Reader Settings

SEHEMU YA 58

Ajenti Alonzo mara baada ya kuona  Amosi alikuwa akishangaa , alijua fika kile ambacho alikuwa akikitaka kutoka kwa Amosi  amekiona.

“Mr Amosi  unaweza kuniambia ni lini ulikuwa na mahusiano na  Jasmine Mahmood?”Aliuliza na Amosi alifikiria kidogo na kisha alitingisha kichwa.

“Ilikuwa ni mwanzoni mwaka 2002, nilikutana  na

Jasmine  mwezi wa kumi na moja  2001 

Amsterdam nikiwa katika msafara wa mheshimiwa  Raisi  kama Aide , Jasmine alikuwa mwandishi wa habari aliesafiri  na mheshimiwa Festos Moga na ndio  urafiki wetu ulianza , mwaka 2002  wakati anafika nchini Tanzania  katika maonyesho ya  riadha ndio tuliingia kwenye mahusiano rasmi ambayo yalidumu kwa muda mfupi sana”Aliongea Amosi.

“Kwanini  mahusiano yenu yalidumu kwa muda mfupi?”

“Sababu kubwa ilikuwa umbali  lakini  pia kazi yangu ilinifanya kushindwa kusafiri  mara  kwa mara nje ya nchi kuonana nae”

“Hii picha  Jasmine aliopiga na  Neema Lindsery   ilikuwa ni  tarahe ishirini na  tano  mwezi wa  kumi na mbili  mwaka  2001 , siku nne kabla  ya  kifo  cha  Naomi, ni picha iliopigwa na Mattia  Tommaso, mara baada ya kifo cha  Naomi  kutokea  Jasmine alionekana nchini  Tanzania  kama mwandishi  wa  habari kutoka Botswana   na   kama ulivyosema ndio kipindi ambacho mliingia kwenye mahusiano , si ndio?” “Ndio”Alijibu Hamza.

“Ukiachana na mahusiano yenu unakumbuka chochote kisichokuwa cha kawaida kutoka kwa  Jasmine?”Aliuliza Alonzo na  kumfanya  Amosi kufikiria kidogo.

Ukweli ni kwamba  katika kipindi hicho ni kama matukio ya nyuma alikuwa akiyakumbuka kwa urahisi mno, kwake ni kama  matukio hayo yalitokea  jana.

Ubongo wake ulikuwa na nguvu  sana ya kukumbuka  mpaka vitu ambavyo  alikuwa amekwisha kuvisahau, hata vile vitu ambavyo havikuwa na msingi  sana katika  kipindi alichokuwa na Jasmine aliweza kukumbuka, ki ufupi ilikuwa ni kama anaangalia  tamthilia ya maisha yake na Jasmine.

“Nadhani nimekumbuka kitu?”Aliongea  Amosi na kumfanya  Alonzo kumkazia macho.

“Umekumbuka nini?”

“Nilikuwa na  mahusiano na Jasmine kwa  miezi  mitatu pekee kabla ya kurudi nchini  kwao  Botswana , katika kipindi hiki tulikuwa na furaha wakati wote  ila  siku moja tu alionekana kunikasirikia sana  kiasi cha kubadilika na kuwa mtu mwingine”Aliongea Amosi.

“Nakusikiliza , nini sababu ya yeye kukasirika?” “Nilishika  mkufu  wake uliokuwa na  kidani chenye  muonekano  wa  kipekee”Aliongea Amosi na kumfanya  Ajenti  Alonzo  midomo yake kucheza kidogo.

“Unaweza kuelezea kidogo  kuhusu   huo mkufu hasa   kidani?”

“Kilikuwa kidani   flani ambacho kilitengenezwa  kwa madini  meupe kama kioo kwa juu na ndani kulikuwa na rangi   za ajabu  zilizojikunja  kunja kama wingu  linalozunguka  na katikati  kuna kitu kama  kijishimo cheusi , upande wa nje  kuna  duara  za vitu kama nyota ,  na eneo ambalo mkufu ule ulishikilia  kuna alama  flani hivi kama sikosei ni kama  zile za miungu  wa  Misri ya kale  inayowakilisha  uhai na kifo”Aliongea  Amosi na kumfanya  Alonzo kuridhika.

“Kuna  sababu yoyote ambayo ilimfanya kukasirika ,  jaribu kufikiria  kila kitu na uelezee katika  jicho la ujasusi”Aliongea na Amosi alifikiria.

