Reader Settings

MALAYSIA-KUALA LAMPUR.

Wakati Tanzania ikiwa ni saa sita za mchana  ndani ya jiji la Kuala Lampur  nchini Malaysia ilikuwa ni saa kumi na moja za jioni.

Nje ya mlango wa kuingilia wodi ya VVIP katika hospitali ya  Gleneeagles  walionekana wanausalama  wakiimarisha ulinzi  , kwa jinsi sura zao zilivyokuwa  zikionekana  hazikuwa za wasiwasi  wala  huzuni  bali  ni za  umakini  zaidi kama kwamba wanahakikisha kile kinachoendelea ndani ya hio wodi kubakia kuwa siri.

Dakika kama kumi hivi  alionekana mwanaume wa umri wa makamo maji ya kunde akisogelea eneo hilo , alikuwa ni msaidizi wa mheshimiwa  Raisi  Samweli Elias Mbilu  ambae anafahamika kwa jina la  Maulidi .

Maulidi anashikiria  majukumu yote ya Chief of Staff  lakini licha ya hivyo alikuwa ni moja ya watu ambao wanaaminiwa sana na mheshimiwa.

“Nipo hapa kwa ajili ya  kuonana  na mheshimiwa , Kanali”Aliongea Maulidi  akiomba ruhusa kutoka kwa kitengo cha ulinzi  kinachongozwa na mpambe wa raisi Kanali Ashrak Chipyangu.

Afande Ashrak aliangalia saa yake  na  alionekana kutingisha kichwa kwa ishara ya kukataa.

“Mheshimiwa  katoa maagizo kuruhusu  mlango wake kugongwa baada ya dakika   therathini,  yupo na mgeni”Aliongea  Ashrak  na kauli ile ilimfanya Maulidi kukunja sura  , alijua  lazima  mgeni atakuwa mwanamke maana kauli hizo ni kama ashazizoea.

Maulidi hakuwa na hiyana zaidi ya kusubiri , isitoshe alikuwa akimjua bosi wake alikuwa akiongoza kwa kupenda  wanawake.

Dakika kumi za kusubiri zilipita na hatimae mlango wa  wodi hio ulifunguliwa kwa ndani na alionekana mwanamke  mrembo akitoka.

Mwanamke yule mara baada ya kukutanisha macho na Maulidi alimkonyeza  kwa ishara ya kichokozi  na kisha kimadaha akaanza kuzipiga hatua kuondoka ndani ya hilo eneo.

“Kanali  naungana na wewe kumchukia huyu  kahaba”Aliongea  Maulidi akimwangalia Kanali Ashrak kwa  tabasamu la uchokozi.

“Sijawahi  kusema namchukia Mr Maulidi”Aliongea Kanali kikauzu.

“Hata mimi naona Afande, unaonekana kumpenda sana”Aliongea  na Kanali hakujali maneno ya kinafiki ya  Maulidi  na alimpa ishara ya kusubiri wakati akimtaarifu mheshimiwa ujio wake.

“Mheshimiwa Mr Maulidi yupo hapa  anataka kuonana na wewe”Aliongea  Kanali na bila sauti upande wa ndani kusikika  Kanali alimfungulia Maulidi  mlango  na kisha kuingia.

“Mheshimiwa  sijawahi kumpenda huyu Tresha hasa katika  nyakati kama hizi”Aliongea Maulidi akimwangalia mheshimiwa Eliasi ambae  alikuwa  akifunga mkanda  wa Bathrobe vizuri.

“Kama ungempenda  inamaanisha  hana vigezo vya kuwa na mimi , nani asiejua  Maulidi  anachukia  wanawake warembo”Aliongea  Mheshimiwa Eliasi huku akitoa tabasamu  lililojaa  kejeli  akisogelea  chupa na kujaza mvinyo kwenye glasi.

“Nazungumzia  kwa kujali usalama  wa misheni zetu mheshimiwa , huu ni muda wa kuwa makini”

“Shida yako upo siriasi sana , wakati huu  wengi wakijua nipo  hospitalini  nadhani ingekuwa vizuri  kuonana na madaktari ili kutibu shida yako ya  kisaikolojia ya kuogopa wanawake warembo”

Ilikuwa ni kweli  Maulidi  Ally Mfinanga   ni mgonjwa wa Caligynephobia,ugonjwa ambao unamfanya mtu kuogopa wanawake  warembo , inasemekana  wakati akiwa katika misheni nje ya nchi aliwahi kupatwa na tukio  ambalo lilimpelekea kupata ugonjwa huo  wa kisaikolojia.

“Nipatie habari za kinachoendelea”.

“Nimepokea taarifa kutoka  Tanzania, mstaafu ameridhia  Abubakari  Kassimu  kuchukua nafasi ya Marehemu Jongwe, japo  maamuzi hayajatangazwa kwa wanachama wote lakini  huo ndio msimamo  wa  chama kwa sasa”Aliongea na kauli yake  haikumbadilisha  muonekano Eliasi.

