SEHEMU YA 43.
Hamza aliwahi kutoka kazini kuliko kawaida ili kuwahi miadi na Prisila , mrembo huyo alikuwa ameshamtaarifu ni wapi amkute hivyo alisogea mpaka Mlimani City na ndani ya dakika tano tu kupita Prisila alitokea , siku hio alikuwa akitumia gari nyingine kabisa aina ya Bentley.
“Inaonekana ni kama nilivyotarajia , unajali muda “Aliongea Prisila huku akimwangalia Hamza na kuonyesha ishara ya kuridhika.
“Umependeza mno Prisila , unaonekana kama wale warembo ma’model’ maarufu?”.Aliongea Hamza na kumfanya Prisila kutabasamu. “Halafu hili gauni nimelinunua muda mrefu sana , lakini sijawahi kupata ujasiri wa kulivaa”Aliongea akiwa na tabasamu.
“Kwanini umepata huo ujasiri leo , kwangu mimi uzuri wako naona hautokani na mavazi”Aliongea.
“Nimepata ujasiri wa kuvaa hivi kwasababu nipo na wewe mbele ya Classmate wangu wa kitambo ”Aliongea na kumfanya Hamza kushangaa.
“Unamaanisha nini?”
“Namaanisha leo unakwenda kuigiza kuwa boyfriend wangu mbele ya wanadarasa zangu wangu wa Highschool , tuna Reunion leo na nimewaambia nina boyfriend”Aliongea Prisila akiwa siriasi , hakuwa hata na aibu kuongea hayo maneno na ndio kitu kilichomshangaza zaidi Hamza.
“Mwanamke mrembo kama wewe unakosaje mpenzi au ndio unapanga kuniingiza kwenye matatizo?”Aliuliza Hamza , aliona haya maswala ya kufanywa boyfriend feki na kila mtu yanaanza kumchosha , swala la kujiingiza kwa Regina lishaanza kumuumiza kichwa kuhusu usalama wake,lakini tena Prisila anamwingiza.
“Ndio ujue sina ,ndio maana upo hapa , kama ningekuwa nae ningehangaika vyote hivi , kabla sijaondoa gari fanya maamuzi hapa hapa, je upo tayari kuigiza kuwa bofriend wangu kwa leo tu?”Aliuliza na kumfanya Hamza kuanza kukuna kichwa.
“Sikia Prisila mimi kazi yangu sio kuigiza kuwa boyfriend feki , nina mpenzi tayari, kwa urembo wako sidhani kama unaweza kukosa mtu ambae anaweza kufanya unachotaka , nipo tayari kulipa fadhila ila sio kwa njia hii”Aliongea Hamza na palepale alifungua mlango wa gari kutoka.
“Huyo mpenzi wako anajua unaigiza kuwa mpenzi wa Regina?”Aliuliza na kumfanya Hamza kusita kwanza na kumgeukia.
“Kwahio kwasababu bosi wako ameniajiri kuwa mpenzi feki na wewe unataka kufanya hivyo, haiwezekani kwa kila mtu , nilichokifanya kwa bosi wako ni shauku ilionifikisha hapa , lakini sio kurudia tena kwa mtu mwingine, kuhusu mpenzi wangu kujua ama kutokujua hili ni swala ambalo lipo juu yangu, nadhani unajua siwezi kuendelea kuwa na bosi wako kwa muda mrefu”Aliongea Hamza.
Prisila alijikuta aking’ata meno , aliamini ingekuwa rahisi kwa mwanamke mrembo kama yeye kukubaliwa na Hamza hata kimaigizo tu, lakini mawazo yake yalikuwa tofauti kabisa , Hamza anamkatalia tena akiwa siriasi kabisa.
Upande wa Hamza mara baada ya kuona mwanamke huyo anawaza ndio aliona ni muda wa kuondoka na alishuka kwenye gari na kuanza kupiga hatua akitaka kuvuka barabara kurudi kwenye kampuni maana hakufika hapo na gari.
Prisila alijikuta akifumba macho kwa dakika kadhaa na kisha alifungua mlango haraka na kutoka. “Hamza wait!!!”
Aliita akimaanisha Hamza amsubiri na Hamza ambae tayari alikuwa ashaanza kupiga hatua kuvuka barabara alisimama akimsubiria.
Ijapokuwa alimkatalia mrembo huyo lakini mara baada ya kushuka kwenye gari muonekano wake ulizidi kumfanya kuonekana mrembo , Prisila alikuwa mwanamke mzuri sana pengine alikuwa akishika nafasi ya pili baada ya Regina.
Hata watu waliokuwa karibu na eneo hilo walimkodolea macho na kwa jinsi ambavyo alimwita Hamza ni kama ilidhidhirisha kuna kitu kinachoendelea baina yao.
Prisila alikaza mwendo na kumsogelea Hamza , awamu hio alikuwa mpole kuliko mwanzo.
“Hakuna namna unaweza kunibadilisha mawazo”Aliongea Hamza.
“Unakumbuka asubuhi ulichosema kwenye simu , upo tayari kufanya hicho kitu baadae , hii ni ahadi umeweka, kosa lako ni kutokuuliza , kwanini
unanikatalia sasa hivi ilihali sina mbadala?”Aliongea.