“Nakumbuka nilimwambia kwanini amekasirika ilihali nimeushika tu bila kufanya chochote  ila hakunipa jibu  la kueleweka ,  moja ya kitu ambacho  ni cha ajabu   mara baada ya kuona ule mkufu  roho yangu ilishikwa na kiu kubwa ya  kutaka niouone tena  kwa mara nyingine , ilikuwa ni kama nimesahau  ulivyo na nilitaka kuuona ili kuanza kuufikiria upya , wakati Jasmine anaondoka  nilimsihi  kuuona tena ila  alinijibu kwamba  haukuwa wa kwake na alirudisha kwa mwenyewe na nisahau kama nimewahi kuuona kwake”Aliongea Amosi..

“Sitilii shaka maelezo yako kabisa , kwasababu  kilichofanyika katika ubongo wako ni kukuwezesha iwe rahisi kwako kukumbuka matukio  yaliopita, Je uliangalia upande wa pili wa  Kidani,  pia  je ulipata nafasi ya  kuangalia kidani hicho kwa umbali kidogo?”

“Ilikuwa ni kwa  sekunde kadhaa  tu  na Jasmine alinipokonya, sikubahatika kuangalia upande wa nyuma wala kwa umbali”Aliongea Amosi na jibu lile lilionekana kumnyong’onyesha  Alonzo.

“Umejibu vizuri kabisa na nimeweza kupata  kila nilichotaka, naomba nikwambie  ukweli sasa , sababu ya wewe kuwa katika hali hii ni kwasababu uliona kitu ambacho  ni binadamu   watatu  tu duniani  waliowahi kuona , siwezi kukuelezea  ulichoona kina maana gani  ila  wewe ni mtu  wa tatu, hii ndio sababu ambayo  tulikupa  kazi ya kumfuatilia  Naomi Lindsey na Rosemary Macha mara baada ya kugundua uliwahi kuwa katika mahusiano  na  Jasmine Mahmood katika wakati ambao ulikuwa na maswali mengi na kutufanya kuona haikuwa bahati mbaya kwenu  kuwa katika mahusiano”Aliongea Alonzo na Amosi alitingisha kichwa.

“Kwanzia sasa utaendelea na misheni yako kama

kawaida , ila malengo yamebadilika , ukishafanikiwa kujua uhusiano kati ya Naomi

Lindsey na Rosemary Macha  tutataka kujua  wapi  Jasmine alipeleka huo  mkufu, taarifa za awali  zinaonyesha mmiliki wa ule mkufu ni  Naomi , hivyo kazi yako ni kufanya uchunguzi je  Jasmine aliweza kukutana na mwanamke aliefahamika kwa jina la Rosemary nchini Tanzania na je ndio mwanamke aliefariki  kwa ajali   ya radi mwaka 2002 , utafuatilia na kujua kila kitu  na  ndipo misheni yako itaingia katika sehemu ya tatu ya malengo makuu”Aliongea  Alonzo na Amosi aliitikia kukubali.

Dakika chache mbele  Alonzo aliweza kuachana na 

Amosi na alirudi  katika ofisi ya  Profesa Maya Thema.

“Profesa  viongozi walikuwa na wasiwasi na mafanikio ya hii operesheni , lakini kama ulivyowaaminisha   imefanikiwa kwa asilimia  kubwa”Aliongea Alonzo kwa Lugha ya  Kihispania  na kumfanya  Dokta Maya Thema kutoa tabasamu.

“Nini kimekuaminisha Ajenti?”

“Katika kipindi chote nilichokutana na wagonjwa  ambao  wamepitia  utaratuibu  maalumu wa ubongo wao kurekebishwa , wengi wao

walitofautiana katika  wingi wa maswali wanayouliza

, lakini kwa Amosi hajauliza swali   hata moja”Aliongea.

“Ili kupima asilimia za mafanikio   mara nyingi  tunaangalia wasiwasi  ambao anakuwa  nao mgonjwa  na tabia kuu  ya kuonyesha ni kwa kiasi gani  yupo na wasiwasi  ni  wingi wa maswali anayouliza , ikitokea hajauliza swali hata moja   basi tunaweza kusema tumeudhibiti ubongo wake kimawazo kwa asilimia mia moja”Aliongea Profesa na Ajenti Alonzo alitingisha  kichwa.

