Reader Settings

SEHEMU YA KWANZA

Dhamiri ni kweli...

Humsuta mtu hasa pale anapotembea njia isiyo sahihi...

Humkumbusha mtu kuwa japokuwa hajakamilika, bado anahitaji kuufukuzia ukamilifu kwa juhudi zake zote.

Na hii ni Sehemu ya kwanza..

Jua zuri la kupendeza, lilionekana likichomoza kutokea upande wa Mashariki wa anga. Mwanga wake mzuri wa dhahabu uliufukuza mwezi ambao nao ulitii bila shuruti na kuanza kufifia mawinguni.

Ndege wa angani wakaanza safari zao za siku zote kila ilipofika mida kama hii, wakaimba na kufanya fujo za kila namna. Ni hizo fujo na kelele za nyimbo zao, vilivyowaamsha wanadamu ambao walikuwa bado wameyakumbatia malazi yao. 

Kulikuwa kumekucha...ilikuwa ni alfajiri.

Naam,

Hata mwanaume huyu alikuwa mmoja kati ya wale waliokuwa bado wameyakumbatia malazi yao alfajiri hii. Yeye akiwa bado ameunatisha mwili wake juu ya godoro hili laini kwa gundi ya ajabu.

Gundi inayowatesa wale wapenda usingizi. Uzembe!

Ni uzembe tu, wenye chembechembe za uchovu, uliomfanya mwanaume huyu aendelee kujilaza kifudifudi palepale kitandani, akiwa ndani ya shuka jepesi lililokuwa na joto la haja. Sio kwamba amesinzia la! Ila kaamua tu, kulifaidi joto la asubuhi lililochanganyikana na uchovu kisha likapigiliwa msumari mzito na uvivu. 

Uchovu? Kwa nini uchovu?

Usiku uliopita alikuwa na shughuli nzito mno ambayo imemfanya aendelee kujilaza palepale kivivu.

Uchovu huuhuu ukamfanya ajihisi mzito sana walau hata kujigeuza ili alale chali. 

Haya, afungue macho basi ili aione dunia, akashindwa!

Badala yake akalivuta shuka na kujikunyata akijiviringa zaidi ndani yake, ingezuka vita ya tatu ya dunia kama mtu angempokonya shuka hili muda huu.

Alizisikia kwa mbali sauti za ndege wanaoimba kwa furaha kuikaribisha siku hii mpya.

Akawaza kuhusu furaha yao,

"...Hawapandi, hawavuni na wala hawaweki ghalani lakini baba wa mbinguni huwalisha hao....je nyinyi si bora kupita hao?..." Akajaribu kurejerea mstari huu katika maandiko matakatifu.

Akasonya baada ya kugundua kuwa yeye sio ndege, hivyo hana namna yoyote ile ya kujilinganisha nao.

Kitendo cha kukumbuka kuwa amerejerea mstari mtakatifu tu, akamkumbuka Mungu,

akalikumbuka kanisa, akamkumbuka mke wake wa ndoa, akaikumbuka familia yake aliyoiacha nyumbani.

Kisha mara moja akaikumbuka shughuli nzito iliyojaa laana aliyoifanya usiku uliopita.

Naam,

Kwa mara ya tano amekutana na binti huyu aliye nje ya ndoa yake na kwa pamoja wameshiriki juu ya vitanda tofauti tofauti, kwenye hoteli tofauti tofauti, katika siku tofauti tofauti-kuisulubu amri ya sita. 

Akapata sononeko la moyo. Alikuwa na kidonda ndugu kilichogoma kupona. Akamfikiria tena mke wake...hakupenda kuisaliti ndoa yake.

Lakini ukorofi na fujo za mke wake zilizokithiri ndizo zilizopageuza nyumbani kwake kuwa kama jehanamu ndogo.

"Mama Junior!...ni kwa nini lakini?" 

Akazungumza yeye na nafsi yake, Akajilaumu peke yake,

Ameoa tayari ana mke,

Lakini bado anajihisi mpweke.

