SEHEMU YA 38.
Saa moja kamili za asubuhi ndio muda ambao Hamza alirudi Egret , baada ya kuingia sebuleni aliweza kumkuta Regina ambae alikuwa ashajiandaa kuelekea kazini na sasa alikuwa akipata kifungua kinywa.
“Hamza umerudi , mbona jana hukupiga hata simu kututoa wasiwasi , Regina alikuwa na wasiwasi”Aliongea Shangazi ambae alikuwa akitokea jikoni.
Kauli ile ilimshangaza Hamza kwani alisahau kabisa jana kupiga simu , sio kwamba alifanya makusudi bali ni kwamba amezoea kuishi mwenyewe kwa muda mrefu hivyo mazoea yalimfanya kusahau kupiga.
“Shangazi unaongea nini , mimi sikuwa hata na wasiwasi , nilichelewa tu kumaliza kazi zangu”Aliongea Regina ambae ni kama ameanza kuwa mwekundu, alijihisi kukosewa kutokana na kauli ya Shangazi.
Upande wa Hamza alijua kabisa Shangazi aliongea hivyo makusudi kabisa lakini hata hivyo aliamua kuichukua kauli yake kama ilivyo.
“Regina siku nyingine nitakuwa napiga simu ili nisikutie wasiwasi”Aliongea Hamza na kumfanya Regina ambae hakutaka hata kuangaliana na Hamza usoni kuinua macho yake akitaka kumfokea lakini alisita mara baada ya kugundua Hamza alikuwa amebadili mavazi mapya kabisa tena yanaonekana kuwa ya bei ghali , kulikuwa pia na harufu ya marashi ya kike ambayo alikuwa akiyanusa.
Nguo ambazo jana Hamza alivaa zilikuwa ni zile ambazo zlipewa na Regina na hata marashi ambayo Hamza anatumia amempatia yeye , sasa mara baada ya kugundua amebadilisha mavazi na pia kunukia marashi ya kike, alijikuta akivuta picha juu ya kile amabcho kilikuwa kikiendelea usiku kucha na kumfanya kurudi asubuhi , muonekano wake ulizidi kuwa na ukauzu usiokuwa wa kawaida na hakuongea neno zaidi ya kuendelea na kifungua kinywa chake kimya kimya.
Hamza mara baada ya kuona ukauzu huo hakutaka kumchokoza zaidi ya kupata kifungua kinywa maana hata yeye hakupata chochote.
Jana baada ya kuondoka katika eneo la tukio , muda ulikuwa umeenda na alitaka kurudi nyumbani moja kwa moja lakini Dina alimzuia na kumwambia akalale nyumbani kwake.
Hamza alitaka kugoma lakini Dina alimuwahi kwa kumwambia atalala katika chumba cha wageni ndio Hamza alikubali, sasa kutokana na mavazi yake aliondoka nayo kuchafuka ilibidi Dina kumwandalia nguo zingine.
Dina hakuwa na hasira tena na Hamza kwani kama sio yeye hakujua ni kwa namna gani tukio la jana lingeisha.vipi.
Mara baada ya chai Hamza hakuwa hata na haja ya kwenda chumbani na aliongozana na Regina kwenye gari kuelekea kazini.
Mara baada ya wote kuingia ndani ya gari pamoja na kumfunga mkanda Regina alimwangalia Hamza kwa macho makavu.
“Hizo nguo zako umepewa na mpenzi wako?”Aliuliza Regina.
“Ah!.. ndio”
Hamza aligwaya kidogo , ukweli alitaka kusema ni rafiki yake wa kike mwingine kabisa lakini aliona asiende mbali , isitoshe aliona namna ambavyo Regina alivyokauzu.
“Vipi kuhusu nguo nilizokupatia?”
“Zimepata misukosuko nikabadili”Alijibu Hamza akiwa na tabasamu.
“Misukosuko gani iliokufanya kukesha usiku mzima”
Hamza alifikiria na kujiuliza au amwambie kilichotokea lakini hata hivyo aliona bado haina maana.
“Misukosuko ya hapa na pale , halafu Regina kuna kitu nataka pia nikwambie..”
“Sitaki kusikia uongo wako , isitoshe sijali unachofanya na mpenzi wako maana hakinihusu”
“Hujali lakini unauliza..”Hamza aliongea kwa chini chini.
