Reader Settings

SEHEMU YA 53

Tuliishia  Bibi yake Regina  ametembelea makao makuu ya kampuni na kuzidiwa Ghafla.

Endelea sasa.

Licha ya kwamba Mirium kuonekana  amepoteza fahamu  lakini ilionyesha ni kiasi gani alikuwa katika maumivu  makali , uso ulipoteza nuru  kabisa na  ulikuwa umejikunja  kana kwamba alikuwa akisikia maumivu makali.

Hamza mara baada ya  kumuona mzee huyo alijua moja kwa moja ni vipindi vya mwisho mwisho vya ugonjwa  huo na muda wowote  anaweza kuondoka.

Lakini namna ambavo Regina alikuwa akilia na   alivyowekewana ahadi na  bibi yake kwa ajili ya kutoka nae Out , aliona kama akifa mapema  Regina atakumbwa  na majuto  na huzuni kubwa , hivyo  mara baada ya kuingia  garini aliliendesha kama kichaa na ilimchukua   dakika ishirini kufika hospitalini.

Mara baada ya Manesi kumchukua  upande wa Regina alikuwa  ni kama  mpira ulioisha upepo  wakati akikaa kwenye benchi.

Hamza alijua hata aongee neno la kumfariji  halitokuwa na maana   kwa muda huo  hivyo na yeye alikaa pembeni yake  kimya akimpa kampani.

Muda nao haukusimama,sekunde baada ya sekunde dakika zilisogea  na hatimae  usiku ukaingia.

Regina aliejichokea aliinua uso wake na kuangalia  saa na  hakuweza hata kujua  muda umesogea vipi kwa kasi namna hio , kwani ilikuwa imetimia saa mbili kamili za usiku tayari.

Aligeuza  uso wake na kumwangalia Hamza na alimuona kuwa na utulivu huku mikono akiwa ameikunja kifuani.

Hamza muda huo alikuwa ni kama sanamu kutokana na mkao wake , ilikuwa ni kama anaogopa kupiga kelele.

“Unaweza kutangulia  ili uwahi chakula cha usiku kabla ya muda haujapitiliza”Aliongea Regina  kwa upole huku macho yake yakiwa  na  majimaji kama mtu  anaetaka kutoa machozi.

“Hata wewe hujakula chakula cha usiku bado”

“Sijisikii kula ,  huna haja ya kuendelea kubaki na mimi hapa , ninaweza kubakia mwenyewe tu”

Aliongea na kumfanya Hamza kuvuta pumzi nyingi na kuzishusha  na kisha alishika  bega lake.

“Kama umechoka unaweza kuegamia  hapa , niwe feki  au halisi  bado cheo changu ni mpenzi wako”

“Haina haja , sijachoka hata hivyo”Aliongea huku akigeuka  na kuangalia pembeni na kumfanya Hamza kuishia kutoa tabasamu  kuonyesha kumwelewa  na kisha aliegamia ukuta.

“Japo sina kumbukumbu  za kutosha wakati nikiwa mtoto , lakini napata nusu nusu ya kumbukumbu za maisha yangu nikiwa mdogo , nakumbuka  nikimuona mama yangu akiwa katika hali ya maumivu makali.. natamani kukumbuka kila kitu lakini bado nashindwa  kuona kila kitu  lakini licha ya kumbukumbu kidogo nilizokuwa nazo  nahisi maumivu  makali ambayo hayavumiliki kila dakika na saa ninapojiwa na  kumbukumbu kuhusu mama yangu”Aliongea Hamza na kumfanya Regina kumwangalia Hamza kwa  shauku.

“Huna kumbukumbu zote za utoto wako?”Aliuliza Regina na  Hamza alitingisha kichwa  kukubali.

“Mama yako amekufaje ,  pia hukumbuki?”

“Sikumbuki kabisa ninachokumbuka ni hisia nilizopata  na kumbukumbu chache za mama yangu  kuwa katika maumivu  makali  mpaka kukata roho, sikumbuki zaidi”.

