Reader Settings

SEHEMU YA PILI

Chimbuko la jamii yoyote ile huanzia kwenye ngazi ya familia.

Familia ni kitovu cha taifa, na ni chemichemi ya tamaduni zote zinazolijenga taifa.

Nguzo za familia zinapoyumba, ni rahisi sana maadili ya jamii kuporomoka na kuzua janga kwa taifa.

Japokuwa malezi ya watoto katika familia ni jukumu mama la wazazi yaani baba na mama,

Hilo halizuii mchango wa jamii kwenye malezi ya watoto wetu.

Malezi ni ya kwetu sote...

Na hii ni sehemu ya pili,

Anaitwa Frolida Pasko,

Walioona kuwa ndimi zao zitapata taabu sana kulitaja jina lote hili, wakamuita Frola ili kuokoa muda.

Hakutegemea kupachikwa jina jingine katika maisha yake. Mpaka pale alipoianza hii shughuli ya ukahaba na kutumika kingono ili apate pesa. 

Alivutia sana kwa urembo wa sura yake, wale waliokuwa wajuvi wa misemo na lugha, wakadai kuwa ati ana sura ya upole na adabu kama ya mtoto mdogo. Wanaoijua ile lugha iliyokuja kwa ndege wakasema ana 'baby face', wakamuita 'baby'. Waswahili wakafunga kazi kwa kumuita 'Bebe'.

Naam,

Muite kwa majina ya Frolida na Frola wakati wa mchana. Lakini anapokuwa kazini, anavaa wajihi mpya kabisa...hapa muite Bebe!

Jina la Bebe likajizolea umaarufu mkubwa, yale mengine yakazikwa kwenye kaburi la sahau.

Malezi?!

Alilelewa ndio, tena na wazazi wawili, baba na mama. Yeye akiwa mtoto wa pekee.

Jinamizi la umasikini liliiwinda familia yao usiku na mchana, likapanua mdomo wake mkubwa na kunyoosha makucha ili kuwaangamiza.

Baba yake, mzee Pasko; hakuwa na kazi maalumu ya kueleweka. Kila siku aliamka asubuhi kisha huyoo anaondoka, anakoelekea hapajulikani. Na aliporudi usiku alikuwa akiyumba na kutoa maneno machafu na yenye aibu.

Alikuwa mlevi wa kupindukia, aliyezifanya baa,vilabu na vijiwe vya pombe za kienyeji kuwa kama nyumba za ibada. Huko alihudhuria asubuhi, mchana na jioni. Alipokosa bia, alizikumbatia pombe za kienyeji.

Pombe zikang'ang'ania kila sarafu yake, zikakamata kila noti yake. Akayasahau majukumu yake kwenye familia kama baba.

Hakuwa na mahusiano na pombe tangu zamani lakini marafiki zake aliofanya nao kazi kwenye kampuni ya ulinzi, ndio hawa waliomsogeza kwenye meza za vilabu na baa mbalimbali. Wakazitambulisha chupa za pombe na bia kwake, wakazinadi kuwa zina uwezo wa kuufukuza msongo wa mawazo na kuleta utulivu wa nafsi.

Ni nani asiyeupenda utulivu wa nafsi?

Umaskini na taabu viliyafinyanga maisha ya Pasko na familia yake, vikamsuta na kumuonyesha kuwa yeye sio baba bora.

Akaikaribisha pombe kwa mikono miwili, akaionja mara ya kwanza na kufinya uso wake kwa ukakasi na uchungu aliouonja, akaambiwa ni kawaida hiyo kwa mtu anayeanza pombe kwa mara ya kwanza.

Akajikaza,

Taratibu...katika namna ya ajabu, uchungu ukageuka kuwa utamu, utamu ukasafiri kooni ukasafisha umio na kutulia tumboni mwake. Baada ya dakika chache tu akahisi faraja ambayo hakuwahi kuihisi popote pale maishani mwake.

Ni hapo, aliposaini mkataba wa maisha na pombe. Akaivisha pete na pombe ikawa kama mke wake wa pili.

Kuvaa miwani ikawa tabia yake ya moja kwa moja...na alipozoea kwenda kazini akiwa amevaa miwani, waajiri wake wakamuachisha kazi mara moja.

Hapo akazidisha mapenzi yake kwa pombe... kwa nguvu zake zote,akili zake zote na moyo wake wote.

Akawa mzigo nyumbani. Wakati anategemewa alete chochote kitu, yeye akawa anategemea akute chochote kitu.

