SEHEMU YA 45
ILIPOISHIA
“Yulia ninachomaanisha usije ukaruhusu mawazo yako yakaenda mbali , nipo ndani ya kampuni ya Dosam kwa ajili ya kutengeneza pesa kama watu wa kawaida , mimi sio mtu ambae umekutana nae miaka saba iliopita”
“Kama huo ndio mpango wako , kwanini usijiunge na kampuni yetu ya PRIMA? Nitakupa nafasi ya kuwa bodigadi wangu, haijalishi Regina anakulipa kiasi gani nipo tayari kulipa zaidi yake”
“Hapana haiwezekani , nimeshasaini nae mkataba , isitoshe kwa ulichosema nadhani anahitaji ulinzi zaidi kuliko wewe”
“Unanionaje , nipo tayari kukuliipa milioni ishirini kwa mwezi , kama haitoshi nitajie kwa ajili yako nipo tayari kulipa kiasi chochote”Aliongea na kumfanya Hamza kuona Yulia anachagua cha kujibu maneno yake na kumfanya acheke.
“Yulia tulikutana kwa muda mchache sana Zurich , hivi unadhani kuniona vile ndio kunijua , ukweli ni kwamba hujui chochote kuhusu mimi halafu unataka niwe bodigadi wako?, mbona kama unaniamini sana kupitiliza”
“Mimi ninachojua wewe sio mtu mbaya , kama kweli ungekuwa ni mtu mbaya usingeniokoa katika dakika zangu za mwisho za uhai”Aliognea huku awamu hio akilegeza sauti na mikono yake kuiweka katika mabega ya Hamza.
“Au upande wako mwingine unakufanya kuwa mbaya , kama ni hivyo nakufaa zaidi ya Regina”Aliongea huku aking’ata lipsi zake kwa namna ya kukonyeza na pumzi yake kuizuia na kufanya jicho kulegea.
Matendo yote ya Yulia yalimfanya Hamza mwili wake kuwaka moto, Yulia alikuwa akijua anachokifanya katika kumpagawisha.
Hamza mara baada ya kuona yanakwenda kumshinda alimshika kwenye shingo kwa spidi ya hali ya juu na kwenda kumbana kwenye ukuta na kusogeza mdomo wake karibu zaidi huku Yulia akiendelea kumwangalia kwa macho ya kumruhusu lakini yaliojaa waswasi kwa wakati mmoja.
ENDELEA
Yulia alikuwa amekabwa kisawa sawa ukutani , umbali kati yao ilikuwa ni sentimita tatu tu.
Muonekano wa Hamza ulikuwa ni ule wa usiriasi , hakukuwa na ishara yoyote ya uzembe , alionekana kama vile ni mtu wa karne nyingi zilizopita na aliinua mkono wake wa kushoto na kukiinua kidevu cha Yulia kwa kukibetua kwa juu.
“Niachie bwana, unaniumiza ujue?”Aliongea akilalamika na hio yote ni mara baada ya kuona macho ya Hamza yalivyokuwa na usiriasi usiokuwa wa kawaida hata kidogo , ule ujasiri wake mbele ya Hamza ulimpotea na sasa alikuwa ni kama Panya mbele ya paka.
Muda huo alikuwa ashapoteza ule muonekano wake wa hadhi ya ubosi , aligeuzwa ghafla tu na kuonekana kama msichana mdogo ambae amekosa msaada.
“Unaonaje ukiondoka hapa Tanzania?”Aliongea Hamza huku akiwa na tabasamu lililojaa uovu na kumfanya Yulia uso wake kuwa wa moto huku mboni za macho yake zikicheza cheza.
“Usije kujaribu kunichezea na kujaribu kuniwekewa mtego , maana nikigundua sina uhakika kama utaendelea kuwa salama”Aliongea Hamza.
“Hmmm..”Yulia aliishia kutingisha kichwa akikubali.
Alikuwa akiamini, kuwa kwake ndani ya jiji la Dar es salaam sehemu aliozaliwa na kuijua vizuri basi angeweza kuwa na uwezo wowote mbele ya wanaume na kuwasumbua , lakini hakuamini Hamza alishajua alichokuwa akiwaza tokea muda mrefu.
Yulia alikuwa akisita kukubali lakini kutokana na muonekano wa kutisha wa Hamza alijikuta akikubali kishingo upande , kwasababu Hamza hakuwa na dalili yoyote ya kutania.
Hamza mara baada ya kuona mwanamke huyo ameshika adabu yake na ameogopa alimwachia.
“Usije kuthubutu kuongea chochote kilichotokea baina yetu jijini Zurich , sitotaka kujiingiza kwenye matatizo kwasababu yako”
“Nimekuelewa , lakini je naweza kukutana na wewe?”Aliuliza Yulia, hakuwa mwanamke mpumbavu asielewe nia ya Hamza.
“Kwanini unataka kukutana na mimi?”Aliuliza .
“Mbona nahisi kama unanichukia?”
“Haipo hivyo , lakini hakuna chochote kati yetu , nilifika Zurich kwa misheni maalumu ya kukuua na nikakuta umeshatekwa tayari nikakuokoa , kama nilichofanya kinachukuliwa kama kuokoa uhai wa mtu basi nitakuwa nimeokoa maelfu ya watu , itakuwa ni kujichosha kuanza kukutana na kila mmoja kwasababu hio tu”Aliongea.
“Sio kweli , hukuniokoa tu , lakini vilevile umenisaidia kulipiza kisasi kwa kundi lote la watu waliomuua mama yangu na mdogo wangu , ni wewe ulienisaidia kulipiza kisasi na ukaenda mbali kunipa nauli ya ndege kurudi nyumbani kwa kunitoa katika lile giza licha ya mbinu yako kuwa rafu”Aliongea huku muda uleule akiinamisha macho yake chini.
“Kwa kipindi chote tokea nirudi nyumbani , nimetumia kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili ya kutuma watu kukutafuta , lakini ilikuwa ngumu kwangu kwani sikuwa nikilifahamu jina lako na unapoishi”
“Ulikuwa ukituma watu kuja kunitafuta?”Aliuliza Hamza huku akicheka.
