Hamza alitegemea angemkuta tu Shangazi nyumbani lakini ajabu yake ni kwamba alimkuta Eliza na Regina wote wakiwa nyumbani.
Regina alikuwa ameketi upande wa kulia mwa Eliza akiwa ameshikilia glasi ya juisi na mara baada ya Eliza kumuita Hamza kwa jina lake alishangaa. “Eliza , unafahamiana na Hamza?”
Ijapokuwa Eliza alikuwa katika mshangao na maswali kibao ya kwanini Hamza yupo nyumbani kwa bosi wake lakini aliitikia.
“Ndio nimefahamiana nae majuzi tu hapa , ndio mtu ambae alinisaidia wakati Amosi na kundi lake walipotaka kunichukua kwa nguvu..”Aliongea Eliza.
Hakutaka kuelezea kama jana Hamza alilala nyumbani kwake na aliondoka asubuhi, isitoshe uhusiano wao ni kama haukuwa wazi kama ni wapenzi au lah.
“Oh!”
Regina hakutegemea kuona kwamba Hamza ndio mtu aliemsaidia Eliza wakati akidhalilishwa , hakuweza kujizuia kushangaa.
“Ilikuwaje akakusaidia, mlifahamiana kabla?”Aliuliza mrembo huyo , alikuwa na mapozi hata wakati wa kuongea.
“Bosi , kwani sio kama yupo hapa kama fundi pia ? , ni mtengenezaji wa AC na kuna mama mmoja ndio alinikutanisha nae baada ya Ac yangu kupata hitilafu , wakati anakuja kutengeneza ndio akanikuta nipo kwenye matatizo akanisaidia , mwenyewe anasema ni fundi wa kila kitu kinachotumia umeme”Aliongea Eliza bila kuacha kuweka chembechembe za kumsifia Hamza.
Lakini kitendo cha kusikia kauli hio , mrembo Regina alijua amedanganywa tena , na kuona ndio maana jana alifika na kuanza kutengeneza TV yake lakini haikuwa hivyo tu alikuwa mwanachuo na mwalimu kwa wakati mmoja na kujiuliza Hamza ana kazi ngapi anafanya.
Hamza upande wake alikuwa ameurudia ule muonekano wake kizembe uliomfanya kupigwa cha mbavu hadharani na Anitha wa chuo,alijifanyisha kutokumjua Eliza kwa undani.
“Boss , umemuita kwa ajili ya ufundi?”Aliuliza Eliza huku akimwangalia Hamza.
Swali lile ni kama ghafla tu lilimletea Regina maumivu ya kichwa ,hakutaka kabisa siri yake ifahamike , alijua kama itakuja kufahamika alikuwa ameajiri mtu wakuigiza kama boyfriend angeonekana mwanamke wa ajabu mno.
“Unaonaje tukienda kuongea maswala ya kazi katika ofisi yangu kwanza , kuna baadhi ya vitu pia nataka ukavifanyie kazi”Aliongea Regina akiwa na muonekano wa kibosi ,Eliza alikuwa ni mwanamke ambae anajali zaidi kazi hivyo asingeendelea kuuliza.
Kitendo cha wanawake hao kupandisha juu , ilimpa Hamza ahueni na haraka haraka alikimbilia jikoni na kuchukua maji ya baridi vikombe vitatu na kushusha vyote ili kuirudisha mudi yake.
Shangazi aliishia kumwangalia tu Hamza , kuna namna flani mwanamama huyo alielewa kinachoendelea na kumfanya hata Hamza kukosa utulivu.
“Regina alikuwa akionyesha kukujali ndio maana alikupigia , kwanini ulimkatia simu bila ya kuongea neno?”Aliuliza shangazi.
“Shangazi mbona unatania , Regina anijali mimi?, si ndio yeye alienifukuza hapa usiku usiku”
“Ni kweli ,lakini baada ya kumwambia maisha yako yalivyo na kwanini uliongea vile alionekana kukuelewa”Aliongea Shangazi , kwa namna moja alionekana kama vile alikuwa akitaka wawili hao wapatane.
Hamza na yeye alionekana kuelewa , na aliona Regina pengine ni tabia yake , ana kauli zenye ukali mno na mwenye kubadilika badilika ila ni mwenye roho nzuri , kwa alichosema Shangazi kilimfanya aone haina haja ya kuondoka.
“Tutabanana hapa hapa mpaka kieleweke, haondoki mtu hapa”Aliwaza Hamza akisahau mkataba wa kuishi maisha mazuri karibu na mrembo wa matawi ya juu unaisha ndani ya miezi mitatu tu.