“Umesemaje?”Aliongea Regina huku akimkodolea Hamza na macho makubwa.
“Sijasema kitu , hakuna nilichosema”Aliongea Hamza huku akitingisha kichwa lakini Regina hasira zilikuwa zimempanda kiasi kwamba hata kuhema alikuwa akishindwa.
“Hamza naomba unisikilize kwa umakini , ijapokuwa nimekuruhusu kuishi nyumbani kwangu , kula chakula changu na kutumia kila kitu changu lakini uvumilivu wangu una mwisho, kwasababu unao uwezo wa kuvaa nguo zinazogharimu kiasi kikubwa cha hela , nenda dukani nunua nguo zako , nunua gari lako na jaza mafuta kwa hela zako na kisha mtoe out mpenzi wako katika gari yako , kwanzia leo na kuendelea nisije kuona unaondoka na gari yangu isipokuwa tu kwa ruhusa yangu wakati wa kazi,umenielewa?”
Hamza hakuelewa kwanini Regina kapaniki asubuhi yote hio , isitoshe ni nguo tu kutoka mara moja na gari yake.
“Nimekuelewa bosi , Vipi nikitumia baiskeli yangu?”
“Utajua mwenyewe , sitaki kukuona unatumia gari yangu kwenda kuzurula zurula na wanawake zako”
“Halafu kingine hakikisha James na baba yake hawajui mambo yako , ukitaka mkataba wetu kuingia dosari basi wewe fanya unavyojisikia tu”
Hamza aliishia kutingisha kichwa kwa haraka haraka ili mradi asiendelee kufokewa.
*****
Upande mwingine ndani ya nyumba ya
Mheshimiwa raisi ya mapumziko katika upande wa vyumba vya kuchukulia mazoezi(GYM), alionekana mwanaume wa makadirio ya miaka kama sitini kwenda sabini hivi akichukua mzoezi kwa kukimbia katika Treadmil.
Hakuwa peke yake , kulikuwa na mwanamke mrembo pia mwenye shepu matata sana ambae alikuwa akifanya pia mazoezi, mwanamke huyo mrembo alionekana kijana sana makadirio ya miaka ishirini na nane hivi kwenda therathini.
Kwa jinsi Mzee huyu alivyokuwa akikimbia kwa spidi na muonekano wake wa kimwili ilionyesha ni kwa namna gani alikuwa akiijali afya yake.
Mzee licha ya kuwa makini na mzoezi hakuacha kukaza macho yake kwenye kioo kikubwa akiangalia shepu la mwanamke mrembo aliekuwa akichukua mazoezi pia.
Baada ya kama nusu saa ya Mzee yule kukimbia alijikuta akizma mashine na kukaa chini huku akihema kwa nguvu na kumfanya na yule mrembo kuzima mashine na kisha kujifuta jasho na kitaulo. “Sam endelea bwana , dakika ishirini kila siku?” “Tresha mpenzi , unataka nishindane na wewe ambae damu yako inachemka”
“Hufanyi mazoezi kushindana , bali unafanya kwa ajili ya kujenga afya yako , kadri ambavyo unapiga hatua moja mbele katika kufanya mazoezi ndio unaongeza dakika hamsini za kuendelea kuishi”.
“Kama ni kuongeza dakika haina haja kufanya mazoezi , ninachopaswa ni kulipa hela na kuingia ndani ya Lazarus Lounge kwa dakika hamsini tu”Aliongea na kumfanya Mrembo Tresha kutoa tabasamu.
“Halafu mpenzi tukizungumzia kuhusu Lazarus Lounge, natamani na mimi siku moja kuingia”Aliongea Tresha huku akilegeza jicho mbele ya Mzee Sam.
“BINAMU wamekuwa na sheria kali sana juu ya nani anaingia ndani ya Lazarus Lounge , Tresha wewe ni mfanyakazi wa Binamu nadhani unajua ninachomaanisha , ila siku wakiondoa vigezo vyao nitahakikisha unakuwa wa kwanza kuingia , kwangu pia imekuwa ngumu kupata nafasi mara kwa mara ndio maana nimekubali kuchukua mazoezi kuweka mwili sawa”Aliongea na mwanamke huyo mrembo alionekana kutokuwa na shida.
Alikuwa ni Mrembo Tresha ndio , muda huo alikuwa mwanamke ambae mbele ya mwanaume lazima ulegee, alikuwa akivutia haswa , kama ndio kuengeneza sura na umbo basi alifanikiwa.