“Ulitaka kufanya nini baada ya kunipata , usiniambie mpango wako ni kunilipa kupitia mwili wako?”Aliuliza Hamza na kumfanya Yulia kumwemwesa lipsi zake , macho yake yalikuwa yamejaa matarajio.
“Kama nipo tayari utaniruhusu?”Aliongea na kumfanya Hamza kumwangalia huyo mrembo na kisha akavuta pumzi na kuzishusha.
“Ijapokuwa ombi lako linavutia sana , nataka kuendelea kuishi maisha ya amani , nikijihusisha kwa namna yoyote na wewe nina uhakika nitajipalia tu makaa na kuingia matatizoni, isitoshe
mimi siwezi kurudi na kuwa wa zamani tena”Aliongea.
“Inaonekana mpango wako ni kukaa Tanzaniwa kwa muda mrefu , kama ni hivyo je naweza kukutafuta japo mara moja moja?”
“Yulia kwa hadhi yako na nguvu ya familia yako , hata kama unataka kupata bodigadi mwenye uwezo wa juu ni kitu chepesi sana , kwanini iwe mimi?”
“Umejuaje ukubwa wa hadhi ya familia yangu , au ulinifanyia uchunguzi kabla?”
“Haina haja ya kuigiza najua mambo mengi kuliko unavyofikiria , katika bango linalotambulisha hoteli yenu , ile Logo inayotambulisha kampuni yenu ni maalumu ambazo zinatolewa kwa familia zenye hadhi na kufanya isitumike kutambulisha biashara za watu wengine duniani , kampuni yako ni kubwa hivyo ni rahisi kukutambulika kimataifa , huwezi kutumia Logo ile bila ya kujua nguvu yake, hivyo moja kwa moja inaniambia familia yako imesajiliwa GREL na kupewa hadhi ambayo inatambulishwa na ile Logo, familia zote ambazo zina usajili wa hadhi ndani ya GREL hupewa alama zinazofanana lakini tofautishi kama ile”Aliongea Hamza.
GREL kirefu chake ni Global Registry of extraordinary lineages. Sio sahihi kuiita GREl kama umoja hadharani kwani haijawahi kutangazwa hivyo bali kwa nje ni kama jarida tu au kitabu cha kutambua hizo familia , lakini kwa siri ni umoja tena wenye nguvu.
Familia ambazo zipo katika orodha ya GREL ni kama vile familia ya Rockfellers , familia ya Rothchild , familia ya Al Saudi kutoka Saudi Arabia, familia ya Fujiwara kutokea Japani na kuendelea.
Kwa lugha nyepesi unaweza kusema familia hizi ndio zenye mizizi ya kihistoria , kiuchumi na ushawishi ndani ya taifa husika au kwa bara zima, yaani ndio sehemu ya familia ambazo zipo ndani ya Deepstate.
Sasa inasemekana wazo la kupatia kila familia yenye nguvu nembo(Logo) lilitoholewa kutoka katika utaratibu wa kifamilia wa familia za damu ya kifalme hususani katika mataifa mengi ya bara la Asia , mfano China na Japani ambapo familia kama vile Tang ina alama yao ya upekee kabisa ambayo haitumiwi katika biashara yoyote ndani ya taifa hilo.
“Wewe ni nani , kwanini unayajua haya yote , umejuaje ile logo ipo katika GREL?”Aliuliza Yulia kwa mshangao.
“Napenda kujifunza vitu vingi nisivyovijua , hivyo niliweza kujua mara moja”Aliongea Hamza.
“Ni kweli familia ninayotokea ipo katika GREL lakini hili linahusiana vipi na wewe kuwa bodigadi wangu?, wewe ndio muokozi wangu nakuamini ndio maana, nimekusubiria kwa muda wote huo , kwanini hunionei huruma?”Aliongea na kumfanya Hamza kumwangalia kwa macho ya kichokozi.
“Haya yameisha , naonekana kuchoka wakati wewe hujachoka , nakubali uwezo wako wa kuigiza ni mkubwa , kwanza umeuchukua uhusika wa mwanamke anaeongojea mwanaume wake kwa muda mrefu kukutana nae na kumlipa kwa kutumia mwili wake , tena sasa hivi umetoka katika uhusika huo na unaigiza kuwa mwanamke kama bikra ambae anaogopa na anahitaji mwanaume wa kumlinda , ki ufupi hakuna ukweli wowote kuhusu wewe , hebu niambie umeweza vipi kunitafuta na ni kipi unataka kutoka kwangu?”Aliuliza Hamza na kumfanya Yulia muonekano wake kubadilika na kuwa wa kikauzu.
Mwishowe Yulia alitoka katika ule muonekano wake wa mapozi na kuwa mwanamke mrembo kauzu ambae amesimama kama roboti. “Umejuaje nakugizia tokea mwanzo , nadhani nilipaswa kuwa makini zaidi”Aliongea
“Uwezo wako wa kuigiza ni mkubwa mno , miaka saba iliopita wakati nakuokoa nilikuwa nishajua muonekano uliokuwa nao ni wa kimaigizo tu”
“Kwanini?”Aliuliza huku akiwa na mshangao , hakuamini Hamza wa miaka saba iliopita aliweza kumtambua mara moja undani wake ukoje.
“Wazazi wako wote na wadogo zako waliuliwa na wale maninja , nilikuokoa na kisha nikakurudisha hotelini , unakumbuka ni kitu gani uliniambia cha kwanza?”
“Nimesahau , nilisema nini?”
