwa staili hii baba si tutashindwa  kabisa kuipiku kampuni ya Dosam,Soko letu linazidi kuminywa na kampuni kubwa ndani ya  Tanzania , muda si mrefu  jina la kampuni yetu litapotea kabisa , hata  kama niweze kumuoa Regina  huko baadae kampuni yetu itamezwa”  

“Unaongea ujinga gani , nani umuoe wewe mpuuzi?, mwanamke wa aina ya Regina  ni kunguni ,  ni nyoka mwenye sumu kali , hawezi kuwa sehemu ya familia yetu kamwe, mtu ana

uwezo wa kudanganya uongozi mzima wa kampuni  bila kujali hisia zao ,  na hajali kabisa , niseme tu  alichoongea  rafiki yangu  Gabusha  ni sahihi ,  kwenye maisha yangu sijawahi kutana  na  mwanamke wa aina hii”  

“Sasa baba tutafanya nini , hatuwezi kurhusu  kampuni ya Dosam kuendelea  kuwa kubwa kama hivi , hisa zetu zinashuka  thamani  ni wazi kabisa   kampuni yetu haina future”Aliongea James na palepale Mzee Benjamini alionekana kuwaza. 

“Kwasababu  huyu mwanamke ameshindikana kwa njia  za kawaida  , kilichobaki ni  kumfanyia uharibifu”Aliongea na James aliishia kumeza mate na  kutingisha kichwa kukubaliana na baba yake. 

****** 

Upande mwingine  masaa kadhaa nyuma  Kanali Dastani  alikuwa akihaha, kitu pekee ambacho kilimpa ahueni ni kwamba familia yake ilikuwa salama  salimini. 

Dakika chache mbele mara baada ya kuhakikisha usalama wa familia yake  aliendesha gari kwa spidi kuelekea upande wa  wa  hospitali ya jeshi , kutoka alipokuwa akiishi na ilipo hospitali hio hapakuwa mbali hivyo   ni dakika ishiririni tu zilimtosha. 

Baada ya kufika  hakutaka hata kuuliza  tukio limetokeaje mpaka Amosi Jasusi mstaafu kutoweka , alienda moja kwa moja mpaka katika chumba cha mitambo ya kuongozea Kamera. 

Na Luteni Usu , Afande Zakayo alimpa ushirikiano wa kutosha wa kuangalia  Kamera hizo. 

Sifa kubwa ya Kanali Dastani jeshini  ni uwezo wake mkubwa wa akili , alikuwa akiaminiwa sana katika  kazi za ki uchunguzi  ambazo zilihitaji kutumia akili , udhaifu wake mkubwa ni kwamba hakuwa na uwezo mkubwa wa kimapambano , yaani alikuwa mwanajeshi  wa kutumia bastora  na bunduki pekee lakini ukimkuta hana siraha basi anakuwa kama Sele tu mnywa  pombe , mateke yako matatu au matano tayari yupo chini anaugulia maumivu. 

Hakujali kitambi chake kugusana na meza , alichotaka   kuona  katika tarakishi zilizokuwa mbele yake ni sura ya Amosi tu pamoja na watu waliohusika kumtoa Amosi  hospitalini , alizidi kukodoa macho na hatimae alichotaka   aliweza kukiona. 

“Afande kuza hio picha ya mwanamke  alievaa Hijab”Aliongea  Kanali  na Afande Zakayo  alifanya kama alivyoambiwa,  mwanamke ambae alikuwa akilengwa ndio  alieonekana akiingia katika wodi  aliolazwa Jasusi Amosi, lakini  Kanali hakuweza kuitambua , kwani mwanamke yule alionekana kuwa Shombeshombe kama sio  mwarabu.  “Zakayo unachoona hapa Amosi anaondoka kwa hiari yake au  analazimishwa?”Aliongea Kanali  , alikuwa ashaona kitu kilichomvutia macho lakini alitaka kuhakiki mawazo ya mwingine.  “Naona anaondoka kwa hiari yake mwenyewe”  

“Angalia vizuri…”Aliongea  lakini  muda huo simu yake ilianza kuita  na mara baada ya kuangalia jina linalopiga  jasho la mikono lilianza kumvaa  lakini hata hivyo alipokea. 

