SEHEMU YA 46.
Regina mara baada ya kuisikia hio kauli uso wake ulipata moto kwa aibu maana ni kama kitu ambacho hakutegemea.
“Bibi unaongea nini , mimi siwezi kuolewa nae?”Aliongea Regina
Hamza hata yeye alikuwa kwenye kuchanganyikiwa , hatua hio aliona ni ya haraka sana , isitoshe hata mwezi haujaisha tokea afahamiane na Regina.
“Hutaki kuolewa nae , kwahio umetafuta boyfriend wa kucheza na akili yangu ili niridhike au ni kama alivyosema Lamla, Hamza ni mpenzi wako feki”
“Sio hivyo bibi , mimi na Hamza ni kweli ni wapenzi”Aliongea Regina kwa kusita sita.
“Kama ndio hivyo nataka muone , sio lazima ya sherehe , kwasababu Hamza ni muislamu na wewe ni mkristo mnaweza hata kwenda kuandikisha ndoa yenu bomani na kuanza kulala pamoja , mkishaona nimekufa mnaweza kuachana kama hampendani”Aliongea
Regina alishikwa na wasiwasi mkubwa mno na aligeuka na kumwangalia Hamza lakini kwa bahati mbaya alikutana na uso uliokuwa na tabasamu zito na kujiambia hili lipuuzi mbona linatabasamu, au ndio mpango wake kutaka kunioa kwa muda mrefu, Regina alijihisi kichaa kinakwenda kumshika.
“Bibi hali yako sio nzuri kwasasa , kwanini tufunge ndoa wakati wewe unateseka , tusubiri ukishapona tutaanza kufikiria swala la ndoa”Aliongea Regina akijitahidi kutafuta kisingizio cha aina yoyote ile ili kumtuliza bibi yake.
Ukweli ni kwamba hakuwahi kuwaza kuolewa na Hamza na sio hivyo tu hakuwaza ingekuwa mapema hivyo baada ya bibi yake kuija Dar kitu cha kwanza anachotaka ni kuona ndoa, yaani ilionekana mzee huyo hajaja kupona bali kumuozesha.
“Hivi unadhani na huu uzee wangu pamoja na kuumwa akili yangu haifanyi kazi , usisahau ni mimi na babu yako tuliopigania kampuni ya Dosam imesimama, hata kama nimekuwa mzee huwezi nidanganya kirahisi”Aliongea na kumfanya Regina kuonyesha muonekano wa kukosa kujiamini.
“Bibi nathubutu vipi kukudanganya?”
“Regina usisahau hisa asilimia hamsini na moja unazoshikilia therathini na mbili ni za kwangu na kumi na tisa ndio zako , hisa zangu ni nyingi hata uunganishe na saba za baba yako”Aliongea.
“Bibi najua hilo..”
Upande wa Hamza ndio kwanza alianza kushangaa , ukweli siku zote alijua Regina ndio mwenye hisa nyingi ndani ya kampuni lakini kumbe ni bibi yake ndio mmiliki mkubwa wa kampuni , sasa ndio anajua bosi mwenyewe wa kampiuni ya Dosam ni Bi Mirium.
“Asilimia kumi na tisa jumlisha asilimia 32 ya hisa zangu jumla yake ni hamsini na moja , hii ndio maana halisi ya kuwa bosi wa kampuni ya Dosam na kuwa na nguvu , wakati babu yako anafariki aliweka wazi katika wosia wake ukiweza kuolewa na kuanzisha familia yako ndio nitakukabidhi moja kwa moja asilimia zangu zote , sasa kama hutaki kuolewa nitampatia baba yako hisa zote therathini na mbili na ndio atakuwa mmiliki halali”Aliongea.
“Bibi!!?”
Regina alijikuta akishangazwa na maamuzi ya bibi yake na kuishia kukunja sura.
“Bibi sio kama nina tamaaa sana lakini wewe mwenyewe unajua baba hana uwezo wa kuiendesha kampuni , isitoshe kama akisikia hivi nina uhakika mtu mwenye nia mbaya atazikwapua hisa zote na kampuni kutoka nje ya umiliki wa familia”
“Unadhani kwa umri huu najali sana hela , kwangu vitu na hela havina maana sana , ukifikia umri wangu utajua ninachomaanisha , sababu babu yako kuacha wosia ule ni kwasababu anataka uwe na familia, kwasababu ndio kitu pekee ambacho kinaweza kukufanya kuwa na furaha na kuvumilia yote, wewe mtoto kwanini huelewi , kila kitu ni kwa ajili yako lakini unashindwa kukubali , babu yako anachotaka ni familia kuongezeka na amenisisitizia hilo na ndio ninachotaka kuona kabla sijaaaga”Aliongea na kumfanya Regina kushangaa , hakuamini babu yake Dosam alikuwa na mpango huo kichwani.