“Ulisema una kiu mno ya maji , yaani mtoto ambae mama yake , baba yake na mdogo wake ndio wametoka kufariki unarudi hotelini na kitu cha kwanza baada ya kulia kwa lisaa limoja ni kumuomba mtu usiemjua maji?,watu wengine wanaweza kuona ni kawaida , lakini kwa upande wangu sikuona kitu kile ni cha kawaida, katika moyo wako hukuwa na machungu kabisa ya
familia yako kupoteza maisha , uliweza kupotezea kwa muda mfupi sana hisia za huzuni ulizokuwa nazo na kuanza kufikira hatua inayofuata”Aliongea na kauli ile ilimfanya Yulia kushangaa.
“Inaonekana sikuwa msiri vya kutosha mbele yako”Aliongea Yulia.
“Makisio yangu ni kwamba na wewe pia una ugonjwa wa akili wa Protesting personality Disorder , nakosea?”Aliuliza Hamza akiwa na tabasamu.
“Hakika una uelewa mkubwa sana , tofauti na mama yangu wewe ni mtu wa pili kuijua siri yangu , ningekuwa na uwezo wa kukuua basi ungekufa leo hii”Aliongea akiwa siriasi.
“Duhh!, ili kutimiza malengo yako unataka kumuua kwanza aliekuokoa , yoyote yule anapaswa kufa hata kama ni kwa kumtishia , hizo ndio dalili za ugonjwa wako”Aliongea Hamza kwa upole.
“Huu sio ugonjwa , ni Mungu ambae ameniumba kwa kutoniwekea uwezo wa kuwa na hisia , ili nisisumbuke na hisia ambazo hazina maana”Aliongea.
Unachopaswa kuelewa ugonjwa ambao anauzungumzia Hamza ni aina ya ugonjwa wa akili ambao mtu anazaliwa nao na tabia yake kubwa ni kwamba mtu akiwa na ugonjwa huu huwezi kumkuta akiishi katika uhalisia wake , maisha yake mwanzo mwisho ni maigizo tu pili hata kama anahitaji msaada na akaupokea kamwe hawezi kukubali alisaidiwa na njia pekee ni kumuua aliemsaidia ili kulinda siri ya kusaidiwa , dalili nyingine ni kwamba watu wa aina hii hawana hisia kabisa, yaani wapo kama maroboti yalivyo , yaani hawahisi maumivu wala furaha tofauti ni kwamba utawakuta wanaigiza kuhisi maumivu au furaha , au kupenda, ndio walivyo, haijawahi kufahamika unasababishwa na nini lakini kitaalamu unaendana na ugonjwa wa akili unaofanana na Munchausen Syndrome.
“Kama hivyo ndio unavyowaza , basi hakuna tatizo , ila usijali siwezi kuwaambia watu kuhusu tatizo lako”Aliongea na kumfanya Yulia aliekuwa kama roboti kupiga hatua moja mbele na kumwangalia Hamza usoni.
“Kama ulijua tokea mwanzo kuhusu tatizo langu kwanini bado ukaendelea kutoa ushirikiano kwangu?”
“Kama ilivyokuwa miaka saba iliopita , tulikutana kwa bahati mbaya , hivyo haina haja ya kuongea chochote kuhusu mimi ili mradi hatutokutana tena , sitaki kujua wewe ni mtu wa aina gani na kipi
unafanya, ki ufupi sitaki kujua chochote kuhusu wewe?”
“Kwanini bado naona unaonekana kujali maisha yangu , mpaka kuijua siri yangu?”
“Hapana , ninachomaanisha ni kwamba sitaki kupitia maigizo yako unitumie na mimi kama kete yako kwenye mipango yako , kwa kusema hayo siwezi kuwa bodigadi wako au mtu yoyote kwako”Aliongea Hamza akiwa siriasi na kumfanya Yulia midomo yake kupinda kwa tabasamu lililojaa uovu.
“Ijapokuwa sijui ni hisia gani ambazo wanawake wanapata wakimpenda mwanaume lakini mimi nahisi nakupenda”Aliongea na kumfanya Hamza kutoa tabasamu huku akijihisi huu upendo utaanza kumbadilisha muda si mrefu.
“Lakini hata hivyo , kuna kitu kimoja ambacho hujapatia”Aliendelea kuongea
“Oh! , ni kitu gani hicho?”
“ Sijakutana na wewe kwa kukutafuta , ni kwa bahati tu tumeonana ndio maana natafsiri kama majaliwa”
“Kama ni hivyo nadhani nilipangiwa kupatwa na hili janga?”
“Ndio , hili ni janga kwako, lakini kwasababu unajua siri yangu basi kwanzia leo hatutojihusisha kwa lolote kati yetu , vinginevyo wewe ufe au mimi nife”Aliongea Yulia na kumfanya Hamza kugeuka na kuzipiga hatua kurudi alikotoka.
“Nadhani pia unapaswa kuomba sana isije ikatokea siku moja nikaliharibu ua kwa ukatili”Aliongea Hamza na kutokomea Kitendo cha Hamza kupotea katika macho yake , Y ulia alitoa simu yake katika mfuko na kubonyeza namba.
“It’s me .. Go find someone Called Hamza , I want all his information..”Aliongea kwa lugha ya kingereza
Baada ya kumaliza kutoa maelekezo aliweka nywele zake sawa pamoja na nguo zake na kurudia muonekano wake na kutoa tabasamu la kimaringo na mapozi na kwa madaha alizipiga hatua kurudi ndani.
Hamza na Yulia walitumia zaidi ya dakika kumi kwenye kuongea tu , lakini kwa watu ambao walikuwa ndani ya chumba binafsi , walikuwa na hisia mchanganyiko kana kwamba ni muda mrefu sana umepita tokea watoke , ikiwemo kwa Prisila ambae ni kama alianza kushikwa na wivu.
Lidya na Bahati walikuwa wakijutia maneno yao kiasi kwamba utumbo wao ulikuwa ukijinyongorota na kufanya nyuso zao kuonekana mbaya.
“Prisila hivi ni kweli Hamza ni fundi wa kawaida tu?”Aliuliza Saidi na kwa upande wa Prisila ukweli ni kwamba alimjua Hamza juzi tu hivyo hakuwa na taarifa za kutosha.
