SEHEMU YA 62.
Kitendo cha Hamza kuonyesha kuishangaa ile picha kama vile mtu huyo anamfahamu ilimpa na Dina shauku ya kutaka kujua ni nani, baada ya kuangalia na kuona ni mwanaume wa kizungu aliekuwa amevalia mavazi ya kifungwa huku akiwa na kipara alimwangalia Hamza.
“Unamjua huyu ni nani?”Aliuliza Dina.
“Naweza kusema ndio namfahamu , lakini hata nikuelezee ni nani huwezi mfahamu, kinachonishangaza sio kwamba huyu ni nani bali ni kuitwa mfungwa wa muda mrefu”Aliongea Hamza.
“Unamaanisha nini?”Aliuliza Dina akiwa hajamuelewa Hamza kabisa.
“Unadhani kuwa mfungwa wa muda mrefu ni kama miaka mingapi hivi?”
“Inaweza kuwa miaka ishirini na zaidi”Aliongea Dina na kauli ile ilimfanya Hamza kutabasamu , lakini tabasamu lake lilikuwa na maana flani hivi.
“Kama hii sura ni ya mtu ninaemfahamu mimi basi huyu hajawahi kuwa mfungwa na kama ni kweli alikuwa mfungwa hapa Tanzania basi aliamua kulifanya Gereza makazi yake ya muda mrefu”Aliongea na kauli ile ilimfanya Dina kushangaa na kujiuliza kuna mfungwa wa aina hio , yaani wa kuweza kukaa ndani ya gereza kwa hiari yake.
“Kwa unavyoongea , kama kweli kahusika kumuua mgombea wa uraisi , unadhani jeshi la polisi litaweza kumkamata?”Aliuliza Dina.
“Kwa asilimia tisini nina uhakika hawatoweza kukamata hata kivuli chake”Aliongea Hamza na kumfanya Dina kumwangalia Hamza kwa shauku , alitamani kumjua huyo mtu ni nani lakini kwa muda huo alishindwa kuuliza hata kwa Lawrence hivyo hivyo.
Keita yeye hakuwa akijua kiswahili, hivyo hakuweza kusikia wanachozungumza ni kitu gani.
Hamza alionyesha kuridhika na ile picha na kisha alimrudishia yule bwana aliemkabidhi simu.
******
Upande wa Las Vegas Big alionekana kuwa na wasiwasi mno , zilikuwa zimepita dakika kumi na tano na kadri dakika zilivyokuwa zikiongezeka ndio jasho lilivyozidi kumtoka.
Mara baada ya simu yake kunguruma ikiashiria kuna ujumbe uliongia haraka haraka aliangalia na kukuta ni wa Keita.
“Bosi tumesamehewa…”Ndio ujumbe ulivyosomeka kwa liugha ya kingereza na kumfanya Big kupumua kwa nguvu ikionyesha amepata ahueni.
Ijapokuwa Keita alijiingiza mwenyewe katika anga za bosi wake lakini alikuwa akiomba asiuliwe , katika watu ambao amefanya nao kazi na waliomwingizia pesa ndefu na wenye ufanisi wa hali ya juu ni Keita, hivyo kama angekufa kwake ingekuwa hasara.
“Mr Mamen , huyo mwanaume kutoka Tanzania ni muhimu sana kiasi hicho , hii hoteli pamoja na Casino vyote ni vyako , kwanini unamuogopa sana?”Aliongea yule mwanamke wa kizungu , alikuwa ameshasikia mtu aliekuwa akiongea nae yupo Tanzania.
“Acha kuongea ujinga , huna unachokielewa”Aliongea Bonge kwa kufoka huku akimsukumia pembeni maana mudi ilikuwa ishapotea tayari.
“Hebu kwanza ondoka , sitaki huduma yako tena”Aliongea Big na mara baada ya yule mwanamke kusikia kauli hio kama nyoka alijikumbatisha katika mwili wa Big.
“Usifanye hivyo mpenzi , bado nina mbinu nyingi ambazo sijakuonyesha bado”
“Sitaki tena mbinu zako”Aliongea Big huku akinyoosha mkono wake kwenye kimeza na kuchukua sigara moja katika pakti na kuiwasha kisha kuanza kuvuta.
Yule kahaba wa kizungu aliona ni kama mpango wake wa kupata maokoto umevurugika na lawama zote alimpelekea Mtanzania aliekuwa akiongea na Big kwenye simu , isitoshe mpaka kupata nafasi ya kumhudumia Big alikuwa amefanya juhudi kubwa za kujilengesha.