“Sijawahi kumuona  Mgweno  kukubali  kirahisi namna hii , inaonekana  familia ya Wanyika  wamefanikiwa kumuweka mkononi”Aliongea huku akipiga pafu la  mvinyo.

“Mheshimiwa licha hili kuwa na faida  kwa upande wako lakini nina wasiwasi  na matokeo yake  kwa nchi yetu”Aliongea Mauidi.

“Niambie Mzalendo, wasiwasi wako ni nini?”

“Licha ya  kwamba inaonekana Wanyika  ndio wamesimamia kila kitu lakini udhaifu wa mheshimiwa  Mgweno  upo chini ya  Raisi Habimana”

“Papa ni mkali baharini akitolewa nje ya maji anakuwa Kambale, Habinana anaweza kuwa na  udhaifu wa Mgweno lakini hauna nguvu yoyote pasipo ya  msaada wa Wanyika”Aliongea  na kumfanya kuchanganyikiwa kidogo.

“Unadhani mimi Eliasi  Mbilu naweza shiriki katika kitu ambacho kinahatarisha usalama wa taifa , wengi wanaamini nipo chini ya  Mgweno  lakini mimi nipo  mwenyewe, Ushawahi kujiuliza kwanini Wanyika  licha ya kutokuwa na umaarufu ndani ya  Tanzania lakini wana nguvu kubwa?”Aliuliza  Eliasi.

“Mara nyingi nimekuwa wa kujiuliza hili swali , ukilinganisha na familia ya Mgweno,  Wanyika utajiri wao na umaarufu wao ni mdogo mno?”

“Ushawishi ni nguvu, katika dunia hii ili uwe na nguvu  ya  ushawishi sio lazima  uwe  tajiri au mwanasiasa, kinachoangaliwa ni ushawishi  unaobebwa na historia  katika kuchangia kile wanachokiita Lengo Kuu moja la Dunia, Mgweno  ana ushawishi ndio  lakini katika jamii  ya kimataifa inayosimamia Lengo kuu moja  la Dunia haimtambui kwasababu ushawishi wake  ni wa msimu na umetokana na siasa  na si vinginevyo, lakini tukija kwa Wanyika  wanatambulika kama Chimbuko, kama familia inayobeba  damu asilia ya nchi, damu ambayo ambayo wanaamini ina mchango mkubwa kuyafikia malengo”Aliongea  na kumfanya Maulidi kuonekana kama hajaelewa.

“Huwezi kuelewa  ninachomaanisha kwasasa , wengi hawajawahi kuelewa , hata Mgweno hajawahi kuelewa, lakini sasa hivi atakuwa anaanza  kuelewa, hata hivyo tukiachana na hilo, sijasikia taarifa   yoyote kutoka kwa  Keita”Aliongea  Mheshimiwa na kumfanya Maulidi kukamaa mwili.

“Mheshimiwa   hilo lilikuwa swala la pili  kuripoti”

“Nini kimetokea?”

“Keita katuma  taarifa ya kuvunja mkataba na malengo yake ya kupitisha  siraha kupitia  bandari  za Tanzania atafikiria upya”Aliongea  na kumfanya mheshimiwa kukunja sura.

“Vipi kuhusu misheni tuliompatia  , ameweza kumtorosha  Chindez?”

“Hakutoa maelezo ya kutosha nilipomuuliza , ila kuna taarifa ambayo  imenifikia kutoka kwa chanzo chetu,  Keita mara baada ya kukutana na Hamza  alimgeuka Pancho na kumuua  na  bado  haijaeleweka sababu ya kufanya hivyo”Aliongea na kauli ile ilimfanya kushangaa.

“Kwanini  kila mara nasikia hili jina la Hamza katika kila mpango ulioharibika?”Aliongea huku akiwa  amekunja sura.

“Bado tunaendelea kumfutilia mheshimiwa ili kumjua ni nani haswa”Aliongea lakini hata hivyo  mheshimiwa alionekana  kutokuwa na wasiwasi.

“Yulia  anasemaje  juu ya hili?”

“Amesema Keita ulikuwa  ni mpango wa dharula”Aliongea na kumfanya  Eliasi kumwangalia Maulidi kana kwamba hakuwa amemsikia vizuri.

“Yaani  wamenitoa Tanzania kuja kujifanyisha mgonjwa  hapa  Malaysia  kwa ajili ya mpango wa Dharula?”

“Mheshimiwa sidhani kuwepo hapa ni mpango wa Dharula , labda kuna kinachoendelea  pasipo ya sisi kujua”

“Hilo ni jukumu lako  la kujua kila kitu kinachoendelea  na kunitaarifu , unadhani nakulipa  posho ili uje kunielezea vitu  vya kukisia?”

