Katika ndoto ambayo aliota jana yake aliweza kuona mwezi wa ule ulimwengu wa ndotoni ulikuwa mwekundu ,sasa mara baada ya kupewa mchoro uliokuwa kama picha na kuona mwezi huo ni mwekundu pia,ilimfanya kushangaa.
“Kwa jinsi ulivyoshangaa nadhani tayari unajua maana yake?”Aliuliza Frida akiwa na shauku.
“Sijui maana yake lakini jana kwenye ndoto niliona mwezi mwekundu , unaweza kuniambia nini maana ya huu mwezi na kwaninni umenionyesha hii picha?”Aliuliza Hamza , mbele ya Frida aliamua kuwa mpole ili kupata kile anachokitaka.
“Inamaanisha mazingira unayoota ni sahihi”Aliongea na kumfanya Hamza kukunja ndita .
“Wewe umejuaje?”
“Nilipewa na dokta Genesha na alinimbia nikijisikia ni muda sahihi wa kukuonyesha hii picha nikupatie , mwanzoni sikumwelewa alikuwa akimaanisha nini , lakini ulivyo uliza swali nilijua nini maana ya picha hii?”Aliongea .
Ukweli ni kwamba licha ya Hamza kujihusisha na Frida hakuwa akimwamini kabisa haikuwa hivyo tu hata kwa Frida alimuona Hamza kama mtu ambae hakuwa akimwanini.
Lakini licha ya hivyo alipaswa kumfanya Hamza kumwamini kwa namna yoyote ile ili tu aweze kumshawishi kutumia mshumaa wakati wa ndoto la sivyo maisha yake yatakuwa hataini.
Hamza alionekana kufikiria kwa dakika kadhaa huku akikodolea macho ile picha , hakuwa na shaka kabisa juu ya picha hio kwani ilionyesha kitu ambacho ameota yeye, alichokuwa akiwaza je haya yote yanayomtokea ndio njia sahihi ya kumpata Mzee kama alivyosema Dokta Genesha.
“Hamza kwa ajili ya hicho unachokiwaza mshumaa ni ufunguo wako , kumbuka maneno yangu niliokuambia juu ya uwepo wa Chumba cha nuru na ni wewe pekee ambae unaweza fikia hiki chumba kwa maelekezo ya Dokta, kadri ambavyo utachelewa kufanya maamuzi ndio unazidi kujiweka katika hatari pamoja na watu wanaokuzunguka”,
“Una amini nikitumia mshumaa nitakuwa salama , sidhani inaweza kuwa hivyo , kwanzia sasa kila ninachofanya juu ya hivi vitu ndio nazidi kujiweka katika hatari”
“Watu wanaokuwinda kwasasa wanachotaka ni kitu ulichokuwa nacho , hata kama wachukue waondoke nacho hakina maana kwao, wewe pia umekishikilia kwasababu bado hujajua maana yake halisi ni nini na kinaelekeza nini , ikitokea umejua kinachoelekeza utakuwa ni wewe tu dunia nzima unaejua hilo na inabakia kuwa siri yako , hata kama ukiwapatia kujiondolea hatari kwako na kwa wapendwa wako, watakuwa wamekushikia tu lakini maana unaijua wewe tu”
“Na siri hio ikitoka inamaanisha nitazidi kuwa hatari zaidi ya mara mbili ya kuwa na kitabu?”Aliongea Hamza huku akitoa tabasamu lililojaa uchungu.
“Ni mpaka wakifahamu juu ya hilo lakini kwa wakati huo utakuwa umejua namna ya kujilinda na kuilinda familia yako, sidhani upo tayari kuruhusu mwanamke kama Regina kuingia katika hatari kwa ajili yako”Aliongea.
“Unajua nina mahusiano na Regina, unaonekana kunifuatilia sana”
“Wewe ni misheni yangu kutoka kwa Dokta Genesha , nipo kwa ajili ya kukuelekeza, ukifeli kwa upande wako na mimi pia nafeli kile nilichomuahidi Dokta , lazima nijue watu ambao unajihusisha nao”
“Sishangai wewe kusema hivyo ndio maana hata mimi kuleta vyungu hapa ulikuwa ni mpango wako na haikuwa bahati mbaya kwa Alex kunipa kibarua”Aliongea Hamza.
Ukweli ni kwamba akikumbuka namna ambavyo amekutana na Frida ilionekana kabisa ulikuwa ni mpango wa Frida kukutana nae.
“Siwezi kukataa na tena kuhusu Alex unapaswa kuwa nae makini?”