“Na wewe kosa lako ni kuamini naweza kukubali kila utakachoniambia na nifanye, hata kama ni kujishusha thamani na kukubali ombi lako”Aliongea Hamza akiwa na uso usiokuwa na hisia zozote. Lakini kauli yake ilimfanya Prisila kushangaa na kujikuta akisugua meno, ilikuwa ni dhahiri alitaka kusema yaani mwanamke mrembo kama yeye kuigiza nae kuwa mpenzi ni kujishusha thamani.
“Basi naomba unisindikize , sina chaguo lingine, nitakutambulisha kama rafiki yangu wa kawaida tu”Aliongea katika hali ya kujishusha , lakini kilichomshangaza ni baada ya kuona Hamza anacheka.
“Unacheka nini .. umekubali au?”Aliuliza .
“Ukweli ni kwamba nilikuwa nishakubali tokea asubuhi , katika kitabu changu cha kumbukumbu sijawahi kushindwa kulipa deni hata liwe kubwa vipi?”Aliongea na palepale alimpa mkono Prisila ambae alikuwa akimshangaa, alipokea kiwasiwasi na wakaanza kupiga hatua kuelekea kwenye gari na awamu hio Hamza hakumwingiza upande wa
dereva bali alimzungusha kwenye siti ya abiria na mara baada ya kumfungulia mlango aliingia ndani.
“Kama ulikuwa umenikubalia kwanini ulikuwa ukinizungusha , ulikuwa unanijaribu?”
“Huwezi kusema nilikuwa nikikujaribu , unaonekana kuwa mtoto unaepndwa na kupewa kila kitu, lakini kumbuka huwezi kupata kila kitu unachohitaji”
“Nani kakuambia napewa kila kitu , ni kweli napendwa na wazazi wangu lakini wakati wao wa kunipa kila ninachohitaji ushaisha na sasa natafuta ninachotaka , nilitaka wewe kuigiza kuwa boyfriend wangu kwa leo kwasababu unanilipa na baada ya hapo kila mtu anajua mambo yake , ningeweza kupata mwanaume yoyote ndio lakini hakuna ninaemdai hivyo watakuwa wananidai , unadhani mimi mtoto wa kike nitakuwa nalipa kwa
njia ipi , watataka mahusiano na mimi na mengineyo, labda hujui tabia yangu , napenda kudai kuliko kudaiwa ndio maana najitahidi kufanya kila namna niwe nadai watu na sio kudaiwa”Aliongea na kumfanya Hamza kutoa tabasamu.
“Kwahio mpango wako ni kunitengenezea deni tokea mwanzo na sio kunisaidia?”
“Nadhani ushaanza kunielewa sasa , lakini katika watu niliowadai wewe ndio nimekupa namna ya kunilipa kirahisi lakini unaleta ujeuri”Aliongea huku akivuta mdomo.
“Hehe… ingekuwa miezi kadhaa iliopia nisingekuzungusha hata kidogo”
“Unamaanisha nini?”
“Ninachomaanisha sikuwa na mpenzi hata wa maigizo , sasa hivi nazungukwa na warembo ni kawaida kwangu kuringa kidogo”Aliongea na kumfanya Prisila kutabasamu.
“Endesha kuelekea Kunduchi Prima hotel”Aliongea na Hamza alikata kulia kwake na kuichukua barabara ya Bagamoyo Road kutoka Sam Nujoma.
Dakika chache mbele walikuwa washafika katika hoteli ya Kunduchi , ilikuwa hoteli ya kisasa na ukweli ni kwamba Hamza hajawahi kufika katika hoteli hio licha ya kwamba sio mara yake ya kwanza kuwa katika hoteli kubwa.
Prisila alikuwa akiungana na wanafunzi wenzake aliosoma nao High school, alikuwa amesoma shule za hela nyingi hivyo ilikuwa ni sawa kukutana katika eneo la hadhi ya juu kama hilo.
Mara baada ya kuingia katika hoteli hio ya rangi nyeupe , Hamza aliweza kuona bango ambalo lina maandishi makubwa yaliokuwa yakitambulisha hoteli hio, lakini kuna kitu ambacho kilimshangaza sana Hamza , ilikuwa ni picha chini ya maandishi ambayo ilitumika kama Logo ya hoteli hio.
“Mbona unashangaa , unaangalia nini?”Aliuliza Prisila kwa shauku.
“Hamna tu”Aliongea na kisha alisogeza gari mpaka eneo la maegesho na wakatoka, ile wanaanza kuzipiga hatua waliweza kuona wenza wengine ambao mwanamke alikuwa amening’inia katika mkono wa mwanaume wakiingia, walionekana kuwa romantic.
Mwanaume alikuwa amevalia shati la mikono mirefu chapa ya Fendi na saa ambayo haikuonekana kwa ukaribu ni ya kampuni gani lakini ilionekana ya thamani.
Mwanamke upande wake alikuwa amevalia gauni la Chanel la mkato wa chini , alikuwa amebeba begi kwenye mikono yake chapa ya Hermes, licha ya kutokuwa mrembo sana lakini alikuwa akivutia na kuonyesha ni wale wanawake wa hadhi ya juu.
“Lidya!!”Aliita Prisila , alionekana kumtambua huyo mrembo.
