Ilimchukua dakika kama kumi tu kwa Ajenti Alonzo kujitambulisha na Amosi kumuelewa , kwa wakati huo Amosi alionekana kuwa kawaida , ki ufupi hakuwa na tofauti sana kitabia , kitu kimoja tu ambacho kilikuwa tofauti ni namna ambavyo alikuwa mtiifu kwa kile ambacho alikuwa akielezewa na Alonzo.
“Mr Amosi kwasasa utafahamika kwa jina la Ajenti Zuku ikimaanisha Askari usie na chimbuko, umenielewa?”
“Ndio Sir”Alijibu Amosi kwa utiifu akiwa ameketi kwenye kiti na kumfanya Ajenti Alonzo kuridhika.
“Kilichofanyika kwako haimaanishi kwamba jina lako katika mazingira ya kawaida linakwenda kuwa tofauti , ukitoka hapa unakwenda kuendelea na maisha yako ya kawaida”
“Ndio Sir”
“Vizuri kabisa , mpaka sasa umefahamu nini katika misheni yako juu ya Naomi Lindsey na Rosemary Macha?”Aliuliza na kumfanya Amosi kufikiria kidogo.
“Sijapata kufahamu kwa uhakika lakini hisia zangu zinaniambia Naomi na Rosemary ni mtu mmoja na kuna uwezekano Naomi alidanganya kifo chake nchini Italy na kisha akakimbilia Tanzania kwa uhusika wa Rosemary Macha”Aliongea Amosi.
Hizo ndio zilikuwa hisia zake tokea siku kadhaa apewe misheni na Chriss na katika uchunguzi wake alikuwa akitaka kuthibitisha swala hili na kisha kuliunganisha na tukio lililotokea mkoani Rukwa huko Sumbawanga.
Hio ndio ilikuwa misheni yake ambayo Chris alimpatia , misheni ya kutafuta mahusiano yaliopo katika ya Rosemary Macha na Naomi Lindsey msanii mkubwa aliefariki nchini Italy.
Ajenti Alonzo alionekana kuridhishwa na jibu la Amosi na muda ule alionekana kutoa kishikwambi katika mkoba aliokuja nao na kupangusa kwa dakika kadhaa na kisha alimwangalia Amosi.
“Unajua nini kuhusu tukio lililotokea Sumbawanga?”Aliuliza
“Sikuwa muhusika wa uchunguzi wa tukio hilo , Ajenti Sedekia Shilla ndio alieweza kufanya uchunguzi na nusu ya ripoti ilifika makao makuu na nusu nyingine haikuweza kufika kutokana na Ajenti Sedekia kutoweka, taarifa ambayo alitoa ni mwanamke ambae hakufahamika jina lake kamili zaidi ya jina la Chakwe ambalo alibatizwa na mmoja ya wanakijiji wa Kizwite aliweza kufika ndani ya kijiji hicho akiwa na watoto kumi wenye asilia ya makabila tofauti tofauti , aliishi ndani ya kijiji cha Kizwite kwa zaidi ya miezi sita na aliweza kumudu mahitaji yake na watoto kupitia kwa misaada mbalimbali ambayo wanakijiji walimpatia , siku kadhaa mara baada ya kupatiwa msaada wa eneo la kuishi ikiwa ni kipindi cha Masika kuliweza kutokea ajali ya radi na kumuua yeye na watoto wake tisa huku mmoja ambae inaaaminika alikuwa na asili ya Kizungu alitolewa eneo la tukio na mtu asiefahamika na kutoweka, Ajenti Sedekia alikusanya ushahidi kutoka kwa mashuhuda wa tukio hilo na aliweza kuwasilisha taarifa hio makao makuu , lakini kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa moja kwa moja kutokana na utata wa tukio hilo kesi ilifungwa kama ajali ya asili iliomuua mama na watoto wake wote”Aliongea Amosi.
“Unadhani ni kwanini Ajenti Sedekia alipotea!?”
“Sina uhakika, lakini naamini utata wa tukio hilo ndio ulimpoteza” “Unamaanisha nini?”