“Nina sababu ya kufanya hivyo?”Aliuliza Hamza .
“Alex ni shushu kutoka watu wa kisiwa cha Binamu , maisha unayomuona nayo Alex ni uwezeshwaji na mbinu ya kulinda kile ambacho anafanya”
“Unamaanisha kusambaza vyungu?”
“Hupaswi kusema ni kusambaza vyungu bali ni kusambaza teknolojia mpya ya dawa inayosisimua ubongo , nadhani unakumbuka nilikuambia natumia vile vyungu kwa ajili ya utafiti wangu?”
“Ndio nakumbuka , kwahio unamaanisha umekwisha kupata majibu?”
“Ndio majibu nimekwisha kuyapata”Aliongea na jambo lile lilimfanya Hamza mwili wake kumsisimka kwa furaha maana ndio kitu ambacho alitaka kujua tokea mwanzo.
“Mpaka sasa sijajua namna dawa hii inavyotengenezwa , lakini ni maarufu kwa jina la Stimula”
“Stimula!!” Hamza alionekana kuhangaa kidogo.
“Ushawahi kusikia?”Aliuliza na Hamza alitingishwa kichwa kukubali.
“Zipo njia nyingi za usafirishaji wa hii Stimula na haina kibali chochote duniani ni kama madawa ya Kulevya , Njia ya utumiaji wa chungu ndio maarufu kwa hapa Tanzania na maeneo mengi ya Afrika”
“Wanasafirisha vipi?”
“Ni rahisi sana , unatumia jiko la umeme na kukifanya chungu kipate moto na dawa itaungua na kudhalisha harufu mfano wa marashi , hii harufu ukiivuta inakulewesha na baada ya hapo huelewi kinachoendelea maana utakuwa ni kama mgonjwa wa akili na dalili ya kwanza utakayokuwa nayo ni uwendawazimu kama vile umetawaliwa na roho nyingine , mtu anakuwa ni kama sio yeye kwani ataanza kuonge vitu ambavyo sio vya kawaida”Aliongea Hamza na kauli hio ilimfanya kukumbuka swala la rafiki yake Amiri juu ya harufu ya marashi nyumbani kwa Mellisa huku akiongea vitu vya ajabu.
“Kwanini haya yote , kuna faida yoyote mtumaji anayopata?”
“Kwasasa hakuna jibu sahihi kama kuna faida yoyote , haijulikani ni kwa ajili ya starehe au kuna zaidi ya sababu, pengine kuna mpango unaoendelezwa ambao si ufahamu , ni ngumu kukupa majibu kwasasa”Aliongea lakini upande wa Hamza bado hakutaka kukubali kirahisi , alijua lazima kuna kitu kinaendelea juu ya hicho kitu kinachoitwa Stimula.
Alitamani kutoendelea kuchimba zaidi lakini alimkumbuka Amiri rafiki yake na alimuahidi atamsaidia , lakini kabla ya hivyo alipaswa kujua kama Mellisa alikuwa moja ya wateja wa Alex wanaonunua hivyo vyungu.
Jambo la kwanza alipaswa kujua mtu aliempa kazi ya kufuatilia lugha aliokuwa akiongea amefikia wapi, na pili ndio afanye maamuzi aidha ya kumwambia Amiri ili ajue cha kufanya ama alifuatlie yeye mwenyewe .
Maana alijua kama swala hilo Mellisa analifanya kwa siri basi ni dhahiri kuna sababu kwanini Amiri hajui.
Hamza hakuwa na haja ya kuendelea kubakia nyumbani kwa Frida , ukweli ni kwamba swala la kutumia mshumaa ama kutokutumia ilikuwa ni maamuzi yake.
Upande wa Frida alimwangalia Hamza mpaka anatokomea na zilipita kama dakika kumi tu ya Hamza kuondoka aliingia mwanaume alievalia suti ndani ya jumba hilo , alikuwa mzungu..
Frida alionekana kumjua yule mtu na hata hakumsalimia , ilikuwa ni kama vile mtu huyo anaishi ndani ya nyumba hio.
“Unaamini atautumia mshumaa kwa kumweleza alichotaka kusikia?”Aliuliza yule mtu na kisha alisogelea makaratasi yaliochanguka mezani na kuchomoa karatasi la plastiki ambalo lilikuwa chini kabisa mwa yale makaratasi na kulinyanyua juu kuliangalia huku akitoa tabasamu na palepale alilikunja na kuliweka kwenye mfuko wa koti la suti.
“Umesikia mazungumzo yetu yote, hii inatosha kuniamini juu ya kusimamia vyema utafiti wangu”Aliongea Frida akiwa siriasi.