Mara akakurupushwa na rabsha ndani ya chumba kile, zilizosababisha ukelele fulani ambao haukumkera...na hapo macho yake yakakubali kufunguka.

Akajitahidi kukipindua kichwa chake, akijipindua kama nyoka pale juu ya kitanda kilichoshirikiana na joto kumshikilia asiamke.

Macho yake yakagota juu ya umbo la mwili wa kike uliokuwa umesitiriwa ndani ya taulo fupi lililolowana kiasi, likiwa limefungwa maridadi kifuani na kuacha wazi mabega yake huku likijitahidi kuyaficha mapaja laini yaliyonona na lisiweze. 

"Huyu hapa huyu..."

Akatamka na nafsi yake kwa mara nyingine,

"Huyu nd'o amekuwa faraja ya moyo wangu...yaani dah! Mama Junior, umenifanya nilale na malaya?" Akazidi kujiuliza na kujijibu mwenyewe.

Ni wazi kuwa binti huyu alikuwa ametoka kuumwagia maji mwili wake. Na sasa huyu hapa ametazamana na kioo kipana kilichobandikwa kwenye kabati, amempa mgongo tu huyu mwanaume na mara binti huyu akafanya tukio ambalo lilisababisha hali ya uchangamfu pale chumbani.

Taratibu bila papara akalifungua taulo lile fupi na kubaki kama alivyokuja duniani, maungo yake yote yakabaki wazi!

Lile jotoridi pale kitandani likaanza kuongezeka. Likazidi na kuiyeyusha ile gundi yote ya uchovu. Bwana huyu akachangamka na kukaa mkao wa kula ili macho yake yasiyo na pazia yafanye jukumu lake la kila siku.

Mwili uliobarikiwa ngozi laini, ulikuwa umelowanishwa kwa tembe chache za maji. Kama embe bichi mwituni.

Rangi yake asili iliyokataa daima kueleweka kama ni nyeusi, machungwa au ile ya maji ya kunde ikaonekana iking'ara. Hii haikuwa ngozi yenye rangi bandia iliyotegemea vipodozi wala kemikali ili ing'ae.

Binti akalikamata taulo lile na kuanza kuupapasa mwili wake taratibu, akijipangusa tembe zile za maji. Alikuwa ni kama anapiga deki.

Mboni za macho ya huyu kiumbe aliyekuwa kitandani yakazidi kufuatisha tu kila kiungo kilichofikiwa na huduma ya taulo lile. Kwa kila kiungo akakifanyia uchambuzi wa kisanii.

Mwinuko wa milima miwili yenye ukubwa wa kadri iliyokuwa na bonde katikati yake, ikibebwa na mapaja manono yenye rangi angavu yaliyojazwa nyama na yakajazika sambamba na miguu mizuri ya kike iliyonyimwa michubuko ya aina yoyote ile.

Hivi ni miguu tu? Akakagua tena na kugundua kuwa kama kuna mchubuko au kipele chochote kile juu ya mwili wa huyu binti; Kama kingekuwepo basi kitakuwa kinapitia dhuluma na aibu ya upweke kwa kukaa mahali isiyostahili.

Kiuno chake chembamba,

Ngozi laini isiyo na magamba, 

Yavutia kwa macho waweza kuilamba, 

Yote hii kazi ya muumba.

Taulo lilipohamia mbele hakuweza kufanya uchambuzi wake. Na hilo likamsononesha upya.

Akapitia mateso kuamini kuwa binti huyu amemaliza kujikausha mwili wake.

"Hivi kweli huyu ndiye nilikuwa naye usiku kucha?" Akajiuliza.

Kila siku alizidi kumuona mpya kabisa machoni mwake, hakuwahi kuuzoea uzuri wake.

Binti huyu akainua mguu wake na kuuweka juu ya stuli ndogo. Taratiibu akaanza kuipakaa ngozi laini ya mwili wake mzuri kwa mafuta.