“Nitapeleka hizi taarifa  makao makuu , zitaendelea kuimarisha nafasi yako katika umoja , lakini hata hivyo  katika wagonjwa wote waliopitia taratibu wengi wao ni  kutaka kujua kile ambacho wanajua na wamesahau  lakini kwa huyu ni tofauti  hivyo Profesa ili  aweze kufanikisha kazi ambayo  umoja inatarajia kutoka kwake  tunataka  arudi katika hali yake ya kawaida  kwa muda”Aliongea Alonzo na kumfanya  Dokta Maya Thema kushangaa kidogo.

“Lakini ni hatari kama tutafanya hivyo , anaweza kupoteza baadhi  ya kumbukumbu za maisha yake ya kawaida yaliopita”Alionge.

“Profesa  haya ndio maelekezo nilioweza kupata kutoka kwa  Askofu  , najua  njia ipo ya kumrejesha katika wakati wake wa kawaida  na kusahau baadhi ya matukio yaliomtokea  wakati huo huo tukimdhibiti  kihisia ili  isitokee  akawa msaliti kwa Sinagogu”Aliongea  Alonzo na kumfanya profesa Maya Thema kufikiria  kwa muda.

“Nilitamani sana kuona maendeleo yake  katika mazingira ya kawaida , huyu ndio mgonjwa wangu wa kwanza kuwa na matokeo chanya  kwa asilimia kubwa  na  kuna mengi niliohitaji kujifunza  kupitia  tabia yake ,  hata hivyo kwasababu ni maagizo ya Sinagogu siwezi kupinga lakini  nikufahamishe  njia iliokuwepo kama itafanyika hatoweza kuishi zaidi ya miaka  mitano”

“Miaka mitano  ni mingi  sana  kwa Amosi kuweza kutimiza  makusudi ya  umoja  wetu Profesa , nadhani unajua ninachomaanisha”Aliongea  lakini licha ya Dokta Maya Thema kuonekana kukubali alionekana kuwa mzito , wito wa kidaktari ulikuwa ukimfanya kuwa na hali ya hatia.Kama Daktari alikuwa na hatia ya   kumfanyia Amosi  operesheni bila ridhaa yake , lakini hatia ilimshika zaidi mara baada ya kuona anakwenda kufanya procedure ambayo  itaweka ukomo wa uhai wa Amosi katika muda wa miaka mitano.

“Kwasababu tunahitaji  matokeo ya haraka sina budi , lakini kama Daktari nina masharti pia”Aliongea “Nakusikiliza Profesa”

“Baada ya kifo chake awekwe kwenye orodha ya mpango  Genesis 210”Aliongea Profesa Maya  Thema na kumfanya  Ajenti Alonzo  macho yake kuchanua.

“Profesa hiki  ni kitu ambacho  siwezi kuidhinisha na hata kama  nilifikishe kwa viongozi   kuna hatua kwa hatua za maamuzi na inaweza kuchukua zaidi ya miezi miwili , nadhani unafahamu ni kwa kiasi gani  Mpango Genesis 210  ulivyo nyeti , hatuna muda wa kusubiri mpaka  ngazi za juu kufanya maamuzi  la sivyo  kile kilichosimamishwa kwa  miaka  mingi baada ya kujitoa kwenye Kanisa kuu kitapotea”

“Huna haja ya kuongea zaidi Ajenti , nimeomba kitu ambacho kinawezekana , mkataba wangu  wakati nikiingia katika maabara za shirika  niliweka masharti nitalinda  haki ya mgonjwa kwa  namna nyingine ikitokea umoja unachonitaka kufanya kinakiuka miiko ya kazi yangu , kama  Askofu  alikuwa  mkweli na ahadi zake basi  atanikubalia katika hili”Aliongea  na kumfanya  Ajenti Alonzo kutoa kitambaa na kufuta jasho. “Nitafanya  mawasiliano”Aliongea. 

******

Saa nne  kamili asubuhi ilimkuta  Kanali  Dastani Mpiji ndani  ya  Wilaya  ya kibaha sehemu ambayo ndio  msiba wa Afande Mchuku ulikuwa  ukifanyikia.

Watu  walikuwa wengi japo sio sana  na Dastani hakufika na usafiri binafsi bali alifika na  Taksi na hio yote ilikuwa ni kuepuka  macho ya watu.

Shida ilikuwa moja tu licha ya kwamba hakutaka macho ya watu mwili wake ulikuwa mkubwa na kumfanya aonekane kama bosi  , hususani  kutokana na Kitambi chake.

