Reader Settings

SEHEMU YA 41.

Regina alijikuta akishindwa kuamini Hamza amemkandamiza kifudifudi kwenye meza na kuanza kumpiga   makofi ya  makalio, alijitahidi kufurukuta lakini alishindwa kabisa  na  vibao viliendelea kumshukia , Hamza  aliona huyu  mwanamke hataki kupokea simu yangu huku akisema hana sababu sasa vibao hivyo vitampa sababu  ya kutopokea simu yake.

“Ongea , siku nyigine utapokea simu yangu au  hutopokea?”Aliongea  Hamza lakini upande wa  Regina aliishia kung’ata meno  huku akivumilia maumivu.

“Pah!”

Kitendo cha kuendelea kuleta ujeuri na kutojibu ilimfanya Hamza kumuongezea vibao , lakini  hata  kama aliyasikia maumivu kiasi gani , hakuwa tayari  kukubali kushindwa.

“Bora uniue hapa hapa , la sivyo  nitakufanya ujutie maisha yako yote”Aliongea Regina.

Ni kweli hakupokea  simu  lakini hakuona hilo ni kosa la kumfanywa  kutendewa huo ukatili  na alijiambia hawezi kuliacha hilo lipite.

Upande wa Hamza aliamini kumshikisha adabu  kwa vibao kadhaa ingemfanya  Regina kutii lakini kadri alivyokuwa akiendelea ndivyo alivyokuwa akizidi kuwa kiburi.

“Unadhani  ni swala la kupokea  simu , unadhani nakulazimisha kupokea simu kama haina umuhimu?”Aliongea  na kumuongezea viwili vya mwisho na kisha alimwachia.

“Muhuni , jambazi  wewe , unaona raha kupiga  wanawake?”Regina alitamani kutafuta  neno baya zaidi  la kumlaani lakini alikosa kabisa , alihisi maumivu makali wakati wa kusimama.

Muda huo  akiwaza kumfukuza  Hamza kazi simu yake ilianza kuita mfululizo., alitaka kuipotezea ili kudili kwanza na Hamza lakini mara baada ya kuona ni Eliza ambae anapiga alipokea.

“Sis Eliza , kuna tatizo?”Aliuliza  Regina ,  mara nyingi wakiwa peke yao  anapenda kumuita Eliza Sis yaani dada  kama kumheshimu maana ni  mkubwa kwake.

“Asante Mungu , Regina nimefurahi upo salama, vipi  umeonana na Hamza?”

“Mbona uko hivyo , kuna kilichotokea?”Aliuliza huku  akiwa na mshangao kidogo  na alimwangalia Hamza.

“Nilikuwa  nikiendesha  gari wakati tukirudi nyumbani na Hamza  na tulipata ajali baada ya gari kubwa ya mizigo  kutugonga , ilikuwa ni makusudi kabisa na Hamza alipatwa na mshaka pengine ni  familia ya James ndio  wamepanga kutusababishia ajali ndio maana kakimbia kuja kukutafuta  baada ya kuambiwa  haupo nyumbani bado..

“Halafu Mkurugenzi kwanini hukupokea simu wakati Hamza anakupigia , umetufanya tuwe na wasiwasi mno”Aliongea Eliza  na kumfanya Regina  kujua kosa liko wapi na aliishia kumwangalia  Hamza , ile hasira aliokuwa nayo   ndani ya moyo wake kwa kitendo Hamza alichomfanyia ilipotea haraka na kumuacha na aibu pamoja  hatia , lakini kwa wakati mmoja alijihisi furaha  bila ya kuelewa sababu ni nini.

“Ndio maana alionekana kuwa na hasira , kumbe hili ndio sababu”Aliwaza Regina kwenye moyo wake.

“Sis .. uko sawa , hujaumia?”Aliuliza Regina.

“Gari limebaribika  lakini  namshukuru Mungu  nipo sawa , kama sio Hamza  kunitoa kwenye gari kwa haraka  sijui ingekuwaje , dereva wa gari  amekufa pia , niliogopa mpaka nikapoteza fahamu , sijui nini kinaendelea ila kama ni  familia ya James ndio wametutengenezea hii ajali  Mkurugenzi unapaswa kuwa makini”Aliongea Eliza  na upande wa pili alikuwa akisikia makelele, ilionekana Eliza bado alikuwa eneo la tukio.

Upande wa Regina wazo  palepale lilimwingia na alishindwa kuzuia  shauku yake.

“Lakini Eliza   imekuwaje mpaka mkawa na Hamza pamoja , mnafahamiana vizuri?”