Juu ya mwili wake laini,

Mijongeo ya vidole vyake kwa umakini, Kajipakaa kutoka juu mpaka chini, 

Akitazamwa tokea pale juu kitandani, Na dume la nyani,

Kwa macho yenye huzuni.

Katikati ya miguu ya mwanaume kulikuwa na askari ambaye daima alikaa chonjo kukabiliana na hali za hatari kama hizi. Tayari alikuwa amesimama wima kwa ukakamavu.

"Amekosa nini huyu binti?"

Likawa swali gumu ambalo daima alijiuliza tangu alipomtia mrembo huyu machoni kwa mara ya kwanza. Alikuwa na urembo wa kutosha kabisa kumfanya shetani aungame makosa yake yote kisha aamini kuwa yupo Mungu anayeishi, muumba wa kila kitu kizuri.

Lakini ajabu!

Mrembo huyu ni changudoa, kahaba, malaya, dada poa...KIBIRITINGOMA! 

Asingekosa mwinyi mwenye pesa za kutosha kumuoa au hata kumfanya hawara. 

Ukute ana mikosi!

Au ana laana kutoka kwa wazazi wake..

Kwani ana wazazi kweli huyu?

Ilikuwa ni foleni ya maswali ambayo iliendelea kujipanga akilini mwa bwana Didas Ambrozi; mkurugenzi wa kampuni, baba wa familia, mzee wa kanisa na mzee wa busara aliye muungwana kama alivyojulikana na jamii.

Kila wadhifa aliokuwa nao, ulitosha kabisa kumfanya aone aibu kutoka nje ya ndoa na kununua makahaba. Mara mia hata angekuwa na hawara wa nje lakini kahaba?!

Hakika alikuwa amepiga hatua ndefu sana ya kujitafutia aibu.

Lakini kwake yeye, aliitazama hii aibu kwa jicho la tofauti kabisa. Wakati nyinyi mnamuona huyu binti kama kahaba na changudoa, yeye alimuona kama hawara au mchepuko wa pembeni!

Kila aliposhambuliwa na vurugu na masimango ya mke wake, alizifuata bashasha na raha kwa huyu binti. 

Alionjeshwa asali, yeye akaamua kuchonga mzinga kabisa.

Bwana Didas Ambrozi akajikohoza kidogo,

"Umeamkaje Bebe." Kwa sauti yenye kitetemeshi akatoa salamu ile akiwa na matarajio kuwa labda binti huyu aitwaye 'Bebe' atamuoena aibu na kujisitiri.

Lakini haikuwa hivyo, kwa nini ajisitiri?

Hakuna alama yoyote ile ya mwili wake isiyojulikana na mwanaume huyu. Wameshakutana kimwili zaidi ya mara nne, wakibadilishana bidhaa ambazo kila mtu alihitaji kutoka kwa mwenzie.

Bebe alihitaji fedha na Bwana Didas alihitaji ladha ya tunda la mti wa katikati. Kwa Didas ikiwa ni burudani lakini kwa Bebe ilikuwa ni kazi iliyoachana kwa sentimita chache sana na neno 'biashara'!

"Salama tu Daddy...vipi wewe!" Kwa sauti changamfu iliyojaa huba, Bebe akamjibu akiwa amemtazama Didas huku sura yake ikivaa tabasamu lenye bashasha. Hapa yakazuka mafumbo mapya kabisa, yaliyohitaji uchambuzi wa kisanii.

Sauti yake ya kinanda,

Nyepesi nyororo isiyo na inda,

Tamu kama soda ya Mirinda, 

Kutoka kinywani mwa huyu kinda,

Bwana Didas ikamshinda!

Macho yake yakagota kwenye sura yake.

Kasura kake kazurii, 

Kamefinyangwa kwa umahiri, 

Anatabasamu kwa desturi, 

Tabasamu tamu la alfajiri, 

Utataka kumtazama adhuhuri, 

Hutachoka mpaka alasiri, 

Si utani Bebe alikuwa zaidi ya neno 'mzuri'!

