Reader Settings

Mwanzo mpya wa safari ya kale.

Mawingu mazito yalining’inia juu ya milima ya Usambara, yakichuruzisha mvua nyepesi kama machozi ya majira ya masika. Baridi la Lushoto lilisambaa polepole, likiingia kupitia nyufa za paa la nyasi kwenye nyumba ya udongo, ambapo ndani yake aliishi mvulana mmoja wa pekee JackXavier.

Alikuwa na miaka minane tu, lakini macho yake makubwa, marefu, na ya kipekee yalionyesha huzuni ya muda mrefu. Kijiji kidogo kilichozungukwa na migomba kilimshuhudia Jack akiwa kimya siku zote, kana kwamba dunia haikumwita kwa jina lake kamwe.

Baada ya ajali ya moto iliyoiteketeza familia yake miaka sita iliyopita, ajali ambayo wengine walihusisha na laana, jinamizi, au kisasi cha ukoo Jack alipelekwa kuishi na Mzee Kijonge, mchimbaji na mgongaji wa mawe aina ya kokoto. Mzee huyu alikuwa mkorofi na mkali sana, na mkewe Mama Amina, alikuwa ni mwanamke mwenye roho ngumu kuliko mawe anayochimba mumewe. Walimlea Jack si kwa upendo, bali kwa huruma iliyojaa dharau na manyanyasho ya kila siku.

Mzee Kijonge alikuwa na watoto watano wa damu, lakini kwao Jack hakuwa lolote. Yeye alikuwa ni Mzigo. Mnyama wa kazi. Aliekosa kauli na nafasi katika familia ya Mzee Kijonge.

Kilichoogopesha zaidi, si kwamba Jack hakuwahi kucheka, kuzungumza, wala kulia bali kwamba hakuwahi hata kujaribu. Tangu akiwa na miaka miwili, alikuwa kimya kabisa. Na hakuna mtu alijaribu kufatilia au aliyempeleka hospitali. Hakuna aliyetaka kujua kwa nini kauli zake zilikuwa zimefunga.
Mama Amina mara kwa mara alimfungia nje usiku mzima kwa makosa madogo yasiyoeleweka, na wakati mwingine alimnyima chakula kwa siku mbili. Lakini Jack hakuwahi kulalamika. Ukimya wake ukawa silaha, silaha ambayo baadhi ya watu waliiheshimu, lakini wengine waliihofia.

Lakini licha ya yote hayo, Jack aliendelea kukua kwa kasi sana. Alikuwa mrefu kupita kawaida ya umri wake, mwili uliojengeka kana kwamba alizaliwa kwa ajili ya kazi ya kupasua miamba. Ngozi yake iling’aa kama shaba iliyong’arihwa motoni. Watu walimuita “Jogoo la mbegu” — wakiamini kama Jack angekuwa mnyama basi wafugaji wangemtumia kwa kuzalisha mifugo majike kwani waliamini mbegu yake ilikuwa bora. Kwa uzuri wa sura aliyokuwa nayo wnakijiji wengi walikuwa wakidhani labda mama yake alikuwa Msomali, na baba kutoka mbali kabisa, labda Mzulu wa Afrika Kusini. Lakini hakuna aliyekuwa na uhakika.

Kwa sababu hakuweza kuongea, hakupelekwa shule. Kila alfajiri, aliungana na Mzee Kijonge kwenye milima ya Lushoto, akipasua mawe kwa ajili ya wakandarasi wa ujenzi. Lakini ndani yake, Jack alikuwa na maswali ambayo hakuweza kuuliza, ndoto ambazo hakuweza kusimulia, na hisia alizozificha kwa macho yake, macho ambayo watu walisema yanaonekana kama yanaona zaidi ya wakati.

Wakati hayo yakitendeka kwa Jack, kijiji hakikunyamaza. Wengi walimhurumia kijana huyo hasa Bi Grace, jirani yao, nesi mstaafu mwenye umri wa miaka 72 aliyesafiri nchi nyingi duniani kupitia shirika la msalaba mwekundu (Red Cross) linaloongozwa na International Committee of the Red Cross (ICRC) ambapo Makao makuu yake yako Geneva, Uswisi (Switzerland).