“Ah..!,Sisi.. ni  marafiki tulikuwa tukirudi nyumbani baada ya kupata chakula pamoja”

“Oh..kumbe..”

Regina  alishindwa kuendelea kuuliza zaidi , kwa akili yake ya haraka  ilimfahamisha baadhi ya vitu na kumfanya kuwa na hali ya mshangao.

Upande wa Hamza aliweza pia kusikia mazungumzo yao  na alijiambia  inaonekana Eliza mbele ya  Regina hana kifua kabisa  cha kuficha siri.

Regina mara baada ya kukata simu   alimwangalia  Hamza , hali ya hewa kidogo ilikuwa  na ukakasi flani hivi  kutokana na kilichotokea.

“Mkurugenzi  nini maamuzi yako, unanifukuza kazi?”

Regina aliishia kukohoa kidogo huku akiangalia pembeni kupoteza  ishara za  aibu zilizomvaa .

“Sikia .. kutokana  na  kilichotokea   na uadilifu wako kwangu,nitakusamehe”Aliongea.

Maneno hayo   kwake  alijihisi ni kama anaisaliti nafsi yake ambayo ilikuwa ni ya kikauzu  na kujikuta akijiona ni kama anakuwa mdhaifu mbele ya Hamza  na  ilimfanya kushindwa kabisa kukutanisha macho, huku akijihisi  ofisi ikiwa na  joto mno licha ya AC kuwa wazi.

Mwanamke kuwa na aibu mbele ya  mwanaume  anageuka  kuwa  kama ua linalochanua kwa namna ambavyo anapendeza , Hamza alijiambia kama huyu mwanamke angekuwa hivyo  muda wote  angekidhi vigezo vyote vya kuwa mke wake.

Alijiambia kwa muonekano huo basi kila siku angekuwa akimuangalia ingemfanya  kuishi maisha  marefu  zaidi.

Lakini hio kwake ilikuwa ni ndoto , Regina alikuwa na  ugonjwa wa kitabia wa mabiti  wengi wa watoto wa kifalme maarufu kama Princess Syndrome.

Hamza  hata hivyo hakuamini alikuwa amechukua maamuzi ya kumpiga Regina , ni kama amefanya kitendo ambacho hakutarajia na mara baada ya kukumbuka  mabao alivyokuwa akimshushia  na kisha kusamehewa alijikjuta akishindwa kujizuia na kucheka.

“Wewe unacheka nini ,  unafikiria  upuuzi wako ulionifanyia?”Aliuliza Regina kwa hasira  huku akijiambia kwanini amesamehe  kiwepesi hivyo. “Hamna , nilikuwa nikiwaza  ni kweli muuaji ametumwa na familia ya James au kuna kitu kinachoendelea sikijui”

“Haijalishi nani  kakutengenezea ajali , tunapaswa kuwa makini  kwanzia sasa hivi , kama wamefeli kwenye jaribio la kwanza lazima watarudia tena”Aliongea Regina.

“Usiwe na wasiwasi , ili mradi utaendelea kunifanya kuwa karibu yako  nitahakikisha nakulinda”

“Nani  akuamini , ukinilinda mimi   wewe utashindwa kujilinda mwenyewe”

“Unanichukulia poa , mimi  ni mwanaume ambae  kumlinda mpenzi wangu  ni  kazi  rahisi tu kama kutafuna  keki”Aliongea Hamza akicheka na kumfanya Regina kuona aibu kidogo.

“Unaongea ujinga gani , bado nina kazi za kufanya hivyo kaa na mimi mbali”

“Unajua sasa hivi ni saa ngapi , na  bado unataka kuendelea kufanya kazi?, hata chakula cha usiku una  mpango wa kula kweli?”

“Sina mpango wa kula  , nimemaliza  na sitokula”Aliongea kijeuri.

“Hizo kazi zinaweza kufanyika hata baadae , lakini  kula ni muhimu , ukiendelea hivi utashikwa na vidonda vya tumbo ushindwe kabisa kufanya kazi” “Inakuhusu nini . nimesema sitakula”

“Usipokula , nitakushushia kipigo tena”Aliongea Hamza huku  akionyesha mkono wake.

“Wewe , thubutu, jaribu  uone”Aliongea huku akirudi nyuma kwa  woga , aliona ni kama Hamza angempiga tena  ilihali bado alikuwa akiyasikia maumivu.

“Unadhani nashindwa?”Aliongea Hamza huku akimsogelea  Regina  taratibu taratibu huku akiwa na tabasamu la kifedhuli.

Regina aliishia kurudi nyuma huku akishindwa kujua afanye nini , ukweli ni kwamba alikuwa akimuogopa  Hamza  atampiga tena.

