Reader Settings

Regina  alijikuta akivuta pumzi ya ahueni mara baada ya kuona  Hamza alikuwa muoga ndio maana kasogea mbali , alijiambia kama atashindwa kumkontrol huyo mwanaume basi ataingia  kwenye kazi nyingine ya kutafuta boyfriend feki mpya.

Lift ile iliwapeleka  mpaka juu kabisa kwenye moja wapo ya mgahawa uliokuwa ukipatikana floor ya mwisho , sehemu ambayo  ukikaa unaona karibia  jiji lote la Dar na maeneo ya mbali.

Meneja wa mgahawa huo alikuwa  ni mwanaume wa makamo Mfaransa, alikuwa amevaa akapendeza   na mara baada ya kumuona Regina alimtambua haraka  na  kumsogelea  huku akiongea  kwa  kuchapia chapia kiswahili.

“Karibu sana Madam Regina CEO”Aliongea akiweka tabasamu lakini kwa wakati mmoja akionyesha namna ya  kushangaa  namna ambavyo Hamza ameshikana mkono na Regina.

Licha ya kwamba alikuwa  Mfaransa  ila   kuishi kwake Tanzania kwa muda mrefu kumemfanya kujua  vitu vingi na kati ya vitu hivyo  ni urembo na ukauzu wa mwanamke  Regina, CEO wa  makampuni makubwa ya Dosam.

Sasa  baada ya kuona  mrembo huyo akiwa ameshikiliwa mkono na mwanaume  aliona   ni swala zito ambalo mashilawadu kama watalifahamu  itakuwa habari kubwa, isitoshe  Regina alikuwa ni kama  kioo cha jamii  ndani ya taifa .

“Wazazi wangu washafika?”Aliuliza.

“Ndio wameshafika tayari , nitawapeleka moja kwa moja  walipo sasa hivi”Aliongea na kisha aliongoza njia.

Wakati wakitembea katika  mgahawa huo mkubwa na wa kuvutia , Regina  alijikuta bila ya kupenda  akimwangalia Hamza, ni kama alikuwa na wasiwasi kwani alijua fika watu wa daraja  la chini kama watafika katika eneo hilo ambalo hutembelewa  na  watu wa vipato vya juu watakuwa na wasiwasi.

Lakini  alionekana kuridhika mara baada ya kumuona Hamza hakuwa na wasiwasi wowote na kuona hapo  kweli ameajiri  mtu sahihi.

Mara baada ya kuingia  katika chumba binafsi kulikuwa tayari kuna watu watatu waliokuwa  wamekaa  kuzunguka meza.

Mmoja wapo alikuwa ni mwanaume  wa  hadhi  wa makamo  na mwingine alikuwa ni  mwanamke  ambae alikuwa amevalia  mavazi ya thamani pamoja na  mkufu wa  thamani kubwa shingoni , kwa  umri wake wa miaka arobaini ilionekana alikuwa akijitahidi sana kuhakikisha  anaonekana kijana bado.

Kulikuwa  na mwanaume pia kijana alievalia shati  la kola,  brand ya Ermenegildo Zegna , alikuwa ni mtanashati mno  lakini pia  alionyesha ni  aina ya wanaume ambao wanadharau kiana hivi kutokana tu na wajihi wake.

Wote watatu  walizidi kuonyesha hali ya dharau mara baada ya macho yao kutua katika sura ya  Hamza  akiingia  hapo  ameongozana na Regina.

“Regina kwanini umekuja  na  Bodigadi  mpaka   hapa ndani , huu ni mkumsanyiko wa  kifamilia hatuihitaji mtu wa nje”Aliongea  mwanaume yule  kijana huku  akimwangalia  Hamza kwa kumnyali.

“James kama unalijua hilo  basi na wewe hupaswi kuwepo hapa  , kuhusu  mwanaume niliekuja nae  naomba nikutambulishe  leo hii , huyu ndio Boyfriend wangu”Aliongea  huku akimsogelea Hamza karibu.

Mara baada ya James  macho  yake  kuona tukio hio  alijikuta  akishikwa na wovu mkali na sura yake kukunjamana..

“Acha kuongea ujinga Regina ,  tangu lini ukawa na boyfriend ghafla tu”

“Tumekutana kupitia njia ya mtandao  zaidi ya mwaka moja uliopita ,  ni  juzi tu hapa nilijua yupo  Dar na tukaamua kuanzisha mahusiano”Aliongea Ragina, kwa namna ambavyo alikuwa amejiandaa kumtambulisha Hamza, alikuwa akijiamini na maneno yake.

Upande wa  Hamza aliweza kuona hali hio  ambayo haikuwa tulivu na ni mwenye kuangaliwa kwa dharau lakini hata hivyo hakujali.

“Mjomba hapo , Shangazi pale  na Braza  mbele hapo,  salamu kwenu ….”

“Nyamaza wewe mjinga , mimi ndio mchumba halali wa Regina sio wewe  bidhaa ya kuokotwa  dakika za mwisho kwa ajili ya maigizo”Aliongea James kwa hasira.

“Braza .. unamaanisha mimi au , haha.. unachekesha mno”Aliongea Hamza na baada ya pale alimpotezea na kisha akamvutia kiti  Regina na kisha  cha kwake na kuketi chini.