Kijiti cha jukumu la kulea familia kikahamia kwa mama moja kwa moja.

Kazi zake ndogondogo za kuuza nyanya,vitunguu na mbogamboga zikawa kama jicho lake pekee alilolitegemea kuilisha familia yake.

Aliitwa Bi Devotha;

Mwanamke ambaye tumbo lake lilibarikiwa kumleta duniani mtoto mmoja pekee. 

Frolida!

Bahati mbaya kwake, hakufanikiwa kupata uzao mwingine, ama mtoto wa kiume kama alivyodai mzee Pasko. Hili likawa doa katika ndoa yake, lililosababisha vurugu na kutoelewana kila kukicha, hasahasa pale Bwana Pasko aliporudi nyumbani akiwa kapandwa na pepo chafu la pombe za kienyeji.

Aligeuka mbogo, akavurumisha matusi na lawama kila kukicha. Leo hii atadai watoto halafu kesho atadai mtoto wa kiume. 

Chumba chao kidogo kiligeuka ulingo wa ndondi kila siku usiku wa manane. Majirani waliuingilia ugomvi huu mpaka pale walipochoka na kuanza kuuchukulia kama ni sehemu ya maisha ya kila siku ya familia hii, wakaanza kuyazoea.

Mazoea...mazoea yakajenga tabia, hakuna hata mmoja aliyechukua hatua.

Mpaka ilipohitimu ile siku ambayo bwana Pasko alikuja akiwa na hasira isiyojulikana ameikotea wapi.

Akampiga mkewe bila huruma na kumjeruhi kwa kipande cha panga butu lenye kutu tumboni.

Akaogopa sana baada ya kushuhudia namna damu inavyofumuka kwa fujo kutoka tumboni kwa mkewe. Pombe yote iliyomhadaa kuwa itamfariji, ikamsaliti. Akaogopa!

Akaamua kutafuta uelekeo na kukimbia kadri miguu yake ilivyoweza kumbeba.

Ukelele usio wa kawaida ukawafanya majirani watoke nje kutazama ni nini kimejiri. Mazoea hayakuchukua nafasi wakati huu.

Bi'Devotha alikuwa hoi...Frola akiipunga mikono yake hewani, macho yakimtazama mama yake pale chini, machozi mengi usoni.

Ilitisha, iliogopesha, ilisikitisha na kuhuzunisha sana kutazama.

Upesi akawahishwa hospitalini kupatiwa matibabu. Na msako mkali dhidi ya bwana Pasko ukaanza. Alitafutwa kwa muda mrefu sana bila mafanikio. Alipotea na kutokomea kusikojulikana.

Huku nyuma, mkewe akabaki hospitalini akipatiwa matibabu. Matibabu ambayo gharama yake isingeweza kukidhiwa na binti peke yake abadani.

Huu mpira ukapigwa pasi kwa jamii yake ya karibu.

Ndugu, jamaa na marafiki wakajichanga mpaka pale walipoweza...lakini wangeweza mpaka wapi?!

Familia kama hii, iliyoishi kwenye mitaa korofi iliyomezwa na umaskini, njaa, maladhi, uhuni, ubakaji, unafiki, wizi na vurugu za kila aina. Wangepata wapi hao ndugu na jamaa wa kutosha kulipia matibabu ya bi.Devotha?!

Tiba yake ikafanyika kwa kipimo kilichostahili malipo yaliyotolewa...mpaka pale kitanda cha hospitali kilipomchoka. 

Bi'Devotha akahamishiwa nyumbani kwake, kidonda chake kikiwa bado hakijapona vyema.

Hakukuwa na namna, ilitakiwa ahudumiwe palepale juu ya godoro lake lililozizoea chaga mbovu, ambazo hazikupenda bughudha ya aina yoyote ile ama sivyo, zinavunjika katika wakati usio na jina.

Baada ya muda fulani, magonjwa ya ajabu ajabu yakaanza kumshambulia. Maumivu ya kidonda yakaikaribisha homa kali na mateso kwenye mwili wa mama yule.

Ule msemo wa asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu, ukamvamia Frola katika namna ya tofauti. Sio kwamba hakuwahi kufunzwa na mamaye, la hasha!

Alifunzwa na kufunzika...lakini sasa alihitajika apate darasa la ulimwengu. Maana kwa wakati huu majukumu yote ya familia yalimgeuzia macho yeye. 