“Nitafuatilia mara  moja mheshimiwa”Aliongea Maulidi  akijitetea.

“Ili niweze  kuishi  kwa  amani baada ya kustaafu ni  kutokufungamana upande wowote ,  Wanyika wanaweza kumdhibiti Mgweno  kwasasa lakini  mimi namjua Mgweno sio mtu  wa kukubali kirahisi  kupokonywa ufalme wake , isitoshe mizizi yake imesambaa kila kona ya nchi”

“Mheshimiwa unapanga kuchukua hatua gani?”

“Licha ya kwamba  mpango wa kumuua Jongwe  ulipangwa na Wanyika   kuna uwezekano mkubwa mpango huu ukanitengenezea udhaifu  na hata nikistaafu madili yangu mengi kukwama kutokana na kukosa  nguvu serikalini ,Maulidi unadhani  ni kwanini Mgweno  licha ya kuonekana kuwa na ushawishi mkubwa bado  ameshindwa kutimiza malengo yake?”.Aliuliza na kumfanya Maulidi kufikitiria kidogo.

“Moja ya sababu kubwa  ni kushindwa  kuimarisha ushawishi wake upande wa underworld Societies”

“Safi kabisa, tafsiri ya underworld ni jamii  ya  watu  ambao wapo nje ya  mfumo wa kawaida wa  kimaisha , katika jamii hizi kinachoangaliwa zaidi  ni nani  anaunganisha  mtandao  kutoka eneo moja kwenda eneo lingine ,  Mgweno alichokosa  ni mtandao ndio maana  mara zote  alikuwa akipambana  kuumiliki mtandao wa  Chatu lakini tamaa zake zimemfanya  kujiingiza kitanzini yeye mwenyewe”

“Mheshimiwa unamaanisha nini  kuhusu tamaa?”

“Tamaa  ni kufanyia  kazi malengo mengi kwa wakati mmoja. Wasiliana na Dina nikirudi nchini nataka  kuonana nae”Aliongea  Mheshimiwa na kumfanya  Maulidi  kushangaa kidogo.

“Mheshimiwa  lakini  kuna uwezekano Dina anafahamu  mpango wa  kutaka kusingizia  kundi lake kujihusisha  na kifo cha Jongwe”.

“Kama ingekuwa rahisi kusingizia mtandao wa  Chatu  kuhusika na  mauaji na kuondoa nguvu yake basi Mgweno angefanikiwa  muda mrefu sana , Mtandao wa Chatu sio mtandao  ambao unaweza kuharibiwa kwa hila nyepesi nyepesi, ukisikia Chatu  ni  kama wamiliki wa geti ndani ya ukanda wa Afrika mashariki na  kati la kuingilia kuzimu , Mgweno alijaribu na matokeo yake akatengenezewa udhaifu ambao  unamfunga mpaka leo hii”

“Mheshimiwa  kama  walikuwa wakiamini Chatu haiingiliki imekuwaje   wakaandaa mpango  wa namna  hii?”

“Kuna uwezekano ni hila za Yulia kutaka kumfahamu  Hamza  au kuna sababu nyijngine nisioijua,  Kadri  huyu Hamza anavyozidi kujihusisha katika  haya maswala ndio anavyozidi  kujiweka wazi  yeye ni nani haswa , nafikiria hii  ndio  sababu , isitoshe si amekuambia Keita  ni  mpango  B wakati mwanzoni alituaminisha ni mpango  A , licha ya kumwambia ni mpango kichaa”

“Mheshimiwa nadhani naanza kupata kitu  pia,  Yulia anajaribu kumtengenezea  Hamza matatizo kumzunguka ili  kadri atakavyojaribu kuyatatua ndio anavyozidi kujiweka wazi yeye ni nani?”

“Nadhani ushaanza kupata picha”

“Kwaninni   sasa mheshimiwa  unataka kuwasiliana  na  Dina?”

“Maulidi , inamaana  hukunielewa  maana ya maneno yangu tokea  mwanzo”

“Sijakuelewa moja kwa moja mheshimiwa”

“Wasiliana na Dina  nataka kuonana nae , kama nilivyosema  Chatu ni Lango la kuingilia  kuzimu  na mimi  nataka kuingia huko  ila  lazima niwe  na mtu wa kuniongoza, sitaki kuwa kama Mgweno  ambae  anadhani kila kitu kinaweza kuwa  chake  kwa kutumia mabavu”

“Mheshimiwa kwahio mpango wako ni  kuimiliki Chatu  kidogo kidogo?”

“Yes! Slow but sure”

*****

“Nani kakuambia?”Aliuliza Hamza.

“Haina haja ya kubadilika kiasi hicho ,  hujafanya  dhambi hii ni taarifa njema”Aliongea Eliza.