“Haya yote ni kutokana na huyu Mtanzania , yeye ndio kaniharibia na kukufanya kukosa mudi ya kuendelea na mimi , Mr Mameni wewe ni mtu mzuri sana kwake lakini kwanini inaonekana hakujali kama rafiki , kama ni kweli anakuheshimu asingekutafuta muda mbovu kama huu”Aliongea akilalama
Kitendo cha kusikia kauli ile kutoka kwa huyo mwanamke , hasira zilimvaa Big palepale na alimkaba shingoni.
“Arghhhhhh..!”
Kahaba yule wa kizungu alijikuta akihangaika kujinasua kutoka kwa Mamen lakini hakutaka kumwachia.
“Wewe mwanamke mpumbavu sana , wewe ni nani mpaka kumsema vibaya bosi wangu”
“Mr Mameni nisamehe , sikujua unamheshimu kiasi hicho , naomba usiniue”Aliongea kwa kuomba lakini Mameni hakuwa na mpango wa kumwachia kabisa na alizidi kumkaba.
“Kumheshimu? , huyo mtu kwangu ndio imani”Aliongea akimaanisha Hamza kwake ndio imani yake na mara baada ya kauli ile alikaza mkono na kuizungusha shingo ya yule mwanamke na palepale alilegea.
Big hakuwa na hatia hata kidogo , baada ya kuona amekwisha kumuua yule mwanamke aliupiga mwili teke na kudondokea chini kwenye Zuria la kiajemi na kisha bila ya nguo alitoka kitandani na kwenda kusimama katika dirisha huku akivuta moshi mwingi wa sigara.
Katika macho yake alionekana kama mtu ambae ameingia katika kumbukumbu ya maisha yaliopita.
******
Hamza alimsamehe Keita na kumwambia aondoke Tanzania na watu wake mara moja na aachane na maswala ya madili ya siraha katika ardhi hii.
Keita alishukuru kusamehewa na kwa haraka sana aliongoza watu wake na kutoweka katika eneo hilo huku wakifuta ushahidi wote wa wao kuwepo nchini.
Kuhusu maswala yaliobakia alimwachia Dina adili nayo , kutokana yamekaa sana kisiasa na hakutaka kujiingiza huko.
Dina alitoa maelekezo ya Mzee Seif kupelekwa Safehouse kwa muda mpaka mambo yatulie na vijana wake walifanya kazi hio.
“Unapanga kufanya nini?”Aliuliza Hamza mara baada ya kungia kwenye gari , alitaka kujua ni hatua gani ambayo Dina atachukua kuhusu swala la kifo cha mgombea wa uraisi.
“Mpaka sasa nimeshindwa kuamini kama Eliasi ameenda mbali namna hii mpaka kumuua mgombea wa uraisi tena wa chama chake huku yeye akiwa mwenyekiti wa Chama, kuna kitu kinaniambia hili hajalitekeleza yeye peke yake , pengine kuna nguvu ilionyuma yake”
“Unamaanisha nguvu ambayo inataka kumpindua Mgweno?”Aliuliza Hamza.
“Ndio , Eliasi ninaemjua mimi sio jasiri kiasi hichi , ijapokuwa Mgweno amekuwa akiitawala hii nchi nyuma ya pazia lakini haimaanishi ana nguvu kila mahali, katika uongozi wake alikuwa na maadui zake pia na ndio namna ambavyo hata mtandao wetu wa Chatu uliweza kuendelea kuwepo licha ya kuupiga vita kwa kipindi kirefu akitaka kuumiliki”Aliongea Dina.
“Kwa ninavyoona kwasasa huu ni mpango ambao haujaisha bado , muuaji kakimbia na sidhani kama wanaweza kumpata tena , pili upande wa Keita mpango umevurugika kwa asilimia kadhaa , kama unavyosema ni sahihi basi nina uhakika pengine Keita alikuwa Plan B ya mpango mzima”Aliongea Hamza na kumfanya Dina kidogo kushangaa.
“Unataka kumaanisha nini?”
“Wewe hebu chukulia , kazi kubwa ya Keita ilikuwa nini katika huu mpango , ni kumtorosha muuaji lakini Keita amemkosa muuaji hii maana yake walikuwa wakiujua uwezo wa muuaji kujitorosha yeye mwenyewe”
“Vipi kitendo cha kutaka kunisingizia mimi kama muhusika?”Aliuliza Dina.
“Ni kukujulisha kinachoendelea kabla ya kukisikia kwenye taarifa ya habari , yule Pancho alikuwa chambo tu”Aliongea Hamza na kumfanya Dina kuanza kufikiri.
