SEHEMU YA 47.
Regina pia alishangaa na kumwangalia Frank kwa ukauzu.
“Frank unachotaka ni nini?”
“Sister hakuna ninachotaka , nataka kuongea na
shemeji yangu sidhani ni tatizo , isitoshe siku zote
kuna mazungumzo ya kiume huwa yanafanyika”Aliongea huku akicheka
“Hamza unaweza kuondoka , Frandk anataka kuongea na wewe sio mbaya , isitoshe Dokta Ronica hajafika bado”Aliongea Bibi huku akijilaza vizuri kwenye kitanda.
“Wapi tunaenda kuongea?”Aliuliza Hamza. “Wewe nifuate tu”Aliongea na kisha alianza kuongoza njia.
Regina alikuwa na wasiwasi , baada ya wote wawili kutoka alimsogelea bibi yake na kumuongelesha kwa sauti ya chini
“Bibi umemuona Frank alivyo katika macho yake anachokiwazia ni hisa zako , haonekani kujali afya yako kabisa”
“Najua.. lakini vyovyote vile ni mdogo wako na ni mjukuu wangu”Aliongea na kumfanya Regina kujawa na hisia zisizoeleweka na aliishia kugeuka na kunyamaza.
Upande mwingine Frank alimchukuaHamza mpaka eneo la kuegeshea magari .
“Shem vipi tena , kwanini umenileta kote huku?”Aliuliza Hamza akiwa na tabasamu.
“F*ck you , nani shemeji yako?”Aliongea kwa hasira huku akimtolea Hamza macho.
“Wewe ndio ulieniita Shemeji wala sijakulazimisha?”
“Unakichaa , unadhani mpuuzi kama wewe masikini masikini unaweza kuwa shemeji yangu?”Aliongea huku akiingiza mkono wake mfukoni.
Hamza aliishia kumwemwesa midomo huku akijiwazia huyu Frank anaonekana kuwa na akili ndogo mno , licha ya kwamba alikuwa na undugu na Regina alijiuliza imekuwaje kuna utofauti mkubwa wa akili baina yao.
“Kwahio umeniita hapa kwa ajili ya kuongea huu upuuzi?”
“Nimekuja kukuambia Dada yagu ataolewa na
James na si vinginevyo , lazima aolewe na familia ya Mzee Benjamini , hivyo kama unajielewa ni bora ukaondoka ndani ya hili jiji mapema na kupotea nisikuone tena”
“Kama niliependana nae ni dada yako wewe kinachokuuma nini , unadhani naweza kusikiliza pumba zako?”
“Wewe huwezi kunielewa kabla ya kufanywa kiwete”Aliongea na muda uleule alipiga simu na kwa sauti kubwa alionekana kuita watu.
Ilionekana kuna watu ambao alikuwa tayari ashawaandaaa kwani ndani ya nusu dakika wanaume wawili warefu na waliojazia waliingia huku wakiwa na vifaa flani vya mawasiliano kwenye masikio yao , walionekana kama wanausalama .
“Hawa wote ni mabodigadi wangu , wamepitia jeshi kabisa , nikitaka kukupiga ni swala la dakika tu , vipi ushaanza kuogopa?”Aliongea na ilionekana alitegemea mabodigadi hao kumuogopesha Hamza.
“Yaani unataka mabodigadi wanipige , huogopi nikikusemea kwa dada na bibi yako?”
“Hio ni baada ya kukugeuza kiwete , unadhani najali ukiwaambia wala kunishitaki , hawawezi kunifanya chochote kwa ajili ya mtu usie na undugu kama wewe”Aliongea huku akicheka.
“Naamini hujawa mjinga kiasi cha kufanya haya maamuzi?”
“Mpuuzi wewe yaani mtu huna mbele wala nyuma lakini unataka kuvunja undugu tunaotaka kutengeneza kati ya familia yetu na ya Mzee James , mimi mrithi wa mali za familia siwezi kuona hili likitokea kwasababu ya wewe na mjinga mwenzako Regina , hivyo nakupa onyo mara ya mwisho unaondoka au huondoki?”