“Eliza nilipaswa kukuambia mapema   kuhusu hili , nilikuwa nikipanga kukuambia tokea muda mrefu”

“Huna  haja ya kujielezea Hamza, naelewa unachomaanisha ,  hata hivyo  sidhani mapenzi yetu yalikuwa siriasi kihivyo , siwezi kusema umenisaliti  au nini, isitoshe pia nashindwa  hata kujua namna  ya kukushukuru  kwa kunisaidia kumpeleka mama yangu nje ya nchi kwa ajili ya kutibiwa , sio hivyo tu umeniokoa   mara kibao , kwangu  wewe nakuchukulia kama mtu  mzuri , hivyo nakutakia  wewe na bosi Regina  furaha…”

Eliza alikuwa akiongea huku akiwa ametabasamu  lakini  upande wa Hamza  maneno  hayo yalimfanya kujihisi ni kama anatambaliwa na mdudu mgongoni.

“Eliza haya maneno yako  ni ya kweli?”Aliuliza Hamza huku akiwa amekunja ndita.

“Kabisa, nawatakia kila  la  kheri , sisi ni watu wazima  hakuna haja ya  kudanganyana , isitoshe  wewe kuoa haimaanishi  hatuwezi kuwa marafiki”

“Lakini  Eliza nakupenda mno ,usiniambie  hukua na hisia zozote juu yangu?”

Eliza alijikuta  mwili wake ukikakamaa  wakati  cheche   za mapenzi zikionekana kwenye macho yake ,  alionekana alikuwa akijitahidi kujizuia kwa kuvuta pumzi nyingi.

“Eliza kadri unavyoonyesha kuwa  sawa  unazidi kunipa wasiwasi ujue”

“Usijali Hamza , mimi nipo sawa  kabisa , japo ni kweli nahisi kujutia  lakini  bado najihisi ni  mwenye bahati kukutana na  wewe  pamoja na bosi  Regina , wote   ni watu wazuri mno kwangu”

Ukweli ni kwamba  Hamza  alikuwa anakosa ujasiri wa kusema  ndoa yake  ni ya mkataba  kwa ajili ya kumsaidia   Regina kupata hisa  za kampuni kutoka kwa bibi yake, aliona hata akisema, ingekuwa  kisingizio  kisichokuwa  na  msingi, maana iwe ni kwa mkataba au  kwa mapenzi hakulazimishwa kufanya maamuzi.

Hamza aliishia kumwangalia Eliza bila  kupata neno la kuongea , kosa kubwa kwake lilikuwa ni  kumdanganya  Eliza tokea mwanzo.

“Usiniangalie hivyo , najua unampenda sana Bosi  , ile siku tulivyopata ajali  na namna ulivyowahi kuwaza  usalama wake niliweza kuona ni kwa namna gani  ni mtu wa muhimu kwako , kwanzia sasa sitaki niwe kikwazo kwenye mahusiano yenu ya   ndoa, hivyo  naomba   mambo yetu yaishie kwenye  maswala ya kikazi”

Ilionekana  Eliza  aliweza kugundua nafasi yake ndani ya moyo wa Hamza  kutokana  na ile ajali ,  kwake aliamini kama kweli Hamza alikuwa akimpenda basi siku ile asingemwacha akiwa  na  hofu  vile na kumkimbilia  Regina , kimantiki  ilikuwa ni sawa  kwa Hamza kukimbilia kwenda kuona usalama wa  Regina lakini kihisia  kwa Eliza alipatwa na hisia  za kutelekezwa njiani.

“Eliza ijapokuwa  naweza kuonekana  kama  nimekosa aibu , lakini ukweli ni kwamba  wewe na  Regina  ni watu muhimu kwangu , sitaki kukupoteza kwasababu ya ndoa yangu  na Regina”

‘Wewe…!”Eliza alijikuta akikosa neno  na alimwangalia  Hamza kwa mshangao ni kama hakutegemea ile kauli.

“Kwasababu tumefikia hapa sina haja ya kukuficha chochote , lakini ukweli  ukiachana wewe na  Regina kuwa  watu muhimu kwangu lakini vilevile nina mwanamke mwingine”Aliongea Hamza akiwa siriasi.

“Hamza kwanini unanifanyia  hivi?”Aliuliza  Eliza huku akijikuta  ni kama  mtu anaejutia , hakujutia kwasababu anaachana na Hamza bali kwasababu tayari ashafungua moyo wake  kwa Hamza muda mrefu tu  na anashindwa namna ya kuufunga.