Dakika chache wakati Mzee Sam na mrembo wake wakijiandaa kuchukua mazoezi ya kunyoosha viungo ili kumalizia bwana mmoja alievalia suti aliingia ndani ya ukumbi huo na kumsogelea Mzee Sam huku akiwa na simu mkononi , bwana huyo alionekana kuwa mlinzi.
“Mheshimiwa kuna simu hapa kutoka kwa mstaafu”Aliongea yule bwana .
“Mgweno ukiona anapiga asubuhi asubuhi jua kuna kitu hakipo sawa”Aliongea na kisha alipokea simu ile na kuweka sikioni mara moja. “Habari za asubuhi Mzee Mgweno?”
“Mbilu umezisikia taarifa juu ya misheni ya jana ilivyoenda”Sauti upande wa pili iliuliza.
“Sijapata taarifa , nasubiria ripoti kutoka kwa Afande Chika”Aliongea Mheshimia Samweli Mbilu huku akikuna sura.
“Basi habari za asubuhi sio nzuri kwako na kwangu , nilikuambia mpango uliokuwa nao hauwezi kufanya kazi mbele ya yule mwanamke”Raisi Samweli Mbilu mara baada ya kusikia kauli hio furaha ya uso ilimpotea
“Nini kilitokea , Chika ameshindwa kumdhibiti Dina licha ya kuruhusu watumie siraha?”
“Taariza zilizonifikia jana kuna kijana anafahamiika kwa jina la Hamza aliefika eneo la tukio na kwa msaada wake alifanikisha kushambulia vijana wote waliokuwa na bunduki na wamepoteza uhai , ndio namna mpango ulivyovurugika”
“Hamza ! kwanini nahisi kama nishawahi kusikia hili jina likitajwa kwenye ripoti?”
“Umelisikia ndio , ni msaidizi ndani ya kampuni ya Dosam na mpenzi wake Regina kwasasa”Mara baada ya Mheshimiwa Sam kusikia kauli hio sasa alikumbuka.
“Nimekumbuka sasa , hili jina nimelisikia kutoka kwa Brigedua Simoni Doswe katika ripoti ya mauaji yaliotokea Zinga, inamaana ni huyu huyu ndio aliejitokeza kumsaidia na Dina?”
“Inaonekana kuwa hivyo , lakini swali langu ni kwanini ausaidie mtandao wa Chatu?”
“Dina nilimdharau , ila inaonekana kajitafutia msaidizi mzuri awamu hii , Mzee Mgweno
nitahakikisha kila kitu kinaenda sawa, kuhusu huyu Hamza MALIBU wanafatilia taarifa zake kwa undani , nadhani ndani ya muda mfupi tutamjua”
“Mbilu hili sio kipaumbele kwasasa , kwanini huulizi kilichowatokea Debora na wenzake,Debora anajua siri nyingi akiropoka kidogo tu mipangyo yangu na yako itaharibika kabisa”Kauli hio ilimfanya Mzee Mbilu kukuna kichwa.
“Mzee Mgweno kuwa na amani , najua nini chakufanya juu ya hili?”.
“Hakikisha hakuna makosa Samweli , kumbuka unaondoka Ikulu na una muda mchache wa kuweka mambo sawa kabla ya Jongwe hajachukua kijiti, nadhani unajua Jongwe sio chaguo letu ndani ya chama , lazima tuwe makini”Aliongea na Mheshimiwa Samweli Mbili alimhakikishia kuwa atafanya kila linalowezekana kukamilisha mpango wao.
Kitendo cha kukaa simu Mheshimiwa Mbilu alijikuta akivuta pumzi nyingi na kumfanya Tresha kumwangalia kwa macho yaliojaa udadisi.
“Maulid Mpigie simu Brigedia Doswe amuachie Dastani hata kama hajahojiwa na afike ikulu mchana bila ya kukosa”
“Sawa Mheshimiwa”
Maulidi alikuwa ni msaisizi wa karibu wa mheshimiwa Mbilu na mara baada ya kupokea maagizo hayo aliondoka kwa ajili ya kuyatekeleza.
