SEHEMU YA 37.
Upande wa pili ilikuwa ni kama vile Lau hakutaka kusikika alikuwa akiongea na simu , licha ya kuwa na wasiwasi lakini sauti yake ilikuwa ya chini sana.
“Lau niambie ni nini kinachoendelea vizuri nikuelewe”Aliongea Hamza.
“Bro hii simu nimekupigia kwa siri mno , naomba usimwambie Madam mimi ndio nimekupigia”
“Ongea bwana kama una cha kuongea , nini kimempata Dina?”Aliuliza Hamza kwa usiriasi kidogo.
“Kamisheni tatu za mtandao wa Chatu kutoka Uganda , Kenya, Rwanda na Tanzania wanaenda kinyume na Madam , nadhani kuna mtu yupo nyuma yao , Madam ameamua kudhibiti hili yeye mwenyewe , ni aidha augawanye mtandao wote wa Chatu au kuzima wale wanaoenda kinyume, lakini kwa chaguo lolote lile naona kabisa ni hatari kwake, hao watu wamekuja leo na walichosema wanataka kuonana na Madam kwa ajli ya mazugumzo pekee”.
‘Kama ni hatari kwanini Dina kaenda?”Aliuliza Hamza.
“Nilijaribu kumbembeleza asiende , lakini hakutaka kunisikiliza,ameondoka akidhamiria kutumia
vitisho ili kutuliza hali”
“Alichofanya ni sahihi, kama ni kiongozi alipaswa aende , ukiwa muoga watu watakudharau”Aliongea Hamza.
“Ndio bro , lakini wasiwasi wangu watu hawa wanaonekana kuwa na njama”
“Hili limetokea kwasababu ya kilichomtokea Zefa na kufanya watu wasiridhike?”Aliuliza Hamza.
“Nadhani ni kuhusu hilo pia, lakini ukiachana na hilo tokea muda mrefu wazee hawakuridhika kuongozwa na mwanamke”
“Huna haja ya kuzunguka katika hili , mimi ndio nimeuwasha moto hivyo ni sawa kuuzima mwenyewe”Aliongea Hamza , alijua swala la kumsaidia Eliza kwa kumpatia Zefa adhabu lilikuwa swala kubwa na lazima kungetokea migongano katika mtandao wote wa Chatu.
Hamza aliomba Lau amwambie eneo husika kikao kinapofanyikia na alitumiwa.
“Kuna sehemu naenda mara moja , mnaweza kuendelea kula tu msinisubiri”Aliongea Hamza mara baada ya kurudi ndani na kabla hata hajaulizwa swali alikuwa ashakimbilia nje tayari.
“Hamza , kula kwanza ndio uende..”Shangazi aliongea kwa nguvu lakini Hamza alikuwa ashaingia kwenye gari tayari.
“Shangazi achana nae ngoja afe na njaa”Aliongea Regina kwa hasira , ijapokuwa ameongea hivyo lakini katika macho yake alikuwa na wasiwasi.
Upande mwingine Hamza alikuwa akiiendesha Lexus ya Regina kama hana akili nzuri.
Muda mrefu tu hakutaka kujiingiza kabisa katika biashara za Dina , lakini kwa muda huo aliona hakuwa na jinsi zaidi ya kuingilia kwani Dina yupo hatarini.,
Mwisho wa siku Dina na yeye ni kama alikuwa na sehemu yake katika moyo wake hivyo alikosa utulivu , wasiwasi ulimjaa.
Hamza aliishia kushika tumbo lake huku akiendesha gari kwa mkono mmoja na aliishia kutabasamu akikumbuka alikuwa na njaa.
“Sijui kutakuwa na msosi?”Alijiuliza.
*******
Ilikuwa ni zaidi ya miezi mitatu tokea kiwanda cha magodoro kufungwa na yote hio ni mara baada ya mmiliki huyo kufirisika , hakujali tena kiwanda hicho tokea itangazwe amefirisika.
Usiku huu hata hivyo magari zaidi ya kumi na mbili yalikuwa yameegeshwa nje ya kiwanda hicho , mengi yakiwa ni Noah na yale ya ki ofisi.
Katika kiwanda hicho kulikuwa na harufu nzito kweli ya oil, ki ufupi hali ya hewa ilikuwa nzito.
Kulikuwa na makundi mawili ya watu waliosimama upande upande , huku makundi yote yakiwa na watu wasiopungua mia moja . upande wa kulia alikuwa ni Dina , upande wa kushoto alikuwa ni kundi la watu wengine.
Kwa jinsi hali ilivyo haikuhitaji elimu ya darasa la saba kujua kinachoendelea, kulionekana kulikuwa na uhasama kati ya kundi la kwanza na na la pili.
Baadhi ya watu katika kila kundi walikuwa na Zana za kushambulia ikiwemo mapanga , visu aina ya Jambia na virungu.
Sura zote zilionekana katika hali ya utayari wa kufanyiana fujo muda wowote na ilionekana ni maagizo tu yaliokuwa yakisubiriwa kutoka pande zote.
Kundi la upande wa kulia lilikuwa likionzowa na Dina mwenyewe na alikuwa na vijana wake waliomzunguka ikiwemo Lau na kundi la pili liliongozwa na mama mmoja , kama ni mfuatiliaji wa wafanyabiashara maarufu kutoka Kenya basi ni dhahiri ungemfahamu, mtu mwingine alikuwa ni mwanaume hakuwa maarufu sana katika jamii lakini kwa wale wanaomfahamu ni balozi kutoka Rwanda, kulikuwa na Mzee Mwingine aliekuwa na Mvi , alionekana kuwa mkubwa kuliko wote waliokuwepo hapo huyu alifahamika kama Mzee Dembe alikuwa ni raia wa Uganda.
Mrembo Dina ambae alikuwa amevalia kitop cha mikono mifupi na jeans nyeusi aliwaangalia watu wale waliomzidi umri yaani kwa macho yaliojaa hisia mchanganyiko.
“Mzee Dembe , Mzee Khu na Madam Debo nyie wote ni wa kuheshimika katika umoja wetu , Madam Debo umekuwa ndani ya umoja kwa miaka ishirini hadi sasa hivi kama sikosei ,lakini kwanini mkaamua kuongoza kundi la wasaliti , au ni kwasababu ya mimi kupewa uraisi ndio maana hamjaridhika, ni lini nimewafanyia ubaya?”