“Maana yake ni kwamba hata kama ningeenda mwenyewe ningeweza kuujua ukweli kutoka kwa Keita?”
“Nina uhakika huo licha ya kwamba ingekuwa ngumu, lakini kama ni kweli basi nguvu iliopo nyuma ya Eliasi inamtafutia udhaifu pia”Aliongea Hamza na upande wa Dina mara baada ya kuanza kufikiria kimantiki, ni kama sasa anaanza kuelewa pointi ambayo Hamza analenga.
“Babu aliweza kuulinda mtandao wa Chatu kwa kuushikilia udhaifu wa mheshimiwa Mgweno lakini hili lililotokea leo pia nimepata ushahidi wa Eliasi kupanga njama na kumuua mgombea wa kiti cha uraisi , hii maana yake Eliasi na Mgweno wote wapo kiganjani kwangu, kuhusu nani atarithi nafasi ya Jongwe lazima atakuwa upande wa Eliasi na kuna uwezekano pia amehusika katika huu mpango.Kama ni hivyo basi napata picha nani yupo nyuma ya Eliasi” Aliongea Dina kana kwamba anajaribu kuunganisha matukio na kumfanya Hamza kutabasamu.
“Naamini atakuwa yule raisi wa Rwanda”Aliongea Hamza huku akimshika Dina kiuno.
“Wewe umajuaje?”
“Babe si ushawahi kuniambia babu yako alifanikisha kumfunga mikono Mgweno kutokana na kumtengenezea udhaifu wa kashfa ya kuuza rasilimali za nchi nchini China kwa ajili ya kumuokoa mtoto wake na mpango ulisukwa na rafiki yake mkubwa raisi wa Rwanda”Aliongea Hamza na kumfanya Dina kuitikia kwa kichwa huku akimwangalia Hamza kwa macho malegevu.
“Huyu mzee anataka kuitawala Afrika mashariki nzima , naona anajaribu kumuweka raisi anaemtaka madarakani huku wakati mmoja akiizima nguvu ya Mgweno ambae ni adui yake mkubwa”Aliongea Dina.
“Mtu wa nje anaweza kuona ni kiongozi mwenye akili sana , lakini upande mwingine wa shilingi sababu ya kuwa na mipango mingi ni kutawala kwa muda mrefu na kuamini nchi ni yake na anajaribu kila namna kuiendeleza licha ya kuwa na rasilimali chache”Aliongea Hamza huku akitabasamu na Dina alitingisha kichwa kukubaliana nae.
“Mbona huniulizi swali lolote licha ya sura yako kuoneysha ina maswali mengi?”Aliongea Hamza mara baada ya kuona Dina alikuwa akimwangalia sana.
“Ndio nina maswali mengi kwa kilichotokea leo lakini kwasasa naona ngoja lipite”
“Ukiuliza nitakuambia kila kitu”Aliongea Hamza.
Ukweli aliona Dina sio Regina anaweza kumweleza kila kitu na wala asipate mabadiliko zaidi ya ushangaa tu.
“Kwasasa sitaki kujua vitu vingi , nahisi bado sina vigezo , siku za baadae nikijihisi kustahili kukujua nitakuuliza, sitaki kujua sasa hivi inaweza kunifanya niwe na mawazo kwa kuona tuna gepu kubwa kati yetu”Aliongea Dina na kumfanya Hamza kutabasamu , hakudhani Dina angekuwa na mawazo ya namna hio.
Mpango wa Dina ilikuwa ni kujiimarisha zaidi uwezo wake binafsi , alikuwa akijua kuna mbinu nyingi za kuwa na uwezo mkubwa ikiwemo mbinu za kujifunza kanuni za mbingu na ardhi , kuamsha nguvu ya ndani, uchawi na mengineyo.
Hamza alikwua ni mtu ambae anaamini ana mafunzo ya nishati za mbingu na ardhi na alitaka ajifunze kutoka kwake na kufikia hatua ambayo atajiona yupo tayari kumjua Hamza.
Kutokana na muda ulikuwa umeenda Hamza hakupanga kurudi nyumbani , ukweli ni kwamba angetaka kurudi ingekuwa rahisi tu maana alikuwa karibu na mji wa kisasa wa Egret lakini aliamua kurudi Kijichi na mrembo Dina.
Mara baada ya kufika nyumbani hakukuwa na chakufanya zaidi ya kwenda kulala , kulikuwa na vyumba vingi vya wageni ndani ya jumba la mrembo huyo lakini Dina alilazimisha walale pamoja.