Regina  alijikuta akishindwa kujizuia na kushikilia sketi yake , ijapokuwa alimuona Hamza akiongea katika hali ya utulivu  lakini  alijisikia vibaya katika moyo wake kusikia  maneno hayo. “Ninachomaanisha ni kwamba najua  ni hisia  gani unazopita  muda huu  na nataka  kukupunguzia mzigo”

Regina aliishia kuinamisha kichwa chake tu na hakuongea neno , upande wa Hamza pia hakuongea neno zaidi  na alifunika macho yake  akiwa ameegamia ukutani  akisubiri.

Dakika  kumi mbele  aliweza kuhisi kitu   kikiyagusa mabega yake  na kumfanya afungue macho na kuangalia  na  hakuweza kujizuia kutabasamu mara baada ya kuona ni Regina aliejiegamiza kwake.

Regina  alionekana  kuwa na waswasi kana kwamba   hakutaka Hamza kumwelewa vibaya.

“Usinifikirie vibaya ,  nimechoka kidogo tu”

“Ndio najua”

Baada ya hapo hakuna alieongea na walisubiria kwa namna hio mpaka lisaa lingine likapita  na hatimae  mlango wa  cha ICU  ulifunguliwa  na  bibi yake Regina alitolewa 

“Dokta vipi hali ya bibi?”Aliuliza  Regina mara baada ya kumkimbilia dokta  na manesi waliokuwa wakimtoa bibi yake.

“Tumejitahidi kadri ya uwezo wetu lakini niseme tu hali yake ya inazidi kudhoofu kadri dakika zinavyosogea na muda wowote anaweza kuondoka, mnapaswa kujiandaa”Aliongea Dokta huyo wa kike wa makamo na kisha aliungana na kundi lake na kuendelea na safari 

Regina aliishia kumwangalia bibi yake kwa huzuni  wakati akitolewa ICU kwenda wodi za VIP.

Haikuchukua dakika nyingi na Shangazi  alifika  kutokea nyumbani  na mara baada ya kusikia Mirium hana muda  mrefu  alijikuta akishikwa na huzuni.

“Baba  bado tu hajafika?”Aliuliza Regina.

“Yupo mkoani  kwa wakwe  zake”Aliongea  Shangazi akiwa katika hali ya  huzuni kidogo.

“Oh..!

Regina alijikuta akikosa neno  , ni kama alitegemea kitu kama hicho  hivyo hakutaka kuwaza zaidi na kujipa matumaini hewa.

“Regina nitakaa hapa hospitalini  kwa siku kadhaa na madam , inabidi mteseka kwa siku kadhaa wenyewe  nyumbani”Aliongea.

Regina hakuwa  na pingamizi , isitoshe alikuwa na majukumu makubwa sana ya kuendesha kampuni hivyo muda wa kukaa hospitalini ulikuwa ni mdogo mno.

Wakati huo  Bibi Mirium ambae amewekewa Oksijeni  aliweza kufumbua macho yake  taratibu kivivu  na kwa  ukungu wa macho aliweza kuwaangalia watu  hao watatu waliokuwa mbele yake.

“Regina …!”Aliita.

“Bibii!!”

Regina mara baada ya kusikia  jina lake linaitwa alikimbilia kitandani  kwa haraka  na kwenda kushikilia mikono  ya bibi yake huku  akiwa ameinama.

“Bibi mimi hapa”Aliongea Regina huku akitabasamu.

“Mjukuu wangu  nataka uniahidi  kitu kimmoja…”Aliongea huku  mikono yake ikionekana kumtetemeka  na kauli yake ilimfanya Shangazi na Hamza kukunja sura kiasi maana ilionekana kabisa  ni maneno ya mwisho mwisho.

“Bibi nakusikiliza , niambie tu.”

“Niahidi kwanza  utafanya  ninachokuambia”

“Bibi sijawahi kwenda kinyume na  ahadi , bibi usiwe na wasiwasi  nakuahidi”

“Hapo sawa .. nataka ufunge ndoa na Hamza hata kama ni ya serikali”Aliongea hatimae.

Dakika ambayo Regina aliyasikia maneno  hayo  macho yake yalichanua kwa mshagao  huku uso wake ukiwa katika hali ya kutokuamini , ilikuwa ni kama vile nafsi imeuacha mwili wake.