Baada ya lisaa kupita , hatimae Eliza alishuka sebuleni na kumuaga Shangazi kama anaondoka , Hamza muda huo alikuwa akiangalia TV huku miguu ikiwa juu ya sofa na Eliza upande wake hakuonyesha hata kujali , kuna namna flanni ilimuambia Hamza anaishi hapo kwa namna alivyokuwa amejiachia kwenye sofa.
Hamza mara baada ya kuona mrembo huyo ameondoka kabla ya kumuaga alimuwahi.
“Eliza naomba unisikilize”Aliongea kabla hata hajaingia kwenye gari lake
“Unataka kuongea nini?”Aliuliza akiwa na uso usiokuwa na masikhara kabisa.
“Sio kama unavyofikiria mimi na Regi..”Hamza alisita kuendelea mara baada ya kukumbuka kipengele cha mkataba kilimtaka uhusiano wao kubakia kuwa siri.
Eliza aliendelea kumkazia Hamza huku akimwangalia namna ambayo anajikuna kichwa kwa kukosa kujiamini lakini kitendo cha kuona mwanaume huyo anavyohangaika kujielezea alitoa kicheko.
“Eliza mbona unacheka, inamaana unajua tayari?”Aliuliza kwa wasiwasi
“Uitana ukifanyia surprise sio , kuna haja gani ya kuficha sasa , nishajua tayari umekuwa mwajiriwa wa kampuni yetu na unaanza jumatano”Aliongea Eliza na kauli ile ilimuacha Hamza mdomo wazi.
“Ajira gani tena?”Ndio wazo la kwanza lililomjia Hamza akilini.
Kabla hata hajaongea chochote sauti kutoka ndani ilimwita.
“Hamza njooo kwenye chumba changu cha kujisomea”
“Tutaongea siku nyingine, nenda haraka bosi anakuita nawahi mwendokasi kwenda Morogoro kikazi bye”Aliongea Eliza huku akimwangalia Hamza kimahaba na kisha aliingia kwenye gari yake na kuondoka.
Hamza hakuwa akielewa chochote na ni kama alikuwa amechanganyikiwa , na kimya kimya alienda mpaka chumba cha kujisomea cha Regina.
Baada ya kuingia ndani akiwa na muonekano wake wa kizembe alifunga mlango na kuanza kujikuna kichwa kama mwanaume ambae amekosa kujiamini. “Regina umemuambia nini Eliza juu yetu?”
“Nimemuambia mimi na wewe tulikuwa marafiki wakati tukiwa wadogo katika kituo cha kulelea Yatima na tumekutana majuzi tu hapa , kwasababu ya maisha yako kuwa magumu sana na unasoma nimeamua kukufanya msaidizi wangu binafsi, kuhusu kuishi hapa nimemuambia ni kwa ajili ya kumsaidia saidia Shangazi kazi za nyumbani na kumpeleka sokoni na gari”
“Na ameamini hayo maneno?”Aliuliza Hamza huku neno ‘maisha magumu sana’ likijirudia rudia kwenye kichwa chake na kufanya midomo yake kucheza.
“Nimefahamiana na Eliza kwa muda mrefu ukiachana kuwa mkubwa kwangu ki umri na uwezo wake mkubwa kazini lakini anapenda kuishi maisha ya kawaida na sio mtu wa kufikiria fikiria watu vibaya bila sababu , ili mradi sikuongea kitu ambacho hakina maana nina uhakika ameamini”
“Huoni kwamba ni vibaya kumdanganya mtu anekuamini?”
“Kwahio vipi sasa kama nimemdanganya , au unataka kila mtu kujua mimi na wewe ni wapenzi feki , halafu inakuuma nini kama nimemdanganya , haya ni mambo yangu binafsi haina haja ya kumwambia kila mtu kinachoendelea kwenye maisha yangu”
Hamza alijikuta akishikwa na bumbuwazi , dakika chache zilizopita aliona Regina ukauzu ulikuwa wa nje tu lakini muda huo anaona kabisa ni mpaka ndani.
“Ni kheri uache kujali ya wengine na usaini hii nyaraka”Aliongea akimpatia Hamza karatasi na
Hamnza aliangalia kilichokuwemo kwenye karatasi. “Kwahio ni kweli unataka niwe msaidizi wako , unadhani ratiba zangu za chuoni zinaniruhusu kuwa kazini masaa yote hayo?”