“Hatuwezi kwenda huko haraka hivyo Frida , upo hapa sio kwasababu Sinagogu wanakuamini bali tunamwamini Dokta Genesha, ulifanya kosa kubwa kumfanya Kuhani kukutilia shaka na sasa umejitengenezea udhaifu”Alionga yule bwana huku akizunguka zunguka kana kwamba kuna kitu anatafuta kwenye hio nyumba.
“Unamaanisha nini kujitengenezea udhaifu?”
“KF ni mtu hatari sana na kadri unavyokutana nae unazidi kumdanganya, ulikuwa na ushawishi mkubwa katika maneno yako ili kumfanya akuamini ili hali kila kitu ni kinyume chake , unadhani akijua unamdaganya itakuwaje?”Aliongea na kauli ile ilimfanya Frida kujawa na ukauzu.
“Kama unalijua hilo haikuwa na haja ya kuniuliza kama ameniamini, unaongea kwa kujaribu kuniogopesha lakini unapaswa kujua kitu kimoja, hii ni kazi ambayo nilifanya maamuzi mimi mwenyewe kuifanya , hivyo vitisho vyako hapa haviwezi kufanya kazi, najua malengo ya kazi yangu”Aliongea na kumfanya yule bwana kuonyesha ishara ya kutabasamu.
“Frida kazi yangu ni kukuangalia na kukisimamia na kuhakikisha kila unachofanya ni kama ulivyomuahidi Kuhani , unapaswa kujua Kanisa halijawahi kukuamini bali tunaamini kile unachofanyia utafiti ndani ya taasisi zetu, wewe ni Wicca na kama ulivyo kwenye taasisi yetu kwa ajili ya kutumiza malengo ya ushirika wako na sisi tupo hapa kukutumia ili kutimiza malengo ya ushirika wetu, hivyo haijalishi nilichoongea unachukulia kama tishio au onyo hio ni juu yako, tutatonana tena baada ya kuona mafanikio, Frida kumbuka naona kila unachofanya”Aliongea na kisha palepale aligeuka na kutoka ndani ya nyumba ile huku akiangaliwa na macho makali ya Frida.
Bwana huyo alikuwa ni yule yule ambae alikutana na Frida juu kabisa ya jengo la Haliz Foundation na ilionekana chochote kila ambacho Frida anafanya anasimamiwa na huyo mtu na pia ilionekana mazungumzo baina ya Hamza na Frida yalifuatiliwa kupitia teknolojia ya karatasi.
*******
Lisaa limoja na nusu mbele Hamza alikuwa akitoka kituo cha Treni ya Mwendokasi ndani ya mkoa wa Morogoro na kuungana na abiri wengi ambao walikuwa wakitoka eneo hilo.
Kutokana na jua kali Hamza hakutaka kupanda pikipiki bali aliingia kwenye taksi ambazo zilipatikana ndani ya eneo hilo.
“Nipeleke Tumaini mkuu?”Aliongea Hamza.
“Tumaini ipi mkuu?”Aliuliza yule bwana na kumfanya Hamza aone hakutoa maelezo ya kutosha.
“Tumaini kituoni kwa watoto Yatima kule”Aliongea Hamza.
“Nimekusoma bosi wangu”Aliongea mwendesha taksi kwa furaha na kisha aliondoa gari kuelekea uelekeo ambao ameelezwa.
Tumaini ni moja ya vituo maarufu kongwe ambavyo hulelea watoto Yatima na wale wenye ulemavu wa ngozi.
Kutoka stendi mpaka kituoni ilikuwa ni umbali wa nusu saa kutembea na gari, eneo lote lilikuwa likimilikiwa na taasisi moja ya kimisaada kutoka Denmark lakini baadae waliacha ufadhili na kwa muda mrefu kituo hicho kipo chini ya taasisi ya FOOT(Friends of orphans Tanzania).
Hamza mara baada ya kushushwa na taksi nje geti la kuingia kituoni hapo alilipa na kisha alisogelea chumba cha mlinzi na ilionekana alikuwa akifahamika kwani hakuandika hata jina lake kwenye kitabu zaidi ya kuruhusiwa kuingia.
Ndani ya kituo hicho kulikuwa na eneo kubwa mno , ijapokuwa majengo yake hayakuwa ya kisasa sana kutokana na kujengwa zamani sana lakini mazingira yalikuwa safi na yenye utulivu wa hali ya juu.
Ilikuwa Jumamosi hivyo watoto wote wanaoishi hapo walikuwa katika shunguli za usafi.