Upande wa mrembo Tresha alionekana kuwa bize wakati wote wa kuchukua mazoezi lakini ukweli ni kwama sikio lake liliweza kusikia maongezi yote na mara baada ya kusikia Mheshimiwa anatoa maagizo ya Kanali Dastani kuachiwa huru alijikuta akitoa tabasamu la chini chini.
“Kazi yangu imemalizika kabla hata sijamshawishi Mbilu”Aliwaa Tresha kwenye akili yake.
Mheshimiwa Mbilu hakuwa hata na hamu ya kuendelea na mazoezi tena na aliambatana na Tresha na kutoka katika ukumbi huo, alihitaji kurudi Ikulu kudili na baadhi ya mambo haraka sana.
“Hili dili lazima lifanikiwe kwa namna yoyote ile kabla ya uapisho wa raisi mpya, Bilioni tisini kwa mwaka ni pesa nyingi sana ninazoweza kupata kama mstaafu..huyu Hamza lazima adhibitiwe kabla hajaniharibia mambo yangu”Aliwaza Samweli Mbiu wakati akiingia katika gari kuianza safari ya kuelekea ikulu.
********
Hamza mara baada ya kufika kazini alienda moja kwa moja mpaka kwenye ofisi yake , alipanga kusubiri hadi saa nne kisha aelekee chuo maana ni zaidi ya wiki hajakanyaga na hakuwa na taarifa ya kinachoendelea hususani maswala ya barua za kuanza field.
Ilipotimia saa tatu na nusu alitoka na kuelekea katika ofisi ya Regina , lengo lake ni kutaka kumwambia anaelekea chuo.
Lakini mara baada ya kuingia ofisini kwa Regina aliweza kumkuta Regina akiongea na simu na alionekana kuwa makini kweli.
“Bibi hii ni fursa adimu sana kwako , unajua ni kwa kiasi gani tuliweza kutafuta mawasiliano nae lakini hatukufanikiwa , huyu Dokta ni bingwa na anakuja hapa Tanzania , ni vizuri kama utaonana nae”Aliongea Regina huku akionekana kama vile anabembeleza , alikuwa ameweka mkono mmoja kwenye paji la uso wake.
“Naomba ulichukulie hili kama ombi langu kwako , najua una huzuni baada ya babu kufariki lakini afya yako ni muhimu kwa sasa ….”
Regina alionekana kubembeleza kwa muda mrefu kidogo lakini muonekano wake ulitosha kuonyesha hakukuwa na mfanikio na aliishia kukata simu. “Mkurugenzi nini tatizo la bibi yako , anaumwa?”Aliuliza Hamza ambae hakuwa akizijua taarifa za Regina kuwa na bibi.
“Unauliza wakati umesikia kila kitu?”Aliongea Regina kichuki chuki , ilionekana hakuwa katika mudi nzuri.
“Kwanini upo hapa?”Aliuliza.
“Naelekea chuo , lolote linaweza kutokea huko hivyo kama nitachelewa unaweza kwenda moja kwa moja nyumbani”
“Hivi kumbe hampo likizo bado?”
“Ni kipindi cha field hiki, semista ya mwisho hii mambo ya kuweka sawa ni mengi”Aliongea Hamza na Regina alitingisha kichwa kuonyesha ishara ya kumwelewa.
Lakini muda huo Linda aliingia ndani ya ofisi hio akionekana kuwa na taarifa.
“Bosi , Dr Ronicas ametua nchini Tanzania muda huu , nimefuatilia ratiba yake inaonekana atakuwa hapa nchini kwa siku mbili au tatu”Aliongea na taarifa hio ilimfanya Regina kuonyesha furaha.
“Linda haraka sana fanya appointment tukiwa wa kwanza itakuwa rahisi kuonana nae”
Hamza mara baada ya kusikia jina la Dokta Roinicas likitajwa macho yake yalichanua.
“Huyu Dokta Kichaa kumbe ni maarufu hivi mpaka
hapa Tanzania ,mpaka Regina anamfahamu”Aliwaza Hamza lakini aliona anafikiria ujinga , kwa matajiri ilikuwa swala la kawaida kuwatambua madaktari bingwa maarufu sana kutatua shida zao za kiafya.
“Lakini bosi Dokta Ronicas amekataa miadi na wagonjwa , msemaji wake amesema Dr Ronica yupo Tanzania kwa ajili ya kukutana na rafiki yake na sio maswala ya kutibu”Aliongea Linda na kufanya furaha ya Regina kuzima mara moja.
