Ilikuwa ni dhahiri kwa mwanaume aliefahamika kwa jina la Mr Alfonso kutokutarajia mtu ambae alipaswa kuonana nae kwa kufanya safari ya kufika Israeli kuwa Frida, kwa muonekano wake wa haraka haraka ilionyesha alikuwa akimfahamu fika Frida na macho yake yalionyesha hofu na wasiwasi kiasi cha kurudi nyuma na kurudia mlango akitaka kutoka.
Mara baada ya kupalamia mlango akihitaji kuufungua haukufunguka na alijikuta akigonga kwa nguvu lakini bado hakuweza kusikia watu kutoka nje na akili yake ilimwambia walinzi wake na wasaidizi wapo chini ya ulinzi wa Frida.
“Mr Alfonso sifa zako haziendani na kile ambacho watu wengi wanaongea kuhusu wewe , sidhani ni sahihi kumuogopa mwanamke ambae hana siraha yoyote”Aliongea Frida huku akitoa sura ile ya usiriasi na kuuvaa ukarimu huku akipiga hatua kumsogelea.
“Wewe ni shetani .. usinisogele?”
“Mimi ni nani?!. Kama kweli mimi ni shetani sidhani unapaswa kuogopa, kwa sifa za cheo chako wanaokufuata wakisikia kiongozi wa Sinagogu anamuogopa mwanamke aliemwita Shetani ni dhahiri haitokuwa taswira nzuri kwako?”Aliongea Frida na kumnyooshea mkono Mr Alfonso.
“Unataka nnini kutoka kwangu , mpaka kuniwekea
mtego kwa kujitambulisha wewe ni Prince?”Aliuliza.
“Sina chochote ninachotaka kutoka kwako , bali sisi ni watu wenye malengo sawa ndio maana umefika kwa haraka bila ya kufanya uhakiki wa ki usalama?, sipo hapa kama adui bali kwa niaba ya Maadam”Aliongea na kumfanya Mr Alfonso kuvuta pumzi nyingi huku bado akimwangalia Frida kwa wasiwasi.
“Historia na kanuni za imani yangu zinanikataza kufanya hivyo, kwanini nikuamini wewe uliekengeuka , haijalishi nini unachohitaji kwangu , kutumia hila kunisafirisha mpaka hapa ni kosa kwa upande wako na sio kwa upande wangu?”Aliongea.
“Kama ni hivyo basi malengo yenu hayawezi kufanikiwa na hili unalijua ndio maana taasisi yako ikanichomesha kwa viongozi wangu , ili nichukuliwe hatua , lakini ajabu malengo yenu hayakutimia na sasa nipo hapa kwa niaba ya jumuiya”.
“Tulichofanya sio kukuchomesha , huwezi kusema hivyo ilihali umeingia katika dhehebu letu kama Double agent na haukuwahi kuwa mmoja wetu, wewe ni msaliti na doa kwa imani yetu na hatuwezi kukaribisha tena”Aliongea na kumfanya Frida kutabasamu.
“Basi nadhani ni muda sahihi wa sisi kukaa chini na kuongea, kama nilivyosema nipo hapa kama muwakilishi wa Wiccan , siku zote hii ndio njia yetu ya kuwasiliana ili kuficha mienendo yetu , hivyo huna haja ya kukasirika na unapaswa kuuliza kwanini umeletwa Israeli kutokea
Brazili”Aliongea Frida na muda ule hakutaka kuongea nae tena akiwa amesimama kwani alirudi katikati ya chumba hicho chenye samani za gharama na kisha akakaaa kwenye sofa.
Mr Alfonso licha ya kuwa na wasiwasi alijikuta akivuta pumzi na kisha kusogea taratibu na kwenda kukaa kwenye masofa mbele ya Frida.
“Utapendelea kinywaji?”Aliuliza Frida huku akimimina mvinyo kwenye glasi.
“Hapana nashukuru , nadhani ni vyema ukienda moja kwa moja kwenye dhumuni lako”Aliongea na kumfanya Frida kutabasamu ki uchokozi.
“Nahitaji nafasi yangu ndani ya taasisi” Aliongea Frida.
“Hilo haliwezekani hatuajiri panya”Aliongea kwa kingereza.
“Taasisi yenu inanihitaji zaidi ya ninavyowahitaji ,sina haja ya kuelezea hili zaidi , isitoshe misheni zenu zote zinategemeana na tafiti zangu”Aliongea Frida.
“Unamaanisha hatuwezi kuishi bila wewe , Miss Frida kama hicho ndio unachowaza umoja wetu haupo tayari kukupokea , wewe ni dosari kwa misheni zetu na hatuwezi kuruhusu makosa kwa mara nyingine”Aliongea Mr Alfonso.
“Vipi kama nikikuambia siri ambayo ni watu wachache mpaka sasa wanaijua , siri ambayo umoja wangu haujawahi kuifahamu?”Aliongea Frida.
“Una siri ya namna hio , najua kila binadamu ana siri lakini kuwa na siri kama gia ya mazungumzo sidhani inaweza kuwa na ushawishi wa kutosha wa kukurudisha kwenye taasisi”Aliongea Mr Alfonso huku akijitahidi kuonekana ni mwenye kujiamini. “Umeshawahi kusikia Agent mwenye jina la msimbo(Codename) 2FcommaG?”
“Unataka kusema nini , hilo ni jina la Ajenti ambae umoja wetu umekuwa ukimfatilia kwa muda mrefu na ni taarifa nyeti zaidi ya daraja la juu, unafahamu vipi hii taarifa?”Aliuliza Mzee Alfonso huku akionekana ishara ya kuchangayikiwa.
“Kwasababu mimi ndio Ajenti 2FcommaG maana ya jina hili ni Frida Franklin Genesha”
“Quee!!!”(What!)
Mzee Alfonso alijikuta akimaka huku akisahau kutumia lugha ya kingereza na kuongea kireno, macho yake yalianza kumwangalia Frida kama kwamba kaona mzimu.
“Vipi?, siri yangu imeweza kukupagawisha kiasi hicho?”
“Najua vipi wewe ni kweli ni Ajent 2F tumeweza kukufuatilia kwa muda wa miaka saba mpaka sasa bila ya kukufahamu , umewezaje kujificha kwa muda wote huo mbali na teknolojia yetu?” “Sikujificha , miaka saba iliopita niliachana moja kwa moja na jina hilo , mlikuwa mkitafuta mtu ambae amekufa na hayupo kwenye ramani hivyo ni sahihi kwenu kushindwa kumpata licha ya kutumia rasilimali nyingi na wanachama wote wa Wiccan tunaishi kwa sura nyingi”Aliongea na muda uileule alichukua kishikwambi kilichokuwa kwenye mkoba wake na kukiweka mezani huku picha ikionekana.
“Najua malengo yenu ya kufungua taasisi ya Haliz foundation nchini Tanzania , pamoja na Dhehebu la kidini , ni kwa ajili ya kutafuta hii alama iliowahi kuwepo miaka mingi na ikapotea..”Aliongea Frida na kumfanya Mzee Alfonso paji la uso wake kutoa jasho.
“Who are you!?”Aliuliza akimaanisha yeye ni nani.
“Wewe ni nani , kwanini unajua siri za juu za dhehebu letu?”Aliuliza na Frida muda huo alikuwa na tabasamu pana.