“Dina hatuwezi kusaliti Umoja wetu ndio umetufikisha tulipo leo hii , lakini kwanini wewe ambae umekuja juzi tu na kulelewa na kiongozi wetu aliepita upewe uongozi , mapenzi yetu kwa huu umoja ni zaidi ya wewe , huu umoja ni wa kwetu na sio wa kifamilia”
“Mlikuwa wapi kipindi cha machafuko, wakati vijana wa umoja wetu wakiua watu Kibiti na kulipwa na watu wenye uroho wa madaraka mlikuwa wapi , wakati vijana wetu walivyoibuka na kujiita Panyaroad na kuvamia watu hovyo, ni Babu ambae alituliza hii hali kwa kujitoa muhanga, ni babu pekee ambae aliona hakuna mwenye uwezo wa kuongoza umoja wetu zaidi yangu”Aliongea Dina.
“Sikuwa hata na tamaa ya kuwa kiongozi wa Umoja lakini kutokana na babu kunibembeleza niliishia kukubali na tokea niingie kwenye uongozi sikuwahi kujinufaisha mimi mwenyewe, zaidi ya kujitoa kuulinda umoja wetu ili usigawanyike”
“Haina haja ya kuongea sasa hivi , tunajuaje kama kweli maneno yako ni ya kwei?”Aliongea Mzee Khu.
“Mmekuja Tanzania kufanya nini , kwanini sio kwenye kamisheni zenu au mpango wenu ni kuigawanya Chatu?”
“Hatuna nia hio Dina , tunachotaka kufanya ni kuhakikisha mtandao wa Chatu unarudi kama mwanzo na ili hili kutimia ni lazima uondoke kwenye uongozi”
“Madam Debo hebu fikiria kwanza mafanikio ya raisi wetu tokea alivyoanza kuongoza umoja, ni majuzi tu watu wasiokuwa na nia nzuri na umoja wetu waliwalipa vijana kujifanyisha ni Panyaroad kwa kuwasambaza Tanzania nzima na kuibua taharuki ili kupata sababu ya kuizima Chatu , lakini Madam Dina kwa ujasiri wa hali ya juu aliweza kusimama imara na leo hii Umoja umerudi katika ubora wake , ni maslahi kiasi gani ambayo unapata kupitia mtandao wa chatu katika biashara zako, kwanini haya yote huyaoni na unakubali kutumika?”Aiongea Lau.
“Lawrence wewe ni mtumwa wa Dina , una hadhi gani ya kuongea na sisi”Aliongea Debora na Lawrence alitaka kuongea tena lakini alizuiwa na Dina.
“Nataka kujua nini kimewafanya kuwa hivi , kwanini mnaona sifai au ni kwasababu ya kumuadhibu Zefa ambae alikuwa akienda kinyume na kanuni za umoja?”
“Huo ni mfano tu wa matumizi mabaya ya madaraka yako , kwanini umemkatili vile mtoto wa Chika ambae hana uhusiano wa moja kwa moja na umoja wetu?”
“Mzee Chika alimpa bichwa mtoto wake kutumia nguvu yetu kuleta madhara kwa watu wasiokuwa na hatia , jambo ambalo ni kinyume na umoja wetu , Chatu ndio imemfikisha Mzee Chika kushika cheo alichokuwa nacho polisi , lakini tofauti na kutoa mchango wa umoja ana haribu taswira yake”
“Huna lolote Dina yule kakijana shombeshombe unaemlelea ndio sababu ya kumuua mtoto wa Afande Chika”
“Huyo mwanaume sio kakijana , unapaswa kumuonyeshea heshima la sivyo usinilaumu kwa kitakachokutokea”
“Hahaha.. hatimae umeionyesha rangi yako halisi , kwa mtu kama wewe kutojali kwanza familia yetu ya Chatu na kujali watu wa nje , tusipokuondoa katika uongozi itafikia mahali hatutoishi kwa amani kwa kuhofia ndugu zetu”Aliongea Mzee Milanzi.
“Kama nia yenu ni kunitoa katika uongozi , basi jaribuni kufanya hivyo”Aliongea Dina na palepale alipelekea mkono kiunoni , kundi lile mara baada ya kuona kitendo kile walichukua tahadhari maana walikuwa wakijua uwezo wa Dina kwenye kutumia visu.
“Dina usiwe na haraka , bado kuna mtu muhimu hajafika “Aliongea Debora huku akiwa na tabasamu lililojaa ukejeli ndani yake.
Muda huo huo baada ya kumaliza sentensi mlango wa kuingilia ulifunguliwa na kuwafanya wote wageuze macho lakini walishangaa kuona mtu ambae walikuwa wakimtarajia sie..
“Hamza?”
“Bro!!”
Dina alimwangalia Hamza kwa macho ya mshituko wakati huo Lau akimwangalia Hamza kwa furaha , wengine wote ni kama vile walikuwa wakimjua Hamza hivyo kuwa na nyuso zilizojaa furaha.
Hamza alishika nywele zake za kizungu kana kwamba anakuna kichwa huu akizungusha macho kuangalia hali halisi ilivyo.
“Imekuwa bahati nzuri sikupata shida ya msongamano wa magari na nimewahi kufika , Dina vipi uko sawa?”Aliuliza Hamza lakini Dina alionekana bado alikuwa na hasira na Hamza hivyo hakuendelea kumwangalia na aligeuza macho yake na kumwangalia Lau.
“Lau nilikwambia usimpigie , kwanini huelewi?”
“Madam , unaweza kuniadhibu utakavyo tukisharudi , lakini mimi na Bro hofu yetu ni usalama wako tu”Aliongea Lau.
“Wewe si umesema hutaki kujiingiza katika maswala yangu , ondoka tu nitadili na hili mwenyewe”Aliongea Dina akimwangalia Hamza.
“Dina nimezoea kuja kwako kunywa chai na chakula unachoniandalia , bila wewe unadhani nitakunywa wapi chai, siwezi kupotezea kama upo hatarini”
“Kwaho unataka kuja kwangu na kunywa na kula bure tu maisha yako yote?”
“Ndio maana yake , kama hotonifukuza nitaendelea kukutegemea maisha yagu yote”Alliongea Hamza akiwa na tabasamu na kumfanya Dina kutabasamu.
“Alichoongea Debora ni sahihi kabisa , hawa wanaonekana kuwa wapenzi, yaani wapo hatarini lakini bado wanaongeleshana bila ya wasiwasi”
Sauti ilisikika ikitokea nje huku ikifuatiwa na hatua za vishindo za viatu na hazikuwa chache zilikuwa ni nyingi.
Mwanaume mwemmbaba na mwenye macho
yaliosinyaa aliingia , alikuwa amevaa shati la rangi ya maua maua na koti la suti pamoja an jeans , nyuma yake kulikuwa na mabaunsa zaidi ya kumi na mbili na kila mmoja alikuwa ameshikilia bastora.