Mwanamke yule mara baada ya kugeuka kwenye macho yake kulionekana aina flani ya wivu lakini alibadilisha na tabasamu bandia.
“Wow! , Kama kawaida yako Prisila , unazidi kuwa mrembo siku hadi siku”
Aliongea lakini upande wa yule mwanaume mara baada ya kumuona Prisila macho yake yalichanua na ilionekana ilikuwa ngumu kuacha kumkagua Prisila juu hadi chini.
“Lidya na huyu ni rafiki yako uliesoma nae?”Aliuliza yule mwanaume huku akiendelea kumchunguza Prisila.
“Ndio jina lake anaitwa Prisila ila alikuwa
akifahamika zaidi kwa jina la Pria , Prisila huyu ni mchumba wangu anaitwa Bahati”
“Mchumba!, aisee hongera zako , naona unaenda kuolewa”Aliongea Prisila akionekana kuwa na furaha juu ya Lidya.
“Bahati wangu usimuone hivi , ni mtoto wa Mzee Mtei mmiliki wa makampuni ya Mtei Enterprise , ijapokuwa huwezi kumuweka katika kundi la vijana
matajiri kama Saidi , lakini ni bilionea kibongobongo, nadhani kuwa kwetu pamoja imepangwa”Aliongea Lidya akitoa taarifa ambao hazikuhitajika kabisa na baada ya kusema hayo aliinua uso wake na kumwangalia kijana mtanashati anaejiita Hamza Mzee.
“Na huyu kaka ni..?”Aliuliza na kumfanya Prisila kusita kumtambulisha Hamza, sio kama hakutaka kumtambulisha bali hakujua amtambulishe vipi.
“Niite Hamza ni zaidi ya rafiki kwa huyu mrembo”Aliongea Hamza akiwa na tabasamu.
“Hamza!!, nakumbuka mara ya mwisho wakati tunakutana Prisila ulisema mpenzi wako amesharudi kutoka nje ya nchi na kwasababu alikuwa bize hakuweza kuhudhuria , Mr Hamza unaweza kutuambia kwanini ukamuacha mrembo kama huyu kuja peke yake , wengi tulidhani huna mapenzi ya kweli kwa Prisila”Aliongea.
“Nadhani wakati mnakutana ndio kipindi ambacho joto la Dar lilikuwa kali sana , hivyo kazi za kutengeneza AC zinakuwa nyingi”Aliongea Hamza.
“Wewe ni fundi wa kutengen4eza AC?”Aliuliza akiwa mshangao na Hamza alitingisha kichwa kukubali.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kusikia mtu alietoka nje ya nchi kuwa fundi wa kutengeneza AC , Are you for real?, unanifanya nitamani kucheka”Aliongea huku akichanganya kiswahili na kingereza.
“Sorry , Prisila nadhani unaijua tabia yangu ya kuropoka, hehe..”Aliongea lakini wanasema ndege wanaofanana huruka pamoja , hata kwa
Bahati Mtei alikuwa na tabasamu lililojaa kejeli.
“Lidya hutakiwi kucheka , unajua fika AC zikiharibika kuna hitajika fundi, hivi ni vitu ambavyo hatuwezi kufanya sisi wenyewe”Aliongea. “Ndio mpenzi , una akili sana”Aliongea
Prisila alionekana kutopenda jambo lile na alikuwa akitaka kusema kitu lakini Hamza alimzuia kwa kumtingishia kichwa akimwashiria asibishane nao.
Hakuona haja ya kubishana nao , ili mradi ashajua tabia zao hilo lilikuwa likitosha hivyo kucheza ngoma yao ni kujishusha.
“Sioni sawa kuchekana kwasababu ya vipato vyetu , hakuna aliezaliwa nacho , wote tunatafuta”Aliongea Prisila.
“Prisila sioni tatizo kwa wao kucheka na kudharau wa chini yao , sio wa kwanza , ni jamii ndio ilivyo, unaweza usiongee waziwazi lakini ubaguzi wa kipato umeshamiri kila kona, hata hili kusanyiko nadhani halijalengwa kukutana na kukuumbushiana habari za shule bali ni kuvimbiana nani ana kipi zaidi ya mwingine”Aliongea Hamza.
“Unanifanya nisitamani kuingia kabisa”Aliongea
Prisila.
“Ushafika , haina haja ya kujificha , ukiondoka watakuonna ni muoga na utawapa sababu za kuendelea kuongea, isitoshe kila aliekuja ni kwa ajili ya kuonyesha anaendelea vizuri kimaisha , hivyo sidhani ni swala baya pia”Aliongea na kumfanya Prisila kumwangalia usoni.
“Unaonekana kuwa mtu mzima na mwenye kujiamini”Aliongea Prisila na kumfanya Hamza kutabasamu.
Kwasababu Lidya na mpenzi wake wameshatangulia kuingia na Hamza na Prisila walianza kuzipiga hatua kuingia ndani pia , lakini Hamza alisimama ghafla mara baada ya kuhisi kuna mtu alikuwa akimwangalia na macho yake alikuwa ameyakazia upande mwingine wa maegesho ya watu mashuhuri na alikodolea macho gari ya Roll Royce na kwasababu kioo cha upande wa kulia kilikuwa kimeshushwa aliweza kuona aliekuwa yupo ndani.