“Mimi ni mtu pekee ambae nahitajika katika taasisi yenu kukamilisha tafiti zangu , najua mpaka sasa mpo njia panda kuthibtishia waumini wenu juu ya ushahidi wa kiimani wa kuzaliwa upya ili kujipatia wafuasi wapya na kuwa na msingi wa kiimani baada ya kujitoa katika Kanisa kuu huku mkijua muda ukiwa si rafiki kwenu , lakini haya yote hayawezi kufanikiwa bila mimi , mimi ndio ufunguo aliouacha Dokta Genesha , ufunguo wa
kuthibitisha nguvu ya kiroho inaweza kuthibitishwa kisayansi, mimi ndio ufunguo wa kuwaonyesha ni nani haswa katika maisha haya anabeba alama yenu iliopotea katika unabii”Aliongea Frida huku wakati huo akiwa amesimama na alionekana kuwa siriasi.
“Umejielezea kuhusu wewe , juu ya kitu unachohitaji , vipi kuhusu Wiccan , wanataka nini kutoka kwetu , sidhani kama ulikuwa na ushahidi wa kutosha wa kujitoa katika adhabu ya kukiuka sheria za umoja wenu wa kipagani?”Aliongea Mr Alfonso na kumfanya Frida kutabasamu na alirudi kwenye sofa na kukaa chini na kumwangalia usoni.
“Hilo ni swali zuri kwa upande wako Mr Alfonso , kama nilivyosema sisi wote tunatafuta kitu kimoja?”
“Unamaanisha hata nyie wapagani mnahitaji kujua nani amebeba alama iliopotea katika maisha haya? , mnataka kujiaminisha nini kupitia alama hio?”
“Mr Alfonso unajua ni kitu gani ambacho dunia
inashindwa kutafsiri maana halisi ya neno Wiccan?”
“Ni rahisi , kwasababu hamuamini uwepo wa Mungu zaidi ya nguvu za giza?”
“Hilo ndio kosa kubwa , sisi sio Wapagani kama
watu wanavyojaribu kututafsiri , sisi pia tunaamini uwepo wa Mungu”
“Hilo ni jipya kwangu kusikia kutoka kwa mpagani?”
“Tunaamini Mungu ni nguvu iliopo katika umoja wakati wa kujitetea na udhihirisho ila sisi tunasimama kwa kuamini katika vitu vingi ambavyo hutengeneza kila kitu kinachoonekana na kisichoonekana ikiwemo Mungu”Aliongea Frida na kumfanya Mr Alfonso macho kuwaka.
“Unaonekana kuwa muumini mtiifu wa Wiccan kwa namna unavyoilezea imani yako , sio jambo baya kwangu kuona unaitetea imani yako , lakini swali langu linasimama palepale mnataka nini kutoka kwetu na ili mdhihirishe nini?”
“Kuijua lugha ambayo imewashinda binadamu wote kuitafsiri mpaka leo ili tuweze kupata vitabu vyote vilivyoelezea uchawi kutoka kanisa kuu”Aliongea na kumfanya Mzee Alfonso macho yake kuchanua.
“Wakati nikihudumu kama Kardinali niliwahi kusikia uzushi mwingi juu ya uwepo wa Manucript za kale zilizohifadhiwa katika maktaba za siri ndani ya makao makuu ya kanisa kuu ,nyaraka ambazo lugha yake haijaweza kutafsiriwa na kujulisha watu zinahusiana na nini , isitoshe sijawahi kuona huo ushahidi wa uwepo wa hizi nyaraka , unachosema wewe kinanifanya niamini pengine ilikuwa kosa upande wangu kupotezea uzushi ule”Aliiongea “Yapo maandiko mengi sana ambayo yametumia lugha ambayo haijawezekana kutafisirika mpaka leo , kutokana na kanisa kuepusha hatari waliamua kuzificha wakati huo wakizifanyia utafiti, moja ya maprofesa wa kiimani waliopewa kazi hio mmoja wapo ni Dokta Genesha na ndio mtu pekee ambae alipata kufahamu uwepo wa andiko lililojaa siri katika simulizi fupi ya Njiwa juu ya mti wa uzima, tulipeleka mapendekezo kwa kanisa kuu kutupatia hizi nyaraka lakini waligoma , Dokta Genesha alipendekeza njia pia ya kutafsiri nyaraka hizi lakini aligoma vilevile na ndio kilichochangia mauaji yake”Aliongea.
“Dokta Genesha alipendekeza kitu gani kwenda kanisa kuu kilichompelekea kupoteza maisha na
vipi kuhusu hii simulizi ya Njiwa juu ya Mti wa Uzima?”
“Askofu sidhani ni sahihi kujua kila kitu , isitoshe kuna kichwa cha habari juu ya simulizi hio lakini kilichoandikwa ndani yake hakifahamiki kwani lugha yake haitafsiriki , lakini kwa mtazamo wa Dokta Genesha ni siri kubwa ambayo inaweza kuhatarisha usalama wa binadamu”
Aliongea na kumfanya kuanza kuonekana kama mwenye kutafakari , hakueleweka alikuwa akifikiria nini.
“Wiccan wanataka kusaidiwa vipi katika hili , hili likifahamika kwa waumini tutapoteza msingi wetu wote wa kiimani na nguvu tuliotumia kupigania uhuru wetu kwa miaka mingi ili kusimama kama kanisa itakuwa ni bure , siwezi kushirikiana na wapagani kirahisi , hata kukutana na wewe hapa ni kosa?”Aliongea Mr Alfonso.
“Ndio maana tumechukua kila tahadhari , tumemtumia mtu ambae unatamani sana kukutana nae , mtu anaefahamika kwa jina la Prince , Mr Alfonso nadhani huwezi kutuchukia katika hili , ilikuwa ni mbinu ya kuweza kufunika mienendo yetu, kuhusu namna ya kutusaidia sisi ni rahisi sana , napaswa kurudi na kuendelea na tafiti zangu ndani ya Haliz foundation siku yoyote nitakayotia mguu nchini Tanzania , sisi kama Wiccan tumetoka mbali shabaha yenu ni shabaha yetu, nataka kuendelea na misheni na wewe kama Askofu mkuu wa Sinagogi B unapaswa kunirudisha kazini”
“Bado sijashawishika kukubali ombi lako , isitoshe wewe ni muumini tu wa chama cha wapagani wanaoamini katika uchawi , wa kuzungumza hili kiitifaki ni mkuu wako na si vinginevyo”
“Nadhani unapaswa kuniambia unachohitaji , huwezi kuonana na mkuu wangu , kama nilivyosema mimi ni mwakilishi , kama una nia ya kuonana na mkuu wetu ni lazima ukubali kutii mila na desturi za Kiwiccan ili kupata jicho la ziada la kuonana nae”Aliongea na kumfanya Mzee Alfonso sura kujikunja.
“Unamaanisha nini?”
“Namaanisha ili uweze kuwa na uwezo wa kuonana nae , unapaswa kuwa na uwezo wa tofauti kidogo na binadamu wa kawaida , na ili kupata hio
nafasi lazima upitie ibada ya kuondoa ukungu wa macho”
“She is Shadow who speaks to me through you?”Aliongea akimaanisha kwamba Frida anatumika na Kivuli kuongea nae. “Unaamini uwepo wetu!!?”Aliuliza Frida.
“The abundunce of informations relating to the existence of so called Night Shadows has been a long-standing topic , we conducted our research to validate the truth”Aliongea akimaanisha kwamba kuna taarifa nyingi zinazozungumzia kuhusu uwepo wa Night Shadows kwa muda mrefu na walifanya utafiti kuujua ukweli” “Na kipi mlipata kupitia utafiti wenu?”