“Regii , anza kukaaa”Aliongea Hamza  akimpa ishara  Regina kukaa  na James  mara baada ya kuona namna  Hamza  anavyomwita Regina kwa nickname  uso wake ulikunjamana.

Hamza hakuona  kabisa  shida juu ya macho mabaya yaliokuwa yakimwangalia   na alikaa mara baada ya Regina kukaa  na kisha akatoa tabasamu akiulizia msosi.

“Mshaagiza tayari , nilipata  chai asubuhi lakini bado najihisi njaa”Aliongea lakini kwa bahati mbaya ni kwamba hakuna ambae alimjibu.

“Regina nini unajaribu kufanya? , hivi unachukulia ndoa kama mchezo sio, James ni mwaminifu  sana  na amekuwa akikusubiria ufanye maamuzi  zaidi ya  miaka sasa , uwe  na ukomo basi  wa ubishi wako”Aliongea mwanamke ambae alionekana kuwa mrembo  licha ya  umri kuenda.

“Nyie ndio ambao mnalazimisha juu ya hii ndoa tokea mwanzo na wala sijakubali ,  kwasasa  nishapata  mwanaume ambae  nataka awe mpenzi wangu , kwanini  ionekane ni kama naleta ukiburi”

“Hey! Leta walinzi mara moja wamfukuze huyu mtu”Aliongea mwanaume wa makamo akiwa siriasi.

“Hakuna wa kumuondoa hapa ,  huyu ni mpenzi wangu , kwanini hakuna ambae anaonekana kunielewa hapa?”Aliongea  Regina huku akijaribu kuonyesha ukiburi.

“Ni kweli  kabisa mimi  na Regi ni wapenzi  na sio kuwa wapenzi tu  tunapendana sana”Hamza alijitahidi kuongea  huku akijiambia hii familia haipo vizuri kimahusiano  na  malumbano yao yatafikia hatua   hawezi kupata chakula tena.

“Sijategemea hii kazi kuwa ngumu hivi , mbona  hakusema kama tayari alikuwa na mchumba , kuja kwangu hapa ni kama kuibua ugomvi tu , hebu kwanza  muangalie huyu anaeitwa mchumba wake , anaonekana ni mtu tajiri  lakini kwa namna anavyoniangalia kwa chuki  nadhani  nimejipalia makaa”

Ningejua tokea mwanzo mambo yanakwenda kuwa magumu hivi juu ya hii kazi,bora hata ningeomba malipo  makubwa zaidi”

Hamza alikuwa akijiwazia yeye mwenyewe ,  alikuwa akijitahidi kuendana na mazingira lakini  kwa namna mazingira yenyewe yalivyo ilionekana ni kazi kubwa sana ambayo  kwa mshahara aliokuwa akipewa katika ajira yake hio   ulionekana  mdogo.

“Regina hebu nisikilize mimi baba yako , kutaka uolewe na James ni kwa ajili ya faida yako mwenyewe ,  hebu acha ukiburi  basi”

“Ni kwa faida yangu au ya kwenu , nadhani majibu kila mmoja anayo katika  moyo wake”Aliongea Regina  na kisha alimwangalia yule mwanamke, ambae jina  lake anaitwa Lamla.

“Regina unaongea nini , usione unaweza kuongea chochote mbele angu kwasababu tu  ni CEO wa Dosam , ijapokuwa  sijakuzaa  lakini mimi ndio nimekulea kwa miaka  kumi , kwanini  unaniona kama mtu mbaya?”Aliongea Lamla  na palepale macho yake yalianza kuwa mekundu akionyesha anataka kulia.

Mzee Wilsoni mara  baada ya kuona mke wake anataka kulia  , haraka sana  aliweka mkono wake  begani  na kuanza kumbembeleza.

“Aiya , Darling  usikasirike , Regina  hajamaanisha hivyo , usimuelewe vibaya..”

“Ni kweli  hajamaanisha hivyo , Regina  ni mtiifu sana  na mkarimu  na hiki ndio ninachokipendea kutoka kwake ndio maana nataka aje kuwa mke wangu kwa namna yoyote ile , anaweza asipende kwasababu  nimewatumia  nyie kumfikishia nia yangu  ndio maana  anagoma kufanya maamuzi”Aliongea James.

“James  wewe ni kijana muelewa ambae una mfahamu vyema Regina , wewe umemsikia mwenzako   namna  anavyojitahidi kukuelewa , kwanini usimuombe radhi  kwa kitendo chako cha kumleta  mwanaume  wa maigizo hapa”

“Daddy , haina haja ya kunilazimisha  na kunisihi , sina mpango wa kuolewa na James mimi”Aliongea na kisha akamgeukia James .

“Jikatie tamaa tu , Dosam ni kampuni niliopewa  na babu yangu  kuiendesha  na sipo tayari kuona inaangukia katika mikono  ya mtu wa nje ya familia , huwezi kunipata na  pia huwezi kuipata  kampuni yangu”

“Regina  , unaongea nini , sina matamanio yoyote na kampuni yako , isitoshe sina akili ya kibiashara kama wewe, macho yangu  na moyo  wangu unakuelekewa wewe tu siku zote , kwanini unashindwa  kuona ni jinsi  gani nakupenda Regina,”

“Haijalishi  unaongea ukweli au uongo  wewe ndio unaejua .. halafu usifikiri sijui wewe  ndio unaehusika   kunyanyasa wafanyakazi wa kampuni yangu”

“Regina unaongea nini , nani ananyanyasa wafanyakazi , mbona sijawahi kusikia juu ya hili?”Aliuliza mzee Wilsoni.