“Kwasababu  mimi ni mimi na sina haja ya kukudanganya tena”

“Wewe ni mbinafsi”

“Ndio mimi ni mbinafsi , na ndio maana sitaki kukupoteza”

Eliza  alikuwa  na hasira mnno  na kama  ni mwanamke mwingine  kwa jinsi ambavyo alikuwa akijisikia kutokana na alichokisema Hamza , angekuwa ashampiga  kibao  tayari, hakuamini mwanaume ambae alikuwa akianza kumpenda  alikuwa na  mwanamke mwingine , kwa Regina tu imemfanya kukosa usingizi lakini  kuna  mwingine.

Lakini hata  hivyo  kutokana  na utu uzima wake na uzoefu katika maisha yake hakutaka kuruhusu akili yake kudanganywa na moyo wake ,  mtu kama Hamza ambae ameonyesha   uwezo wa  tofauti tofauti usio kuwa  wa kawaida , ilikuwa ni ngumu  kuwa Single , isitoshe  pia hakujua maisha ya Hamza ya nyuma yalivyokuwa.

‘Nadhani  nakuelewa , isitoshe  sina ninachojua  kuhusu maisha yako ya nyuma , lakini ninaweza kuotea wewe sio mtu wa kawaida , unaonekana kuwa na nguvu kubwa,  upande wangu mimi ni msichana   kutoka familia ya kawaida niliebahatika kuajiriwa katika kampuni kubwa  sioni kama nina haki ya kukukosoa wala kukuhukumu , kitu pekee ninachoweza kufanya  ni kuishinda aibu ya moyo wangu”

“Eliza  unajaribu kumaanisha nini?”

“Ninachomaanisha ni kwamba siwezi  kukataa kama sikuwa na hisia  za kimapenzi kwako na upo  tayari  kuzipokea,  lakini licha ya hivyo najali utu wangu ,  hata kama sistahili kukataa mwanaume kama wewe, sitaki kumsaliti  Regina”

“Nimekuelewa ,  lakini vipi kama Regina anakubaki tuendelee na mahusiano yetu , bado utaniacha?”

“Labda..”

“Regina  hana shida na sisi  kuwa katika mahusiano ,  kwanza hanipendi  la sivyo asingeniambia  nitafute mwanamke mwingine”

“Sio kweli ,  Regina anaweza kuonekana  hakupendi lakini ukweli anakupenda la sivyo asingekubali mfunge ndoa,  nimemjua  bosi  kwa muda mrefu sana  na nailewa tabia yake ,  kama angekuwa hakupendi hata  angepigwa mpaka kufa asingekubali”Aliongea Eliza.

Hamza mara baada ya kusikia maneno hayo alishindwa kujiuia  na kuona yana ukweli wake , ilionekana  swala la wao  kusajili ndoa  halikuwa la kimkataba pekee  ila  kuna sababu  nyingine , vinginevyo kwa ukiburi aliokuwa nao Regina asingekubali  ndoa kirahisi  hata kama  ni kuikosa kampuni.

Eliza alionekana kuhitaji muda zaidi , alikuwa akimpenda  Hamza lakini vilevile hakutaka kuwa mchepuko , katika maisha  yake alitamani  kuitwa  mke wa mtu na sio mchepuko wa mtu , ijapokuwa  ni kweli alikuwa akimpenda Hamza hakutaka kuziruhusu hisia zake kumpelekesha , alitaka kukaa chini na kufikiria.

Mara baada ya chakula cha mchana  safari ya kurudi ilianza na  hawakuchukua muda mrefu barabarani mpaka kufika, Eliza alimsisitizia Hamza  kwa  kipindi hicho wapunguze ukaribu wao na  uendelee kuwa  wa kikazi zaidi ,  Kwasababu Eliza alionekana kuwa siriasi Hamza  hakuona haja ya kuendelea  kumpa wakati mgumu , isitoshe  yeye ndio alieonekana kuwa na makosa , lakini alimuahidi ikitokea Regina  akikubali  waendelee basi atahakikisha hampotezi.

Baada ya Eliza kuelekea idara ya Finance upande wa  Hamza alichukua lift iliompelekea moja kwa moja mpaka  juu , akitaka kwenda  kuonana na Regina maana alimpigia kuwahi.

Dakika ambayo lift inafunguka  Regina alikuwa mbele yake akionekana alikuwa tayari   ashamaliza siku.

“Huna haja ya kutoka tunaelekea hospitalini”Aliongea Regina huku akimwangalia  Hamza  bila ya kubadilisha  muonekano wake

Muda huo wakati Hamza akimwangalia mrembo huyo ni kama anakumbuka maneno ya   Eliza kwamba  Regina anampenda ila  ni kutokana na kwamba anamwigizia tu  na ilimfanya kutabasamu.

Hamza anaweza kuonekana kutokuwa mtu wa kawaida na ambae  ana uzoefu wa aina tofauti  tofauti lakini   ni mwanaume kama mwanaume  mwingine  tu, hakuna  mwanaume ambae hatojisikia vizuri kuhisi mwanamke mrembo kama Regina anampenda.