“Tulipata ushahidi wa uwepo wa nguvu ya ziada kwa watu wote waliosema walitawaliwa na kivuli kisichokuwa cha kwao lakini utafiti wetu ulikuwa wa kiroho zaidi , jamii za wanasayansi duniani wamekataa uwepo wenu kutokana na kukosa ushahidi unaonekana”
“Basi wewe ni kiongozi wa kwanza mkubwa kuongea na sisi , muda wangu wa kutawala kivuli cha Frida umekaribia mwisho , kama tulivyoongea unapaswa kukubali kila nilichoongea kama unataka kufanikiwa na sisi kufanikiwa, ili uwepo wetu kuwa wazi tunahitaji kuwafundisha lugha yetu na matumaini yetu yapo katika tafiti ya Frida”Aliongea Frida na muda uleule mlango wa kuingilia katika chumba hiko ulifunguliwa na mtu wa kwanza kuingia ni msaidizi wa Mr Alfonso na alionekana kuwa na ahueni mara baada ya kumuona bosi wake akiwa mzima.
“Mr Alfonso upo sawa?”
“Niko sawa Pretta”Aliongea huku akimwangalia Frida usoni.
“Umeondoka?!”Aliuliza Mr Alfonso alionekana kuwa na swali lingine.
“Unamaanisha mimi au Madam?”Aliongea Frida huku akiwa na tabasamu na kumfanya mzee huyo kushngaa.
“Ulikuwa ukijua anakutumia?”
“Ndio, lakini ndani ya Israeli pekee”Aliongea Frida huku akitabasamu.
“Unamaanisha nini?”Aliongea na kumfanya Frida kumwangalia Pretta msaidizi wa Mr Alfonso.
“Pretta subiri nje kwanza , namalizia maongezi”Aliongea na Pretta alikubali na kutoka nje.
“Shadows wapo kila mahali ni viumbe wasionekana lakini wenye ufahamu , udhaifu wao mkubwa hawawezi kusafiri kuvuka bahari hata kwa vifaa , hivyo Shadows waliopo bara la Afrika hawawezi kuwa bara la Australia au Amerika lakini haimaanishi hakuna mawasiliano baina yao”Aliongea na kumfanya Mr Alfonso kushangaa.
“Kwanini wapo katika hali ya kivuli na malengo yao ya mwisho ni nini , sidhani swala la Lugha linaweza kuwa mwisho?”
“Kuhusu malengo yao ya mwisho sina uhakika , lakini nina hisia juu ya kile ambacho wanahitaji, naamini wanataka kuonekana kama sisi tunavyoonekana”Aliongea na kumfanya kukunja ndita.
“Hilo haliwezi kuwezekana”
“Kama nakumbuka vizuri ni wewe ambae ulipinga vikali juu ya imani ya kuzaliwa upya”Aliongea Frida huku akitoa tabasamu.
*******
Lawrence alionekana kuwa na wasiwasi akiwa ameketi katika eneo la kusubiri , wasiwasi wake ni kile ambacho kinaendelea ndani alikoingia bosi wake , hakujua kama Dina anaweza kuwa salama na alitamani kumpigia Hamza kumjulisha kile kinachoendelea lakini aliona akifanya hivyo angemkasirisha bosi wake , isitoshe alimwambia amuamini katika hilo.
“Madam hili eneo ni miliki ya mheshimiwa na lolote linaweza kutokea , kwasasa una maadui wengi kwanini nisiongee na Bro kwanza tumfahamishe kinachoendelea?”Aliuliza Lau dakika kadhaa kabla ya kuingiza gari katika makao makuu ya mheshimiwa mstaafu.
“Wewe ndio ulieniletea taarifa yupo bize na CEO wa Dosam lakini unataka kumsumbua , Lau najua unawasiwasi juu yangu lakini Hamza amekwisha kutusiadia vya kutosha na alisema nidili na hili mwenyewe , niamini nitalimaliza , siwezi kuruhusu juhudi za babu kupotea”Aliongea.
“Wasiwasi wangu ni huyu mzee , alikuwa ni moja ya adui mkubwa kwa bosi wetu aliepita , ni ngumu sana kumuamini”
“Hata mimi nimekuja hapa sio kwasababu namuamini , nimekuja kwasababu nina kete ya kucheza na kwa vyovyote vile hawezi fanya chochote”Aliongea na Lau kishingo upande aliingiza gari katika makazi hayo ya kifahari.
Makazi ya mstaafu Mgweno kwa barabarani unaweza kudhani ni ya kawaida , lakini ndani yake ilikuwa ni hekalu la kifalme ambalo limejengwa kwa mtindo wa kitamaduni wa nyumba za kirumi.
Lau mara baada ya kuegesha gari alipokewa na moja ya mtumishi wa nyumba hio na kupitia maelekezo Lau aliambiwa asubiri katika eneo maalumu la wageni huku Dina akipelekwa moja kwa moja katika chumba cha mikutano.
Sasa nusu saa zilikuwa zimepita bila ya Dina kutoka na jambo hilo ndio lilimfanya Lau kuzidi kuwa na wasiwasi , alitamani kuingia alipoingia bosi wake lakini walinzi walionekana wapo tayari kumfanyia chochote akifanya fujo.
Hatimae mara baada ya kujishauri kusubiri dakika kumi na tano nyingine bosi wake alitoka na kujikuta akihema kwa ahueni.
Upande wa Dina hakukuwa na ishara ya utani katika macho yake na mara baada ya kumfikia Lau alimpa ishara ya kuondoka na alitii haraka haraka na kuingia ndani ya gari.
“Tukitoka hapa fanya utaratibu wa kuaachilia huru Balozi , Debora na yule mzee”Aliongea Dina.
“Madam kwanini umefikia haya maamuzi?”
“Nimempa alichokitaka na nikapata nilichokitaka lakini mzani umelemea kwangu hivyo naweza kusema kilichonileta kimefanikiwa”Aliongea Frida huku akionyesha tabasamu hafifu na Lau alitabasamu na kisha akaliondoa gari.
“Katika kipindi hiki chote nitahitaji utulivu ndani ya mtandao wetu , hakikisha vijana wetu hawatumiki bila ruhusa yangu , dawa ya msema kweli imeshapatikana lakini kosa kidogo linaweza kuifanya ikose nguvu , umenielewa ninachomaanisha?”
“Ndio Madam”Aliongea Lau huku muda huo akiitoa gari katika makazi hayo ya mheshimiwa.
*******
Licha ya Kanali Dastani kuwa katika uchunguzi ndani ya kitengo kwa muda haikumaanisha alikuwa ametolewa katika kitengo cha MALIBU , nafasi yake ndani ya kitengo hicho ilikuwepo na alikuwa akifika kazini , isitoshe hakukuwa na ushahidi wa kutosha wa kumthibitisha alikuwa msaliti wa taifa.
Saa saba na nusu mchana alikuwa katika ofisi yake na alionekana kuegamia kiti chake kama kawaida huku akiwaza hili na lile.
Moja ya kitu ambacho kilikuwa kikimfanya kuwaza ni juu ya Afande Mchuku na Amosi, alimuwaza Afande Mchuku kwa kuamini kitendo chake cha kuwasiliana nae kupitia simu kimemponza na kumfanya kukumbwa na umauti.
Alikuwa akimuwaza Amosi kwa kuwahi eneo la tukio sehemu ambayo ndio kifo cha Afande Mchuku kimetokea.