“Regina  labda utakuwa umekosea , James hawezi kuhusika”Aliongea Lamla.

Upande wa Hamza mara baada ya kusikia kauli hio alijua pengine tukio la Eliza  kunyanyaswa na wale wadeni wake lilikuwa likihusiana na  swala analoongelea Regina , ila hakuwa na uhakika.

Regina  hakuwa hata na mpango wa kuendelea  kuzungumzia swala hilo , maana hata kama aseme hakuwa na ushahidi wa moja kwa moja.

“Kama nilivyosema , nishapata  mpenzi tayari   hivyo  kwanzia sasa sitaki kusikia maswala ya ndoa”Aliongea

James licha ya kwamba alikuwa na tabasamu lakini  uso wake ulikuwa wa kikauzu mno , ilionekana alikuwa akilazimisha furaha.

“Haha…haina shida Regina ,  mimi ni mtu mvumilivu, nani anajua , pengine  mnaweza kuachana kesho  au kesho kutwa , nadhani wakati huo utanifikiria”Aliongea James huku akitoa kicheko, na maneno yake  yalionekana kuwa na zaidi ya maana.

“Wilson  sitaki kumuona huyu masikini mbele yangu , hebu ita watu waje wamtoe  kama unataka niendelee kubakia hapa”Aliongea  Lamla.

“Akiondoka na mimi  naondoka”Aliongea  Regina.

“Wewe..”

“Madam  usiwe na hasira , haijalishi  akikaa  hapa na kula chakula tulichoandaa ,  iwe ni familia yenu au yetu  pesa sio tatizo , chukulia  tu kama msaada kwa mpitaji, sidhani kama ni tatizo”

“Mh! , Kwasababu wewe ndio umeongea James basi sina jinsi na kumuacha”Alijibu Lamla..

Upande wa  Regina  alikuwa na wasiwasi  , aliogopa  James anaweza akawa na mpango kichwani  usio mzuri anapanga kuufanya 

Muda  uleule  alimwita  mhudumu wa mgahawa huo wa kifaransa   na kisha alibadili  kutoka lugha ya kiswahili na kuongea kifaransa.

“Prenez la commande  de ce monsieur , soyez pls professionel..”Aliongea   akimwamlisha muhudumu kuchukua oda kutoka kwa Hamza  lakini awe profesheno zaidi huku wakati uleule akimkonyeza.

Muhudumu yule wa kike ambae  alikuwa akifanya kazi katika mgahawa wa matawi ya juu kama huo alikuwa akijua kuongea kifaransa   na  alielewa  kauli ya  James kwa haraka sana .

“Mmonsieur , Que desirez-vous?”.

Mhudumu huyo alikuwa ni mbongo tena mrembo  aliejazia kifua , lakini licha ya hivyo aliweza kuajiriwa katika mgahawa huo wa hadhi ya juu utokana na elimu yake na Exposure , ilikuwa hivyo kwa wahudumu wote.

Upande wa Regina alikuwa ashausoma mchezo tayari , alichokuwa akitaka kufanya   James  ni kumuaibisha  Hamza  na kumchezesha shere kama mjinga.

Ni kama alikuwa akitaka kumwonyesha yeye  ni wa daraja la chini , mtu ambae hakuwa  akistahili kuingia katika mgahawa wa  hadhi ya juu kama huo.

Regina mwenyewe hakuwa vizuri kwenye lugha ya kifaransa hivyo alitaka  kuingilia kwa lugha ya kingereza akimtaka  yule mhudumu kuongea  kingereza.

“Waitress please speak ..”

“Le-menu  s’il-vous -platue me consillez Vous?”(“Niletee  menu  ya mapendekezo ya vyakula  nichague”)

Wakati Regina anataka kuongea , palepale alijikuta akisikia sentensi ambayo hata yeye hakuielewa ikimtoka Hamza.

Hali ya ukimya  ilivaa watu wote waliouwa ndani ya chumba  hich cha hoteli , Mzee Wilsoni , Lamla na James wote walikuwa katika hali ya mshituko.

Aliekuwa katika hali ya kushangaaa zaidi alikuwa ni  Regina , macho yake  mazuri yaliongezeka ukubwa huku akimwangalia  Hamza.

Upande  wa muhudumu mara baada ya kuona  amejibiwa alijikuta akishangaa kidogo lakini akaupotezea mshangao wake kwa haraka.

“Sir , nitaenda kukuletea Menu  haraka , nisamehe kama nimekuwa mkorofi”Aliongea yule mhudumu , alikuwa amesikia vizuri Hamza  na kumuelewa  kwani  alikuwa ameongea kifaransa kilichonyooka ,  na matamshi ya Hamza kwa uzoefu wake   aliona hata yeye hakuwa vizuri , hivyo hakutaka kuleta ujanja tena wa kuongea kifaransa mbele ya mtaalamu wa lugha hio.