“Alikuwa fundi ndio , lakini sasa hivi ana kazi yake nzuri tu”Aliongea Prisila akilenga Hamza kuwa boyfriend feki wa Regina na pia msaidizi wake.
Ijapokuwa Prisila aliongea hivyo lakini hakuna ambae aliweza kuelewa kile alichomaanisha haswa , ilikuwa ni kama kauli yake ni nyepesi sana kwa swali gumu ambalo ameulizwa.
Muda huo wakitaka kumchimba zaidi ndio muda ambao Hamza alirudi na mara baada ya kundi lote kuona hakuna anaekula zaidi ya kuonekana kama watu wanaesubiria mtu alijikuta akishindwa kujizuia na kutoa tabasamu.
“Nyie mnafanya nini , mbona kama mpo kwenye kikao?”Aliuliza. lakini ilikuwa ndio nafasi ya kila mmoja kuanza kumuuliza maswali Hamza. “Hamza kwanini hukutuambia unafahamiania na bosi Yulia?”
“Hamza umefahamiana vipi na bosi Yulia?”
“Bro Hamza , Kaka mkubwa , hebu kwanza kunywa hii Wine nadhani itakidhi radha ya ulimi wako?”
Yaani ki ufupi bila aibu kila mtu alianza kuwa chawa kwa kujipendekeza kwa Hamza
Lakini Hamza hakuwa na mudi ya kuendelea kula tena na alichotaka ni kuedelea kumpa kampani Prisila hivyo aliwapotezea kabisa , isitoshe alijua kabisa taifa hili lazima lipo chini ya Yulia , hivyo chochote atakachofanya kinaweza kumletea shida.
“Prisila vipi chakula ni kitamu?”Aliuliza Hamza na Prisila kwa kumwangalia tu Hamza ni kama kuna kitu amekisoma.
“Ni kitamu ila nimeshiba , unaonaje tukitangulia kuondoka , nahitaji kwenda kupumzika”
“Hakuna shida nitakusindikiza”Aliongea na muda huo huo wote walisimama ili kuondoka na watu hao waliona aibu kwa kuona kwamba Hamza amechoshwa na kujipendekeza kwao.
Muda huo ambao Hamza anataka kuondoka Yulia alirudi na kuingia na mara baada ya kuona Hamza anaondoka alitoa tabasamu la kumuaga.
“Hamza , siku nyingine ukiwa na muda jaribu kuja hata mara moja moja basi , haina haja ya kuwa mpole mbele yangu”Aliongea na Hamza alitoa tabasamu hafifu.
Muda uleule Yulia alichukua kadi ya madini ya dhababu kutoka kwa msaidizi wake.
“Hii ni kadi ya daraja la juu kabisa ya uanachama wa hoteli zetu, ndani ya jiji hili wanazo watu wasiopungua kumi , ichukue na unaweza kuja hapa muda wowote ndani ya masaa ishirini na nne na hutoweza kulipia hata shilingi”Aliongea
Lidya, Bahati na tajiri Saidi mara baada ya kuona hio kadi macho yao yaliwatoka kwa matamanio na wivu , hata kadi ya unachama ya Bosi Side haikuwa ya daraja la juu kama hio, kadi hio ilimaanisha unaweza kuingia ndani ya hoteli hio na kupata huduma bila ya kulipia hata shilingi.
Sasa walijiuliza kadi ya hali ya juu ya namna hio inakuwaje Yulia anampatia Hamza, lakini sasa wakati kila mtu akiitamani upande wa Hamza aliikataa.
“Nashukuru sana , lakini haina haja”
Lidya na wenzake kichaa kilitaka kuwapnda , ni kama walikuwa wamesikia tofauti hata kwa bosi Side alijikuta akikunja ndita bila ya kupenda.
Ukweli ni kwamba maana halisi ya kadi hio sio kwa ajili tu ya kupata huduma bure katika mahoteli yote ya Prima , bali ilikuwa ikiashiria hadh, sasa inakuwaje Hamza hataki kadi kama hio tena kwa kumkatalia mtu mwenye nguvu kama Yulia.
Upande wa Yulia licha ya kukataliwa waziwazi hakujali sana , alijua Hamza alikuwa akifanya hivyo ili kumuepuka , lakini sasa kadri ambavyo Hamza alijifanya kumkataa ndio alivyozidi kumtaka.
“Upo sahihi , kwasababu tunafahamina huitaji uthibitisho , unaweza kuja hapa muda wowote , au kuja makao makuu ya kampuni yangu au nyumbani , wewe nipigie tu simu”Aliongea huku akiwa na tabasamu.
Na watu nyuma ya Yulia walijikuta wakishindwa kupumua vizuri , ukweli ni kwamba Yulia hakuwahi hata kumjali raisi wa Jamhuri iweje leo aoneshe udhaifu mbele ya Hamza.
Hamza alijua kabisa huyo mwanamke hakuwa na mpango wa kumuacha kirahisi , lakini alijiambia ili mradi havuki mpaka basi atamuacha aendelee kuongea anavyotaka.
Wakati Hamza akiingia katika gari na kuliondoa ndani ya hoteli hio watu wale wote walijipanga mstari kwa ishara ya kumsindikiza,pengine walifanya hivyo kwasababu Yulia alikuwepo pia akisindikiza gari ya Hamza kwa macho.
Hamza mara baada ya kufika barabara ya kuingia
Salasala aliingiza gari katika moja ya mgahawa, alifanya hivyo kwani alijua kabisa Prisila alikuwa na njaa na pia muda ulikuwa umeenda.
Prisila alijikuta akifurahi kuona Hamza alikuwa na uwezo wa kuona ishara ndogo ndogo na kuzifanyia kazi , mfano kujua alikuwa na njaa na kumleta mgahawani.
Muda huo ndio sasa Prisila alipata ujasiri wa kumuuliza Hamza kuhusu Yulia , imekuwaje kuwaje amefahamiana nae , maana njia nzima alikuwa kimya.
“Umefahamiana vipi na Yulia ?”