Swali lilikuwa ni moja tu , imekuwaje Amosi akawahi eneo la tukio kabla yake , maana kwa mahesabu ya muda aliona kabisa Amosi sio muhusika wa kifo cha Mchuku bali ni mtu mwingine ila kuna hisia zilimwambia Amosi alikuwa akijua kitu ambacho Mchuku alikuwa amebeba.
“Au Mchuku aliwasiliana na Amosi pia?”Aliwaza
Kanali lakini swali hilo pia liligoma , alimjua Mchuku kwa muda mrefu isingekuwa rahisi kuwasiliana na Amosi.
“Kesho napaswa kwenda kuhudhuria mazishi Ikwiriri ninaamini nitapata pakuanzia”Aliwaza kanali , ukweli licha ya kwamba kifo cha Afande Mchuku kimetoka bado aliamini rekodi ya sauti ambayo alikuwa nayo Mchuku mpaka kuuwawa bado haijaingia katika mikono ya mtu mwingine.
Wakati akiwaza simu yake ilimtoa katika mawazo kwa kuanza kuita, baada ya kuangalia jina la anaepiga ni katibu wa mheshimiwa raisi na hapo hapo tumbo lilianza kumchemka , alikumbuka misheni ambayo mheshimiwa alimpatia kuikamilisha na akashindwa , misheni ya kumuua Hamza.
“Habari za saa hizi Mr Dastani?”Sauti upande wa pili ilisalimia mara baada tu ya Kanali kupokea simu.
“Salama katibu habari za mchana”
“Ni njema Kanali , mheshimiwa anakuhitaji ofisini saa nane kamili”Aliongea Katibu na kumfanya Kanali kuangalia saa ya ukutani na sura yake ilijikunja mara moja.
“Sawa katibu nitakuwa hapo ndani ya muda”Alijibu huku simu ikikatwa upande wa pili , alikuwa na dakika kumi na tano kutoka hapo mpaka kufika Ikulu , uzuri ni kwamba kitengo chao hakikuwa mbali sana na ilipo ikulu.
Kwa cheo chake hakuhitaji kuomba ruhusa zaidi ya kutoa taarifa hio kwa Sekretari na moja kwa moja aliingia katika gari lake na kuelekea Ikulu.
Baada ya kupitia itifaki zote za ki usalama hatimae aliweza kuongozwa na katibu moja kwa moja mpaka ndani ya ofisi ya Mheshimiwa.
Katika kipindi hicho ambacho Raisi Eliasi Mbilu alikuwa akimalizia muda wake kichwa chake hakikuwa kikiwaza kuwatumikia wananchi kabisa , alikuwa akiwaza maisha yake baada ya kutoka Ikulu , sio kama kiinua mgongo kulingana na katiba hakikuwa kikimtosha , ukweli ni kwamba hata baada ya kustaafu serikali inamlipa lakini pesa hizo aliona hazikumtosha , hivyo mikataba mbalimbali ya kumnufaisha ambayo hakuikamilisha ndio ulikuwa wakati wake na kumfanya kuwa bize sana na wageni wengi waliingia na kutoka Ikulu.
“Dastani sitaki hata kuanza kuongea kilichotokea juu ya kazi niliokupatia , naelekea Nchini Malaysia masaa mawili yajayo hivyo nipo bize , kuna swala moja nataka ulifanyie kazi na nahitaji majibu ya haraka”Aliongea Mheshimiwa huku akivuka hatua ya salamu. “Nipo tayari mheshimiwa”
“Sio tu upo tayari Dastani , kwa miezi hii miwili sijaona matokeo ya kuridhisha kutoka kwako , naweza kustaafu hata kesho lakini kumbuka nguvu yangu serikalini haiwezi kuisha mara moja, kama unataka kuendelea kupata kinga kutoka kwangu unapaswa kunifurahisha, una maadui wengi wanaosubiria nikupe mkono wa kwaheri”Aliongea na kumfanya Kanali kutingisha kichwa.
“Nadhani umezisikia habari za kifo cha mkuu wa Gereza la Silo na sababu ya kifo chake unazijua , sitaki kujua umeanza lini biashara na Afande Mchuku hayo ni makandokando yako na ni sehemu ya ubinadamu , ninachotaka ufanyie kazi ni kupata rekodi alioacha Afande Mchuku mara moja , fanya juu chini uipate, ina taarifa ambayo haipaswi kumfikia mtu yoyote ni swala la kidiplomasia, umeleewa Afande?”
“Mheshimiwa unamaanisha Afande Mchuku….”
“Unataka kuuliza kilichomkuta Afande Mchuku kinahusiana na mimi? , sidhani ni swala la kushangaza , Mchuku alikiuka miiko yake ya kazi na kilichompata kastahili, baada ya tukio Mchuku alikuwa na USB drive na tuliamini ndio yenye maongezi ya wageni waliofika kuonana na mfungwa lakini kwa hila za Mchuku kilichokuwa kwenye USB drive ni picha za nyumba yake anayojenga”Aliongea Mheshimiwa na kumfanya Kanali kushangaa lakini kutabasamu ndani kwa ndani baada ya kujua wazo lake lilikuwa sahihi Mchuku hakupoteza kitu muhimu.
“Mheshimiwa nitalifanyia kazi hili ndani ya muda mchache nitapata majibu na kukupatia taarifa?”
“Ukishapata faili haina haja ya kuja moja kwa moja kwangu wasiliana na wasaidizi wa Mgweno na ukabidhi”Aliongea na kumfanya Dastani kushangaa kidogo.
“Sawa mheshimiwa?”Aliongea
“Sikia Dastani nakupa onyo, hakikisha ukipata hio flashi hufanyi kitu kingine tofauti na kukabidhi , sitokuwa na namna yoyote ya kukulinda ukienda kinyume na maagizo yangu”Aliongea Mheshimiwa huku akimkazia Dastani macho.
“Mheshimiwa kama hutaki nikisikiliza kilichomo kwanini unanipatia hii kazi mimi?”Aliuliza na kumfanya mheshimiwa kumwangalia kwa sura iliojaa uchunguzi.
“Naitambua tabia yako Dastani ndio maana unafaa katika hii kazi , kumbuka maelekezo yangu pekee , watu wanaohitaji hii kazi kumalizika wana nguvu kuliko unavyodhani, hawapo kama sisi, wanachotaka ni kuficha kile walichoongea na mfungwa basi”Aliongea na Kanali aliishia kutingisha kichwa kukubali.
Dakika chache mbele Kanali Dastani alikuwa ndani ya gari lake , ukweli bwana huyo alianza kujifikiria na kuona kazi nyingi ambazo anafanya sio za kitengo cha MALIBU bali ni za kitengo cha TISA.
“Mheshimiwa anajua kuongea kwa lugha mbili kwa wakati mmoja , anachotaka ni kujua kilichopo katika rekodi alioacha Afande Mchuku , hii inaniambia moja kwa moja sio yeye alietoa ruhusa ya hao wazungu kuonana na mfungwa , lazima kuna mkono wa mheshimiwa Mgweno , lakini kama ni hivyo wameongea nini? , kwanini hawakuchukua tahadhari mpaka wakaruhusu Mchuku kuweza kuwarekodi, hii kesi ya huyu mwanamke ina siri gani kubwa mpaka watu kuwa makini namna hii??”
