SEHEMU YA 42.
“Mchomeni mchawi huyo , Aderon kutoka Cathedral anakwenda kuchoma mchawi”
“Burn that damn witch to ashes”
Woga na mshituko uliweza kumshika kwa kusikia lugha ya kingereza ambayo waongeaji wake lafudhi zao zilimchanganya.
Swali lilimvaa pale na kujiuliza yupo wapi , ni ulimwengu gani ambao mchungaji anashiriki kumchoma mchawi moto.
Hamza aliweza kuhisi kabisa kuna kitu hakipo sawa na kuna jambo kubwa ambalo anakwenda kushuhudia , lakini mawazo yake yalikata mara baada ya kishindo kusikika kutoka katika mlango wa kuingilia katika chumba ambacho yupo.
Dakika ileile aliweza kuona mlango ukifunguliwa na akaingia kijana mzungu kabisa wa miaka kama kumi na tatu hivi.
“Luther !!” Yule kijana mdogo mwenye nywele zake za rangi ya kahawia aliita , alikuwa amevalia nguo za kitani ambazo zimemfika magotini na alikwenda kusimama kandokado ya kitanda alichokuwa amelala Hamza huku akimwangalia kwa macho ya mshangao.
“You’re awake , thanks God”
Hamza alijikuta akimwangalia yule mvulana wa kizungu namna mavazi yake yalivyo na aliishia kutingisha kichwa bila ya kujielewa.
“Luther , Mchawi , Cathedral , kuchoma mchawi”Mawazo hayo yalianza kupita katika kichwa cha Hamza na kujiuliza yupo wapi na amefikaje , ilikuwa ni kama vile anaangalia filamu zilizoigizwa kwa kuiga mazingira kati ya Karne ya tano mpaka kumi na tano maarufu kama Middle ages ndani ya bara la Ulaya , kipindi ambacho kulikuwa na matukio makubwa ya kuwinda wachawi na kuwaua.
Rangi ya kijana aliekuwa mbele yake na mavazi yake , ilikuwa ni ushahidi tosha wa kile ambacho anakiwazia
Yule kijana mdogo mzungu ambae alikuwa na uchafu mweusi kwenye paji la uso wake alionyesha kuwa na furaha kubwa.
“Mama hakuniamini na kuendelea kulia usiku wa manane kila mtu akiwa amelala huku akitaja jina lako kana kwamba ushakufa na kuzikwa tayari, baba hakujua cha kufanya na aliamua kumtuma Simoni kwenda kwa Lord Venn, akiomba kaka kurudi nyumbani , sasa hivi amekuwa Knight(mwanajeshi), mbele ya kaka yule daktari asingekataa kukutibia , lakini ona sasa juhudi hazikuwa za bure hatimae umeamka , nilijua tu huwezi kufa”Yule kijana aliongea kwa sauti huku akionyesha ni kwa kiasi gani ana furaha na baada ya sentensi hio alimshika Hamza mkono.
“Hebu twende nje kwanza, wanaenda kumchoma yule mchawi aliesababisha uende jela na kuhojiwa usiku kucha na walinzi wa kanisa”
Hamza hakujua kinachoendelea , kijana aliekuwa mbele yake hakuwa akimfahamu na wala hakujua eneo alipo , alihitaji muda wa kufikiria amefikaje hapo na sio kwenda nje.
“Huyo mchawi anahusiana vipi na mimi?”Swali liliingia katika akili ya Hamza na alijikuta akibadili mawazo palepale na alimshikilia mkono yule mzungu na akajikokota kutoka nje.
Hamza mara baada ya kutoka alijikuta akiangalia mazingira na watu wake na alijikuta akipagawa , watu wote walikuwa wamevaa mavasi staili inayofanana , nguo za kitani za mikono mirefu , ukiachana na hali ya joto lakini mazingira yalikuwa tofauti kabisa.