Dakika chache tu Menu ililetwa na  Hamza alitoa oda yake kwa kutumia lugha ya kifaransa  na kisha akamgeukia  na  Regina.

“Regi, una agiza nini , nadhani uonje Oulesarinires , desert , Clafautis ….  na kuhusu  kinywaji  nadhani itakuwa vyema  kama ukitumia mvinyo wa Ubelgiji  usio na kilevi , lakini  nadhani hawauzi  hapa , unaweza kutumia tu  mvinyo mweupe..”Aliongea Hamza kama vile  yeye ndio aliekuwa  mwenyewe  na aliowakuta  ni wageni.

“Sir unao uelewa mkubwa na vyakula vya kifaransa,  unapendelea kula  mara kwa mara nini?”Aliuliza yule mhudumu akishangaa kidogo kwnai muonekano wa Hamza ulikuwa tofauti na  matamshi yake.

“Haha.. nakuaje mara kwa mara wakati mimi masikini tu ,  ni kwamba tu nina mazoea ya kusoma soma vitu  ndio maana..”

Baada ya kuongea hivyo ilimfanya kila mmoja sasa angalau kuelewa  , huku wakijiambia hakuna uwezekano masikini kama Hamza kuwa na uelewa wa vyakula vya kifaransa.

lakini upande wa  Regina   yeye alikuwa tofauti , hakushawishika kabisa na maneno ya Hamza , alijiambia  hata kama ni kweli anaweza kusoma  kuhusu vyakula vya kifaransa katika vitabu , vipi kuhusu rafudhi yake  namna anavyoongea kifaransa ,  swala la mtu kujifunza lugha nyingine halikuwa jepesi mno  na lilihitaji muda tena  wa kuishinda ni ya mazingira ya wazungumzaji wa kifaransa.

Kitu kingine ambacho kilimfanya  Regine asiamini ni namna ambavyo  Hamza hakuwa na wasiwasi wakati wakuingia ndani ya mgahawa huo , ilionekana ni kama vile  maeneo  hayo hayakuwa mageni kwake.

Kwa namna moja Regina aliona mwanaume  ambae ni boyfriend wa  maigizo alikuwa   ni mwenye kushangaza  kiana.

 Baada ya kaupepo kale kupita , hatimae chakula kiliwekwa mezani  na kila mtu kuanza kudili  na sahani yake , lakini kwa Mzee Wilsoni alionekaa  bado dukuduku lake juu ya Hamza haikuisha.

“Mr Hamza  umejifunzia wapi kuongea  kifaransa?”

“Ah ,  mimi ni mwanachuo mwaka wa mwisho , na wakati wa masomo yangu  A-Level niliongeza somo  la kifaransa kama la ziada , tokea hapo nimekuwa nikipendelea kuongea kifaransa”

“Kwahio kumbe wewe bado ni mwanafunzi , nilijua pengine ushahitimu kutoka  vyuo vya ufaransa  ndio maana  rafudhi yako kuwa nzuri kumbe bado unasoma , ngoja nikuambie ukitoka hapa achana kabisa na Regina , naweza kukupatia hata kiasi kikubwa cha pesa”Aliongea Lamla.

“Mama .. sihitaji kabisa pesa zako , najua kwasasa  mimi ni masikini  lakini nina nguvu ya upambanaji , nitahakikisha natafuta pesa ya kumtunza  Regina  kwa mahitaji yake yote atakayotaka”Aliongea Hamza.

Upande wa Regina licha ya kujua Hamza alikuwa akiongea hivyo kimaigizo , lakini hakuacha  kuona  aibu kidogo kwani ni kama vile  kauli ile ilikuwa ikimaanisha ukweli.

“Unadhani ni kiasi gani unachoweza kupata kumhudumia  Regina , hivi  unajua ni bilioni ngapi  kampuni ya Dosam inatengeneza kwa mwaka , unamiliki nini mpaka sasa ,  hata ufanye kazi kwa miaka mingapi sio  rahisi   kufika katika daraja ambao tumefikia…”Aliongea Lamla kwa dharau.

Hamza mara baada ya kauli ile alilipiza kwa kumvuta Regina  kwake  na kisha akambusu kwenye shavu  kwa sauti ‘Pop’.

 Regina   aliekuwa bize akijipatia chakula chake alishindwa kuelewa hata tukio  lilivyotokea , kwani kitendo chake cha kuzubaa tayari alikuwa amepigwa busu.

“Kila kitu sio pesa ,  Regina ni zaidi ya pesa”Aliongea  Hamza huku akicheka.

Regina alitaka kumpiga ngumi Hamza , lakini  mara baada ya kukumbuka alikuwa kwenye maigizo alijikuta akivumilia kwa kile alichofanyiwa, ijapokuwa alikuwa na hasira lakini uzuri wake ulimfanya aonekane kama mwanamke ambae anaona aibu kwa kubusiwa mbele ya wazazi wake.

“Paah!!”

James  aligonganisha glasi  ya mvinyo kwenye meza  na kisha akasimama.

“Vizuri , vizuri sana ..”Jamaa huyo mara baada ya kuona mrembo Regina akibusiwa mbele yake alikosa kabisa uvumilivu , aishindwa kumuaibisha  Hamza kupitia mhudumu  lakini vilevile alikuwa amesababisha mchumba wake mwenyewe kubusiwa , hivyo alishindwa kabisa kuendelea kuvumilia.