Aliutumia uchangamfu wake kusalimiana na baadhi ya wanaume waliokuwa  eneo la msiba huku akitoa pole , licha ya wengi kutomfahamu lakini walimchangamkia , isitoshe   Afande Mchuku alikuwa mtu wa watu hivyo watu wengi walimfahamu.

Pembeni ya  uwanja palipo wekwa maturubai kulikuwa na nyumba ambayo ilionekana haijamalizika kabisa na kwa haraka  haraka fahamu zake zilimwambia lazima ndio nyumba ambayo  Mchuku alikuwa akiizungumzia , aliishia kutingisha kichwa na kuona   Afande Mchuku licha ya kutumia hila nyingi kujiongezea kipato  lakini hela zake hakuzimaliza katika Starehe , ilikuwa nyumba kubwa mno  ambayo tayari ishawekwa Grill , Milango na Plasta na  kulikuwa na vitu  vichache sana vya kumalizia ikiwemo madirisha ya Aluminium , kwa haraka haraka  alipiga mahesabu na kujiambia kama  Afande Mchuku angepata  hela  ambayo alitakiwa kumlipa kwa ajili ya kupata rekodi basi  angeweza kumalizia jengo hilo moja kwa moja.

“Swahiba  poleni na Msiba”Kijana mmoja alimsalimia Kanali Dastani , alikuwa ni bwana wa makamo kama miaka therathini hivi alievalia Kanzu na kibakrashia.

“Asante ostaz  tumepoa”Aliongea  Dastani na bwana yule alimpita na kuendelea kusalimiana na wazee wengine  na mara baada ya kumaliza alirudi  kukaa karibu na  Dastani.

“Siamini Mchuku ametutoka , watu wema  na tegemezi siku zote  ndio  wanaotangulia”Aliongea Kanali akianzisha maongezi.

“Binadamu siku ambayo anazaliwa mwisho wake umeshaandikwa, watu wote tunazaliwa tukiwa wema, dunia  tu ndio inatubadilisha, mwisho wa siku tuwe wema au tuwe wabaya  siku  ikiwadia  haichagui mwema au mtu muovu”Aliongea yule bwana huku akirekebisha  kibarakashia chake.

“Nakubaliana na wewe , lakini muda mwingine katika jicho la kibinadamu tunatamani  yule ambae ndio  msingi wa familia kuendelea kuishi”

“Mwenyezi Mungu ni wa haki na anayajua yote ,

Anawajua  Wema na waovu , anamlipa kila mtu  na matendo yake , Labda Mchuku  amepata kheri ya milele  mbali  na  maumivu ya dunia hii”.

“Huzuni yangu ni kwa wale aliowaacha , alionekana  mtu mwenye malengo makubwa ya kimaisha”

“Mwenyezi Mungu awape nguvu na amani katika kipindi hiki kigumu , awe faraja kwao”Aliongea yule Ostaz na kabla  hata  hajaingiza neno lingine la udadisi  kuliibuka kilio cha mwanamke na kufanya  karibia watu wote kugeuka na kutokana na kilio cha mwanamke huyo minon’gono iliibuka.

“Uwiii baba  Nasra wee! , uwiii , mbona umeondoka  mapema hivi mume

wanguu..”Kilikuwa kilio kilichowafanya wanawake waliokuwa wamekaa  upande  mwingine baadhi yao kumsogelea yule mwanamke.

Upande wa Kanali ni kama  tukio  lile lilimvutia , ukweli ni kwamba sio yeye tu ambae lilimvutia.

“Ostazi huyu ndio mke wa Mchuku!?”Aliuliza  Kanali  na kumfanya yule Ostaz kumshangaa kidogo.

“Nilijua una ukaribu  na  Mchuku”

“Ndio Ostaz, Mchuku ni rafiki yangu mkubwa na pia ni mfanyakazi mwenzake hatujawahi kuongea maswala yetu  binafsi”Aliongea Kanali akiharakisha kujitetea.

“Inawezekana , wengi hapa ni watu ambao  ni marafiki  wa Mchuku , alikuwa mtu mwema, huyo ni mke wa pili ni daktari mwajiriwa huko mikoa ya Lindi”Aliongea  yule Ostazi  na kumfanya  Dastani sasa kujibu  kitu ambacho kilimvutia.