Upande waShangazi alionekana kuwa katika  tafakari ya kina huku akimwangalia Hamza.

Ijapokuwa Hamza aliikuwa ametegemea hilo lakini  hakuamini bibi huyo  atatumia dakika zake  za mwisho  kumtaka Regina kufanya jambo hilo.

Ukweli ni kwamba  katika hali aliokuwa nao  ilikuwa ni  jambo lisilokuwa la kawaida kuongea  , lakini ilionekana  kutokana na uzoefu na ugumu  mzee huyo aliopitia  ndio maana akaongea hivyo.

Alionekana akijua hakuwa na muda wa kusubiri Regina aamue mwenyewe kuolewa na Hamza ndio maana alitaka  kitendo hiko kifanyike kabla hajakata roho.

Upande wa Hamza na yeye alikuwa akimwangalia  Shangazi na kwa  jinsi  alivyokuwa akimuona  alijiambia tu lazima kuna maneno ambayo  Shangazi ameongea kwenda kwa Bibi Mirium, isitoshe  licha  ya kumuonaShangazi kuwa kama mama wa nyumbani lakini siku ya kwanza tu kumuona alijua sio mtu wa kawaida.

“Bibi unapaswa kupumzika ,  unajichosha zaidi ukiongea”Aliongea Regina akitaka kuingilia  anachotaka kusema bibi yake kwa mara ya pii.

Lakini  Mzee huyo alimshikilia Regina kwa nguvu zake zote huku akijitahidi kumkazia macho, alionekana kuwa siriasi  mno  kile ambacho anataka  Regina kufanya.

“Niahidi hapa hapa kama utakubali ninachokuambia”

Regina alijikuta  akiingiwa na hisia  mchanganyiko , ilikuwa ni hisia za maumivu , majonzi , kuchanganyikiwa, aibu na  uoga.

Baada ya dakika  moja ya ukimya  aliishia kutoa tabasamu la kukubal.

“Nakuahidi nitafanya hivyo lakini swala la ndoa  ni la makubalianyo ya watu wawili , Hamza anaweza asikubali”Aliongea Regina  na kisha alimgeukia Hamza na kumpa ishara  ya kukataa.

Hamza alimwangalia Regina namna alivyokuwa siriasi akimpa ishara za kukataa  na alijikuta akisita kidogo.

“Mimi sina tatizo , nakubali ndoas”Aliongea  

“Wewe..!!”

Regina alijikuta akifoka katika hali ya aibu na hasira kwa wakati mmoja  huku  akijimbia Hamza anawaza nini.

Bibi Mirium mara baada ya kusikia kauli hio kutoka kwa  Hamza  alijikuta akipandisha kifua na kukishusha kwa nguvu na kumwachia  Regina, ilikuwa ni kama kila anavyovuta pumzi  na kupumua  ameongeza mwaka mmoja wa kupumua.

“Vizuri …nyie wote ni watoto wazuri na nataka kuwaona mkiwa pamoja kwa kifungo cha ndoa”

Hamza aliishia kuvuta pumzi huku akimwangalia Regina kwa kumuonea huruma ,  kumbukumbu za kile ambacho Yulia alimwambia kilimjia  na aliona pengine ndio maana bibi yake Regina anafosi  wafunge ndoa.

“Naenda kupunga kidogo upepo hapo nje , kama  unataka tuongee utanikuta”Aliongea Hamza na kisha bila ya kujali  alitoka nje  mpaka eneo la maegesho ya magari na kwenda kuegamia  kwenye mtende na  kukodolea macho mwezi huku akionekana kuwa katika  mawazo.

Alijikuta akiingiza  mkono kwenye mfuko na kutoa simu yake na alienda upande wa  namba  za simu na alijikuta akiiangalia namba ya  Eliza kwa muda na kisha alienda  katika namba ya Dina na kuiangalia  na  alijikuta akirudisha simu mfukoni.

Swali lilikuwa moja tu , vipi kama  kweli atafunga ndoa  na Regina , Eliza atachukuliaje swala hilo? , si ataumia  mno , vipi atakubali kuendelea nae , vipi kuhusu Dina.