Mara baada ya kuona kundi hilo la watu wakiwa na siraha , watu wa Dina walijikuta wakipauka kwa hofu.
Inaeleweka wazi kabisa nchi ya Tanzania uhalifu upo chini sana tofautii na nchi kubwa kama Italia , Japani na China na likija swala la umiliki wa siraha kuna sheria ngumu mno hivyo kufanya watu wachache mno kuwa nazo.
Hivyo ni ngumu kuona kundi la watu wakiwa wamebeba siraha za moto kama hvyo , tena watu ambao sio watu wa usalama.
“Chika hatimae umeweza kufika ndani ya muda , tulichokuwa tukisubiri ni ujio wako tu wewe na Nasri”
“Haha.. Debora umekuwa na jeuri sana , tokea uuokote utajiri hujawahi kuniita kaka tena, saivi kwenye macho yako unaniona mimi ni mdogo wako”Aliongea Afande Chika, alikuwa ndio baba yake Zefa.
Mwanamama Debora na Afande Chika walikuwa ni ndugu wa damu. Miaka kadhaa nyuma mara baada ya Debora kuolewa na mfanyabiashara wa kutengeneza Bia kutoka Kenya aliukana Uraia na rasmi akawa Raia wa Kenya, baada ya kifo cha mume wake ndio alirithi kila kitu chake na hatimae kuwa moja ya wanawake matajiri ndani ya jiji la Nairobi.
Wakati wa kifo cha Tajiri Barasa kinatokea , ulitokea uvumi kwamba tajiri huyo ameuliwa na Debora kwa kushirikiana na Samweli Mbilu raisi wa Tanzania anaemaliza muda wake,lakini uvumi huo haukuwa na ushahidi na ndani ya miezi kadhaa ya kuzikwa kwa Barasa ulizima wenyewe.
Nguvu ya Debora ndani ya mtandao wa Chatu ilimuwezesha kumfanya Afande Chika kuwa DCP(Deputy Commisioner of police).
Upande wa Dina mara baada ya kuangalia watu waliongozana na Mzee Chika sura yake ilijikunja mno.
“Binamu huna haja ya kuniangalia kwa macho ya chuki hivyo , nimerudi nyumbani”Aliongea bwana mmoja wa makamo mwenye umri makadirio ya miaka kama therathini na sita hivi kauli yake ikimlenga Dina.
“Nasri nimekupeleka Australia na kila mwezi nakutumia hela ya matumizi ya kukutosha kufanya kila aina ya starehe , lakini bado umepata ujasiri na kuungana na maadui zangu na kujionyesha hapa?”Aliongea Dina kwa hasira.
“Kwahio utanifanya nini kama nimerudi , unadhani naweza kuridhika kwa vichenchi ambavyo ulikuwa ukinitumia , huna undugu wowote na babu lakini akakupatia urithi na uongozi usiostahili , nimerudi rasmi kupata haki yangu ya urithi”Aliongea Nasri.
Hamza hakuelewa chochote kinachoendelea na alimwangalia Dina kwa kuhitaji maelezo. “Unakumbuka nishawahi kukuambia Chatu ilikuwa ikifahamika kama Panyaroad na kwanini tuliamua kubadilisha jina?”Aliuliza Dina na Hamza alikumbuka.
Kwa maelezo ya Dina ni kwamba Panyaroad ulikuwa ni mtandao wa kimaslahi ulioanzishwa chini Tanzania , mtandao huu ulianzishwa kwa lengo la kufanya biashara haramu ikiwemo madawa ya kulevya , kuuza pembe za ndovu na biashara nyingine ambazo sio halali.
Njia ambazo zilikuwa zikitumika katika kufanya biashara hii ziliitwa njia za Panya, zilikuwa ni njia za siri mno ambazo serikali ilishindwa kudhibiti njia hizi katika kuingiza na kusafirisha bidhaa haramu.
Kutokana na biashara zisizohalali kupamba moto hatimae wafanyabiasha wengi waliongezeka na
walihitaji kutumia njia ya usafirishaji ya Panyaroad kuingiza na kusafirisha biashara zao na hapa sasa Mzee Mninga tajiri mkubwa ndani ya Tanzania na mwanzilishi wa Panyaroad alivyoona kutumia njia za Panyaroad kama fursa ya kujitengenezea pesa zaidi , alichokifanya ilikuwa ni kutumia mdandao wake wa ki usafirishaji na kuingiza na kutoa bidhaa nyingi za kimagendo na zile ambazo si halali ikiwemo madawa ya kulevya, vitu hivyo ambavyo alisafirisha vilikuwa vya wafanyabiashara wengine yeye alikuwa akikusanya ada ya usafirishaji pekee na fursa hio ilimpatia hela nyingi mno kwa Tanzania , lakini hata hivyo hakutosheka , wahenga wanasema pesa mwanaharamu , hivyo alitengeneza mtandao mwingine wa usafirishaji katika mataifa mengi ambayo yanapakana na Tanzania.
Ki ufupi ni kwamba matajiri wengi ndani ya nchi za jumuia ya Afrika Mashariki na kati walinufaika na kutajirika sana kupitia mtandao wa usafirishaji huu uliopewa jina la Panyaroad.
Kwa lugha nyepesi Panyaroad ilikuwa ni kama kampuni ya kusafirisha bidhaa haramu hilo ndio lilikuwa chimbuko lake.
Wahenga wanasema penye riziki hapakosi fitina ndio kilichotokea miaka kadhaa nyuma kipindi cha uongozi wa serikali iliojaa neema, kulitokea tukio la vijana wahalifu waliojiita Panyaroad na kuanza kushambulia watu mitaani na kuwapora mali.
Ukweli wa tukio hili ulitokea mara baada ya Tajiri Mninga kukataa kutoa sehemu ya umiliki wa mtandao wa Panyaroad kwenda kwa kiongozi mkubwa wa kisiasa ambae alikuwa akitumia njia ya Panyaroad kwa muda mrefu kufanyabiashara hizo haramu na kutokana na hilo kiongozi huyo akaanza kutumia nguvu yake ya kimadaraka kutoka kumiliki mtandao wote wa Panyaroad kwa nguvu, kete ambayo aliamua kucheza ilikuwa ni kutengeneza Panyaroad watu ambao ndio hao wahalifu walioanza kukata watu na mapanga na kupora.