Yule mwanamke alionekana mrembo na pili ni aina ya wanawake ambao ukiangalia tu unaweza  kujua hadhi yake ya kisomi. Jambo lile lilimfanya Dastani  kumfikiria  Mchuku kwa  namna ya kumsifia, ijapokuwa hakumuona bado mke mkubwa  lakini mke huyo wa pili  alikuwa mrembo.

“Nasikia jamaa  alimwambia mke wake mkubwa akifariki asimlilie”Moja ya Vijana waliokuwa nyuma  ya  Dastani walikuwa wakiongea na kauli ile ilimfanya  masikio ya antena ya Kanali kunyaka mawimbi.

Aligeuka na kumwangalia Ostazi kama na yeye anasikia lakini  aliweza kumuona  Ostazi  akiwa bize kusalimiana  na mwanaume mmoja wa makamo  ambae alionekana kama Shekh.

“Jamaa si alimwambia hivyo kwasababu  alijua  muda na saa yoyote ataondoka , licha ya  huyu  mwanamke kuwa mrembo lakini bado Mchuku alimpenda mke mkubwa”

“Tino  wewe ndio huelewi , mchuku alimpenda huyu mwanamke lakini  alishindwana nae  kutokana na kutotulia , Mke mkubwa  alikuwa mvumilivu  na  mwepesi wa kusamehe”Aliongea mwingine lakini  Dastani ni kama hakuwa ameridhika hivi.

“Wadau kwani nini ilikuwa shida ya jamaa  mpaka kupatwa na umauti?”

“Bro wewe  ni mgeni?”Aliongea  kijana mwingine  na walionekana kuanza  kumchangakia  Dastani pengine  ni  kama wameona jamaa anaweza kuwapa fursa.

“Ni mgeni wa haya maeneo  lakini   Mchuku ni rafiki yangu wa kitambo , hatujawasiliana kwa muda mrefu na ndio nimesikia habari za kifo chake nikaona nihudhurie”Aliongea Kanali  na kuwafanya wale vijana kumwelewa.

“Jamaa alikuwa na Kansa ya mapafu  na alidondoka  ghafla tu  akiwa bar ndio ikawa hivyo”

“Ee bwana ee , sijujua  kumbe  jamaa alikuwa mgonjwa”Aliongea Kanali.

“Wengi hawakujua jamaa alikuwa mgonjwa , ila waliokuwa wakijua wakimkuta  sehemu za starehe jamaa anawaambia anatumia  siku zake  vizuri za mwisho mwisho maana akhera hakuna bia’

“Jamaa alikiona kifo chake aisee”

“Ndio hivyo bro, jamaa ni kama alijua , nasikia mchana  yake alienda kabisa na kumuaga mtoto wake  wa kwanza  shuleni”Aliongea mwingine huku zile kelele za mke wa pili hazikusikika kabisa.

“Alienda shuleni?”Aliuliza Kanali  huku machale yakianza kumcheza.

“Kwa maelezo ya  Abduli ndio alivyosema  baba yake alimtembelea mchana”

“Dogo atakuwa ameshikwa na huzuni sana , ana miaka mingapi?”

“Ni chalii mdogo kabisa  , umri wake sijui ila yupo pale St Joseph  Mbagala kidato cha pili , Mchuku alikuwa  akijisifia sana na  Abduli kwamba  ni  jiniasi na amerirhi akili zake”Aliongea

“Dastani palepale akili yake ilifanya kazi na  kwa haraka  aliruhusu  akili yake kutizama swala hilo  kwa  jicho la ujasusi.

“Mchuku alienda shuleni  kumtembelea Abduli mtoto wake tena  tarehe  kumi ya huu mwezi, lazima kuna sababu  ya kwenda kumtembelea  Abduli katikati ya mwezi ,  nitaanza na Abduli  lazima atanipeleka  lilipo faili  la sauti , lakini kwanza nijue  kama kuna sheria ya kuruhusu wazazi kutembelea watoto katikati ya mwezi”Aliwaza Kanali na muda ule alitoa simu yake akiingia mtandaoni, ilikikuwa ni muda wa chakula na  hata wale vijana  walimpotezea kabisa na umakini wao waliweka kwenye chakula.

Dastani hakutaka kuungana na  waombolezaji kwa ajili ya chakula na aliitafuta namba  ya Tresha   Noah na kuipiga huku akisogea pembeni nje ya maturubai.