“Pengine kuna kitu ambacho Ajenti Sedekia aliweza kupata kuhusu utata wa tukio hilo na kuna watu ambao walitaka kuficha taarifa hio ndio maana akapotea” “Kwanini unahisi hivyo?”
“Wakati nikiwa Ajenti nimeweza kusikia tetesi kuhitimishwa kwa kesi ile kama ajali ya kawaida ulitoka kwa Kiongozi wa juu kabisa wa nchi na kuna taarifa pia zinasema kuna nguvu ya nje ya nchi iliohusika, hisia zangu nguvu hio ndio iliompoteza Ajenti Sedekia”Aliongea Amosi kitiifu kabisa.
“Umesema wakati ukiwa Ajenti , sasa hivi wewe sio Ajenti?”Aliuliza na kumfanya Amosi kutulia kidogo na kumfanya Alonzo kumkazia macho.
“Nilikuwa Ajenti wa kitengo cha Intellijensia za kimkakati cha TISA kwasasa mimi ni Ajenti wa siri wa Kitengo cha jeshi cha kupambana na nguvu zisizoonekana kiitwacho MALIBU”Aliongea na kumfanya Ajenti Alonzo kutoa tabasamu. “Nielezee zaidi kuhusu ulichopata tokea kuanza kazi ya kuchunguza uhusiano wa Naomi Lindsey na Rosemary Macha?”Aliongea na kumfanya Amosi kufikiria kidogo.
“Katika uchunguzi wangu nimeweza kugundua watu wa kisiwa cha Binamu hawakutaka niendelee na uchunguzi sijajua kwasababu ni nini lakini kupitia kazi hio niliwekewa mtego wa kuuwawa na moja ya mkuu wangu wa kazi na kwa bahati nzuri niliweza kunusurika”
“Unadhani mkuu wako alikuwa akishirikiana na watu kutoka kisiwa cha Binamu”
“Ndio , nina uhakika ni mshirika na watu kutoka Binamu”
“Kwa ninavyojua ufanisi wa watu kutoka kisiwa
Binamu ulivyo mkubwa usingeweza kuepuka kifo , hujawahi kufikiria pengine waliamua kukuacha hai makusudi au kuna sababu nyingine ambayo wakaacha kukuwinda?”Aliuliza
Licha ya Amosi kuulizwa maswali mengi lakini alionekana kutokereka kabisa wala kuchoka , ilikuwa ni tofauti na tabia yake , pengine ni kile ambacho ubongo wake ulifanyiwa.
“Kuhusu hili nimefikiria pia , lakini mkuu wa kitengo aliniambia niendelee na uchunguzi na ameshaongea na Kitengo cha TISA kwa ajili ya Kinga”
“Kwa maelezo yako ulipokea kazi kutoka kwa Chriss sio kwasababu ya pesa , unaweza kuniambia kwanini ulipokea kazi hii licha ya kuonekana kuwa na uhatari?”
“Mwanzoni nilipokea kutokana na shauku , lakini nilipata hamasa zaidi mara baada ya kujua ni kazi ambayo inahusiana na tukio la mwaka 2002 lililomfanya Ajenti Sedekia kupotea, nimekuwa chini ya kitengo cha MALIBU kama ajenti hai kwa miaka saba, kabla ya kupewa misheni nyingine ambayo ilinifanya kuwa Undercover kwa kivuli cha kustaafu na kuanza kuwa mtumwa wa kazi za kihalifu za vigogo wa nchi”
“Misheni!, ilikuwa misheni gani?”Aliuliza Ajenti Alonzo.
Licha ya Amosi kujua kabisa anatoa siri za kitengo lakini alishindwa kujizuia kuongea.
“Nilipewa misheni ya kufuatilia tetesi za uwepo wa watu Vivuli maarufu kama ‘Night Shadows’ na kuongezeka kwa wimbi la wagonjwa wenye ‘split Personality Disorder’”Aliongea na kumfanya Alonzo kutingisha kichwa na muda ule aliangalia kishikwambi chake.