Ni maswali ambayo Kanali alikuwa akijiuliza lakini kadri ambavyo aliona anazidi kupiga hatua kuisogelea kesi hio kwa ukaribu ndio usalama wake unavyopungua.
Wakati akiwa ashatoka nje kabisa ya geti la ikulu simu yake ilianza kuita na mara baada ya kuangalia anaepiga alijikuta akitabasamu kijeuri na kuipokea.
“Kuna nini Tresha!!?”
“Uko wapi?”Sura ya Kanali ilijikunja.
“Kwanini haraka hivyo? , kuna kilichotokea?”
“Nadhani Amosi kafanya kile tulichokuwa tukijilinda nacho muda mrefu, nimeangalia Kamera za ulinzi na kumhoji Mwanaidi amekubali Amosi alikuwa ndani ya pub na vifaa vya kusikilizia sauti na Kamera..!!”Kanali mara baada ya kusikia taarifa hio alifunga breki mara moja huku kichwa kikianza kuwaka moto.
“Sikia Dastani huna haja ya kufikiria sana , nadhani ameamua kutumia nyendo zako kufanya uchunguzi wake kwa hilo nampa credit, lakini haipaswi hii kuendelea , Amosi atavuruga mipango yetu yote , hebu fikiria picha zikifika kwa Eliasi atachukua maamuzi gani?”
“Tresha unazunguka zunguka, unataka nitafanye nini?”
“Kwahili hata mimi nimechangia , lakini ukweli hauwezi kupingika haukuwa makini Dastani , tabia yako ya kumdharau Amosi itakuletea matatizo , nimempa kazi mtu kumtafuta Amosi popote pale na kumuua, hili swala lishakuwa binafsi tayari”
“Tresha hebu subiri….”Kanali alijikuta akipiga usukani wa gari mara baada ya simu kukatwa , dakika ileile alipiga tena simu kwenda kwa Tresha lakini simu ilikuwa haipatikani hewani.
“Tresha ataniingiza kwenye matatizo huyu Ma*ya kwa kukurupuka, nakiri nilikosea kumdharau Amosi lakini namjua Amosi nje ndani sio mtu wa kukurupuka na hachukulii vitu kuwa binafsi, sio mwepesi kuvujisha picha”Aliongea chini chini huku akikanyaga pedeli na kusogeza gari lake makao makuu ya kitengo huku wazo namba moja ni kumtafuta alipo Amosi kabla hajafikiwa na Tresha.
********
“Hukujumuishwa?”Aliuliza Regina huku akimwangalia Hamza kwa macho makavu.
“Mbona unauliza kimkato mkato sio tabia yako hii?”Aliongea Hamza akilalamika.
“Ninachomaanisha leo kuna mashindano ya
Basketball , mbona katika taarifa ilionifikia wewe pia umejumuishwa kama mchezaji?”Aliongea Regina na sasa kumfanya Hamza kukumbuka.
Siku kadhaa nyuma anakumbuka alifuatwa na moja ya wafanyakazi aliefahamika kwa jina la
Aroni wa kampuni na kumuomba kujiunga na timu yao ya kampuni kwa ajili ya mchezo wa basketball,
kilichomfunga Hamza ni mara baada ya wafanyakazi hao kumuuliza kama anaujua mchezo huo na aliitikia kama anaujua na moja kwa moja wafanyakazi wale walimwambia ashiriki kama mchezaji lakini kwake Hamza alisema anaujua na sio kujua kucheza.
Ukweli katika mambo ambayo hayakuwa na umuhimu katika kichwa cha Hamza hilo lilikuwa namba moja ndio maana alisahau kabisa na hata kwenda kwenye mazoezi hakukumbuka.
“Waliniandika kama mchezaji bila ridhaa yangu, waliniuliza kama naujua mchezo wa Basketiball nikawaambia naujua nadhani wamenielewa vibaya nani asieujua mchezo wa Basketball , halafu kwani kuna umuhimu wa kushiriki?”Aliuliza Hamza huku akikuna kichwa.
“Kwako wewe inaweza isiwe na umuhimu kwasababu umejiunga na kampuni juzi , lakini huu umekuwa utaratibu wa muda mrefu wa wafanyakazi wa kampuni mbalimbali kushindana katika michezo mbalimbali ikiwemo mpita wa miguu, Marathon na Basketball, nikuambie tu leo Mkuu wa Mkoa na viongozi wengine wamealikwa
hivyyo wewe kama mchezaji nahitaji ushindi”Aliongea Regina.
“Lakini sijasema mimi ni mchezaji kwanini unaniamrisha nikupe ushindi?”
“Iwe jina lako limeandikwa bila ridhaa yako au kwa hiari wewe ni mchezaji na majina yashatolewa tayari , unapaswa kuelewa kampuni yetu haina wafanyakazi wa kiume wengi hivyo endesha gari kurudi kazini , mchezo unaanza mchana”Hamza alijikuta akishindwa kujua alie au acheke , licha ya kwamba ni kweli anajua mchezo huo lakini hakuwa na mpango wa kucheza kabisa na alitamani kumpigia simu Aroni msimamizi wa mchezo huo na kumwambia hakuwa tayari kuhusika.
“Regina hebu subiri kwanza , kwahio haya mashindano mshindi anazawadiwa nini au ndio mnacheza kujifurahisha?”
“Hujakubali hata kuwa mchezaji unaanza kuuliza zawadi utakayopewa , hebu tuondoke muda unaenda”Aliongea Regina huku kwa wakati mmoja akitamani kumpiga Hamza teke, alishindwa kujielewa kwanini muda wote anahisi kukerwa na Hamza lakini kwa wakati mmoja akiifurahia kampani yake, kilichokuwa kikimuuzi zaidi Regina ni maigizo ya Hamza alijua sio mtu masikini lakini muda wote anawaza pesa.
Lisaa limoja mbele Hamza na Regina waliwasili katika uwanja wa Basketi wa chuo kikuu cha Dar es salaam.
Sehemu hio ilikuwa imezingirwa na polisi waliokuwa wameshikilia siraha na hio yote ni kutokana na uwepo wa viongozi wa kiserikali ambao walialikwa kushuhudia mchezo huo.
Ijapokuwa ni mashindano ambayo yalihusisha wafanyakazi wa jiji lote lakini yalifanyika siku moja tu.
Mpira huo wa kikapu sheria zake sio kama za mpira wa miguu , raundi zilikuwa ni kila dakika ishirini ishitini.
Kulikuwa na timu jumla kumi na sita ambazo zinashiriki , kimsingi mashindano hayo huanza mchana mpaka usiku na ndio hufikia mwisho , ilikuwa hivyo kwasababu viongozi ambao wamealikwa hawawezi kuhudhuria kila siku kwa ajili ya mechi kadhaa , kingine wachezaji karibia wote ni wafanyakazi wa makampuni hivyo muda wao wa kucheza mechi hizo kila siku ni mdogo.
Moja ya sababu kubwa kwa mashindano hayo na kwa timu ambayo inaweza kushinda ni kujitangaza bila ya kutumia pesa kwa kupiga picha pamoja na viongozi wa kiserikali , ukweli ni kwamba tuzo ya mshindi sio kitu kinachotafutwa sana hapo.
Hamza mara baada ya kufika tu alisogelewa na
Aronni ambae alionyesha furaha kumuona , Hamza alilalamika kama sio mchezaji lakini Aroni alimwambia anapaswa kushiriki kwani idadi yao ni ndogo na kutokana na macho ya Regina yalivyokuwa siriasi ilimfanya Hamza kutingisha kichwa kukubali.
