Brigedia Doswe aliishia kumwangalia Amosi kwa macho ya maswali bila ya kupokea salamu yake.
“Amosi sina muda wa kuongea na wewe sasa hivi , asubuhi kesho fika na ripoti kamili ya wapi ulipokuwa na ulichokuwa ukifanya”Aliongea.
“Sawa Afande”Aliitikia kwa heshima na Doswe aliondoka akionekana kuwa na haraka ya kuelekea kwenye kikao.
Dastani na Amosi waliishia kuangaliana , ukweli ni kwamba Dastani alikuwa akimtafuta Amosi lakini hakuweza kumpata , hata alivyoomba kitengo cha usalama wa taifa kujaribu kumfuatilia alishindwa na hisia zake zilimwambia pengine Tresha kuna alichomfanyia Amosi.
“Afande Amosi nimekutafuta sana , nilidhani kuna kitu kimekupata”Aliongea Dastani.
“Na amini ulifurahia kutokuonekana kwangu”
“Unamaanisha nini kusema hivyo Afande”Aliuliza na kumfanya Amosi kutabasamu kifedhuli.
“Nani ambae aliniandalia mtego mpaka kutaka kuwawa, Acha maigizo Kanali nina uhakika hata kutekwa kwangu unahusika”Aliongea na kumfanya Kanali kushikwa na hatia na mshangao kwa wakati mmoja.
“Unamaanisha nini kuhusika na kutekwa kwako , inamaana kupotea kwako ulikuwa umetekwa!?”Aliuliza na kumfanya Amosi kumwangalia kwa macho yaliojaa chuki bila ya kuongea neno.
“Amosi licha ya kwamba sijawahi kukupenda lakini huwezi kuongea vitu ambavyo havina ushahidi kulingana na taaluma yako”
“Umeshakiri kabisa hujawahi kunipenda , hio ni sababu tosha, kama niliweza kuingia katika mtego ulioniundia kwanini nisikushuku na hili lililonitokea”
“Kama unachozungumza ni kweli ulikuwa umetekwa, nipe sababu ambazo zinakufanya uone nahusika”Aliongea Kanali huku akionyesha hali ya usiriasi kwenye macho yake.
“Unataka sababu? , kama unataka sababu nitakutajia , unajua fika mimi ndio najua una mahusiano ya siri na Tresha na niliwapiga picha , walioniteka walinisurubu kwa kutaka niwatajie wapi nimeficha ushahidi wa picha”Aliongea Amosi na kauli ile ilimfanya Dastani mapigo ya Moyo kudunda kwa nguvu, kutokana na kile ambacho Tresha aliongea alijua fika lazima atakuwa amehusika kumteka Amosi na kama ni hivyo moja kwa moja hata yeye anahusika.
“Kanali kesho naandaa ripoti ya mambo yalionikuta katika siku zote ambazo sikuwa nikionekana , juu ya kutekwa kwangu na walioniteka walichokuwa wakitaka , nitaelezea kila kitu katika hio ripoti unapaswa kujiandaa katika hili”Aliongea Amosi , haikujulikana alikuwa akidanganya makusudi au kutokana na kupandikizwa kitu kwenye ubongo wake inamfanya adanganye , lakini kwa vyvoyte vile uongo wake ulionekana kufanya kazi.
Upande wa Dastani alihisi hatari , alijua kama kweli Amosi alitekwa na waliomteka ni watu wa Tresha basi moja kwa moja swala hilo linamuunganisha na yeye , pili faili la Tresha kwa muda mrefu lilikuwa ndani ya kitengo chao akifahamika kama mfanyakazi kutoka Binamu na ni juzi tu yeye pia alihusishwa kushirikiana na watu wa Binamu, sasa kama Amosi akiwa na ushahidi wa picha na pia ikionekana kutekwa kwake kuna uhusiano wa moja kwa moja na yeye, basi kuna uwezekano akaondolewa katika vitengo nyeti vya kijeshi na kurudi kuwa mwanajeshi wa kawaida au kufukuzwa kabisa maana ushahidi uakuwa wazi, sio hivyo tu alikuwa pia na kesi ya kuvunja vifungu vya utaratibu wa kitengo cha MALIBU kwa kujichukulia kesi mkononi bila ya kuomba ruhusa kwa wakubwa zake.
“Amosi unataka nini kutoka kwangu?”Aliuliza Kanali Dastani akiwa siriasi.
“Unaniuliza nataka nini kutoka kwako , sina ninachotaka”
“Kama huna unachotaka kutoka kwangu , usingeongea chochote na ungendaa ripoti moja kwa moja na kuikabidhi kwa Brigedia”
“Kwahio unakiri wewe na Tresha ndio mlinniteka?”Aliuliza Amosi huku akiwa na tabasamu lililojaa uovu.