“Twende Hamza , mbona umesimama
tena?”Aliuliza Prisila na kumshitua Hamza.
“Ulikuwa ukiangalia nini , ni mara ya pili nakuona unashangaa”
“Hamna kitu, nadhani utanashati wangu unafanya watu kuniangalia sana, kuna mtu alikuwa akinikodolea macho”Aliongea huku akiwa na tabasamu na kumfanya Prisila kutingisha kichwa chake kwa masikitiko.
Walipokewa na mhudumu wa hoteli ambaye aliwaongoza moja kwa moja mpaka katika chumba binafsi ambacho kilikuwa na meza kubwa iliojaa wanaume na wanawake.
Watu wale mara baada ya kumuona Bahati na Lidya akiingia walianza kuongea chini kwa chini wao kwa wao na baada ya kuonekana kwa Prisila walizidisha.
“Prisila!!”
Mwanaume mrefu wa mita kama moja na nusu hivi aliita , na alionekana kumwangalia Prisila kwa sekunde kadhaa kabla ya kuhamishia macho yake kwa Hamza.
Prisila aliishia kutoa tabasamu na waliingia ndani na alichukua nafasi hio kumtambulisha Hamza na walionekana kuridhika nae , pengine ni kwasababu ya mavazi yake , lakini upande wa Lidya hakuwa na kifua.
“Oteeni kazi anayofanya mpenzi wa mrembo wa darasa”
“Kwa muonekano wake nadhani anahela za kutosha , sio watu wa kawaida wenye kudumu mavazi ya bei hio, muonekano wake unaongea kila kitu”
“Ahah , muonekano wapi , ni fundi wa kurekebisha AC zilizoharibika”Aliongea Lidya.
“Nini!!?”
Watu wote waliokuwa ndani ya eneo hilo walionekana kushangaa, sio kwamba walikuwa wakishangaa kazi ya Hamza bali walikuwa wakishangaa Prisila mwanamke ambae alikuwa mrembo wa darasa wakati wakiwa shule kuwa na mpenzi ambae ni fundi wa kawaida na wengi walianza kumwangalia Hamza kwa kejeli.
Asilimia kubwa ya waliokuwa hapo ndani walikuwa wametokea katika zie familia za matajiri , ijapokuwa Prisila famiia yake ilikuwa na pesa lakini hawakuwa matajiri , baba yake ambae ni profesa hakupata mshahara wa kuitwa tajiri, hivyo ni kama yeye ndio ambae familia yake ipo kinyonge zaidi.
“Mbona mnashangaa , hamjawahi kusikia wala kuona mafundi?”Aliongea Prisila huku akionyesha kukosa utulivu.
“Haha.. usituelewe vibaya Prisila , kwa urembo wako na hadhi uliokuwa nayo wote tulitegemea mpenzi wako kuwa wa hadhi ya juu, nilitarajia ungekuja na Chriss mtoto wa tajiri Gabusha labda ndio maana tulikuwa na hamu ya kumjua”Aliongea mwanaume ambae alikuwa akiitwa Dismasi.
“Umejuaje nina mawasiliano na Chriss?”Aliuuliza
Prisila.
“Karibia marafiki zote wa Chriss wanajua nyie ni wapenzi , nimeshangaa kuona ukimtambulisha mtu mwigine”Aliongea na kumfanya Hamza kumwangalia Prisila.
“Hata kama , sina mahusiano na Chriss ni mwanaume ambae ananifuatiia ila hana kigezo cha kuwa mpenzi wangu”Aliongea.
“Prisila unamaanisha nini hana kigezo, ni kipi ambacho huyu Hamza wako kamzidi , kama ni ushombeshombe hata Chriss anao na kubwa zaidi ndio mtoto wa pekee wa Mzee Gabusha hivyo mali zote za baba yake ni za kwake”Aliongea Lidya huku akiona kabisa Prisila anajaribu kujikweza mbele yao, Lidya alijiambia kama Chriss yupo tayari kutoka nae kimapenzi basi angeachana na Bahati saa hio hio bila huruma yoyote.
“Hivyo ni vigezo vyako usitake kila mmoja avitumie katika kuchagua watu sahihi, unaongea kama vile Hamza hana vigezo , unamjua vizuri au
kisa umnemuona leo ndio unaanza kumhukumu?”Aliongea Prisila alionekana kukasirika mno , angejua hilo lingetoka asingekuja kabisa na Hamza.
Aliona amemleta mtu wa watu kwa ajili ya kupokea vichambo , lakini mara baada ya kugeuza macho yake pembeni kumwangalia Hamza ambae anasemwa , alionnekana kuwa bize na chakula ambacho kimeandaliwa.
Hamza hakutaka kuwa na hasira , aliona kuwa na hasira ni kujishusha kuwa katika levo sawa na wao, kwake hali hio ilikuwa ikimfurahisha sana kwani aliona ni kama vichaa wamekutana na kuanza kulumbana.
“Jamani haya mambo yametoka wapi , hii ni mara ya kwanza kwa Prisila kumtambulisha mpenzi wake kwetu , tunachoongea hakina umuhimu kabisa , kazi yake inahusiana vipi , isitoshe hata kazi yake ni muhimu pia, nani kati yenu anajua kutengeneza AC?”Aliongea Saidi kijana tajiri zaidi ambae ndio kiongozi wa kuandaa mkusanyiko huo wa wanafunzi wenzake kila mwaka.
