Frida alijua kabisa anakwenda kufa na kifo chake kuja kuwa utata , aliweza kuona kilichokuwa kimemkaba kooni ni kivuli lakini hakuweza kufanya chochote.
Kwa mtu wa kawaida unaweza useme Frida alikuwa amepatwa na ukichaa au ugonjwa wa ajabu lakini ukweli ni kwamba kuna nguvu iliokuwa ikimkaba kupitia kivuli.
Wakati akiwa amekata tamaa ghafla tu ule utulivu wa kile chumba ulitoweka , ilikuwa ni kama upepo umeongezeka kwa kiasi kikubwa na kufumba na kufumbua kivuli kile kilipotea na kumfanya Frida kuanza kukohoa kwa nguvu , mpaka anakuja kutulia alijikuta akishituka mara baada ya kugundua kuna mtu mwingine ndani ya chumba chake alievalia joho la rangi nyeusi, alitaka kupiga yowe lakini mtu yule alimpa ishara ya kutulia.
“Wewe ni nani?”Aliuliza Frida kwa sauti ya chini huku akiwa ameshika shingo yake , ilikuwa bado hakuamini kama alikuwa amepona.
“Msimamizi wako na mlinzi wako mpya”Aliongea kwa lugha ya kingereza na kumfanya Frida kuchangayikiwa.
“Sikuwa na msimamizi na mlinzi , kwanini unajitambulisha kama mlinzi wangu mpya , nataka kujua unatokea upande upi , Wiccan au Sinagogu?”Aliongea Frida kwa sauti kubwa kidogo.
“Mimi ni mu’ alkemi kutoka makao makuu ya Wiccan , nipo hapa kwa maagizo ya Madame, mlinzi wako wa zamani amepoteza maisha”Aliongea na kumfanya Frida kuzidi kuchanganyikiwa lakini mara baada ya kusikia mtu huyo yupo hapo kwa maagizo ya Madame alipata ahueni.
“Mlinzi wangu wa zamani , unamaanisha mlinzi gani?”
“Alietaka kukuua amemuua mlinzi wako , kwanzia sasa utakuwa chini ya ulinzi wa binadamu”Aliongea huku akisogea karibu na mlango.
“Nilikuwa na mlinzi kivuli!!?”
“Wewe ni wa muhimu sana kwa Madame kuwasiliana na waumini wa ulimwengu wa nje ya kivuli , kwa namna yoyote unapaswa kuwa salama”Aliongea.
“Kwanini alitaka kuniua?”Aliuliza Frida, alikuwa akijua mtu ambae alitaka kumuua ni kivuli au watu ambao wamepata umaarufu kwa jina la Night Shadows(Vivuli vya watu vinavyoonekana usiku).
“Sina majibu kuhusu swali lako lakini nina ujumbe kutoka makao makuu”Aliongea kama roboti.
“Ujumbe gani?”
“Hakikisha anatumia mshumaa kurekodi ndoto zake ndio utakuwa salama, kadri atakavyoota bila ndoto zake kurekodiwa mtiririko wa matukio utakosekana na mpango wote kuingia dosari”Aliongea.
“Unamaanisha Ha…”
“Sikutajiwa jina , huu ndio ujumbe kutoka makao makuu unaopaswa kufanyia kazi”Aliongea yule bwana. Frida alitaka kuuliza swali zaidi lakini alijua asingepata majibu.
Yule bwana alievalia joho la rangi nyeusi mara baada ya kuridhika kwa kuona Frida alikuwa ameelewa aliaga.
“Wakati wowote ukiwa katika hatari na kuhitaji msaada wangu tamka neno , Grishav nitaitikia wito wako”Aliongea na palepale bila ya Frida kujibu aliinama chini na kufumba na kufumbua alipotea.
Frida alijikuta akiingia katika maswali mengi na swali kubwa lilikuwa juu ya ule mshumaa , alijua maelekezo yale yalikuwa yakimlenga Hamza lakini alishangaa mara baada ya kuambiwa Hamza anapaswa kutumia mshumaa ule ili kurekodi ndoto zake.
Swali ambalo alijiuliza inakuwaje mshumaa ambao alipatiwa na Dokta Genesha kuwa na uwezo wa kurekodi ndoto , kitu ambacho Wiccan walitaka iwe hivyo , inamaana kuna mpango uliokuwa ukiendelea kati ya Dokta Genesha na Wiccan kiasi cha kumkabidhi Mshumaa wa Nuru kwa ajili ya kumpatia Hamza.