Hamza licha ya kukubali alijitahidi asimfanye chochote mwanamke huyo, baada ya Dina kuuliza maswali kibao kuhusu namna ya kuwa bora katika eneo la mapigano na kujua nguvu iliojificha katika mwili wake hatimae alipotelea usingizini , lakini upande wa Hamza kama mwanaume rijali ilikuwa ngumu kwake kulala , alijikuta akikaa macho mpaka kunakucha.
*****
Wakati ikiwa ni siku nzuri kwa watu wengine upande mwingine haikuwa siku nzuri kabisa kwa mheshimiwa mstaafu Mgweno.
Taarifa ya kifo cha mheshimiwa Jongwe aliweza kuzisikia usiku wa manane saa saba na tokea apate taarifa hizo hakuweza kupata usingizi kabisa , kwanza anaanza vipi kupata huo usingizi , kitendo cha kuuwawa na bomu kwa Jongwe tena akiwa ndani ya gari ilimaanisha kuna mtu anataka kumpindua ki nguvu ndani ya Tanzania , jambo ambalo hakuwa tayari kuona likitimia, lakini hata hivyo kama ilikuwa kweli aliona wanaotaka kumpindua walikuwa wamepiga hatua.
Usiku mzima kwa kuambizana na msaidizi wake Jonathani Machete walipanga kila aina ya mpango wa kurudisha hali hio katika mstari wake. Hata mtoto wake ambae alikuwa kwenye siasa akifuata nyayo zake alimpigia simu kumweleza kile kinachoendelea.
“Baba tunafanyaje juu ya hili swala?”Kijana huyo aliuliza kwa wasiwasi mkubwa , nafasi yake ya Uwaziri mkuu alikuwa akiona ikienda na maji.
Kitu ambacho Mgweno alikosea ni kukubaliana na Eliasi Mbilu kwamba kutokana na yeye kuweka mtu ambae ni chaguo lake kuwania kiti cha uraisi basi Mbilu yeye ataweka makamu wa raisi ambae ni chaguo lake , sasa wakati huo alipokaa chini na kufikiria aliona kabisa alijipiga risasi mguuni , ilionekana Mbilu tokea muda mrefu alikuwa na mipango ya kumuweka raisi anaemtaka madarakani kwa namna yoyote ile.
“Bakari wahi nyumbani asubuhi , kwasasa sina cha kukuambia”Aliongea Mheshimiwa.
“Sawa baba, nitapanda ndege binafsi kufika asubuhi na mapema”Aliongea Bakari Mgweno , alikuwa nyumbani kwao mkoani ambako ndio jimbo analogombea lilipo , kama angetaka kuwa Waziri Mlkuu ilimpasa kushinda kwanza ubunge.
Mheshimiwa usiku huo mara baada ya kukata simu alimgeukia Jona Machete ambae alikuwa bize.
“Vipi Machete umefanikiwa kuwasiliana nao wote”
“Ndio mheshimiwa nimetoa taarifa na wote asubuhi watakuwepo kwenye kikao”Aliongea Machete na kumfanya Mheshimiwa kukaa kwenye sofa huku akionekana kuwaza , bado hakuonekana kuridhika licha ya hatua ya kwanza kuichukua.
“Kabla ya asubuhi kuingia wasiliana na meneja wa Benki wa Sychelles napaswa kujiandaa kwa lolote”Aliongea Mheshimiwa.
“Sawa Mheshimiwa”
Mgweno kuna kila hisia mbaya ambayo ilikuwa ikimtawala, alijua fika Eliasi alikuwa akihusika katika hili lakini ushahidi wa moja kwa moja hakuwa nao.
“Mheshimiwa, Bi Zalha anasema ameshindwa kuunganisha mawasiliano na mheshimiwa Eliasi”Aliongea Jona akipokea simu kutoka kwa Zalha katibu wake ndani ya ofisi ya mheshimiwa mstaafu Oysterbay.
“Ametoa sababu ,inawezekana vipi raisi wa nchi kutopatikana hewani”
“Wanasema mheshimiwa kapata dharula ya kiafya, yupo chumba cha uangalizi katika hospitali ya Rufaa ya Gleneagles nchini Malaysia”Aliongea Jona na kumfanya Mgweno kutoa tabasamu la kifedhuli.
“Eliasi ana maigizo sana , ila hajui kwamba mimi ni mtoto wa mjini na ndio nilimwingiza Ikulu”Aliongea huku aking’ata meno kwa hasira na Jona aliishia kukaa kimya.