Karibia watu wote alioona walikuwa ni wazungu na nywele zao ni za rangi ya kahawia , walikuwa wamevaa viatu ambavyo havikuwa na visigino , wanawake walikuwa wamevaa magauni ambayo yalikuwa na mifuko mirefu mno.
“Hizi ni zama za kale ndani ya Ulaya?”Alijiuliza Hamza na sasa wakati huo ndio alianza kujichunguza mwili wake , alijishangaa baada ya kujiona anafanana kila kitu na watu wale , kilichompagawisha hakuwa na muonekano wake wa Hamza aliokuwa nao , bali alikuwa ni mzungu kamili ambae hajachanganya rangi , huku akiwa na mavazi kama ya wale wengine tu.
Nyumba zilizokuwepo zilikuwa ni zile ambazo zlikuwa akiziona ni za hali ya chini , mara nyingi ungeziona katika bara la Afrika , vilikuwa ni vijumba vingi vilivyojipanga.
Baada ya kutokezea nje kabisa hatimae aliweza kuona jengo kubwa ambalo lilikuwa mbele yake , ambalo paa lake lilikuwa limeenda hewani na kuchongoka kama mkuki huku katika ncha yake kukiwa na Msalaba wa rangi nyeupe , vidirisha vya kanisa hivyo vilikuwa vyembamba mno.
Watu wengi walikuwa wamejikusanya mbele ya uwanja wa kanisa hilo , Hamza alikuwa hajui kinachoendelea na alikuwa akionekana mshamba mshamba na alichofanya ni kumfuata yule kijana mdogo wa kizungu , Hamza alimuiga yule kijana kwa kusukuma watu pembeni na kujipenyeza ili kupita mbele kabisa katika kundi la watu hao na vitendo vyao viliwafanya watu kukasirika na kuwaangalia kwa macho makali.
Hatimae Hamza aliweza kuona mbele kabisa ya eneo hilo , walikuwa wamefika mbele ya kundi lile la watu.
Katikati ya sehemu ambayo ilikuwa ni kama steji ya kanisa alionekana mwanamke mrembo wa kizungu ambae amevalia nguo mfano wa kaniki nyeusi , alikuwa amefungwa kwenye msalaba kwanzia mikono yake na watu walikuwa wakimtupia mawe na vipande vya kunni huku wakiongea kwa nguvu kutaka mwanamke huyo kuchomwa moto.
“Go to hell!! Damned witch”(Nenda kuzimu wewe mchawi mpumbavu)
“You wanted everyone in Aderon to die(Ulitaka kila mtu ndani ya Aderon kufa).
“Jamani Tracy , amekufa mwezi mmoja uliopita , lazima umemua wewe shetani”
Mwanamke yule ambae alikuwa katika joho la rangi nyeusi alikuwa akipokea kila lawama pamoja na kurushiwa kila kilichowezekana kurushwa , lakini jambo la ajabu , yule mwanamke alikuwa amemkazia macho Hamza pekee , ilikuwa ni kama alikuwa akimtambua na hali ile ilimfanya Hamza kuwa na wasiwasi , ngozi yake haikuwa tofauti na wale wazungu , lakini kwanini mwanamke yule alikuwa akimwangalia kwa kumkazia macho , tena kila alipokuwa akipokgea pigo na kugeuzwa uso wake pembeni aligeuza na kumwangalia Hamza kwa macho yaliojaa ujumbe.
Watu hawakujiuliza alikuwa akiangalia wapi , ni Hamza pekee ambae alikuwa akipata hisia mwanamke yule alikuwa akimwangalia yeye.
Pembeni ya mwanamke huyo alikuwa amesimama mwanaume wa makamo , alikuwa amevalia joho la rangi nyeupe ambalo lilikuwa limedariziwa na michoro ya aina yake , kichwani alikuwa amevalia kofia aina ya bereti , huku mkononi akiwa ameshikilia msalaba , alionekana kuwa kimya muda wote , akiwa na hali ya kumakinika na heshima , kulikuwa na wanawake na wanaume ambao walikuwa nyuma yake wote pia walikuwa wamevalia majoho ya rangi nyeupe , walikuwa na sura angavu na zenye kudhihilisha hadhi yao .
