SEHEMU YA 55.
USIKU WA JANA.
Hamza mara baada ya kutoka nje ya geti alisogelea moja ya gari ya Mercedenz iliokuwa imesimama mita kadhaa kutoka katika geti la nyumba yao na kisha aligonga kioo cha mbele na muda uleule kioo kile kilishushwa na ndani ya gari hio alionekana mwanaume alievalia suti, mweusi mwenye makadirio kama ya miaka therathini hivi.
“Bosi pole kwa kusubiri muda mrefu?”Aliongea Hamza kinafiki na kumfanya yule bwana kutoa tabasamu na kisha aliangalia chini.
“Umejuaje nakusubiri Bro”
“Huna haja ya kujifanya mjinga, ilihali umefanya kila hila ya kupata ‘Attention’ yangu nijue unanifuatilia”Aliongea Hamza na kumfanya yule bwana kutoa tabasamu.
“Ni kama nilivyodhania umeniona , unaonaje ukiingia ndani ya gari Bro”Aliongea na kumfanya Hamza kuzunguka upande wa pili na kuingia katika ile gari.
Kilichomfanya Hamza kujua gari hio ilikuwa ikimfuatlia ni mara baada ya kuiona zadi ya mara tatu katika safari nzima ya kutoka hospitalini mpaka kufika Kigamboni.
Wakati alipokuwa akiongea na Regina nje ya hospitalini karibu na maegesho ya magari aliweza kuiona na wakati wanasubiria Taksi kuwachukua kwenda nyumbani iliwapita , Hamza mwanzoni hakuitilia sana maanani kutokana na dereva kutoonekana kuwa na nia yote mbaya lakini mara baada ya kuona ikiwa imesimama mita kadhaa kutoka kwenye geti la nyumba yao aliona kabisa dereva wa gari hio alikuwa akifanya makusudi ili kumjulisha kwamba anamtafuta.
“Bro wewe sio wa kawaida , umeweza kuwashinda wale Maninja wa kundi la Nyoka na kisha kumuokoa Bosi Regina katika mlipuko wa gari , uwezo ulioonyesha sio wa mwanajeshi wa kawaida aliepitia mafunzo ya kikomandoo, naweza kusema wewe ni zaidi ya mwanajeshi. unaweza kuniambia mafunzo yako ni ya namna gani na uwezo wako kwa ujumla?”Aliongea yule bwana huku akiwa na hali ya urafiki katika macho yake.
“Na wewe unaweza kuniambia ni nani haswa na kwanini umefanya kila hila nikutambue?”
“Oh , Samahani bro kwa kutokujitambulisha, Naitwa Norbert Geza kutoka kitengo cha usalama wa nchi”Alongea na kumfanya Hamza kutingisha kichwa.
“Sawa bwana Geza , je kuna sababu yoyote ya jeshi kunifuatilia?”
“Ni maswala ya Usalama wa nchi ndugu Hamza ,
tukio kama la leo tuna kila sababu ya kukufuatilia”Aliongea na kumfanya Hamza amwangalie.
“Mnapanga kufanya nini kuhusu tukio la leo , maana kama mlivyoona kuna watu wanataka kuniua mimi na bosi wangu, mpango wenu ni nini au mnapoteza muda kunifuatilia ila hakuna chochote mnachofanya”
“Tunapanga kulichukulia hatua swala hili lakini hatua ya kwanza ni hii ya kuongea na wewe , nipo hapa kwa ajili ya kukutuliza na kukutaarifu kwamba wote waliohusika hapa tutawaonya wasirudie tena kuyumbisha usalama wa nchi na raia wake”
“Haha.. mbona kama kauli yako ni ya kimaigizo na onyo kwa wakati mmoja, mimi ndio nimeshambuliwa lakini ninachoona hapa unanipa onyo nisichukue hatua kwa wale waliohusika, kama watu wameweza kukodi kundi hatari kama
hili kwa ajili ya kuhakikisha tunapoteza uhai, unadhani unachoongea hapa kinaweza kutekelezeka?”
“Kama nilivyojitambulisha Mr Hamza , kupitia vitengo vyetu ya kiusaama vya nchi tutafanya kila linalowezekana , Tanzania ni nchi inayoendeshwa kwa misingi ya haki na sheria , hatuwezi kumruhusu mtu kufanya anachotaka , hivyo naomba usiingilie kazi ya jeshi na kusababisha matatizo zaidi , Idara ya usalama wa nchi haiwezi kufumbia macho maswala kama haya”
“Unaongea ujinga na upuuzi , nilikuona kule hospitalini na nikakuona tena baada ya mlipuko , hii inamaanisha mlijua tukio kama hili litatokea , nyie kama kweli ni sehemu ya usalama wa nchi , kwanini hamkuzuia tukio kama hili, hii moja kwa moja inaniaminisha kwamba watu waliohusika wapo ndani ya idara zenu na walikuwa wakiangalia nini kinachokwenda kutokea , sasa kwasababu umejileta mwenyewe unaonaje ukinitajia kabisa wahusika”
“Hamza unamaanisha nini , kwahio unataka kwenda kinyume na msimamo wa idara ya usalama wa nchi?”Aliuliza yule bwana na kumfanya Hamza macho yake kuchanua na kumwangalia kwa umakini.
“Kama huna taarifa yenye maana kwangu basi naweza kusema muda umeenda na nataka kwenda kulala”Aliongea Hamza na kisha alifungua mlango na kutoka nje.
Norbert aliishia kumwangalia tu , isitoshe alikuwa akimhofia kwa kile alichokuwa amekiona leo hivyo hakuona haja ya kubembeleza.
Mara baada ya kumuona Hamza akirudi ndani aliendesha gari mpaka mita kadhaa kwenye moja ya nyumba iliokuwa geti la njano katika mtaa huo huo na mlango ulifunguliwa na wanaume wanne waliovalia mavazi ya kiraia na kisha kuingia ndani ya gari ile.
“Kapteni vipi kuhusu Hamza amekuelewa ?”
“Sina uhakika , huyu dogo inakuwa ngumu mno kujua ni kitu gani anapanga kufanya , tunapaswa kuwa makini tusiruhusu akasababisha matatizo hasa kipindi hiki cha uchaguzi”
“Haya yote ni kutokana na tamaa za mheshimiwa mstaafu na familia ya Mzee Benjamini na kuendelea kumchokoza Bosi Regina kila siku , anadhani kwasababu ya kuwa mstaafu anaweza kufanya chochote na kujimilikisha hii nchi”Aliongea mmoja ya wale watu kwa chuki kubw.