“Naomba utulie, kwasababu unadhamira  safi ya  kunijali  nitaenda kula”Aliongea akimzuia na kumfanya Hamza kutabasamu   na kuona kumbe muda mwingine  kumtishia kunafanya kazi.

Baada ya   Regina  kukusanya kila kilichokuwa chake  waliongozana mpaka kwenye maegesho ya  magari na kwenda mpaka Mlimani City.

“Unataka kula nini?”Aliuliza Hamza mara baada  ya kuingia  ndani.

“Mmekula nini na Eliza?”Aliuliza Regina na swali lake lilimshitua Hamza.

“Linahusiana vipi na swala la wewe   kuchagua  chakula”

“Siruhusiwi  kuuliza?”

“Kwannini unataka kujua , Regina unaona wivu?”Aliuliza Hamza huku akiwa na tabasamu.

“Wivu!,sh*nzi , nimeghaili sitaki kula chochote”Aliongea Regina  huku akijifanyisha kununa.

“Kama hutaki kula chochote unaonaje  Doghnut , hapa  wanauza kila kitu”Aliongea  na kumfanya  Regina kutoa macho na mara baada ya kugeuza macho ni kweli aliweza kuona kabati la kioo lililojaa Doughnut.

Dakika ile anataka kukubali , alijihisi kuna tatizo , alijiuliza kama akila Doughnut si  atamkubusha Hamza lile tukio la kula  kiroho roho na kumfanya amcheke.

“Kula Doughnut muda huu kama chakula cha usiku sio vizuri” 

“Wewe unajali nini kama sio  vizuri , ili mradi ni kitu  unachopenda haina haja ya  kuwazia wengine wanavyokuona”

“Kama ni hivyo basi wewe ndio umenilazimisha  na sina jinsi zaidi ya kula”Aliongea Regina  akitafuta kisingizio .

“Hakuna shida  chukulia kama vile

nimekulazimisha”Aliongea  Hamza ambae muda huo hakujua acheke ama alie, mhudumu aliwasogelea na  kuwauliza  wanachotaka kupatiwa.

“Nataka Doghnut nne  zilizochanganywa na  Strawberry  na juisi ya  nanasi”Aliongea Regina  na mhudumu alishangaa kidogo lakini alichukua oda yake.

“Na wewe kaka vipi , unaagiza nini?”

“Mimi nipe doughnut  nane,  nne ziwe za kawaida na nne nyingine zikiwa na Strawberry itafaa, nipatie na chai ya maziwa”Aliongea Hamza akiagiza na yeye  Doughnut.

“Zote niweke kwenye sahani au niwafungie?”Aliuliza.

“Tunakula hapa hapa zote”Aliongea Hamza na kumfanya mhudumu kushangaa kidogo  na alitingisha kichwa kwenda kutimiza  oda ya wateja., hakushangaa sana kwani  kuna wanaume wanakula sana , alishangaa kwasababu mara nyingi wanaofika katika mgahawa huo walikuwa wakila kidogo sana. “Na wewe unapenda  Doughnut?”

“Nitakula nne za kawaida , zilizobakia   zenye strawberry ni za kwako”

“Mimi nataka kula nne tu”Aliongea  lakini alisikika kutokujiamini  alikuwa  nataka sitaki.

“Kama  hutokula  nitazimaliza tu hakuna shida”

“Mhmh..”Regina aliishia kuguna huku akitingisha kichwa.

Mara baada ya kupashwa kidogo hatimae ziliwekwa kwenye meza yao , muda  huo Regina mara baada ya kunusa harufu nzuri inayotoka kwenye donati hizo , tumbo lake lilianza kunguruma  kwa njaa na kwa haraka haraka alishika moja na kung’ata kidogo.

Hamza aliishia kumwangalia Regina  na tabasamu tu  kwa namna ambavyo  alionekana kuridhika kula kitu kama hicho  na alijiuliza  kwanini Regina anapenda vitu yva aina hio , maana kwa mwanamke  mwenye hela kama yeye angeagiza cha maana.

“Hivi kwako ni tamu sana?, mimi huwa naziona  ni kama andazi  lenye  sukari nyingi”Aliongea Hamza na  kauli ile ili mfanya  Regina kumwangalia kwa usiriasi.

“Unaingea ujinga , hivi unajua  namna zinavyotengenezwa?”

“Unakasirika nini sasa , kwani kuna nilipokosea?”Aliongea huku akicheka.