Kulikuwa na walinzi pia ambao walikuwa wameshikilia mikuki kama wale wanajeshi wa Crusaders , wapigania dini ya kikristo.
Mwanaume yule wa makamo aliangalia saa yake ya mfukoni na kisha alipiga hatua kusogea mbele na kisha akainua bango ndogo ya mviringo na ghafla tu wale watu wote waliokuwa wakipiga makelele walinyamaza.
Hamza bado alikuwa amekutanisha macho ya yule mwanamke muda wote, huku mapigo yake ya moyo yakienda mbio.
Kitendo kile cha utii wa ghafla mbele ya yule mwanaume alieonekana kama mchungaji ilimfanya Hamza kushangaa lakini pia kuona namna watu hao walivyokuwa watiifu, na palepale swali lilimwingia na kujiuliza huyo mwanaume ana mamlaka gani kiasi cha kutuliza watu wote hao kwa kunyanyua tu lile bango iliokuwa kwenye mkono wake.
Yule mwanaume mara baada ya watu kutulia alianza kuongea kwa sauti ya kupenya katika kila ngoma za masikio ya kila mmoja
“Ewe Mkosefu uliejaa dhambi , umedanganywa na shetani, tamaa ikakuvaa na kuufanya mwili wako na
nafsi yako kujaa ufisadi , ni nuru pekee itakayokusafisha , ni hukumu yako lakini vilevile ni rehema za mwenyezi Mungu”
“Burn her , Burn her !!”Watu walianza kupiga mayowe huku wakiinua mikono yao juu wakitaka yule mwanamke kuchomwa moto.
Sauti hizo za watu kukemewa mwanamke huyo kuchomwa moto na namna ambavyo yule mwanamke alievyokuwa akimwangalia kwa kumkazia macho ilimfanya Hamza kujawa na hofu na kuona pengine yule mwanamke anaweza kumjumuisha kama mshirika wake na wakachomwa wote.
“Kabla ya kivuli cha nuru hakijawa juu yako , ungama dhambi zako , toba ya kweli inaweza kuokoa roho yako , ndipo roho yako itapaa mbinguni anapoishi Mungu”Aliongea yule Askofu.
Yule mwanamke ghafla tu alianza kucheka kwa sauti kubwa , sauti yake ilikuwa na nguvu kiasi kwamba ilikuwa ikitisha na alianza kuongea kwa nguvu.
“Ninachotafuta na kuamini ni nguvu halisi ya uchawi , si nguvu ya kimungu , nichome tu , Nitazishuhudia mbingu za Mungu wako zikiharibika na kanisa lako likiungua kwa miale ya moto”Aliongea na kuonyesha tabasamu huku akimwangalia Hamza.
“Kichaa huyo”
“Ana wazimu”
“Amechanganyikiwa”
“Amemlaani Askofu , wachawi wote na wauwawe wakifuatiwa na majini”
“Achomwe mpaka awe majivu”
Yule askofu alionekana kuwa kimya , lakini makelele ya watu yalizidi kusikika zaidi na zaidi , chuki katika sauti za watu hao ndio ambacho Hamza aliweza kusikia.
“Kwanini nipo hapa , nafanya nini?”
Hamza alitamani kwenda kumuokoa yule mwanamke , ni kama kuangaliwa na yule mwanamke alikuwa akiomba msaada , lakini kundi hilo la watu wengi aliona kabisa ni kitendo ambacho hawezi , swala lingine hakujua kama alikuwa na uwezo huo, maana mwili wake ulikuwa umebadilika.
Swali palepale liliingia katika akili ya Hamza na kujiuliza , wanakwenda kumchoma vipi ilihali hakukuwa na kuni zaidi ya mwanamke yule kufungwa juu ya msalaba.
Yule askofu alianza kuomba kwa nguvu na kadri alivyokuwa akiendelea ni kama sauti yake ilikuwa ikibadilika kutoka katika hali ya kubembeleza na kuwa ya kikauzu.