“Sikutaka kukulazimisha swala la kuolewa kwasababu nilitaka wewe mwenyewe utafute mtu unaempenda bila ya kujali hali yake ya kimaisha wala dini , ndio maana hata baba yako aliposema anataka uolewa na mtoto wa mzee Benjamini sikuongea chochote , sasa Hamza huyu hapa umemtafuta mwenyewe lazima nihakikishe mnafunga ndoa, au nimekosea, mimi sijakulazimisha kuolewa na mtu usiempenda , si umesema mwenyewe Hamza ni mpenzi wako
?”Aliongea mzee huyo , ilikuwa ni kama vile ndio misheni yake ya mwisho anayotaka kuikamilisha kabla ya kufunga ndoa,
Regina alijikuta akikosa neno la kuongea , alitamani kusema Hamza sio mpenzi wake lakini hakuwa akiweza kufanya hivyo na kumfanya kutamani kulia , isitoshe alijua Hamza ana mpenzi wake hivyo asingemlazimisha kuolewa nae.
“Halafu ili uelewe vizuri kabla ya kufanya safari ya kuja hapa nishaongea na mwanasheria kwa ajili ya kuandaa nyaraka za kusaini , muda wa kupoteza sina ni aidha iwe sahihi yako au ya baba yako ,
kila kitu kinategemeana na maamuzi yako na Hamza mtakayoamua”
Mara baada ya kuongea kauli hio alifumba macho yake na kujifunika vizuri shuka akionekana kabisa hakutaka kuendelea kuongea.
Regina kihasira hasira alienda mpaka kwenye chumba chake cha kujisomea na Hamza alifuata nyuma nyuma.
“Regina inamaana ni kweli tunakwenda kufunga ndoa?”Aliuliza Hamza kizembe.
“Ndio unachotaka?”
“Sijamaanisha hivyo , siwezi kufunga ndoa na wewe mimi,, nadhani unajua hilo vizuri”Aliongea Hamza lakini maneno hayo hayakuwa na radha nzuri
kabisa kwenye masikio yake, alijihisi kuumia kuona Hamza hakuwa hata na wazo la kumuoa.
“Kwannini unaongea hivyo , unaonekana kutonipenda kabisa, nachukiza sana?”Aliongea Regina huku akizidi kuwa kauzu.
“Sio hivyo , unajua wewe ni mrembo sana na pia ni mwanamke tajiri , ni bahati sana kuweza kupata mwanamke wa aina yako..”
“Hebu acha kuongea , mpaka sasa hata sijui nani ni rajiri zaidi kati yetu”Aliongea , Regina hakusahau Hamza alikuwa akivaa mavazi ya bei ghali mno ambayo hajawahi kuyavaa kwenye maisha yake licha ya kutambulika kama mwanamke tajiri.
“Isitoshe hata huyo Master Alex fundi wako simfahamu vizuri , bado kuna Dokta Ronica ambae siwezi hata kula nae sahani moja”
“Bosi Regina hebu acha kunishangaza , mimi nipo chini yako ?”
“Nani unamaanisha haswa?”
“Utajua mwenyewe kama hujaelewa “Aliongea Hamza , hakuwa kabisa na mpango wa kujibishana nae , lakini kwa wakati mmoja alijikuta akifurahia ndani kwa ndani , sio kwamba alifurahia kwasababu ya pendekezo la Bibi Mirium , ila ni kwasababu hakujua ni maauzi gani ambayo Regina na ukauzu wake atayachukua, alitaka kusoma mchezo hadi mwisho utakavyokuwa. “Hebu ondoka kwanza nataka kufanya kazi”
“Bado unataka kufanya kazi , umekuwa bize siku nzima kwanini usipumzike”
“Jali mambo yako , Tokaa!”
Hamza alishia kujisikitikia na kutoka kisha akafunga mlango , ukweli ni kwamba kila ambacho alikisioma mtandaonni kuhusu Regina alikuwa akikishuhdia katika mazingira halisi.