“Donati sio kama andazi  la kawaida, andazi likishaumuka moja kwa moja unalikaanga na mafuta ,  lakini Donati  ni tofauti , mfano hilo tundu katikati  linapimwa  kuendana na ukubwa wa  mviringo wa nje  lakini pia  na radha yake na ulaini , mfano  ukiona   yenye tundu dogo  mara nyingi inakuwa ni  laini kutafuna  , lakini ikiwa na tundu kubwa  ukitafuna ni kama biscuit , sukari  yake  pia inakuwa ni ya kiwango   sahihi , mara nyingi  huwa ni kati ya  gramu tano  au  sita”

“Aisee  inaonekana kweli  unazipenda mpaka kuwa mtaalamu”Aliongea Hamza huku akishangaa, lakini Regina hakujali   na kuendelea kula  donati nyingine na ndani ya dakika chache  nane zote  zilikuwa zimeisha.

Muda wa kuondoka Regina alionekana kuwa na uso unaong’aa kwa furaha , ilionyesha ni dhahiri  akili yake imemkaa sawa mara baada ya  kula  Donati.

“Twende moja kwa moja nyumbani au  tuzunguke zunguke?”Aliuliza Hamza.

“Vyovyote vile”Aliongea na  Hamza aliona   wazunguke zunguke , isitoshe ni mara  chache kwa Regina kuwa na mudi ya kuzunguka zunguka nae kama hivyo.

“Basi tuzunguke zunguke  tuone kama kuna kitu tunaweza nunua”

“Sitaki kununua chochote”

“Sio kwa ajili yako  , tunamnunulia shangazi”Aliongea Hamza.

“Ah ..Shangazi anapenda sana Korosho , tununue hizo”

“Kama ni hivyo basi tupitie upande  ule wa supermarket”Aliongea  Hamza na Regina alitingisha kichwa huku akitoa tabasamu.

Tabasamu lile ilimfanya  Hamza kumwangalia  Regina kwa umakini maana  ni kama ameona kitu  cha ajabu.

“Mbona unaniangalia sana?”

“Nimejikuta nikiwaza,  nakuona itakuwa vizuri  ukiwa unacheka  mara kwa mara ,  unaonekana kupendeza zaidi”Aliongea Hamza na kumfanya Regina kushangaa  huku akiganda.

“Kwanini nicheke?”

“Unazidi kuwa mrembo  ukicheka?”Alijibu Hamza  huku akimkazia macho na kumfanya  Regina uso wake kuwa laini kutokana na kupata joto.

“Ukiendelea kuongea ujinga nitakupotezea mazima na kurudi zangu nyumbani”Aliongea akiwa siriasi na kumfanya Hamza kuchezesha ulimi na kufunga mdomo wake  na kuanza kutembea  huku  wakipita kila  maduka.

“Regina   kwanini unapenda sana kula Donati?, au  ni kwasababu zina sukari maana wanawake wengi mnapenda vitu vitamu?”

“Kwasababu mama ndio  chakula kikubwa ambacho alikuwa akipenda wakati akiwa  ni mjamzito wa mimi?”Aliongea.

“Mama yako akiwa mjanzito , wewe umejuaje?”

“Niliambiwa na watu waliokuwa karibu  na mama , inasemekana mama  alikuwa ni masikini  mno  na  mimba ilimpelekesha  hivyo  hakupenda kula chochote  zaidi ya Donut, kutokana na habari hizo nilijikuta  nikijaribu  kula  mara kwa mara   nikiwa kituoni  na nilijikuta nikizipenda mno, sina uhakika  kama  ninachopenda ni radha au ni kwasababu ya  kutamani  mama yangu angekuwa hai”Aliongea Regina kwa huzuni  na kumfanya  Hamza kumuonea huruma kidogo.

“Nisamehe kwa kukuuliza swali ambalo limekutia huzuni”

“Huna haja ya kuomba msahama , ni mambo yaliopita  isitoshe  namjua mama kwenye picha pekee , nilichosikia  mama alininyoshesha kwa wiki mbili tu ndio akapoteza maisha, kwangu hizi Doughnut ndio kitu pekee  kinachoniweka karibu na marehemu mama yangu”

Hamza alijikuta akiona  ni haki yake kuzipenda , ilionekana  hata hivyo  ndio kitu pekee ambacho alishirikiana na mama yake kula.

Asilimia kubwa  ya  ulaji wa mtoto baada ya kuzaliwa huathiriwa na  mama,ikitokea mama wakati akiwa mjamzito anapenda  kula kitu flani mara kwa mara kwasababu ya kukipenda  inatengeneza  radha ya kitu kile  katika  majimaji  yaliopo ndani ya mfuko wa uzazi hivyo kadri mtoto anavyokuwa  ndio ambavyo  radha ya kitu kile inapozoeleka katika ulimii wake , akija kuzaliwa  akionja kitu hicho ulimi wake utatambua na kukikubali moja kwa  moja na kuona ndio kitu kitamu zaidi, kitaalamu inaitwa  Amniotic

fluid flavor effect.