Tajiri Mninga alikuwa ni moja ya watu ambao wana akili sana ukiachana na uwezo wake wa kifedha , asingekuwa na akili asingeweza kumiliki mtandao wa usafirishaji katika mataifa yote yaliopo ndani ya ukanda wa Afrika mashariki nzima, hivyo ili kumshinda mwenye nchi akaingia dili na moja ya kiongozi mkubwa kutoka nchi jirani na mpango wa kuzuia mtandao wa Panyaroad usimilikiwe kimabavu ukasukwa, wakati huo huo Mninga akamwahidi kiongozi wa nchi ya jirani kusafirisha zana zote kwenda kwa Wazalendo waliokuwa wakipambania maslahi ya asili katika nchi ya jirani.
Kiongozi wa nchi ya Jirani ni mwenye uwezo mkubwa wa akili na uwezo wake umeonekana kwa namna ambavyo aliitoa nchi yake katika umasikini wa harufu ya damu mpaka kuwa moja ya nchi yenye uchumi unaokuwa kwa kasi, tena nchi ikiwa ina rasilimali kidogo mno za asili.
Tajiri Mninga ili kuepuka makucha ya mwenye madaraka akahamisha makazi yake kwa muda na kwenda kuishi nchini Denmark huku akilindwa na ulinzi mkali sana katika makazi yake , aliamua kujihamisha kutoka Tanzania kusubiria mpango wa rafiki yake kutoka nchi ya jirani kukamilika na kweli kila kitu kilienda sawa , akiwa nchini Denmark alizipokea taarifa za kukamatwa kwa mtoto wa adui yake katika nchi ya Kimagnesiamu akiwa na furushi la madawa ya kulevya na kupelekwa jela.
Siku chache mbele Mninga alikabidhiwa ushahidi uliokuwa ukionyesha adui yake kuuza rasilimali za nchi kwenda nchi ya Kimagnesiamu kwa ajili ya kumuokoa mtoto wake kuachiwa huru, rafiki yake kutoka nchi ya jirani alimwambia autumie ushahidi huo kurudisha mtandao wake wa Panyaroad katika mstari na kuendeleza dili lao la kusafirisha Zana kwenda nchi ya Madini..
Mheshimiwa mara baada ya kukaa kikao na Mninga hakutaka mambo yaende mbali alikubali masharti yote ya Mninga ili siri yake kuendelea kubakia siri.
Mninga mara baada ya kurudisha nguvu yake ndani ya mtandao hakutaka kuzembea tena , aliamua kuweka mipango ambayo itaifanya mandao wake wa Panyaroad kujilinda wenyewe na katika mpango huo ndipo alipoamua kuitoa Panyaroad kutoka kuwa kampuni ya usafirisjai wa bidhaa haramu na kuitengeneza kuwa Umoja wa siri wa kimaslahi kwa kila mwanachama na alifanikiwa hilo kwa kuhusisha watu wengi serikalini katika mataifa yote ambayo mtandao wake ulikuwa ukifanya kazi.
Awamu ya uongozi wa neema nchini Tanzania ulipita na ikaingia awamu nyingine na hii ilimpa changamoto kweli Mninga kuendelea kuimarisha umoja wake ndani ya Tanzania kiasi ambacho ilimfanya kuamua kupeana mkono na aliekuwa adui yake..
Tajiri Mninga katika kipindi hicho alikuwa haamini
mtu kabisa , alikuwa na marafiki lakini hakuwaamini kwa asilimia mia moja , wakati anarudi Tanzania kutokea Ulaya alirudi akiwa na msichana mdogo ambae alimtambulisha kama mjukuu wake , Msichana ambae alifahamika kwa jina la Dina.
Ukweli ni kwamba licha ya Dina kuwa kufahamika kama mjukuu wa tajiri Mninga lakini pia alikuwa ni mlinzi wake wa siri na kupitia Dina majaribio mengi ambayo yalikusudiwa kumuua Tajjiri Mninga yalifeli kwani msichana huyo ukiachana na urembo wake alikuwa ni hatari mno likija swala zima la mapigano na kufanya watu kuwa na maswali ni wapi Mzee Mninga alikomtoa msichana huyo , lakini hata familia yake hakuiweka wazi juu ya wapi alikomtoa Dina zaidi ya kusema kwamba Dina ni mjukuu wake hivyo ni mwanafamilia ambae anapaswa kupata haki zote.
Jambo hilo lilimfanya Nasri mjukuu wa tajiri Mninga kumchukia mno Dina lakini licha ya chuki zake hakuweza kumfanya chochote.
Licha ya tajiri Mninga kupeana mkono na adui wake wa Zamani lakini adui yake alikuwa akimchukia kwa moyo wa dhati kabisa na alijaribu kufanya mpango mwingine wa kujimilikisha mtandao wa Panyaroad kwa kutaka kumtumia mtangulizi wake , na ili kufanikisha hilo akatumia mbinu nyingine katika moja ya wilaya ndani ya pwani , mbinu ambayo ilimwaga damu lakini kwa bahati mbaya mpango ukafeli lakini licha ya kufeli kwa mpango huo ilikuja kugundulika Nasri mjukuu wa Mzee Mninga alihusika katika hilo na hata majaribio ya mara kadhaa ya Tajiri Mninga kutaka kupoteza maisha ni Nasri mjukuu wake ambae alihusika.
Mzee Mninga baada ya kuona familia yake ilikuwa haimtakii mema na hakuna ambae alikuwa na uwezo wa kuongoza mtandao mkubwa kama wa Chatu ndipo alipompatia Dina mlinzi wake ambae aliamua kumfanya mjukuu kuwa kiongozi , jambo hilo lilikuwa ni la kushangaza kwa msichana mdogo kama Dina kuwa kiongozi na iliibuwa migongano ndani ya umoja lakini baadae lilikuja kukubalika na Dina akawa kiongozi rasmi.
Moja ya mfanikio makubwa ambayo Dina aliyapata tokea kufariki kwa babu yake ni kudhibiti tukio la mara ya pili ambalo lilifanywa na adui wa babu yake kwa kutumia mbinu ileile ya Panyaroad , ilitumika miaka kadhaa nyuma , tukio hilo lilitikisa sana nchi ya Tanzania kiasi kwamba mara baada ya Dina kufanikiwa kulizimisha aliamua kubadili jina la mtandao wa Panyaroad na kuubatiza jina la Chatu.
Maswala hayo yote tokea kuanzishwa kwake kwa mtandao huu wa kimaslahi mpaka kubadilika jina lake ilikuwa ni siri kabisa , ni swala ambalo lilikuwa likifanyika katika ulimwengu wa underwold.
Dina mara baada ya Nasri ambae ni binadamu yake sasa kuasi kundi kwa kumuua tajiri Mninga aliamua kumtoa nchini kwenda kuishi nchini Australia huku akimtumia hela ya matumizi hakutaka kumpa adhabu kutokana na kwamba bado alikuwa ni familia ya tajiri Mninga.