Regina alitambulika mtandaoni kama mfanyabishara katili likija swala la kutengeneza pesa na ndio ambacho alikuwa akiona na wengi walitafsiri hivyo na kuna wengine ambao walienda mbali na kuwaza Labda Regina alikuwa ametengenezwa na Mzee Dosam kuwa roboti la kutengeneza pesa.
Hamza aliishia kumuonea huruma na kujiwazia kama kampiuni itakuwa katika mikono ya baba yake moja kwa moja itamilikiwa na Lamla na familia ya James na ikifikiria hatua hio Regina atakuwa katika hali gani.
*****
Upande wa chumba cha Bibi Mirium , Shangazi alikuwa akimfunika vizuri
“Madam natoka kwenda kupumzika sasa , uwe na usiku mwema”Aliongea.
“Mariposa hebu niambie , unadhani Hamza anao uwezo wa kumlinda Regina?”Aliuliza na kumfanya Shangazi kugeuka.
“Ndio nina uhakika asilimia mia , ijapokuwa sijui ametokea nchi gani na ni nani haswa lakini kwa kipindi chote nilichomfuatilia , sio mtu mwepesi”
“Kwa uzoefu wako tokea ukiwa kitengoni mpaka sasa , kama umesema sio mtu mwepesi basi naaamini asilimia mia, mimi ndio nishazeeka hivyo , wasiwasi wangu Wilsoni na Regina watapata shida sana , wakati Mzee Dosam ananiambia nisije kumchagulia Regina mume na mtu wa kwanza atakaemchagua nihakikishe wanafunga ndoa nadhani naanza kuamini alichokuwa akimaanisha , huu ni muongozo alionipatia na naona umekuja nikiwa siku zangu za mwisho”
“Lakini madam licha ya kwamba Hamza anaonekana kuwa na uwezo lakini anaonekana kuwa na matatizo kidogo , labda ila sina uhakika..”Aliongea Shangazi akisita sita.
“Unamaanisha nini?”
“Kwa uchunguzi wangu wa kimya kimya nilioweza kufanya nimeweza kugundua yupo kwenye mahusiano ya kimapenzi na Eliza , mpaka sasa nashindwa kujua kama Regina anafahamu hilo”
“Unamaanisha huyu Eliza mtoto wa mzee Mlowe?”
“Ndio”
“Haha.. Hii inaonyesha ni kwa kiasi gani Eliza amekuwa vizuri licha ya changamoto alizopitia , huyu Hamza inaonekana ana jicho la kuona mbali yule mtoto anafiti kila idara, lakini kama anataka kuendelea kuwa na Hamza lazima akubali baadhi ya ndoto zake kutotimia”Aliongea.
“Madam unamaanisha..”
“Wanaume siku zote ambao wana uwezo mkubwa , hawajawahi kuwa waaminifu , Dosam mpuuzi yule alinisaliti mchana kweupe bila hata ya kujutia , nadhani unajua ninachomaanisha Mariposa”Aliongea lakini kauli ile ilimfanya Shangazi kupiga magoti mara moja.
“Madam samahani sana haikuwa nia yangu…”
“Inatosha sasa , wote tushazeeka sasa , japo mimi ndio naonekana kizee wewe bado kijana , mbinu yako imefanya kazi nadhani ndio maana Dosam alikupenda , lakini hayo yamepita kwasasa tumekuwa kama dada, huna haja ya kuomba msamaha wakulaumiwa ni Dosam sio wewe,ila bora alikupenda wewe ndio maana sikuwa na tatizo , ingekuwa ni mwanamke mwingine ningeachana nae mara moja”Aliongea Bi Mirium. “Asante sana kwa kuniona mtu mzuri”
“Kuhusu huyu Eliza muda si mrefu nitaonana nae na kumfanya anitambue mimi ni nani , kuhusu Hamza kama uwezo anao sio kosa lake kuwa na wanawake wawili watatu, isitoshe unajua fika Regina sio rahisi kudii nae hususani ugonjwa wake ukiamka, kama akikubali kuolewa na Hamza naamini atakuwa na njia zake za kudili na michepuko ya Hamza, hili ni swala ambalo sisi tulioishi muda mrefu hatupaswi kuingilia”
“Madam upo sahihi , na mimi naona hivyo hivyo kwasababu ni watu wazima watafanya maamuzi yao wenyewe”
“Mariposa hebu simama acha kuendelea kupiga magoti , nakutegemgea siku za usoni wewe ndio utakuwa mlinzi wa mtoto wangu na mjukuu wangu , najua ni misheni yako kumlinda Regina kwasababu ya nafsi yake nyingine lakini mimi awe
Regina au yule mwingine wote ni wajukuu wangu.. nakuomba uhakikishe Regina anakuwa salama , ndio namna pekee ya Wilsoni kuwa salama pia”
“Madam mimi Iris nitaulinda ukoo wako mpaka hatua ya mwisho ya uhai wangu”Aliongea Shangazi akijiita Iris huku akikakamaa kama mwanajeshi.