Kundi hilo la watu walicheka na kukubaliana nae , huku wengi wakijikomba kwake kwa kumpamba kama mtu mwenye busara.
Gharama zote za kukutana zilikuwa juu ya Saidi Mohamed na vyakula vya bei ghali viliandaliwa na kubadilishwa kila dakika na jambo hilo liliwafanya watu wote kuendelea kuwa chawa kwa kumsifia sifia na kujipendekeza.
“Nimesikia kutokana na wateja wengi kuipenda hii hoteli , mmiliki ametengeneza mfumo wa kutoa kadi za uanachama kwa baadhi ya watu wa hadhi ya juu tu, hivyo kukaa hapa lazima uwe mwanachama na si vinginevyo, nasikia bosi wa mahoteli yote ya Prima ni mwanamke”
“Sio hivyo tu , nasikia pia asilimia kubwa ya wanachama ni wale ambao wanafahamiana na mkurugenzi , Bro Side mpaka kutupatia nafasi ya kukutana katika hii hoteli lazima uzito wako baada tu ya kurudi Tanzania umeongezeka”Aliongea Lidya.
“Hivi ni kweli hii hoteli ipo chini ya Prima Real Estate , nilichosikia Boss Yulia anatokea katika familia kubwa tu hapa nchini”Aliongea Dismasi.
“Haishangazi sana , ulimwengu wa kitajiri ni wa tofauti sana na watu wa kawaida”Aliongea bwana aliefahamika kwa jina la Jimmy.
“Nasikia kampuni ya Prima licha ya kuwa na sifa za kuingia katika soko la hisa ilishindikana kutokana na asili ya wanaoimiliki , lakini kama ingeingia katika orodha ya soko la hisa ingekuwa moja ya kampuni yenye thamani kubwa sana kimtaji, ijapokuwa kuna usiri mkubwa juu ya familia anayotokea Yulia lakini hata mimi naamini
atakuwa na koneksheni kubwa ndani ya serikali”Aliongea mwingine.
“Boss Side , umewezaje kupata kadi ya uanachama ndani ya hii hoteli , utaratibu wao wa kutoa uanachama huwa unakuwaje?”Aliuliza Lidya.
“Ilikuwa kama bahati tu nikakutana na Mkurugenzi na ndio alinialika kwa kunipatia kadi ya uanachama”Aliongea Saidi na muda uleule aliingiza mkono kwenye koti lake la suti na kuchomoa kadi na kumpatia Lidya.
“Aiyaa .. kadi inapendeza kweli , Bosi Side hebu tuione na sisi”Waliongea huku wakigombania.
Lakini upande wa Side alionekana kama vile hajaridhika mara baada ya kuona Prisila hakuwa akijali kabisa jambo lile.
“Jamani ilivyokuwa nzito , nadhani imetengenezwa kweli na madini ya dhahabu kama walivyosema”
“Ni Gold kweli , Lidya hebu acha kukaa nayo muda mrefu , nipe na mimi nione”Aliongea mwingine
“Subirini kwanza , bila ya kapicha hili halipiti hivi hivi”Aliongea huku akitoa simu yake ya I phone na kuanza kupiga selfie.
Bahati mpenzi wake alionekan kutoifurahia tabia ya mpenzi wake kumpapatikia Saidi, aliona ni kama vile anapotezewa licha ya yeye pia kuwa tajiri.
Lidya hakuishia kupiga picha akiwa ameshikilia ile kadi, lakini vilevile alipiga Selfie akiwa na Bosi Side na dakika ileile aliposti huku akiandika Caption
“It feels so good to have a meal with Director Said Mohamed of Vodocum Corporation”
Mara baada ya kuona Lidya alichokuwa akifanya wanawake waliokuwa hapo pia walitumia nafasi hio kupiga picha na Saidi Mohamedi , Mkurugenzi mtendaji wa kampuni kubwa ya mtandao ya Vodocum.
“Prisila angalia na wewe , ni watu wachache sana wanabahatika kushika kadi kama hizi kwenye maisha yao yote”Aliongea mwanadada aliefahamika kwa jina la Phina.
“Nishaiona tayari , mnaweza kuendelea tu kuiangalia”Aliongea Prisila akiwakatalia.
Bahati licha ya kuwa bosi wa kampuni ndogo hakutaka kujishusha lakini hata hivyo hakutaka kukaa kizembe kutotumia fursa hio na palepale alitoa kadi yake ya biashara.
“Mkurugenzi mimi ni GM kutokea kampuni ya Mtei Enterprise.tafadhari naomba upokee kadi
yangu ya biashara kwa ajili ya
mawasiliano”Aliongea lakini Bosi Side aliishia kuipokea na kuiweka juu ya meza.
“Uniwie radhi ndugu , tupo hapa kwa ajili ya kukutana na sio kuongea maswala ya kazi , hivyo hatuwezi kubadilishana mawasiliano.”