“Umesema huwezi kuruhusu mtu kama mimi lakini kwanini unamwingiza na dada yako?”
“Kwahio nini sasa au ndio unategemea mwanamke kuja kukusaidia hapa, wewe ni..”Kabla hata hajamaliza sentensi yake alijikuta macho yake yakiingiwa na ukungu.
Frank alijikuta akipiga ukulele huku mikono yake ikiwa mdomoni kwake kutokana na maumivu makali ambayo alikuwa akiyasikia.
Ilikuwa ni pigo kutoka kwa Hamza alilomlenga usoni , ijapokuwa hakutumia nguvu lakini ngumi yake ilitosha kumletea maumivu makali mtoto wa kudekezwa kama huyo.
“Takataka kama wewe unajilinganisha vipi na mimi
, ushukuru tu sina mpango wa kukuua”Aliongea Hamza huku akimwangalia Frank ambae ashaanza kulia.
“Mpigeni huyu mshenzi , mpigeni mpaka afe”Aliamrisha mabodigadi wake.
Mabodigadi wale walijikuta wakianza kumshambulia Hamza kulia na kushoto lakini Hamza hakuongea chochote ilikuwa ni teke lake moja na ngumi yake moja aliwafurusha wale mabodigadi kama vifurushi na kwenda kujigonga kwenye magari.
Kitendo kile kiliwafanya waanze kumwangalia Hamza kwa hofu , ukweli ni kwamba hawakujua hata wamepigwa vipi kwani walijikuta tu wakiogelea hewani.
Hamza baada ya kuwapatia kipigo cha kushitukiza wale mabodigadi alimsogelea Frank na kisha alimshika kola na kumning’iniza hewani na kuanza kumwangalia na macho yasiokuwa ya kawaida , kitendo kile kilimfanya Frank kuanza kushikwa na ubaridi wa hali ya juu mno kiasi kwamba kidogo tu angejikojolea.
“Bro.. hapana shemeji naomba unisamehe sitorudia tena , nimekosea usinipige”Aliongea huku akilia kama litoto jinga.
“Kumbuka hakuna dawa ya majuto kwenye maisha , ukichagua kufanya jambo baya basi ni kosa lako la maisha, lakini hata hivyo mimi ni mvumilivu sana , hivyo leo nakupa onyo lakini kumbuka kwenye maisha yangu sijawahi kumpatia mtu nafasi mara mbili”
Frank alikuwa ni kama amechanganyikiwa , hakuweza hata kumsikia Hamza vizuri kwani alikuwa akiogopa mno.
Hamza aliishia kumtupa Frank kama furushi kwenye lami na kisha alitoa gomba mfukoni na kuitoa karatasi na kuanza kuitafuna bila ya wasiwasi huku akirudi alikotoka.
Mara baada ya kufika katika wodi , kulikuwa na watu wengi wamesimama mlangoni na karibia wote walikuwa ni viongozi wa hospitali.
“Ilikuwa ni dhahiri Ronica ashafika na kuanza matibabu , Hamza hata hakujali watu hao na alijiminya minya na kuingia ndani na hatimae aliweza kumuona Regina akiongea na Dokta Ronica na Flora mara baada ya kumuona Hamza alimkonyeza huku akitabasamu.
“Well , do you want a CT?”Aliuliza Hamza akimaanisha je anahitaji vipimo vya CT scan.
“No need , I‘ve already seen them all , there are migratory thrombophlebitis and arterial thrombosis..”Aliongea
“Duuh , ndio ipo hivyo…”Aliongea Hamza huku akionyesha kukunja sura.
Mara baada ya Regina kuona Flora na Hamza wanaongea kingereza huku wakitumia maneno ya kitabibu alijikuta akizidi kujiambia Hamza anazidi kutokuwa mtu wa kawaida.
Isitoshe mtu wa kawaida asingelewa maneno ya kitabibu lakini Flora aliongea kama vile Hamza anamuelewa.