Darasa la ulimwengu likamdai ada kubwa, akiwa kidato cha tatu tu. Akaanza kuugawanya muda wake wa masomo na kumtazama mgonjwa. Akaamua aache masomo ili achague moja, ndipo akaanza biashara ndogondogo ili apate fedha za kumhudumia mama yake na kupata chakula.

Naam,

Ulimwengu haukuwa na huruma kwa huyu binti wa miaka kumi na nane, Frolida Pasko akasulubiwa na maisha. Akaulaani sana ulimwengu, akamlaumu sana Mungu aliyeruhusu yeye azaliwe kwenye familia yenye baba aina ya mzee Pasko.

Jahazi la maisha yao likayumba...wakala kwa taabu, wakavaa kwa taabu na wakalala kwa taabu...sahau kuhusu kusoma, sahau kuhusu majaribu aliyokutana nayo Frola mitaani kutoka kwa wanaume na vijana wenye uchu wa ngono.

Usiku mmoja ulioambatana na mvua za rasharasha sambamba na radi zenye ngurumo za kutisha. Familia hii duni, iliyosahaulika kwenye mgao wa bahati na furaha, ilikuwa imejihifadhi chini ya paa lilelile lenye mabati yenye kutu yanayogongana daima, kukiwa na hali ya upepo wenye fujo.

Kwa mwangaza hafifu wa kibatari kilichokuwa kinakata viuno baada ya kufyonza mafuta bila haya, Frola alikuwa amempakata mama yake.

Ule ukimya wa 'shetani amepita' ndio ulitawala. Kisha ghafla,

"Frolida binti yangu..."

Sauti ya kufifia, iliyolazimishwa kutoka kinywani mwa Bi Devotha ilitamka kwa upole. 

"Abee mama." 

Akajibu, akiwa ameyaruhusu mapaja yake yatumike kama mto wa kulalia, amekipakata kichwa cha mama yake...mikono yake ikijaribu kumliwaza mama huyu ambaye mwili wake umekataa katakata kuuacha urembo wake wa ujanani, japokuwa ulionekana kuwa umepitia suluba na uchovu wa kutosha kuukaribia uzee.

"Nisameheni sana mwanangu,

Najua kuwa nakuchosha, nimekuwa mzigo kwako binti yangu. Haikutakiwa uishi haya maisha hata kidogo!" 

Akakatishwa mara moja,

"Mama...mama usiseme hivyo mama. Wewe sio mzigo kwangu bhana...Na hata siku moja hautakuja kuwa mzigo kwangu mama!" Kwa sauti ya kudeka, Frola akamfariji huku mkono wake ukitambaa taratibu kichwani mwa mamaye. Bado huyu alikuwa ni mama yake, kwa nini asideke? Mtoto hakui mbele ya mama.

"Haya sio maisha niliyotaka uishi mwanangu, sio kabisa! Lakini baba yako...kho!kho!kho!"

Kikohozi kikamvamia, upesi kikombe kilichojaa maji kikasogezwa, Frola akamnywesha mama yake kwa taabu.

"Niliwahi kuwa binti kama wewe enzi zangu. Niliwahi kuwa mrembo kama ulivyo wewe. 

Pale kijijini kwetu, niliweza kuwazuzua vijana wengi sana, ambao walinitamani sana kimapenzi. Wazazi wangu wakanikanya na kunizuia kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi katika umri ule. 

Nilianza kwa kuwaelewa mpaka nilipokutana na Pasko. Huyu akanifanya nisahau makanyo yote ya wazazi wangu, nikampa moyo wangu wote, nikampenda kwa kila namna inayostahili kuitwa upendo wa kweli. Sikujua...kumbe nilimkumbatia shetani mwenye mapembe saba kichwani na mkia mrefu.

"Akanilubuni na kwa mara ya kwanza nikakutana na mwanaume kimwili. Ilikuwa mara ya kwanza lakini haikuwa ya mwisho, tukazini tena na tena. Nikapata mimba na akanishawishi nizitoe mara kwa mara ili tusigundulike kwa urahisi.

Zilikuwa mbio za sakafuni tu...na tulipoishia ukingoni tulikuwa tumechelewa sana. Niligundulika baada ya kukamatwa nikiwa kwenye jaribio la kutoa mimba. 

Hali ikawa zaidi ya hatari, wazazi wangu wakageuka mbogo.