****
Hamza mara baada ya kurudi kwenye chumba chake alimtafuta kwanza mpenzi wake Eliza na kumuulizia swala la mama yake lilivyoenda.
Eliza alionekana kuwa na furaha mno akisema kwamba Dr Ronica kamhakikishia mama yake anaweza kupona na kurudi katika hali ya kawaida na mtu ataagizwa kuja Tanzania kwa ajili ya kusafiri nae kwenda nje ya nchi.
Eliza pia alikuwa ashafanya utafiti wake na kujua
Dr Ronicas anatokea Mayo Medical Center kutoka Rochester Minnesota , akiwa kama daktari namba moja katika hospitali hio yenye matawi Marekani nzima lakini pia namba moja dunnia nzima.
Sasa mara baada ya kujua Dokta Flora Ronicas ndio Dean wa hospitali hio ya chuo na pia CV yake kwa ujumla alijikuta akishangaa na hakuwaza kabisa siku moja mama yake anaweza kutibiwa na mtu mzito kama huyo , ilimfanya kujawa na shauku ya kutaka kumjua Hamza mara moja.
*******
Hakujua hata ametumia masaa mangapi tokea apoteze fahamu , lakini mara baada ya kushituka aliweza kujua alikuwa katika chumba ambacho kilikuwa ni kama hospitali.
Amosi alijikuta akivuta kumbukumbu zake vizuri na kujiuliza ni nani ambae amemkamata kwa kumzimisha na kumleta katika eneo hilo ambalo lilionekana kama hospitali lakini kwa upande mwingine lilionekana kama maabara.
Alikuwa amefungwa katika kitanda ambacho mara nyingi aliviona katika filamu za kisayansi , juu yake kulikuwa na kitu kama helmeti ambalo lin vidole vilivyokuwa katika muundo wa chuma , ilikuwa ni kama roboti na ni harufu hafifu tu ndio iliompa nafasi ya kuona eneo hilo sio la kawaida hata kidogo.
Kutokana na kufungwa vizuri hakuweza kukagua eneo lote kwani hakuweza kuangalia nyuma , vitu ambavyo aliweza kuona ni mbele yake na kulia na kushoto kwake.
Alijaribu kufurukukta lakini ilikuwa ni ngumu mno kujitoa, alikuwa amefungwa na chuma na sio pingu.
Alijikuta akiishia kutoleta ukinzani na hio ni mara baada ya kuona kuna Kamera ambazo zilikuwa zikimmulika na moja kwa moja alijua kabisa kila anachofanya kinaonekana.
Na kweli ndani ya dakika chache alisikia mlango kuslide , ijapokuwa hakuweza kuona kutokana na kwamba hawezi kuangalia vitu vya jyuma yake lakini alihisi uwepo wa mtu.
Dakika ileile akiwa na matarajio makubwa ya kumuona mtu alieingia na kumuuliza kwanini amefungwa hapo alishangaa baada ya kuona sura ya mwanamke mrembo alievalia Hijabu , macho
yake hayakuwa yakimdanganya mwanamke aliekuwa mbele yake alikuwa ni Sister kutokana na mavazi yake.
“Sister naomba unifungue , hapa ni wapi?”Aliuliza Amosi huku akiwa na wasiwasi, ukweli ni kwamba
alijihisi hayupo Tanzania na kuna hisia zilimwambia pengine amelala muda mrefu akiwa hajitambui.
“Kuwa mtulivu Mr Amosi , kadri unavyohangaika ndio unavyojiumiza , isitoshe kidonda bado hakijapona vizuri”Aliongea Yule Sister na kumfanya Amosi kushangaa.