“Sawa bosi , nitaendesha gari”Aliongea huku akiwa na tabasamu kama pana usoni ,   Regina  kwa jinsi alivomuona Hamza akitabasamu  alishindwa kujizuia na kujihisi kitu cha ajabu moyoni mwake lakini hisia za bibi yake kutokuwa na muda mrefu kuishi zilizima hali ile haraka.

Wakati Hamza akiendesha gari kuelekea  hospitalini , alikuwa amefungulia mziki  laini  ambao ulimkonga moyo wake  na kujikuta akiangalia kio cha nyuma kuona kama  na Regina anafurahia mziki.

“Wife , vipi  nizime mziki?”

“Usiniite na hilo jina lako”

“Bado   hasira hazijaisha tu, basi nitakuitwa babe” Aliongea lakini Regina  hakutaka kujibishana nae.

“Mmewezaje kupata hela  yote?”Aliuliza Regina , ukweli ni kwamba tokea mwanzo alishachukulia deni lao  kwa kampuni ya Dede ni hasara maana haliwezi kulipwa, licha ya kwamba   bosi Laizer  alikuwa na uwezo wa kulipa lakini  ni ngumu kutoa milioni mia nane yote kwa wakati mmoja.

Hamza  muda huo aliona  hio ndio nafasi  adhimu kumpigia debe  Eliza  ili hata ikitokea wakiendeleza mahusiano yao  Regina  atoe baraka zote.

“Mimi sikufanya chochote  kila kitu alimaliza  Lizzie, ana uwezo mkubwa sana  likija swala la kazi , ni mwanamke mmoja mwenye   msimamo sana , tukija kwenye tabia yaani hata usiseme..”

“Lizzie!”Regina alijikuta akimkatisha  Hamza mara baada ya kusikia  Hamza akitaja jina la  Eliza kwa kulibadilisha kuwa Lizzie.

“Naona leo ndio unakiri , Eliza ndio mpenzi wako”

“Kwani nilishawahi kukataa .  halafu unajua tokea muda mrefu unajikausha , kama ungekuwa hujui ungemwambia kuhusu   kusajili ndoa?”

“Unaongea ujinga gani wewe , ni saa ngapi niliongea na  Eliza kuhusu kusajili ndoa? , nilishasema  hii ni siri yetu , kama ni kujua  mna mahusiano  zilikuwa hisia tu  baada ya ile siku  wakati wa mashindano niliona namna mlivyokuwa  mkionyesheana ishara za kimapenzi”Aliongea Regina kwa sauti kubwa kana kwamba Hamza alikuwa na shida ya masikio.

“Haha.. Regina unajua nini huna haja ya  kuficha  wakati kila kitu kipo wazi ,  leo  Eliza kaniambia anajua  kuhusu sisi kusajili ndoa ,  kama sio wewe  uliemwambia nani mwingine?”

“Sijui hata unaongea nini!, Hamza nakwambia ukweli sijaongea chochote  na Eliza kuhusu maswala ya ndoa”

“Kama sio wewe  ni nani sasa?”Aliongea  Hamza lakini  kwa jinsi Regina alivyokuwa akionekana , ilionyesha hakuwa akidanganhya.

“Mimi sijui lakini kweli sio mimi”

“Nilivyoona umempatia gari la bei  ghali  na alivyoniambia anajua kuhusu sisi nilijua umempa gari kwa ajili ya kumtuliza , kumbe sio wewe?”

Kwa bahati nzuri au mbaya , kitendo cha Hamza kutamka hayo  maneno hayakumfurahisha kabisa  Regina na alinuna palepale  zaidi ya alivyokuwa mwanzo

“Unaongea nini wewe , kwahio unadhani  nimempa gari ili niwe  na wewe, unajikuta nani kwa mfano”

Hamza mara baada ya kusikia sauti hio ya chuki kutoka kwa Regina alijikuta akinywea , hakujua kama maneno yake yalikuwa  na zaidi ya maana

“Sijamaanisha hivyo ,  wewe ni mwanamke unaejiamini na mrembo  huna haja ya kujishusha mbele yake , ninachomaanisha  niliamini  kutokana na moyo wako mzuri  umempa kwa nia  njema tu…”

Hamza  alitaka kujielezea kadri awezavyo lakini aliona kadri alivyokuwa akiongea ni kama  anazidi kukosea.

Regina upande wake alikuwa na hasira kiasi kwamba  kifua kilikuwa kikipanda na kushuka.

“Kwahio unadhani  nakupenda sana kiasi cha kutaka kukugombania  na Eliza , mshenzi  wewe shuka kwenye gari yangu?”