(Anakohoa)

"Baba alinipiga sana akitishia kuniua, nikaogopa na kukimbia. Huko nyuma, akaagiza watu wanitafute. Woga ukanizidia, ukali wa baba niliuelewa kwa maneno na vitendo. Ili kuitafuta salama yangu, nikajitahidi kumuepuka kadri niwezavyo.

Giza la usiku nalo likaanza kuiinamia ardhi katika namna ya kutisha. 

Sikuwa na kimbilio, zaidi ya kuelekea kwa

Pasko, ambaye naye alikuwa katika harakati za kutoroka pale kijijini, hofu ikionekana waziwazi usoni mwake. Akanishurutisha kuwa tutorokee jijini Dar, akidai kuwa huko anao ndugu na jamaa watakaoweza kutupa hifadhi kwa siku chache akiwa anaweka mambo yake sawa.

Ni hapo nilipoanza kuuona waziwazi uongo wake aliokuwa ameuvisha nguo hapo kabla.

Kuwa ana biashara zake nyingi huko mjini na nyumba ya kuishi.

"Bila kufikiria mara mbili, nikakubali huyo shetani anidanganye kwa mara ya pili. Usiku wa siku hiyo hiyo Pasko akanitorosha. Chozi la kwaheri likanitoka nilipokuwa nakiaga kijiji changu cha nyumbani.

Tulifika Dar-es-Salaam tukiwa hoi baada ya ugumu wa safari,iliyokuwa ya kubangaiza.

Ajabu na kweli!

Ile Dar niliyokuwa nasimuliwa na baba yako pale kisimani, haikuwa kama nilivyoikuta.

Mara moja, jiji likanipokea na ugumu wa maisha ukaanza kunisigina bila huruma. 

Mpaka wewe unazaliwa mwanangu...kho! Kho! Kho!"

Kikohozi kikamzidia...

Mara hii alikohoa sana kama aliyekabwa na kitu kigumu kooni. Frola akaruka na kusogeza kikombe cha maji, akamnywesha kwa taabu kabla hajatulia tena na kuhema juujuu.

"Frola..." Akamuita, bado koo lake liko vitani na pumzi zinazopishana kwa nguvu. 

 "Abee mama."

"Nife leo, nife kesho mwanangu.

Kuwa makini sana na wanaume! Hata siku moja, usimwaamini mwanaume...

Fanya yote lakini tambua kuwa wanaume ni watu wabaya." Na hapo kikohozi kikamvamia upya kwa fujo.

Akashindwa kuendelea na Frola akampumzisha juu ya kitanda. Anatetemeka kwa baridi japo tembe za jasho zilionekana kuulowanisha mwili wake.

Frola akayaandaa malazi yake pale juu ya sakafu ya baridi, na kujitanda kwa shuka jepesi kuusubiri usingizi ambao ungejileta wenyewe wakati ambao ungefaa. 

Hali ya hewa huko nje ilitisha sana, ngurumo za radi na miale ya kushtukiza vilizidi kuikoleza historia ya usiku huu na kuufanya uwe wa kukumbukwa zaidi kwenye maisha ya Frola.

Na kweli!

Ulikuwa ni usiku wa kihistoria haswaa..

Alipoamka asubuhi hakuamini kile ambacho macho yake yalikishuhudia.

Bi. Devotha, mama yake kipenzi...alikuwa marehemu.

Angejaza mapipa kwa machozi, angetamka kila aina ya laana, angeulalamikia ulimwengu...lakini asingeweza kuurejesha uhai wa mama yake.

Hakukosea yule aliyetamka kuwa,

"Gharama ya maisha itamhusu marehemu mwenyewe, lakini gharama za mazishi ni ya wale waliobaki duniani...hii haitamuhusu marehemu moja kwa moja". 

Na kweli, mwili wa Bi.Devotha ulirejeshwa upesi mavumbini japo katika namna ya tofauti. Jamii ikachukua jukumu la kuusindikiza mwili wa marehemu kaburini. Ulikuwa msiba wa kushangaza hakika, huu ulipingana na ile methali ya wahenga unaodai kwa kila msiba una mwenziwe. 

Kama mtu angetaka kuifahamu tofauti kati ya kuzikwa na kufukiwa ardhini, basi angejionea mwenyewe katika msiba huu mubashara. 

Hakukuwa na ndugu wa karibu zaidi ya Frola peke yake. Akaachwa katika shimo la majonzi akiwa mkiwa, yatima ambaye chuki za maisha magumu ya dunia na laana zake vyote vilikuwa vimejiandaa kumshambulia kwa uchu.