“Ni kwasababu hakuna anaeweza kumfanya chochote Mstaafu , nchi ilimwacha afanye chochote na sasa mizizi yake ipo kila kona ya nchi kwanzia kwenye uchumi mpaka kwenye siasa, Familia ya Benjamini ni sehemu ndogo sana katika Ngome yake”
“Ndio maana wanadharauliwa na huyu Hamza kwa kutumika kizembe”
“Hii ni misheni yetu ya kuhakikisha nchi inakuwa salama , sisi ni wanajeshi na lazima kila tunachofanya kinazingatia sheria na katiba ya nchi , vinginevyo hatuwezi kuwa tofauti na wahalifu”Aliongea mwingine.
“Haina haja ya kulalamika, kwasasa tokea tuanze kufatilia matukio yote yanayoendelea hatuwezi kusema usalama wa nchi upo hatarini , tunapaswa kuendelea kuwa makini na kila hatua wanazochukua , lazima tutimize kila wajibu ambao tumepewa na wakuu wetu”Aliongea Kapteni. “Ndio tumekuelewa Kapteni?”
“Ayubu vipi bado hujampata Amosi?”
“Afande Rama anaendelea na uchunguzi bado ,
Jasusi mara ya mwisho alionekana katika Mgahawa Masaki na baada ya hapo hajaonekana tena na hakuna alama alioacha nyuma inayoweza kutufanya kupiga hatua ya kujua alipo”
“Vipi ndani ya Kanisa la Wabrazili , hakuna ‘Movement’ zozote za kutilia mashaka?”
“Kuna mtu wentu ndani ya kanisa na mpaka sasa hajawasilisha taarifa yoyote , nadhani bado hakuna cha kutilia mashaka”Aliongea Ayubu na kumfanya Kapteni Norbert kufikiria kidogo.
“Kuna kitu lazima kinaendelea, nimesikia na Afande Danieli anamtafuta Amosi, Mzize wewe kwanzia kesho endelea kumfatilia Kanali Dastani kila hatua anayopiga na kisha unipe Ripoti. Fadhili wewe utaendelea kumfuatilia Hamza pamoja na washikaji zako” “Sawa Kapteni”
“Hebu waulize kwanza tujue kama Hamza bado yupo nyumbani”Aliongea na kumfanya bwana alieitwa Fadhili kutoa simu palepale na aliongea kwa dakika kadhaa na kukata.
“Bado yupo nyumbani Kapteni , hakuna Kamera inayoonyesha akitoka”
“Vizuri, kama kuna lolote litakalotokea mtanijuza naenda nyumbani”Aliongea na mabwana wale walikubali na kisha walishuka katika ile gari na kuingia ndani ya nyumba ile yenye geti na Kapteni Norbert alitoweka katika eeo hilo.
Sasa upande mwingine wakati wakijua Hamza yupo nyumbani ukweli ni kwamba alikuwa ashaondoka muda mrefu kwa kuzikwepa Kamera na hata simu yake aliacha hapo hapo nyumbani maana alijua lazima Ma ajenti hao wanafuatilia hadi simu yake.
Muda ulikuwa umeenda na kuna maeneo ndani ya mtaa huo wa Egret yalifunikwa na vivuli vya miti na ndio aliotumia kupotelea mpaka kwenda kutokea katika mtaa mwingine kabisa.
Hamza mara baada ya kuona amefika mbali kabisa na nyumbani alitoa simu ndoto ya batani na kisha alitafuta namba ya Lawrence msaidizi wa Dina.
“Bro muda umeenda sana , kuna kitu unataka nikusaidie?”
“Kundi la kininja la Black Eared Snake lipo Tanzania , nataka kujua eneo walipo?”
“Bro ! , Umejuaje wapo Tanzania na kwanini unataka kujua walipo?”Aliuliza Lau upande wa pili.
Hamza alikuwa akijua moja ya kanuni kubwa ya kundi hilo la kininja ni kusafiri kimakundi , kwa mfano ikitokea kazi ya kuua mtu katika eneo husika lazima na kiongozi wao asafiri kwenda kuweka makazi ya muda katika eneo hilo, Hamza alijua akimkamata kiongozi ndio atakavyyoweza kumpata mtu ambae anataka kumuua kwa kumsababishia ajali za mara kwa mara.
“Wewe niambie wapo wapi , kwa Network yenu lazima mtakuwa na taarifa zote”
“Lakini Madam ashalala tayari , unaonaje nikimuamsha na kumwambia kwanza?”
“Ukiendelea kuongea ujinga sitokutambua kama Bro tena , sasa chagua kuniambia au kwenda kumuamsha bosi wako”Aliongea Hamza kwa sauti ya kibabe.
Lawrence upande wa pili hakuweza kumkatalia kwani alimhofia Hamza licha ya kwamba alikuwa ni kama rafiki yake hivyo aliamua kumtajia eneo walipo.
Hamza mara baaada ya kuambiwa eneo husika aliona ni umbali mrefu mno hivyo aliona hawezi kutembea zaidi ya kupanda Taksi ya kumfikisha huko. ******
Upande mwingine ndani ya jumba la kifahari linalopatikana katika eneo la Tegeta walionekana baadhi ya watu wakiwa wameketi eneo la ukumbi.
Walikuwa ni mabosi wenye pesa nyingi na walionekana kuwa na mabodigadi waliombatana nao na kulikuwa na kikao kilichokuwa kikiendelea.
Alionekana Kanali Mstaafu Fanueli Yowe akiwa amekaa kwa kuegamia kwenye Sofa akimwangalia kwa macho ya ukauzu bwana aliekuwa amekaa mbele yake , ambae amevalia Jaketi la leather , bwana huyo alikuwa mweusi tii na amejaa makovu usoni.
“Mr Snake, umoja wetu umekuwa ukishirikiana na kundi lako la Black Eared Snake kwa miaka saba sasa , katika kipindi hicho chote tumeweza kusimamia madili mbalimbali ya siraha ambazo ziliingia nchini kwako na umeweza kujiimarisha kwa kiasi kikubwa na kuweza kufanya kundi lako kutambulika duniani kutokana na uwezo wa juu , lakini leo ndio mara ya kwanza umetuangusha na kutukatisha tamaa kabisa”Aliongea Fanueli Yowe , huyu ndio bwana ambae ni kiongozi wa kundi la watu wenye ujuzi wa sanaa ya mapigano.