“Siwezi kukiri wala kukataa kwasababu nina siku kadhaa sijampta Tresha hewani , ni kweli nakiri nina mahusiano ya siri na wewe una ushahidi, kama Tresha ndio kahusika hili ni swala linaloniunganisha na mimi”Aliongea na kumfanya Amosi kutoa tabasamu.
“Kanali licha ya kwamba hunipendi lakini mimi nakuheshimu kama moja ya Ajenti wenye uwezo mkubwa katika kitengo chetu, nakuheshimu kwa mafanikio yako nakuheshimu pia kwa kunitangulia jeshini, lakini matendo yako ambayo ni kinyume na sheria yanafunika mafanikio yako kwa kasi kubwa..”
“Amosi haina haja ya kuongea sana , niambie ni kipi ambacho unataka kutoka kwangu na katika ripoti yako usihusishe swala la mahusiano yangu na Tresha”Aliongea Dastani huku akionyesha hali ya wasiwasi.
“Nataka ripoti yote ya kesi faili namba tisini na tisa na juu ya muuaji aliehusika na kifo cha Afande Mchuku na wapi lilipo faili la sauti ambalo ameacha, naamini kwa siku ambazo sikuwepo mengi yametokea kwenye uchunguzi wako”Aliongea na Kanali hakubadilika muonekano , ni kama alitegemea Amosi angeomba kitu kama hicho.
“Jana kumetokea ajali ya gari la Mheshimiwa Jongwe kulipuka na kupoteza Maisha, nilishuhudia hii ajali baada ya kupata intellijensia kwamba yupo hatarini , muda huu nimetokea kuongea na Brigedia na sijamaliza kumwelezea kilichotokea na ameniambia naandae ripoti ,, nitaandaa nakala mbili kwa wakati mmoja moja nitakupatia wewe na nyingine nitamtumia Brigedia”Aliongea Kanali na kumfanya Amosi kutoa tabasamu.
“Vipi kuhusu rekodi ya sauti ambayo Mchuku alikuahidi kukupatia?”Aliuliza Amosi.
“Bado sijaipata ila kuna mwelekeo wa kuweza kuipata , katika ripoti ambayo nitaandaa utaweza kuona”Aliongea.
Dastani hakuwa na jinsi ya kumpatia kila kitu Amosi alichoweza kupata katika uchunguzi wake, kwake yeye ripoti ya aina hio haikuwa na umuhimu mkubwa kwani sio kwamba alikuwa akitafuta kupandishwa cheo bali alikuwa na mpango mkubwa na Tresha na hakutaka kuona mpango huo ukiharibika kwa ripoti ambayo Amosi anataka.
Upande wa Amosi ni kweli alitekwa lakini hakutekwa na watu wa Tresha bali alitekwa na watu wa taasisi ya Haliz Foundation na kufanyiwa upandikizaji wa kifaa kwenye ubongo wake.
Gia ambayo aliambiwa aitumie akiulizwa alikuwa wapi kwa kutoonekana kwa kipindi chote ni kusema alitekwa , kuhusu Dastani kuamini maneno yake alipaswa kuamini kwani kabla ya Amosi kuchukuliwa na watu wa Haliz alikuwa akifuatiliwa na kundi linguine la watu ambao walitumwa na Tresha kwa ajili ya kumuua , sasa haikueleweka ilitokea vipi ila kundi lile liliweza kukamatwa na watu wa Haliz foundation na hapo ndio sababu ilipotokea ya Amosi kuambiwa akiulizwa alikuwa wapi kusingizia watu hao waliokuwa wakitaka kumteka.
Mpango wote huo ulikuwa umeandaliwa na Ajenti Alonzo na Amosi baada ya kuambiwa mpango huo aliona pia ni nafasi ya kutumia udhaifu wa Dastani ili kujua ni wapi amefikia katika uchunguzi wa kifo cha Afande Mchuku na wapi alipoacha faili la sauti ya Wazungu wakiongea na Mfungwa Gerezani.
Ki ufupi ni kwamba Amosi alikuwa katika akili yake lakini kwa wakati huo alikuwa mtiifu kwa Umoja wa Sinagogu.
Alikuwa na misheni moja tu ya kufuatilia kujua kwa undani tukio la Ajali ya radi iliotokea mwaka 2002 na pia kujua wapi ulipo mkufu ambao aliuona kwa marehemu ex wake Jasmine.
Kwasababu Brigedia alimwambia amtumie ripoti ya tukio zima la jana Dastani hakuchelewa kwenda ofisini kwake kuandaa ripoti hio na upande wa Amosi ilibidi asubiri mpaka apate ripoti , alikuwa akifanya kazi kama roboti na alikuwa na siku chache za kukamilisha kazi aliopewa.
“Huyu mfungwa ndio amehusika na kifo cha mheshimiwa Jongwe na vilevile ndio Mchuku aliekuwa akimzungumzia?”Aliuliza Amosi mara baada ya kukabidhiwa nakala yake na Kanali.