“Jambo Afande”  

“Dastani Rdui makao makuu haraka”Sauti ya kibabe  iliongea kwenye simu. 

“Lakini  Afande..”  

“Kama unafuatilia swala la Amosi achana nalo , Rudi kituoni nataka ripoti ya mauaji  Zinga” Sauti iliongea mara ya pili na palepale simu ilikatwa. 

Swali la kwanza lililomwingia akilini Kanali Dastani ni kujiuliza nini kinaendelea , inamaana makao makuu wanajua swala la kupotea kwa  Amosi au kuna kitu asichokuwa akikifahamu. 

“Afande  hebu angalia  Kamera za  nje”Aliongea na Zakayo  alienda moja wa moja mpaka kwenye picha  zilizorekodiwa upande wa Kamera za nje , Amosi aliongeza umakini. 

“Sh*t ni TISA hawa”Aliongea  na palepale  aliweza kuelewa nini kinaendelea ,Aling’;ata meno yake kwa hasira na kisha alitoka  na kuondoka. 

“Kwanini TISA wamekuja kumchukua Amosi , nini kinaendelea “Aliwaza  Amosi huku wasiwasi ukiwa katika macho yake , kwa muda mrefu  mpaka  kitengo cha  Tanzania  intelligency  Service Agency  kuingilia  jambo  basi jua swala hilo limemfikia mheshimiwa Raisi moja kwa moja. 

Ndani ya nusu saa tu   Kanali alikuwa ashakaribia makao makuu ya jeshi  kitengo cha MALIBU. 

MALIBU na TISA ni vitengo viwili tofauti kabisa  vyenye kubeba majukumu tofauti , hakukuwa na kirefu  cha aina yoyote cha kitengo MALIBU bali   ni jina la kiheshima  kutoka kwa aliewahi kuwa Mkuu wa Majeshi  Afande Athumani  Abdalah Malibu. 

Kama  moja ya watu waliotoa  pendekezo la  jeshi  kuunda kitengo kinachodili na nguvu zisizoonekana  ndio  maana  jina lake la mwisho likachukuliwa na kufanywa  ndio  jina la kitengo hicho jeshini. 

Miaka kadhaa  nyuma  katika historia ya moja ya nchi  ya  Afrika  kuliibuka tukio la ajabu ambalo  lilihusisha  wanaume kupoteza  viungo vyao  vya uzazi, lilikuwa tukio la kushangaza na  kugusa ambalo lilitikisa sana , jeshi la polisi kutoka nchi  hio walijitahidi  kuwinda muhusika wa tukio  hilo lakini  matukio ya namna hio  yalizidi kupamba moto na wanaume walizidi kupoteza viungo vyao , mwisho wa siku  jeshi la polisi walitoa ripoti  tukio hilo halikuwa la kawaida na  kulihusisha na nguvu za giza. 

Baada ya tukio hilo  miaka michache mbele  likaibuka tukio lingine  maarufu ambalo lilipatiwa  jina la Popobawa ambalo lilianzia katika kisiwa cha Pemba na kusambaa mpaka  jiji  la Dar es salaam,  tukio hilo na lenyewe lilikosa  majibu na kuhusishwa na nguvu za giza. 

Haikuwa tukio hilo tu , matukio mengi yaliweza kutokea  ndani   na nje ya Afrika ambayo yalihusishwa na nguvu za giza na  kutokana na matatizo hayo  serikali mbalimbali zilianzisha mpango wa kudhibiti hali kama hizo pale zinapotokea   na hapo  ndipo Afande Athumani Abdala Malibu alipopendekeza kuundwa kitengo cha  kudili na  nguvu  ambazo sio za kawaida , ikiwemo uchawi  na  nguvu za giza  na  ndipo ilipozaliwa  Malibu. 

Mwanzoni Malibu haikuwa na nguvu sana lakini mara baada ya waanajeshi kupelekwa katika vyuo mbalimbali duniani  ikiwemo China , Brazili na  kwingineko hatimae  kitengo cha MALIBU kikaanza  kushamiri, lakini baadae  sasa kitengo kilikosa kazi  kwani matukio ya nguvu za giza yalikuwa machache  hivyo kikapewa majukumu mengine ambayo  ni  kunasa  mtu yoyote au  kikundi  chochote cha watu wanaotumia nguvu za ziada, kitengo hiki kilienda mbali mpaka kufatilia  watumishi wa Mungu ambao  nguvu zao zilikuwa sio za kawaida kabisa na kuanza kuwachunguza na pale inapobainika kuna  ukakasi  uchunguzi hufanyika mara moja. 