“Vipi kuhusu wewe?”Aliuliza Regina  mara baada  ya kumaliza kuongea.

“Mimi nini!?”

“Nimekuambia  kuhusu mama yangu , vipi kuhusu wewe wazazi wako,kwa mfano mimi namuwaza sana mama wakati nikila Donati , vipi wewe  ni kipi ukifanya  unamkumbuka sana mama yako?”

Swali lile lilimfanya Hamza kujawa na mawazo  na alijikuta akipiga hatua mbele akimuacha Regina.

“Kama hutaki kusema  acha..”Aliongea Regina.

“Sina kumbukumbu nyingi kuhusu mama , ila namkumbuka wakati wote , kila saa kila dakika  na  natamani kukumbuka kila kitu  kuhusu mama  lakini siwezi”Aliongea   na kumfanya  Regina kumuonea huruma.

“Usitie huruma sana , sina mpango wa kukufariji mimi”

“Hehe.. ni mambo yaliopita   hata hivyo  sihitaji faraja” Aliongea Hamza na kumfanya Regina kuwa na ahueni.

Baada ya kuzunguka zunguka walinunua  Korosho nyingi tu pamoja na  baadhi ya vitu   na kurudi garini   kuanza safari ya kurudi  nyumbani.

Regina kama kawaida alipendelea kukaa nyuma na wakati akiwa anasinzia sinzia kwa kushiba  simu yake ilimshitua na alipoangalia anaepiga ni Linda msaidizi wake.

“Linda vipi   uchunguzi wako umefikia wapi?, Dokta Ronicas yupo Tanzania kwa ajili ya nani?”

“Mkurugenzi , unaweza usiamini  ,  hata mimi mwenyewe bado nimeshindwa kuamini”

“Kwanini  hebu  niambie vizuri”

“Ilikuwa ni  ngumu  kuipata ratiba yake , kwa nilichopata kesho  anaelekea Mbutu  nyumbani  kwao Eliza”Aliongea Linda.

“Nini.. nyumbani kwa Eliza?”

“Ndio  , ineonakana yupo Tanzania kwa ajili ya mama yake Eliza meneja wa idara ya mauzo ,  wiki iliopita Eliza amemtoa mama yake  kwenye hospitali aliokuwa akipatiwa matibabu na kumpeleka kwenye nyumba yao, hili limenifanya kushangaa  ndio maana mpaka sasa nimeshindwa kuamini”

“Hebu ngoja niwasiliane na Eliza kwanza  kuhakikisha , umefanya kazi kubwa  pumzika sasa”Aliongea Regina na kukata simu na  mara moja alimpigia Eliza.

“Mkurugenzi  habari za usiku , kuna tatizo?”Aliongea Eliza mara tu   baada ya kupokea simu.

“Eliza  hivi  unamfahamu Dokta Ronicas?”Aliuliza Regina kwa sauti ya chini.

“Ndio ,kwani  Hamza hajakuambia , namjua ni Dokta ambae  anakuja kesho kumwangalia mama”Alijibu

Eliza  na kumfanya Regina mikono yake kutetemeka.

“Kwahio unamaanisha unafahamiana  nae ?”

“Ndio namjua , nimekutana nae leo kwa mara ya

kwanza , ni rafiki yake Hamza na ndio aliniombea aje kumwangalia mama”

“Nini Hamza ndio kamuomba..!!?”Aliongea Regina kwa mshituko huku akimwangaliaHamza ambae alikuwa bize kuangalia  barabarani.

Hamza alitamani kucheka tokea dakika ambayo  Linda anapiga simu , alikuwa na mpango wa kumwambia  licha ya kwamba  alionekana kumltea jeuri wakati wa mchana, lakini staili hio ya Regina kuujua ukweli ilimfanya kufurahi.

Regina aliishia kumwangalia Hamza kwa macho yasio ya kawaida na  kujiambia huyu Hamza ni nani mbona anamchanganya akili yake , ilitosha  kufahamiana na  fundi cherehani wa kushonea nguo wafalme , lakini sasa hivi alikuwa na uwezo wa kumuita dokta maaurufu duniani kuja kumtibia mama yake Eliza , kitu ambacho  licha ya kuwa na pesa nyingi alishindwa kuweka miadi  na dokta huyo kuonana nchini kwake sembuse kumuita  Tanzania.