“Nina uhakika asilimia mia moja ndio mhusika na hisia zangu zinaniambia anaweza akawa ndio amemuua Mchuku”
“Kwahio unamaanisha ametolewa Gerezani na kukamilisha yote haya?, kwa nilivyoweza kusikia mauzngumzo yako na Mchuku inaonekana huyu ndio aliehusika na kifo cha Ajenti Sedekia”Aliongea Amosi.
“Amosi hii ni taarifa nyeti ya serikali na kwa cheo chako haikupaswi kujua haya ki undan”Aliongea Dastani huku akiwa na macho ya msisitizo.
“Afande huyu sio mfungwa tena , huyu ni muhalifu na anapaswa kudhibitiwa , kuna haja gani ya kumlinda mhalifu wa namna hii , kamuua Sedekia na kisha kamuua Jongwe na Martini kwanini raia wasimjue?”
“Upo sahihi , huyu ni mhalifu na anapaswa kushughulikuwa lakini hujiulizi kwanini anaweza kufanya haya yote tena wakati huo ikiaminika ni mfungwa ndani ya Gereza la Silo , lazima kuna mkono wa viongozi hapa unahusika”Aliongea na kumfanya Amosi kutingisha kichwa.
“Kwahio imekuwaje kuwaje umempoteza wakati ukimfukuzia?”Aliuliza Amosi huku akisoma mwisho wa ripoti hio.
Ilionekana Dastani alikuwa na uhakika msababishi wa ajali iliopelekea kifo cha Jongwe alimfahamu ni Chendezi.
“Sikumpoteza Amosi , alikuwa akiendesha pikipiki, mimi gari unadhani ni rahisi kumpata kwa jinsi mpangilio wa mji ulivyo , kuna maeneo gari haiwezi kupita lakini pikipiki inaweza kupita, lakini hata hivyo nishajua alipo kwasasa ”Aliongea.
“Una uhakika?!”
“Nina uhakika nimempata”
“Unamaanisha nini?”
“Siwezi kukuambia ninachomaanisha , nimekupatia hio nakala lakini picha za mimi na Tresha unazo , sikuamini Amosi mpaka nione umezifuta”
Amosi alitoa simu yake na kumpatia Kanali na kumuonyesha picha hizo.
“Hizo hapo unaweza kufuta lakini kumbuka bado naijua siri yako, hivyo unapaswa kuniambia unamaanisha nini kusema umempata”Aliongea Amosi akiwa siriasi.
“Sina uhakika kwa asilimia mia moja ila atakuwepo chini ya bosi Laizer makao makuu ya Dede , hiki ndio ninachoweza kukuambia, Sikia Amosi hili swala lina mkono wa viongozi wa juu hivyo unapaswa kulisogelea kwa umakini mkubwa sana , sitaki uzembe wako uje kuniunganisha na mimi , isitoshe hii ni kesi ambayo haina vigezo vya kuwa chini ya kitengo chetu”
“Mimi ni Ajenti huru na sifungwi na kazi zilizopo ndani ama nje ya kitengo, naweza kubeba majukumu ya kitengo cha TISA na MALIBU muda wowote”Aliongea na kumfanya Dastani kutingisha kichwa.
Licha ya kwamba Chendezi au Maddog kuwa makini sana kuweza kumshinda Kanali katika mbio za pikipiki yake kitu pekee ambacho kilimfanya Dastani kumpata ni kwamba alikuwa bado ni mfungwa.
Hivyo mara baada ya kwenda Gereza la Silo na kumkosa pamoja na kumhoji nyapara juu ya mambo yanayoendelea hapo ndani ilikuwa rahisi kwake kujua lazima Chendezi atakuwa makao makuu ya Dede.
“Kuna kitu kimoja nataka tukubaliane baada ya hapa”Aliongea Dastani.
“Nakusikiliza”
“Kwanzia sasa uchunguzi wa kesi faili namba tisini na tisa tutashirikiana, kesho unaonaje ukipendekeza hili kwa Mkurugenzzi, naamini kama tukishirikishana utaalamu wetu itakuwa rahisi kufumbua fumbo lote kwa wepesi”Aliongea Dastani alijua kwasababu Amosi alikuwa akiaminniwa sana na Mkurugenzi akimpendekeza hata swala lake la kuvunja vifungu vya sheria za kitengo atasamehewa.
“Tokea ile siku uniingize kwenye mtego, nimetokea kukuchukia sana Kanali lakini kwa maslahi ya nchi nipo tayari ya kuweka nyuma chuki yangu , nipo tayari tushirikiane lakini tu kama Mkurugenzi ataridhia”Aliongea na kumfanya Kanali Dastani kutoa tabasamu.
*****
Hamza kabla hajapiga hatua kuingia ndani aliweza kusikia sauti ya Yonesi katika hali ya kufoka.