"Eeer...mi mzima! Naona leo umewahi kuamka aisee!" Akajitahidi kulazimisha tabasamu usoni mwake, akafanya jitihada za kusimama huku akimficha askari wake aliyekuwa tayari kupigana asubuhi hii.

"Mh...jamani Daddy, sa ulitaka nilale mpaka saa ngapi. Nina kazi nyingi zinanisubiri asubuhi hii mwenzioo"

Bebe akamjibu kwa sauti ileile ya madeko akianza kuvaa nguo zake za ndani moja baada ya nyingine. Mwisho akamalizia na kigauni kifupi chekundu kilichokataa katakata kuyafunika yale mapaja yake yaliyokuwa na uwezo wa ajabu wa kuamsha ashiki ya dume lolote lile rijali.

Bwana Didas akajinyoosha huku akipiga mwayo mrefu, mkono wake wa kulia ukahamia kiunoni, na ule wa kushoto ukakipapasa kitambi chake chepesi kisha akarejea upya juu ya kitanda na kuketi.

Bado macho yake yako kwa Bebe. 

Umbo lake matata likijisanifu vyema ndani ya kigauni kile kilichoung'ang'ania mwili wake kwa kuubana kiasi.

Bebe akachukua pochi yake ndogo na kupiga hatua zake kwa madaha, miguu yake ikijikata kwa mwendo wa paka 'catwalk' mpaka pale juu ya kitanda na kuketi kando ya Bwana Didas.

Viganja vyake laini vikavikamata viganja vigumu vya Didas na kuanza kuvitomasa katika namna upole na kubembeleza.

"Daddy..."

Akamtazama usoni kwa macho ya kusinzia, Katika namna ya kurembua, 

Kwa sauti ya kichokozi, 

Akalitaja jina kwa mapozi, 

Ambalo siku zote liliyapoza maumivu yote ya moyo wa Didas Ambrozi.

"Niambie mrembo..." Didas akamjibu kwa upole...tayari ameshalainishwa akalainika.

"Mi nd'o naondoka hivyo..." Soni ikauvamia uso wake akazihamisha mboni zake mpaka kwenye vile viganja alivyokuwa anacheza navyo.

Didas akashusha pumzi kwa nguvu kisha akauruhusu mkono wake wa kulia umzunguke Bebe na kumkumbatia.

"Asante sana kipenzi...umeugeuza usiku wangu wa jana kuwa sawa na sikukuu!Nimefurahi sana." Akatamka kwa mahaba huku akiusaili uso wa Bebe uliobarikiwa uzuri.

"Mmh jamani kwelii?..." mrembo akauliza kwa sauti ya kinanda.

"Haswaa...na laiti kama ningekuwa na uwezo ningekufanya mke wangu wa pili. Ni vile tu dini yangu hainiruhusu." Didas akatema cheche.

Bebe akaishia kuguna bila kusema neno. Ukimya wake ukamruhusu Didas aendelee kutumia vyema uwanja wa mazungumzo.

"Kuna swali nataka nikuulize Bebe...kama hautojali lakini." Akameza funda jepesi la mate kwa woga.

"Uliza tu"

"Uum...utaishi haya maisha mpaka lini Bebe?!" Akaweka pumziko na kumkazia macho usoni, macho yaliyohitaji majibu.

Bebe akatazama sakafu na kuufyata mdomo wake mdogo, akabaki kimya.

Didas akaendelea,

"Wewe ni msichana mrembo sana. Na najua fika kuwa hili unalijua, hata kioo ulichokuwa unakiangalia muda mfupi uliopita hakikukudanganya. Lakini ni kwanini unafanya hii biashara?!" Akamuongezea swali jingine bila kujibiwa lile la kwanza. Bado Bebe aliendelea kubaki kimya.

