Hamza mara baada ya kuonana na Eliza, mrembo huyo alionekana kama amechoka mno licha ya kwamba ilikuwa asubuhi, ni kama vile alikuwa ameachwa na mpenzi.
“Eliza kwanini unaonekana kuchoka hivyo?”Aliuliza Hamza na mara bada ya Eliza kukutanisha macho na Hamza alionyesha kulazimisha tabasamu.
“Labda ni kwasababu nilikosa usingizi jana , vipi kwanini umekuja ofisini kwangu?”
“Linda kasema kuna hela za malipo unazokwenda kukusanya leo , ameniambia niende na wewe kama mlinzi”
“Kwahio tunaenda pamoja?”
“Ndio”
“Nikweli nilikubali kwenda lakini pamoja na Kapteni Yonesi kama mlinzi wangu”Aliongea Eliza.
Ombi la kampuni hio kutaka Eliza kwenda kuchukua hayo malipo lililetwa kabla ya Yonesi kupatwa na matatizo mpaka kulazwa.
“Hivi hii kampuni ya Dede inatisha namna hio , nimewahi kusoma mtandaoni kuna mdau analalamika ndugu yake kupoteea ndani ya kampuni hio”Aliongea Hamza.
“Kumekuwa na taarifa nyingi kuielezea lakini haijulikani kama ni za kweli ama za uongo, polisi pia hawajawahi kukanusha ndio maana wafanyakazi wengi wanaogopa , lakini wana wateja wengi tu wapenda starehe”Aliongea Eliza , ilionekana hata yeye hakuwa na uhakika kama hio kampuni ina shida.
“Kama kampuni haijulikani uendeshwaji wake kwanini mnafanya nayo biashara?”
“Mteja huwezi kumkatalia kumhudumia kwasababu umesikia tetesi ni mtu mbaya , labda kuwe na ushahidi wa wazi unaothibitisha hayo madai , vinginevyo kama amekidhi vigezo ukimkatalia lazima umpe sababu ya kuelezeka, Kampuni ni taasisi na haikopeshi wateja kulingana na tabia zao, inaangalia vigezo”Aliongea Eliza na kumfanya Hamza kutingisha kichwa kukubaliana nae.
“Kama ni hivyo angetafutwa mtu mwingine wa kwenda , kampuni ina watu wengi wa kudai madeni sio lazima wewe?”
“Mara ya mwisho alienda mtu kwa niaba yangu lakini hakuweza kukutana kabisa na mkurugenzi wao, lakini ilisemekana alikuwepo na baada ya kuwatishia kuwachukulia hatua za kisheria ndio bosi wao akasema anataka mimi niende nikapatiwe cash”
“Huoni sasa kuna mtego?”
“Najua ndio maana sikutaka kwenda mwenyewe , nilipanga kwenda na Kapteni Yonesi”Aliongea Eliza.
Mara baada ya wawili hao kutoka nje ya lift sehemu ya maegesho , Eliza alisogelea gari ya mjerumaini Porsche Macan ya rangi nyekundu , ilionekana ile gari ya Toyota ambayo ilipata ajali ilibadilishwa na kupewa gari nyingine.
“Eliza ni lini umenunua gari kali namna hii?”Aliuliza Hamza kwa mshangao maana ilikuwa ni gari ya hadhi mno na kwa haraka haraka alijua sio chini ya milioni mia thamani yake.
“Sijanunua mimi , hii ni zawadi kanipa Regina kutokana na kufanikisha dili la ile kampuni kutoka Morogoro?, ni gari ya bei sana najua lakini nilishindwa kuikataa maana mwenyewe ndio kanipa”Aliongea Eliza na kumfanya Hamza kushangaa , ilionekana Regina alikuwa akimjali mno Eliza lakini bado ni kama kuna kitu kilimpa ishara tofauti , ilionekana kulikuwa na zaidi ya sababu kwa Regina kumpatia Eliza gari ya bei ghali namna hio.