“Wasiliana na IGP nahitaji taarifa kutoka kwake sasa hivi juu ya mshukiwa wa mauaji”Aliongea na Jona dakika ileile alifanya mawasiliano na mara baada ya simu kupokeleiwa alifowadi kwenda kwa simu ya mheshimiwa
“IGP yupo hewani mheshimiwa”Aliongea na Mgweno alitoa simu yake na kupokea haraka haraka na kuweka sikioni.
“Mheshimiwa nadhani tumewasiliana dakika ishirini zilizopita”Sauti upande wapili iliongea.
“Sanga tumekubaliana kila baada ya dakika kumi unanipa ripoti , dakika ishirini zimepita naona kimya”Aliongea.
“Mheshimiwa hakuna ripoti ya kukupatia mpaka sasa , vijana wapo eneo la tukio , maiti ya mheshimiwa Jongwe na Mzee Martini pamoja na dereva zimefikishwa hospitalini kwa ajili ya kuhifadhiwa”
“Nataka ripoti Afande , kwanini Jongwe alikuwa kwenye gari la Martini tena usiku akiwa hana ulinzi wa kutosha?”
“Msaidizi wake namba mbili hakuwa na taarifa ya mheshimiwa kutoka , kuhusu msaidizi wake namba moja mpaka sasa hatujapata taarifa zake, hakuwepo kwenye ajali ya gari lakini pia nyumbani kwake hayupo”Aliongea IGP akiwa mpole lakini upande wa Mgweno aliishia kung’ata meno yake kwa hasira.
Katika taarifa ya tukio hili ilisemekana Mheshimiwa Jongwe alikuwa nyumbani kwa mzee Martini na wakati wa kuondoka alitoka na Martini na ndipo gari yao ilipolipuka mara baada ya kusafiiri kwa umbali wa kilomita nne kutoka nyumbani kwa Martini, swali lilikuwa moja , licha ya kwamba inafahamika Martini na Jongwe ni marafiki lakini ilikuwaje Jongwe akatoka nyumbani kwake bila ya wasaidizi wake kujua na akaenda kwa Mzee Martini.
Mheshimiwa alijiuliza maswali mengi lakini aliamua kufuata ule msemo wa ‘The dead have no tales to tell’ yaani mfu hana stori tena ya kusimulia.
Sasa akiwa ameshapanga mikakati ya kuchukua , hatimae asubuhi ikaingia akiwa hajalala kabisa na muda huo alikuwa akisubiria viongozi waliokuwa upande wake ndani ya chama kufika nyumbani kwake kwa ajili ya kikao cha siri na cha dharula kabla ya kifo cha Jongwe kutangazwa,alikuwa amezuia kifo hicho kisitangazwe kabla ya muafaka wa kuamua nani aingie Ikulu.
Saa mbili kamili ilikuwa ndio muda wa kikao lakini ajabu mpaka inafika saa mbili na nusu viongozi waliofika kwa ajili ya kikao walikuwa saba tu tena watatu kati yao wakiwa sio wale wenye vyeo vikubwa kwenye Chama.
“Jona mbona hawajafika mpaka muda huu , una uhakika ulifanya mawasiliano nao?”
“Ndio mheshimiwa na niliwapa muda sahihi wa kikao ni saa mbili kamili”Aliongea Jona na kumfanya mheshimiwa kuanza kuzunguka chumba kama vile amekuwa kichaa.
“Kuna jambo halipo sawa, hebu ongea na vijana wafuatilie sasa hivi unipe majibu”
“Mheshimiwa pengine wamechelewa tu , kwanini tusiwape muda angalau nusu saa?”
“Jona mimi sio mjinga kukuambia ongea na vijana wafuatilie , umeanza lini kwenda kinyume na ninachoagiza?”Alifoka mstaafu.
“Nitawasiliana na vijana mara moja mheshimiwa”Aliongea Jona na kutoka katika sebuleni na muda huo alipishana na mke wa Mstaafu akingia akiwa amebeba Trey.
“Mgweno punguza wasiwasi , hebu kunywa chochote kwanza ndio mengine yafuate”
“Mama Bakari unadhani kwa kinachoendelea nina muda wa kuweka kitu mdomoni?”Aliongea akiwa kakereka na kumfanya Mama Rahma kuweka ile Tray kwenye meza na kuanza kuandaa.