“Tuliwahi kukutana mara moja na nilimsaidia , sio kama nafahamiana nae sana ile tu kwasababu ya
msaada wangu ndio maana kanichangamkia”Aliongea.
“Kumbe..”Aliongea Prisila huku akiona kabisa Hamza kuna vitu anaficha , mwanamke huyu kuna muda alikuwa akiwaza imekuwaje Hamza ndio ambae alikubali malipo kwa kuwa boyfriend feki , maana yeye ndio alibandika lile Tangazo. “Imekuwaje mara baada ya kuona tangazo kule kwenye mtandao ukaamua kutuma ujumbe wa kuwa tayari?”Aliuliza Prisila na kumfanya Hamza kucheka.
“Kama nitakuwa na jibu basi naweza kusema baba yako alichangia kwa kiasi kikubwa”
“Nini, Baba yangu, kivipi?”Aliuliza Prisila kwa mshangao , alikuwa akijua Hamza alikuwa chini ya profesa Singano ambae ni baba yake chuoni.
“Unajua tokea niujue mtandao wa JamiiFroum , nimekuwa nikipenda sana kusoma maoni ya hapa na pale wakati ambao nakuwa sina kazi , sasa siku naona lile Tangazo siku iliofuata baba yako ndio alifundisha kuhusu shauku”Aliongea Hamza akiwa na tabasamu.
“Kwahio ulikuja PM kwasababu ulikuwa na shauku ya kujua kama aliebandika tangazo yupo siriasi?”Aliuliza a Hamza alitingisha kichwa na kumfanya Prisila kutabasamu.
“Mimi sio mtumiaji sana wa mtandao wa JF , ila baba ni mtumiaji mkubwa na ameanza kuutumia muda mrefu tu”
“Unaonekana kabisa , mtandao wako pendwa utakuwa ni Insta na Tiktok?”
“Mimi napendelea Insta na Linkedin , sina akaunti Tiktok ila muda mwingine natumia”Aliongea na kumfanya Hamza kuelewa.
“Ila mpaka Regina kukupa kazi ya kumtafutia mchumba feki , inaonekana anakuamini sana?”Aliuliza Hamza.
“Sio kuniamini tu namwamini pia , Regina sijafahamiana nae kazini , tulicheza wote tukiwa wadogo?, nimeweza kumfanya rafiki licha ya tabia yake yake ya kupenda kuwa peke yake , nakumbuka hakuna ambae aliweza kufanya nae urafiki kati yangu wakati analetwa na babu yake, alikuwa mpole mno na Bibi Mirium ndio alikuja kwetu kuniomba nicheze na Regina kumchangamsha”Aliongea Prisila akiwa katika tabasamu kana kwamba anakumbuka matukio ya utoto.
“Ulifanya kazi kubwa kwelikwel?”Aliongea Hamza na kumfanya Prisila kucheka sana kana kwamba anajua anachomaanisha.
“Ndio maana siwezi kuondoka katika kampuni ya Dosam , kwasababu ni mimi pekee ambae anaweza kunifungukia kuhusu anachojisikia”.
“Namini nikuulize swali , ilikuwaje katika wote waliotuma maombi ukachagua jina langu?”Aliuliza Hamza.
“Niseme tu licha ya watu kutoa lugha chafu katika maoni yao lakini kulikuwa na maombi zaidi ya mia tano?”Aliongea
“Zaidi ya Mia tano!?”Aliuliza Hamza na palepale alijikuta akicheka.
“Ndio , hata mimi nilishangaa na nilikesha sana kupitia”
‘Sasa ilikuwaje ukanichagua mimi?”
“Regina ndio alikuchagua , ukweli ni kwamba aliangalia nani aliandika ujumbe mfupi zaidi na unaoeleweka na ulikuwa ni wa kwako na akaniambia niwasiliane na wewe niweke miadi, alionekana kuwa na uhakika utamfaa, nadhani ilipangwa lakini kila nikifikiria ni uchizi unajua siku Regina alivyoniambia nimtafutie boyfriend feki”Aliongea huku akianza kucheka na kumfanya kupendeza mno, Prisila alionekana kujiachia mno mbele ya Hamza kiasi kwamba alijishangaa.
Mpaka wanakuja kutoka walitumia saa moja kamili na Hamza kwasababu hakuwa na usafiri ilibidi aite Uber mpaka mawasiliano ili achukue gari yake hivyo aliagana na Prisila ambae anaishi Makongo juu.
****
Upande mwingine ndani ya gari aina ya Porche Cayenne, Bahati na Lidya walikuwa ndani .
Ukweli ni kwamba kitendo cha Hamza na Prisila kuondoka ni kama ile vibe ilipotea na kufanya hata bosi Side kukosa mudi ya kuendelea hivyo kila mtu alitawanyika.
Sasa wawili hao walikuwa wakirudi nyumbani na walikumbana na foleni ya magari mengi barabarani kuliko isivyokawaida na kufanya waonyeshe kukosa uvumilivu.
“Hivi nini kinaendelea kuhusu yule
Hamza?”Aliuliza Lidya huku akiwa amekunja uso
.
“Haijalishi kilichotokea , ilikuwa ni makosa yako kuanza kumdharau tokea mwanzo na kuniweka katika hali tatanishi namna ile , ki ufupi leo tumedhalilika sana”Aliongea Bahati
“Kwa misingi gani unanibebesha lawama zote mimi , usijione mtakatifu sana wakati muda wote ulikuwa ukimkodolea macho Prisila unadhani sijaona , kama umempenda si useme tu?”Aliongea Lidya kwa hasira.
“Unaongea upuuzi gani hebu acha kubadili topiki”Aliongea Bahati
“Sikia bahati usije ukanionyeshea dharau ukidhani nimekosa soko , naweza kuolewa muda wowote , wapo wanaume kibao wanaonitaka , halafu kama sio mimi usingeweza hata kukaa meza moja na Side”Aliongea Lidya huku akionyesha maringo.
