Reader Settings

Sehemu ya pili

Ayubu hakuweza kulala usiku ule. Alilala kitandani mwake kwenye chumba kidogo cha kupanga pale Magomeni, akitazama dari lililokuwa na nyufa ndogo ndogo. Kila sekunde, kichwa chake kilikuwa na maswali yasiyo na majibu. "Chanzo ni wewe." Maneno hayo yalizidi kumzunguka akilini kama mzinga wa nyuki usiotulia.

Kwa nini walikuwa wakimfuata? Hawa vijana walikuwa kina nani? Na kwa nini yeye, mtu asiyejua hata majina ya wazazi wake, awe "chanzo" cha kitu chochote?

Alijigeuza kitandani, akijaribu kuupuuza mkanganyiko huo, lakini kila akifunga macho, aliona sura za wale vijana. Macho yao yalikuwa na jambo — kama walimjua zaidi ya alivyojijua mwenyewe. Na hilo ndilo lililomnyima usingizi.

Asubuhi ilipofika, Ayubu alijilazimisha kutoka kitandani. Alivaa fulana yake ya zamani na suruali iliyochakaa, akafunga kamba za viatu kwa haraka, kisha akatoka nje bila hata kuoga.

Dar es Salaam ilikuwa tayari imeamka. Kelele za bajaji, honi za mabasi ya mwendo kasi, na milio ya wito wa biashara zilijaza mitaa. Lakini kwake, jiji hilo lilihisi tofauti. Alihisi macho yakimfuatilia. Alihisi kivuli kisicho cha kawaida kikimlalia mgongoni.

Alienda kwenye kibanda cha chai, pale ambako Juma na Salim walikuwa tayari wamekaa wakicheka na kupiga soga.

"Kijana, mbona unakuja kama umeona jini?" Juma aliuliza huku akimkaribisha kwenye kiti cha plastiki.

Ayubu alijaribu kucheka, lakini ilikuwa wazi kicheko chake kilikuwa cha bandia. "Muda mwingine, bro, unaweza kuamka ukahisi dunia nzima imepinduka," alisema huku akichukua kikombe cha chai kilichomwagwa kwa nusu.

Salim alimtazama kwa macho ya udadisi. "Unamaanisha nini? Kuna nini kinaendelea, Ayubu?"

Alitaka kuwaambia kila kitu. Lakini kuna sauti ndani yake ilimzuia. Sauti ya hofu.

"Hakuna," alijibu haraka. "Labda nimesinzia vibaya tu."

Waliendelea kupiga stori za kawaida, lakini Ayubu hakuweza kuunganisha mawazo yake na mazungumzo yao. Alihisi kana kwamba maisha yake yalikuwa sinema, na yeye ndiye mhusika mkuu asiyeelewa script.

Mwendesha Baiskeli wa Ajabu

Baada ya chai, Ayubu aliamua kwenda Bahari Beach kutuliza akili. Alitembea polepole kwenye mchanga, miguu yake ikiingia kwenye maji ya bahari kwa upole. Upepo wa bahari ulilainisha mwili wake uliokakamaa, lakini akili yake bado haikuwa na amani.

Lakini kilichomtia hofu zaidi ni yule mwendesha baiskeli aliyemfuata kutoka umbali wa mita mia moja. Alikuwa akizunguka eneo lile kwa mizunguko isiyoeleweka, lakini kila mara alipogeuka, alikuta yule mtu bado yupo.

Alipohisi moyo wake unapiga kwa kasi, Ayubu aliamua kutoweka haraka. Alipanda daladala la kwanza kuelekea Tegeta, akijaribu kujinasua. Lakini hata baada ya kushuka, alipogeuka nyuma, bado alimwona yule mwendesha baiskeli akiendelea kumfuata kwa umbali wa kutisha.

Hakujua aende wapi. Hakujua nani wa kumwamini.

Aliamua kukimbilia kwenye jengo la zamani lililokuwa limeachwa. Alijificha nyuma ya ukuta ulioanguka nusu, akijaribu kuzuia pumzi yake isisikike. Alikaa pale kwa zaidi ya saa mbili, mpaka jua lilipoanza kuzama.

Alikuwa peke yake. Mwisho wa mbio. Mwisho wa uvumilivu.

Tafakari ya Giza

Akiwa amekaa chini ya ukuta ule, Ayubu alianza kujiuliza maswali ambayo alikua ameyakimbia kwa miaka mingi.

"Mimi ni nani, kweli?" aliwaza huku macho yake yakitazama anga lililokuwa likibadilika rangi.

Alijua alikua yatima. Alikua amekulia kwenye mitaa ya Kariakoo, akihangaika na maisha tangu akiwa mdogo. Lakini hakuwahi kujua wazazi wake walikuwa kina nani, wala kwa nini walimwacha.

Alikumbuka jinsi alivyojikuta akiwa na umri wa miaka mitano, akihangaika kwenye soko la Tandale. Hakuwa na kumbukumbu ya kabla ya hapo. Hakujua jina lake la ukoo. Hakujua hata kama "Ayubu" lilikuwa jina lake halisi au la mtaa.

"Mbona naishi kama kivuli?" aliwaza huku machozi yakimlengalenga. "Kwanini hawa watu wanasema mimi ni chanzo? Chanzo cha nini? Na kama kweli mimi ni chanzo cha jambo kubwa, mbona mimi mwenyewe sijui chochote?"

Alijaribu kukumbuka chochote kutoka utotoni — sauti za wazazi, sura zao, maneno yao. Lakini kila mara akili yake ilikua tupu kama karatasi nyeupe.

Ghafla, Ayubu alihisi hofu ikimkaba koo. Labda hii ilikuwa zaidi ya yeye kufuatiliwa. Labda yeye mwenyewe alikuwa sehemu ya jambo kubwa ambalo akili yake ilifutwa ili asikumbuke.

Alisimama, akipiga hatua taratibu kutoka kwenye maficho yake. Alijua jambo moja tu — hakuweza tena kurudi kwenye maisha ya kawaida.

Ilimbidi ajue ukweli wake.

Na hata kama ukweli huo ungekuwa mchungu kiasi gani, alikua tayari kuukumbatia.

Previoua Next