“Huyu  malaya  kapotelea wapi au kasafiri na Mheshimiwa , Kama kampoteza Amosi  ataibeba kesi mwenyewe”Aliwaza Kanali huku aking’ata meno yake kwa hasira kwa kitendo cha  Tresha kumzimia simu tokea mara ya mwisho alivyowasiliana nae.

Wakai akiwa pembeni aliona kabisa hana chakufanya  lakini  hakutaka kuondoka mapema , aliona   atafute namna ya kusalimiana na mke  mkubwa wa Mchuku pengine anaweza kupata kitu  kingine cha ziada katoka  uchunguzi wake wa kusaka mahali Mchuku alipoficha  rekodi ya sauti.

****

Kapteni Norbert alikuwa  haelewi vijana wake wamekosea kosea vipi kushindwa kujua kama Hamza ametoka  na kwenda kuua  na kurudi bila ya wao kuweza kumuona kabisa wakati akitoka na kurudi.

Jambo  hili licha ya kwamba  liliwafanya kuona Hamza ni mtu hatari lakini vilevile waliingiwa na hofu  maana  kwa jinsi Kamera walivyozitega  ndani ya eneo lile ilikuwa ngumu kwa mtu  yoyote kuweza  kuepuka kamera hizo na kupita bila ya kunaswa , kubwa zaidi ni kwamba kijana wao  mtehama alikuwa ameweza kudukua Kamera zote zilizokuwa ndani ya  jumba la Regina.

Wakati akijua hali ni shwari na vijana wake kumwambia kuwa  jamaa alilala kumbe alikwisha kutoka na kusababisha mauaji na kuondoka kimya kimya  na  asubuhi  akiwa katikati ya kulifurahia tendo la ndoa  anaanza kufokewa na wakuu wake wa kazi kwa kutokuwa makini kupitia simu  kitu kilichomfanya kughailisha kumwagiliwa ua.

Licha ya kwamba Norbert aliona ni kosa kwa  vijana wake kutokumuona Hamza wakati akitoka lakini vilevile aliona ni kama wakuu zake wanamuonea  bure ,  maana ndio hao wakuu  wanaomchekea Mstaafu  akiendelea  kumchokoza  Hamza kupitia genge lake.

Hakupatwa na huzuni yoyote  ya  kifo cha Kanali mstaafu  Fanueli Yowe  wala Afande  Sucre , ukweli ni kwamba  alishaachaga kuwaheshimu tokea muda mrefu   japo  Afande Fanueli wakati akiwa mafunzoni ndio aliekuwa mkufunzi wake.

Norbert licha ya kwamba  alikuwa akitumikia  mfumo ambao ulikuwa umeharibiwa na watu wenye tamaa na siasa chafu lakini bado hakusahau wajibu wake kama  mwanajeshi , katika  jeshi  iwe ni la  polisi au ulinzi kazi yake kubwa ilikuwa ni kutii  maagizo lakini  licha ya hivyo hakuwahi kujichukulia kama mtumwa wa maagizo machafu ya wakubwa wake.

Wakati akitoka nyumbani kwake  akielekea kazini alikuwa  akimshukuru  Hamza  kwa namna moja ama nyingine kwa kufanya kazi ambayo ilipaswa mwanajeshi kama yeye ambae anapenda haki   kuifanya, lakini kwa jicho la usalama aliona  alichokifanya Hamza ni kosa na anapaswa kuadhibiwa.

“Muda mwingine tunahitaji  vichaa kama hawa kuendelea kutusafishia nchi”Aliwaza wakati  akiagana na mke wake.

Wakati akiwa njiani mkuu wake  alimwambia haina haja ya kufika kazini bali aelekee moja kwa moja  kwenda kumkamata  Hamza na apelekwe kituoni.

Hilo halikuwa tatizo kwake na aliitikia kwamba atafanya hivyo , lakini ilimshangaza wakati akiwa ndani ya viunga vya hospitali   pamoja na timu yake  wakimsubiria Hamza na Regina kufika hapo kumuona Mgonjwa ili amkamate anapokea  taarifa ya pili kutoka kwa mkuu wake.

“Achana nae”

“Mkuu  ni achane na nani?” Norbert aliuliza akiwa kwenye simu mara baada ya bosi wake kuwa na kauli moja tu ambayo ilikaa kiswahili sana.