"Nisikilize Bebe...nataka niyabadilishe maisha yako. Huu mwili wako haukuumbwa ili uishi kwenye madanguro, nataka nikupe jumba kubwa la kifahari ukae, uishi kwa raha. Ngozi yako hii mama, haikufumwa ili ipigwe na vumbi mpenzi, wala miguu yako haistahili adhabu ya kutembea zaidi ya hatua kumi mama yangu. Nitakupa gari la kutembelea. Sipendi kukuona unaishi hivi mrembo..."

Wakiwa wametazamana uso kwa uso, Didas akiwa amekishika kidevu cha Bebe kilichochongoka kama embe. Akaendelea kumshawishi Bebe akubaliane na ombi lake la siku nyingi. Aachane na biashara hii ya kujiuza na aishi kwa kutulia akihudumiwa na yeye mwenyewe.

Bebe akayalegeza macho yake makubwa na kurembua kimahaba akauondoa taratibu mkono wa Didas kwenye kidevu chake. Akatumia mkono wake kukishika kidevu cha Didas kilichoota ndevu nyingi mithili ya 'steelwire' akakisogeza karibu na akaivamia midomo yake kwa papi za midomo yake.

Kilichofuata ni kitendo cha kubadilishana mate kwa sekunde kadhaa.

Kisha Bebe akaondoa midomo yake na kumtamkia kwa ukaribu,

"Daddy...Uko tayari kumuacha mke wako kwa ajili yangu?!... Uko tayari kuandikisha mali zako zote kwa jina langu?!...Uko tayari kunioa kwa ndoa ya kifahari...Ndoa itakayofanyika kwenye fukwe za Uarabuni?! Nijibu Daddy uko tayari?!..."

Maswali yake yakageuka shubiri kinywani mwa Didas. Yalikuwa machungu mno...hakuweza kuyajibu na akaishia kuguna.

"Hayo yote nimehaidiwa na wanaume tofauti sijui ni nani mkweli na nani mdanganyifu. Lakini wote wamenipatia sifa zilezile. Kama unazonipatia wewe." Akatamka akisimama taratibu.

"Kila mmoja amenihaidi pete ya ndoa. Lakini wote hawa wanajua fika kuwa mimi sifai kuwa mke wa mtu. Nimzalie watoto, niwe mama wa familia...mnalijua hilo kabisa! Kwanza ni mwanaume gani timamu atakubali kumuoa malaya?!" Akaliacha swali lake lielee hewani. Likamfanya Didas aone aibu na kutazama chini. Jibu alilolipata lilimfanya ajione sawasawa na kuwa uchi hadharani. 

"Sitaki kufungwa kwenye gereza la pete. Sitaki nipitie mateso ya pingu za maisha.Furaha yangu ni pesa! Ndoa yangu ni pesa, ninachokitaka ni pesa tu, pesa mezani!" Akatamka huku akiunyoosha mkono wake kwa Didas ambaye alielewa alichokimaanisha.

Upesi huku akitetemeka akalipekua suruali lake na kuibuka na waleti. Akahesabu noti kumi na tano nyekundu na kumpatia Bebe.

Bebe akazihesabu na kushangaa,

"Eh? Kilo na nusu?!" Akauliza Bebe baada ya kuona kazidishiwa ujira.

"Eeh..wala usiwaze...chukua zote hizo!" Akajibu kwa kigugumizi Didas. Kijasho chembamba kikianza kumvuja makwapani.

Bila kujibu kitu Bebe akazisukuma kwenye pochi yake, akainama na kuachia busu la hewani kuelekea usoni kwa Didas, aliyelazimisha tabasamu.

"Bye bye Daddy...mpaka kesho tu utakuwa umenisahau tayari!"

Akageuka nyuzi mia tatu sitini kwa maringo, na kupiga hatua kuondoka pale chumbani.

Viatu vyake vya kuchuchumia vyenye visigino vilivyoinuka, vikaifanya marumaru ya sakafu ile iziimbe sifa zake.