“Mkurugenzi mbona umekaa kimya?”Upande wa pili sauti ya Eliza ilisikika.

“Eliza hivi unaijua hadhi ya Dokta Ronicas  katika  fani ya matibabu?”

“Kutokna na ajali ilionitokea leo nimejikuta   na mawazo mengi , na ndio nimemaliza kuoga hapa  , bado hata sijamfuatilia”

“Kama ni hivyo hebu  ingia mtandaoni  na utafuje jina lake  kwanza, mimi nakata simu”Aliongea na Regina alikata simu muda uleule.

Baada ya kuvuta pumzi nyingi na kuzishusha  alimwangalia  Hamza kwa macho ya  maswali. “Kwanini hukuniambia unafahamina nae ?” “Nadhani ushasahau , hukumbuki nilipoingia kwenye ofisi yako na kuulizia hali ya bibi yako  ukaishia kufukuza , unadhani ningeanza vipi kukuambia”

“Sikujua , ungeniambia  kama unafahamiana nae?”Aliongea Regina kwa sauti ya chini.

“Ulisema hutojutia , vipi sasa hivi unajjisikiaje?, nikwambie tabia yako ya kukasirika bila sababu   kwa kutolea watu hasira zako inafanya watu wakuogope na  pengine kukuchukia kabisa”

Regina alitaka kupanda juu lakini mara baada ya kufikiria  hali aliokuwa nayo alijikuta akiwa mpole.

“Naomba unisaidie kumuomba basi Dokta Ronica kuangalia  shida ya bibi yangu”

“Kama  bibi yako atakubali mimi sina shida, nitamuambia”

“Usiwe na wasiwasi , ili mradi Dokta Ronica akikubali nitahakikisha na bibi anakubali kufanyiwa uchunguzi”Aliongea Regina akiwa siriasi

“Nilivyokuona namna ambavyo hampatani na  baba yako nikajua ni hivyo hivyo kwa bibi yako pia , ila kumbe  unamjali?”

“Wakati  babu alivyonileta  katika familia   nilikuwa na miaka kumi  na mtu pekee ambae alinikaribisha kwa ukarimu ni bibi ,  Namheshimu babu kwasababu alinifundisha nini maana ya biashara  lakini  bibi ndio aliekuwa  mtu wa karibu na mimi zaidi , ukiachana na Shangazi  ambae  alikuwa mlezi wangu,  familia nzima  ambae alikuwa akinipenda ni  bibi pekee , wakati ambapo Lamla mke wa baba  akinifokea ni bibi ambae alinikingia kifua, baada ya  babu kufariki ni bibi  ambae alihakikisha nakuwa CEO wa kampuni, hivyo  naweza kutumia kiasi chochote cha pesa kuhakikisha bibi anapona”Aliongea na Hamza alimwelewa.

“Nitaongea na Flora , nadhani hawezi kunikatalia”Aliongea Hamza na kumfanya Regina kufurahi  na alipumua kwa nguvu kuonyesha amepata ahueni.

“Lakini imekuwaje ukafahamiana na mtu mkubwa kama Dokta Ronicas?”

“Sisi ni…”

“Unataka kusema tena umekutana nae Bar sio?”Aliingilia Regina mara bada  ya kuhisi uongo wa Hamza.

“Ndio  , umejuaje?”Aliongea Hamza huku akicheka.

“Unadhani mimi  ni  mjinga , kama unataka kuniongopea  angalau tunga uongo mzuri”Aliongea .

“Kwasababu unaonekana kunijua vizuri unaonaje tukiachana na hilo , si  kikubwa ni bibi   yetu kutibiwa”

“Ni bibi yangu sio  wetu”

“Haha..  haijalishi  ni kweli au hapana , lakini mbele ya macho ya watu sisi ni wapenzi hivyo ni bibi yetu”Aliongea  na   kumfanya Regina kuvuta mdomo.

******

Upande mwingine  usiku huo huo katika moja ya Club   maarufu iliokuwa kipatikana Mbezi mwisho  , ifahamikayo kwa jina la Nipe tano pub  alionekana Kanali Dastani akiwa katika  chumba binafsi amekaa kivivu kwenye masofa , mbele yake kulikuwa na  chumba za Whiskey  mbili moja ikiwa imeisha nyingine ikiwa nusu , ikionyesha  alikuwa hapo muda mrefu kidogo.

Alionekana kuwa siriasi kidogo na  alikuwa akiangalia  saa yake  mara kwa mara kana kwamba kuna mtu aliekuwa akimsubiria.