“Dokta Ronica unaweza kuelezea shida yake , sijaelewa kitu”
“Wewe niite tu Flora , ni mpenzi wa Hamza hivyo haina haja ya kuonyesha heshima kiasi hicho mbele yangu”Aliongea na kumfanya Regina kuona aibu huku akitaka kuelezea yeye sio kama anavyofikiria lakini alishindwa kutokana na uwepo wa bibi yake.
“Miss Regina , ijapokuwa naweza kuonekana mkatili kwa kauli yangu , lakini naomba niseme tu kwamba huna haja tena ya kupoteza nguvu na pesa zako kutafuta madaktari , kitu pekee unachoweza kufanya ni kumuandaa mgonjwa kwa ajili ya saa yake ya mwisho”Aliongea na kauli ile ilimfanya Regina sura yake kujikunja.
“Dokta hata wewe huwezi kufanya chochote?”
“I am so sorry , I am a doctor not a God”Aliongea kwa sauti ya radhi huku akimwambia kwamba yeye ni daktari na sio Mungu.
“Ukweli ni kwamba mara nyingi nakutana na wagonjwa ambao kesi zao zinakuwa ni ngumu sana kimatibabu na katika utaalamu wangu ni asilimia therathini tu ya wagonjwa waliopona , asilimia sabini wengi wao hawatibiki”Aliongea.
Ijapokuwa Regina alikuwa amejiandaa kwa taarifa hio lakini ilikuwa ni huzuni kwake kusikia hakuna tumaini lolote kabisa na alijikuta machozi yakimtoka.
Bibi nae alikuwa akisikia kila kitu juu ya afya yake na mara baada ya kuona namna mjukuu wake alivyokuwa na huzuni aliishia kumwambia asogee karibu yake.
Ukweli ni kwamba tokea jana mara baada ya
Ronica kupokea taarifa ya kimatibabu ya Bibi Mirium alishajua anakufa na ni swala la muda tu ila kufika kwake ni kwa ajili ya kumheshimisha Hamza pekee.
Lakini yeye kama dokta alishakutana na hali kama hizo mara nyingi na huwa hampi mgonjwa matumaini hewa.
Baada ya hapo Dokta aliaga na kisha alimpa ishara Hamza kuongozana nae nje na waienda kusimama kwenye balkoni.
“Unaondoka leo?”
“Ndio , nitaondoka mchana lakini kabla ya kuondoka nimesikia taarifa inayokuhusu”Aliongea.
“Nini?”
“Kuna mtu alivunja katika maabara ya Profesa na aliweza kupata anuani ya mahali unapoishi kwa sasa , hivyo ni sawa na kusema inajulikana unaishi Dar es salaam”
“Umeshachelewa kuniambia mbona , watu tayari walishatumwa na kuanza kuniletea matatizo”Aliongea na kumfanya Flora kushangaa.
“Mapema hivyo?”
“Doctor Genesha amejua kuniletea matatizo mno , nataka ukifika ukusanye kila kinachomuhusu na uchome moto , ndio namna pekee ya kuniepushia na matatizo”
“Vipi kuhusu tafiti ya Mti Wa uzima , unataka na zenyewe zichomwe moto?”
“Bado tu unazo hizo tafiti , zitakuletea mtatizo mno , ijapokuwa hatujapiga hatua yoyote kwenye kutafsiri lakini huwezi zuia shauku na matamanio ya watu wenye tamaa”
“Lakini tafiti ile ndio maisha ya Mwalimu na alikufa kwa ajili ya kuilinda”Aliongea Flora kwa kusita.
“Utafiti wake haujakamilika na Tembo wa Trishaza ameshakufa , chukulia tu kama ndoto nzuri na baada ya kuamka sio uhalisia”Aliongea Hamza akiwa siriasi.
“Sidhani kama ni kweli , taarifa za siri nilizosikia ni kwamba kabla ya Profesa kupoteza maisha alishafanikiwa na matokeo ya tafiti yake alimpatia rafiki yake wa karibu , kwa ninavyojua Profesa hajawahi kuwa na rafiki wa karibu tofauti yako”Aliongea na kumfanya Hamza kumwangalia Flora na macho yaliojaa usiriasi.