“Haina shida , umekuwa role model wangu katika maswala ya kibiashara sio rahisi kuongoza kampiuni kubwa ya mabilioni ya fedha kwa umri mdogo , baba pia mara nyingi amekuwa akiniambia niige mfano kwako, ni juzi tu kutokana na mwelekeo wa kampuni yako tulikuwa tkipanga kuwekeza kwa kununua hisa Vodocum”
“Nadhani tule kwanza , tutaongea baadae kama tutapata nafasi hio”Aliongea akimkatisha.
“Oh .. basi hakuna shida”Bahati alijikuta akinywea , alitamani kuwa na ukaribu na mtu mzito kama Side katika orodha ya mawasiliano yake,alitamani hata kuwa na namba yake tu ili kwenda kujigamba kwa wenzake, lakini Side alionekana kumkataa mbele ya watu.
“Side hebu fanya hivyo kwa ajili yangu bwana na kumpokea Bahati kwa mikono miwili , Mtei Enterprise sio kampunni ndogo naamini baadae itakuja kuwa kubwa, kwasasa kampuni yao ina thamni ya bilioni kumi, sidhani kama inaweza kuitwa kampuni ndogo”Aliongea Lidya.
“Lidya naona mchumba wako anatokea katika familia ya kitajiri , hongera sana ukiolewa na wewe moja kwa moja unakuwa tajiri”Aliongea Phina kwa wivu na kauli ile ilimfanya Bahati kuona angalau sasa na yeye ameanza kuonekana.
“Ukiilinganisha kampuni yetu na Vodocum sisi ni kama sisimizi tu”Aliongea akijaribu kwa mara ya pili kuwa chawa.
Ki ufupi kusanyiko hilo halikuwa na ile hali ya kuvutia kwani kila mtu alikuwa akiongea kile alichokuwa nacho na walichokamilisha huku wengine wakiwa chawa na walisahau hata kula.
Upande wa Hamza alikuwa bize na Kambakochi ya bei ghali ambayo imeandaliwa na alimwangalia Prisila na kuona mwanamke huyo alikuwa na wasiwasi mno.
“Prisila huna njaa , kula hata kidogo?”Aliongea Hamza na kumfanya Prisila kutoa tabasamu baada ya kuona Hamza hakuathirika na kilichoendelea na angalau alipata hamu ya kuanza kula japo kidogo.
“Prisila ombi langu la mara ya mwisho juu ya kuja kufanya kazi katika kampuni yetu bado lipo hai , lakini sijasikia majibu yoyote kutoka kwako?”
“Boss Side unataka Prisila kwenda kufanya kazi katika kampuni yenu , nasikia licha ya Dosam kuwa kampuni kubwa na kulipa vizuri lakini kwa
Vodocum ni habari nyingine”
“Vodocum ni kampiuni Kongwe ina matawi Afrika nzima , kuna rafiki yangu mjomba wake licha ya kuwa kitengo cha kawaida lakini ana maisha”
“Prisila uwezo wake ni mkubwa sana , makampuni mengi yanamhitaji kwa ajili ya kufanya nae kazi , si jambo la ajabu kuombwa na sisi aje afanye kazi Vodocum Tanzania na kutokana na thamani yake kuwa juu nipo tayari kwenda juu zaidi katika mshahara wake kuliko anaopata pale Dosam”
“Boss tupo wafanyakazi wenye uwezo zaidi ya Prisila mbona , au kuna sababu za kutaka kumuajiri yeye tu ,unampenda nini tajiri?”Aliongea mmoja wapo lakini Side alimpotezea.
“Kwasasa niseme napenda kazi yangu katika
kampuni ya Dosam ,Bosi Side uniwie radhi sipo tayari”
“Hakuna shida , una muda wa kutosha wa kufikiria”
“Prisila unasita sita nini , kufanya kazi ndani ya kampuni ya Vodocum sio swala la mshahara tu, unajitambulisha kimataifa, pili ndio nafasi pekee ya kuwa karibu na bosi Side , unajuaje tunaweza kukuita Mrs Side haha..”Baada ya baadhi yao kusikia kauli hio waliishia kutoa tabasamu la kinafiki, lakini kauli ile ilikuwa ni kama imemkera zaidi Prisila.
“Nyie mkiendelea kuongea ujinga , nitakasirika”Aliongea Prisila akiwa siriasi.
“Acheni kumtania Prisila ,ninachofanya ni kuhakikisha Prisila hadhi yake inapanda ndio maana , hakuna zaidi ya hilo”Aliongea Side.
“Prisila usimuangushe bosi , ni bahati ujue kufuatwa na bosi mwenyewe kutaka kufanya nae kazi, unaweza kuona sio maamuzi sahihi lakini kumbe ulioshikilia ndio maamuzi mabaya”Aliongea Lidya.
“Lidya kuna haja gani ya kuzunguka zunguka , unamlenga Hamza , kwanini usimwambie moja kwa moja “Aliongea Dismasi.
“Sijataja mtu jina ,mnikome”Aliongea na kufanya watu kuanza kucheka kinafiki huku wakimwangalia Hamza , hakuna ambae anajali kama Hamza anaweza kukasirika au Lah na jambo lile lilimchosha Prisila na kumshika mkono Hamza.
“Tuondoke , siwezi kuendelea kukaa hapa”Aliongea na kumshitua Hamza ambae alikuwa akimalizia kubeba kipande cha mwisho cha nyama.