Nyama zake za makalio zikipata mtikisiko, 

Sakafu chini ya viatu vyake ikalia ko!ko!ko!,

Nyuma yake akaacha masikitiko, 

Didas akabaki na masononeko, 

Hawezi kulipikia peke yake hili jiko,

Kumbe wapo wengi wale wavuta kiko, 

Wenye nasaba bora wanaomzidi mshiko, 

Labda atumie hirizi na mazindiko,

Lakini ye mzee wa kanisa, ushirikina mwiko!

"Aiseee!" Ikamtoka bwana Didas, hakuamini anachokiona. Kifurushi kilichosheheni kila aina ya baraka ya uumbaji nd'o kileee kilikuwa kinamuacha peke yake chumbani. Bebe alikuwa ni tafsiri halisi ya 'complete package' ya neno 'mwanamke mzuri'. 

Alikuwa amemzoea Bebe. Lakini kila siku alimuona mpya.

Akaachwa chumbani mle akifanya tafakuri. Bebe alimuachia sentensi tata mno iliyomdai aiandikie insha yenye kichwa,

"NDOA YA MWANAUME TIMAMU NA CHANGUDOA!"

Hakika alipewa darasa huru, darasa la bure.

Akarejerea tena kulitafari neno la Mungu.

*****

Nje ya hoteli hii ndogo...Bebe akasimama na kuvuta hewa safi kwa sekunde nne. Upepo mwanana ukamlaki na kuuburudisha mwili wake kwa kumpepea.

Naam, ilikuwa siku mpya!

Akatabasamu na kuifungua pochi yake, akahesabu upya noti zile huku akiuhisi ushindi moyoni mwake.

Upesi akazitenga noti tano na kuzifutika kwenye sidiria yake, huenda hizi zilikuwa za ziada.

Akaitazama simu yake aliyokuwa ameiamuru iwe bubu kwa kuiseti katika 'silent mode' usiku kucha. Akakuta jumbe nyingi na simu nyingi zilizomtafuta bila mafanikio.

Zilimtafuta nyingi lakini ni moja tu iliyokuwa na umuhimu kuliko zote.

MADAM SALLY!

Ndivyo alivyohiifadhi.

Akaipigia upesi akiwa tayari kupokea lawama, matusi, shutuma na malalamiko yote.

Na kweli! Hakukuwa na salamu.

Mvua ya matusi ya nguoni na lawama ilimnyeshea kutokea upande wa pili.

"Madam, madam...calm down madam! Nd'o nilikuwa nakuja jamani. Kanikamia huyo, hakutaka niondoke haraka!" Akajitetea.

"Kwa hiyo unataka kusema umempa na 'Cha asubuhi au?'...we ruka ruka tu huko. Ukitapeliwa shauri yako!"

Sauti ile kavu ya kike ikafoka.

"Nakuja jamani madam nipo njiani hapa!"

"We hata usipokuja...ili mradi hela yangu inifikie huku mie!" 

Simu ikakatwa.

Bebe akatazama kulia na kushoto, akapunga mkono kumuita dereva bodaboda.

Akasimama na akapanda huku akimpatia maelekezo ya wapi anapokwenda. Pikipiki ikachochewa moto, ikaviringisha matari yake na kuondoka.

Nyinyi hamkuwepo,

Lakini acheni mimi niwasimulie...Hakika Bebe hakufanania hata kidogo na kupanda bodaboda. Huenda bwana Didas Ambrozi alikuwa sahihi, akampa fursa lakini Bebe akaikataa na kuendelea kuyakumbatia maisha yaliyozidi kumparua kwa makucha makali.

Kwa nini akatae?

Hata mimi sijui,

Maana ukiona mtu anatema asali kwa nguvu kisha akakimbilia kulamba pilipili tena kwa hamu kubwa, lipo jambo! Hakika lipo jambo. 

Tena sio jambo dogo!

Itaendelea....

Next