Tukio la Zinga lilihusisha  kukundi cha  maninja kutoka  kisiwa cha Samar , lakini ukweli ni kwamba ukisikia Samar utajua tu ni kisiwa lakini  kuna  kitu  cha ziada kuhusu kundi hilo la maninja. 

Inasemekana asilimia kubwa ya  maninja wote  waliopo chini ya  Samar  wanatokea katika mji unaoitwa Biringan. 

Lakini ki uhaisia  hakuna mji huo ndani ya Samar  Ufilipino baki ni sehemu ambayo ipo katika hadithi tu , ni sawa na kusema  Gamboshi  sehemu ambayo ni ya kusemekana pekee au Antlatis. 

Hakuna ushahidi wa moja kwa moja kama kweli maninja hao wanatokea Biringan lakini ni uhalisia kwamba Maninja kutoka Samar ambao waliingia Tanzania  wanafahamika kama wawindaji(Bounty hunters) daraja B , uwezo wa hawa maninja sio wa  kawaida,  ki ufupi ni kwamba wana pua  za mbwa , wanao uwezo wa kukuwinda  kwa kuijua harufu yako tu jambo ambalo sio  la kawaida kwa binadamu. 

Sasa maninja kama wale wanakufa vifo  vya ajabu namna ile ni dhahiri kwamba  ni kesi ambayo inapaswa kuwa  chini ya kitengo cha MALIBU. 

Upande wa TISA  ni  kitengo cha usalama wa taifa ambacho  kipo chini ya ofisi ya Raisi,  kitengo hiki kinadili sana na ukusanyaji wa intellijensia ambazo  zina ushahidi wa ki uhalisia. 

Amosi alikuwa amepewa kazi na wabrazili kupitia  Chriss  na  katika kazi hio  anajikuta  anaingia katika  rada za watu  kutoka kisiwa cha Binamu, lakini TISA wanakuja kumtoa  Amosi kimyakimya

hospitalini , ilimaanisha  walitaka kumhoji   au  kuna kingine kinachoendelea. 

Hayo ndio yaikuwa mawazo ya Kanali Dastani wakati akiwa katika  gari  akielekea makao makuu. 

Zilimchukua dakika kadhaa tu  kuingia makao makuu na alielekea moja kwa moja katika ofisi ya mkuu  wa kitengo hicho  , Brigedia Doswe, lakini kabla ya kuingia katika ofisi ya mkuu wake alipitia katika ofisi yake kwanza , alihitaji  ripoti alioandaa  kwa ajili ya  kuitoa  juu ya uchunguzi wa  vifo vya  maninja kutoka  Samar. 

Mara baada ya kupata ripoti yake moja kwa moja  alielekea katika ofisi ya mkuu wake wa kazi kwa ajli ya kuripoti  na mara baada ya kugonga mlango  aliruhusiwa kuingia. 

Bigedia Doswe alikuwa peke yake  katika ofisi hio na kumfanya  Kanali kuvuta pumzi , aliamini hali sio  mbaya kama alivyodhania maana kama ingekuwa tofauti basi Kanali Msuya msaidizi wake asingekosekana ndani ya ofisi hio, baada ya kumsalimia, Afande Doswe alitoka katika meza yake na kwenda kuketi katika  masofa. 

“Dastani  kabla ya kuzungumzia swala lililitokea leo , twende moja kwa moja kwenye ripoti, niambie umekwisha kumpata muhusika?”  

“Afande  japo hakuna ushahidi wa kutosha  lakini  nadhani mhusika tunae”Aliongea  kanali na kumfanya  Afande Doswe kumwangalia kwa macho yenye  umakini na  kanali alimpatia haraka  mkuu wake  karatasi kadhaa alizoshika mkononi. 