Zilipita dakika kama  tano hivi simu yake ilianza kuita  na alichukua haraka na kupokea. “Niambie taarifa nzuri  Afande?”

“Dastani  mpango umekwama , sijui nini kilichotokea lakini hakuna  madhara yaliowapata walengwa , Bunji amekutwa eneo la tukio akiwa  hana  uhai”Sauti iliongea  na   jibu lile lilimfanya Kanali uso wake  kujikunja  na alimimina  Whiskey kwenye glasi na kupeleka  yote mdomoni.

“Sagenti , nilikuambia  unitafutie kijana anaejiua kazi , ila umetafuta mtu wa kujitoa muhanga?”

“Tajiri,  Bunji ndio  mfungwa ambae  alikidhi vigezo vyote ulivyohitaji  na nimeshangaa kusikia amepoteza uhai kwa  kujimaliza  , hii sio kazi yake ya kwanza kufanya”Sauti upande wa pili ilijitetea na kumfanya  Kanali  kufikiria kidogo.

“Hakikisha swala la Bunji linabakia kuwa siri , isitokee  minong’ono kwa wafungwa wengine  na ikaleta ukakasi”

“Tahadhari nimezichukua , kuhusu  hilo usiwaze kabisa..”Sauti ilisikika na kumfanya  Kanali kupumua.

“Malipo yako  yataingizwa kama kawaida”

“Bosi  kuna taarifa nyingine   nadhani napaswa kuiripoti kwako  nadhani  ni taarifa ya kukufanya    uniongezee ongezee , uchumi mgumu bila kujiongeza mambo  hayaendi”

“Mchuku  huwezi kunipatia hio ripoti  mpaka  uhusishe hela?”

“Sio kama  napenda kuhusisha fedha  Bosi ,  unajua kabisa mjengo wangu upo hatua za mwisho  na mama watoto  amechoka kukaa Kota za Magereza” Sauti iliongea na kumfanya Kanali kutoa tabasamu  la kejeli.

“Nipe hint , nikiona  inanifaaa nitakuongezea  kitu”

“Ni kuhusu  yule Mfungwa wa Kimexico , Ninja wa kundi la Dragon tooth, nadhani bosi unajua hii kesi ilivyokuwa siri,  kukuambia hivi   nahatarisha kibarua changu  cha ukuu  wa gereza”

Kanali mara baada ya kusikia sauti hio palepale akili yake ilicheza  mfungwa , kesi ya mfungwa hio  ilikuwa siri, ndio mtu ambae alihusika katika mauaji ya  jasusi wa  kitengo cha usalama wa taifa , jasusi muadilifu Sedekia Kunembe  ambae alipewa  misheni ya kufuatilia  tukio  la radi  mkoani Rukwa miaka kadhaa iliopita.

“Ngapi unataka niongeze?”Aliongea  Kanali huku aking’ata meno  kwa hasira, maada Afande Mchuku alikuwa akijua kumtoa hela  sana , ni hivyo tu   alikuwa ni  wa faida ndio maana alimpatia.

“Milioni sita  tu  bosi wangu ,  kama nilivyosema  hii ripoti  inakufikia wewe kabla ya kitengo cha TISA walioniambia nitoe  ripoti  kwa kila kinachoendelea kwa yule mfungwa”

“Nitaongeza nne kamili nielezee”Aliongea Kanali na upande wa pili  ulinyamaza kidogo.

“Kuna  wazungu wanne  wamefika leo kumtembelea”Aliongea na kumfanya  Kanali macho yake kuchanua kidogo.

“Wazungu , nilidhani  ni  mfungwa ambae hapaswi kuruhusiwa kuonana na mtu yoyote wa nje?”

“Ilikuwa ngumu kuwakatalia , walikuwa na kibali kutoka kwa Lughalila”

“Unamaanisha Waziri ndio ambae ameruhusu?!”

“Ndio maana nikaona  hii ni habari ambayo inaweza kunipa  posho  ikianza kukufikia wewe?”

“Kitu  gani wameongea  , umeweza kujua  walichoongea”

“Kuhusu hilo Kanali  sijajua , ila wametumia ofisi yangu   kufanyia maongezi yao”Aliongea Mchuku na kumfanya  Kanali kutamani kutoa  tusi kwa mtego wa Mchuku.