“Umekasirika kwasababu ya wao kunicheka?”Aliuliza Hamza.
Prisila hakutaka kumfanya Hamza kujisikia vibaya , ijapokuwa alikuwa akitafuta hela kwa shida , lakini hakuona ni tatizo tofauti na hao watoto wa matajiri ambao wanadhani pesa ndio kila kitu.
Upande wa Hamza licha ya kwamba hakuwa
akijali , lakini alihisi furaha mara baada ya kuona Prisila hataki kuona akiendelea kuchekwa.
“Nisisikie mtu anamuongelea tena Hamza , huyu ni braza wangu kuanzia leo hii”Aliongea Side , shida yake ilikuwa ni kutokumfanya Prisila asiondoke maana alikuwa akifurahi kumwangalia.
‘Prisila usikasirike , leo ni siku nzuri na tumekutana na kumjua mpenzi wako hivyo anapaswa kupewa heshima yake”Aliongea na kauli yake iliwafanya wote sasa kutulia.
Prisila alikuwa bado anasita sita kuendelea kubaki , lakini kwasababu Side ndio kaongea aliamua kutulia.
Sasa dakika hio hio mlango wa chumba hicho ulifunguliwa na wafanyakazi waliovalia sare nadhifu walitengeneza njia huku wakionyesha heshima juu ya mwanamke ambae alikuwa akiingia.
“Nini tatizo , mbona kama nahisi kuna mtu anataka kuondoka tayari?”Aliongea kwa kingereza , alikuwa ni mwanamke mchangamfu.
Alikuwa amevaa shati la mikono mirefu la michirizi myeupe na mieusi huku akiachia vifungo kadhaa kifuani , huku chini akiwa amevalia suruali ya rangi ya kahawia akimalizia na koti la surti ya rangi ya kahawia , mavazi hayo yalimfanya kuwa mrembo sana na kuchora umbo lake la kuvutia.
Alikuwa amesuka nywele zake kwa mtindo wa Crochet na kumfanya nyuzi nyuzi ndefu kumwagika begani , alikuwa na weusi angavu rangi ya chocolate, hadhi yake ilikuwa ni ile ya mwanawake wa daraja la juu.
Alikuwa mrembo mno tembea yake kutumia viatu vya skuna na harufu ya marashi yake ya bei ghali ilifanya wanaume kumeza mate.
Kingine cha kuvutia zaidi ni kwamba namna yake ya kuongea ilijaa mapozi na cheo kwa wakati mmoja, ni aina flani ya haiba ambayo mwanamke wa kawaida hawezi kuwa nayo, ni haiba ambayo mtu hufunzwa na sio kuzaliwa nayo.
Mwanamke pekee ambae alikuwa na uwezo wa kushindana nae katika muonekano ni Prisila peke yake , lakini bado haiba yake na utulivu wa macho hakumfikia.
Kitendo cha Hamza kumuona mwanamke huyo akiingia muonekano wake ulibadilika na kuonekana wa usiriasi kidogo na ghafla ni kama amekumbuka kitu alichosahau kuona na kujikuta akitoa tabasamu ambalo limejaa uchungu.
Tatizo pekee ambalo aliliona ni moja tu na kujiuliza imekuwaje huyu mwanamke akawa Tanzania tena katika mazingira kama hayo.
Upande wa mwanamke macho yake yote yalikuwa yamemkazia Hamza , huku akionyesha ishara flani ya kuzuia hisia zake.
Upande wa watu waliokuwa hapo ndani pia walikuwa katika hali ya mshangao , walishangazwa na kivuli cha mwanamke huyo kilivyokuwa na nguvu na kuwasabibishia msisimko.
Alieanza kusimama kwa heshima alikuwa ni Saidi Muhamehd au bosi Side.
“Bosi Yulia! , sikutarajia kama utakuwepo leo?”Aliongea Saidi.
Wengine wote mara baada ya kusikia jina la Bosi Yulia walielewa ni nani anaongelewa na walijikuta wakisimama mara moja , huku maswali yakiwavaa ,wakijiuliza inamaana huyu ndio moja ya mataikoni wa kike ndani ya taifa la Tanzania, mmiliki wa makampuni ya Prima.
Hakuna ambae ashawahi kudhania bosi Yulia angeonekana kuwa kijana na mrembo hivyo, isitoshe wanawake ambao walikuwa ni matajiri hawakuwa na muonekano wa kuvutia tofauti ya Regina na Yulia.
Kila mmoja alionyesha heshima , huyo alikuwa ni bosi zaidi ya Saidi .
Bahati alikuwa na furaha mno kiasi kwamba hakujua ni wapi aweke mikono yake , moyo wake ulikuwa umejaa furaha , mwanzoni mpango wake ulikuwa ni kumtumia Lidya ili kujenga ukaribu na Tajiri Side ndio maana akalazimisha kushiriki kusanyiko hilo lakini sasa anamuona Yulia shabaha yake ilibadilika mara moja.
Muda huo wanadarasa hao walikuwa wakimuonea wivu Saidi mno kutokana na kuwa na ukaribu na bosi mkubwa kama huyo tena mrembo.