“Hata mimi naona hukuwa na haja ya kukataa , isitoshe unahitaji usafiri”Aliongea Hamza.
“Ndio , bosi ananijali ndio maana sitaki kumwangusha”Aliongea Eliza huku akiwa na muonekano usioweza kuelezeka ni wa furaha au wa huzuni.
Kwa namna ambavyo Eliza alikuwa akiongea ilizidi kumpa wasiwasi Hamza na kujiambia kuna kitu ambacho hakipo sawa kabisa lakini hakuelewa nini kinaendelea, isitoshe Eliza pia alionekana kutokuwa na raha kabisa.
Kwasababu Hamza ndio aliekuwa akiendesha Eliza alisema analala kidogo.
Kampuni hio ilikuwa maeneo ya Msata-Bagamoyo hivyo ilikuwa ni safari ya kama masaa mawili hivi.
Kutokana na Eliza kulala Hamza aliendesha gari kwa spidi kubwa ya wastani na ndani ya muda mfupi aliweza kufika na kuingia kwenye barabara inayokunja kushoto akipishana na kituo cha kujazia mafuta cha Lake oil.
Dede licha ya kwamba ilikuwa ikiitwa kampuni lakini ilikuwa ni kama hoteli tu.
Tajiri Laizer mara baada ya kupata madini makubwa yaliompa zaidi ya utajiri wa dolla milioni kumi za Kimarekani ndio alijenga katika eneo hilo ambalo ilikuwa ni shamba lao kabla hata ya kutajirika.
Hamza mara baada ya kuegesha gari Eliza aliweka nywele zake vizuri na wote wakashuka na kuanza kutembea kulisogelea geti na mara baadaya kufika getini hawakuweza kuigia maana lilikuwa limefungwa na waliishia kugonga.
“Mnaenda wapi?”Sauti ya mmasai ilisikika kupitia kijidirisha kidogo.
“Tunatokea kampuni ya Dosam , tuna miadi na Mr Laizer ”Aliongea Eliza.
“Dosam?, hebu subiri kwanza tutoe taarifa”Aliongea yule mlinzi na kisha kidirisha kilifungwa , walionekana kuwa makini kama vile wanafanya biashara haramu humo ndani.
Mpaka dakika tano zinaisha ndio mlango wa geti dogo ulifunguliwa na mwanamke alievalia sare za uhudumu.
“Nadhani utakuwa unaitwa Eliza meneja kutoka kampuni ya Dosam , unaweza kunifuata”Aliongea yule mwanamke na Hamza na Eliza waliingia ndani.
Lilikuwa eneo kubwa mno lenye bustani zilizotengenezwa na kuvutia , kulikuwa hadi na sanamu kubwa ya ng’ome katikati ya bustani.
Jengo la kampuni hio lilikuwa limeenda hewani kwa floor kama nne hivi na pana.
Ukweli licha ya kuambiwa hio ni kampuni lakini alishindwa kuelewa ni kampuni ya aina gani , Hamza alijiambia pengine ni biashara ilioandikishwa kama kampuni pekee lakini sio kampuni.
Walimfuata yule mhudumu ambae aliwaingiza katika korido ndefu iliokuwa na kila aina ya michoro ya wamasai ikiwemo Morani na viongozi wakubwa wa kimasai waliowahi kutamba katika historia , kulikuwa hadi na picha za baadhi ya tamaduni zao ikiwemo vinyago na mengineyo.
Licha ya michoro hio, jengo hilo lilinukia harufu ya kitajri , ni aina flani ya harufu hata benki unaweza kuweza kuinusa.
Waliweza kupishana na watu tofauti tofauti ikiwemo wanawake na wanaume na walikuwa wamevaa na wakapendeza mavazi ya pesa nyingi na kuna hata wale ambao Hamza aliweza kuona walikuwa na mafunzo ya mapigano.