“Regina  usiwe na hasira , nimekosea kweli , sikumaanisha hivyo , sijui hata ubongo wangu unafikiria nini mpaka kuonge ahivyo , nisamehe”

“Eti nimekosea  , hiko ndio kilichopo  ndani ya moyo wako”

“Hamna, sio kweli”

“Ndio unachowaza”

“Kila mtu anakosea Regina , haina haja ya  kutafuna meneno yangu kama yalivyo”

“Kutafuna!, kwahio unaniona nimekuwa mbuzi ,unamaanisha  naongea kitu ambacho hakina msingi?”

“No, no , no , no… Regina sio hivyo…, punguza jazba basi , mwenyewe  nina mawazo kibao hapa , yaani hata  sijui nani kamwambia nimekuoa?”

“Shenzi  wewe , mjinga…  usije kuniongelesha tena”

Regina  alikuwa  amekasirika kiasi cha kutaka kutukana kila  aina ya tusi analolijua   lakini alishindwa kupata matusi na kujikuta  macho yakiwa mekundu , aliishia  kugeuzia macho yake  nje ya dirisha la gari  ili  asionekane  anataka kulia.

Hamza  alijikuta akihema kwa nguvu na kujiambia anapaswa kujifunza vizuri kiswahili maana  kauli zake zinaonyesha kubeba zaidi ya maana na kumkasirisha mrembo huyo kila akiongea,

Mara  baada ya kufika  hospitalini na kwenda wodi ya Bibi Mirium walichokiona  kiliwashangaza , Bibi yake  Regina ni kama  alikuwa ameshapona na  amekaa kitandani akipiga stori na  Shangazi huku wakicheka.

“Bibi  hali yako imeimarika , naona dawa zimefanya kazi”Aliongea  Regina  huku akiwa na furaha kubwa , lakini upande wa  Hamza alizidi kushikwa na huzuni .

Hamza alijua fika unafuu huo aliokuwa nao  Bibi Mirium  ni ishara  kwamba muda wake wa kuondoka umewadia , hio ni kutokana  na uzoefu  wake.

Bibi huyo  aliishia kuinua  mkono wake na kumshika Regina mashavu  huku  wakati mmoja akimwangalia  Hamza

“Hamza  kuna kitu nataka kukwambia mimi mwenyewe”

“Nakusikiliza bibi niambie ni kitu gani”

“Kuna  kitu ambacho mume wangu alinipatia  kwa kuniusia nimpatie mume wake Regina  na kwasababu ni wewe  nadhani ndio muda wa kupokea”Aliongea  na kumfanya Hamza mwili wake kumsisimka , pengine bibi huyu alikuwa akiharakisha  swala la yeye kufunga ndoa na Regina kwa ajili ya kukamisiha  misheni yake ya kumpatia kitu hicho.

Muda huo  Bi Mirium  alipandisha mikono yake  shingoni na  kufungua mkufu aliokuwa ameuvaa  na  palepale ilionekana  pete iliokuwa imening’inizwa katika huo mkufu , ilikuwa ni pete ambayo  licha ya kwamba ilionekana kama ya kawaida lakini ilikuwa  ni ya aina yake, Hata  Hamza alishindwa  kuelewa imetengengezwa na madini gani.

Regina upande wake alionekana kutokuwa na mshangao , ni kama ameshawahi kuona hio pete muda mrefu.

“Bibi kwanini unataka kumpatia hio pete wakati sio  mwanafamilia?”Aliongea Regina , ukweli ni kwamba hata yeye alishangazwa na maneno ya  bibi yake , alikuwa akiijua hio pete ilikuwa ni ya thamani sana kwa  babu yake na hakuwahi kuivua kipindi cha uhai wake.

“Hamza  Tayari ni mume wako hivyo ni mwanfamilia  na  dakika anayovaa hii pete  amerithi nafasi ya babu  yako kama  kiongozi wa familia”Aliongea Bibi Mirium huku akionekana kuwa siriasi.

Lakini upande  wa Regina alijikuta akisaga meno  baada ya kuona hana uwezo  wa kumkatalia bibi yake , aliamua  kutulia huku akijiambia  atampokonya Hamza baadae.

Upande wa Hamza alijikuta  akiingiwa na furaha  akitamani kuona pete hio , hivyo  kwa tabasamu kama  lote aliipokea kwa mikono miwili  na unyenyekevu  mkubwa   kama   vile anapokea mkate  wa sakramenti kanisani.

“Bibi   wewe ni mkarimu  mn…”

Hamza alitaka kuanza kumsifia  Bibi Mirium lakini alijikuta akiishia  katikati mara baada ya kuona kitu kisichokuwa  cha kawaida juu ya pete hio.

Kulikuwa na mchoro wa ajabu juu ya hio pete  na kwa namna ulivyowekwa ni kama vile  ni  pete  ya kupigia mhuli.

Hamza alijikuta  mapigo yake yakienda mbio huku akizidi  kuikodolea  macho.