“Naomba uondoke sitaki kukuona”Alisikika Yonesi na ilionekana aliekuwa akimwambia ni mwanaume alievalia kombati za jeshi zenye nyota tatu ikimaanisha ni kapteni.
Regina ndio aliekuwa wa kwanza kutangulia kuingia na ndani hakukuwa na mwanaume mmoja tu , walikuwa ni wanaume wawili wote wakiwa katika sare za jeshi, mwingine akiwa ni luteni usu yaani nyota moja na jina la Diksoni J Mkandala lilisomeka kwenye kifua cha kombati zake.
“Yonesi hawa wanajeshi kwanini wapo hapa!!?”Aliuliza Regina mara baada ya kushikwa na wasiwasi kutokana na muonekano wake..
“Bosi kwanini umekuja mpaka huku hospitalini?”Aliuliza Yonesi huku akiwa na wasiwasi..
“Nilikuwa bize sana kwenye siku hizi mbili na nikashindwa kuja kukutembelea, vipi hali yako?”
“Niko sawa kwasasa bosi , asante kwa kuja kuniona”Aliongea na yule mjeda mwenye kombati zenye jina la Johnson G Mdudu aligeuza kichwa chake na kumwangalia Regina kwa macho yaliojaa kebehi.
“Lazima wewe utakuwa ni bosi wa kampuni ya Dosam , kwanini umempa kazi ya ulinzi mchumba wangu na kumfanya aumie?”Aliuliza na swali lake lilimfanya Regina na Hamza kushangaa.
“Yonesi kumbe una mchumba tayari!!?”Aliuliza Regina.
“Hapana bosi , usimsikilizze anaongea ujinga”Aliongea Yonesi na kugeuza macho yake na kumwangalia huyo mjeda kwa ukali.
“Mdudu unaongea upuuzi gani?”Aliongea.
“Yaani naongea upuuzi wakati ni kweli na umekimbia harusi hatua za mwisho na kuniabisha”
“Nilishasema sikutaki lakini unatumia nguvu ya baba yako kumpanikisha baba yangu ili unioe , nimekimbia ndio na sitokaa niolewe na wewe”
“Wazazi wetu ndio wametaka kuunganisha familia zetu kupitia ndoa , ile siku uliokubali kupokea pete ya uchumba rasmi ukawa mwanamke wangu na huwezi badilisha”Aliongea kwa hasira na kisha alimgeukia Regina.
“Mchumba wangu namtoa hapa kumpeleka hospitali nzuri ya hadhi yake, ole wako nisikie umemfanya kuwa mlinzi tena”Aliongea kwa hasira.
Hamza mara baada ya kusikia kauli zake za kibabe alijikuta akicheka chini chini, kwa namna Afande Mdudu alivyokuwa akiongea ilionyesha ni lazima anatokea katika moja ya familia yenye nguvu la sivyo asingejiamini hivyo.
“Mdudu siwezi kwenda popote na wewe , nipo radhi kufa na sio kuolewa na wewe”Aliongea Yonesi kwa hasira na kumfanya Regina aingilie.
“Yonesi ni mfanyakazi wangu na rafiki yangu , siwezi kukuruhusu kumuondoa hapa kwa nguvu , hata kama wewe ni mwanajeshi huna mamlaka ya kumlazimisha”Aliongea Regina na kumfanya Mdudu kuanza kucheka.
“Unaanza kuongea maswala ya sheria mbele yangu , unanijua mimi ni nani?”
“Haina maana ya kujisifia wewe ni nani kama matendo yako ni ya kipuuzi”
“Una kauli mbovu kwa mfanyabiashara kama wewe , Hamza kwanini unashindwa kumdhibiti mkeo?”
Regina na Yonesi mara baada ya kusikia kauli ya Afande Mdudu muonekano wao ulibadilika mara moja.
Regina alishangaa imekuwaje mjeda huyo kujua amefunga ndoa na Hamza.
Upande wa Yonesi alishangaa kwa kutoamini kama Hamza na Regina walikuwa na mahusiano ya aina hio.
Hamza yeye hakushangaa lakini muonekano wake ulikuwa ni wa kikauzu mno.
“Unanijua mimi?”Aliuliza Hamza swali likienda kwa Mdudu.
“Nakujua ndio , najua pia wewe ndio uliemuumiza kapteni Norbert , unajiamini sana mpaka kumshambulia mwanajeshi”Aliongea huku akiwa na mwonekano usiokuwa siriasi sana , ni kama alifurahia kitendo alichofanya Hamza..
Hamza muda huo aliweza kujua lazima huyu afande atakuwa ni moja ya kikosi ambacho kinamfatilia kama ilivyokuwa kwa Kapteni Norbet, lakini hata hivyo hakujali sana , kama walikuwa wakimfatilia ilikuwa rahisi kwao kuweza kupata taarifa za yeye na Regina kusajili ndoa Bomani.