Kabla ya mashindano kuanza kulikuwa na sherehe za ufunguzi na kitu ambacho Hamza aliweza kusikia ni sauti za watu asiowafahamu wakiuongea juu ya jukwaa.
Baada ya hotuba kutoka kwa viongozi na wakuu wa kampuni husika Hamza na wachezaji wengine waliokuwa wakishiriki walienda moja kwa moja mpaka kwenye vyumba vya kubadilishia
Lakini kitendo cha kuingia ndani ya korido ya vyumba hivyo aliweza kukutana na sura ya mtu ambae anamfahamu.
Aliekuwa mbele yake alikuwa ni James na Chriss wote wakionekana ni mabosi kutoka timu tofauti , Chriss akiwakilisha kampuni yao na upande wa James akiwakilisha kampuni yao.
Chriss alikuwa na kundi la wachezaji nyuma yake huku James pia hivyo hivyo, licha ya timu kuwa tofauti lakini kulionekana ukaribu kati yao.
“Hamza!!”Aliita James huku akisogea kiswaga kumsogelea Hamza , mara baada ya Chriss kusikia jina la Hamza na yeye macho yake yalichanua na kusogea.
Ukweli ni kwamba Chriss hakuwa akimjua Hamza vizuri zaidi ya kumsikia tu na alitamani kuonana nae , sasa ilikuwa ni kama bahati maana alikuwa na hasira sana na bwana huyo kwa kujihusisha na Prisila.
Ki ufupi James alikuwa na hasira na Hamza kwasababu ya Rregina , huku Chriss akiwa na kisasi na Hamza kwasababu ya Prisila.
Upande wa timu ya Hamza mara baada ya kuona kundi la James walionekana kama vile walikuwa wameona maadui wakubwa.
“Na nyie mpo hapa kwenye mashindano?”Aliuliza Hamza.
“Unauliza au umejijibu , unadhani kampuni kubwa kama yetu inakosaje nafasi ya ushiriki ,sisi ndio waasisi wa mashindano haya”Alionge na kisha alimgeukia Chriss.
“Chriss huyu boya ndio Hamza ambae anatusumbua” Aliongea James huku akimwangalia Chriss.
Ukweli upande wa Chriss hakumwangalia Hamza kwa macho ya dharau alikuwa katika hali ya kumtathimini, kimwonekano hawakuwa wamezidiana sana ni kwamba Hamza alikuwa na asili ya kizungu huku Chriss akiwa na asili ya kiarabu.
Kitu pekee kinachowatofautisha ni kwamba Hamza anaonekana kuwa mkakamavu zaidi kuliko Chriss wakati huo Chriss akionekana aliestaarabika zaidi kuliko Hamza.
“Chriss mbona huongei chochote? Huyu boya ndio alietambulishwa na Prisila?”Aliongea James na kumfanya Hamza kushangaa kidogo.
“Mimi kutambulishwa na Prisila kuna tatizo gani mpaka kutaka mshikaji hapo aongee?”
“Mimi ndio mpenzi wa Prisila , naitwa Chriss Gabusha”Aliongea Chriss akiwa katika hali ya tabasamu.
Ukweli ni kwammba asubuhi mara baada ya Chriss kuamka hasira yake zidi ya Hamza ni kama ilishuka mara baada ya kuongea na Prisila.
Upande wa Prisila hakujua kama Hamza alikuwa akifahamika kwa Chriss sasa ili kulinda siri ya Regina ilibidi aseme Hamza sio mpenzi wake bali jana alimsindikiza tu kama rafiki wa rafiki yake yaani Regina.
Upande wa Hamza hakutaka mambo kuwa mengi hivyo alipokea salamu ya Chriss isitoshe hakuwa na mahusiano na Prisila hivyo hakutaka kuingilia sana maswala yake, maana Regina alimpa
tahadhari kutofanya chochote ambacho kinaweza kumfanya James kuona mahusiano yao ni feki.
“Hamza na wewe upo hapa kwa ajili ya mashindano?”Aliuliza Chirss.
“Ndio na nyie vipi?”
“Unataka kujilinganisha na mimi , kwanini nishindane mwenyewe wakati wafanyakazi kama wewe wapo?”Aliongea James akiingilia maongezi.
“Upo sahihi , nadhani kutokana hata kupigana hujui mwili wako ni dhaifu hivyo ni ngumu kwako kucheza mpira wa kikapu?”Aliongea Hamza.
“Wewe mpuuzi unajikuta nani kuniita dhaifu , labda hujui ila mwaka jana kampuni yetu ndio ilishinda na tunataka na mwaka huu kushinda pia, tukikutana kama timu nitahakikisha nakuabisha mbele ya Regina”Aliongea kijeuri , alikuwa akimchukia mno Hamza kiasi kwamba alitamani kuongea kila neno baya lakini muda hakuwa nao.
Hamza na yeye alimpotezea na kwenda kubadilisha mavazi , mwanzoni hakuwa na mudi kabida ya kucheza mchezo huo lakini uwepo wa James ni kama umempa motisha.
“Bro imekuwaje ukawa na uadui na James , wale wachezaji wa kampuni yake licha ya kuwa wachezaji lakini pia ni walinzi waliopitia mafunzo maalumu na wanajua mno kucheza rafu hivyo uwe makini”Aliongea Aroni.
“Haina haja ya kuwa na wasiwasi tunaenda kushindana kurusha mpira na sio
kupigana”Aliongea Hamza na kumfanya Aroni na wenzake kuwa na sura ziliozokunjamana.
Asilimia kubwa ya wachezaji wenzake Hamza hakuwa akiwajua vizuri kwasababu walikuwa wakifanyakazi nje na makao makuu .
Nusu saa mbele mechi ilianza katika viwanja vyote vinne , Hamza mara baada ya kuingia katika Court aligundua wafanyakazi baadhi kutoka makao makuu wamefika pia na walikuwa wakishangalia kwa kutaja jina lake kitendo kilichomfanya kuhisi damu kuanza kumsisimka na kuona ni mahali pake pakujichukulia pointi kwa warembo hao.
Wafanyakazi hao walikuwa ni kutoka idara ya mauzo walioambatana na Eliza na mara baada ya mrembo huyo kukutanisha macho na Hamza aliishia kutoa tabasamu huku akimpungia mkono , alikuwa na macho yaliojaa matamanio kana kwamba anajaribu kuwaambia watu kupitia hisia yule ni mpenzi wangu.
Upande wa Regina kama bosi wa kampuni alikuwa ameungana na mabosi wengine wa kampuni na walikuwa wamekaa kwenye jukwaa la VIP.
Sasa kitendo cha kumuona Hamza akipungiana mkono na Eliza na namna Eliza alivyokuwa akitabasamu uso wake na macho yake yalijawa na hali ambayo haikutafsirika.
Muda huo James akiwa na tabasamu zito alisogea na kwenda kukaa pembeni ya Regina.
“Mrembo , nadhani hutojali nikikaa pembeni yako?”Aliongea lakini upande wa Regina hakuwa na hisia zozote katika macho yake na hata hakujisumbua kumjibu.
James alijikuta akijisikia aibu kidogo kutokana na macho ya watu wengi yalikuwa yakimwangalia, alijikuta akijitafuta mwenyewe na kukaa chini na hazikupita dakika tano lazima ageuze macho kumwangalia mrembo Regina.