Eliza alikuwa mwanamke mrembo na kitendo cha kuingia eneo hilo ilikuwa ni kama anaingia kwenye shamba lililojaa mbwa mwitu, kila mwanaume aliekuwa akimwangalia alionekana kumtamani.
Hata Hamza aliweza kuona namna ambavyo Eliza alikuwa na wasiwasi lakini hakuongea chochote , ili kumuondolea wasiwasi aliamua kumshika mkono
Eliza mara baada ya kushikwa mkono na Hamza alishituka kidogo lakini kwa wakati mmoja alionekana kujisikia vizuri kwenye moyo wake , lakini macho yake alipokuwa akimwangalia Hamza ni kama alikuwa akionyesha hisia za mwanamke mpweke, ni kama zile hisia ambazo michepuko wanakuwa nazo wakati wakiwasindikiza kwa macho waume za watu wakirudi nyumbani kuonana na familia zao.
Mara baada ya kutembea kwa takribani dakika saba waliweza kufika katika eneo ambalo lilikuwa kama sebule , kulikuwa na kila aina ya samani za bei ghali na kulikuwa hadi na kitanda chembaba cha kupumzikia.
“Mtasubiri hapa chumba cha mapokezi kwa dakika chache , bosi kwasasa yupo bize na baadhi ya kazi”Aliongea yule mhudumu na kisha akaondoka na kuacha ukimya ndani ya eneo hilo, kulikuwa na runinga pekee ambayo ilikuwa ikionyesha habari za kifo cha mgombea wa uiraisi wa chama tawala ambazo hazikumvutia Eliza kwa muda huo
“Hili eneo ni kama vile tupo Ikulu , ndio maana kuna malalamishi mengi kuhusu hili eneo”Aliongea Hamza maana ukimya wa hilo eneo ni kama vile hakuna kinachoendelea.
“Nimepitia mengi na kuna kila dalili zinazoniambia kuna kitu hakipo sawa , tunapaswa kuwa makini”Aliongea Eliza na kumfanya Hamza atake kumuuliza swala ambalo aliambiwa na Dina kutaka kutengenezwa na mheshimiwa Mgweno kama shushu wao wa karibu na Regina.
“Una hisi hivyo?”
“Ndio , unaweza ukawa hujapitia changamoto nyingi lakini kama meneja wa idara ya mauzo nimekutana na kila aina ya wateja kukamilisha mauzo ,hatujaambiwa hata ni muda gani tunakutana na Mr Laizer hii inaonyesha wametukalisha hapa makusudi kuvuta muda”Aliongea na kumfanya Hamza kutabasamu.
“Eliza wa nyumbani ni tofauti sana na wa kazini unaonekana kuwa makini mno”Aliongea Hamza.
“Sina utofauti wowote nyumbani na kazini nipo makini”Aliongea Eliza kwa kulalamika lakini kitendo cha kulainisha midomo na mate ni kama ilimpa hamasa Hamza kutaka kumkisi hapo hapo baada ya kuona wapo wenyewe tu na alichowaza ndio alifanya , alimshika kiuno Eliza na kumsogelea.
“Ah , wewe unafanya nini?”Aliongea lakini alionekana kulegea mbele ya Hamza na ilikuwa ni kama ishara nzuri kwa Hamza na kuzidi kumsogelea ili kumkisi lakini Eliza aliwahi kumziba Hamza mdomo na kiganja chake.
“Hamza usiwe hivi bwana , hatuwezi..”Aliongea Eliza akijitahidi kuwa siriasi na muda huo ni kama Hamza na yeye alikumbuka kuhusu swala la ndoa kwamba bado hajamuambia ukweli.
“Sorry Eliza , shida ni kwamba tukiwa wenyewe hivi nashindwa kujizuia kukuangalia unavyovutia”Aliongea Hamza.
“Kwasasa tuwe bize na kazi kwanza”Aliongea Eliza kikauzu huku akisogea mbali kidogo na Hamza na kitendo kile kilimfanya Hama kuona huyu sio Eliza aliemzoea.