“Mimi na wewe uhusiaon wetu ni wa kikazi zaidi na ili kuficha kazi yako ya kuigiza ni kheri tuwe na namna ya kujitambulisha pindi tutakapoonekana pamoja , isitoshe huu ndio uongo niliomwambia Eliza , hivyo lazima uongo wangu uwe kweli, kingine una vikazi vingi kibao mara fundi mara sijui mwalimu, nani anajua kesho utakuwa unafanya kazi gani nyingine , ili usije kujiingiza kwenye matatizo ni kheri kuwa na kazi ya kueleweka inayoendana na usalama wako
Nilikupigia muda ule lakini ukawa kama vile hujataka kupokea simu yangu, nikajua labda upo na tatizo , mimi kama bosi wako usalama wako pia ni kipaumbele changu”Aliongea bila ya kuwa na hisia zozote usoni.
“Regina muda ule wakati ukiwa unapiga nilikuwa sehemu mbaya … sikuona kama itakuwa vizuri tukiongea ndio maana nilikata simu” “Sijakuambia ujielezee na sijali unachofanya , hayo ni maisha yako binafsi , ninachotaka ni usaini mkataba huu wa kazi”Aliongea kibabe kana kwamba anajaribu kumuogopesha na Hamza akiwa katika muonekano wa kizembe alichukua karatasi na kusaini haraka haraka.
“Watu na bahati zetu bwana , mshahara milioni moja , ukijumlisha na zile … nani wa kukataa kusaini mkataba mnono aina hii”Aliongea Hamza mara baada ya kusoma karatasi hio na kutia saini kwa mbwembwe zote huku akiwa na tabasamu zito usoni , alionekana mtu anaependa pesa mno kuliko kitu chochote..
Laki tano kwa mwezi kuwa boyfriend feki ukijumlisha marupurupu ,milioni moja nyingine ya kuwa msaidizi binafsi , ki ufupi ni kwamba ndani ya miezi hio mitatu aliona atakuwa na kitita cha kutosha.
“Huyu mwanaume muonekano wake ni mzuri , anaonekana kuwa na akili na pia anajua kuongea kifaransa , kinachosikitisha ni kwamba udhaifu wake hufichi hata kidogo , yupo tayari kufanya lolote kwa ajili ya hela”Aliwaza Regina.
“Bosi kwanzia sasa mimi ni msaidizi wako binafsi , lakini vilevile ni boyfriend wako wa maigizo”Aliongea Hamza kijeshi huku akipiga saluti akiwa na tabasamu pana usoni na kitendo kile kilimfanya Regina kutoa tabasamu.
“Usichokijua ni kwamba hadhi ya msaidizi wangu
binafsi mshahara wake ni milioni nne na nusu kwa mwezi…”
“Nini!!.. kwahio unanifanyia dhuluma?”
“Hii ndio njjia ya kudili na mtu kama wewe mpenda hela kupindukia , ambae unaongea kama bila tuo , hii kitaalamu inatiwa jino kwa jino , hakikisha unazingatia vipengele vya mkataba, utakatwa nusu ya mshahara wako kila unapokiuka vipengele”
Kauli ile ilimnyong’onyeza kabisa Hamza na kuona alimchukulia poa huyo mwanamke lakini anazo mbinu za kimafia za kumdhibiti.
Siku iliofuata Hamza alienda chuo kama kawaida na alikuwa na test , alifanya na akamaliza na kisha aligeuza zake na safari yake haikuwa nyumbani bali alienda Kijichi kumuona Dina lakini bahati mbaya hakumkuta hivyo alichukua baiskeli yake na kuanza safari ya kurudi Kigamboni.
Saa kumi kamili ndio muda ambao alifika na Shangazi alimshangaa sana Hamza kurudi akiwa na baisikeli ambayo ilikuwa imechakaa lakini hata hivyo hakuongea sana na Hamza alienda kupaki usafiri wake pembeni na ile Maserati ya Regina tena kwa kuigamiza.
Muda wa jioni wakati Regina anarudi kazini na kukuta ile baiskeli alikasirika mno mara baada ya kugundua alieileta hapo ni Hamza na kumwambia aitoe nyumbani kwake lakini Hamza aligoma na kumwambia ana koneksheni ya kiroho na hio baiskeli hivyo haiendi popote , mgogoro ulikuwa mkubwa mpaka Shangazi akaingilia na Regina akatulia.
Siku iliofuata Hamza hakuwa na kipindi kabisa chuoni , ki ufupi wiki hio hawakuwa na vipindi mpaka wiki inaofuata maana walikuwa mwishoni mwa semista na wangefunga moja kwa moja ingekuwa ni field na Hamza aliona ni kama kupiga ndege wawili na jiwe moja maana anao uwezo wakuomba field moja kwa moja ndani ya kampuni ya Regina.