“Bosi Regina kumbe umeolewa!?”Aliuliza Yonesi kwa mshangao , licha ya kwamba Regina alimchukulia kama rafiki yake ulikuwa sio ule urafiki wa kufuatiliana maisha yao binafsi.
Regina aliishia kuangalia chini huku akiwa ameng’ata lips za mdomo wake, hakudhani ingefahamika haraka hivyo juu ya ndoa yake na Hamza.
“Ndio tumesajili ndoa yetu , ila sikutaka watu wengi kujua”Aliongea
“Oh , kumbee…!”
Yonesi alijihisi kama vile amekuwa mtupu na mjinga kwa wakati mmoja , siku ya kwanza aliomuona Hamza na kumpeleka nyumbani hakutarajia Hamza angekuwa na mahusiano ya aina hio na Regina.
Kubwa zaidi kuliko yote ni kwamba alikuwa akimchukulia Hamza kama mwanaume muhuni , ambae hana mipaka, akikumbuka matukio kati yake na Hamza na taarifa hio alijikuta akishikwa na hasira.
“Hamza usijione kidume kwasababu umeweza kumshambulia KapteniNorbert ukahisi tutakuacha salama , una kesi kadhaa zinazokukabili na tunakwenda kuzifanyia uchunguzi, kama una akili ni kheri kujisalimisha mapema”
Regina alijihisi kupaniki maana hakutarajia serikali ingetuma watu kwa ajili ya kumchunguza Hamza na alijiuliza inamaana Hamza anakwenda kufungwa kwa kumuua mtu.
“Kwangu bora kapteni Norbet kidogo naona ana weledi , ila wewe unachojua ni kuongea tu , kama unao uwezo wa kunikamata huna haja ya kunipiga mikwara hapa”Aliongea Hamza na kauli yeke ilimfanya Afande Mdudu kujaa sumu , lakini licha ya hivyo alikuwa akimhofia Hamza hivyo hakufanya chochote na hakutaka kuzidi kumkasirisha.
Lakini hata kama alikuwa akimuogopa aliamini kama akiamua kumkamata ataweza.
“Wapo watalamu wengi wa mapigano ndani ya hii nchi ambao wanaweza kukushinda , hivyo acha ukiburi , hatujaamua tu kukuchulia hatua kwasababu tunaangalia muda sahihi wa kufanya hivyo”Aliongea.
“Kama umemaliza kuongea ondoka maana hakuna anaonekana kukukaribisha hapa”Aliongea Hamza.
“Unanifukuza kama nani ,nilivyosema Ypnesi ni mwanamke wangu hujanielewa , wewe ndio unatakiwa uondoe hapa”
“Kama una uwezo jaribu kumchukua Yonesi kinguvu uone”
“Wewe ni mjinga kuleta ukiburi mbele ya mtu ambae hata hujui nguvu yake?”
“Ndio sikujui na sitaki kujua”Aliongea Hamza huku akitingisha mabega.
Yonesi mara baada ya kuona wawili hao wanaanza kupandishiana alijikuta akiingiwa na wasiwasi.
“Hamza acha kujibishana , Bosi nitaondoka nae tu”Aliongea Yonesi, japo majeraha yake yalikuwa yamepona lakini bado alihitaji muda wa kupumzika kwanza zaidi.
“Yonesi kwanini, si ulisema hutaki kuondoka nae?”
“Kwa ajili yangu sitaki kukuingiza kwenye matatizo”Aliongea na hapo Regina alijua lazima itakuwa ni kuhusu nguvu ya Afande Mdudu ndio maana ameamua kwa hiari yake kuondoka ile isijetokea wakaingia kwenye ugomvi na Hamza.
Regina hakuwa mtu wa kukurupuka hata hivyo , alikuwa akijaribu kupima faida na hasara , hata kama alikuwa akimiliki kampuni kubwa lakini bado ataishia kuwa mfanyabiashara tu mbele ya wanasiasa na wanajeshi.
“Yonesi hukuona unaisababishia familia yako matatizo kwa kukimbilia huku , huu ni muda wa kurudi nyumbani na usiwe na wasiwasi kabisa, tukifika nyumbani nitaongea na baba yako ili tuweze kufunga ndoa haraka haraka na tuanze kufikiria swala la Watoto”
Wakati huo akiongea alikuwa akikiangalia kifua cha Yonesi kwa macho yaliojaa uchu wa kimatamanio.
“Endelea kuota , siwezi kukubali kuolewa na mtu mwenye majigambo kama wewe”
“Hehe , hilo sio juu yako kuamua, tukisharudi kila kitu kitaenda kutokana na mipango ya familia, baba yako amekuvumilia muda mrefu na licha ya kujua unaishi hapa Dar hakuchukua hatua y a kukulazimisha kurudi , alikuwa akikupa muda ili mwisho wa siku uelewe kwamba mimi ndio mwanaume sahihi wa kukuoa, ni mimi pia ambao sikutaka wakusumbue niliwaambia wakupe muda”Aliongea kwa majingambo.