“Mzee , Madam  kuna kitu napaswa kwenda kushughulikia  , hivyo nitatangulia , tutaonana siku nyingine”Aliongea  na baada ya hapo alizipiga hatua lakini kabla ya kutoka nje kabisa alimwangalia Hamza kwa chuki kali mno.

Regina alikuwa na hasira na  Hamza lakini mara baada ya kuona sura ya hasira ya James alianza kuona wasiwasi juu ya  usalama wa  Hamza

Waziwazi wa Regina  mara baada ya kuona kitendo cha Regina , mtoto ambae  hajawahi kuwa na boyfriend maisha yake yote kukubali kubusiwa mbele yao  walijua lazima ni kweli atakuwa kwenye mahusiano hivyo  hakuwataka kuendelea kuongea na mara baada ya chakula  waliondoka wakiwa hawana furaha.

Upande wa Hamza alimshika mkono mrembo Regina  na   kwa kujiamini kabisa  waliingia katika  lift.

Kitendo cha kuingia kwene lift tu Regina alitaka kumchapa  Hamza kibao  lakini Hamza alimuwahi na kuudaka mkono wake.

“Regina , unataka kufanya nini?”

“Nani kakuambia unibusu?”Aliuliza mwanamke huyo huku akionekana kama mbogo, katika maisha yake hakuwahi kufanyiwa kitendo cha  namna hio na mwanaume bila ya ridhaa yake.

“Sijakubusu  , nilichofanya ni kuigiza kukubusu shavuni , kuna haja gani ya kuonyesha hasira , isitoshe hii ni kazi yangu , unadhani  ningewaaminisha vipi wazazi wako waliokuwa wakiniita  mtu wa maigizo?”

“Mkataba unaeleza wazi kabisa , kama kuna  haja ya sisi kufanya migusano  ni mpaka nitoe ridhaa , kwani hukusoma vipengele?”Aliongea kwa hasira ,Ukwei Regina alikuwa akijiuliza vipi kama pela angegeuka bahati mbaya , pengine wangeishia kugusanisha lipsi  na alizidi kukasirika.

 “Hukuelezea  kwenye mkataba wa kazi kama unamchumba tayari , umenileta hapa   na kufanya watu waanze kuwa  na chuki na mimi , hivi unadhani  walivyokuwa wakinifanyia ni vizuri?, nilikubusu kuwakomoa pia”Aliongea.

“Wewe..”Regina aliishia kutoweza kuongea zaidi ,  aliona  ni kama  kweli lilikuwa kosa lake.

Lakini  yote hayo alifanya kwasababu ya usumbufu wa James kwake kutumia wazazi wake kutaka  afungishwe ndoa , ndio maana akafikia uamuzi mgumu , lakini haikuwa hivyo tu  ili kutii masharti ya  urithi alioachiwa na kutunza siri ya ugonjwa wake.

Moja ya sharti  la  urithi wa kampuni alilopewa Regina  katika wosia wa babu yake ni kuolewa  ndio atakuwa mrithi  kamili  wa kampuni ya Dosam , na kama hatokidhi kigezo hicho  ndani ya miaka  kumi  basi  baba yake angekuwa  mrithi wa  mali za familia.

“Unaongeaka hata wewe unamjua yule  James sio mtu mzuri , nilitaka kumuaminisha wewe ni mpenzi angu , ili akuache , mtu kama yule huwezi kumkataa kwa  maneno tu , kwa urembo wako kama huu  hawezi kukata tamaa kirahisi  labda  tu  umwaminishe umeolewa  na si vinginevyo”

“Sidhani kama ni kweli , kuna wanawake warembo sana ,  anachotaka yeye ni mimi  tu kwasababu kampuni yake haifanyi vizuri  kwa miaka mitatu mfululizo  na anashindwa kushindana na mimi  likija swala la mauzo , anachotaka ni  mimi niolewe nae ili kuimeza  Dosam”

“Wazazi wako hawajuia juu ya hilo?”

“Sio swala jepesi kukuelezea  na hupaswi kujisumbua pia juu ya hili”Aliongea na kisha alirudia ukauzu wake na ndani  ya dakika chache tu walitokea katika maegesho ya magari.

“Unajua kuendesha gari?”Aliuliza Regina na kumfanya Hamza kushangaa maana alikuwa ashajidaa kuondoka zake  lakini ilionekana bosi  wake alikuwa na mipango mingine na yeye.

“Najua ndio ila sina leseni”

“Kuna taarifa ya kikao   nataka kuindaa na nimechelewa ,  nisaidie kuendesha  mpaka ofisini kwangu”Aliongea.

Hamza hakuwa na hiyana , hata hivyo ni kama ashajiuza kwa  pesa taslimi  kwa mkataba hivyo hakuona haja  ya kukataa.

Hamza alitoa gari hio kwenye maegesho  huku akipewa onyo asiendeshe kwa spidi kubwa  na alitii ,  safari nzima mrembo huyo alikuwa  bize na Ipad  yake akionekana kufanya kazi akiwa hana habari kabisa.