“Nimekuambia achana nae , kipi huelewi  Norbert , rudi na watu wako kituoni  mara moja kuna kazi nyingi za kufanya”Upande wa pili  simu ilikatwa  na kumfanya  Kapteni Norbert kushangaazwa na kauli ile na muda uleule ni kama hakutaka  kuamini

kauli ya mkuu wake wa kazi na  alitoa simu yake  ya kawaida na kuitafuta namba.

“Umefanikiwa?”Sauti upande wa pili  ilisikika.

“Nimepokea maagizo mengine , Mkuu  anasema niachane nae”Aliongea.

“Kwanini!?”

“Sijajua ila nimepewa kauli  moja tu  na anaonekana kukasirika sana”

“Kukasirika ni lazima , Fanueli alikuwa  rafiki yake wa karibu  sana”

“Najuua lakini  Afande hili  ni swala  la kisheria  pia , kwanini niache kuondoka na mhalifu?”

“Norbert  nadhani unapaswa kumsikiliza mkuu wako wa kazi kwasasa , kama amekuambia achana nae lazima  ni  maagizo kutoka  juu, unatakiwa 

kutii ili kulinda uhusika wako mwingine, mimi pia  namuunga mkono”

“Lakini  Mkuu”

“Hakuna cha mkuu  Norbert fanya hivyo”

“Sawa Afande”

“Vizuri”Sauti upande wa pili ilisikika na  simu ilikatwa palepale, muda huo huo ndio Norbert aliweza kuiona Mercedenz Benz Maybach ikiingia hospitalini hapo  na aliweza kujua moja kwa moja lazima  ni bosi Regina maana ni Watanzania wachache wa kutembelea magari  ya bei ghali namna hio.

“Hata kama wakuu wanamuogopa siwezi kumuogopa, pengine bosi wake hata hajui  alichofanya  usiku”Alijiwazia Norbert huku akishika pingu zake na kuwapa ishara wenzake na kumsogelea Hamza na Regina , sio kwamba alikuwa akikiuka maagizo bali alitaka kumpiga mkwara Hamza  na pili kuhakikisha  Regina anajua kama  mtu anemwita msaidizi wake  ni muuaji.

Ukweli ni kwamba licha ya Norbert kuona  matukio kadhaa ya Hamza  akidhihirisha uwezo

wake lakini bado nafsi yake ilikuwa ikipinga kwanini  dogo  mzembe mzembe kama huyo anatikisa hadi watu wazito , kila akikumbuka mafunzo makali aliopitia jeshini  na kupewa nishani za kila aina kutokana na ukakamavu  wake alijikuta akipandwa na hasira  kumuona  Hamza mzembe mzembe ndio anaabudiwa, hali ya ujivuni  kwa kujilinganisha na Hamza ilimvaa.

“Mr Hamza upo chini ya ulinzi kwa  kosa la mauaji’Aliongea  kibabe akitaka kumfunga Hamza pingu lakini Hamza  hakuwa mzembe wa kukubali  mikono yake ifungwe pingu kizembe.

Regina ambae alishitushwa na   kauli ile ya Norbert alijikuta akirudi katika uhalisia , alikwisha  kumjua Norbert ni  polisi pamoja na wenzake licha ya kuvalia kiraia.

“Afande subirini  kwanza”Aliongea Regina huku uso wake ukizidi kuwa na usiriasi  na alimkinga Hamza kwa mbele.

“Madam  unazuia jeshi la polisi kufanya kazi yake”Aliongea Norbert huku  kwa  namna flani akionyesha heshima mbele ya  Regina , peingine uzuri wa mwanamke huyo ulimfanya  kukosa kujiamini  kiasi, pengine siku hio ndio mara yake ya kwanza kuona uso mzuri wa   Regina kwa ukaribu hivyo, kwenye maisha ya kiraia Regina alihesabika  kama mtu adimu kuonekana.

Ilikuwa  ni ngumu sana kumuona Regina kutokana na kwamba  akitoka kazini  maegesho ya magari yapo chini ya jengo  na  gari lake  lilikuwa na vioo visivyompa mtu nafasi kuona aliekuwa ndani.

“Kama wewe ni polisi   nadhani unajua ni kosa  kisheria  kutaka kumkamata mtu bila  kibali  , isitoshe  Hamza hawezi kuwa muuaji . bila Waranti hamuwezi kumkamata  na  hamuwezi kuongea nae chochote  pasipo ya kuwepo  mwanasheria wangu , hii imekuwa tabia yenu polisi kukiuka  haki ya uhuru  wa raia”

“Sheria hio hio inatuambia tunaweza kumkamata Muuaji bila ya  kibali , mbele ya  muuaji  kwanini  tujali uhuru wake”Aliongea Norbert huku hali ya kuanza kujiamini mbele ya mrembo Regina ikirudi upya.