“Unakodoa macho ya nini sasa, hujawahi kuona pete zenye mchoro wa mhuli”Aliongea Regina huku ikionyesha  ni dhahiri hakufurahishwa  Hamza kupewa ile pete.

Tofauti na Hamza hakuwa akishangaa  kama pete hio  ni ya muhuli , alikuwa akishangaa mchoro uliokuwa katika pete hio   huku akijiuliza maswali  babu yake  Regina aliitolea wapi.

“Bibi  hii pete  inaonekana ni ya thamani  kubwa… sioni kama ni sahihi kuopokea”

“Unaongea nini ,  inamaana unakataa zawadi yangu?”Aliongea   huku tabasamu lake likimpotea.

Hamza alijikuta akikosa namna ya kujitetea , aliona kitu pekee cha  kuepukana na hio pete ni  kumtelekeza Regina  lakini  kama atakubali kuwa nae karibu basi  atabeba majukumu  yote  yanayoambatana na  hio pete.

“Kila maamuzi yana  gharama yake , kumuoa huyu mwanamke  inaonekana naenda kulipa gaharama kubwa mno ,  sijui nini  kinakwenda kutokea”Aliwaza Hamza kwenye moyo wake huku  wasiwasi ukimvaa.

Licha ya wasiwasi huo kwasababu yeye ndio alifanya maamuzi  aliona hana cha kufanya zaidi ya kukubali.

Hamza hakuwa mtu wa kuogopa  kitu , kwa mtu mwingine  kwa namna ambavyo amekutana na Regina  na pete hio  kumfikia mkononni mwake  angeweza kujiita mtu mwenye bahati lakini   kwa jicho lingine  inaweza kuwa zaidi ya bahati.

“Sio kama naikataa bibi , ni kwamba  nimeona ni ya thamani sana”Aliongea Hamza akijibaraguza na kumfanya Bibi Marium  kutabasamu huku muda huo akiangaliana na Shangazi kwa macho yaliojaa zaidi ya maana.

“Hamza nina maombi mawili”

“Nakusikiliza bibi”

“Kwanza  katika  kipindi chote  Regina  akiitwa mkeo naomba usiivue  ili  ikuletee bahati ya kupata watoto  haraka , pili   naomba  kati ya watoto wako,  wapili kuzaliwa   jina lake la ukoo  aitwe Dosam”Aliongea  na kumfanya Hamza  kuona maneno   ni kama yanazaidi  ya maana ila hata hivyo aliishia kukubali.

“Nitatimiza bibi”Aliongea Hamza  na kauli ile ilimfanya Bibi Mirium kulipukwa na furaha.

Upande wa Regina  alikuwa mwekundu kama yai , kadri dakika zilivyokuwa zikienda  akiwa na  Hamza  ni kama  mahusiano  yao yanazidi kuwa siriasi.

“Asante sana kwa kuahidi ,   ya kwangu ni hayo tu ,  unaweza kuondoka sasa, kuna vitu nataka kuongea na Regina”

Hamza hakuwa na hiyana hivyo aliwaacha na kutoka nje.

“Bibi kwanini umempa  ile pete ya babu?”Aliongea Regina  kwa sauti ya kubembeleza kana kwamba anataka kumwambia bii yake ampokonye Hamza  hio pete.

“Kwasababu amekubali kuipokea mwenyewe hii inamaanisha yupo tayari  kuwa na  wewe , hili pia ni jaribio kwako”

“Lakini bibi mimi simpendi , namchukia na  napanga  kuachana nae , kwanini  umekazania mimi  kuolewa  nae?”

“Hebu acha kuongea ujinga,  unaongeaje hivyo wakati   ndio kwanza umeolewa?”Aliongea kwa kufoka kidogo  lakini   alijua amemfokea hivyo alimshika mkono tena kwa  ishara ya kumbembeleza.

“Mjukuu wangu najua Hamza anaonekana kuwa na mapugufu mengi, lakini   unapaswa kuniamini mimi bibi yako , ndio  mwanaume pekee anaekufaa  dunia hii”

“Kwanini  bibi?”

“Kwasasa hata nikikuelezea huwezi  kuelewa , ila baadae utakuja kunielewa”

“Bibi  naogopa nitakuangusha maana sina muda wa kusubiri mpaka baadae , wakati tunakuja hapa  nilitaka kumtoa kwenye gari yangu.Mtu  hawezi kuchuma ua na akapenda zaidi  mti wake ,  kwake  mbele  ya kila mwanamke mrembo ni dhaifu  na   masaa  yote kila kinachomtoka kwenye mdomo wake ni uongo”Aliongea Regina.

“Regina  ni kweli humpendi Hamza?”Aliuliza  Bibi Mirium huku  akiwa  na hali ya wasiwasi.

 

Previoua Next