Sasa kitendo cha kuona Nasri akiwa ametangulizan ana Afande Chika basi alijua kuna mpango unaendelea chini kwa chini na swala la Zefa kupewa adhabu sio sehemu bali ni kisingizio tu cha kuficha mpango wa muda mrefu.
Hamza na yeye sasa aliweza kuelewa, Hamza alikuwa akiujua ukubwa wa kundi hilo la Chatu ndio maana hakutaka kujiingiza tokea muda mrefu , ki ufupi alijua Dina alikuwa na majukumu makubwa mno kuhakikisha operesheni za mtandao huo zinafanya kazi.
“Kwahio huyu ndio Nasri ambae alimuua babu yake kwa kumtumia Daktari , ili aweze kuwa kiongozi .. sasa kama mtu unaweza kumuua babu yako wa damu, unaweza vipi kuongoza umoja wa mtandao wa Chatu..”Aliongea Hamza.
“Acha kuongea ujinga , sikumuua babu mimi , huyo m*laya ametunga uongo ili watu kumuamini , babu aliamua kumfanya kuwa mjukuu wake akiwa hana hata familia lakini akaamua kuulipa ukarimu wake na chuki , ndio ambae amenipokonya urithi wangu kwa kusambaza uongo”
“Kama unachosema ni kweli kwanini babu yako akaamua kumpatia Dina uongozi na sio wewe?”
“Kwasababu alikuwa mzee na tayari uzee ulimfanya kuwa mjinga”
“Duuh , unadhani ni sahihi kumuita marehemu babu yako mjinga?”Aliuliza Hamza na palepale Nasri alijua ameongea ujinga na alibadilisha topiki haraka.
“Wewe shombeshombe , siku ya leo nimeisubiri kwa muda mrefu , tunakwenda kusafisha
wasiohusika na umoja wetu moja kwa moja”Kauli ile ilimfanya Dina kutoa tabasamu na alipiga hatua mbili mbele.
“Kwahio mmeamua kulea fujo kwasababu mmeshamrudisha Nasri kutoka Australia , hivi mnadhani kinachoufanya mtandao wa Chatu kuendelea kuimarika ni kwa kumrudisha Nasri?”
“Mnadhani huu umoja unaendeshwa kwa sheria za kifalme sio , kwamba kwasababu Nasri anadamu ya Mzee Mninga anaweza kuwa kiongozi , mnapaswa kujua Nasri anatumika tu na wanasiasa ambao wanataka kujimilikisha mtandao huu , mimi Dina ikitokea mmeleta mtu ambae hana makando kando na wanasiasa nipo tayari kuachia ngazi, lakini kama mnaleta hili shushu lenu ndio liwe kiongozi , hata mnikamue damu yangu mpaka tone la mwisho sipo tayari kukabidhi uongozi”
“Dina sio juu yako kuamua kuhusu hili , Nasri ana sapoti ya wazee kutoka Congo , Rwanda, Kenya na Uganda , na tunaamini anaweza kurithi mikoba ya babu yake , usidhani kwasababu ya kutaka kuleta fujo zako hapa unaweza kufanikiwa”Aliongea Debora.
“Dina umesikia , mimi ni Nasri Mninga mtoto wa Mzee Rama Mninga nina damu ya Mzee na babu yangu , hivyo mimi ndio mrithi halali , wewe ni yatima tu”
“Huna unachokijua Nasri , babu hakuniachia uongozi kwasababu ya damu yake , aliniachia kuongoza kwasababu aliona ni mimi pekee ambae naweza kuendeleza alichokianzisha”Aliongea Dina na kisha alimgeukia Afande Chika”
“Afande Chika naona umeamua kuungana na kundi na kundi la kihalifu na kuwakabidhi siraha za moto , huoni hili likitoka nje ya hapa itakuwa skendo kwako?”
“Nyamaza wewe (tusi), unadhani nimeaacha mlumbane kwasababu sina cha kuongea , ulichomfanyia kijana wangu leo nalipiza kisasi kwa kuondoa kiungo kimoja kimoja katika mwili wako”Aliongea Afande Chika ka hasira mno.
“Nilichokifanya ni kumuadabisha kijana wako kwa tabia zake chafu baada ya wewe kutumia cheo chako kumkingia kifua, na siogipi vitisho vyako maana hutonifanya chochote , halafu wewe Nasri muda mwingine tumia hata akili za kuzaliwa , umakuja na watu wamepewa siraha za moto , hujui hili hata lina maana ngani ndani ya nchi kama Tanzania , huoni kwamba inatafutwa sababu ya kuugawanya umoja wetu?”aliongea Dina kwa hasira.
“Dina kama unaona woga wewe sema naona woga , acha visingizio , maamuzi yashafanyika , tunajua uwezo wako wa kininja lakini mbele ya chuma cha moto uwezo wako unafikia mwisho…haha”Aliongea Nasri.
“Sikuwa na mpango wa kukuua kwasababu ya uhusiano wako na babu lakini naona sina jinsi , ili
kufanikiwa kuendeleza alichokianzisha babu inabidi niwaue wote na kurudisha amani katika mtandao wetu”
“Sogea utuue kama huo uwezo unao , agizo langu moja tu hakuna ambae atabakia hai kwenye kundi lako”Baada ya kuongea hivyo Debora na wenzake wote walisogea nyuma ya wale mabaunsa wenye siraha wakihofia watapigwa risasi.
Dina upande wake aligeukia wale watu wake aliokuja nao waliokuwa na sura za kijeshi lakini hawana siraha kwa kuwathaminisha.
“Ndugu zangu leo tunavita ya damu na jasho na adui yetu ana bunduki , kama mnaogopa kufa bila sababu mnaweza kuondoka , mkibaki piganeni na mimi, naahidi nitaenzi utiifu na uaminifu wenu maisha yangu yu yote”Aliongea Dina kwa nguvu. “Tupo tayari kwa ajili yako Raisi wetu”Aliongea Mmoja wapo wa vijana wale na wengine wakafuatia.
“Utiiifu kwa raisi wetu Dina , vifo kwa wasaliti”Waliongea kwa nguvu huku wakionekana kuchangamka.
Dina mara baada ya kuona tukio hilo alijikuta akipatwa na hali ya msisimko , hakuamini watu wake walikuwa wakimwamini hivyo.
Hamza upande wake mara baada ya kuona hali ilivyo alijikuta akivuta pumzi , ilikuwa ni kama anakummbuka matukio ya nyuma ambayo
alishawahi kufanya na muda ule alitoa tabasamu lililojaa uovu ndani yake.