Hatimae kipenga kilipulizwa na mechi zote nne kwa wakati mmoja zilianza
Upande wa Hamza timu waliokuwa wakishindana nayo ilikuwa imejaa wachina na baadhi ya watanzania wachache na kwa muonekano wao walionekana ni wataalamu wa mchezo huo kwa namna miili yao ulivyojaa mazoezi.
Kwa macho yao walionekana kuwadharau wafanyakazi wa Dosam , licha ya kwamba ni kweli hata upande wa Hamza wachezaji wake walionekana kuwa na miili iliojengeka kimazoezi lakini kutokana na uzoefu wao mchezo wa kikapu sio swala la kuwa na nguvu bali ni swala la nguvu , ujuzi na muunganiko kitimu.
Lakini licha ya hivyo walishangaa kukutana na ukinzani mkubwa wa kimashambulizi kutoka kwa timu ya Hamza.
Timu ya Dosam haikuonyesha kujali sana kuonyesha mbwembwe zaidi ya kurushiana mpira mpaka eneo la pointi tatu na mtu wa mwisho kupata mpira kama mwanariadha aliruka na kwenda kuutumbukiza mpira kwenye kikapu
“Suui!!!
Mpira uliingia na kelele kama zote na hatimae Dosam kujikuta wakianza na kupata pointi mbili.
Kampuni ya Dosam ilikuwa imebarikiwa na wanawake warembo na walikuwa wakishangilia kwa shangwe na sauti tamu mara baada ya kuona timu yao imeshinda.
“Hamza tupo nyuma yako , twende kazi, tuheshimishe baba!!!”Wakina Asha na Mirium walipiga kelele na wengine wote waliunga na kuanza kulitaja jina la Hamza.
Eliza alikuwa na tabasamu kama lote , alijihisi kuwa na furaha kumuona mpenzi wake akicheza mpira wa kikapu kama hivyo. “Pumbavu wana bahati hawa”
Wapinzani wao walijikuta wakisemezana wao kwa wao wakiwa na mshangao na hatua iliofuata waliingai katika pambano la kuzuia na kushambulia kwa wakati mmoja.
Upande wa Hamza ni kama alikuwa akitalii , ukweli ni kwamba alikuwa akitembea kurudi nyuma na kwenda mbele na hata uwezo wake wa kuzuia ulionekana mdogo.
Upande wa Aroni na wenzake mara baada ya kudaka mpira wa Rebounds palepale walimrushia Hamza na hakurembesha kwani kwa jicho lake la kichawi alisogea mpaka eneo la pointi tatu na kisha akarusha mpira na uliingia bila kugusa kigo za gori na kilichosikika ni mkwaruzano tu wa nyavu.
Mpaka dakika ishirini zinaisha Hamza alikuwa ameonyesha uwezo wa kurusha mpira kwenye kikapu wa hali ya juu mno , hakuonekana kama mchezaji wa basketbal ila alionekana kama mtaalamu wa kulenga shabaha.
Matokeo ya mwisho Dosam iliishinda kampuni ya kutengeneza rangi kwa pointi 43 kwa 25.
Jambo hilo lilifanya wanawake wa kampuni ya Dosam kumpigia kelele Hamza huku kila kilichowakalia mdomoni waliongea , ukweli ni kwamba hata Aroni na wenzake walikuwa wakimshangaa Hamza kwa uwezo wake wa kulenga kikapu na mpira.
Na wakati wa kucheza kwao kote ni kama wameona namna ya kushinda hivyo kila wakipata mpira walikuwa wakimpelekea Hamza ili kutupia.
Hakuna alietegemea kampuni ya Dosam inaweza kuvuka hata mechi ya kwanza na kwenda hatua inayofuata , maana siku zote Dosam ndio iliokuwa ikiongoza kwa kuwa wa mwisho katika mchezo huo.
“Haha.. Bro aisee umenishangaza sana , uwezo wako wa kulenga sio wa kawaida ni kama sio binadamu vile”Aliongea Aroni.
“Aroni wakati unasema huyu ni moja ya mchezaji nilijua umetupiga na kitu kizito na tunaenda kuonyesha tu tumeshiriki, Bro una heshima yangu katika mchezo wa Basktetball”
Wachezaji walianza kumsifia Hamza kutokana na uwezo wake , mpaka hapo walijiona hawakuwa na hofu tena ya kushinda mechi zinazofuatia.
Hamza alienda mpaka pembeni ya uwanja na kisha akachukua chupa ya maji na kunywa kidogo huku akijiambia anapaswa kupunguza namna anavyoshinda la sivyo watamuona sio wa kawaida , ili mradi timu ishinde basi haina haja ya kuonyesha kupatia kulenga kila dakika anayopata mpira.
Upande wa Regina alijikuta akipata ahueni na mara baada ya kusikia mabosi wenzake wanavyojadili namna Hamza alivyokuwa na uwezo wa kulenga kikapu alijikuta akijihisi furaha moyoni mwake.
“Regina timu yako inacheza vizuri , lakini usiombee ikutane na timu yetu”Aliongea James
Regina aliishia kumwangalia kwa ukauzu tu huku akishikwa na wasiwasi , hofu yake ni kwamba James anaweza akawa na kitu kibaya anapanga.
“Mr James nimesikia kampuni yenu imekuwa katika ushindani mkali na Dosam hivi karibuni, sidhani pia kama mkikutana utakuwa mchezo rahisi, ninachoona hapa kila timu inacheza kwa ajili ya kuheshimisha kampuni yake”Aliongea Mkuu wa mkoa Mheshimiwa Chamali Ngala mara baada ya kusikia maneno ya James kwenda kwa Regina
“Mheshimiwa kumbe na wewe una wasiwasi na kampuni zetu pia , niwie radhi kama maneno yangu yameonekana sio mazuri kwa mpiuzani”Aliongea James huku upande wa Regina
pia akitingisha kichwa kukubaliana na Mheshimiwa.
“Zena na Dosam ni moja ya kampuni kubwa zinazolipa kodi kubwa ndani ya Tanzania , mimi kama kiongozi ni swala la kawaida kujua kinachoendelea , matumaini yangu ni kuona kampuni zote zinakuwa na kustawi vizuri kwa manufaa ya taifa zima , mashindano kama haya ni kawaida lakini hata kama kampuni ni kubwa vipi haiwezi kuwa juu ya sheria za nchi”Aliongea Mheshimiwa.
“Ni kweli kabisa mheshimiwa , tutazingatia maelekezo yako”Aliongea James huku akitabasamu kinafiki ni kama yeye ndio aliekuwa akisemwa.
Upande wa Regina hakuongea chochote zaidi ya kutoa tabasamu hafifu.
Kwa bahati nzuri Mheshiimiwa Chamali na Jopo la Mameya wa jiji hilo walikuwa wakiijua fika tabia ya Regina na washamzoea sio mtu wa kuongea neno , hivyo ni kama walijua kumvumilia.
Ilikuwa tabia ya Regina hata mara baada ya kuombwa na wagombea wa kiti cha uraisi kufadhili kampeni lakini Regina alikuwa na jibu moja tu kwamba hatofadhili upande wowote maana hakutaka kuiingiza kampuni yake na maswala ya kisiasa.
Baada ya kumpumzika kwa dakika kadhaa hatimae raundi ya pili ilianza na Hamza aliongea na wenzake na kuwaambia wakipata mpira wampasie, Hamza aliona iwe hivyo kwasababu hakuwa na mbinu nyingine ya kuonyesha zaidi ya kuujaza mpira kwenye kikapu.