Regina kabla ya kuendelea  kubishana na polisi alimgeukia kwanza Hamza na kumwangalia , ukweli ni kwamba  kutokana na  namna ambavyo Norbert alikuwa akijiamini  na vilevile  siri ambazo Hamza alikuwa akimficha alijikuta akipatwa na wasiwasi kidogo na kupoteza msimamo.

“Kamuua nani , kwanini mnasingizia watu  asubuhi asubuhi , mnadhani kuua  ni rahisi?”Aliongea

Regina na  Hamza  kauli ile ilimfanya  aone kama  Norbert ataendelea kuropoka basi itakuwa ni taarifa kubwa kwa Regina.

“Regina tangulia kamuone bibi kwanza , nitadili na  hii hali”Aliongea Hamza na kumfanya Regina kukunja mikono  yake na kumwangalia hamza kwa macho ya kikauzu.

“Wamesema  umemuaa mtu  ni kweli?”

“Sikia Regina  tangulia kwanza kwenda ndani , tutaongea vizuri baadae”

“Kwanini , kama hujaua  kuna haja gani ya kuongea na mimi baadae?”Aliongea Regina alikuwa na wasiwasi mno  na alitaka  Hamza aseme hajaua.

Ijapokuwa alimuona Hamza kama mtu ambae alikuwa na maisha yake kabla ya kukutana nae na historia yake kwa ujumla haijawa wazi lakini  kitendo cha  kuandikisha  ndoa yao ni kama  alijihisi  kutaka kuwajibika kwakile ambacho kinamzunguka Hamza.

Nafsi yake ni kama  ilikuwa ikimwambia hakuwa tayari kuwa karibu na mtu ambae ni  mbalifu tena sio mhalifu wa kawaida bali mhalifu wa makosa  ya kimauaji.

Upande wa Hamza  aliona yupo katika wakati mgumu , ukweli  ni kwamba  tokea afike nchini amekuwa akijitahidi  kujificha  ili asionekane  sio wa kawaida hata kujipa usumbufu na kuanza masomo ya chuo ambayo hayakuwa na  faida yoyote kwake zaidi ya kupoteza muda.

Alitaka kuwa na maisha ya kawaida kabla ya kukaribia  kupata kumjua mzee ni nani , historia yake ya maisha ilianzia Tanzania ndio maana alifika nchini  Tanzania lakini  kama mwenyewe alivyosema muda  ni fumbo,  saa na siku hio alikuwa kwenye mtego mwingine.

Hakuua makusudi  iwe amefanya kama mfanyakazi wa Regina au kama mtu wake wa karibu  yote juu ya yote hakutaka kuona mwanamke huyo akiendelea kukumbwa na hatari , alitaka kutoa onyo ambalo linaweza kueleweka kwa wale  wanaomuwinda, kama amekubali  kuandikisha cheti cha ndoa na  mwanamke huyo na bibi yake kulazimisha  swala hilo kufanikiwa basi  ilikuwa pia ni jukumu  lake kumalizia kila kitu na sio kufanya vitu nusu nusu , alikubali kuandikisha  cheti kwa ajili ya kumlinda  lakini hata kama  amefanikisha hilo bado kuna hatari nyingine ambazo ni yeye  ambae alipaswa kuzimaliza.

“Ndio nimemuua mtu jana”Aliongea Hamza huku muonekano wake ukitoka  katika hali ya uzembe  na sasa kuwa kama mtu mwingine ambae amekuwa mtu mzima ghafla , hata  Aura yake ilibadilika mara moja.

Jambo lile lilimfanya  Afande Norbert kushangaa  na kujiuliza inakuwaje mtu anaweza kubadilika kwa dakika chache namna hio , lakini kitendo  cha Hamza kukiri ilimfanya hasira kumvaa na kupata kibali cha kumkamata.

Upande wa Regina mara baada ya kusikia kauli hio ya Hamza alijikuta akipiga hatua kadhaa kurudi nyuma kana kwamba alikuwa ameona hatari mbele yake.

Kichwa chake ni kama hakikuwa kikifanya kazi vizuri na ghafla tu kilimsahaulisha na kuanza kujiuliza  Hamza ni nani.

Previoua Next