Lakini  jibu  lilikuwa ni  ndio, akimuoa Regina  atamuumiza mno mpenzi wake  Eliza , ni kweli hakuwa akimpenda Regina  kiviile   na pengine ni  kutokana  na kutokumjua  kwake kwa muda mrefu , lakini mahesabu yake  ni kama yalikuwa yakimwambia alimuona  Regina  kwanza kabla ya kumuona Eliza , pili Regina alionekana kuhitaji ulinzi  mno kulingana na  maadui zake pamoja na kile alichokifahamu  kuhusu Regina kuwa na ugonjwa wa akili , haya yote ndio yaliomsababishia kusema  ndio , lakini bado moyo wake  ulikuwa mzito mno kila alipokuwa akimfikiria  mpenzi wake Eliza.

Hamza alionekana kuwa na wasiwasi pia kwa wakati  mmoja , hakufika Tanzania kwa ajili ya kufunga ndoa  bali alifika  Tanzania kwa ajili ya kumfahamu Mzee ni nani, wasiwasi wake hakujua katika misheni yake hio ni hatari za aina ngapi ataweza kupitia maana  Mzee  hakuonekana kuwa mtu wa kawaida.

“Kwanini umekubaliana na alichosema bibi?”Aliuliza Regina ambae alionekana kuwa  katika  hasira  na kumfanya Hamza kumwangalia Regina kwa muda bila ya kutoa jibu , ni kama aikuwa akimchunguza lakini upande wa Regina alionekana alikuwa akitaka majibu.

“Kuna sababu gani ipi nyingine , nimeamua kujipandisha cheo  kutoka kuwa Boyfriend mpaka kuwa Mume , naamini  mshahara wangu utaongezeka mara mbili”Aliongea  Hamza.

“Hebu geukia huko  kwanza , sipo hapa kutaniana na wewe”Aliongea Regina huku  akiona aibu  kidogo.

“Hebu ingia kwenye gari  tutafute eneo lolote tule chakula , hata kama njaa huna mimi njaa ninayo , tutaongea huku tunakula, sitanii”Aliongea Hamza akiwa siriasi na kumfahya  Regina kuingia  ndani ya gari kihasira hasira .

Hamza hakujali  ubora wa Mgahawa  kwa muda huo alijali kushibisha tumbo  lake tu hivyo  aliendesha  gari na kwenda kupaki katika Mgahawa mdogo tu lakini ulionekana kuwa na mazingira safi na ilikuwa bahati Regina hakuwa na pingamizi.

Mmiliki wa mgahawa huo pamoja na wafanyakazi wake  mara baada ya kuona gari hio ya Lexus ambayo imekaa kama zile zinazoendeshwa na wanasiasia waliishia kumkazia macho  Regina  na mmoja ya wafanyakazi hao ni kama alimfahamu Regina.

Walishangaa maana mgahawa wao ulikuwa  ni  wa hadhi ya   wateja wa kawaida na sio matajiri, isitoshe hawakuwa na vyakula  vya aina nyingi.

Hamza mara baada ya kukaa aliuliza ni chakula gani kinapatikana na mhudumu alimwambia. “Vipi unaonaje tukiagiza Tambi na  rosti ya mainu , unapenda?”

“Kwanini sipendi , dada  niwekee  hizo tambi na maini tu ila usiweke  mchuzi mchuzi wenye vitunguu  naomba na pilipili, pia utaniletea juisi ya embe ya Cereals”Aliongea  Regina na kumfanya  bosi wa mgahawa huo kutingisha kichwa huku akitoa tabasamu ni kama vile anaifurahia sauti ya Regina kama sio kumuonea  wivu kutokana na uzuri wake.

Hamza alijikuta akinyamaza kimya, kwa jinsi Regina alivyochangamka ni kama alikuwa mzoefu wa migahawa ya  namna hio na ilimfanya kumwangalia kwa tabasamu.

“Unaniangalia nini?”

“Sijakuangalia , ila kuna muda nakuona kama  malaika  uliemuasi Mungu”

“Unaongea upuuzi”Aliongea Regina huku  akiona  uvivu wa kujibishana na Hamza.