“Mr Hamza!!”Sauti iliita kutokea upande wa kulia wa bustani na kumfanya Hamza kugeuka .
“Madam Dorisi! Habari za siku?”Alisalimia Hamza.
Mwanamke ambae alifahamika kwa jina la Dorisi alikuwa mfupi na mnene na alionyesha tabasamu kumuona Hamza.
“Ni nzuri kabisa, sijategemea kukuona leo huku?”Aliongea huku akimwangalia Hamza kwa kumchunguza mavazi yake ni kama alikuwa akishangazwa na mabadiliko ya Hamza.
“Ulitegemea kuniona lini Madam?”Aliongea Hamza na yule mwalimu ni kama alijua ameongea kitu cha kijinga na kumfanya aanze kujibaraguza.
“Nilitegemea kukuona siku yoyote kwanzia kesho ila sio leo?”
“Hayo ni maratajio au sio!?”
“Kabisa , karibu sana , kama unavyoona nawasimamia watoto kufanya usafi wao wa kimwili”Aliongea na Hamza alitingisha kichwa kumwelewa.
Kila mtoto alionekana kuwa bize , wengine wakifua wengine walikuwa wakiogesha watoto wadogo.
“Nipo hapa kwa ajili ya kuonana na Mkuu wa kituo nadhani sijamkosa maana nimekuja bila miadi?”
“Yupo kuna wageni wengine anawasubiria leo”Aliongea na kumfanya Hamza kutabasamu na kisha kumuaga Madam Dorisi kuendelea na mambo yake.
Hamza alitembea kwa mwendo usio wa haraka sana na usiokuwa wa kivivu sana akielekea jengo ambalo ofisi za walezi , mkuu wa kituo na walimu zinapatikana.
Jengo la ofisi hizo lilikuwa limechakaa kidogo kutokana na stali yake ya kizamani , kwa nje usingejua kama ni jengo la Ghorofa mpaka uingie ndani.
Hamza wakati akiingia eneo la ukumbi chini kabisa ya jengo hilo aliweza kuonekana mwanaume mzee hivi kama miaka sitini kwenda therathini, hakuwa peke yake bali kulikuwa na mwanaume kijana ambae ameshika daftari kubwa na ilionekana kuna kitu ambacho walikuwa wakishaurina kwa namna walivyokuwa siraisi.
“Hamza leo naona umetukumbuka?”Aliongea yule mzee huku akionyesha hali ya kutabasamu.
“Sijawahi kukusahau mzee wangu, halafu naona hali ya hewa Morogoro kidogo ni ya ubaridi na upepo mwingi , kwa mavazi hayo huogopi kuumwa?”
“Ni kweli hali imebadilika , japo naonekana kuwa na mvi tayari lakini sijazeeka , Karibu sana”Aliongea na Hamza alionyeshwa sehemu ya kukaa huku akisalimiana na yule bwana ambae alionekana kuwa na kaunta book, kwa haraka haraka Hamza alimfahamu alikuwa ni Mgavi wa hiko kituo.
“Dean nitaenda kumalizia ili kubalansi mahesabu , ikishindikana kabisa kwa watu tunaowatarajia nifanye mawasiliano na Wizara”Aliongea yule mwanaume.
“Fanya unachoona kinafaa kwa utashi wako , hakikisha unagawa pasipo ya kubadili utaratibu licha ya kupelea kibajeti”Aliongea na yule bwana alitingisha kichwa.
Kwa namna ambavyo walikuwa wakiongea Hamza alijua tu , kituo kitakuwa kinapitia wakati mgumu kwenye maswala ya bajeti na alijiambia alifanya vizuri kuja siku hio.
“Nimesikia kutoka kwa Madam Dorisi unasubiria wageni ndio maana hujatoka leo?”Aliongea Hamza.
“Amekuambia wageni!, mimi nimemwambia kuna mtu namsubiri na sio wageni , Dorisi bwana”Aliongea huku akitabasamu na kumfanya Hamza kucheka.
“Tena una bahati kuja leo, ninaemsubiria itakuwa unamjua kama kumbukumbu za utoto wako zinafanya kazi vizuri, pengine anaweza kuwa msaada kwenye swala lako”Aliongea na kauli yake ilimfanya Hamza macho kuchanua.
“Ni moja ya watoto waliolelewa hapa!?”
“Kama una kumbukumbu nzuri, unakumbuka wakati unarejewa na fahamu kuna msichana mdogo aliekuwa pembeni yako akilia!!?”Aliuliza Dean huku alimwangalia Hamza machoni kwa matarajio.