“Elezea kila kitu ulichofanya ili kufanikisha uchunguzi wa Naomi Lindsey na Rosemary Macha”
“Baada ya kunusurika kifo niliweza kuendelea na uchunguzi na kwa kumfuatilia Kanali Dastani aliekuwa mkuu wangu wa kazi niliweza kugundua kuna mfungwa ambae kuna uwezekano mkubwa
alihusika na kupotea kwa Sedekia Shilla , niliweza kupata taarifa hii kwa kufuatilia mazungumzo ya simu kati ya Dastani na moja ya aliekuwa Mkuu wa Gereza la Silo, kwa kile nilichoweza kupata kusikia ilionekana kuna watu walimtembelea huyo mfungwa Gerezani na Mkuu wa Gereza hilo aliweza kurekodi maongezi kati ya watu hao na mfungwa , kwa bahati mbaya katika harakati za kutaka kumfikia mkuu wa Gereza ili kujua walichoongea mkuu huyo wa Gereza alikumbwa na umauti na imani yangu inaniambia kifo chake kinahusiana na kitendo alichofanya cha kurekodi mazungumzo hayo”Aliongea na kumfanya Ajenti Alonzo kutingisha kichwa.
“Katika maelezo yako umesema unadhani Naomi
Lindsey ni Rosemary macha , je unadhani pia Rosemary Macha anaweza kuwa mwanamke
aliefariki katika ajali ya radi akiwa na watoto wake?”
“Wakati nikiwa Ajenti nilibahatika kuona picha ya Chakwe mhangwa wa ajali ya radi na picha yake inafanana kwa asilimia mia moja na picha ya Naomi Lindsey na Rosemary Macha , hivyo naweza kusema wote wanaweza kuwa mtu mmoja”
“Kwa hitoria ya Naomi Lindsey hajawahi kabisa kuwa na mtoto katika maisha yake na pia kulingana na umri wake ni ngumu kuwa na watoto kumi , tena wa baba tofauti tofauti , lakini pia kuna historia ya kimatibabu ambayo inaonyesha Naomi
Lindsey hawezi kubeba ujauzito kutokana na kukosa kizazi , kama unachodhania ni sahihi unadhani watoto aliokuwa nao Chakwe ni wa nani?”Aliuliza Alonzo na kumfanya Amosi akili yake kufanya kazi na sasa ni kama anapata kitu kipya na kujiambia kwanini hakuwahi kufikiria hilo.
“Nadhani Mr Amosi utakuwa na maswali kwanini nakuuliza maswali yote haya , kabla ya kujua unachokwenda kufanyia kazi nilitaka kujua unachojua kwanza, nadhani wakati unakutana na Chriss alikuelezea wewe ndio mtu sahihi katika misheni aliokupatia si ndio?”
“Ndio alisema hivyo na ilinishangaza pia kusikia hivyo?”
“Kuna sababu yoyote ambayo unadhani kwanini tulikuchagua kwa hii misheni?”
“Sijui , labda ni kwasababu nishawahi kuwa chini ya kitengo cha TISA na kuhusika kwa namna moja na kesi hio ya Radi”Aliongea Amosi na Alonzo alitingisha kichwa kukataa na palepale aliangalia tablet yake na alionekana kupangusa pangusa na kisha alimpatia Amosi.
Katika Tablet ile kulionekana picha ya watu wawili , mwanaume na mwanamke na kwa jinsi pozi lao lilivyo katika picha ni aidha watu hao walikuwa wapenzi au marafiki”Amosi alishangaa mara baada ya kuona ni picha ambayo alikuwa akiifahamu na yeye ni moja ya mhusika aliekuwa katika hio picha.
“Unaweza kuniambia huyu mwanamke pembeni yako alikuwa nani kwako?”
“Huyu ni Jasmine Mahmood niliwahi kuwa nae katika mahusiano kwa muda mfupi, alikuwa raia kutoka Botswana aliwahi kuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Aljazeera English nchini Qatar”Aliongea na kumfanya Alonzo kuchukua kile kishikwambi kwa mara nyingine na kisha alionekana kutafuta kitu na kumpatia.
Ilikuwa picha nyingine ikimuonyesha Jasmine Mahmood akiwa na Naomi Lindsey katika pozi la tabasamu na picha ile ilimshangaza mno Amosi.
Comments