Bi Grace alikuwa amemwona Jack akiteseka kwa macho yake mwenyewe, na alijaribu mara kwa mara kumkemea Mama Amina bila mafanikio.

Bi Grace alikuwa mcha Mungu wa kweli. Kila Jumapili alisali katika kanisa la Kikatoliki lililopo pale kijijini, ambako pia ndipo Padre mpya kutoka Marekani, Father Ian Smith alikuwa akihudumu.

Father Ian Smith alikuja Tanzania kupitia mpango maalum wa kubadilishana mapadre kati ya Baraza la Maaskofu wa Marekani na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC). Mpango huo, uliofadhiliwa kwa ushirikiano na Vatican na mashirika ya kimisionari, ulikuwa na lengo la kubadilishana uzoefu kati ya makanisa ya Kusini mwa dunia na yale ya Magharibi, huku ukilenga kuinua huduma za kijamii na kijumuiya katika parokia za pembezoni.
Father Ian alikuwa mmoja wa vijana wachache waliochaguliwa kwa makini kutokana na taaluma yake ya falsafa, uchaji wake kwa Mungu, na bidii yake katika kazi za huruma. Alipangiwa kwa muda wa miezi sita kuhudumu katika parokia ya Lushoto, ambako alijitahidi kujifunza Kiswahili na kujenga uhusiano wa karibu na wakazi wa eneo hilo.

Mara tu baada ya kuwasili kijijini, Padre Ian alipata rafiki wa kipekee sana, Bi Grace.
Walikutana mara ya kwanza baada ya ibada, alipomkaribisha kunywa chai nyumbani kwake. Kuanzia siku hiyo, walikuwa wanakutana mara mbili au tatu kwa wiki, wakizungumza mambo ya Biblia, historia ya Kanisa, na maisha ya huduma.
Kitu kilichomvutia zaidi Padre Ian kuhusu Bi Grace ni uwezo wake wa kuzungumza lugha zaidi ya nne, ikiwa ni pamoja na Kiitaliano, lugha rasmi ya Vatican. Kwa kijana kutoka Texas aliyekuwa ameandaliwa kwenda Roma baada ya Tanzania, hili lilimfurahisha mno. Mara nyingi walizungumza kwa Kiitaliano, wakicheka na kushiriki hekima.
Katika mojawapo ya vikao vyao vya chai, Bi Grace alimtazama Ian kwa macho yenye uzito na kusema:

"C'è un ragazzo qui nel villaggio... che soffre, e il suo volto è sempre pieno di tristezza e di un silenzio davvero misterioso. Ma se lo guardi con gli occhi dell’anima, appare molto diverso, ed è proprio questo che ha fatto nascere in me un interesse per lui. Sta soffrendo. Ho cercato di aiutarlo, ma temo che sia al di là delle mie capacità."

Akimaanisha……“Kuna kijana mmoja hapa kijijini… ambaye anateseka na mara zote uso wake umejaa huzuni na ukimya wa ajabu sana, lakini ukimtizama kwa macho ya rohoni anaonekana tofauti sana na hilo ndilo limenifanya mpaka nikawa interested naye. Anateseka. Nimejaribu kumsaidia, lakini naogopa ni nje ya uwezo wangu.”

Padre Ian alimsikiliza kwa makini. Kadiri Bi Grace alivyomsimulia zaidi kuhusu JackXavier yatima, bubu, mwenye mateso yasiyoelezeka, ndivyo moyo wake ulivyozidi kuchoma kwa huzuni na huruma.
Ndipo akasema:

"Se possiamo offrirgli anche solo una piccola opportunità, chiederò aiuto. Il Vaticano ha un programma di borse di studio per orfani con bisogni speciali. Se riusciremo a ottenere le sue informazioni, e se lui sarà disposto, credo di poter contattare il comitato educativo del Vaticano."

“Ikiwa tunaweza kumpa nafasi, hata ndogo, nitaomba msaada. Vatican ina mpango wa scholarship kwa watoto yatima wenye mahitaji maalum. Tukiweza kupata taarifa zake, na kama yupo tayari, naamini naweza kuwasiliana na kamati ya elimu ya Vatican.”