Mr Snake ndio aliekuwa kiongozi wa kundi la kininja la Black Eared Snake , kutokana na kundi lake kupewa misheni ndani ya Tanzania iliokuwa na malipo mazuri ndio maana alisafiri na maninja wake kukamilisha kazi ya kumuua Hamza na Regina.
Genge la mabosi wala keki ya taifa ambao wameamua kujipa jina la kuzugia la Martial Art Association walikuwa ni washirika wakubwa na kundi hilo la kininja kwa muda mrefu ndio maana hata kazi ya kumuua Regina walipewa wao.
Unaweza kushangaa kwanini kundi hili litake kumuua Hamza na Regina, ukiachana na kwamba Master Konki ambae alikuwa mwanachama kupewa kibano na Hamza kiasi cha kuwa na chuki lakini upande mwingine kundi hili lilikuwa na sababu za kutaka kuona Regina pia anakufa.
Mwanzilishi wa kundi hili alikuwa ni Mheshimiwa Mgwenno ambae ndoto yake kubwa baada ya kuwa kiongozi mkuu wa taifa ni kutaka kuimiliki Tanzania.
Mheshimiwa Mgweno katika mbinu za kutaka kuimiliki Tanzania ndio alianzisha makundi mengi ambayo hakujihusisha moja kwa moja lakini alikuwa na nguvu ya kimaamuzi na moja wapo ni kundi hili la Umoja wa watu wanaojua Mapigano, moja ya sababu kubwa aliofanya kuunda kundi hili ni kuhakikisha katika kuendeleza kuwa na maslahi yake anakuwa upande mzuri na jeshi , isitoshe pia alikuwa mwanajeshi Komandoo kabisa kabla ya kuingia katika siasa hivyo ilikuwa rahisi kwake kushawishi wanajeshi kutengeneza kundi hilo.
Sasa kutokana na wanajeshi hao kupata pesa nyingi na pesa kuwanogea walitoka katika miiko ya kazi na kuwa wahalifu wanaojilinda katika vazi la kujiita makomandoo na jambo hilo lilimfurahisha sana Mheshimiwa Mgweno na katika kukamilisha mambo yake aliwatumia sana.
Sasa mara baada ya swala la Hamza na Regina kuletwa mezani na kiongozi wa kundi hilo Fanueli Yowe akimwakilisha mheshimiwa Mgweno moja kwa moja waliona kazi ya kumuua Hamza wawapatie washirika wao wa muda mrefu yaani Assassin wa Black Eared Snake kumaliza kazi hio, hayo yote ni kutokana na kuona uwezekano ni mdogo wa kupambana na Hamza ana kwa ana.
“Kundi letu la Nyoka Mwenye masikio meusi linahistoria ya miaka ishirini tokea kuanzishwa kwake na hatua kwa hatua tuliweza kutambulika kimataifa na ni juzi tu hapa miaka kumi iliopita tuliweza kutambuliwa na Surety International Association na kupewa cheo cha daraja C katika ulimwengu wa maninnja, uzoefu wa kazi za kuua tunazo ni kwamba tu mtu ambae mmetupa kazi ya kumuua awamu hii anaonekana kuwa na mafunzo ya juu na pengine ashawahi kuwa mwanajeshi, Afande Yowe huna haja ya kuwa na wasiwasi , kwasababu mmeshatulipa pesa nyingi juu ya hii kazi nina wahakikishia tutaimaliza haraka iwezekanavyo”
“Unaongea ujinga , tulikuambia kabisa hili ni swala ambalo linatakiwa kufanyika mara moja , lakini angalia mmefeli na kufanya mkuu wa majeshi anatupa tahadhari , kazi imekushinda tunataka urudishe malipo tuliokupatia”Aliongea bwana mmoja mwenye kitambi aliekuwa amekaa pembeni.
“Turudishe hela! Chochote ambacho sisi Noka wa Masikio meusi tunameza hatuwezi kutapika”
“Kazi imewashinda na mnataka kula pesa yetu , hamna aibu?”Aliongea yule bwana kwa hasira huku akigonga meza , alifahamika kwa jina la Afande Sucre.
Maneno ya Sucre yalionyesha kumkasilisha mmno Mr Snake huku akionyesha nia ya kutokubaliana nae kabisa.
“Mzee Sucre kaa chini ili tuweze kusikia mpango B wa Mr Snake”
Muda uleule Mr Snake alichomoa kisu chenye kifimbo chekundu , kilikuwa kidogo mno urefu wa kidole cha mkono na kilionekana chepesi na alitumia kisu kile kujikata kucha huku akiongea.
“Wote hapa ni wanajeshi lakini sijui kama mshawahi kusikia neno maarufu katika vita lifahamikalo kama Original Strike?” “Unaongea upuuzi gani ?”Aliongea Sucre kwa hasira.
“Katika ulimwengu wa kimasenari ikitokea umeshambuliwa kitu cha kwanza unachopaswa kufanya ni kutafuta chanzo cha shambulizi kwani ndio njia nzuri zaidi ya kutatua tatizo , kama hisia zangu ni sahihi huyu kijana wenu mnaemwita Hamza lazima atatafuta namna ya kututafuta ili kulipiza”
“Unamaanisha nini , kwahio unasema anaweza kuja ndani ya hili eneo?”
“Sidhanin kama ni mjinga kuja eneo hili , maana itakuwa ni kujitafutia kifo”Aliongea bwana mmoja mwwenye mwili mkakamavu.
“Mnakosea, kwa taarifa mlizonipatia makisio yangu ni sahihi , anajiona ni mpiganaji mzuri na lazima ataamini anao uwezo wa kutudhibiti , hivyo atatudharau , isitoshe wengi wenu hapa mnaonekana wazembe wazembe”Aliongea na kumfanya Afande Yowe macho yake kusinyaa, ni kweli kabisa katika mapigano licha ya kwamba wanajiita wanajeshi lakini ni wanajeshi wa kutumia siraha na sio kupigana.
“Mr Snake kama kweli Hamza akija hapa , unadhani vijana uliokuja nao watatosha kudili nae?”Aliuliza na kumfanya Mr Snake kwa kujivunia kabisa kugeuza macho yake na kuangalia wanaume waliosimama nyuma yake , walikuwa ni wanaume wenye miili iliojengeka kimazoezi huku wakiwa wamenyoa vipara, hawakuwa na ishara ya uzembe hata kidogo. “Kama akijileta ndio mtajua nini kitakachotokea?”