Frida alijiuliza ni kitu gani ambacho kinaendelea yeye hakijui na kwanini amenusurika katika kifo.
Alikumbuka kwamba asipofanikisha Hamza kutotumia mshumaa basi atakuwa hatarini lakini swali lingine liliibuka inamaana Hamza alikuwa akiota bila ya kutumia ule mshumaa.
Kitu ambacho Frida alikuwa akijua ni kwamba mshumaa ule ulikuwa ni kwa ajili ya kumletea Hamza ndoto tu ili kujua maisha yake ambayo ameyasahau , hayo ndio yalikuwa maelekezo kutoka kwa Dokta Genesha na hakuelezwa kwamba mshumaa ule ni kifaa cha kurekodi ndoto, alijiuliza kama ni hivyo kinarekodi vipi hizo ndoto , ni sayansi ya namna gani ambayo imetumika.
Alijikuta hata usingizi ukimpelea kabisa licha ya kwamba alijihisi uchomvu mkubwa , hofu ilimvaa na hisia zake zilimwambia pengine anachofanya sio kuhatarisha usalama wake tu bali anahatarisha na usalama wa Hamza.
“Sina jinsi kwasasa lazima nihakikishe Hamza anatumia mshumaa ili kuwa salama , wakati nikitafuta majibu ya maswali yangu yote. Lakini nitafanya nini kumfanya atumie mshumaa kama yeye mwenyewe haniamini vya kutosha mpaka kuutumia?”Aliwaza Frida.
******
Hamza mara baada ya Side na wenzake kuondoka alibakia na mrembo Dina , wote wawili hawakuwa na ile mudi ya kwenda floor za juu kwa ajili ya kulewa vileo na kufanya starehe zingine kama kucheza kamari.
Kitu pekee ambacho Dina alipenda ndani ya Club hio ni kutumia siraha kulenga shabaha na hata Hamza alikuwa akipenda kitu kama hiko , kwake hakuwa mpenzi sana wa vileo na kucheza disco.
Walitumia zaidi ya lisaa limoja na nusu kulenga shabaha kwa kutumia bunduki za aina mbalimbali.
Ilipotimia saa tano kasoro njaa zilikuwa zikiwauma na Hamza alipendekeza warudi Kijichi ndio wakapate chakula huko na Dina hakupiinga.
Mara baada ya kufika kijichi chakula kiliandaliwa na wote wakaanza kula pamoja.
“Unaonaje baada ya hapa ukaangalie maendeleo ya vijana wangu , tokea siku ile ulivyowafundisha kiasi namna ya kucheza Karate na Kung Fu hukuwaona tena”Aliongea Dina.
Hamza kipindi kabla ya kukutana na Regina alikuwa ameshawahi kuwafundisha vijana wa Dina mafunzo ya Karate na Kung Fu mara moja na hakuwahi kwenda tena kuwaona.
“Hakuna shida , kuna kitu pia nataka kwenda kukifanyia mazoezi”Aliongea Hamza.
“Kitu gani , ni kuvuna nishati za mbingu na ardhi au kitu kingine?”Aliuliza Dina kwa shauku alikuwa akijua Hamza ana mafunzo ya kuvuna nishati za nguvu ya asili ya ardhi na mbingu na alitamani kujifunza pia siku moja.
“Hutoelewa hata nikikuambia ni kama maneno ya kutamka nataka kuyafanyia majaribio”Aliongea Hamza.
Ukweli ni kwamba kitu ambacho alikuwa akienda kufanyia majaribio ni yale maneno ambayo
Yonesi alimtajia wakati akiwa hospitalini , siku ile wakati akifanya tahajudi kwa kupitia yale maneno aliona sura ya mwanamke ambae anamuona katika ndoto , bado shauku yake juu ya tukio lile haikuwa imeisha na alitaka kwenda kujaribu tena.
Baada ya kumaliza kula Hamza alitoka akiongozana na Dina pamoja na Lawrence na kwenda katika ukumbi maalumu ambao ni kama eneo la mafunzo ya kimapigano.
Hakukuwa na matumizi ya siraha , ilikuwa ni sehemu ambayo watu wa Dina walikuwa wakijifunza namna ya kupigana kwa kutumia mbinu mbalimbali za sanaa ya mapigano , eneo hilo lilikuwa likitambulika hata kwa serikali na lilikuwa na kibali kabisa.