“Wewe mchawi , binadamu mkosefu mbele za Mungu sehemu yako ni Kuzimu, na nakupeleka huko kwa nguvu ya Nuru”Aliongea vile na ghafla tu ule msalaba aliokuwa ameshikilia ulitoa mwanga mkali kama vile ni wa radi , ulikuwa mkali kiasi kwamba Hamza alishindwa kuuangalia.
Ilikuwa ni kama vile Askofu yule alikuwa ameshikiria jua dogo katika mkono wake , mwanga ule ulikuwa msafi na wa kutisha wenye msisimko wa ajabu , watu wote katika lile kundi pamoja na yule kijana ambae alimwita Hamza kwa jina la Luther waliinamisha vichwa vyao chini kwa heshima.
Yule mchawi alianza kuongea kwa nguvu kana kwamba anaimba ushairi kwa lugha ya kingereza.
“In the blazes I will see your shrewd paradise demolished”(Katika miale ya moto nitashuhudia patadiso yako iliojaa hila ikiharibika)
“In the blazes I will see your fabulous house of God Crumbling”(Katika miale ya moto nitashuhudia nyumba kubwa ya Mungu wako ikidondoka)
“In the Blazes , I will see your indiduals evelastingly worsened”(Katika miale ya moto nitashuhudia watu wako wakiteseka milele)
Alizidi kuongea maneno mengi kwa kurudia rudia sehemu ya mwanzo na kumalizia tofauti mwishoni , huku ule mwanga ukizidi kumuunguza.
“Hapana hapa sio duniani , huu ni ulimwengu mwingine , mimi sio Hamza , mimi ni Luthe…”
Ilikuwa ni kama vile kuna mtu aliemsukuma na kudondoka chini , Hamza alijikuta akishituka huku akihema kwa nguvu , jasho jingi lilikuwa likimtoka usoni.
Alijikuta akikimbilia taa na kuiwasha haraka haraka na kuangaza huku na huko , alijikagua mikono yake na kujiona ni yeye Hamza mzungu wa kuchnganya rangi au Shombeshombe.
Katika maisha yake hakuwahi kukumbwa na hali ya namna hio , alijikuta akihema kwa nguvu kwa namna ya ahueni.
“Afadhali ilikuwa ndoto”Aliongea Hamza huku akikaa kitandani na aligundua alikuwa ameloanisha shuka kwa jasho, lakini muda huo kadri akili yake ilivyokuwa ikikubaliana kwamba alichokuwa akiota ni ndoto hali nyingine ilimuanza , haikuwa hali ilikuwa ni harufu ambayo ilianza kugusana na pua zake.
“Haya marashi yanatokea wapi?”Hamza alijikuta akishangaa , chumba kizima kilikuwa kimebadilika harufu, haikuwa marashi kama marashi ni harufu ambayo haikuwa ikielezeka yenye kuvutia na kukera kwa wakati mmoja, ilikuwa ikipenyeza kwenye pua zake kama vile ni udi.
Hamza alijikuta akiangaza kulia na kushoto kutafuta marashi yalipokuwa yakitokea na mara baada ya kuangalia kwenye bedside ya kitanda chake alijikuta akishangaa.
“Huu mshumaa nani ameuchomeka kwenye umeme?”
Ndio swali ambalo lilimvaa Hamza palepale, huku asiamini kilichokuwa mbele yake , alikuwa akikumbuka kabisa mara ya mwisho mshumaa huo ulikuwa kwenye boksi lake na alihifadhi katika kabati sehemu ambayo aliona ni salama , lakini cha kushangaza ulikuwa kwenye Bedside tena ukiwa umechomekwa kwenye umeme.
Hamza sasa ni kama anapata mwanga wa kile ambacho kilikuwa kikiendelea , pengine harufu hio pamoja na ndoto ya ajabu aliokuwa ameota imetokana na mshumaa huo kuwa katika umeme.