“Inamaana hata wewe huniamini?”
“I am Sorry my Prince , I‘m just curios”
“Curiosity is sometimes not a good thing”Aliongea akimaanisha kwamba shauku muda mwingine sio nzuri na Flora alitingisha kichwa kumwelewa.
“Nitaondoka kwanza , napaswa kwenda kuangalia kinachoendelea”Aliongea Hamza na Flora alitingisha kichwa.
Wakati Hamza anakaribia mlango ulifunguliwa na Regina alitoka , ukiachana na macho yake kuwa mekundu lakini alikuwa amerudi katika hali yake ya kikauzu.
“Nipeleke kazini”Aliongea.
“Hutaki kuongozana na bibi kurudi nyumbani?”
“Nitaongozana na wewe, isitoshe napaswa kukujua kidogo kwa muda haina haja ya kuwa na haraka sana , vipi au huoni unapaswa kujiandaa?”
“Kujiandaa na nini?”Aliuliza Hamza akimwangalia Regina kwa mshangao,
*******
TEL AVIV- ISRAEL, 13;25.
Ni saa saba dakika ishirini na tano katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Tel Aviv Israeli , katika eneo la maegesho ya magari ziliingia gari tatu mbili zikiwa gari ndogo za kifahari na moja ilikuwa ni gari ndefu ya kifahari aina ya Cadillac escalade ESV isiopitisha risasi.
Baada ya gari zile kusimama gari iliokuwa mbele kabisa walishuka vijana wakiyahudi waliovalia suti na miwani pamoja na vifaa vya mawasiliano.
Haikuhitaji akili kujua kuna mtu mzito ambae anapokewa ndani ya eneo hilo na ilikuwa kweli kwani ndani ya dakika chache baada ya ndege ya kifahari kutua , alitoka mwanaume katika mlango wa watu mashuhuri mzee wa makamo ambae ameongozana na watu wanne kati yao mmoja alikuwa mwanamke na kwa tembea yake ilipaswa kuonekana wale wote walikuwa ni wasaidizi wa yule mzee aliekuwa na mvi wa umri kama wa miaka sabini hivi.
Dakika ileile mara baada ya mzee yule kutoka nje kabisa wale watu ambao walikuja na gari la kifahari walimsogelea yule mzee na kumzingira huku kiongozi wa msafara akijitambulisha kwa dakika chache na baada ya pale walioekana kuelewana na kusogelea lile gari la milango mingi na bwana yule aliingia pamoja na yule mwanamke na bwana mwingine na kisha waliobakia mmoja aliingia katika gari ya nyuma huku mwingine akiingia katika gari ya mbele.
Ilichukua dakika chache tu gari zile zilikwenda
kusimama katika jengo la hoteli ya David Kempisky na kupokelewa na wahudumu waliokuwa nadhifu na kumuelekeza moja kwa moja kuingia ndani.
Lakini Mzee yule mwenye nywele zake nyeupe kadri alivyokuwa akipiga hatua ni kama kuna hali ya wasiwasi iliokuwa ikionekana katika macho yake, mara nyingi kwa kufika hotelini alipaswa kuwa na hali ya utulivu kwa kuelekea sehemu ya kupumzikia lakini kulikuwa na wasiwasi.
Yule mwanamke wa makadirio ya miaka kama therathini hivi mwenye nywele zake nyeusi ni kama aliona hali aliokuwa nayo bosi wake na alitoa kitu kama bublish kutoka kwenye mkoba na kumpatia na kisha akampatia na maji na mara baada ya dakika moja tu alijikuta akivuta pumzi na kutulia na hatimae lift ilifunguka na safari ya kuingi katika korido ilisonga huku wakipokelewa na Maneja na walienda kusimama katika mlango uliokuwa na maandishi makubwa ya VVIP na kwa nje alionekana kuwepo mwanamke mlinzi ambae alikuwa amekakamaa mwili na baada ya kupewa kadi na yule mwanamke, alionekana kuelewa na kisha aliongea kupitia kifaa cha mawasiliano na mlango uifunguka palepale.