Padri Ian aliguswa sana. Aliahidi kufanya jambo. Alimweleza Bi Grace kuhusu fursa ya scholarship kutoka Vatican kwa watoto yatima kwa undani zaidi. “Nikipata jina lake kamili na baadhi ya taarifa zake,” aliahidi, “naweza kuwasilisha ombi la dharura.”

Siku iliyofuata kwa ushawishi wake katika kijiji, Bi Grace aliwasiliana na mwenyekiti wa serikali za mtaa, na wote walikubaliana kwamba Jack anahitaji msaada. Siku hiyo hiyo, waliwasiliana na Padre Ian kwa maandalizi.

Miezi hiyo michache kabla ya kurudi Marekani, Padri Ian alipata idhini kutoka Baraza la Elimu la Vatican kusaidia ombi hilo. Na hivyo basi, jioni moja, watu hao watatu  Bi Grace, Padre Ian, na Mwenyekiti Mzee Hamza waliongozana pamoja mpaka nyumbani kwa Mzee Kijonge.

Walifika na kukaribishwa na mama Amina mpaka sebuleni, na mzee Kijonge ndio alikuwa ametoka kuswali tarawei akiwa na tasibihi yake mkononi walimkuta ameketi kwenye makochi yao ya mbao akisoma vitabu vyake. Baada ya kukaribishwa na kuketi waliweza kueleza kwa upole kuhusu nafasi aliyopata Jack kusoma nje ya nchi, nafasi ambayo ingeweza kubadilisha kila kitu. Lakini kabla hata hawajamaliza, Mzee Kijonge alilipuka kwa hasira kali, macho yake yakitoa cheche kama moto wa kisasi.

“Hapana kabisa!” alinguruma, akipiga meza kwa ngumi nzito. “Huyo ni mtoto wa Kiislamu! Hatokwenda Kanisani! Hatotoka hapa kwangu. Huyo ni wangu! Mlikuwa wapi miaka yote nikiteseka nae?”

Mama Amina akaingilia kwa dharau isiyo na huruma, macho yake yakiwa kama miiba:
“Huyo Jack haelewi chochote kinachoendelea. Hio nafasi ni bora mara kumi mkampatia Musa, huyo ataenda tu kuwatia hasara”

Ukimya ukatawala ghafla,... Halafu Mwenyekiti, kwa sauti ya busara iliyojaa ukomavu, alisema:
“Mimi nimekuja kwa niaba ya serikali, na ndie niliewakabidhi huyu mtoto mikononi mwenu, na kama nafasi njema zaidi imetokea kwa ajili yake sin abudi kufanya kila linalowezekana kufikisha taarifa hii kwa wahusika. Hivyo naomba msilichulie hili swala kwa haraka na hasira ,nashauri tumuite kijana na tumpe nafasi halafu tutajua kama yuko tayari au vip.”

Baada ya kauli nzito ya Mwenyekiti Hamza lililobakia lilikuwa ni kumuuita Jack kama ambavyo Mzee hamza ameagiza. Mlango wa ukumbi ukafunguliwa kwa taratibu na JackXavier akaonekana kwa mara ya kwanza mbele ya macho ya watu waliokuwa wakibishana juu ya hatima yake.

Na ndipo macho ya Father Ian yakakutana na kijana huyo mdogo.
Na dunia ikasimama kwa muda mfupi.

JackXavier alikuwa kijana wa kuvutia sana kwa namna isiyo ya kawaida kabisa, alikuwa na aura ya ajabu sana. Kwa kumwangalia tu, alikuwa na baby face, ambayo kutokana na ugumu wa maisha aliopitia ilikuwa vigumu kuamini ni yeye amabye anafanya kazi ngumu namna ile. Uso wake ulikuwa umebebwa na (Jawline)taya iliokuwa imara kama imechongwa. Pia alikuwa na kijidimple katikati ya kidevu kilichomfanya kuonekana kuwa matured ili hali alikuwa na umri mdogo sana.