Walikaa kwa zaidi ya dakika ishirini bila ya mtu yoyote kufika na hawakukaribishwa hata kinywaji , Hamza alijikuta akianza kuchoka na kuanza kupiga miayo na walisubiri kwa nusu saa nyingine lakini hakutokea mtu na muda wa chakula cha mchana ulifika na kumfanya Hamza kuhisi njaa.
“Inaonekana wanataka kuendelea kutukalisha hapa”Aliongea Hamza
“Tusubiri kidogo?”
“Mimi naona tunapoteza tu muda , kwanini tusiende kumtafuta wenyewe,tunaweza hata kuuliza wafanyakazi watuambie ofisi yake ilipo”Aliongea
“Unafikiri itakuwa rahisi wafanyakazi kutuambia?”Aliongea Eliza na muda huo huo mlango ulifunguliwa na alionekana mwanaume aliejazia mwili alievalia singlend tu kama mcheza basketball.
Mwanaume huyo alikuwa akinuka pombe tu na alikuwa ameshikilia chupa ya Whiskey mkononi na macho yake yalikuwa kwa Eliza muda wote kama vile anamtathimini.
“Mrembo nilieandaliwa leo naona hana ubaya mwenye , kazurii..”Aliongea huku akitabasamu kifedhuli na kauli yake ilimfanya Eliza kubadilika.
“Wewe ni nani?”Aliuliza Eliza na swali lile ni kama lilikuwa kichekesho kwa yule mwanaume kwani alianza kucheka kwa sauti huku akimsogelea Eliza.
“Unauliza nini wakati umeletwa kwa ajili yangu , halafu kwanini umevaa nguo nyingi namna hii au ndio unatunza joto , hii mbinu nimeipenda”Aliongea kilevi huku akinyoosha mkono kutaka kushika kola ya shati la Eliza lakini Hamza alikuwa ashamkinga Eliza kwa mbele tayari.
“Bro , nadhani umekosea chumba?”Aliongea Hamza na kumfanya yule bwana kumwangalia Hamza kwa macho yaliojaa ukauzu.
“Dogo wewe ni nani , kwanini unanizuia kuigusa mali yangu?”
“Narudia tena , Bro umekosea chumba “Aliongea Hamza na kumfanya yule mlevi kukasirika na aliinua chupa yake na kutaka kumpiga nayo Hamza ya kichwa na kitendo kile kilimfanya Eliza kupiga kelele , lakini Hamza aliweza kuidaka kabla hata haijampiga na ni pombe tu ilioishia kumwagikia usoni na aliishia kulamba maji maji yaliomfikia mdomoni.
“Sijui nafanya nini , hata mimi naona nishalewa”Aliongea Hamza.
Lakini yule mlevi alijikuta akikasirika zaidi na aliinua mkono kutaka kumpiga Hamza kibao lakini kabla ya kumfikia Hamza alikuwa ashainua mguu na kumpiga nao tumboni.
“Bang!!”
Yule mlevi alijikuta akishindwa kuhimili nguvu iliomsukuma na kwenda kuvaa pot ya maua na kudondoka nayo
“Fuc*k you”
Bwana yule alijkuta akitukana na alisimama kwa tabu na kumsogela Hamza kwa mara nyingine huku akiwa amekunja ngumi , lakini Hamza alisimama katika eneo moja na baada ya kumkaribia alimpiga ngumi ya kifuani iliomfanya yule bwana kudondoka tena chini huku akiwa amepiga magoti na kuanza kutapika pombe iliochangayikana na damu.
Eliza aliekuwa nyuma aliweza kuona Hamza alikuwa amemuadhibu yule mlevi kwa mashambulizi mawili tu mpaka kutapika damu , alishindwa kujizuia na kuishia kushikwa na hofu asijue cha kufanya.