Moja ya sifa ya Mdudu ni kuwa mpole mbele ya wakubwa zake kijeshi , lakinni ukimkuta mbele ya watu waliochini yake ni mjivuni wa kiwango cha daraja A.
Regina mara baada ya kusikia maneno hayo na kuona namna Yonesi alivyokuwa katika hali ya huzuni alijikuta akimuonea huruma , hata yeye alikuwa akiyajua machungu ya kulazimishwa kuolewa.
Kwake aliona licha ya Hamza kuwa na mapungufu yake lakini alikuwa afadhali kuliko Mdudu.
“Eunice kama hutaki kwenda haina haja ya kujilazimisha , ndoa ni swala la hiari na ukiona hupati haki yako shirikisha hata wanasheria wa mambo ya haki za binadamu”Aliongea Regina.
“Ashirikishe wanasheria! , Regina wewe ni mjinga kutaka kuingilia mambo yetu”.
Yonesi mara baada ya kuona Regina alikuwa akimtetea alijisikia vizuri ,ni mara ya kwanza kwake kutetewa kama hivyo , nyumbani wakati analazimishwa kuolewa hakuna ambae alimkingia kifua mpaka alipofanya maamuzi ya kukimbilia Dar es Salaam.
“Mkurugenzi asante sana kwa kusimama upande wangu na kunijali mwanamke kama mimi ambae ninachojua ni kupigana tu kwa miaka yote mitatu tokea tukutane , nisamehe siwezi kuendelea kufanya kazi chni yako tena”Aliongea Yonesi kwa sauti iliojaa huzuni na maneno yake yalimfanya Regina kuzidi kushikwa na huzuni iliochanganyika na hasira.
Muda huo Yonesi alikuwa ashatoka kitandani kwa ajili ya kuondoka,hakutaka hata kumwangalia Hamza ambae alikuwa amekaa nyuma.
Kitendo cha Yonesi kutaka kuondoka bila ya kumuaga , kilimtoa Hamza aliposimama na kwenda kumzuia kwa mbele.
“Yaani tumekula chakula cha mchana mara kibao halafu unataka kuondoka bila hata ya kuniaga”Aliuliza Hamza.
Kauli yake ilimfanya Yonesi kukumbuka siku ambazo alifahamiana na Hamza mpaka kuzoea kula nae chakula kwenye meza moja.
“Wewe ni muongo siku zote kumbe ni mume wa bosi halafu umenikalia kimya , nimekasirika sitaki hata kukuaga mimi”
“Sawa Kapteni, lakini haina haja ya kujilazimisha kuondoka”
“Kuna baadhi ya mambo kwenye dunia hii yapo nje ya hiari yetu”
“Ndio yapo mambo mengi ambayo hatuna hiari nayo, ikiwemo kifo na kuumwa , lakini swala la kuolewa na mtu kama huyu ni kuamua , kama hutaki hutaki”
“Hamza acha kuniongelea vibaya ukidhani siwezi kukufanya chochote , hujui hata kipi ni kizuri na kibaya kwako kwa kujaribu kuingilia mambo yangu na mchumba wangu”
“Eti wewe na mchumba wako, bro unaziabisha hizo kombati za jeshi kama unashindwa kujua ndoa ni makubaliano ya watu wawili , wewe unamwita mchumba lakini Kapteni hakutaki Zaidi ya kufosi”Aliongea na kumfanya Afande Mdudu kumsogelea Hamza karibu na kumwangalia kwa macho makali.
“Sitaki kupoteza muda wangu na mhalifu kama wewe ,ukiendelea na mbovu zako nitakufanya ulazwe hapa hospitalini”
“Acha hasira bro , sina mpango wa kuingilia mambo yako , kinachonipa wasiwasi ni juu ya mke wang tu”
“Hili linahusiana vipi na mkeo?”Aliuliza Mdudu.
“Wewe ndio uniambie , unadhani ni kitu gani muhimu cha kuzingatia kama mwanaume kabla ya ndoa?”
“Kwanini nikujibu?”
“Huwezi kunijibu kwasababu kwa macho yako unadhani kuoa ni kama kunfunga kondoo Kamba na kumpeleka nyumbani , unachotaka kufanya hapa ni kumchukulia Kapteni ni kama mnyama ambae unaweza kumuweka nyumbani bila ya kujali hisia zake”
“Unataka kumaanisha nini?”Aliuliza , sio kama hakuelewa ila hakutaka kuelewa.
Sababu ya Mdudu kumlazimisha Yonesi kuolewa nae ni kwasababu ya uzuri pamoja na familia anayotokea , hakujali hisia zake , pengine hayo yote yalichangizwa na namna ya familia zao zilivyo, kwao ndoa ni kama biashara ya kuunganisha familia mbili zenye nguvu.