“Welcome Mr Alfonso!!”
Sauti ya kike iliongea na kumfanya yule mzee kupagawa na mara baada ya kuangalia mtu aliekuwa mbele yake sura yake ilianza kujikunja na hata ule wasiwasi kupotea.
“Frida kwanini ni wewe hapa?, yupo wapi Prince?”Aliuliza na swali lake lilimfanya Frida kutoka katika tabasamu na kuwa na uso uliojaa usiriasi na kuanza kupiga hatua kiasi cha kufanya bwana alieitwa Alfonso kurudi nyuma kwa hofu. ******
Upande mwingine katika makazi ya Raisi Mstaafu Mzee Mgweno Mandia kulikuwa na kikao kilichokuwa kikiendelea , kikao hiki kilikuwa kikihusisha kamati ya kampeni ya Mheshimiwa Jongwe pamoja na wadhamini wake wakuu.
Moja ya watu ambao walikuwa wakitambulika kwa sura alikuwa ni MzeeBenjamini mmiliki wa kampuni ya Zena.
Watu wote walikuwa wamekaa kwenye masofa ya gharama na mtu ambae alionekana kukosekana ni Mzee Mgweno mwenyewe , ilikuwa ikionyesha ni yeye pekee ambae alikuwa akisubriwa.
“Mzee Benjamini misheni yako naona inazidi kuchukua muda , imekuwaje ukashindwa kuimeza kampuni ya Dosam , unarudisha nyuma juhudi za mheshimiwa katika ujenzi wa ngome yake , umeshakuwa ufa tofauti ya gundi”Aliongea.
“Kwavava unaongea nini? , kitu pekee ambacho una mchango katika ujenzi wa ngome ya mheshimiwa ni cheo chako cha umakamu ndani ya kitengo cha MALIBU , ukivuliwa hicho cheo wewe sio tofali tena unabakia kuwa tope”Aliongea Mzee Benjamini na kauli ile ilifanya baadhi ya watu kutabasamu na baadhi ya watu kuingiwa na wasiwasi.
“Acha kujipa umuhimu ambao hujapewa , mtu mwepesi kama wewe huwezi hata kutofautisha kati ya seruji na tope ndio maana huwezi kuona umuhimu wangu , Shame on you”Aliongea na kumfanya Benjamini kutaka kupandisha lakini alizuiwa na bwana aliekuwa karibu yake.
“Kwavava hivi ni lini mtakuja kukaa meza moja bila ya kugombana , sisi wote ni familia moja maswala yenu binafsi hapa hayana nafasi , kwa nje Afande Kwavava unaaminiwa kuwa na busara lakini mbele ya Benjamini unashindwa kujizuia ni kipi kinaendelea kati yenu?”Aliongea na kuwafanya wote wawili kunywea.
“Mzee Jongwe kama kawaida yako , nadhani mheshimiwa hakukosea kukupigia chapuo mpaka sasa unapeperusha bendera ya chama , neno lako moja tu kelele kwisha”Aliongea na kauli yake ilimfanya Mzee Jongwe kutoa tabasamu hafifu.
“Mheshimiwa Lughalila huna haja ya kwenda mbali kwenye kunisifia , kama nilivyosema nafasi yako baada ya kushinda ipo wazi”Aliongea Jongwe na kumfanya jamaa alieitwa Lughalila kutoa tabasamu.
Dakika ileile mlango ulifunguliwa na msaidizi wa Mheshimiwa mstaafu na aliingia kana kwamba yeye ndio anaeongoza nchi , maana watu waliokuwa hapo ndani kila mmoja alikuwa na cheo , kama sio mwanajeshi basi ni mwanasiasa.
Mheshimiwa Jongwe licha ya kwamba ni mstaafu lakini bado afya yake ni imara kabisa , ndio mstaafu pekee ambae alikuwa hai mara baada ya watangulizi wake wote kutangulia mbele za haki.