Hamza alikumbuka wakati wa Frida anampatia huo mshumaa alimwambia auchomeke kwenye umeme kati ya saa tano mpaka sita , Hamza mara baada ya kukumbuka jambo hilo alikimbilia simu yake ili kuangalia saa na ile anawasha tu ile simu kilichoanza kuonekana katika macho yake ni ujumbe wa meseji, ambao ulifanya mapigo yake ya moo kwenda mbio.
“Mzee!!”
Ndio neno la kwanza ambalo alianza kulitamka katika mdomo wake huku hofu ikimvaa.
Hamza kwa haraka haraka alifungua ule ujumbe na aliweza kuusoma kwa hofu kubwa , ulikuwa umeandikwa kwa kingereza.
“The history of your past life in onother world has already begun to echo , if you fail to inherit your history , it will be the end of your life in this world,
Your greatest enemy has already awakened” “Historia ya maisha yako ya nyuma katika ulimwengu mwingine imeanza kuita, kama utashindwa kurithi historia yako , itakuwa ni mwisho wa uhai wako katika huu ulimwengu , adui yako mkubwa amekwisha kuamka”
Hamza alijikuta akisoma ujumbe ule kwa kurudia rudia , hakuwa akielewa sentensi nzima ya ujumbe huo ilikuwa ikimaanisha nini , hakuelewa nini maana ya adui yake , kila kitu kilikuwa kipya kwake na alitamani maelezo , alishangaa pia kuona mtu ambae ametuma ujumbe huo ni Mzee na jambo hilo lilimfanya kupagawa zaidi.
Usingizi wote ulimpotea , alikuwa ni jasiri lakini likija swala la Mzee Hamza alikuwa dhaifu sana , sio kwamba alikuwa akimuogopa lakini ni kwamba hakujua Mzee ni adui yake au ni rafiki kwake na mbaya zaidi hakuwahi kumuona na ghafla tu anaota ndoto ya ajabu .
Hamza alikaa akianza kuwaza hisia zilimwambia pengine ni huyo mzee ambae ameweka mshumaa huo kwenye umeme. Hisia mbaya zilimvaa , kifaa hicho kisingejichomeka chenyewe , lazima kuna mtu alikichomeka.
“Kwahio Mzee alikuwa hapa, inawezekana vipi?”
Hamza aliamka kutoka kitandani na alijaribu kufungua mlango wa chumba chake na ulionekana kuwa wazi , lakini hakushangaa maana ilikuwa tabia yake kuacha mlango wazi , alijikuta akikosa namna ya kujitengenezea sababu ya kuamini mzee alikuwa hapo , sio madiirsha ya kutokea kwenye balkoni na sio mlango kila kitu aliacha wazi wakati wa kulala.
Hamza hakutaka kuwazia sana kuhusu Mzee kufika hapo au kutokufika, ukweli ni kwamba sio mara ya kwanza kutokewa na tukio la namna hio , anakumbuka siku ambayo alikaidi maagizo ya Mzee na hali iliomkuta ilimfanya kuitikia kila kitu ambacho alikuwa akiagizwa na mzee licha ya mtu huyo kutokumuona kabisa wala kumtambua.
Usiku Mzima Hamza aliwaza jambo ambalo lilimpata , alijikuta akiwaza ndoto aliona na maana ya maneno katika ujumbe ule na alijikuta akiona pengine historia ambayo Mzee anamaanisha ni kuhusiana na kile alichoota , isitoshe sio mara ya kwanza, hata Frida kabla ya kumpatia huo mshumaa alimuuliza kama ashaanza kuota ndoto.
Mpaka kunakucha Hamza hakuweza kupata usingizi tena , baada ya saa kumi na moja kufika ili kupotezea mawazo yaliokuwa yakimwandama alitoka mpaka nje na kuanza kuchukua mazoezi kwa kasi sana , siku hio alianza kucheza ule mdundiko kama hana akili nzuri.