Lakini sasa kabla ya mtifuanno huo haujaanza simu ya Hamza ya kichina ilianza kuita kwa nguvu , mwito ulikuwa wa juu kiasi kwamba ulisababisha watu wote kumwangalia.
Wale maadui walimwangalia kwa waswwasi wakidhania pengine Hamza kuna kitu ambacho anapanga , kwanini simu kuia katika muda kama huo.
Hamza hakujali macho yao , aliingiza mkono mfukoni na kutoa simu na kisha akaanza kuongea.
“Ndio , nimekuambia ni kwenye kiwanda mwisho kabisa huku , ukikaribia utaona kuna magari mengi yameegeshwa nje , ukikaribia wewe gonga nitapokea”Aliongea Hamza na kisha akakata simu.
“Ulikuwa ukiongea na nani?”Aliuliza Dina.
“Niliagiza chakula kwenye Bar moja hapo , nina njaa sio ya kawaida , hawa watu ambao wanataka kukuua wasubiri kwanza nishibe, ni kheri kufa ukiwa umeshiba kuliko kufa na njaa”Aliongea Hamza.
Kauli yake iliwaacha mdomo wazi kila mtu aliekuwa hapo ndani na hata wale wa upande wa uadui.
“Haha… Dina umewakataa vibopa wengii lakini leo hii umekuja kupenda mpuuzi kama huyo, ambae anataka kushiba kwanza ndio ashuhudie kifo chako”Aliongea Nasri kwa kejeli.
Upande wa Dina alikuwa kwenye mawazo , ijapokuwa matendo ya Hamza yalichekesha lakini upande mwingine ilionyesha kwa kiasi gani hakuwa na wasiwasi juu ya hatari iliokuwa mbele yake.
Dakika chache tu mtu wa delivery alifika na Hamza mara baada ya kusikia mlango ukigonghwa alikimbilia na kwenda kuufungua.
“Bro mbona magari mengi hivi hili eneo , kazi zinafanyika hadi usiku??”Aiongea yule kijana mara baada ya kumkabidhi Hamza parcel ya chakula na baada ya pale kwa umbea aliingiza kichwa ndani na kupiga chabo na alijikuka akikamaa mwili mara baada ya kuona watu wakiwa na bunduki na alimwangalia Hamza kwa hofu.
“Dogo usiwe na wasiwasi tunashoot filamu ya kimapigano , hizo bunduki ni za risasi za plastiki”Aliongea Hamza,
“Kumbe , aisee kwa hizo bunduki zinavyoonekana kama za ukweli naamini litakuwa bonge la muvi, lakini kwanini wengine hawana bundiki wamebeba mapanga na virungu?”Aliuliza bwana huyo ambae alikuwa na rafudhi yake ya watu wa kanda ya ziwa. “Dogo inamaana kwenye muvi hujawahi kuona watu wanapambana na mapanga?”
“Nimeona bro”
“Nadhani sasa umeelewa , hii ni pesa yako chenchi utakunywa soda”Aliongea Hamza akimkabidhi na bwana yule alipokea na badala ya kuondoka alisogea pembeni akitaka kuangalia.
“Dogo wewe nenda kaendelee na mishe zako , hii filamu utaoiona wakati wa kutoka “
“Nitajie basi hata jina ili ikitoka niwe wa kwanza kuicheki?”
“Itakuwa inaitwa Ngumi ya uzalendo”
“Poa Bro nasubiria kwa hamu zote”Aliongea na kisha aliruhusiwa kuondoka na Hamza alifunga mlango wa geti kwa ndani.
Hamza mara baada ya mtu wa delivery kuondoka alitembea mpaka kwenye bodi ya trella la gari na kukaa chini.
“Dina nimeagiza nyama ya mbuzi ya kukaanga na ndizi , njoo tule , usafi umezingatiwa”Aliongea Hamza huku akishika toothpick vizuri akibeba vipande vya ndizi.
“Wewe endelea tu , sina njaa”
“Kama wew huna njaa basi sina haja ya kuwakaribisha wengine , nisubirini dakika chache nimalize kula haraka mambo mengine yaendelee”
Nyama zile zilikuwa nyingi mno na zililikuwa zikitoa harufu nzuri mno kiasi kwamba watu walikuwa washasahau kilichokuwa kikiendelea na kumkodolea Hamza kwa macho ya uroho.
“Bro wewe malizia chapu tuwashughulikie hawa wasaliti”Aliongea Lau mara baada ya Hamza kumpa ishara ya kusogea kujiunga nae lakini akakataa huku akivaa gloves zake nyeusi vizuri.
“Lau ijapokuwa umekunywa sana damu ya mbwa mwitu lakini huwezi kushindana na risasi”Aliongea Nasri.
“Achana na mimi Nasri”Aliongea Lau kwa hasira , walikuwa marafiki hapo mwanzo kabla ya kuhitalafiana.
“Alichosema Nasri ni sahihi , Lau tunaujua uwezo wako , kama upo tayari kujisalimisha tutakuacha uendelee kuwa na sehemu yako ndani ya umoja”Aliongea Debora lakini Lau alimpotezea.
“Afande Chika kama unataka kuendelea kuwa na cheo ndani ya jeshi la polisi ondoka na watu wako na washauri na wengine waache uhasama tutahakikisha mnaendelea kupata maslahi ndani ya mtandao”
“Acha kuongea ujinga , sisi ndio wenye siraha za moto na unaongea ujinga , Lau nakushauti umshauri bosi wako Dina akubali kujisalimisha kuliko kumwaga damu zenu ambazo hazina hatia”
“Hayo ni mawazo yako , nipo tayari kwa ajili ya Madam muda wowote , kama sio yeye ningekuwa gerezani sasa hivi , kwangu tokea siku ile ni Madam alienipatia nafasi ya mara ya pili ya kuishi . sio mimi tu kila mmoja upande wetu amepitia changamoto nyingi ambazo Madam amesaidia sana kuzitatua , kwetu sisi Madam ni wa kwanza kabla ya nafsi zetu” “Master Lau tupo tayari kukufauta na kumlinda Madam”Wengine wote walimuunga mkono kwa sauti na muda uleule wale wanaume mabaunsa waliokuwa na bunduki walisogea mbele na kukoki siraha zao kuelekea kundi la Dina huku wakiwa wamezifunga viwambo vya kuzuia sauti.
“Bro’s kwa ajili ya umoja wetu ni muda wa kupambana kwa ajili ya kiongozi wetu”Aliongea Lau kwa nguvu akisogea mbele bila hofu.
Lakini muda huo huo kivuli kilisogea mbele kwa spidi ya ajabu , alikuwa ni Dina mwendo wake ulikuwa sio wa kawaida hata kidogo na alikuwa akijongea kama vile ni nyoka aina ya Cobra aliekuwa ameinua shingo yake juu.