Hamza alikiri mwanamke huyo   alikuwa na ukauzu sio wa kawaida , pengine ndio maana  hakuwa na boyfriend mpaka akatangaza ajira.

Wakati  Hamza akiingia Morogoro Road macho yake yalicheza mara baada ya kugundua gari alioona  wakati wakitoka  kule hotelini ikiwa ipo nyuma ya na aliishia kutoa tabasamu hafifu  na kujiambia   tayari ashayakoroga  lakini hata hivyo  ni kama hakuwa na uhakika kama  alikuwa akifatiliwa yeye  au alikuwa akifatiliwa  Regina.

Hakutaka kujali wala kuwapoteza , aliendesha gari polepole mpaka  maeneo  ya mawasiliano  sehemu ambayo   makao makuu ya kampuni ya Dosam hupatikana.

Jengo  la  makao makuu ya Dosam  lilikuwa likivutia mno , lilijengwa kwa usanifu wa hali ya uu na ilikuwa ni fahari ya macho kwa  eneo hilo, ilikuwa refu kwenda juu kwa  ghorofa  arobaini. Hivi na  lote lilitumika kwa  kampuni , ilikuwa ni kama   ishara  ya jinsi kampuni ya Dosam ilivyokuwa kubwa.

Hamza  mara baada ya kuingiza gari  hio katika maegesho kwa maelekezo ya Regina mbele yake aliona  mwanamke ambae alikuwa amesimama kikakamavu katika eneo la maegesho , ilikuwa ni kama vile alikuwa akiwasubiria na huyo alikuwa tofauti na aliekutana nae kule  hotelini wakati wa usaili.

Kwa macho ya haraka haraka tu , Hamza aliamini mwanamke huyo atakuwa ni bodigadi  kama ambavyo  Regina alisema alikuwa na bodigadi.

Mara baada ya kusimamaisha gari mwanamke yule  kikakamavu kabisa alisogelea gari hio na kisha akafungua mlango wa abiria  akimpa nafasi  Regina kutoka.

Hamza alijikuta akiangaliwa kwa macho ya  kikauzu   na mwanamke yule mara baada ya kushuka kwenye gari hio , ilikuwa ni kama vile mwanamke  yule anataka kummeza  na hata pale alipotaka kumsogelea karibu Regina alizuiwa kwa mbele jambo ambalo lilimfanya Regina kutabasamu na kujiambia huyu mtukutu  mbele ya  bodigadi wake hawezi kumchukulia faida.

Kwa kumwangalia mwanamke huyo licha ya kwamba alikuwa  na sura ya kirembo  iliofichwa na ukakamavu wake , lakini ilioneysha alikuwa na mazoezi makali  ya kijeshi.

Hamza alikuwa na uwezo wa kuona namna muunganiko wa mwili wa mwanamke huyo ulivyokuwa sahihi.

‘Yonesi Dustani’ Secirity team leader’ ndio jina ambalo lilisomeka kwenye  kitambulisho chake.

“Yones hali ya  Eliza ikoje?”Aliuliza Regina.

“Madam CEO ,  sijui  nini kimetokea lakini leo  amefika  Amosi  na kuomba msamaha  kwa Eliza  na kuahidi deni lake kwanzia muda huo limeisha”Aliongea  Yonesi na kumfanya  Regina kushangaa.

“Kwanini  wabadilike  wakati katika ile vidio  walionyesha kumdhalilisha  Eliza  kiasi kile?”Aliongea Regina   na  kauli yake ile ni kama sasa ilimfanya  Hamza kujua kinachoendelea.

“Hata mimi nimeshindwa kuelewa ,vipi  tuendelee kuwachukulia  hatua kama ulivyotoa maagizo?”

“Kama  wameahidi kutokumsumbua tena , haina haja ya kwenda mbali , isitoshe  wanaonekana kuwa na mtu nyuma yao, nitaongea na   Eliza”Aliongea  Regina  na  Yonesi alitingisha kichwa na muda uleule  Regina alimgeukia Hamza.

“Utaishi  nyumbani kwangu kwanzia leo hii  na kuendelea ,  kama una mizigo nitamwagiza  Yonesi kukusindikiza”Aliongea.

“Nini ,  unataka tuishi pamoja?”Aliuliza  Hamza kwa mshangao.

Hata yule mwanamke aliefahamika kwa jina la Yonesi alikuwa katika mshangao pia, hakutaka sana kujali maisha binafsi ya  bosi wake  lakini ilikuwa ngumu kwa mwanamke  wa hadhi ya juu kama Regina anaweza kukubali kuishi  na mwanaume wa   kawaida  kama huyo na alijiuliza ni nani.

Mara baada ya  Regina kusikia neno kuishi pamoja  muonekano wake ulibadilika  na akavuta pumzi nyingi za masikitiko.

“Ulinzi  nyumbani kwangu ni mzuri , hivyo angalau kwa   muda hamia , unachokifikiria  hakipo”Aliongea

Hamza  mara baada ya kusikia  kauli hio  kavu   kiasi flani alijisikia vizuri  na kuona kwamba mwanamke huyo alikuwa akijali usalama wake, isitoshe alikuwa tayari ashatengeneza maadui kwa kutangazwa kama boyfriend , ijapokuwa aikuwa feki lakini watu wale walimchukulia siriasi.