Afande Doshwe alichukua karatasi zile na kuanza kuzisoma  kwa umakini  na  macho yake yalichanua kidogo  lakini  hakuna mshangao katika sura yake.  “Huyu Hamza  Mzee ndio muhusika, ukiachana na  hii  taarifa ya  kuonekana  katika gari ya Bosi wa Dosam  je kuna  kitu kingine kinachothibitisha hili?”Aliuliza.  

“Hii ni Vidio  iliopatikana juzi , anaeonekana katika vidio hio ni Hizza Joseph Mahimbo , nimefuatlia taarifa zake kupitia jeshi , amewahi  kuwa mwanajeshi  wa jeshi  la Tanzania kabla ya kuachishwa kwa  kosa la utomvu  wa nidhamu , mwaka  1998   alihamia nchini Thailland , hakuna taarifa  wakati alipokuwa Thailland alifanya nini ila  mwaka huu  amerudi  nchini Tanzania , na  kuna  habari   ambazo hazijathibitishwa  katika kipindi

chote alikuwa  chini ya kundi la kininja la Black 

Hawk .inaaminika ni moja ya wataalamu wakubwa wa matumizi  ya mbinu ya kimapigano ya  Vidole vya Tai na anafahamika kwa jina maarufu la Mzee  wa Konki”Aliongea  Dastani  na kumfanya  Afande Doswe kuvutiwa na  taarifa hio  na aliangalia Vidio  hio kwa umakini mkubwa na  sasa hali ya mshangao ilimvaa. 

“Kama amefanikiwa kumdhibiti Yonesi basi sio wa kawaida , lakini swala la kudhibitiwa na huyu kijana…”Aliongea huku akionyesha mshangao.  

“Nadhani sasa naelewa unachotaka kumaanisha  Dastani , unaamini  huyu Hamza  ndio aliehusika na mauaji  ya hawa wawindaji wa Samar?”  

“Kwa maelezo ya bosi wa kampuni ya  Dosam amekiri  kutekwa  na hii inadhihirisha watekaji walitumia gari yake kumpeleka mpaka  kijiji  cha wavuvi , anakiri pia  Hamza  ambae ni mpenzi wake  ndio alimuokoa”  

“Huyu Hamza mwenyewe anasemaje?”  

“Amekiri kweli kumuokoa Regina , lakini  anasema hakuhusika na mauaji  na  pili aliwapiga  hawa maninja na baada ya hapo ndio akamuokoa mpenzi wake , tunaamini  amehusika  moja kwa moja na mauji yao lakini  hakuna ushahidi, Hizi ni taarifa fupi zinazomuhusu Hamza Mzee”Aliongea na kisha alimkabidhi kishikwambi. 

Afande Doswe alisoma  kwa umakini  na alionyesha ishara ya kukunja ndita kana kwamba  hakuwa akiamini taarifa hio. 

“Hii ripoti haina shida, uthibitisho wa cheti  cha kuzaliwa  upo ,?” lakini   kwanini adai  uraia  wake mara baada ya kuishi nje muda mrefu?, nadhani kuna taarifa  ambayo haijaorodheshwa , hususani alipokuwa nje ya nchi alifanya nini kwa miaka kumi yote”  

“Ndio Afande kwa tathimini ya  tukio la  Regina kutekwa inaonesha kabisa  waliekuwa wakimlenga  ni huyu Hamza , kama hisia zangu zitakuwa sahihi kuna  kitu  wanakitaka kutoka kwa Hamza na njia nyepesi ilikuwa ni kumtumia  Regina kama Mateka”Aliongea na Afande Doswe alitingisha kichwa  kukubaliana nae. 

“Afande naomba unipe muda zaidi ,  nitafuatilia hili  mpaka  nilijue undani wake , nimejawa na shauku ya kutaka kumjua huyu Hamza ni nani”Aliongea Kanali Dastani.  

“Haina haja  ya kuendelea na hii kesi ,  kwa namna ilivyo  haikidhi vigezo  vya kuendelea kubakia chini 

ya kitengo cha MALIBU  hapa makao makuu ya jeshi”  

“Afande lakini hawa  Maninja sio  wa kawaida, tuna kila sababu ya kutaka kujua  wapo hapa Tanzania kwa ajili ya  nini , watu kama hawa kufika Tanzania  basi wanaemtafuta anaweza asiwe wa kawaida kama wao”.  