Ni eneo ambalo lilijengwa katika mgawanyo wa sehemu mbili , sehemu ya kwanza ilikuwa ni kwa kufanyia mazoezi ya kawaida kama Gym na mazoezi ya boksa, Karate na Judo upande mwingine ulikuwa ni wa tahajudi.
Katika sanaa ya mapigano tahajudi ilikuwa ni sehemu ya mazoezi kwa ajili ya kuujua mwili wako ulivo, ukifanya tahajudi kama binadamu utajuwa wapi kuna udhaifu wako na wapi nguvu zako zinakaa kwa wingi na namna gani ya kushinda udhaifu wako.
Hamza mara baada ya kuona vijana wa Dina wakichukua mazoezi aliridhika , aliweza kuona wengi walikuwa wamepiga hatua kwa kufuata maelekezo yake.
“Bro , unapanga kufanya mazoezi ya namna gani , unataka kufanya tahajudi?”Aliuliza Lauwrence mara baada ya kumuona Hamza akichagua upande wa wanaofanya Tahajudi.
Dina na Lawrence siku zote walikuwa na shauku ya kutaka kumuona Hamza akichukua mazoezi hivyo walimwangalia.
“Kaa kimya Lau acha maswali mengi”Aliongea Dina akimzuia Lau kutokumsumbua Hamza na maswali yake.
Kutokana na wale wanafunzi kumuona Hamza na wao wote waliacha na kumpatia Hamza nafasi , kwao ni kama kuna kitu ambacho walitaka kujifunza kwa kumuangalia ndio maana walisimama pembeni.
Wakati Hamza akiwa katika mkao wa kufanya tahajudi huku midomo yake ikicheza ghafla tu watu wote walijikuta wakikumbwa na msisimko wa ajabu , ilikuwa ni kama kuna kiumbe cha ajabu kimefika ndani ya eneo hilo na kuwafanya kuanza kushindwa hata kupumua vizuri huku eneo ambalo Hamza alikuwa amekaa anga lake ni kama lilikuwa likitingishika.
Dina alijikuta jasho la paji la uso likimtoka huku akimwangalia Hamza kwa wasiwasi , alipatwa na hisia kama vile Hamza amekuwa mfalme ghafla na yeye ni kijakazi wake.
Upande wa Hamza hakuwa hata akielewa kilichokuwa kikiendelea kwa nje , kama alivyotarajia maneno yale yalikuwa ni kama anamwita yule mwanamke , mara ya kwanza wakati alivyofanya kule wodini alimuona kwa mbali yule mwanamke , lakini wakati huo kadri alivyokuwa akiimarisha umakini wake wa ubongo na kuzidi kuyatamka yale maneno alimuona ni kama vile yule mwanamke mchawi anaemuona kwenye ndoto alikuwa akimsogelea kutoka angani kwa spidi ya ajabu.
Zilipita kama dakika nne tu yule mwanamke aliweza kumuona kwa ukaribu zaidi, lakini jambo ambalo lilimshangaza Hamza ni kitu ambacho alikuwa ameshikilia mkononi.
Kadri alivyokuwa akizidi kuongea yale maneno mwanamke yule alizidi kusogea , lakini ilifikia hatua ni kama hawezi kumfanya asogee zaidi na yule mwanamke ni kama alijua Hamza hawezi kumuita karibu zaidi na alichokifanya ilikuwa ni kunyoosha kile kitu alichoshikilia mkononi mwake na Hamza mara baada ya kuangalia vizuri alijikuta akipagwa , ulikuwa ni ule mshumaa ambao Frida alimpatia akimwambia umetoka kwa Dokta Genesha, Mshumaa wa Nuru.
Hamza alichanganyikiwa mshumaa wa nuru kwanini upo katika mikono ya huyo mwanamke , katika ndoto yule mwanake alimuona kama mchawi ambae anachomwa moto baada ya kukamatika lakini kwanini akashika kitu cha nuru ilihali nuru na uchawi ni vitu viwili tofauti.
Yule mwanamke ni kama alikuwa akitaka Hamza amsogeze karibu aweze kushika ule mshumaa , upande wa Hamza alionekana kusita kuupokea ule mshumaa na yule mwanamke ni kama aliliona hilo na alitamka neno kwa kunyanyua mdomo wake kwa juu bila kutoa sauti akihakikisha Hamza anasoma lipsi zake.
NISAIDIE!(Help me)
Ndio neno ambalo aliongea huku akimpa ishara Hamza kupokea ule mshumaa.