“Mume wangu hivi sio namna nilivyokuzoea, tumekuwa pamoja kwa muda mrefu na tumepitia makubwa kuliko hili na kipindi chote hicho hukuwahi kupoteza utulivu wako , wewe mwenyewe unamwambia Bakari kila siku hatua ya kwanza ya kutatua tatizo ni kujipa utulivu lakini naona unaenda kinyume na maneno yako”Aliongea na muda ule ni kama amekumbushwa kuhusu Bakari.
“Kuhusu Bakari mpaka sasa hivi hajafika tu?”Aliuliza
“Baba nipo hapa , hebu kwanza angalia taarifa ya habari”Sauti ya mtu kuingia ndani ya sebule hio mkuku mkuku ilisikika.
“Bakari kuna nini?”Aliongea mama yake lakini Bakari alikuwa mwepesi mno kuikimbilia rimoti ya TV na kuweka taarifa ya habari.
Kitendo cha Mstaafu Mgweno kuona ile habari alijikuta vigoti vya miguu vikilegea , ilikuwa ni habari ya kifo cha Jongwe mgombea wa Chama, licha ya kwamba Mgweno hakuruhusu taarifa hizo kutolewa kilichomlegeza ni sababu ya kifo cha Jongwe.
Kulingana na uchunguzi wa jeshi la polisi wanasema ni kweli mheshimiwa Jongwe amefariki na wamethibitisha mhusika mkuu ni Yohana Kamote msaidizi namba mmoja wa mheshimiwa Jongwe, polisi wanasema wamemkuta Kamote hotelini akiwa amejinyonga na kuacha wosia , akisema kwamba mheshimiwa Jongwe alimuiba mpenzi wake Janeth yaani mke wa Mheshimiwa Jongwe , Kamote anadai alikuwa kwenye mapenzi na Janeth kabla ya kuolewa na Jongwe na mapenzi yao yaliendelea hata wakati Janeth akiwa ameolewa tayari na wamezaa mtoto mmoja ambae anafahamika ni wa Jongwe , Kamote anasema Janeth alianza kubadiika baada ya mume wake kupewa dhamana ya kupeperusha bendera ya Chama na kutokana na wivu ameamua kumuua Jongwe na kujiua yeye mwenyewe kumkomoa Janeth, Polisi wanasema Janeth ameshikiliwa na jeshi la polisi kwa ajili ya mahojiano kuthibitisha kama kuna ukweli juu ya maneno ya Marehemu Kamote.
Mstaafu Mgweno alijikuta akinyong’onyea , upande wa Mama Rahma pia hata ile mudi ya kumlazimisha mume wake kunywa chai haikuwepo kabisa.
“Jamani mama Lebroni nili…!!”
Mke wa Mstaafu alijikuta akiropoka na kumfanya Bakari na mume wake kumwangalia kwa macho yaliojaa maswali.
“Mama unajua nini?”Aliuliza Bakari na Mama Rahma alianza kumwangalia mume wake kwa wasiwasi.
“Mama Bakari unajua nini , mbona huongei unaniangalia , usiniambie kinachosemwa na Polisi ni cha kweli?”
“Mume wangu naomba unisamehe sikukuambia kuhusu hili maana sikuwahi kuona ni muhimu , ni kweli nimejua muda mrefu Janeth alikuwa akitembea na Marehemu …”Alijikuta akishindwa kuendelea kuongea na kuanza kulia.
Mgweno alitamani kumvamia mke wake kumdunda lakini Bakari alionekana kuwa makini na baba yake kumsogelea mama yake , sio kwamba alikuwa akimtetea mama yake , lakini baba yake alikuwa na tabia ya kumpiga mama yake na hakuwa akipenda.
Mgweno hakutaka kusikiliza neno lingine na alitoka ndani ya sebule hio na kuelekea moja kwa moja kwenye ukumbi wa mikutano lakini mara baada ya kuona hakuna ambae ameongezeka alijikuta hofu ikimwingia.
“Mheshimiwa kuna ujumbe wako”Sauti ya Jonna ilisikika na kumfanya mstaafu na wale waliokuwa ndani ya ukumbi kumwangalia Jona kwa shauku.
“Taarifa imefika ofisini kwako asubuhi hii , unahitajika kwenye kikao cha dharula cha Halmashauri kuu ya Chama , saa tatu kamili ndio kinaanza ukumbi wa makao makuu”Aliongea Jonna.
“Kikao saa tatu kamili taarifa naeletewa saa mbili na nusu , Jona nini kinaendelea?”