Hamza alimsogelea yule mwanaume na kisha alimkanyaga mgongoni na kumfanya alale kifundi fudi.
“Sema wapi alipo Laizer”Aliongea Hamza
“Unajitafutia kifo , mimi ni mgeni hapa unathubutu vipi kunishambulia?”Aliongea kijeuri na kumfanya Hamza anyanyue mguu na kumkandamiza kwa nguvu kwenye bega lake na kumfanya apige mayowe kwa maumivu makali.
“Ongea wapi alipo Laizer?”Alirudia Hamza.
“Sijui alipo , mimi sijui kweli”Mtu yule wa miraba minne alijikuta akianza kuingiwa na woga .
“Unaendelea kujifanya mtiifu sio , mpaka muda huu bado unaigiza?”Aliongea Hamza huku akizidi kumkandamiza kwenye bega lake.
“Nilikuwa nikifuata maagizo tu , mimi sijui kweli alipo”Aliongea yule bwana na muda huo ni kama Eliza alishituka.
“Hamza anasema ametumwa na Mr Laizer?”.
“Kuna haja hata ya kuuliza , huyu katumwa kuja kukuigizia hapa kukuogopesha ili usahau hata kuulizia hela”Aliongea Hamza.
“Mbona wameenda mbali hivyo , sidhani Mr Laizer anaweza kukosa milioni themanini iliobaki”
******
Upande wa makao makuu, Regina akiwa ndani ya ofisi yake alijaribu kumpigia Hamza lakini ajabu alikuwa akiambiwa simu yake haipatikani.
Na alianza kushikwa na wasiwasi kutokana na bibi yake alimsisitizia kupitia simu anataka kuonana na Hamza siku hio bila ya kukosa , sasa kwa mtu ambae alikuwa siku za mwisho mwisho ombi lake lilipaswa kutimizwa bila ya kuchelewa ndio maana Regiina alikuwa na wasiwasi.
Lakini anajaribu kupiga simu yake sasa haipatikani , muda uleule aliamua kumuita Linda ofisini kwake.
“Mkurugenzi kuna maagizo yoyote?”Aliongea Linda.
“Hamza yupo wapi?”Aliuliza na kumfanya Linda mwili kumkakamaa.
“Ametoka nje ya ofisi kikazi?”
“Kwenda nje kikazi , nje ya wapi na ni kazi gani?”Aliuliza Regina kutokana na kwamba hata yeye alishangaa kusikia kauli hio.
“Kuna zile pesa zilizobakia za tenda kutoka kampuni ya Dede Bagamoyo , mkurugenzi wao alipiga simu na kusema atafanya malipo ya Cash na Meneja Eliza anapaswa kuyafuata leo , ilipangwa Eliza kwenda na Kapteni Yonesi kama mlinzi wake lakini bado hajapona kabisa , hivyo nilimpa kazi hio Hamza kwenda nae , maana anaonekana kuwa na nguvu zaidi ya Kapteni..”Aliongea Linda na kumfanya Regina ukauzu kumvaa.
“Nani kakuambia umpangie kazi ya namna hio?”
“Lakini bosi si ulisema nimpe kazi asikae bure”
“Hebu nyamaza , Hamza ni msaidizi wangu mimi , inakuwaje atoke hapa aende kuwa bodigadi wa meneja wa idara ya mauzo , nimekwambia mpangie kazi na sio kumhamisha idara , akili yako inawaza nini?, hivi unadhani mimi nimekuwa kipofu , hata kama una wivu kutokana na uwezo wake kwenye baadhi ya mambo hupaswi kuonyesha wivu wako kwa kufanya maamuzi ya namna hii , yaani umefanya kazi na mimi kwa zaidi ya miaka mitatu lakini unashindwa kukua kimawazo” Regina alibadilika na kuwa mbongo na kuanza kumfokea sekretari wake.
Linda macho yaligeuka kuwa mekundu huku akiinamisha kichwa kwa hofu kubwa.