“Mimi sijui wengine wanachowaza ila kwangu kitu cha kuzingatiwa kwa mwanaume kuoa ni ule utayari wa mwanaume kubeba majukumu yote ya kifamilia , ndoa inaweza isiwe kamilifu lakini uwajibikaji ni lazima , kwa mke wangu mimi anamchukulia Kapteni kama Rafiki yake wa karibu, kama Kapteni hana furaha na mke wangu hawezi kuwa na furaha, na kwasababu sitaki kumuona Regina akiwa na huzuni Yonesi anabakia hapa , haendi popote”
Regina licha ya kutopendezwa na Hamza kumuita mke , lakini bado moyo wake ulilainika kwa namna ambavyo alionekana kuwa siriasi kujali kile ambacho anataka.
Hata kwa Yonesi ilikuwa ni hivyo hivyo alikuwa na hisia mchanganyiko , aliguswa na namna Hamza alivyoonekana kusimama mbele yake kumkingia kifua
Kauli ya Hamza ilimfanya Afande Mdudu kuchomoa bastora kiunoni na kumuwekea Hamza kwenye paji la uso.
*******
Saa nane za mchana ndani ya dhehebu la kiimani la The Chosen Faith’s, maarufu kama Kanisa la Wabrazili alionekana Ajenti Alonzo akiwa amekaa kwenye benchi ndani ya kanisa hilo.
Kanisa hili lilikuwa likipatikana Bunju B ndani ya jiji la Dar es salaam, kwasababu ilikuwa ni mchana hakukuwa na waumini wowote wa Dhehebu hilo.
Alonzo alionekana kukodolea skrini iliofungwa juu ya dari ikionyesha ratiba mbalimbali za ibada.
Moja ya sababu kubwa ya kanisa hili kujipatia umaarufu duniani kote ni kutokana na taratibu zao za ibada , lilikuwa dhehebu ambalo linakaribisha kila aina ya Imani kasoro waumini wa Wiccan pekee.
Yaani kila kitu ndani ya kanisa hilo kilikuwa kikifanyika kinyume , ilikuwa pia sio sahihi kuliita kanisa kutokana na utaratibu wao.
Kama ni muumini wa Rastafarians kulikuwa na ratiba yake ya ibada, kama ni muumini wa Kibudha kulikuwa na ratiba yake ya ibada , kama ni muumini wa kikristo kulikuwa na ratiba yake ya Ibada, kama ni muumini wa Caodaism kulikuwa na ratiba yake ya ibada , ki ufupi ni kwamba dhehebu hili lilikuwa likitilia mkazo kila Imani ya mtu bila kumbagua, kasoro tu wapagani wa kisasa ambao maarufu hufahamika kama Wicca.
Inasemekana kwamba licha ya kanisa hili kuwa na ibada ya kila Imani lakini siku moja ambayo ni Jumamosi wanakuwa na ibada ambayo inawakutanisha waumini wa Imani zote na mafundisho yanayotolewa katika siku hio ni kufundisha elementi ambazo zinaunganisha dini zote.
Yaani kwa lugha nyepesi kinachoangaliwa ni vipi Imani ya Rastafarian inafanana na Imani ya Kibudha , hivyo hivyo ni vipi Imani ya Kihindu inafanana na ya Kiyahudi , sasa hizo sababu zote ambazo zinatengeneza mshahibiano ndio msingi mkuu wa Imani ya kanisa hilo la Wabrazili au The Chosen faith’s.
Mbele ya Madhabahu ya kanisa hilo kulikuwa na kila aina ya vitabu vya dini ambavyo hutumiwa na Imani tofauti tofauti kwanzia Satanic Bible, Black Book , Mishefa na vinginevyo.
Baada ya dakika chache kupita pembeni ya Alonzo aliweza kufika mwanaume wa kizungu alievalia joho la rangi nyekundu na kukaa pembeni yake.
“Shalom Shalom!”Alisalimia yule mwanaume wa kizungu alievalia joho.
“Merry meet , Raeli”Aliitikia Alonzo kwa Imani yake na kumpa heshima yule mtu kwa Imani yake.
Merry meet ilimaanisha kuitikia salamu kwa muumini wa kipagani ambae sio Wicca na Raeli ni cheo cha mtumishi kutoka Imani ya Raelism.
“Tupo na kipi cha kuzungumzia leo?”Aliuliza
“Nipo kwa ajili ya kuripoti kazi yangu nchini Tanzania imekamilika”Aliongea.
“Kuhani alinipa taarifa juu ya ushawishi wako mbele ya Profesa Maya Thema, kazi nzuri Ajenti”.
“Asante Raeli kwa kunitambua”Aliongea Alonzo akionekana kufurahia kusifiwa .