“Mheshimiwa hata mimi nimeshangaa ila ni Zalha ndio kafikisha hii taarifa”Aliongea Jonna na mheshimiwa alimwangalia msaidizi wake kwa udadisi na hakuongea neno alihisi harufu kubwa ya usaliti kwa vijana wake aliowaamini.
“Ahirisha hiki kikao , tunaelekea makao makuu”Aliongea Mgweno huku akitoka ndani ya eneo hilo kwa pupa.
Kuna jambo alikuwa akiliwaza katika akili yake lakini hakutaka kulipa kipaumbele kwa wakati huo , alitaka kuwahi kwanza maana kama akichelewa na maamuzi yakifanyika hata kama ana ushawishi mkubwa hatokuwa na uwezo wa kupinga maamuzi ya watu wengi.
*****
Hamza asubuhi na mapema alikuwa ashaondoka nyumbani kwa Dina.
Siku hio mpango wake ni kwenda kazini na kisha akutane na Eliza amweleze kuhusu ndoa feki aliofunga na Regina.
Hamza hakutaka kabisa kumkosa Eliza lakini aliona sio vizuri pia kumdanganya.
Baada ya kufika ndani ya kampuni alikuwa amewahi sana na hata Eliza hakuwa amefika bado , hivyo hakuwa na chaguzi zaidi ya kwenda ofisini kwake na kuangalia kazi ambazo anapaswa kufanya.
Na mara baada ya kufika tu Linda alionekana kumtafuta na alimwangalia Hamza kwa ukauzu mkubwa.
“Umekuwaje wewe , unasiku ngapi hujaripoti kazini na kwanini unachelewa , yaani bosi kafika wewe ndio unaingia kazini?”Aliuliza Linda kana kwamba yeye ndio bosi.
Hamza alitaka kumwambia mwanamke huyo yeye ni nani wa kumpandishia ilihali amemuoa bosi wake ila alijizuia.
“Nilikuwa na maswala binafsi ndio maana?”
“Hii ni tabia gani unayojaribu kuonyesha, maswala binafsi ni ya kwako na hayapaswi kuingiliana na maswala yako ya kazi , usijione kwasababu unajua watu maarufu ndio unaweza kufanya chochote kile unachotaka”Hamza alifokewa na alijifanyisha mzembe kama kawaida na kutingisha kichwa lakini upande wa Linda ni kama hajaridhika aliishia kuchukia mara baada ya kuona hakuna dalili ya woga kabisa kutoka kwa Hamza.
Alikuwa na kila haki ya kukasirika, wote na Hamza walikuwa nafasi sawa lakini yeye muda wote alikuwa bize kuhakikisha ratiba za bosi wake zinaenda sawa , sasa Hamza ambae wapo nafasi sawa anafanya anachotaka , aliishia kumwangalia Hamza kwa macho mabaya na kisha aligeukia ofisi ya bosi wake na kwenda ndani.
Regina muda huo alikuwa ameshafika kazini tayari na aliwahi kwani alikuwa na viporo vingi vya kufanyia kazi.
Hata pale jana aliporudi na kutokumkuta Hamza nyumbani wala hakujali kabisa na kila alipohisi kupandwa na hasira alijiambia cheti chao cha ndoa ni kwa ajili ya kupata hisa za bibi yake tu na hakuna kingine.
“Bosi…”Aliita Linda kwa unyenyekevu mara baada ya kuingia katika ofisi ya Regina na aliongea mara baada ya Regina kumwangalia.
“Kuna tatizo nataka kukushirikisha”
“Tatizo gani?”Aliongea Regina huku akirudisha macho yake kwenye karatasi aliokuwa akiangalia.
“Ni kuhusu Hamza”Aliongea Linda na kauli yake ilimfanya Regina mikono yake kutetemeka kidogo na kisha alimwangalia Linda kwa shauku.
“Nini kimemtokea?”
“Anaonyesha tabia ambayo si nzuri kazini , kwanzia siku ziliozopita anafika kazini kwa kuchelewa na siku zingine haonekani kabisa na hakuna taarifa , tukimuacha akiendelea kama hivi ni taswira mbaya kwa kampuni”
“Unaona tumfanye nini sasa?”Aliuliza Regina lakini Linda kidogo alishangaa maana ni mara chache sana kwa Regina kuuliza swali kama hilo , ki ufupi alikuwa na majibu kwa kila kitu.
“Naona ni vizuri tukimfukuza tu”
“Hapana”Aliongea Regina haraka na kumfanya Linda kuinamisha kichwa chake chini kwa kusikitika
“Bosi ni kwasababu anafahamiana na Master Alec?”