“Wawe  wakawaida  wasiwe wa kawaida ,  uchunguzi uendelee ama usiendelee  Dastani  huwezi kuhusika na hii kesi itachukuliwa na watu wengine”  

“Mheshimiwa unataka …”Kabla  hata hajamaliza kuongea mlango wa  mkuu wake ulifunguliwa  na wanajeshi  waliovalia Gwanda za kijeshi waliingia. 

“Dastani mpaka  sasa upo chini  ya ulinzi  kwa kosa la kusaliti  jeshi na Jamhuri..”Aliongea Afande Doswe  na palepale  Kanali Dastani alijikuta akitokwa na macho huku akimwangalia  mkuu wake kwa macho  yasiokuwa ya kawaida. 

“Afande sio kweli ,  naipenda nchi  yangu , sijawahi kusaliti jeshi…”.  

“Kama hujasaliti jeshi  na  Jamhuri  itajulikana Dastani  kwasasa utafuata utaratibu wa  ki uchunguzi”Aliongea na palepale aliwapa ishara  wale wanajeshi  na  kwa  haraka sana  Kanali Dastani alidhibitiwa  na kutolewa. 

Wakati  mlango wa kuingia kwenye lift unafunguka ili  Kanali Dastani kuingizwa   lift hio ilionekana kuwa na mtu , Kanali mara baada ya kunyanyua macho yake alijikuta akipigwa  na  mshangao. 

“Amosi!!!”  

Alijikuta akimwemwesa midomo yake kwa mshangao, Amosi aliekuwa mbeleyake ni kama vile hakuwa  ametoka hospitalini , alikuwa amevalia suti huku akipambwa na tabasamu. 

Ndio alikuwa ni  Amosi  mwenyewe aliesalimika kuwawa  kutoka katika mikono ya  watu wa Binamu wakiongozwa na mwanamke Tresha Noah. 

Amosi  aliishia kumuonyeshea  Kanali Dastani ishara ya bastora kwa vidole na kisha akatoka kwenye lift  akiwa na tabasamu. 

Kwa namna flani  Kanali Dastani  hisia zake zlimwambia  Amosi alikuwa akihusika na kesi  yake. 

Amosi alienda moja kwa moja kuingia katika ofisi   ya Afande Doswe  na  mara baada ya kuingia alipiga  saluti ya kubana msuli  na kisha alipewa ishara ya kukaa huku Afande Doswe akiwa na tabasamu. 

“Amosi una muda mchache sana wa kututhibitishia   kama Night Shadows wapo kweli  au lah, kwanzia sasa ripoti ya misheni utaripoti  kwangu moja kwa moja na sio kwa Kanali Dastani”  

“Sawa Afande”  

“Kabla ya  hilo tunataka kujua  kwanini  kanisa la Wabrazili  linafuatilia  kesi ambayo ilifungwa zaidi ya miaka ishirini iliopita  na kwanini Binamu wanazuia   uchunguzi huu  mpaka Kanali Dastani  akakuuza , kwanzia  sasa utaanza mahojiano yako na Kanali,  Amosi  tunataka kujua kila kitu ambacho Dastani anatuficha  na muunganiko wake  na Wiccan”  

“Afande lakini vipi kuhusu agizo la mimi kuuwawa kutoka Binamu?” 

“Hilo linashughulikiwa chini ya  kitengo cha  TISA

, kwasasa  tunahitaji  akili  yako  kujikita kwenye  misheni yako, kingine jina lako halijabadilika , nadhani unaelewa nninachomaanisha?” “Ndio Afande”.  

Dakika kadhaa mara baada ya  Amosi  kutoka  katika makao makuu kwa siri  sana  aliweza kumpigia simu  Chriss. 

“Jasusi  kwanini wiki nzima sikupati hewani?”Ndio swali la kwanza ambalo  Amosi alisikia kutoka kwa Chriss , lakini  ni kama alitegemea. 

“Nitakuelezea  baada ya kuonana ana kwa ana , tuonane saa mbili kamili usiku Las Vegas”Aliongea  na mara baada ya kauli ile  Amosi alikata simu na kisha alitoa tabasamu. 

Previoua Next