“F**ck you Hamza , jiafanye mjinga na ujilete hapa nitampasua na risasi moja tu”Aliongea Sucre na kitambi chake huku akikoki kwa mbwembwe bastora yake.
“Mkuu mimi sidhani kama atakuja hapa na muda umeenda , nadhani kikao kishaisha, nina miadi hivyo nitatangulia kuondoka”Aliongea Afande Sucre na kusimama akifuatiwa na mabodigadi wake.
Lakini sasa muda ambao anafikia mlango ili kuufungua ulifunguliwa kwa kishindo na mara baada ya kuangalia vizuri ni mabodigadi waliokuwa wakilinda kwa nje, walikuwa wamepoteza fahamu wakiwa wamerushiwa mlangoni.
Muda huo watu wote walikodolea macho mlango na waliweza kumuona kijana mdogo akiwa amesimama kwenye mlango huku akitafuna bublish na nyuma yake walionekana mabodigadi waliokuwa wakilinda wakiwa chini wengine wakionekana hawana fahamu na wengine walikuwa wakiugulia maumivu.
Afande Sucre alijikuta akimeza mate mengi huku akimwangalia Hamza kwa wasiwasi.
“Wewe ni nani?”Aliongea huku mkono ukiwa umeshafika kwenye kiuno sehemu iliopo siraha yake.
“Naitwa Hamza Mzee, mtu ambae unataka kumpiga risasi na hio bastora yako”Aliongea
Hamza akiwa na muonekano uliojaa uzembe.
Afande Yowe macho yake yalimtoka , hakuamini Hamza angefika hapo kama alivyosema Mr Snake.
Afande Sucre alijikuta akirudi nyuma kwa namna ya kujihami na kuungana na wezake.
Upande wa wanajeshi wote wa kundi hilo wanaojiita wanaojua mapigano walijikuta wakisimama kwa wasiwasi na mshangao.
“Wewe ni jasiri mno , hakika unasttahili kuitwa mwanajeshi kwa kujileta hapa”Aliongea Mr Snake akiwa na tabasamu usoni akijiambia anakwenda kuimaliza kazi muda huo huo ndani ya eneo hilo.
Ukweli ni kwamba licha ya kundi hilo kusikia habari za Hamza wengi wao hawakuwahi kuonana nae ana kwa ana zaidi ya Master Konki ambae hakuwepo kwenye kikao hicho..
“Mr Snake ulichoongea kimeonekana kuwa kweli , nipo tayari kuona kile ambacho
umeandaa”Aliongea Afande Yowe na wenzake wote walitingisha kichwa.
“Subirini kwanza?”Aliongea Hamza akinyoosha mkono.
“Unataka kuongea nini , usije ukasema unaona woga wakati umejiingiza kwenye pango la Simba”
“Sijaja hapa kupigana wala kuibua mzozo na mtu , kwa ninavyoona hapa wengi wenu mnaonekana kuwa na vyeo serikalini hivyo sitaki kujiletea matatizo”Aliongea Hamza na kuwafanya wale watu kumwangalia kwa mshangao.
“Kama hujaja hapa kupigana umekuja kufanya nini?”Aliuliza Mzee Yowe.
“Nimekuja kuwapa onyo, leo baada ya kushambuliwa na maninja wa kundi la nyoka nilijua fika kuna mkono wa mtu wenye nguvu umehusika , hivyo sitaki ugmvi na mtu yoyote na muache kushambulia watu wa karibu yangu”
“Onyo!! , Wewe ni nani wa kutupa onyo , unajua vyeo vyetu katika jeshi , kwanini mtoto mdogo kama wewe tukubali onyo lako, ukiburi umekujaa”
“Kwamaneno yako naona kabisa haupo tayari kuikumbatia hii fursa ninayokupatia , hebu jifikirie
mara mbilimbili kabla ya kuendelea kunichokoza”Aliongea .
“Wewe mtoto ni kichaa na bora umejilera mwenyewe, kama hukufunzwa adabu tutakufunza leo”Aliongea Sucre.
“Upo siriasi?”
“Unadhani natania , unadhani naweza kuogopa panya mdogo kama wewe”Aliongea.
“Mr Hamza asante kwa kufika hapa kwa ajili yangu ili niwaonyeshe ni kwa namna gani naenda kudili na mtu kama wewe”
“Na mimi nimekuja kuona unadili vipi na mimi?”Aliongea Hamza na muda uleule Mr Snake alipiga mluzi na kufumba na kufumbua kundi la watu waliovalia mavazi meusi walijitokeza na kuingia katika ukumbi huo huku wakiwa wameshikilia siraha.
Kitendo cha watu wale kutokeza kiliwafanya watu wote kushangaa akiwemo Mzee Fanueli.
“Mr Snake kumbe ulikuwa na kundi la watu wengi namna hii?”
“Nisamehee afande kwa kukutokutaarifu mapema , nilikuwa nimejiandaa kudili na huyu mtu ndio maana nimechukua kila tahadhari”
“Sidhani kuna haja ya kupoteza nguvu za vijana wetu , risasi zinamtosha”Aliongea Afande Sucre na alitoa bastora yake akifuatiwa a mabodigadi na bila ya kujiuliza mara mbilimbili walimfyatulia Hamza mfululizo mpaka bunduki zikaishwa risasi lakini kitu cha ajabu ni kwamba risasi zile ni kama zilikuwa zikipiga hewa , Hamza walikuwa wakimuona mbele yao lakini ilikuwa ni kama holograph ya Hamza , ile wanamaliza Hamza alikuwa palepale mbele yao akiwa na tabasamu.
Swala lile liliwashangaza mno wale mabwana na hofu na wasiwasi iliwavaa, walimuona Hamza kama mzimu.
“Wewe ni binadamu au Mzimu!!!”
Mr Snake alijikuta akibung’aa huku akimwangalia Hamza kwa hofu na kuna kila hali iliokuwa ikimwambia Hamza aliwafanyia kiini macho ili waamini alikuwa mbele yao lakini muda mrefu alikuwa ashapotea na amerudi baada ya kuacha kushambuliwa.
Aliona kama hisia zake ni sahihi basi njia moja tu ya kudili nae ni kushambulia ana kwa ana na sio kwa kutumia siraha kama bunduki.