“Swiii.. Swiii!!!”
Nyota mbili zenye makali kama ya kisu zilifyatuliwa na Dina na kabla ya wale mabaunsa wenye bunduki hawajainua siraha zao walikuwa washatobolewa kwenye mapaji ya nyuso zao na kudondoka chini.
Debora na wenzake waliofika hapo ambao hawakuwa wakijua nini maana ya uninja walijikua wakitetemeka kwa hofu.
“Acheni kushangaa mnasita nini mshambulieni asiwasogelee”Aliongea kwa nguvu Chika maana wale mabaunsa ni kama wamezubaa na baada ya kuambiwa hivyo walishituka.
“Tuutu , tuuu , tuuu”
Kitendo cha wale watu kuanza kushambulia Dina hakutaka kufanya uzembe aliruka sarakasi na kwenda kutua kwenye kabati la chuma kulia kwake. “Ding , Ding !!”
Sauti ya risasi kugongana na chuma ndio iliosikika , kilichowasaidia watu wa upande wa Dina ni kwamba walikuwa wamesimama upande wenye magari na mashine za vyuma.
Kitu kilichompa ahueni Dina ni mara baada ya kuona wale mabausa licha ya kuwa na bunduki lakini hawakuwa na uwezo wa kulenga ikimaanisha walikosa mafunzo.
“Wasogeleeeni kwa spidi , hawana mafunzo ya kutumia bunduki”Aliuongea Lawrence kwa nguvu lakinin kabla hata hawajachukua hatua Hamza aliwazuia kwa mbele.
“Bro!!”Aliongea Lau asijue Hamza anataka kufanya nini.
“Hamza acha kusimama mbele utashambuliwa na risasi”Aliongea Dina ambae alikuwa amejificha nyuma ya chuma.
Kwasababu Hamza alikuwa mbele basi risasi yoyote ingeanza kumpata yeye kabla ya wengine.
“Huwa inaleta faraja ukipigana huku ukiwa umeshiba ..”Aliongea Hamza.
“Bro Hamza najua uwezo wako ni mkubwa lakini usiwe na haraka watakupasua na risasi , tushambulie kwa pamoja kuwapunguzia umakini” “Haina haja”Aliongea Hamza.
“Kwanini?”
Lakini Hamza alikuwa ashaondoka mbele yake na ile anakuja kurudi alimuwekea Hamza lile boksi ililokuwa na chakula ndani yake.
“Nishikie chakula changu sijashiba vizuri bado”Aliongea na kisha akasogea mbele , kila mtu alimshangaa hata Dina mwenyewe alikuwa kwenye mshangao na alitamani kwenda kumzuia lakini aliogopa akijitokeza bila plan wataanza kushambulia.
Upande wa Nasri na Afande Chika hawakuwa na wasiwasi kabisa , walishajua vita ni yao hivyo walikuwa wakisubiri wajitokeze washambulie , sasa baada ya kuona Hamza anawasogelea bila ya wasiwasi walijikuta wakimshangaa.
“Huyu mpuuzi kweli ni kichaa”Aliongea Nasri akimwangalia Hamza.
“Mshambulieni kabla hajawafikia”sauti ilisikika kwa nguvu na muda huo sauti ya risasi kugongana na vyuma zilianza kusikika kama mvua nyingine zikimsogelea Hamza.
Lakini kitu cha ajabu ni kama Hamza alikuwa akiwasoma mawazo na matendo yao ya mikono , kwani alianza kukwepa kwa namna flani hivi kama anacheza mziki na kila risasi iliomfikia iliweza kumpita , haikuwa spidi ya kawaida kwa binadamu hata kidogo.
Wale mabaunsa walijikuta wakishikwa na mshangao wa uwezo usiokuwa wa kawaida wa Hamza na walipaniki na kuanza kurusha risasi haraka haraka.
Ilikuwa ni kufumba na kufumbua Hamza alikuwa mbele yao huku baadhi risasi zikiwaishia na walimwangalia kama vile wamekutana na Israeli mtoa roho.
Hamza hakutaka hata kuwapa nafasi ya kufikiria amewafikiajena kwa kutumia toothpick tatu
alizisukumizia zote katika koo la moja ya baunsa na ni damu tu zilizoanza kutoka.
“Pumbavu ,muueni haraka”Alipiga kelele Nasri mara baada ya kuona moja ya watu wake ashadondoka na anatapatapa akitokwa na damu eneo la shingoni.
Kitu cha ajabu kilitokea muda uleule wale mabaunsa walijikuta wakimwangalia Hamza bila ya kumfanya chochote , ilikuwa ni kama wanamshangaa lakini haikuwa hivyo viungo vyao vya mwili ni kama vilikuwa vimeshikiliwa na kitu na kufanya wasiweze kufanya chochote , Hamza kwa kutumia vidole viwili aliwapitia kwa spidi na kuwaangusha mmoja baada ya mwingine na ndani ya dakika moja wote waliokuwa na bunduki walikuwa wamekufa wengine wakipoteza fahamu.
Mzee Dembe alijikuta midomo yake ikicheza cheza kama anakifafa asiamini kile anachoona mbele yake.
Wale wa upande wa Dina mara baada ya tukio lile waliwahi bunduki na kuwasogelea wale wazee walioongoza usaliti na kuwalenga.
“Msije kufyatua, subiri kwanza”Debora alikuwa ndio wa kwanza kujihami huku Afande Chika akiwa haeleweki alikuwa katika hali ya namna gani zaidi ya kumwangalia Hamza tu kwa mshangao.
Hamza mpango wake ni kudhibiti waliokuwa na bunduki pekee na hilo lilifanikiwa ndani ya dakika moja tu.
Dina aliekuwa amejificha alijikuta akisimama kwa mshangao usiokuwa na kifani , ilkuwa ni mara yake ya kwanza kuona tukio la namna hio.
“Dina nimekuondolea hatari tayari , ni juu yako kudhibiti waliobaki , hakikisha huleti huruma”Aliongea Hamza na kisha alinawa mikono kwa maji ya bomba kwenye tanki na kisha alimsogelea Lau na kuchukua chakula chake na kuendelea kula.
Dina aliishia kumwangalia Hamza tu na haikueleweka mrembo huyo alikuwa akifikiria nini.
Mwanzoni alikuwa akijua Hamza ni mtu mwenye uwezo wa hali ya juu wa kimapigano lakini hakujua kama ni zaidi ya alichoweza kuona.