Mbinu hio ya mazoezi kwa mtu mtaalamu angeweza kuifahamu kwa jina lake maarufu la Mdundiko wa jini.
Kadri ambavyo alikuwa akicheza ndio alivyoweza kuifanya akili yake kutulia na mawazo kumpotea , mpaka inafika saa moja hatimae alihisi kurudi kwenye ari yake.
Upande wa Regina mara baada tu ya kuamka alimwambia Hamza kuongea na Dokta kwani siku hio haendi kabisa kazini ili kushughulikia swala la bibi yake na Hamza hakubisha , alimpigia Flora simu na kumuomba na hakukataa kabisa , jambo ambalo lilimfanya Regina kuzidi kushangaa zaidi na kujiuliza mengi kuhusu Hamza, lakini hakukuwa na namna ya kupata majibu kwani Hamza alikuwa akiishia kumdanganya.
Licha ya Regina kutokwenda kazini Hamza alipaswa kwenda lakini aliona uvivu kwani kazini hata Eliza pia siku hio hakuwa na ratiba ya kwenda kutokana na daktari kwenda nyumbani kwao kumtibia mama yake.
Hamza ilibidi kutoka na gari nyingine kabisa BMW X7 ya 2022 na hayo yalikuwa maelekezo ya Regina ambae alitaka kutumia ile Lexus.
Hamza akiwa ndio anakaribia kutoka nje tu ya geti kuelekea kazini simu yake ilianza kuita mfululizo na alipoangalia anaepiga ilikuwa ni namba mpya na alipokea palepale huku akisimamisha gari kwanza.
“Hello!!”
“Wewe baba ninaekudai habari za asubuhi”Sauti upande wa pili ilisikika , ilikuwa ni sauti tamu kweli na kumfanya Hamza kuitambua mara moja , ijapokuwa aliisikia kama mara moja au mara mbili hivi lakini haikusahaulika.
“Prisila!!”
“Eh! wewe mwanaume hujasahau sauti yangu?” “Nasahau vipi sauti ya mrembo kama wewe , niambie kuna shida ndio naelekea kazini?”
“Najua ndio ni muda wa kazi , lakini kwasababu nakudia naweza kupiga muda wowote, au umesahau una deni langu?”Prisila aliongea na kumfanya Hamza kutoa tabasamu.
“Nakumbuka na nipo tayari ya kulipa ila sio sasa hivi?”
“Hakuna haja ya kujikaza , mimi najua kudai kistaarabu, ili kulipa, baadae tukutane?”
“Tukutane!, unamaanisha nini tukutane?”
“Namaanisha tukutane , kuna kipi cha kushangaa hapo?”
Hamza mara baada ya kusikia sauti hio ilivyokuwa siriasi aliishia kujiuliza huyu mwaamke mbona amekaa kibabe sana , hata hajamuuliza kama ana ratiba gani lakini anataka wakutane.
“Namaanisha hatuna sababu ya kukutana maana hatuna mahusiano , au usiniambie ndio unataka yaanze?”Aliongea na upande wa pili ulitulia kidogo. “Kuna kitu nataka tufanye pamoja baadae , sitaki kumuomba mtu msaada wewe nakudai hivyo ni sawa kukuambia tuonane muda huo , kama haupo tayari kulipa deni langu sitokulazimisha”Hamza hakujua alie au acheke ila aliona tu akubali kwasabau alikuwa akidaiwa fadhila.
“Okey nipo tayari kufanya hicho kitu pamoja hapo baadae , niambie tu muda na eneo”
“Nitakutumia ujumbe kwa meseji”Aliongea na simu palepale ilikatwa, Hamza aliona ilikuwa ikileta maana Prisila alizisikia habari zake juu juu , wakati akiwa kazini alikuwa pia ni mwanamke siriasi sana ambae anajua anachokitaka.
“Kampuni ya Dosam imejaa wanawake vichaa tu kasoro Eliza”Aliwaza Hamza na kuondosha gari haraka. Kuelekea kazini.
Comments