“Nisamehe bosi , nimekosea.. , nitampigia mara moja arudi’Aliongea Linda akijitetea.
“Haina haja nishampigia mara kadhaa na simu yake haipo hewani , nadhani kaizima au hakuna mtandao”
“Lakini bosi wanazimaje simu , wameenda Msata makao makuu ya Dede kwanini mtandao usipatikane”Aliongea Linda na muda ule ni kama Regina anasikia vizuri sasa.
“Dede si wana ofisi yao Posta na ndio tulikubaliana makabidhiano ya malipo yatafanyikia hapo , kwanini wameenda Msata?”Aliuliza Regina ni kama aliona kuna taarifa ambazo hajaletewa.
“Ndio walivyotoa maelekezo , mara ya mwisho siku yao ya kulipa waliomba kuongezewa siku mpaka leo na Eliza ndio afuate Cash, idara ya mauzo ndio walifanya makubaliano na Dede na ofisi ya Finance wameipa siku kumi idara ya sales kukamilisha hesabu la sivyo wataripoti idara ya sheria…”
“Kwahio wamemwambia Eliza aende na akakubali kwenda , hivi ni habari ngapi mmesikia kuhusu mambo yanayofanyika huko Msata , ukute hata hizo Cash wanazotaka kutoa ni kwa ajili ya kutakatisha hela , mlipaswa kuwakatalia na sio kwenda kichwa kichwa ,si walikubaliana wakutane Posta kwenye makabidhiano?”Aliuliza Regina lakini Linda hakuwa na jibu zaidi ya kukaa kimya
“Dede wanafahamika kwa kutapeli watu kupitia madeni yao , wakikataaa deni lao Eliza ana uzoefu wa kutolazimisha na kuacha sheria ichukue mkondo wake , lakini wewe umemjumuisha Hamza ambae anapenda kujichukulia sheria mkononi , unataka akaibue matatizo mengine?”Aliongea Regina huku akimwangalia Linda kwa macho ya kukatishwa tamaa.
“Nisamehe bosi sikufikiria mbali”Alijitetea lakini Regina hakuwa na mudi kabisa ya kuendelea kumuona.
“Unaweza kuondoka , unapaswa kuomba yasitokee matatizo na warudi wakiwa salama la sivyo jiandae kuandika barua ya kuacha kazi”Aliongea Regina kikauzu na kumfanya Linda kuinua uso wake huku akimwangalia bosi wake kwa kutoamini.
“Bosi , kwani Hamza ni wa muhimu sana?”Aliuliza Linda.
“Ndio ni wa muhimu”Aliongea kikauzu na kauli yake ilimfanya Linda kutetemeka na aliishia kuondoka kwa hatua hafifu na kufunga mlango.
Ukweli ni kwamba Regina hakujua kwanini alikuwa na wasiwasi Hamza angesababisha matatizo huko Msata , kulikuwa na mambo mengi yanaendelea nchini ikiwemo taarifa za mgombea wa uraisi kuuliwa na mengineyo na aliona Hamza anaweza kutibua zaidi hali.
Baada ya kukaa akiwaza cha kufanya palepale alichukua simu yake na kuitafuta namba ya Meneja wa hoteli yao ya nyota tano Bagamoyo mjini.
“Mkurugenzi habari za mchana , kuna maagizo yoyote?”Sauti ya mwanaume ikiongea kwa heshima ilisikika.
“Hebu tuma mtu yoyote kutoka hotelini aende Dede kuangalia kinachoendelea, Meneja Eliza na msaidizi wangu wapo huko na hawapatikani hewani”Aliongea
“Sawa Mkurugenzi nina mtu yupo maeneo ya Msata nadhani itakuwa rahisi kwenda kuangalia nitakupa majibu muda si mrefu”Aliognea mkurugenzi na Regina alikata simu.
Hamza ametengenezwa mpango wa kwenda Dede bila kujua , ngoja uone.
Comments