“Kutokana na uwezo wako wa hali ya juu unapaswa kuendelea kubakia nchini Tanzania kwa kazi nyingine”Aliongea Raeli na kumfanya Ajenti kushangaa.
“Kazi nyingine!!”
“Ndio , kazi hii ni muhimu na kama utaweza kuifanikisha nafasi yako ndani ya umoja itapanda , Ajenti Alonzo upo tayari kupokea kazi nyingine?”
“Moyo wangu ni kwa ajili ya Umoja , nipo tayari kwa kazi nyingine”Aliongea na kumfanya Raeli kutoa tabasamu.
“Kama Sinagogi tunaamini uwepo wa viumbe wengine ambao wanaishi hapa duniani pamoja na sisi , uchunguzi wetu wa kisayansi umeweza kuthibitisha uwepo wao , lakini jamii za kimataifa zimekataa kuamini kutokana na kutokuwepo kwa Ushahidi wa kuonekana kwa macho, Shukrani kwa Dokta Genesha kwasasa tuna teknolojia ya kunasa nguvu zisizoonekana”
“Raeli unamaanisha hawa Night Shadows!!”Aliuliza Alonzo na Raeli alitingisha kichwa kukubali.
“Kwa taarifa iliosambazwa na Kuhani mkuu duniani kote inapambanua Viumbe hawa wanaweza kujidhihirisha kwa binadamu kwa kutawala kivuli chao, tunaamini viumbe hawa wamekosa miili ya kibinadamu ndio maana tunashindwa kuwaona , Kuhani kupitia andiko lake anasema viumbe hawa wapo kila sehemu ndani ya dunia , lakini viumbe waliopo America hawawezi kuvuka bahari na kufika bara la Afrika , hivyo hivyo kwa mabara mengine ambayo utenganisho wao ni maji”Aliongea na kauli ile ilimfanya Alonzo kuwa katika hali ya mshangao kana kwamba alikuwa amepata taarifa ambayo hakuwahi kuisikia , yeye kama ajenti wa Sinagogi alikuwa akijua uwepo wa hao walioitwa Night Shadows lakini hakuwahi kupata uzoefu wa kivuli chake kutawaliwa na hao viumbe.
“Ndugu Raeli, maelezo yako ni yenye kunishangaza mpaka sasa , na sijajua ni kazi gani nyingine nakwenda kufanya”
“Naelekea huko Ajenti wakati nikimalizia kukusimulia barua ya Kuhani, kwa maelezo ya Kuhani anaamini kuna njia za mawasiliano baina ya hawa viumbe kutoka bara lingine kwenda bara lingine na Nadharia ambayo imeibuliwa na haadhi ya watafiti wetu ni juu ya matumizi ya kinachoitwa Stimula”
“Stimula!!”
“Ndio ni kama aina ya moshi wa harufu ambao humfanya binadamu kupata msisimko wa hali ya juu wa ubongo wake na kufanya kazi kwa uwezo wa juu kabisa, Hapa Tanzania imegundulika kuna matumizi ya siri sana ya hizi Stimula ambazo husafirishwa kwa njia ya vyungu”Aliongea na kauli ile ilimfanya Alonzo kushangaa.
“Hizi Stimula zinatokea wapi kama zinatumika dunia nzima?”
“Kwasasa hakuna Ushahidi wa moja kwa moja wapi zinatokea na kipi kipo nyuma ya teknolojia ya udhalishaji wake , wanasayansi wetu wanaendelea na utafiti , uchunguzi wa awali tunahisia hizi Stimula zinatokea kisiwa Cha Binamu”
“Binamu!!”
“Ndio, nadhani sina haja ya kukuelezea kuhusu Binamu?”?Aliuliza na Alonzo alitingisha kichwa kukubali.
“Kazi yako nchini Tanzania sio kujua wapi hizi Stimula zinatokea wala juu ya kazi yake, unachokwenda kufanyia kazi ni kujua watu wote wanaotumia hizi Stimula , Kuhani anaamini wateja wa hizi Stimula ndio njia ya mawasiliano ya hizi roho ambazo hujidhihirisha kwa njia ya kivuli”Aliongea na kauli ile ilimfanya Alonzo kutingisha kichwa.
“Kwa maana kazi yangu itakuwa ni kuwatambua na kuwafuatilia hawa watu wanaotumia hizi Stimula na kuona kama kuna mawasiliano yanayofanyika?”
“Hakika umeweza kuelewa ninachomaanisha Mr Alonzo , ninachokukumbusha kazi hii inapaswa kufanyika kwa siri sana na isitokee ikagundulika unafuatilia hili swala , kazi yako kubwa ni kujua kama kuna mawasiliano yoyote yanayofanyika wakati wa matumizi ya hizo Stimula na kama yapo ni kipi kinaongelewa”Aliongea na Alonzo alitingisha kichwa kuelewa.
Comments