Muda uleule Hamza aliacha kutamka yale maneno na kitendo kile kilifanya yule mwanamke ni kama vile kuna nguvu iliokuwa ikimvuta na kuzidi kurudishwa nyuma mbali na yeye , lakini bado hakuacha kumnyooshea ule mshumaa kama ishara ya kumuomba amsaidie.
Muda ileule wakati kila mtu akiwa ameloa jasho kana kwamba eneo lote limekumbwa na joto kali Hamza aliweza kufungua macho yake huku akionyesha hali ya kuwashangaa waliokuwa wakimwangalia .
“Nini kimetokea, Dina mbona upo hivyo?”Aliuliza Hamza mara baada ya kumuona
“Bado tu unapata muda wa kuuliza , ni kitu gani ulichokuwa ukifanya?”Aliuliza Dina na kumfanya Hamza sasa kuelewa kilichokuwa kikiendelea , licha ya yeye mwenyewe kuwa na wasiwasi lakini aliishia kucheka.
“I am sorry !, hii ni mara yangu ya kwanza kujaribisha hiki kitu , sikuweza kujizuia kile kinachonizunguka”AliongeaHamza na kisha alipiga hatua kuondoka katika eneo hilo.
Na wakati wakianza kutembea ndio sasa waligundua paa la jengo hili lilitingishika sana na kutokana na mchwa kula mbao unga unga ulidondoka chini kwenye tailizi na kila walipokuwa wakipiga hatua walikuwa wakiacha nyuma alama za miguu.
“Muda umeenda sana , nataka nirudi nyumbani”Aliongea Hamza.
“Hamza ni mafunzo gani yale , ni nguvu ya ndani au nishati ya mbingu na maji?”
“Ilianza mbingu ikaja ardhi halafu mbingu ikaleta maji na uhai , hizi ni kanuni za mafunzo ya nishati za mbingu na ardhi na ni kitu ninachoweza kufanya pia , lakini kuhusu nilichofanya sasa hivi hata sijui ni kitu gani , kama nilivyosema nipo kwenye utafiti”Aliongea Hamza
“Hata jina lake hujui?”Aliuliza Dina kwa mshangao.
“Ndio ila kwasasa nitaiita hii kama Wito, kwasababu ukiifanya ni kama kuna kitu unakiiita”
“Huwa haifurahishi kusikiliza pekee”Aliongea Dina kwa macho yaliojaa huzuni na shauku.
“Usiongee hivyo , hiki ni kitu ambacho siwezi kukuruhusu ufanye kabla sijakipatia majibu , nguvu yake ni kubwa kiasi kwamba ni kama sijakula kabisa”Aliongea Hamza huku akijihisi ni mwenye njaa kali.
Dina alimwambia twende ukale na Hamza hakuwa na aibu ya kukataa kwani alikuwa na njaa , muda huo hawakurudi kwenye mgahawa bali Hamza alienda mpaka yalipo makazi ya Dina mita kadhaa kutoka mgahawa wake ulipo na mfanyakazi aliagizwa kuandaa chakula na Hamza alikaa chini na kuanza kukifakamia huku Dina akimwangalia kwa macho yaliojaa mahaba.
“Unajua nilishangaa baada ya mstaafu Mgweno kunipigia simu akisema yaishe”Aliongea Dina. “Kwanini yeye ndio kakupigia simu?”,
“Unaweza kushangaa , licha ya kwamba kwa nje inaonekana familia ya Benjamini ndio inataka Regina kuolewa na James lakini upange mwingine ni mipango ya Mheshimiwa Mgweno”Aliongea Dina.
“Unataka kumaanisha nini?”
“Labda utakuwa hujui tu , ila kampuni ya Dosam ni kubwa Tanzania na inachangia zaidi ya asilimia tatu ya pato lote la Taifa , imeshikilia uchumi wa nchi katika maeneo nyeti, Benki namba moja ya kibiashara inayoongoza kwa Tanzania na Afrika mashariki yote ni Dosam Commercial Bank huu ni kama utawala wa mzunguko wa fedha nchini , hapa bado hujazungumzia usafiri wa anga , mahoteli na usambazaji wa bidhaa mbalimbali kwa matumizi ya majumbani, Kabla ya mheshimiwa Mgweno hajaingia madarakani Kampuni ya Zena ilikuwa ya kawaida tu kulinganisha na Dosam lakini baada ya Mgweno kuingia madarakani ilikua kwa spidi ya hali ya juu na yote hii ilikuwa ni uwekezaji mkubwa ambao mheshimiwa alifanya kwa kuiba hela za wananchi”Aliongea Dina.