Yaani mtu ameweza kutoguswa na risasi nyingi namna hio na kisha kuua karibia watu wote waliokuwa na bunduki tena kwa kutumia vidole tu na toothpick.
Unapaswa kuelewa mtu wa kawaida akinyooshewa bunduki atahisi woga wa hali ya juu na ataishia kunyoosha mikono juu kujisalimisha , lakini kwa mtu kama Hamza alikuwa na uwezo wa kuona risasi itapita wapi na ni kipi afanye , mbinu hio ilihitaji kiwango kikubwa cha kudhibiti saikolojia na uwezo wa ajabu.
“Lau huyu bwana siku nyingi nilikuwa
nikikudharau kumpa heshima , lakini inaonekana ulikuwa ukimjua nje ndani , huu uwezo alionyesha sio wa kawaida”
“Sijawahi kushuhudia binadamu wa hivi, nadhani kuna siri , Lau hebu tuambie unadhani huyu jamaa ni wa kawaida?”
“Hebu acheni kuongea ujinga , Bro Hamza anaweza asifurahi akisikia juu ya hili”
Hamza hakujali kama alikuwa ameua mtu , hamu yake ya kula haikumpotea kabisa , kwa namna moja ama nyingine usingedhani huyu ni Hamza ambae wiki kadhaa nyuma au mwezi alionekana kuwa mzembe , haikujulikana kulikuwa na siri gani anaficha , lakini ilikuwa ni dhahiri hakuwa kiumbe wa kawaida, alikuwa ni kama roboti.
Kulingana na sheria za umoja wa Chatu wasaliti walipaswa kuuliwa mara mmoja
“Nasri ulipanga mauaji ya kumuua Babu na nikakusamehe na leo tena ukakubali kutumiwa na kufanya usaliti , leo hakuna msamaha zaidi ya kifo”Aliuongea Dina mara baada ya kurudi katika hali yake ya kawaida.
Nasri aliwaangalia mabaunsa waliobaki ambao walikuwa ni sehemu ya mtandao wa Chatu.
“Okoteni bunduki mumshambulie”Aliongea Nasri kwa nguvu lakini hata afande Chika hakuwa na nguvu ya kunyanyua bunduki , alikuwa akimwangalia Hamza kwa hofu kubwa mno huku akifikiria namna ya kujiokoa.
Wale mabodigadi tofauti na kumtii Nasri wote walipiga magoti chini wakiomba kusamehewa , kitendo kile kilimfanya Hamza aliekuwa akitafuna nyama kutoa tabasamu.
Walitoa kila sababu ya kujitetea na kwa bahati nzuri Dina hakutaka kuua watu wengi usiku huo , isitoshe wengi wao walikuwa wakifuata maagizo, waliokuwa wamebakia ni Mzee Dembe , Debora , Balozi Khumeriana na Afande Chika pamoja na Nasri.
“Yoyote ambae yupo tayari kupiga magoti na kuahidi utiifu na uaminifu kwangu , nitamtoa katika kundi la wanaokufa leo hii”Aliongea.
“Dina hebu fikiria kwanza , unadhani sisi pekee ndio tumeamua kufanya usaliti , unadhani silaha kama hizi katika taifa kama Tanzania tungezipata wapi?”Aliongea Debora kwa sauti na Dina aliendelea kuwasogelea taratibu taratibu.
“Hiuna haja ya kuongea chochote , najua ambaye yupo nyuma yenu ni Samweli Mbilu hawala wako wa muda mrefu”Aliongea Dina na kumfanya Debora kutoa macho.
“Wewe umejuaj….?”
“Unadhani kwasababu nafanya kazi ya kuuza chai sijui nani ni adui yangu na nani ni rafiki yangu , unadhani mtandao wa chatu ni kuitwa kiongozi tu, Nasri unadhani kwanini babu aliniamini na kunipatia uongozi , ni kwasababu akili yangu ishatoka nje ya boksi muda mrefu , kukupeleka Australia haikumaanisha sifuatiliii unachokifanya kila siku , vikao vako na balozi wa Tanzania nchini Australia nilikuwa nikipata ripoti ya kila mnachozungumza”Aliongea Dina.
“Sikutaka kukuchukulia hatua tu kwasababu ya undugu wa damu na Mzee Mninga , lakini leo hii umevuka mpaka tena ulichonikasirisha zaidi ni kukubali kutumiwa na Raisi Mbilu ili ajimilikishe mtandao wetu”Aliongea kwa hasira na palepale Nasri mara baada a kusikia hivyo alijikuta akilainika na alijikuta akipiga magoti bila ya kupenda.
“Cousin , cousin kwasababu mimi ni ndugu yako naomba unisamehe , sito…”
Kabla hata hajamaliza sentensi yake kisu tayari kishatoboa paji la uso wake na kudondoka chini akitoa macho.
Tukio lile liliwafanya waliobaki kutetemeka mno na aliekuwa wa kwanza kupiga magoti alikuwa ni Afande Chika na wakafuatia wengine.
“Madam , mimi Chika nimefanya mengi yasiostahili kwa kutumia madaraka ya cheo changu na kuumiza watu wengi , nakiri makosa yagu naomba uyasamehe maisha yangu , mimi na
Debora tupo kukupaia siri ili utusamehe”
“Siri gani hio ambayo inaweza kulingana na uhai wenu”Aliongea Dina huku akimkazia macho mwanamaa Debora.
Chika alimwangalia mdogo wake kwa kumpa ishara amwelezee Dina lakini upande wa Debora alionekana kuwa na wasiwasi.
“Mpango wa kuudhoofisha mtandao wa Chatu haujasukwa na Samweli”Aliongea Debora huku akiwa na wasiwasi.
“Kama sio Samweli ni nani mwingine mwenye madaraka ya kuwapatia mpaka siraha kwa ajili ya kunishambulia?”
“Kuna watu wapo nyuma yake”Aliongea Debora na kisha alimpa ishara Dina kusogea karibu na palepale alimnong’oneza jambo, kitendo kile kilimfanhya Hamza aliekuwa mbali kuongeza umakini kwa Debora asije kuwa na hila.
“Wahusika wakuu ni watu kutoka Binamu Island”Aliongea Debora na kauli ile ilimfanya Dina kushangaa kidogo na palepale tabasamu la uovu lilimtoka na kufumba na kufumbua Debora aliguswa shingoni na kudondoka chini kama furushi. “Debora..!!”
Afande Chika aliishia kushikwa na hofu akidhania mdogo wake Debora ashapoteza maisha.
“Sijamalizana na nyie bado”Aliongea na kisha aimgeukia Lau.
“Lau wapelekwe Chimbo , Adhabu yao ya usaliti itafuatia baada ya kukutana na Mbilu”
Comments