“Sijaja hapa kujibu maswali , nimewapa nafasi mmeikataa”Aliongea Hamza huku akipiga hatua lakini Mr Snake alifyatuka na kumsogelea Hamza kwa spidi akiwa na kisu amekitanguliza mbele kininja kwa kumlenga eneo la shingoni.
Kitendo cha Mr Snake kumfikia Hamza usawa wa shingo mkono wake ulioshikilia kisu ulidakwa kwa spidi ya juu kiasi cha kushindwa kukwepa na kuzungushwa kwa nguvu na maumivu aliohisi alijikuta akikiachia kile kisu mwenyewe.
Hamza hakuchelewesha wakati kisu kule kinadondoka katika mikono ya Mr Snake alikidaka na mkono wa kushoto na bila ya huruma alimkita nacho Mr Snake katika paji la uso na kuzama ndani kabisa.
“Master!!!”
Maninja wawili waliokuwa karibu na bosi wao mara baada ya kuona amekitwa na kisu cha paji la uso walijikuta wakipiga yowe na kwa hasira kubwa waliinua mapanga yao na kumsogelea Hamza kwa spidi kana kwamba wanataka kumtenganisha shingo na kiwiliwili.
Wa kwanza mara baada ya kumsogelea Hamza kwa spidi kwa mtindo wa kutaka kumfyeka shingoni ,Hamza alimkwepa kuinama chini na upanga ulipita hewani na kisha palepale kwa ustadi wa hali ya juu aliachia ngumi nzito iliompiga bwana yule eneo la moyo na kilichoweza kusikika ni mbavu zake kuvunjika na alidondokea mbali huku akikodoa macho na kutema damu kisha akadondoka chini isieleweke kama amekufa au amezimia ,hakuzubaa baada ya shambulizi lile mwingine alikuwa ashamfikia akinuia kutaka kumchoma na upanga eneo la tumboni lakini Hamza alikuwa mwepesi kwani alikwepa kisu kile na kupita kwenye mbavu kiasi cha kuchana nguo aliovaa na palepale alimpiga bwana yule teke la kigoti na kumfanya kupinda na ilikuwa ni nafasi ambayo Hamza aliitaka kwani alimtandika ngumi nzito ya paji la uso iliomdondosha Ninja yule chini na kuzima palepale.
Haikuwa kwa Sucre na wenzake ama kwa kiongozi wao Afande Yowe , wote walijikuta wakipatwa na mshituko usio na kifani huku hali ya woga ikiwavaa , Afande Yowe Bastora yake ilikuwa na risasi lakini alishindwa kuchukua maamuzi ya kuitumia kutokana na kile alichoona baada a Hamza kutoathirika na risasi.
Wale maninja wengine mara baada ya kuona wenzao walivyojeruhiwa walisita kufanya mashambulizi na kumwangalia tu kwa wasiwasi , isitoshe mkuu wao alikuwa ndio mtaalamu wa hali ya juu na mabwana wawili waliozimishwa kwa ngumi moja moja tu ndio walikuwa wakifuatilia kwa uwezo sasa wanawezaje kumshambulia mtu ambae amemuua mkuu wao kwa shambulizi moja.
“Kajikundi kadogo ka daraja C wanaona wanaweza kushindana na mtu kama mimi”Aliongea Hamza mara baada ya kuona kazi yake ni njema na alipiga hatua kumsogelea Fanueli.
“Unajua kwanini tumefikia hatua hii?”Aliuliza Hamza na kumfanya Afande Fanueli kutingisha kichwa kusema hajui.
“Mmekodi watu kwa zaidi ya mara tatu sasa kwa ajili ya kuja kunishambulia na hata kutuma hawa wapuuzi mkiamini wanaweza kunishinda, lakini yote hayo yaliotokea mmeshindwa kujiuliza swali moja jepesi tu, na swali lenyewe mlipaswa kujiuliza mimi ni nani kwanza kabla ya kuchukua hatua , tokea mwanzo nilijua tu mnajitafutia matatizo kwa kunichokoza , nilitaka kuwavumila lakini inaonekana nguvu yenu hapa nchini imewapa kiburi na hamuwezi kunusa hatari”
“Mr Hamza tafadhali tunaomba usitufanyie chochote , tupo tayari kufanya chochote , najua unamahusiano makubwa na kiongozi wa mtandao wa Chatu nipo tayari kuongezea nguvu mtandao huo, tumefanya haya yote kutokana na presha kubwa kutoka kwa familia ya Mzee
Benjamini”Aliongea lakini Hamza hakumjali na muda uleule alimgeukia Afande Sucre.
“Wewe mzee njoo hapa”Aliongea Hamza na kumfanya Afande Sucre kutetemeka lakini kwa hofu kubwa alimsogelea Hamza.
“Mr Hamza kama kuna chochote unataka niambie nitafanya”Aliongea kwa kunyenyekea na kufanya wenzake kumwangalia kwa macho yaliojaa dharau kwa namna alivyonywea. “Nipe hio Bastora yako”
“Eeh!”
“Hutaki kunipa?”
“Hii hapa”Aliongea Sucre kwa haraka mara baada ya kusika sita kumpatia Hamza
Hamza mara baada ya kuishika ile bastora aliangalia ndani yake kama ina risasi na ilionekana kuwa nazo tatu na kitendo cha kuiweka sawa alikuwa ashaachia risasi ambayo ilitoboa paji la uso la mzee Sucre
Sucre hata hakujua amepigwaje risasi maana mkono wa Hamza ulifyatuka kwa spidi kubwa mno lakini ndio hivyo ilikuwa mwisho wake.
Hamza hakujali maiti ile na alimgeukia Fanueli ambae alikuwa akitetemeka kwa hofu pamoja na kundi lake.
“Nilisema kabisa sijaja kupigana lakini ukaamua kunidharau”
“Mr Hamza nilikosea tafadhari naomba unisamehe hili lipi…”
Kabla hata hajamaliza sentensi yake alikuwa ashachapwa lisasi mbili za kichwa na kudondoka chini.
Ndani ya dakika chache Hamza alikuwa ashamuua kiongozi wa kundi la Nyoka Mwenye masikio Meusi na Kanali Mstaafu Afande Fanueli Yowe.
“Kuna mwingine anataka kufa?”Aliuliza Hamza huku akiwaangalai waliobaki na kila mmoja alionekana kuwa katika hali ya kutetemeka huku baadhi wakitaka kujikojolea na waliishia kutingisha vichvwa vyao wakitia huruma.