“Yonesi naomba  umsaidie kumpa  ulinzi huyu mtu  , yupo kwenye matatizo , nenda nae anapoishi na  mchukue mzigo yake  na kisha   umpeleke nyumbani kwangu , Aunt Maliposa  atajua cha kufanya”Aliongea Regine asitake kumpa nafasi Hamza kuropoka tena.

“Sawa, Madam”

Licha ya kwamba  alikuwa na  wasiwasi pamoja na kusita lakini alitii maagizo ya bosi wake.

Hamza aliona  namna ambavyo  Regina aliongea kibosi , lakini kwasababu   ilikuwa ni kwa ajili yake  aliona  haina mbaya  kuishi kwake licha yeye kama mwanaume hakutaka kuishi kwenye nyummba ya mwanamke.

“Hey ,Acha  ndoto za mchana , ingia garini”Yonesi aliongea kwa kufoka.

“”Hey Mjeda , niite  Hamza tu inatosha , siitwi Hey”

“Unaishi wapi ?”Aliuliza hata asimjai Hamza.

“Gongo la mboto Kivule”Aliongea Hamza na kumfanya  Yonesi kumwangalia  Hamza na mavazi yake ya kisasa kabisa ya bei ghali  na alijikuta akikunja ndita.

“Mh , unaishi  huko uswahilini  kweli?”

“Yeah  kunaweza kuwa uswahilini  , lakini ndio ambako  kodi ipo chini, nilipanga nikitoboa  kimaisha  naja kwenye maeneo ya kifahari, usiangalie sana mavazi yangu , Regi ndio ambae ameninunulia , sio za kwangu”AliongeaHamza akijihami.

******

Saa saba mchana Frida  alionekana akiingiza gari ndani ya  hospitali  na taasisi ya kitafiti ya Neuroscience  inayopatikana Kibaha , kilomita kadhaa kutoka   ilipo hospitali ya Tumbi.

Ilikuwa ni  hospitali kubwa mno na ya kisasa yenye jengo moja lililoenda hewani kwa ghorofa  kumi kumi na  nane hivi  na kufanya kuwa jengo refu zaidi ndani ya  mkoa wote wa Pwani.

Hospitali  hio ilijengwa  kwa msaada wa watu wa Marekani kupitia  shirika na taasisi isiokuwa ya kiserikali ifahamikayo kama  Haliz Neuroscience Foundation(HNF).

Taasisi ya Haliz ilisifika dunia nzima kwa kujikita zaidi katika kuutafiti ubongo na  maswala ya neva kwa ujumla wake , sera ya taasisi hio  ilikuwa ni kuwezesha mataifa mengi kujifunza namna mfumo wa ubongo na neva unavyofanya kazi  na hii imechangia sana kufungua matawi yake mengi karibia nchi nyingi duniani.

Mashirika ya Afya ya umoja wa kimataifa yalikuwa yakiunga mkono kazi kubwa ambayo ilikuwa ikifanywa na taasisi hii kubwa ya  kimarekanni  isiokuwa ya faida(Non-profit organisation).

Katika miaka ya hivi karibuni  maendeleo ya sayansi ya neva  na ubongo yalikuwa yamepiga hatua kubwa sana , wale wagonjwa ambao walikuwa wamepoteza kumbukumbu ilikuwa rahisi kurejeshewa  kumbukummbu zao ndani ya muda mfupi  tu chini ya taasisi hii ya Haliz.

Haikuwa wagonjwa waliopoteza kumbukummbu tu , watu wengi ambao walionekana kusahau mambo muhimu katika maisha yao , iwe ni  kubukumbu za utotini  au  za ukubwani  taasisi ya Haliz ilikuwa na teknolojia ya tiba ya kurahisisha hayo yote.

Licha ya taasisi hio  kufanikiwa lakini bado utafiti wa kuujua  ubongo wa binadamu ulikuwa ukiendelea zaidi , kwani  wanasayansi wanaamini  ubongo uwezo wake ni  mkubwa kuliko ile ambavyo  inadhaniwa  , hivyo wanaamini kuuwezesha ubongo kufikia uwezo wake kamili kimatumizi  italeta maendeleo makubwa.

Frida alitembea kwa kujiamini kabisa  ndani ya hospitali hio huku akipokelewa na harufu ya taasisi hio  yenye kuzoeleka katika pua zake, kwa namna baadhi ya wafanyakazi wa taasisi hio walivyokuwa wakimsalimia  kwa kutingisha vichwa ilionekana  alikuwa ni mfanyakazi mwenye cheo.

Aliishia kutoa tabasamu huku akitingisha kichwa  kwa kuonyesha tabasamu kwa baadhi ya watu aliopishana nao ndani na  ndani ya dakika kadhaa aliweza kuzifikia  lift na kuingia ndani, lakini kabla hata ya  mlango wa lift haujajifunga mwanaume  mzungu wa makamo alievalia koti la kimaabara   aliweza kuzuia lift hio na kuingia ndani.

Alikuwa  ni mtanashati kweli  aliependezeshwa na miwani   ya macho ,  huku akiwa amepambwa na tabasamu.

“Well!. Fancy meeting you here, Frida”Aliongea yule mzungu na kumfanya  Frida kutoa tabasamu.