“Nafasi ya Gabusha mbona ipo wapi?”Aliuliza mara baada ya kusalimiana na viongozi hao na kauli ile ilimfanya kila mtu kumwangalia Mzee Benjamini.
“Gabusha yupo mkoani Kigoma kujiimarisha?”Aliongea Benjamini na kumfanya Mstaafu kukunja sura.
“Ina maana mambo yake na yule mwanamke hayajakaa sawa mpaka kwenda kujitoa fidia?”
“Mheshimiwa mambo hayakuwa mepesi , kizingiti kilichomkuta Gabusha kimenikuta na mimi?”Aliongea.
“Benjamini unamaanisha nini , usiniambie umeshindwa kutimiza kazi yako mpaka sasa?”Aliuliza na kumfanya Mzee Benjamini kukunja sura.
“Mheshimiwa mpango ulikuwa ukienda vizuri , lakini mara baada ya huyu bwana anaeitwa Hamza kujitokeza kila kitu kimeenda ndivyo sivyo , kila tunalopanga linaenda Kombo”Aliongea kwa namna ya kujitetea huku akisimama na kumfanya Mheshimiwa kumwangalia kwa kutoridhika.
“Unaweza kukaa chini tuanze kikao chetu , isitoshe Ajenda yetu pia inahusiana na huyu anaeitwa Hamza , nilimpotezea mwanzo ila naona anaanza kuwa tatizo”Aliongea na kumfanya Mzee Benjamini kupata ahueni na baada ya hapo alianza
kupitia sura ya kila mmoja aliehudhuria na alikuja kusimamisha macho yake kwa Mheshimiwa Jongwe.
“Jongwe hali ya mwitikio katika kampeni zako kwa wananchi zinaendaje?”
“Mheshimiwa kampeni zinaendelea vizuri sana na nimerudi Dar es salaam kwa ajili ya kufunga kampeni , kwani mwezi ujao tunaingia moja kwa moja katika upigaji kura”
“Una uhakika wa kushinda, vipi kuhusu mpinzani wako?”Aliuliza na kumfanya Mzee Jongwe kusita kidogo lakini alianza kuongea.
“Kuhusu Msemakweli amekuwa tatizo na hivi baada ya tukio la kupotea kwa Tajiri wa Kenya na Balozi wa Rwanda na jambo hili kulihusisha na mtandao wa Panyaroad ameanza kuteka fikra za wananchi, mheshimiwa kwannini nisitangaze moja ya nia yangu ni kuitokomeza Chatu?”Aliongea na kumfanya Mheshimiwa kukunja ndita kidogo. “Uko juu juu sana Jongwe kimawazo , ndio kitu ninachokupendea na kutokukupenda kwa wakati mmoja kwani inakufanya kuwa dhaifu, mpaka sasa kushinda kwako kwa uchaguzi kupo katika mikono ya mtu mmoja , inategemea na namna utakavyomshawishi katika kikao hichi , la sivyo tutatumia nguvu nyingi sana kukuweka Ikulu au Waangalizi watushitukie kuiba kura na kuhatarisha amani ya nchi”Aliongea na kufanya watu wote hapo ndani kutoelewa kauli yake inamaanisha nini , lakini dakika ileile walielewa alichomaanisha kwani mlango ulifunguliwa na hapo ndipo walipojua Mheshimiwa alikuwa akimaanisha nini.
“Nadhani wote mnajua huyu , sina haja ya kuwatambulisha , lakini kabla hajaenda kuongea na kuanza kikao nataka kutoa maelekezo kwamba tukio la kupotea kwa balozi , kifo cha Kamishina msaidizi na wengine linahusiana na yeye”Aliongea na kisha alilazimisha tabasamu na kumwangalia Dina kwa namna ya kumkaribisha.
“Siwezi kuhatarisha mtandao wa Chatu kuteteleka , ndio msingi wa ngome yangu , nitakutumia kuimarisha na kuvuta kipindi hiki cha mpito na baada ya hapo nitakutoa kwa ulazima”Aliwaza mheshimiwa huku akimwangalia mrembo huyo kwa macho yaliojaa ufeki na matamanio.
Comments