Hamza hakuwa na mpango wa kumuua mtu
wakati anakuja hapo lakini uchokozi ulizidi hivyo alilazimika kutoa fundisho.
“Mimi ni kijana mpole sana tena mwanachuo , lakini naomba niwaambie tu Sipendi
Uchokozi”Aliongea Hamza na kisha alirusha ile bastora chini kisha alitoa simu yake ya batani na kuangalia saa na aliweza kuona muda ulikuwa umeenda sana.
“Nadhani taarifa zitamfikia anaewapa kiburi cha kutaka kufanya chochote ndani ya nchi hii, mwambieni ajifikirie mara mbili mbili kabla sijamchukulia hatua”Aliongea Hamza na kisha aliondoka ndani ya eneo hilo.
*****
“Wakati ulipokuwa umelela sijafanya chochote mbona?”Aliongea Hamza akiwa katika simu na Dina.
“Bado unaongea kimatani tu , asubuhi nimesikia taarifa umemuua Mzee Fanueli Yowe, mstaafu Mgweno ametoka kunipigia hapa anaomba yaishe”Aliongea Dina na kumfanya Hamza kucheka , ilionekana onyo ambalo alitoa jana limefanya kazi.
“Kuna onyo nilijaribu kutoa jana usiku na limefanya kazi , tumia nafasi hii kujiimarisha”Aliongea Hamza.
“Unajua kusababisha matatizo sana , sidhani pia kama ameomba kuyamaliza kwa nia ya dhati , kuna uchaguzi mwezi ujao ndio maana kaamua kujishusha, Mgweno ninaemjua mimi sio mtu wa kukubali yaishe kirahisi’
“Kama hajanielewa muache aje hata baada ya huo uchaguzi, mimi sipendi uchokozi ni hivyo tu basi , nitapambana kulinda amani yangu”Aliongea
Hamza na upande wa pili ulionekana kuwa kimya.
“Vipi baadae unakuja kunisalimia , sijakuona muda mrefu?”
“Muda mrefu wapi wakati ni juzi tu hapa?”
“Hata kama hakikisha unakuja usiku la sivyo nitakuja kuruka ukuta na kuingia ndani ya hilo kasri unaloishi siku hizi”Aliongea na kumfanya Hamza kuishia kukubali tu.
Hamza mara baada ya kumaliza kuongea na Dina alikata simu mara moja na muda huo ndio alikumbuka alikuwa ameghairisha mara kibao kwenda nyumbani kwa Eliza na pia kulingana na ratiba za siku hio aliona ingekuwa ngumu pia kwenda hivyo alimpigia simu na kumwelezea kuwa hatoweza kumtembelea.
Baada ya kuoga alivaa nguo na kisha alishuka chini sebuleni na aliweza kumkuta Regina akiwa bize jikoni akitengeneza Sandwich kwa kutumia kutumia Sausage.
“Regina unatengeneza Sandwichi au kitu gani?”Aliuliza Hamza.
“Sio lazima kujua ninachotengeneza”Aliongea huku akizidi kuwa bize, alionekana kujivunia kwa kile alichokuwa akifanya.
Kutokana na Shangazi kutokuwepo nyumbani aliona aingie mwenyewe jikoni.
Hamza alikumbuka Shangazi akimwambia Regina hakuwa akijua chochote kuhusu kupika hivyo alishangaa kumkuta jikoni.
Alijua Regina atatengenea utopolo wa chakula hivyo alifungua friji na kutoa mayai, tambi na nyama , vitunguu na pilipili hoho. “Unafanya nini , utachafua vyombo tu”
“Nitaviosha baadae nikirudi”
“Unadhani kula sana ndio afya , kwanini usisubiri tule hiki ninachopika?”
“Haijalishi nakula sana , sijui nitaishi kwa miaka mingapi mbeleni , mtu unapaswa kula kila unachojisikia maana hujui ni lini utashindwa kula”
“Mawazo yako yanasikitisha , kwahio unadhani kwasababu huwezi kuishi muda mrefu unachopaswa ni kula tu na sio kufanya vitu vingine ya msingi?”Aliongea huku akikunja sura lakini Hamza alikuwa mvivu kujibishana nae na alianza kusaga saga ile nyama.
Muda huo vipande viwili vya mkate vilichomoka ndani ya kibaniko.
“Aiyaa..”Regina alijikuta akishangaa huku akikunja ndita.
“Nini tatizo?” Aliuliza Hamza na huku akimgeukia na mara baada ya kuangalia kilichokuwa kikimshangaza Regina alijikuta akianza kucheka
“Haha.. Regina huo ni mkate au ni pande la mkaa?”
Vipande hivyo vya mkate vilikuwa vimegeuka kuwa vyeusi tii na sio Brown kama alivyotarajia.
“Unacheka nini sasa , nimezidisha moto ndio maana umeungua”Aliongea na kumfanya Hamza kusogea karibu na kuangalia
“Aina ya hii mikate inahitajika nyuzi tatu tu za joto kuubanika, sasa wewe umeweka sita unadhani nini kitatokea?”Aliongea na kumfanya Regina kuangalia mashine hio ya kibaniko na kuona kweli aliweka joto la juu mno.
“Nilikosea”Aliongea huku akirekebisha na kuanza kubanika upya vipande vya mikate ili ajazie na Sausage.
“Nilijua ni mzoefu wa kutumia hizo mashine za kupikia”
“Endelea na unachokifanya achana na mimi”Alimsukumia pembeni huku akiendela kuwa bize.
Baada kama ya nusu saa kila mtu alikuwa ameshamaliza kutengeneza kile alichokuwa akitengeneza , Hamza alitengeneza tambi za mayai nyama na kuweka na Regina alikuwa ametengeneza Sandwich zake za Soseji.
Baada ya kukaa mezani kila mtu alikula kile alichoandaa mwenyewe.
Sasa Regina ile anapeleka mdomoni kung’ata kipande cha mkate alijikuta akikunja sura na alitema palepale.
“Hizi Soseji nadhani zilikuwa zimeshaharibika , ni chachu mno”
“Kwahio ulipika bila ya kuangalia kama muda wake umeisha?”Aliuliza Hamza na kumfanya Regina kuwaza kwanini hakuangalia kabla.