Upande wa Bahati aliishia kumdharau kimoyomoyo Lidya na alikuwa akijiuliza kama kuna uwezekano wa wao kuendelea na swala lao la ndoa au ndio mahusiano yao yamefika mwisho , ukweli hakuona uwezekano wa kuweza kuishi na mwanamke kama Lidya, mwanzoni alimtongoza kwasababu aliona kuna ukaribu kati ya Lidya na Side lakini baada ya kilichotokea leo kwa Side kumpotezea alimdharau zaidi Lidya na moyo wake ulizidi kubadilika mara baada ya kumuona Prisila, akili zake zilimwambbia kabisa anahitaji mwanamke kariba ya Prisila, mstaarabu ambae hababaishwi na vitu vya kupita.
Wakati akiendelea kuwaza namna ya kumalizana na Lidya , kioo cha gari kiligongwa kwa nje na kufanya Lidya na Bahati wote kugeuka na kuangalia na walishangaa mara baada ya kuona sura ya polisi
“Ndugu afande kuna tatizo gani?”Aliuliza Bahati.
“Simamisheni gari pembeni , nahitaji kuwahoji”
“Kutuhoji! , kuna kosa lolote ambalo tumefanya?”Aliuliza Bahati kwa mshangao.
“Sio kuhusu nyie , tunafanya uchunguzi juu ya mwanaume anaefahamika kwa jina la Hamza Mzee, nadhani mnaweza kutusaidia kwa kujibu maswali yetu mawili matatu”Aliongea Polisi yule na kumfanya Lidya na Bahati kuangaliana na mwishowe walikubaliana.
Kitu ambacho hawakujua ni kwamba kila mtu ambae alifika katika hoteli ile ukimtoa Prisila alihojiwa na polisi hao , lakini ukweli ni kwamba sio polisi bali ni watu waliovalia mavazi ya kipolisi.
Kitendo cha polisi kuwahoji kiliwafanya waone kabisa kuna kitu ambacho kinaendelea katika maisha ya Hamza na jambo hilo liliwafanya kuwa na waswasi nae.
******
Upande mwingine katika moja ya Bar iliokuwa ikipatikana ndani ya eneo la Masaki alionekana Chriss akibugia bia mfululizo kama hana akili nzuri huku macho y ake yakiwa mekundu.
Pembeni yake alikuwepo Amosi Jasusi mstaafu ambae alikuwa akimwangalia Chriss kwa macho yaliokuwa na mashaka.
“Bwana Chriss nadhani kwa hali hii hatuwezi kuendelea na maongezi yetu”Aliongea Amosi.
“Sikia Jasusi bado sijalewa tunaweza kuongea , niambie uchunguzi wako umefikia wapi?”Aliongea Chriss huku akiongea kwa sauti ya juu kiasi cha kumfanya Amosi kugeuka na kuangalia nyuma kama kuna watu wamesikia kauli yake.
“Nimepoteza muda wangu kuja hapa , ukiwa sawa kiakili tutaongea”Aliongea Amosi huku akisimama kuondoka.
“Sikia Mzee Amosi nishasema sijalewa bado , akili yangu inafanya kazi , au na wewe pia unanidharau , mimi sijalewa kaa chini tuongeee”Aliongea kwa nguvu lakini Amosi alijua kama akiendelea kubakia katika eneo hilo basi siri ya uchunguzi anaofanya itabumbuluka hivyo maamuzi ni kumuacha.
“Prisila nitamfanya mbaya huyo boya uliemtambulisha leo , Mimi ndio Chriss Gabusha, uwezo ninao na nia ninayo , Ma**na zako Prisila unaniumizaje kiasi hichi , ni mwaka wa ngapi huu nimekufuatilia na kutaka uwe wangu….”Chriss aliendelea kuongea kwa hasira kiasi kwamba watu walishaelewsa bwana huyo alikuwa ametoswa , wanawake waliokuwa hapo ndani ambao walikuwa wkaimfahamu Chriss walishangaa na kujiuliza ni mwanamke gani anaweza kumuumiza mwanaume
mtanashati na tajiri kama Chriss , lakini licha ya maswali yao huo ndio ukweli kwamba ametoswa , Prisila hakuwa akimpenda na hicho ndio kilichomuumiza maana alikuwa amemfuatilia msichana huo kwa miaka miwili mfululizo bila ya mafanikio.
Sasa habari za Prisila kumtambulisha mpenzi wake katika kusanyiko lao zilimfikia kutoka kwa Saidi huku akienda mbali kumwambia mtu ambae ametambulishwa anaonekana kuwa na ukaribu na Yulia, huku akimbeza kwa kumtania kwamba maneno yake yote yalikuwa ni bure , Side alifanya hivyo kwasababu alikuwa akimpenda pia Prisila na alikuwa na kinyongo na Chriss ambae alimuona kama mwanakauzibe.
Muda huo wakati bwana huyo akiendelea kufakamia kilevi Alex na James waliweza kuingia na kusogea katika meza aliokaa Chriss huku wakimwangalia kwa mshangao na kisha waliangaliana.
“Chriss hebu punguza kunywa bwana , unajiabisha ujue”Aliongea Alex huku akimpokonya Chriss chupa ya Whiskey.
“James , yule boya wako aliekuchukulia mwanamke wako amemchukua na wangu”Aliongea Chriss na kumfanya James kushangaa.
“Chriss unamaanisha nini , ongea vizuri nikuelewe?”
“Nimesema boya wako kamchukua na demu
wangu fullsto…p”Aliongea na dakika ileile alijilaza kwenye meza na haikueleweka alikuwa usingizini au pombe zimemzidia na kupoteza fahamu.
“Anamaanisha nini huyu mpuuzi?”Aliuliza James na kumfanya Alex kutingisha mabega.
“Mimi najuaje , hebu tumbebe tumrudishe home”Aliongea Alex na James alikubali na walianza kumkokota Chriss na kumtoa ndani ya Bar hio.