“Kwahio unachomaanisha ni kwamba kampuni ya
Zena inamilikiwa na Mheshimiwa mstaafu Mgweno?”
“Ndio kwa asilimia zaidi ya arobaini na tisa, ukifuatilia wana hisa wa kampuni ya Zena utagundua wengi wanaomiliki hisa hizo ni kampuni kutoka nje ya nchi , ukifuatilia kampuni hizo nje ya nchi utagundua kwamba ni kampiuni ambazo zimepewa haki kisheria ya kumiliki hisa hizo na kampuni nyingine , mzunguko unaendelea hivyo hivyo, zote ni njama za Mgweno kuficha wananchi kwamba anaimiliki Zena , sio kampuni moja tu , kila kampuni kubwa ana ushawishi wa kimaamuzi”
“Zote hizo ni hela za rushwa!?”
“Ndio lakini hakuna ushahidi wa kuthibitisha kama ndio mmiliki, sehemu pekee ambapo amekosa umiliki na ushawishi ni kampiuni ya Dosam peke yake na hii ni kutokana na msimamo wa aliekuwa kuongozi wa kampuni yaani babu yake Regina”Aliongea Dina na sasa ni kama Hamza alikuwa akipata picha.
“Kwahio anajaribu kuitumia familia ya Benjamini
kwa ajili ya kuingiza ushawishi wake katika kampuni ya Dosam?”
“Ipo hivyo , mwanzoni walijua mambo yataenda sawa kama Regina atakubali kuolewa na James lakini mambo yamekuwa magumu , Regina karithi tabia zote za waanzilishi wa ile kampuni”
“Unamaanisha bibi yake na babu yake, unachoongea kinaonekana kuwa sahihi”Aliongea Hamza.
“Mgweno anachotaka ni kuimiliki Tanzania katika kila nyanja , kwanzia mtandao wa biashara haramu , biashara halali na kisiasa , hii itaifanya familia yake kuwa ya kifalme na raisi ni kama waziri mkuu tu anaepokea maagizo kutoka kwao”
“Kama ndio anachowaza anajidanganya , kuna mifano mingi ya kihistoria ni ngumu sana kuuchimba msingi wa nchi na kutengeneza nyufa pasipo kushitua wamiliki wake”
“Pengine anaelewa ila anaona ni kheri kujaribu kuliko kufa bila ya kujaribu”
“Kwahio baada ya kuona familia ya mzee Benjamini imekwama njia pekee alioona ni kumuua Regina maana urithi utaenda kwa mtoto wa pili?”
“Ndio lakini mipango yake inaonekana kukwama kutokana na uwepo wako , niseme tu umetibua mambo mengi sana , najua hata kunipigia simu ni kutokana na kujua ukaribu wetu na anatangeneza mazingira ya kujihami, lakini kwa wanaojua Mgweno kuna kitu lazima anapanga, walijaribu hadi mbinu ya kutaka kumtengeneza mtu wao ambae yupo karibu zaidi na Regina”Aliongea Dina na kumshangaza kidogo Hamza.
“Unamaanisha wale wazee ambao Regina amewafurumusha?”Aliuliza.
“Huo haukuwa mpango , wale wazee walikuwa wakifahamika tokea kipindi kirefu wapo kinyume na uongozi wa Regina”
“Ni nani ambae walikuwa wakimlenga?”
“Mchepuko wako alieniingiza kwenye matatizo”Aliongea huku akivuta midomo”
“Eliza!?”
Dina alitingisha mabega lakini kabla ya Hamza hajauliza swali lingine mlango wa kuingilai uligongwa kwa nguvu na Lawrence alionekana akiingia kwa pupa.
“Kuna nini Lawrence?”Aliuliza.
“Nimeletewa taarifa muda huu na vijana ,
Mheshimiwa Jongwe amefariki dunia kwa ajali ya gari na jeshi la polisi limeishikilia familia ya Mzee Seif kama washukiwa namba moja”Aliongea Lawrence na habari ile ilimtoa macho Dina. “Unamaanisha mgombea wa kiti cha uraisi kupitia chama tawala , Jongwe amefariki, tena kwa ajali , kwanini familia ya mzee Seif ihusishwe kama ni ajali?”Aliongea Dina.
“Inawezekana sio ajali ya kawaida”Aliongea Hamza.