Alijikuta akitia huruma huku akiangalia kitafunwa alichoandaa kilichokuwa kimeshachacha na kujikuta akiangalia sahani ya Hamza iliojaa tambi za mayai kama vile ni Pizza, alijikuta akimeza mate kutokana na harufu yake nzuri.
Hamza aliweza kujua mwanamke huyo alikuwa akitaka cha kwake lakini alikuwa akishindwa kuongea.
“Regina nadhani haitakuwa vizuri kuharibu chakula , unaonaje tukiambizana kumaliza hiki cha kwangu”Aliongea Hamza akimaanisha wasaidiane kula na kumfanya Regina kusafisha koo.
“Kwasababu umeniomba nikusaidie nitafanya hivyo , nitakula kidogo kukupunguzia mzigo”
“Asante kwa msaada wako bosi”Aliongea Hamza huku akimpunguzia kwenye sahani yake.
Kitendo cha Regina kuonja alijikuta macho yakimtoka na palepale alijiambia inakuwaje Hamza anajua kupika namna hio , japo tambi hizo zilionekana za kawaida kwa kupikwa na nyama pamoja na mayai lakini hakuamini zingekuwa na radha tamu kama hio.
“Hey! , hivi ushawahi kuwa mpishi?” Regina alishindwa kujizuia na kuuliza.
“Hapana”?”
“Sasa inakuwaje unajua kupika namna hi”
“Labda ni kwasababu sio rahisi kuishi, ndio maana ni vizuri kuhakikisha unajua namna ya kuridhisha tumbo lako”Aliongea Hamza lakini jibu lake ni kama halikumridhisha Regina na shauku kubwa ilimvaa.
“Regina unanisifia?”
“Kidogo tu”Aliongea Regina kwa sauti ya chini na kumfanya Hamza kutabasamu.
Baada ya kifungua kinywa walindoka kwa pamoja wakiwa na nyaraka maalumu na kuelekea Bomani kwa ajili ya kukitafuta cheti cha ndoa.
Kwasababu Lexus ilikuwa imelipuka walitumia Mercedenz Benz Maybach , ilikuwa gari nzuri ambayo haikupitisha risasi.
Kutokana na ukubwa wake katika jamii swala zima la kupata cheti halikuchuwa muda , mwanadada ambae alikuwa amesimamia swala zima alijikuta akimuonea wivu Hamza kwa kuweza kupata mwanamke mzuri kama Regina.
Mara baada ya kurudi kwenye gari , Regina alionekana kuwa na hisia mchanganyiko mara baada ya kuona picha zao katika cheti
Hamza aliishia kumuangalia kupitia kioo cha nyuma na kuona ni kwa namna gani Regina alionekana kuwa na wasiwasi.
“Vipi sasa , unahisi kuna chochote kilichobadilika?”
“Sioni chochote cha ajabu , nimefanya yote haya kwa ajili ya kumridhisha bibi tu ili anipe hisa zake”Aliongea Regina.
“Ndio unaona ipo hivyo , muda ni fumbo kubwa mno sikudhania nitajikuta katika hali kama hii , ila inanifanya niwe na furaha bila sababu ya msingi”Aliongea Hamza.
“Hiki ni cheti tu , unaweza kuoa muda wowote unaotaka , hili likipita tutafuata taratibu na kufuta hiki cheti , hakikisha mpenzi wako hajui sitaki matatizo”
“Swala la kufuta cheti ni mimi kuamua kama nakubali au lah , lakini usijali sana , muda una majibu mengi”Aliongea Hamza , lakini licha ya kuonekana ana furaha upande wa Regina hakuwa na furaha na alimtaka Hamza kuendesha gari kuelekea hospitalini ili kumuonyesha bibi yake cheti aridhie kumkabidhi hisa zote za kampuni.
Lakini sasa wakati wanafika ndani ya maegesho ya magari katika hospitali hio ni kama Hamza alikuwa akisubiriwa kwani walikuwepo Polisi wakiongozwa na Nobert.
“Mr Hamza upo chini ya ulinzi kwa makosa ya mauaji yaliotokea jana usiku”AliongeaNobert akiwa siriasi na polisi wenzake walimzingira kutaka kumfunga pingu huku wakiwa katika hali ya tahadhari na siraha zao.
Regina alijikuta akitoa macho mara baada ya kusikia kauli hio, ilikuwa ni kama hajasikia vizuri.
*****
Upande mwingine ndani ya makao makuu yya
Taasisi ya Haliz Foundation katika floor ya nne kwenda chini ya vyumba vya Ardhi, Amosi alionekana kuwa macho licha ya kwamba bado mikono yake ilikuwa imefungwa na vitu kama pingu katika kitanda na kumfanya ashindwe kusimama.
Alionekana kuwa na utulivu wa hali ya juu na alikuwa kama mtu ambae alikuwa akisubiria mtu aingie kwenye wodi hio.
Upande mwingine nyuma ya chumba alicholazwa Amosi kulikuwa na watu wanne waliovalia makoti ya kidaktari mmoja wapo akiwa ni Sister Maya Thema na mwingine alikuwa ni Frida ambae alionekana kuwa na mshangao akiangalia Skrini iliokuwa ukutani ikimuonyesha Amosi.
“Profesa kama hili lingekuwa swala ambalo jamii inapaswa kuambiwa basi katika historia Tanzania inaingia katika nchi tatu ambazo upandikizaji wa Chip kwenye ubongo wa binadamu umefanikiwa kwa asilimia mia moja”Aliongea Frida na kumfanya Dokta Maya Thema kutingisha kichwa kukubaliana nae.
“Kwasasa hii teknolojia wakuu hawataki ikitangazwa kwa jamii ya watu mpaka kukamilisha mipango yao , lakini licha ya hivyo imenipa hali ya kujivunia kufanikisha operesheni hii kwa mara ya kwanza katika Ardhi ya Afrika”Aliongea.
“Nini hatua inayofuatia baada ya hapa?”Aliuliza Frida huku akiwa na macho yaliojaa shauku.
“Sisi ni wanasayansi pekee na kazi yetu ni kukamilisha kile ambacho wafadhili wetu wanataka kufanya, hatua inayofuatia ipo chini ya Ajenti wa umoja wa Sinagogu”Aliongea.
“Profesa kwahio kwasasa pale yupo imara kiakili , hakuna athari zozote nje ya zile zilizotarajiwa zilizoweza kuonekana kupitia tabia yake?”Aliuliza Frida.