Dakika kadhaa  waliletewa chakula na kutokana na njaa kila mtu alijikuta akiwa bize  na chakula ,  muda huo  Regina aliona midomo yake ilikuwa imejaa mafuta  na kabla hata hajatafuta namna ya kujifuta  Hamza alikuwa ashamchomolea tishu na kumpatia.

Regina  aliishia kumwangalia Hamza kwa  macho makavu kwa  sekunde na kisha  aliichukua ile tishu na kujifuta midomo.

“Ongea sasa  kwanini umemkubalia bibi ilihali mimi sitaki”Aliongea  Regina.

“Niongee nini tena ,  wakati  kama huu bibi  akiwa katika  hali nzuri kidogo tunapaswa kwenda kujisajili na kupata cheti cha ndoa , isitoshe babe siwezi kubadili dini  kwa ajili yako  hehe”

“Acha kujipelekesha kimawazo , siwezi kuolewa na wewe”

“Lakini ushamuahidi bibi yako  tayari  na nimekubali mbele yake”

“Lakini wewe si una mpenzi wako?”

“Upo sahihi nina mpenzi  na tupo hatua nzuri  lakini  hili lisikupe shida nitadili nalo mwenyewe”Aliongea Hamza na kumfanya Regina kuvuta pumzi nyingi na kuzishusha na  muonekano wake ulizidi  kuwa wa kikauzu.

“Ngoja nikuambie tu , mimi  sijawahi kuamini  maswala ya ndoa kabisa  na tokea nikiwa mdogo nilijiapiza sitokuja kuolewa”

“Kwanini  unasema hivyo , usiniambie ni kwasabqabu ya baba yako?”Aliuliza  Hamza na Regina aliishia kuwa kimya kuonyesha ndio sababu.

Hamza alihisi    kumwelewa Regina , isitoshe  alikuwa ni mtoto wa nje ya ndoa.

“Sio kwasababu ya baba tu , ila nyie wanaume  hamuaminiki kabisa , angalia kama wewe sasa hivi  una mpenzi tayari na anaonekana kukupenda lakini bado unataka tufunge ndoa , unadhani ni kitu kizuri kwa mpenzi wako?”Aliongea Regina  na kauli ile ilimfanya Hamza kutingisha kichwa kukubaliana nae.

“Nadhani sasa  ushanielewa ninachomaanisha , hivyo achana na  hayo mawazo kabisa , sina mpango wa kuolewa, kwangu mimi  kuzikamilisha  ndoto zangu  naona  kuna maana zaidi kuliko  kuingia  katika ndoa zilizojaa mateso” “Unadanganya?”Aliongea Hamza.

“Kwanini nikudanganye?”

“Namaanisha  hunidanganyi mimi ila unajidanganya mwenyewe”Aliongea  na kumfanya Regina kukosa neno  lakini kushangaa  zaidi kutaka kujua Hamza anachomaanisha.

“Kama kweli huamini  swala la ndoa  basi unao uwezo wa kuolewa  na yoyote yule, sio mimi tu  hata  awe  James , kuna msemo wa kingereza wanasema  ‘The more you care the  more you will

resist’ , kwa lugha nyepesi kama kweli  ungekubali

kuolewa na mtu yoyote ili kumridhisha  bibi yako basi  ni kweli hujali na huamini  swala la ndoa”

“Sio kweli”Regina alikataa na kumfanya Hamza kumwangalia Regina  na macho ya ki uchunguzi kana kwamba anajairbu kuangalia kilichopo ndani ya moyo wake.

“Basi ngoja nikuulize swali?, kwanini siku hizi umeanza  kujilemba , kwanini umekuwa  makini sana na mavazi yako  na kwanini muda mwingine unakua mchangamfu na  muda mwingine unakuwa kauzu mbele yangu?”Aliuliza Hamza na kumfanya  Regina uso wake kuwa mwekundu.

“Unadhani nafanya hayo yote kwa ajili yako?, nafanya kila  ninachotaka”

“Kama ni hivyo kwanini ulikasirika mimi kutokurudi nyumbani usiku  na  ukakasirika zaidi kutokana na kutorudi na  nguo ulizonipa , kwanini  umenisamehe kirahisi vile baada ya kukupiga vibao , kwanini unaonyesha hali ya kunitegemea  katika  baadhi ya vitu?”