“Hapana , ni kwasababu hawezi kuachishwa kazi”
“Lakini…”
“Unaonaje tukifanya hivi .. muandalie kazi ambazo zinahitaji muda na nguvu , wewe mpe kazi hakikisha muda wote ana kitu cha kufanya”Aliongea Regina na Linda alikubali na kutoka ofisini.
Linda akiwa kwenye ofisi yake alikuwa ashaona ni kazi gani ambayo anapaswa kumpatia Hamza, kulikuwa na kesi mbalimbali ambazo zimetoka kwenye kampuni tanzu na moja ya kesi iliokuwepo ni kutoka idara ya Sales and Business development , walikuwa wakitoa taarifa juu ya kampuni ya Dede kutoka Bagamoyo wamepitiliza siku za kulipa pesa wanaozodaiwa na walijaribu kufanya mawasiliano na kampuni hio lakini wametoa taarifa kwamba watalipa kwa Cash na anaepaswa kufuata hayo malipo ni Eliza meneja wa idara ya mauzo.
Kipindi ambacho kampuni ya Dede inaingia katika tenda ya kibiashara na Dosam dili hilo lilisimamiwa na meneja wa idara ya mauzo yaani Eliza, lakini kutokana na Dede kukosa kiasi chote cha pesa waliomba kufanikishiwa tenda yao na watalipa kiasi kilichobakia katika muda wa miezi mitatu na Eliza aliweza kuidhinisha.
Ilikuwa ni ngumu kuona kampuni inamuwekewa masharti mtu ambae amemkopesha , hii ni kwasababu ya nguvu ya kampuni hio ya Dede , ndio kampuni ilioaminika kuongoza kwa utapeli , ilikuwa kampuni ambayo inamilikiwa na Mmasai na huyo mmasai alikuwa akiaminisha wamasai wenzake kwamba hio ni kampuni ya kabila lao.
Sasa ilishangaza wamiliki wa kampuni hio kumtaka Eliza ndio akachukue malipo , ilionekana ni kama kuna mtego, sasa mara baada ya Linda kukumbuka Hamza anajua mbinu kadhaa za mapigano aliiona ni kazi ambayo inamfaa sana.
“Linda kuna kazi ninayopaswa kufanya?”Aliuliza Hamza mara baada ya kumuona Linda akiingia ofisini kwake.
“Ndio ila sio kutafsiri kama ulivyozoea , leo kuna kazi nyingine nje ya ofisi, kuna malipo yetu ya mwisho ya mwisho ya mauzo na tunaowadai wanataka twende tukachukue Cash”
“Kwanini mimi nikamilishe hayo malipo , hii ni kazi ambayo inapaswa kufanya na idara ya mikopo , ya fedha au mauzo kwanini niwe mimi?”Aliuliza Hamza.
“Upo sahihi lakini kampuni tunayoidai kidogo ina upekee wake , hivyo tusipomtuma mtu ambae sio makini anaweza kupata matatizo, umeonyesha una uwezo wa kupigana , hivyo utaenda kama bodigadi kuhakikisha Meneja Eliza hapati shida”Aliongea Linda.
“Ni kampuni gani?”Aliuliza Hamza maana baada ya kusikia ataenda na Eliza kidogo aliingiwa na utayari wa kwenda lakini alitaka kujua ni kampuni gani kwanza.
“Inaitwa Dede Entertainment”Aliongea na kumfanya Hamza kuona huyu Linda ni kama anamtafutia matatizo, Hamza aliwahi kusikia kuhusu hio kampuni mtandaoni lakini hakuwahi kuingia , kulikuwa na taarifa za malalamishi kibao kwenye mitandao zikiilalamikia serikali kuhusu watu wengi kupotea ndani ya kampiuni hio na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa.
“Hili swala wameweka masharti watalipa Cash tunataka kuona kama kweli wanayonia ya kulipa na kama hawana tuchukue hatua za kisheria kuwadai , lakini kama tukiwashitaki itachukua muda mwingi mpaka kushinda kesi hivyo kama wapo tayari kulipa kwa Cash haina haja ya kukataa kwenda kuzichukua hizo hela”Aliongea Linda.
Hamza mara baada ya kumwangalia huyu mwanamke alivyokuwa akimpa maelekezo aliona ni kama anataka kumwingiza matatizoni.
Lakini kwasababu hakuwa na mpango wa kuendelea kubishana na huyo mwanamke ambae ni kama anamuonea wivu kwa kula bata kazini aliamua kukubali na alitoka ofisini kwenda kumtafuta Eliza.
Comments