“Kwanini iwe hivyo , si daktari?”
“Bosi hauna haja ya kuwa na huzuni , Dokta Ronica anafahamika kwa kuchagua wagonjwa anaotaka kutibia , umaarufu wake duniani unampa uwezo huo ndio maana sio mtu wa kupokea miadi ya kuonana na wagonjwa wa kila aina , kwa umaarufu wake ndani ya dunia kila mgonjwa mwenye pesa nyingi na watu maarufu watataka kutibiwa nae , nadhani asipokuwa na vigezo atakuwa bize mno”
“Lakini Bibi ugonjwa wake umekuwa changamoto mno kwa madaktari wengi. Hata Dokta ambae alialikwa kumtibia mara ya mwisho kutoka India amesema tumaini la mwisho ni labda Dokta Ronica kumfanyia tiba, kwa afya ya bibi imeshauriwa asisafiri kwa ndege umbali mrefu, bahati imekuwa upande wake Dokta Ronica yupo hapa Tanzania, hii ni nafasi pekee ya kuhakikisha anamuona bibi”Aliongea Regina na kumfanya Linda kumuonea huruma bosi wake.
“Bosi lakini si wamesema yupo hapa nchini kwa ajili ya kuonana na rafiki yake , kwanini tusitumie ushawishi wetu kumjua mtu huyu mzito ni nani , pengine anaweza kutusaidia kukutana nae”
“Upo sahihi Linda , hebu nenda kafanye uchunguzi ni rafiki gani anazungumziwa , itakuwa njia rahisi zaidi”
Upande wa Hamza alijifanyisha kuwa bize na simu yake lakini alikuwa akisikiliza maongezi yao.
“Regina bibi yako anaumwa nini?”Aliuliza Hamza akiwa na huzuni usoni.
“Kuumwa kwa bibi yangu hakukuhusu , ondoka ofisini kwangu kwanza”Aliongea Regina kihasira , hakuwa na mudi kabisa ya kuongea na Hamza.
“Hey , nimeuliza tu kwa nia nzuri , unajuaje pengine naweza kukusaidia”Aliongea Hamza.
“Anaumwa na saratani ya Kongosho na anatumia betri ya moyo”Aliongea Regina kivivu na Hamza aliweza kuona ni kweli bibi yake ilionekana alikuwa na tatizo kubwa ,saratani ya Kongosho haikuwa ya kawaida.
“Haya umejua sasa anachoumwa , unaweza kumtibu?”Aliuliza Regina.
“Mimi sijui kutibu”Aliongea Hamza na jibu lake lilimfanya Regie mudi yake kuzidi kuwa mbaya.
“Ndio uondoke sasa , unauliza nini kama huna msaada , wewe ondoka zako sijui unaenda chuo kweli au kuonana na mpenzi wako yote ni kheri , sipendi uendelee kunisumbua , sitaki kukuona unaweza kulala huko huko ukijisikia”Aliongea.
Kitendo cha Hamza kufokewa ilihali anajaribu kuonyesha kujali kilimfanya kushikwa na hasira , alikuwa na uvumilivu ndio lakini hasira za Regina mbele yake zilimfanya kuona itafikia siku atakosa uvumilivu .
“Kama ni hivyo naondoka , ila usije kujutia tu maneno yako”Aliongea Hamza huku akijitahidi kuzuia hasira yake isijionyeshe.
Upande wa Regina mara baada ya kusikia kauli hio kiasi flani aliona ni kama ameenda mbali , lakini hata hivyo tabia yake isingemuwezesha kujishusha kabisa.
Alikuwa na hasira na Hamza sana , kila akifikiria namna ambavyo Hamza ameondoka na kwenda kulala huko na mwanamke wake usiku kucha mpaka kuacha mavazi aliompatia na kuja na mengine nyumbani hasira ndio zilizidi kumkaba.
“Usiwe na wasiwasi kabisa , Mimi Regina siwezi kujutia maneno yangu”Alijibu Regina kwa jeuri.
Hamza mara baada ya kupokea jibu hilo hakuina haja ya kuendelea kuongea na alitoka.
Kitendo cha Hamza kutoka tu palepale simu yake ilianza kuita na mara baada ya kuangalia namba ilikuwa ngeni ila alipokea moja kwa moja.
“Hey ! Prince Rich , did you miss me…”
Comments