“Sija.. umenielewa vibaya Hamza”

Regina alijikuta akishindwa kuwa na neno sahihi la kuongea na alijikuta akikwepesha macho yake na Hamza , mapigo ya moyo yalikuwa yakimwenda mbio mno na  kauli za  Hamza kusema ukweli zimemfanya  kuhisi hali ya kupaniki. “Regina!”Aliita Hamza na kumfanya Regina kumwangalia.

“Sikia kama kweli hujali ndoa basi hupaswi kuweka matarajio yoyote  yae katika ndoa , kwasababu ndoa ni neno tu  na hata  cheti cha ndoa  siku zote ni ushahidi  tu wa kimaandishi , usidhanie  kwasababu watu wanatambulika  kama  mke na mume na wanatambulika  furaha wanayo au wanapendana, chukulia  mfano baba yako na mama yako wa kambo, hivi unadhani wanafuraha  kwasababu ni wanandoa?”

“Mama yako  hakuwa ameolewa lakini alikuwa tayari kukuzaa  ikimaanisha hakujutia kuzaaa na baba yako  licha ya kutokuwa ndani ya  ndoa , unadhani  kama angekuwepo  hai sasa hivi akikuangalia angejiona ni mwanamke  mwenye  laana kukuzaa  nje ya ndoa?”

Maneno ya Hamza yalimfanya Regina machozi kuanza kujitengeneza katika mboni za macho yake.

“Tokea dakika ambayo mtoto anaanza kulia baada ya kuzaliwa  moyo wake hupevuka palepale na hauna tofauti yoyote  na wa mtu mzima , ili mradi una moyo na ni binadamu   basi uwe ndani ya ndoa au nje ya ndoa  haimaanishi  kwamba  huwezi kupenda, ndoa  kama ndoa sio tatizo , tatizo ni watu , au nasema uongo?”

“Kupenda… kupenda… kwahio kwa mawazo yako unadhani  nakupenda,  hebu acha  ukichaa wako”Aliongea Regina kwa hasira.

“Sawa unaweza kuniona kama kichaa  na kunichukulia kama kichaa  lakini  kwa niaba ya kile anachopenda kuona bibi yako  katika nyakati za mwisho  wa uhai  wake  na kwa ajili  ya wafanyakazi wote wa kampuni ya Dosam ,  tunapaswa kujiandikisha ili kupata cheti cha ndoa , kulingana na  mtazamo wako  hujali  kabisa  maswala ya ndoa  na kwa mantiki hio  kujisajili kama wanandoa  haiwezi kukuathiri  isitoshe  utakuwa  umepiga ndege wawii kwa jiwe moja , utamfurahisha bibi yako na utaikoa kampuni isiende kwenye mikono ya  watu wasio na nia nzuri”

“Sitaki maswala ya ndoa fullstop”Aliongea Regina huku akigonga meza kabisa kutilia mkazo na kufanya baadhi ya wateja kumwangalia mrembo huyo  na kujiuliza kuna nini mpaka kuonekana kuwa na hasria.

Regina hakuendelea kubakia ndani ya mgahawa huo , aliichukua mkoba wake na kuondoka haraka haraka

Hamza hakujali  gharama ya chakula  alitoa noti tatu za elfu kumi na kuziweka mezani na kumkimbilia Regina ambae alikuwa akilisogelea gari.

“Regina  nitaendesha mimi?”Aliongea Hamza lakini  Regina  alimsukuma  na kisha alifungua mlango wa  dereva na kuingia.

“Sitaki kukuona tena , ondoka”

Regina alijihisi kuchanganyikiwa  sio kwasababu

Hamza  alikosea  ni kwasababu kila alichoongea  Hamza ulikuwa ukweli ambao alikuwa katika vita nao.

“Bosi umesahau funguo za gari ninazo mimi?” “Nipe funguo”Aliongea Regina mara baada ya kugundua  hakuwa na funguo na anataka kuwa dereva.