Asubuhi ya jumatano hio ndio siku ambayo Hamza anaenda kazini na Regina kama msaidizi binafsi
Nguo zote ambazo alikuwa amevaa alipatiwa na Regina , kuanzia viatu mpaka tai , haikueleweka hata leseni ametolea wapi lakini Hamza alikabidhiwa leseni ya jina lake kabisa.
Hamza alishindwa kujizuia na kuishia kutoa pumzi nyingi ya kushangaa na aliona namna ambavyo pesa ilikuwa na nguvu , mwingine kufuatilia leseni ingechukua hata mwezi lakini kwa Regina ilikuwa ni masaa tu alikuwa nayo mkononi , gepu hilo halikuwa dogo hata kidogo.
Akiwa kama dereva ndani ya gari ya Lexus 570 nyeusi, Hamza alikuwa akiboreka kwani foleni ilikuwa kubwa mno , yaani hata baiskeli yake aliona spidi yake ilikuwa kubwa.
Hamza aliangalia kupitia kioo cha nyuma na aliweza kuona Regina alikuwa bize na Mackbook yake akifanya kazi , hakuonekana kuathirika kabisa na foleni ya magari.
Kwa jinsi ambavyo alikuwa amevalia na kupendeza ni kama vile hakuwa akielekea kazini , alikuwa amevaa gauni ambalo limevuka magoti pamoja na blazer ya rangi ya ugoro hivi na alikuwa amepiga nne na kufanya miguu yake ilionona kuwa nje nje.
Hamza alijikuta akimeza mate mengi na kujiambia inakuwaje mwanamke huyu kuwa mrembo namna
hio , kwanini ngozi yake inaonekana laini hata kabla ya kuigusa.
“Pipii..!!Papaaa!!”
Sauti ya honi ya gari iliokuwa nyuma ilianza kupiga honi mara baada ya gari ya Hamza kutosogea mbele licha ya foleni kuisha.
Regina ndio aliekuwa wa kwanza kushituka na alikunja sura mara baada ya kujua Hamza alikuwa akimwangalia kwa kupitia kioo cha nyuma na kushindwa hata kuona taa ya kijani ilikuwa ishawaka.
“Hamza , unaangalia nini, taa ya kijani ishawaka”Aliongea Regina kwa kukaripia na hali ile ilimfanya Hamza uso kupata moto huku akiwahi kuendesha kusogea mbele , alikuwa amejisahau akimakinika na urembo wa Regina.
“Kwanini unanikodolea mimacho yako?”Aliuliza Regina huku akionekana hana masikhara hata kidogo
“Sikuwa nikikuangalia nilishikwa na ka usingizi ,niliamka mapema”Aliongea Hamza akiwa na sura ya mikausho kabisa kama hakujatokea kitu.
“Muongo sana ,mbahiri , tamaa zimekujaa na umekaa kihuni huni tofauti na muonekano wako , wewe ni mwanaume jitahidi hata kujizuia , huoni hata aibu”
“Mbona unanibebesha tabia ambazo sina , mimi nakubali ni mbahili ndio na napenda hela , nani hapendi hele dunia hii , kama shida nikukuangalia, ndio nilikuwa nikikuangalia , unadhani ni mwanaume gani rijali asiependa kuangalia wanawake warembo”
“Bado tu unautetea ushenzi wako? Haya nimeacha kuongea kuhusu baiskeli yako , vipi kuhusu hizi..”
Aliongea na palepale alirusha mfuko wa nguo mbele ya Hamza , ilikuwa ni mfuko ambao ulikuwa na nguo chakavu za Hamza ambazo alivaa siku ile wakati anaenda kukutana na wazazi wa Regina , sasa alizisahau kwenye gari.
“Kama sio mbahili wewe ni mtu gani ,nguo ikichakaa unabadilisha lakni wewe jana uko bize mpaka kuzipiga pasi , mpaka nguo za kazini nimekuandalia mimi , chuo ulikuwa ukienda na nguo gani , inamana hizo kazi zako hazikutoshi hata kununua nguo za bei rahisi ,halafu unaongea kwa kujiamini mbele yangu”
Ukweli ni kwamba Regina alikuwa na kisirani cha asubuhi, wakati Hamza anashuka asubuhi kwa ajili ya kwenda kazini alikuwa amevaa suruali ya pundamilia ya mtumba na tisheti ya jezi yenye bonge la chata la MoExtra.
Shangazi licha ya kwamba alikuwa mtu mzima na ambae hakujali sana mavazi lakini alichovaa Hamza kwa ajili ya kwendea kazini kilimfanya kucheka.