Upande mwingine mara baada ya Amosi kutoka ndani ya Bar ile akiwa ameshindwa kuongea na Chriss aliingia kwenye gari lake kama kawaida , lakini sasa kitendo cha kuvuta pumzi alijikuta akinasa harufu ya marashi ambayo imeongezeka ndani ya gari yake na palepale alihisi hatari lakini hata hivyo alichelewa kwani kabla hata ya kugeuka alijikuta akifunikwa na Helmet zito kichwani na kumfanya kukosa pumzi na kupoteza fahamu.
******
Hamza akiwa njiani kuelekea nyumbani aliweza kupokea simu kutoka Amiri rafiki yake akimuulizia juu ya lile swala la lugha na Hamza ukweli ni kwamba hakuweza kulipatia ufumbuzi kabisa.
Amiri upande wake anasema Mellisa anazidi kubadilika kitu ambacho kinampa mawazo , ijapokuwa hakuongea anabadilika kivipi lakini Hamza alielewa na kuona ngoja alifanyie kazi.
Baada ya kufika nyumbani aliweza kugundua nyumba yote ilikuwa kimya ikiashiria hakukuwa na mtu nyumbani , ilikuwa ni bahati tu Hamza alikuwa na kadi pamoja na nywira za kufungulia mlango hivyo hakupta shida ya kuingia ndani.
Mara baada ya kuingia katika chumba chake tu , jambo la kwanza alilofanya ni kuwasha laptop aliopewa na Regina na kisha alihamisha lile faili la Amiri kutoka kwenye simu yake na kulituma kwa njia ya Email kwenda kwa barua pepe ambayo aliijua yeye.
Baada ya kufanya hivyo alijiunga kifurushi cha kimataifa na kuingiza namba ya nje ya nchi na kupiga simu na hazikuchukuwa dakika nyingi sauti ya mwanamke aliekuwa akitumia lugha ya Kiswedish ilisikika.
“My Prince hatimae umenitafuta baada ya kimya cha muda mrefu”Sauti ilisikika hivyo huku ikionekana upande wa pili alikuwa akijaribu kuzuia hisia zake.
“Niwie radhi sana Sally sio makusudi”Aliongea Hamza akiwa na tabasamu kana kwamba alifurahia kusikia sauti hio.
“Haina haja ya kuomba radhi najua umechoka na ulihitaji kupumzika”
“Naomba radhi kwa kukuachia matatizo na kufanya uyafanyie kazi , utakuwa umechoka sana kurekebisha makosa yangu”
“Sio kweli , kuniamini kwako na kuniachia familia yako niiangalie ni heshima kubwa kwangu, kwanini nichoke?”
“Huwa navutiwa sana na ukamilifu wako , ni wewe pekee ambae najua unaweza kunisaidia mambo mengi , vipi hali ya ndugu zangu?”Aliuliza Hamza.
“Kila mtu yupo bize na mambo yake , wewe ndio uliwaambia wasikutafute na wamejitahidi kupotezea mawazo ya kukumbuka kwa kujiweka bize , kila mtu yuko sawa..”Aliongea na kumfanya Hamza kucheka kidogo
“Ungenifuata pengine sasa hivi ungekuwa na maisha magumu sana , angalau kuwa nao karibu kunakufanya upumue”
“Ukiongea hivyo unakosea , maisha yangu yote natamani kuwa karibu yako katika mazingira yoyote yale”Sauti ilisikika na kumfanya Hamza kutoa tabasamu la uchungu.
“Anyway , nimekutafuta kwasababu kuna kitu nataka ujaribu kukifanyia uchunguzi?”
“Nielekeze tafadhari”
“Nimetuma faili la sauti kupitia barua pepe yako , hebu sikiliza lugha iliotumika nataka kujua ni sehemu gani duniani wanazungumza lugha hio , nitafute ukiwa na majibu ya uhakika”Aliongea
“Hakuna shaka nitampa kazi mtu wa lugha kufanyia kazi , naamini mpaka wewe kushindwa kuijua hio lugha basi itakuwa ni ngeni kwenye masikio yako”
“Nadhani umenielewa , Sally nashukuru kwa kila unachofanya kwa ajili yangu..”Aliongea Hamza na hakusbiri jibu upande wa pili na hio ni mara baada ya kusikia sauti za viatu kutoka chini.
Hamza mara baada ya kushusha pumzi na kujituliza alitoka kwenye chumba chake na kushuka chini sebuleni , ilikuwa ni kama alivyohisi Shangazi na Regina walikuwa wamerudi.
Kilichomshangaza Hamza ni kwamba baba yake Regina na mke wake walikuwepo pia na walikuwa wakisukuma kiti cha magurudumu ambacho kimekaliwa na mwanamke mzee.
Bibi huyo licha ya kuonekana kuwa mzee lakini alikuwa na muoekano wa hadhi. Licha ya sura yake kujikunja lakini mpangilio wa uso wake ilionyesha alikuwa ni mwanamke mrembo wakati wa ujana wake.
Hamza hakuwa na haja ya kujua bibi huyo ni nani , alijua fika atakuwa ndio bibi yake Regina, hivyo alimsogelea na kumsalimia.
“Nimefurahi kukutana na wewe bibi , jina langu
naitwa Hamza mzee , Mpenzi wa
Regina”Alisalimia bila ya kumjali mzee Wilsoni na mke wake.
“Kwahio wewe ndio Hamza , sio mbaya , sio mbaya , unaonekana kuwa mtoto mzuri , ushakula chakula cha usiku?”Aliuliza. “Ndio bibi , vipi wewe umeshakula?”
“Wote tumekula”Aliongea na kumfanya Hamza kutingisha kichwa na alisimama na kumwangalia Regina.
“Vipi hali ya bibi , mbona anaonekana kuchoka sana?”
“Sijachoka kabisa , baada ya kuona ni kweli Regina kapata mchumba nimefurahi mno , sijachoka kabisa”Aliongea.
Upande wa Regina alijikuta akizungusha macho yake mara baada ya kuona namna Hamza alivyokuwa akiongea na bibi yake bila wasiwasi.