“Kidonda , unamaanisha kidonda gani?”Aliuliza Amosi huku akijaribu kudhibiti mwili wake kujihisi kama kuna maumivu sehemu , lakini hata sehemu ambayo alipatwa na jeraha la risasi palikuwa pashapona na hakusa na maumivu.
Sister yule alionyesha kutoa tabasamu na dakika ileile alipiga makofi mawili na kitanda alicholalia Amosi kilianza kubinuka taratibu na kumfanya akae kitako na baada ya pale kiti kile kiligeuka kama kiti cha saluni na kumgeuzia upande mwingine.
Hakukuwa na kitu cha kushangaza zaidi ya Runinga iliokuwa mbele yake, ki ufupi alikuwa wodini , utofauti ni kwamba wodi aliokuwa ilikuwa imeendelea zaidi .
“Hello Mr Amosi , naitwa Dokta Maya Thema kutoka kitengo cha tiba ya fahamu ilioendelea chini ya Sinagogu , unachokwenda kuona ni hatua kwa hatua za operesheni ya kupandikiza Chip kwenye ubongo wako bila kufungua kichwa chako , tunatumia teknolojia maalumu ambayo ina uwezo wa kutengeneza Chip ndani ya ubongo wako kwa kukuingizia mionzi isiokuwa na madhara ambayo huambatana na madini maalumu , kazi kubwa ya chip hii ni kuushitua ubongo wako na kutengeneza daraja la kimawasiliano kati ya ubongo wako na vifaa vyetu vya
kielektroniki..”Amosi alijikuta akishangazwa na
kauli ile , sauti iliokuwa ikisikika ndio ya Sister aliekuwa ndani ya chumba hicho japo kwenye Skrini alionekana kuvalia barakoa na PPE. “Sister nani anakwenda kufanyiwa hio operesheni ya kupandikizwa Chip?”Aliuliza Amosi huku akiwa na hali ya kuchanganyikiwa.
“Mr Amosi operesheni imekwisha kufanyika , unachopaswa ni kuangalia na majibu ya maswali yako yote utayapata”Aliongea yule Sister na kumfanya Amosi kugeuza macho yake kwenye Runinga.
Hazikupita dakika chache Skrini ilianza kuonyesha taaarifa za mgonjwa ambae amefanyiwa operesheni, kitu cha kwanza ambacho kilimfanya Amosi kushikwa na mshituko ni mara baada ya kuona jina lake , Amosi Sembe..”.
“Hapana , haiwezekani”Aliongea Amosi na kuanza kufurukuta kwa nguvu akitngisha kile kitanda na kumfanya yule Sister kumwangalia kwa macho ya masikitiko na palepale aliangalia Kamera na kutoa ishara flani na ni ndani ya sekunde tu Amosi alishikwa na usingizi na kulala tena.
“Tutaendelea baadae akionyesha kuukubali ukweli ,ninachowahakikishia upasuaji umeenda vizuri kwa asilimia mia moja na baada ya hapa atakuwa Agent mahili na kukamilisha misheni zenu zote”Aliongea yule Sister huku akionyesha ishara ya heshima kwa kuangalia zile Kamera , ilionyesha ni dhahiri kuna watu ambao walikuwa wakiangalia, haikueleweka Amosi alikuwa wapi.
*********
Siku iliofuata Regina na Hamza hawakuenda kazini bali walimchukua bibi yao kumpeleka hospitali ya chuo ya Muhimbili .
Kwasababu Ronicas alitarajiwa kukutana na wanafunzi wote wanaosomea udaktari na kutoa hotuba yake ilibidi wapelekwe kabisa katika upande wa wodi za watu mashuhuri kwa ajili ya kusubiri.
Bibi Mirium alitumia nafasi hio kumuuliza
Hamza kuhusu maisha yake kwa ujumla wapi alipotokea na familia yake ilipo , lakini alishia kutunga uongo ulioenda shule lakini upande wa
Bibi huyo alionekana kuamini na kuishia kufurahi.
Wakati wakiendelea kusubiri mlango ulifunguliwa na akaingia mwanaume mrefu alieenda hewani alievalia shati la mikono mirefu, alikuwa mweusi aliependeza kwa kufuga nywele zake na kuwa ndefu.
Mara baada ya kuingia tu alionyesha hali ya furaha katika uso wake na kumsogelea Bibi Mirium.