“Kwa maelezo niliopatiwa gari ambayo alikuwa amepanda imelipuka na ndani yake alikuwa ameambatana na Mzee Martin”Aliongea Lawrence na alivyoongea ni kama alijua taarifa ile itamshitua bosi wake na ilikuwa kweli kwani Dina alijikuta akisimama akiwa kama haamini.
“Mzee Seif na Mzee Martini mbona kama ushawahi kunitajia hawa watu?”Aliuliza Hamza.
“Ndio Bro hawa ndio washirika wetu wakubwa, japo mara nyingi inaaminika Mzee Seif ana uadui wa kisiasa na Mzee Martini”Aliongea Lawrence.
“Kwanini inaaminika hivyo ?”
“Kwasababu wote ni wanasiasa wa vyama tofauti ,
Mzee Seif ni kutokea chama cha upinzani na
Martini ni kutoka chama tawala na wamekuwa wakipishana kama wabunge katika jimbo moja kwa zamu , uchaguzi huu akishika mzee Martini mwaka mwingine anashika Mzee Seif , awamu hii inayoisha Mzee Seif anamaliza muda wake lakini uelekeo wa kura upo upande wa Mzee Martini ,
siasa zao mara nyingi ni za kurushiana maneno”Aliongea Lawrence.
“Kwahio jeshi limemkamata Mzee Seif kwa kuamini kwamba ametegesha bomu katika gari la Mzee Martini ili ashinde uchaguzi , kama ni hivyo mgombea wa uraisi wa chama tawala kwanini amekufa pamoja na Martini?”Aliuliza Hamza lakini ni kama alikuwa akiipata picha.
“Lazima kuna kitu Mgweno anajaribu kufanya , hizi zote ni hila za kutaka kubomoa mtandao wa Chatu”Aliongea Dina kwa hasira.
“Lakini Madam Mheshimiwa Jongwe ni mgombea ambae amepata sapoti kubwa kutoka kwa mheshimiwa Mgweno , kwanini afanye hila ya kumuua mgombea ilihali zimebakia wiki chache kabla ya wananchi kupiga kura”
“Kesho kutwa pia ndio ilitarajiwa mkutano wa mwisho wa chama tawala kufanyika ili kufunga kampeni”Aliendelea kuongea Lawrence.
“Kuna picha inanijia akilini”Aliongea Hamza lakini upande wa Dina alionekana kuwa katika majonzi ya kumpoteza Mzee Martini, alikuwa ni moja ya mhimili wa mtandao wake.
“Lawrence polisi wanamshikilia kituo gani Mzee Seif?”
“Nasikia hawajamkamata bali wameizingira nyumba yake huko Kigamboni Mbutu B”Aliongea Lawrence.
“Yaani baada ya dakika kadhaa mlipuko kutokea na kuua watu, tayari washafikia maamuzi Mzee Seif ndio muhusika , mbona haingii akilini , hii lazima ni njama ya kutaka sisi twende tukamsaidie”Aliongea Dina.
“Tena nina uhakika hata hao wanaoitwa polisi ni feki”Aliongea Hamza huku akiweka kijiko chini.
“Madam tunapaswa kufanya nini?”Aliuliza Lau. “Kama ninachofikiria ni sahihi lazima hili linahusiana na kikao nilichofanya na mheshimiwa Mgweno siku kadhaa zilizopita , mtandao wetu wote unajua ni kwa namna gani Mzee Seif alikuwa mwaminifu , nisipoingilia na kulifanyia hili maamuzi unadhani nitaonekanaje , Lawrence kusanya vijana wote ambao hawako mbali tutaenda kuangalai kinachoendelea”Aliongea Dina.
“Lakini Madam ulitoa maelekezo ya vijana karibia wote wakae chimbo , waliopo karibu na mjini hawazidi hata hamsini?”
“Haina haja”Aliongea Hamza huku akisimama.
“Watu hamsini ni wengi sana na hili linaweza kuwa ni mtego , hebu ita wale kumi kutoka jumba la mazoezi waje hapa , wanatosha sana” “Bro unataka na wewe…”
“Hamza na wewe unataka kwenda?”
“Nataka nikajionee kinachoendelea , kama kweli huu mpango kaupanga Mgweno basi atakuwa katumia akili , unadhani kwa katiba yao ya chama nini kinafuata mara baada ya mgombea mkuu wa chama kufariki ghafla?”Aliuliza Hamza.
Comments