“Bibi unapaswa kupumzika mapema , kesho utaendelea kufanyiwa uchunguzi wa afya yako”Aliongea Regina.
Kiasili familia ya walikuwa wakiishi Mkoani Tanga Wilaya ya Bumbuli, ni umbali mrefu kidogo mpaka mpaka kufika Dar es salaam , hivyo kwa mzee kama huyo atakuwa amechoka sana.
“Regina kwanini unataka kunipumzisha mapema
,bibi yako nataka kuongea kidogo na Hamza”Aliongea
“Mtoto masikini kama huyu utaongea nae nini?”Aliongea Lamla.
“Wewe Lamla unaongea nini , baba mkwe wako alikuwa masikini pia wakati akianza kufanya biashara kutoka chini , kwahio unanidharau na mimi kuolewa na mwanaume masikini?”Aliongea na kumfanya Lamla uso kumuiva.
“Mama sijamaanisha hivyo?”
“Miaka mingi imeenda lakini sioni mabadiliko yako , Vipi kwanza Frank anafanya nini siku hizi?”
Alikuwa akiulizia mdogo wake Regina yaani mtoto wa Lamla na Mzee Wilson, na swali lile lilimfanya Lamla sura kuwa mbaya.
“Frank yupo bize siku hizi kufanya Research yake , ndio maana hajaweza kufika ndani ya muda”Aliongea
“Mtu sio kama anasomea nje ya nchi , yaani hapo UDSM tu ameshindwa kuja kumsalimia mtu alietoka Tanga?”Aliongea huku akionyesha kutoridhika kabisa.
“Hapana mama , ni kwamba tu yupo bize ,kila siku anasema atakuja kutembelea lakini imekuwa ngumu kutokana na ratiba za chuoni”
“Hebu acha kumtetea , lini alikuja kunisalimia, inamaana hata kupiga simu kumshinda?, kwanini anashindwa kuwa na tabia ya Regina , licha ya umri mdogo lakini ameweza kuendeleza alipoishia babu yake na kuwa bosi wa kampuni lakini bado anapata muda wa kunitafuta”
“Mama nitamrekebisha Frank , hajui hata anachofanya kama anakosea”Aliongea Mzee Wilsoni.
“Mnaweza kuondoka sasa , nitalala hapa nyumbani kwa Regina”Aliongea
“Mama , hebu fikiria vizuri , tumeshakuandalia chumba chako cha siku zote”Aliongea Mzee Wilsoni kwa uchungu.
“Nimekuja Dar mwenyewe na nitaishi ninapotaka kuishi , rudini nyumbani mkamuadabishe mtoto wenu”Aliongea akiwa siriasi na kwasababu walimjua hakawii kukasirika , Mzee Wilsoni na mke wake walishia kumwangalia Regina kwa dakika na kisha wakaondoka.
“Mariposa hebu nipeleke chumbani kwangu”
“Sawa Madam”Aliongea Shangazi na kumwendesha bibi kuelekea katika chumba chake Kulikuwa na chumba kikubwa cha Master floor ya kwanza , ni kwa ajili ya wageni lakini kutokana na kwamba ni ngumu kumpandisha juu hivyo chumba hicho kilimfaa bibi yake Regina.
“Dokta Ronicas hajakuambia ni wapi tunapaswa kuonana nae kwa ajili ya kuonana na bibi?”Aliuliza Regina.
“Ni hospitali ya Muhimbili , kaalikwa kutoa hotuba kwa wanafunzi katika chuo cha MUHAS, baada ya hapo ataingia hospitalini”Aliongea Hamza na kumfanya Regina kumwangalia kwa maswali.
“Asante kwa hili?”
“Huna haja ya kunishukuru , isitoshe tunakaribia kuzeeka ndani ya ndoa yetu”Aliongea Hamza akijaribu kumtania.
“Unaongea upuuzi gani , nani anakaribia kuzeeka?”Aliongea huku akimkodolea Hamza na kujiambia kadri wanavyozidi kuzoeana ndio ambavyo Hamza anazidi kushindikana.
Muda huo Shangazi aliweza kutoka na kuwaita Hamza na Regina.
“Regina na Hamza mnaitwa , Bibi yenu anataka kuongea na nyie”Aliongea na kufanya Hamza na Regina kushangaa , Regina alijiuliza ni kitu gani ambacho bibi yake anataka kuongea maana ni kama wameongea kila kitu njia nzima.
Baada ya kuingia Bibi Mirium alikuwa ameshalala tayari na alionekana kuchoka.
Kwa kuangalia tu Hamza aliweza kuona bibi huyo yupo katika hatua za mwisho za ugonjwa wake.
Ijapokuwa hakuwa daktari lakini alijua fika kwa hali ambayo amefikia hakuna kitu ambacho Flora anaweza kufanya kumtibia, labda kuwe na teknolojia mpya.
“Bibi kwanini usipumzike kwanza ni kitu gani unataka kuongea?”Aliuliza Regina akikaa pembeni ya kichwa cha bibi yake.
“Sidhani kuna haja ya mimi kupumzika haraka haraka , isitoshe ninakwenda kupumzika kwa muda mrefu siku chache zijazo”
“Bibi usiongeee hivyo , hakuna kitakachokutokea , kesho utakutana na Dokta Ronicas , ni dokta namba moja dunia nzima anaeaminiwa hata kutibia wafalme , nina uhakika ataweza kukuponyesha”Aliongea Reigna lakini Bi Mirium hakuona haja ya kuongea zaidi na alimshika mkono Regina.
“Kama kweli unataka niishi japo kwa siku chache , unapaswa kunipa tumaini…”
“Nipo tayari Bibi , ni kipi nifanye?”
“Nataka muoane haraka iwezekanavyo , nikishaona umebeba ujauzito sitotaka kuondoka kwa haraka mpaka nimuone mjukuu wangu ili
nikikutana na babu yako niwe na stori nzuri ya kumwambia”Aliongea
Comments