“Kwahio kumbe ni wewe bosi Side ndio umeandaa hii party , mniwie radhi kwa bughuza”Aliongea kwa lugha ya kingereza. Na maneno yake mbele ya wasomi hao yaliwashangaza , ilikuwa ni kama wanajiuliza inamaana amefika kwa ajili ya kuangalia party ambayo imeandaliwa na Saidi , lakini sasa kilichotokea mbele kiliwashangaza.
Bosi Yulia alizipiga hatua na kumsogelea Hamza huku akimwemwesa lipsi zake kama mtu aliekosa kujiamini.
“Sikuwahi kuwaza nitakuja kukutana na wewe hapa , nilidhani sitokuja kukuona kamwe”Aliongea na kulikuwa na ishara ya uchungu katika sauti yake.
“It real is fate”Alijibu Hamza kwa lugha ya kingereza akimaanisha ni majaliwa huku akitoa tabasamu.
“Yaani , nilipokuona pale kwenye maegesho ya gari nilijiuliza ninaota au, hata kuja hapa sijaamini kama ni wewe, nimekuja kuhakiki , lakini ni wewe kweli?”Aliongea bila ya kupepesa jicho.
“Bosi Yulia , unafahamiana na Hamza muda mrefu?”Aliuliza Saidi na kufanya kila mtu kutegemea jibu.
“Hamza!! , kumbe ndio jina lako?”Aliongea yulia na kufanya watu kuzidi kushangaa huku wakijiuliza wanafahamina vipi huku hawajuani majina au Hamza hakuwa na jina hapo kabla.
“Ndio”
“Umefika lini na kwanini Tanzania?”Aliuliza Yulia.
“Ni stori ndefu”Alijibu Hamza na kumfanya Yulia kutabasamu.
“Niambie taratibu taratibu , sio rahisi kukutana na wewe hapa , awamu hii nadhani haitakuwa haraka , bado hata sijakushukuru kwa kilichotokea wakati ule kama isingekuwa wewe ning….”
“Miss Yulia , its not convinient to talk about it here “Aliongea Hamza akimaanisha kwamba sio vizuri kuongelea hilo hapo.
“Nini tatizo , kwanini umebadilika sana , wewe katika kumbukumbu zangu sio mpole hivi”Aliongea Yulia.
Watu wote waliokuwa hapo walijikuta wakishangaa kwa kuwaangalia wawili hao na maongezi yao , ilionekana ni kama vile Hamza amemfanyia Yulia kitu cha ajabu nje ya nchi , ndio walivyotafsiri.
Yulia alionekana kuelewa na hapo hapo alimsogelea Hamza karibu kabisa, huku akiona hali hio aliokuwa nayo Hamza inamvutia mno , walisogelena karibu kiasi kwamba mpaka pumzi zao zinagusana ngozi ya kila mmoja.
“Then do you want to come to my house ?, just me and you alone , we can have a good chat”Aliongea akimaanisha au anataka aende nae kwake wakiwa wawili tu na kufanya maongezi yawe mazuri zaidi.
Alichokuwa akifanya Yulia ni kumpagawisha Hamza mazima tena bila ya kificho.
Sasa fikiria bosi mkubwa kama Yulia anamfanyia hivyo Hamza ambae sisi tunamjua ni mzembemzembe.
Kauli hio ilimfanya Prisila na wenzake wote kutoa midomo kiasi kwamba ukiwawekea yai linapita.
Walijiuliza Hamza ana nini mpaka mwanamke wa aina hio kumwalika kwa kimitego namna hio.
Tajiri Side hata yeye muonekano wake ulibadilika , ulikuwa muonekano mzito , hasa baada ya kupotezewa kabisa na Yulia.
“Just who is Hamza!!?”Ndio swali ambalo lilimvaa mara moja.
Prisila alikuwa akimjua Yulia vizuri kwa kumsikia , lakini kitendo cha mwanamke huyo kumfahamu Hamza ilimfanya awe na shauku ya kutaka kujua kwanini Hamza anafahamiana nae , ukweli ni kwamba hio ni mara ya pili kwa Hamza kumsahngaza , mara ya kwanza ilikuwa ni mwanasayansi nguli wa hisia za kibinadamu wa taasisi ya Felizi yaani Frida na leo ni tajiri Yulia.
Kitendo cha Hamza kuwa katika hali kama hio na mwanamke tajiri na mrembo kama huyo ilikuwa ni vibao chapuchapu kwa kila mtu ambae alikuwa akimbeza kuwa fundi.
Watu hao ambao waliona hawawezi hata kukaa
meza moja kula chakula na Yulia na sasa walikuwa wakimbeza mwanaume ambae alionekana ana historia nae.
Wale wote ambao walicheka sana walianza kumwangalia Lidya kwa macho ya hasira, walijiambia kama sio Lidya kuongea upuuzi wake na umbea umbea wasingejiweka upande mbaya na Hamza na pengine wangeweza kupata walau nafasi ya kujipendekeza kwa Yulia.
Upande wa Hamza hakuwa na mawazo hayo kabisa , alijua kama Yulia ataendelea kuropoka itamletea shida kabisa hususani katika matukio ambayo yamekwisha kupita
Hivyo Hamza bila kujifikiria mara mbilimbili alimshika Yulia mkono na kisha akamvuta kumtoa katika chumba hicho.
“Niufuate” Aliongea.
Comments