Hamza mara baada ya kuona namna alivyokuwa siriasi aliishia kuzunguka upande mwingine na kuingia kwenye gari na kisha alimkabidhi ufunguo.

“Toka kwenye gari”

“Sitoki, kama nilivyosema kesho   naenda kuaga ubachela”

“Wewe endelea tu kunichokoza”

“Nitakuchokoza mpaka uwe mke wangu”Aliongea Hamza.

Ukweli ni kwamba  sio kama alikuwa akitaka sana kumuoa  Regina bali aliona ndio njia pekee ya kumsaidia kwa wakati huo , ki ufupi hakuwa na jinsi na ili kufanya hivyo alitaka angalau kuonekana siriasi,ijapokuwa Regina anakataa lakini yeye ndio  njia ya kutatua tatizo.

Regina aliishia kumwangalia Hamza kwa dakika kadhaa  huku akijiuliza ni mkosi gani amejiingiza mpaka kukutana na Hamza, licha ya kwamba mwanzoni  mpango wake ni kumridhisha bibi yake angalau kuwa na boyfriend feki lakini muda huo alijihisi kukosa amani kabisa, aliishia kuwasha gari na kulitoa ndani ya eneo hilo  kurudi nyumbani.

“Regina mimi sio mtu mbaya  ki hivyo , ukifikiria vizuri  utaona nimekuokoa  ulivyotekwa , hebu

fikiria  stori inavyonoga mtu akisikia  namna shujaa Hamza alivyomuokoa mwanamke  mrembo katika mikono ya watekaji , hili kitalaamu tunasema ni Penzi  la papo kwa papo”

“Tunalikaribia daraja  la Kigamboni , unadhani  nashindwa kulitumbukiza gari baharini na  wote kupotea, wewe endelea kuongea”

“Damn .. acha kuniogopesha namna hio .. siongei tena”

Regina  hakuwa mkataa ndoa bali alikuwa  anaiogopa ndoa , ki ufupi wengi wanaosema  ni wakataa ndoa mara nyingi  wanaona aibu  kusema  wanaogopa ndoa.

“Usinikodolee macho  angalia pembeni”Regina  hakuweza kuhimili macho makali ya Hamza

Muda ambao  Hamza anaangalia pembeni kama alivyoambiwa hisia mbaya zilimvaa muda uleule mara baada ya kuona pikipiki ambayo ilikuwa  nyuma yao kwa muda mrefu.

Ilikuwa ni Ducat 1299 igales  inayovuma kwa uwezo wake  wa mbio na kusafiri kilomita nyingi, thamani yake ilikuwa sawa tu na BMW X3 au zaidi , sasa juu ya pikipiki hio kulikuwa na wanaume wawili  ambao wamevalia  helmeti nyeusi na kufanya sura zao zisionekane.

Kilichomfanya Hamza kuhisi  hali isiokawaida ni kutokana na  msisimko wa nia ovu ya  kimauji iliowavaa watu wale ni hisia ambazo mtu wa kawaida hawezi kuzipata.

“Regina simamisha gari”Aliongea Hamza  mara baada ya kuona   usalama wao ndani ya gari ni mdogo.

“Unataka nini tena?”

“Kuna watu wanatufuatilia , haraka simamisha gari pembeni”Aliongea Hamza.

“Tunafuatiliwa…!”Regina palepale  akili yake iliamka  na kukanyaga breki  lakini mara baada ya kuikanyaga  uso wake ulifubaa.

Hamza palepale aligundua kuna kitu hakipo sawa  na alimgeukia na kumwangalia.

“Nini tatizo?”

“Breki  hazifanyi kazi”Aliongea Regina na kumfanya Hamza kukunja ndita  na palepale alijua  watu ambao wapo  kwenye pikipiki mmoja wao ameshikilia kifaa  kinachofanana na simu kwenye mkono wake.

“Wanatumia kifaa maalumu kudhibiti  mfumo wa  kielektroniki wa gari , naona  wanatumia mbinu hii kutusababishia ajali  ili ionekane ni ajali   ya kawaida kabisa baada ya  uchunguzi”

Previoua Next