Hatimae mara baada ya dakika kumalizika upande wa Hamza ulishinda tena kwa faida ya Hamza kurusha mpira kutoka mbali na kuujaza na hatimae raudi tatu zilipita na ikafikia hatua ya nusu fainali.
Na sasa ilikuwa ni zamu ya kampuni ya Zena kushindana na kampuni ya Dosam.
Aroni na wenzake alikuwa wameloa jasho lakini walikuwa na morali kubwa mno ya kushinda mechi.
Hasa pale walipokuwa wakitajwa majina yao na warembo wa kampuni yao hali ya kujiamini iliongezeka huku wakiamini wakishindwa itakuwa rahisi kuwaopoa hao warembo.
“Bro Hamza kama tukifanikiwa kushinda hii timu nina uhakika tutaweza kuwa bingwa , hii ndio timu ngumu pekee hivyo tunakutegemea”Aliongea Aroni.
“Ndio Bro tutahakikisha tunausaka mpira kwa namna yoyote na wewe ndio utakuwa kete yetu ya ushindi”
Walishauriana huku wakimuona Hamza kama shujaa wao wa mchezo ambae amewatoa katika mateso ya kuonewa kila mashindano hayo yakianza.
Hamza licha ya kwamba hakuwa amezoeana na watu wengi lakini kupitia mechi hio ni kama ameweza kupata marafiki ndani ya kampuni kwa haraka sana.
“Haina noma , nyie nipasieni mpira nitatupia”Aliongea Hamza na kisha waliwekeana mikono ya kitimu na kisha kujipanga kusubiria kipenga cha refa.
Nadhani moja ya sababu ya wachezaji wa kampuni ya Zena kushinda ni urefu wao , walikuwa wameenda hewani mno, wote walikuwa katika makadirio ya mita moja pointi tisa ki urefu, hivyo iliwapa faida ya kushambulia na kushinda kwa uharaka.
Mara baada ya mchezaji wa Dosam kupata mpira alimpasia Hamza na lijamaa lirefu la upande wa Zena lilimsogelea haraka na kumzuia kwa mbele akinyoosha mikono yake.
Lakini ajabu Hamza aliruka juu zaidi kwenda angani kiasi cha kumzidi kimo yule mwamba na kuurusha mpira kirahisi.
Kadri mechi ilivyokuwa ikiendelea ilionyesha ni namna gani urefu wao na ukubwa wa miili haukuwa na athari zote mbele ya Hamza kwani wakimzuia hivi Hamza anafanya hivi na kushinda.
Ijapokuwa hata wao walikuwa wakishinda lakini ilikuwa ni pointi mbili kwa tatu , yaani wakishinda mbili Hamza anashinda tatu.
“CEO Regina yule bwana wa pointi tatu tatu naona sio wa kawaida kabisa”Aliongea Mheshimiwa huku akipiga makofi.
Regina upande wake mdomo wake ulicheza kwa tabasamu na kujiambia asije akajitia aibu kutokana na furaha yake hivyo alijitahidi kujizuia kutoamka kushangilia.
“Yupo vizuri”Aliongea .
‘Upande wa wafanyakazi wa Dosam walikuwa na furaha , kuishinda kampuni ya Zena ilikuwa na msisimko mkubwa kuliko kushinda timu yoyote ile.
“Eliza , Hamza ameshinda tena”
“Jamani jamani na alivyo Handsome , lazima nijishobokeshe kwake , sijui atanipenda”
“Hebu acheni kujishebedua , Hamza ni wa kwetu na haendi popote..”Aliongea Mirium na Aisha wakishindana na wafanyakazi wa benki ya Dosam katika kundi hilo alikuwepo Mellisa mpenzi wake Amiri ambae alionekana kuwa tofauti kidogo na wenzake licha ya kuwa na furaha, alikuwa mrembo haswa , ilikuwa haki kwa Amiri kulilia penzi.
Upande wa Eliza alikuwa na furaha kwasababu ya uwezo wa Hamza , lakini mara baada ya kusikia kila mwanamke alikuwa akimtaka Hamza wasiwasi ulimvaa.
Alikuwa na wasiwasi kutokana na umaarufu Hamza aliojipatia ni lazima warembo wa kampuni watamshobokea.
Kutokana na Hamza kushinda mara kwa mara James wasiwasi ulimvaa mara moja na aliangaliana na Chriss ambae alikuwa amekaa upande wa nyuma akimwangalia Hamza kwa mshangao na palepale James alitoa simu na kuonekana akituma meseji na hali ya uovu ilionekana kwenye macho yake.
Baada ya awamu ya pili kuanza wachezaji wa kampuni ya Zena walikuwa na mwonekano wa kikatili na ilionekana mpango wao ni kucheza rafu na ndio kilichotokea , wakati wa kushindania
Rebounds mchezaji wa kati aliruka na ghafla tu alimpiga Aroni kwenye kifua kwa kiwiko cha mkono
Kitendo cha Aroni kupiga ukulele kwa rafu ile yule mchezaji alishuka chini na kumkanyaga kwenye enka ya mguu.
“Arghhhh..!!!”
Ukulele wa Aroni ulishitua baadhi ya watu na Refa aliwahi kupuliza filimbi akionyesha kuwa ni faulu.
“Aroni vipi hali yako?”
“Refa hawachezi kushinda ila ni rafu”Aliongea Aroni akiwa na maumivu na wachezaji wenzake mara baada ya kuona hilo walianza kugombana na wachezaji wa upande wa Zena.
Lakini upande wa timu ya Zena walionyesha hali za upole wakiashiria kwamba faulu hio haikufanyika makusudi.
Kitendo kile Regina alishindwa kukivumilia na kumgeukia James akimwangalia kwa macho makali.
“James wachezaji wako wanafanya makusudi kuumiza wachezaji wetu””
Ukweli ni kwamba James alitoa maelekezo ya Hamza asiguwe maana atawadhalilisha kwa kujua mapigano hivyo alitoa maelekezo kwa wachezaji wenzake ndio waumie
“Regina hatimae umeanza kuniongelesha mwenyewe , lakini mbona unanisingizia , tukio kama lile ni la kawaida kwenye mchezo wa kikapu”
Regina alijikuta akisugua meno kwa hasira , alijitahidi kujizuia kwasababu alikuwa amezungukwa na watu wa heshima , hivyo aliachana na James na pamoja na Linda walishuka mpaka chini kwenda kumwangalia Aroni.
“Vipi hali yako , umeumia sana?”Aliuliza Regina .
Aroni mara baada ya kumuona bosi amekuja kumwangalia alijitahidi kusimama ili aongee nae lakini alijikuta akidondoka bila ya kupenda chini kutokana na maumivu makali
“Bosi Regina una mchezaji mwingine wa hakiba kwenye timu yako?”Aliuliza Refarii huyo wa kike
“Mchezaji mwingine!?”
Regina alijikuta akishindwa kuongea mara baada ya kujua hakuna mchezaji mwingine
“Refa kwani kuna ulazima wa kucheza watu watano ili kuendelea na mechi?”
“Ndio , hatuwezi kupindisha sheria ya mchezo”Aliongea Refa na kumfanya Hamza kufikiria.
“Kama ni hivyo unaonaje Aroni akiendelea kubakia uwanjani hata kwa kukaa?”Aliuliza na kufanya kila mtu kushangazwa na pendekezo lake.
“Unachomaanisha aendelee kubakia mchezoni?”
Comments