Kama isingekuwa Regina kuandaa nguo kwa ajili ya Hamza asingekubali kuondoka nae.
Hamza aliishia kumuona Regina kama mwanamke ambae hachuji maneno kwenye kumwambia vitu na kujiona kama mtoto mdogo.
Lakini hata hivyo hakutaka kujibishana nae, kama ilivyokuwa asubuhi alivyofokewa kwa kuvaa jezi na suruali yake pendwa ya pundamilia ndio ambavyo aliona awe mtulivu asiendelee kujibishana nae.
Hamza alijiambia yeye ni mwanaume na haina haja ya kujibishana na mwanamke, kwake nguo sio kupendeza bali ni athari za faida za nguo husika katika ulimwengu wa kiroho.
Mara baada ya kufika katika eneo la maegesho ,
Valet alimpa ishara ya eneo maalumu ambalo CEO ndio gari yake inaegeshwa na Hamza alienda kuisimamisha hapo , ilikuwa ni ndani kabisa ya jengo.
“Kumbuka masharti mawili niliokusisitizia jana”Aliongea Regina kabla ya kutoka nje ya gari.
“Nakumbuka bosi , sipaswi kukuita Regina bali nikuite bosi na vilevile nisitoe siri juu ya mahusiano yetu feki”Aliongea
Mara baada ya Regina kuridhika alishuka kwenye gari na akafuatia Hamza na kisha walizisogea lift maalumu ambazo hutumiwa na wafanyakazi wa ngazi ya juu wa kampuni.
Pembeni ya lift hio kulikuwa na mdada ambae alikuwa amesimama,makadirio ya umri miaka
ishirini na sita hivi.alievalia suti nyeusi.mfupi wa wastani hakuwa mrembo sana lakini alikuwa mtanashati.
“Goodmornining Madam”Alisalimia yule mdada kwa heshima na Regina aliishia kutingisha kichwa kupokea salamu yake.
“Huyu ni Linda , msaidizi wangu namba moja , hakikisha unajifunza kutoka kwake”Aliongea Regina akimtambulisha Hamza.
“Hello , naitwa Hamza Mzee natumaini kujifunza mengi kutoka kwako”Aliongea Hamza akimpatia mkono Linda.
Linda alionekana kusita kwa sekunde kadhaa lakini aliishia kupeana mkono na Hamza ukweli sio mkono bali aligusanisha vidole tu na mkono wa Hamza , hakuonekana kumchukulia siriasi kabisa Hamza.
Hamza aliona ndio maana ni msaidizi wa Regina , wanaonekana kufanana kabisa wote ni makauzu na maringo yamewajaa.
Linda muda uleule alishikilia kishikwambi chake vizuri na kuanza kumsomea Regina ratiba yake ya siku hio.
“Madam , leo ratiba yako ya asubuhi ni saba , tisa , kumi na tanu , kumi na nane , ishirini , ishirini na moja na ishirini na mbili..”
Aliongea Linda na ilimfanya Hamza kushindwa kuelewa anachomaanisha lakini aliishia kufuata
nyuma nyuma mara baada ya Regina kuingia kwenye lift
Sekunde ambayo lift inajifunga , muonekano wa Regina ulizidi kubadilika na sasa kuwa na usiriasi mno kama vile ni mkuu wa nchi , hali ile ilimfanya hata Hamza kumeza mate mengi na kujiambia kwahio huu ndio muonekano wake akiwa kazini, kwanini ni kama vile ni mtu tofauti na yule Regina wa nyumbani.
Regina alibinya namba mfuluulizo akianzia saba , tisa , kumi na tano na kuendelea bila kukosea kulingana na maelezo aliotaja Linda , jambo lile lilimshangaza Hamza kwani Regina alisikia mara moja tu lakini alikuwa akikumbuka vizuri , muda huo ndio sasa Hamza alielewa herufi zile zilikuwa zikimaanisha floor za jengo hilo.
“Boss , floor ya ofisi yako si mwisho kabisa , kwanini unabonyeza floor za chini?”Aliuliza Hamza ,jana yake alishasoma maelezo ya mwanzo juu ya mazingira ya kazi ya Regina hivyo alikuwa akijua ni floor ipi ofisi ya CEO inapatikana.
“Kila Floor CEO anakuwa na kikao , atatatua baadhi ya shida katika idara husika , kwa njia hii ndio namna anavyookoa muda wa wafanyakazi kupanda na kushuka kwenda ofisini kwake hivyo kuongea ufanisi wa kazi”Aliongea Linda.
Comments