“Mchuku acha kuzunguka zunguka , najua ofisi yako haijawahi kuwa sehemu salama ya kufanyia maongezi”

“Hehe… Kanali  nilichofanya ni kukupa taarifa tu , kuhusu walichoongea sidhani  napaswa kukwambia kila kitu , kama nilivyosema hili swala linaweza kuniingiza kwenye matatizo”

Kanali Dastani aliishia kugugumia Whiskey , katika maisha yake hajawahi kukutana na mtu ambae anajua kufanya biashara  kihuni kama  Mchuku , wakati wakiwa katika mafunzo ya  upolisi  hakuelewa kwanini Mchuku alichagua uelekeo wa Magereza na  kukataa kuwa polisi wa kawaida, kumbe kwake aliona fursa  gerezani  na  kweli fursa alikuwa akiitumia vizuri.

“Mchuku nataka kujua kila kitu walichoongea, ni muhimu kwangu, nitalipa kiasi chochote unachotaka”

“Kanali kama nilivyosema  ilikuwa ngumu kwangu  kusikia wanachoongea , isitoshe  walikuwa wakitumia Lugha  nisioijua?”

“Umeweza  kujua walikuwa wakitumia  lugha  usioijuas , halafu unasema ilikuwa ngumu kujua wanachoongea , unaonaje  nikikupatia  pesa ya kumaliza nyumba yako moja kwa moja  na kumaliza mkopo wako wa benki?”

“Tajiri   tutaongea kesho, nikishafikiria vizuri”

“Nyumba , mkopo benki  na lile gari la ndoto zako, unaonaje?”Aliongea  Kanali , alijua kabisa Mchuku sio mtu wa kufikiria fikiria , akikwambia ngoja afikirie  ujue hajaridhika na malipo.

“Hela ya  malipo ya  Bunji  na ripoti ya kukuelezea hii issue  yanajitegemea”

“Sawa , niambie  sasa, je umeweza kujua wanachoongea?”

“Kama nilivyosema walikuwa wakitumia ligha nisioijua , ila  nimerekodi maongezi yao yote”Aliongea  Mchuku  na kumfanya Afande kutoa tabasamu, japo alikuwa na wasiwasi  maongezi hayo yanaweza yasmpe anachokitaka , lakini alikuwa tayari  kulipa , isitoshe hela hizo hazikuwa zikitoka kwenye mifuko yake.

Baada ya kukubaliana na Mchuku siku inayofuata waonane kwa ajili ya  makabidhiano , Kanali aliitafuta namba   ambayo alikuwa ameisave  kama Tajiri  na kisha akaipiga.

“Madam!!,”Aliongea Kanali  mara  tu baada ya simu kupokelewa.

“Salama Madam , nimepata  dalili ya muongozo , ila upande wa pili unahitaji  motisha….”

“Oh sawa , Madam  namba ni  ileile , ndio, kesho nikipata lolote nitakurudia, Asante sana  nahakikisha  hili swala tunalijua ki undani kabisa”Aliongea Kanali   na muda uleule simu ilikatwa, haikueleweka  aliekuwa akiongea ni nani.

Muda huo huo mara baada ya simu kukatwa mlango wa chumba hiko  ulifunguliwa  na  mara baada ya Kanali kugeuka alijikuta akitabasamu , alikuwa ni mrembo Tresha Noah ambae alikuwa amevaa akapendeza , alikuwa amevaa kimtego na kumfanya Kanali kumeza mate mengi.

Kitendo cha  Tresha kuingia  moja kwa moja alimvamia  Kanali na busu  zito la  mdomoni ,  haikuhitaji kuambiwa kinachoendelea , ilionekana wawili hao walikuwa  wapenzi  wa siri.

Chumba kinachofuata alikuwepo  Jausi Mstaafu mzee

Amosi  akiwa amekaa huku  akiwa  amevaa

Headphone,  alikuwa ameshikilia simu janja mkononi na alikuwa ameikazia macho na kumfanya  kutabasamu.

“Hii kitaalamu inaitwa kupiga ndege  wawili kwa jiwe moja , Dastani mwisho wa siku na wewe ni binadamu tu ambae unafanya makosa”Aliongea  na  bila ya kuchelewa  alitoa maburungutu mawili ya  hela na kuyeka juu ya meza na kisha alitoka ndani ya chumba hicho na kutokomea akiwa  na tabasamu usoni.

“Kazi yangu ya kwanza ni kumuwahi Mchuku kabla ya Dastani , lazima  ni swala linalohusiana na  hii  misheni ya mwanamke”Aliwaza Amosi  na alijikuta akiona mpango wake wa kuja  katika Pub hio haukuwa mbaya kabisa.

Amosi  alikubali  Dastani amemzidi vitu vingi likija swala la ujaususi wa ki uchunguzi na kuliona hilo , siku  nzima alikuwa akimfuatilia nyuma nyuma  ili kujua kila ambacho anafanya  na mazungumzo yake yalivyo na mpango wake ulimlipa.

Previoua Next