“Grandma , I missed you so much”Aliongea kwa sauti laini isiokuwa ikiendana na muonekano wake , ukweli Hamza alidhania bwana huyo angekuwa na sauti nzito lakini alivyoongea alionekana kama aina ya wale watoto walioharibiwa na wazazi wao kwa kudekezwa.
“Naona hatimae umezileta ngula zako hapa Frank”Aliongea Bibi Mirium huku akitabasamu.
Upande wa Regina kwa namna ambavyo alionekana ilikuwa ni dhahiri kabisa hakuwa na mpango wa kusalimiana na Frank.
Hamza pia ilikuwa mara yake ya kwanza kuonana na mdogo wake Regina na kwa kumwangalia tu bwana huyo licha ya kubarikiwa mwili mzuri lakini alikuwa dhaifu mno kiasi kwamba ilionyesha alikuwa akifanya sana ngono.
Frank mara baada ya kusalimiana na bibi yake alisimama na kumwangalia Hamza huku akiweka tabasamu bandia.
“Kwahio huyu ndio boyfriend wa dada yangu , Shemeji yangu sio?”Aliuliza.
“Habari yako mzee”Aliongea Hamza huku akionyesha kutotaka kuendelea zaidi kuongea nae.
“Wewe Frank ni lini utaanza kufanya intership yako ndani ya kampuni , ongea na dada yako akupatie nafasi uanzie chini kabisa”Aliongea bibi lakini kauli ile ilimfanya Regina kukunja sura , ilionyesha dhahiri hakupenda.
“Bibi mimi pia ni mwanafamilia , sidhani kuna haja ya mimi kufanya intership , unaonaje ukinikopesha bilioni mbili napanga kuanzisha kampuni ya Mutual fund”
“Yaanni huna hata uzoefu wa kufanya kazi ndani ya kampuni unataka kuanzisha kampuni?”Aliongea Bibi Mirium huku akimkodolea macho Frank. “Lakini tayari Dada ashakuwa CEO , sihitaji uzoefu kwani nina uwezo wa kuajiri watu wazoefu ambao wanaweza kuniongoza , bibi nadhani unanijua mwenyewe mjukuu wako ninaweza kujifunza haraka , sihitaji uzoefu kabisa”
“Usinione kichaa wewe mtukutu , ni aidha ukatafute kazi au ukaanze kufanya kazi ndani ya Dosam katika ngazi ya chini kabisa, unadhani dada yako amekuwa CEO kwa kupendelewa , wakati akiwa chuo ashaanzisha kampuni yake na kuipa thamani mpaka akafanikiwa kuiuza kwa Bilioni kumi na ndio tulitumia nafasi hio kushawishi wakurugenzi kumpigia kura kuwa CEO, lakini wewe ni tofauti , unachoweza ni kucheza tu na hutaki hata kutumia ujuzi na akili halafu unataka nikupe hela yote hio uongoze kampuni , unadhani mimi kichaa”Aliongea na kumfanya Frank kutabasamu kwa kufosi.
“Basi bibi yaishe , mwakani namaliza chuo , utanipa hisa zako lini?Aliongea na kumfanya Bi Mirium kumpiga konzi.
“Yaani mimi nikosiriasi unaanza kufikiria kuhusu hisa zangu , ni lini utajifunza , kama nikitoa hisa zangu itakuwa ni aidha kwenda kwa baba yako au kwa dada yako, sio zamu yako”
“Bibi unachofanya ni upendeleo , Dada anakwenda kuolewa muda si mrefu na mimi ndio mtu pekee wa kuendeleza ukoo , Da Regina tayari ana hisa kumi na tisa ila mimi hata hisa moja sina”
“Hela ya matumizi unayopewa ni zaidi ya bilioni moja , unataka hisa za nini?”Aliuliza Bi Mirium huku akionyesha hana furaha.
“Bibi..”Frank alijikuta akishindwa kuendelea kuongea zaidi na alikuwa na hasira mno kiasi cha kusugua meno yake kwa hasira.
“Basi bibi haina shida nitakusikiliza kwasasa chochote unachoongea”Mara baada ya kauli hio alimsogelea Hamza.
“Shem , unaonaje tukienda kuongea kidogo hapo nje?”Aliuliza na kumfanya Hamza kushangaa na kujiuliza huyu bwana anataka nini.
Comments