“Leo ni siku yake ya nne tokea kufanyiwa operesheni , siku ya kwanza alikuwa kwenye hali ya kawaida ya mshituko na kuikataa hali aliokuwa nayo , lakini kwa kushitua mishipa yake ya fahamu eneo la hisia tumeweza kufanikisha kumfanya kuwa katika hali ya mazoea , kuhusu tabia ambazo zipo nje ya matarajio bado hatujaona na hatuna budi kumfuatilia hata akiwa katika mazingira ya kawaida”
“Profesa hii sio operesheni ya kwanza kufanyika , mbili ziliweza kufanyika nchini Uingereza na moja nchini Marekani na mbili Israeli na ni zaidi ya miaka kadhaa imepita tokea kufanikiwa kwa operesheni hizo , kwanini tusitumie Follow up ya
data za wagonjwa waliopita?”Aliuliza Dokta John moja ya wanasayansi wa taasisi hio.
“Kila operesheni inayofanyika katika upandikizaji wa Chip katika Ubongo inabeba malengo tofauti hivyo matokeo ya kitabia kuwa tofauti pia , Katika historia ya Dunia Operesheni ya kwanza ya kupandikiza kifaa kwenye ubongo ilifanyika nchini Ujerumani chini ya Usimamizi na ufadhili wa Nazi , malengo ya upasuaji ule yalilenga kufanya wanajeshi kuwa imara zaidi katika kubuni mbinu za kumshinda adui , unachopaswa kuelewa utofauti wa operesheni ile na wa leo ni kwamba ule ulifanyika katika kufunua kichwa cha binadamu na kisha kuweka kifaa lakini huu umefanyika bila ya kufungua kichwa cha binadamu ikimaanisha dunia ilipiga hatua kutoka wakati ule , tulichelewa miaka mingi kuendeleza sayansi ya upandikizaji Chip tokea vita ya pili ya Dunia mpaka sasa kutokana na Josef Mengele kumuua Dokta Douglas kwa sumu akiwa katika maabara ambae ndio alibeba jukumu kubwa la tafiti za ubongo wa binadamu, hakuishia kumuua Dokta Douglas tu bali alichoma tafiti zake zote na kitendo kile kilirudisha dunia hatua moja nyuma katika maswala ya tafiti za kibailojia”Aliongea Dokta Maya na jibu lile kidogo lilionekana kumshangaza na Frida.
“Profesa unamaanisha Joseph Mengele huyu ambae katika historia alifahamika kama Malaika wa kifo , sijawahi kusikia jina la Dokta Douglas katika historia kwanini alimuua?”
“Hakuna ambae ashawahi kumsikia Dokta Douglas kwasababu alikuwa ni mwanasayansi ambae anapiga hatua na hakukuwa na matokeo ya wazi ya tafiti zake , mgonjwa wake wa kwanza ambae alimpandikiza kifaa katika Ubongo hakuonyesha matokeo makubwa sana kama nadharia ilivyokuwa, pengine alifanikiwa au pengine hakufanikiwa ndio maana Josef Mengele alimuua na kuchoma tafiti zake”.Aliongea Dokta Maya Thema.
“Imekuaje ukawa na taarifa ya swala hili , Profesa kwa umri wako…”
“Frida si kila kitu ndani ya dunia hii kipo wazi na sio kila mwenye umri mkubwa anafahamu kila kitu , historia ipo leo kwasababu imetunzwa , kabla ya
kuwa muumini wa Sinagogu nilikuwa mwanasayansi nchini ya Kanisa kuu”Aliongea Maya na kumfanya Frida kutingisha kichwa.
Alielewa watu wengi ambao walikuwa na historia kubwa na Kanisa kuu walikuwa wakijua mambo mengi.
Muda ule wakati wakiongea katika Floor hio aliingia bwana mmoja alievalia suti , alikuwa ni kijana ambae ana muonekano wa kidominikani au kilatini kwa lugha nyepesi, ikimaanisha kwamba alikuwa na asili ya makabila matatu yaani Mzungu kwa asilimia hamsini , Mwafrika kwa asilimia arobaini na mlatino kwa asilimia kumi.
“Ajenti Alonzo karibu sana”Aliongea Maya Thema alionekana kumfahamu yule bwana ambae tembea yake ilionyesha ni kwa jinsi gani alikuwa mkakamavu.
“Asante sana Profesa”Aliongea na kisha macho yake yalitua katika sura ya Frida na kumfanya ProfesaMaya kuchukua jukumu la mara moja kumtambulisha Frida na Dokta John.
“Mr Alonzo huyu ni Dokta Frida Franklin mkuu wa idara ya CST , kutana pia na Dokta John mtaalamu wa Neva”Aliongea na Ajenti Alonzo alisalimiana nao.
“Nimefurahi kukutana na wewe Frida , nimelisikia jina lako mara kadhaa na imekuwa heshima kwangu kukutana na mwanasayansi kama wewe”
“Asante sana”Aliongea huku akitoa tabasamu la ukarimu na muda uleule Ajenti Alonzo macho yake yalitua katika Skrini iliokuwa ikimuonyesha Amosi.
“Nimeambiwa kila kitu kwa upande wako kimekamilika , nipo hapa kwa ajili ya kukamilisha hatua ya pili, kwanini bado amefungwa kwenye kitanda?”Aliuliza.
“Tumeamua kuchukua tahadhari , lakini kutokana na utendaji kazi wa ubongo wake sidhani kama anaweza kuwa hatari ”Aliongea Dokta Maya.
“Operesheni hii sio kwa ajili ya kumfanya kuwa mwanajeshi mwenye uwezo bali kuwa Ajenti mtiifu na Muaminifu kwa Sinagogu ambae anaweza kutuambia kila kitu, kama kutakuwa na matumizi ya nguvu kumuweka sawa , basi mimi ni mwanajeshi”Aliongea na kumfanya Dokta Maya kukubaliana nae na aliongozwa kuelekea mpaka kwenye chumba alichokuwemo Amosi.
Ajenti Alonzo akiwa ameingia na Dokta Maya Thema kabla ya salamu aliomba Amosi afunguliwe mikono na awe huru na Dokta Maya alifanya hivyo.
“Profesa kwanzia hapa nitaendelea mwenyewe , naomba Kamera zote kuzimwa”Aliongea.
“Bila shaka Ajenti”Alijibu Profesa na kisha palepale Profesa alitoka na kumuacha Amosi na Ajenti Alonzo.
Comments