“Una ajenda gani kukimbilia lift Blake, huu si muda wako wa kufanya Demostrations na wanafunzi?”Aliuliza Frida na kumfana Blake kutoa kicheko kama anakohoa.

“Ndio nimemaliza, kulikuwa na mabadilishano  na Dr John , Vipi wewe  ndio umekuja kutubariki  na utaalamu wako?,nilidhani upo likizo?”

“Nipo likizo ndio ,  lakini haimaanishi sipaswi kufika  hapa , nina biashara  katika floor ya  kumi na saba”

“Wow!, Wow! , Floor  ya wabobevu, sina neno la kuongezea, it’s nice to see you Frida”Aliongea Dr Blake na  ni muda uleule Lift ilisimama  katika floor  ya  kumi na  bwana huyo mzungu alitoka akimuacha Frida kuendelea na safari yake.

Frida aliishia kutoa tabasamu tu huku akiangalia namna ambavyo  Blake anapotelea kwenye macho yake wakati lift ikijifunga.

Haikuwa kama ambavyo  amesema Frida  kwani mara baada ya lift kufika  katika foor  ya  kumi na saba  alitoka katika lift na kuingia katika floor hio ambayo ilikuwa na utulivu wa hali ya juu , ilikuwa ni ubaridi tu na  harufu ya kuvutia , huku rangi ya taa zisizokuwa na mwanga mkali zikipendezesha eneo hilo.

Frida hakuingia ndani ya Foor hio bali alizunguka upande wa kushoto kwake na kuanza kupandisha ngazi kuelekea juu  na ndani ya dakika chache tu aliweza kutokezea juu kabisa ya jengo hilo.

Licha ya kwamba alionekana kutembea kwa haraka, lakini kwa namna ambavyo alikuwa na spidi hakuonyesha hata kuchoka, alionekana kama aina ya wanawake ambao walikuwa na mazoezi makali.

Baada ya kutoka katika paa kabisa ya  jengo hilo refu na kumfanya kuona mazingira ya mji wa Kibaha na baadhi ya maeneo ya Dar es salaam na Bagamoyo  alivuta pumzi na kisha aliendelea kupiga hatua kusogea mbele.

Hali ya hewa haikuwa ya jua kali ,ilikuwa ni kama vile mvua ingenyesha muda wowote.

Mbele yake Frida alikuwa amesimama mwanaume alievalia suti  ya rangi ya bluu akiangalia upande wa  maeneo ya  Dar es salaam kwa umakini mkubwa kana kwamba  kuna kitu alichokuwa akitafuta.

Alikuwa ni mzungu kwa muonekao wa nywele  tu  na kadri Frida ambavyo alikuwa akitembea  hatua  zake zilionyesha hali ya  kuwa dhaifu  kiasi.

Kama ilivyo mwanaume yule alivyosimama ndio namna ambavyo Frida alienda kusimama katika ukingo wa jengo hilo na kuendela kuangalia upande wa mbele yake, ilikuwa ni kama vile anamwigizia yule mtu , na upande wa yule mtu hakugeuka kabisa  ni kama alijua   nani amefika  hapo na kusimama pembeni yake.

“Any progress on KF-Target?”Aliongea  yule mzungu kwa sauti nzito.

“We are  almost there ,I’ve initiated  a plan to bring him closer to me, his curiosity will ensure our swift entry  into the next phase”Aliongea akimaanisha  kwamba  anakaribia kumaliza ,  na ameanzisha mpango  wa kumuweka karibu , anasema  shauku yake itawafanya waingie  hatua   inayofuata kwa haraka”

“Elezea”Aliongea.

“Nimemfanya  anifanyie Delivery  ya  Viungo  vya akili kutoka Binamu , uhakika ni kwamba atauliza maswali juu ya  malipo makubwa yanayolipwa kwa ajili ya chungu kimoja kama njia ya usafirishaji, kwa kile nilichoona amevutiwa”

“A risky move”

“Calculated Risky Sir”Aliongea Frida kwa kingereza na jibu lake  lilimridhisha.

“Vipi kuhusu  wale wengine , namaanisha wanaoangalia kutoka mafichoni?”

“We are keeping eye on them , once we have what we need, they ‘ll be nothing more than loose ends”

“Endelea  na kazi kwa umakini , hatuwezi kuruhusu kosa lolote”

“Umeeleweka”

“Sinagogi  wanataka  hii misheni  kumalizika  kwa haraka , siku zijazo utashughulikia na zaidi ya mtu mmoja katika tafiti yako , mategemeo makubwa yamewekwa juu ya hii sayansi mpya Frida ,natumaini  kila kitu kitaenda sawa,Hatuwezi kuruhusu washindani wetu kupiga hatua kablsa yetu”

“Ili mradi malengo yanakuwa wazi ,  kila  kitu kitaenda sawa , natumaini utakuwa vizuri kwenye kuwatoa  wasiwasi”

“Kama ni hivyo tutaonana   tena katika hatua  inayofuata kujua maendeleo”Aliongea yule mwanaume na ilitokea kitu kama upepo tu kwani alipotea palepale na wala  hali ile isimuogofye  Frida ikionyesha ni jambo  ambalo amezoea.

 

 

Previoua Next