Dunia ikamuinamia, akapoteza tumaini la maisha. Kama lilivyo jani la mti lidondokavyo kutoka kwenye tawi lake, mzee Pasko alipotea moja kwa moja. Achana na kutojulikana alikimbilia wapi, jamii ilimsahau moja kwa moja.

Huruma pekee aliyoonewa Frola, ni kusikitikiwa tu, maana hali aliyoachwa nayo haikupe

Frola akashika hatamu za uongozi wa familia hii mpya inayohusisha mtu mmoja tu. Yeye mwenyewe akiwa baba na yeye mwenyewe akiwa kama mama pia. 

Pesa kiduchu za rambirambi zilizokusanywa zisingemtosha kulisukuma gurudumu la maisha yake. Mtoto huyu wa kike akaamua kujifunga kibwebwe na kutafuta shughuli yoyote ile... 

Mradi mkono uende kinywani,

Hana wa kumlisha abadani,

Alishaitupa kalamu zamani,

Usishangae kutomuona shuleni,

Binti kibwebwe kiunoni,

Kafunga aingie vitani,

Kupigana na adui gani,

Nani mwingine zaidi ya umaskini?

Akaanza kwa kufanya kazi kwenye migahawa kadhaa, lakini huko hakudumu sana kabla hajasumbuliwa na wateja wa kiume wa migahawa hio.

Hawa walimhusudu katika namna ya kugombea na kushabikia kuhudumiwa na yeye peke yake. Wakamsifia kwa urembo wake na haiba yake nzuri, wengine wakaanza kumtongoza. 

Ni usiku mmoja tu, ulitosha kabisa kumkaribisha kwenye dunia mpya.

Siku hii alichelewa kurudi nyumbani baada ya kuhudumia wateja kwenye mgahawa ule mdogo aliokuwa ameajiriwa.

Hakujua kama alikosea kona au alipita kwenye kona hio katika muda usio sahihi. Yeye alishtukia ameparamiwa na kuzibwa kinywa kwa nguvu. Kisha akaburutwa mpaka kwenye jumba ambalo halijamalizika ujenzi wake. 

Bila salamu, wala kujitambulisha.

Vijana watatu mashababi walioonekana kuwa walimpania kwa muda mrefu, wakamvamia na kumbaka kwa zamu.

Frola alilia sana akihitaji msaada na hakukuwa na msaada wowote ule kwa ajili yake usiku huu eneo lile. 

Baada ya kukidhi haja zao za kimwili, vijana wale waliokosa utu wakapotea gizani. Wakamuacha pale Frola akiwa hajielewi, amezirai? Amekufa? Hawakujali, ili mradi wamemaliza haja zao basi. 

Fahamu zilimrejea Frola akiwa kwenye chumba cha matibabu hospitalini. Hakujua amefika vipi pale, hakujua amelala pale kwa siku ngapi. Alichokiona ni dripu iliyofungwa kwenye mkono wake wa kuume na akagundua kuwa kuna tabasamu lipo pale kando yake likimtazama.

Mwanamke mmoja mnene wa kadri, aliyevaa mavazi ya gharama kiasi na kuukamilisha urembo wake kwa vipodozi vilivyoigeuza rangi ya uso wake kutoka kwenye asili yake mpaka kuwa mwekundu.

"Pole kipenzi!..." 

Alitamka akiwa bado anatabasamu. Tabasamu kama hili alikuwa amewahi kuliona mahala...aliliona wapi?

Mama mzazi!

Lilikuwa tabasamu kama la marehemu mama yake. Tabasamu la upendo.

Halafu ghafla akaukumbuka unyama aliotendewa na wale vijana madhalimu.

Chozi likamdondoka Frola.

"Pole mamy...daktari atakuja hivi punde!"

Akatamka huku akifanya jitihada za kumfunika Frola kwa shuka lile jeupe.

"Niite madam Salome...ama waweza kuniita Madam Sally."

Akajitambulisha kwa mara ya kwanza maishani mwa Frola.

Mara ya kwanza na mara moja tu!

Na ni huyu akawa mama mpya kwa Frola, mama aliyesababisha apate jina jipya kabisa la Bebe.

Ni huyuhuyu,

Madam Sally amempigia simu na kumuuliza ni wapi alipo mpaka muda huu.

Na kwake ndiko anakoelekea...

ITAENDELEA.....

Previoua