Nyusi zake zilikuwa nene, zimejipanga kwa namna ya asili, zikimpa uso wake uzito na ujasiri. Macho yake yalikuwa makubwa na mazuri, yenye weusi wa kina, kama kioo kilichoficha ndoto nyingi zilizotekwa kimya. Nywele zake nyeusi tii na ndefu kiasi, zikiwa zimeshikwa nyuma bila mpangilio, zilimpa sura ya mtu wa ajabu: kijana wa kijijini, lakini aliye na kitu cha kifalme ndani yake.

Alikuwa amejengeka vizuri, si kwa mazoezi ya kifahari, bali kwa kazi za mikono mashambani, kubeba kuni, kulima, kupasua mawe na kuchota maji kila siku kwa matumiziya familia nzima. Mikono yake ilikuwa migumu, yenye nguvu, miguu imara, na mwili wake ulionyesha alivyokuwa mnyenyekevu mbele ya maisha, lakini si dhaifu.

Alipovuka mlango wa ukumbi huo, kwa mara ya kwanza, Father Ian alimtazama na alishindwa kugeuza macho yake.
Hakuona tu mvulana.
Aliona kuna kitu cha ziada ndani ya huyu kijana.
Aliona uzuri uliotengenezwa na mateso, ukijificha kwenye mwanga wa kijana ambaye hakuwa hata na hakika kama anaruhusiwa kuonekana.

Na bado, alikuwa amesimama.

Mavazi yake yalikuwa ya kawaida sana  tisheti ya zamani, suruali iliyokosa kiuno.
Lakini kulikuwa na kitu kingine. Kitu kisichoelezeka.

Father Ian hakuelewa alichokiona mara ya kwanza. Lakini alihisi.
Kulikuwa na kitu kwenye ukimya wa huyo kijana — kitu cha kina sana.
Sio maarifa. Sio ujasiri.
Ni… uzito.
Uzito wa mtu ambaye hajui anachobeba, lakini tayari anatembea nacho.

Ndipo JackXavier akasimama katikati ya chumba, mbele ya macho ya dunia ndogo iliyokuwa ikimhukumu. Hakukuwa na hofu usoni mwake — lakini pia hakukuwa na ushindi.
Ilikuwa kama vile alikubali kuwa mvua isiyoepukika imemwendea, na sasa alisimama tu mvulana, mkavu, bila mwavuli.

Sauti yake ilipotoka, ilikuwa tulivu. Hapakuwa na miujiza. Hapakuwa na sauti ya mbinguni. Lakini palikuwa na ukweli.
Baada ya Xavier kufika na kusimama katikati ya ile sebule, Mzee Hamza alianza kuongea kumuelewesha nini kinaendelea na mwishoni akamuuliza kama angependa fursa ya kwenda kusoma nje kwa scholarship ya kanisa.

“Ndiyo. Nimekubali.”

Ukimya ulichoma. Kama barafu moyoni.

Ukimya ulitanda kama wingu la radi. Bi Grace alishika kinywaji chake mikononi kwa mshangao.
Mama Amina alipigwa bumbuazi na kushusha macho chini, akiwa hana cha kusema.
Mzee Kijonge alitetemeka kwa hasira, lakini hakuwa na maneno.

Jack alikuwa amesema neno lake la kwanza, na si neno la kawaida — bali ni chaguo la hatima.
Wengine walishangaa. Wengine walihisi huzuni.
Lakini kwa Father Ian…
Mara hiyo hiyo, alijua:
“Huyu si mtoto wa kawaida.”
Alijua — si kwa akili, bali kwa moyo — kwamba maisha yake mwenyewe yangekuwa tofauti kuanzia leo.

Na bila hata kuelewa kwa nini, alimwomba Mungu kimyakimya:
“Nioneshe njia. Kwa sababu sasa, nimekutana naye.”

Mzee Kijonge alikosa maneno. Pasipo kupoteza muda, Padre Ian alimwambia Jack aandae mizigo. Usiku huo huo, waliondoka kuelekea kanisani, tayari kwa maandalizi ya safari ya wiki inayofuata — safari ya kuelekea Texas.

Next