Haikuwa ngumu kwa Hamza kuvuta kumbukumbu za kituoni hapo wakati akiwa mdogo, ukweli ni kwamba sehemu hio miaka zaidi ya ishirini iliopira ndio sehemu ambayo kwa mara ya kwanza alisikia jina la Mzee na hio ni mara baada ya kurejewa na fahamu akiwepo hapo huku akiwa hana kumbukumbu ya kilichomtokea nyuma , alijua tu alipata ajali ambayo ilimfanya kupoteza fahamu kwa kipindi cha miezi minne.
“Nadhani kweli nakumbuka , kulikuwa na mtoto kibonge aliekuwa na mashavu makubwa”Aliongea Hamza na kumfanya Dean kucheka.
“Ndio huyo,nilidhani umemsahau kabisa, ila naona umemkumbuka”Aliongea na kumfanya Hamza hamu ya kutaka kumuona huyo mtu kuongezeka.
“Mzee kwa jinsi unavyoonekana nadhani amefanya vizuri sana wakati akiwa hapa?”Aliongea Hamza na Mzee yule alitingisha kichwa kukataa.
“Hapa hakukaa kabisa na hapakuwa kwao , wakati unaondoka na yeye alichukuliwa na baba yake, amefanya vizuri sana akiwa kwa wazazi wake mpaka kupata elimu ya juu kabisa na sasa ni mwajiriwa wa kampuni kubwa hapa nchini, licha ya hivyo mpaka leo hajawahi kutusahau, amekuwa moja ya wafadhili tegemezi hapa”Aliongea na Hamza alitingisha kichwa kukubaliana nae.
Na wakati huo wakiongea Madam Dorisi alijiiunga nao na stori ziliendelea .
Zilipita dakika chache tu mgeni ambae alikuwa akisubiriwa aliweza kufika , Hamza alikuwa na hamu kubwa ya kumuona kweli maana hata Madam Dorisi alionekana kumsifia kama ni mrembo sana huku akimtania akimwambia aangalie asije kupagawa.
Shida ilianza pale Hamza alipo ona gari ambayo iliingia ndani ya eneo hilo,gari hio ni kama alikuwa akiitambua vizuri, kabla hata hajashuka mgeni alimtambua vizuri alikuwa ni Prisila.
Hamza hakuwa hakuamini na alihitaji uthibitisho kutoka kwa Mzee Hizza na alitingisha kichwa kwamba ni yeye huku akiwa na tabasamu. Mzee huyo mara baada ya kuona wawili wakionyesha ishara kama wanafahamina baada ya kuangaliaana kuna kitu aligundua.
Prisila alikuwa amependeza licha ya kwamba alikuwa amevalia kistaarabu sana , hakuvaa mavazi ya kumfanya aonekane wa matawi ya juu sana wala wa hali ya chini sana , alikuwa katikati.
Baada ya kumuona Hamza ndani ya hilo eneo hata yeye alishangaa maana ni kama hakuwa ametarajia kumuona.
Prisila alikumbatiana kwanza na Dorisi huku akimpatia Mzee Hizza mkono na kisha ndio alimsogelea Hamza.
“Ningejua unakuja huku nisingepanda treni , ungenipa lift tu”Aliongea Hamza huku akijifikiria kwanini kila anapomaliza kikao chake na Frida mtu anaekutana nae baada ya hapo ni Prisila , ilikuwa ni kama mara ya pili hio inatokea.
“Kumbe mnafahamiana?”Aliuliza Dorisi aliekuwa na tabasamu na mshangao.
“Nafahamina nae huyu ni mfanyakazi wetu , nimeshangaa kumkuta huku”Aliongea Prisila huku akiongea kwa macho yaliojaa wasiwasi na jambo lile hata Hamza aliliona.
“Hapa ni nyumbani, amekuja kusalimia”Aliongea Mzee Hizza na kumfanya Prisila kushangaa kidogo.
“Njooni tukae kwanza ili tujue mmekutana lini tena kwa mara ya pili mkiwa wakubwa”Aliongea akicheka na kauli ile ilimfanya Prisila kushangaa zaidi na kujawa na maswali mengi.
“Dada Dorisi ongea na Agustino, kuna oda nimeweka Msamvu dukani kwa Mzee Salum , sikutaka kununua vitu bila ya kujua kipi kimepelea”Aliongea na Dorisi aliitikia na kuondoka na kubakia Hamza na Prisila.
“Prisila yule bwana niliekuambia ni huyu na yeye anaonekana kukumbuka, Hamza huyu ndio Prisila uliesema ana mashavu makubwa akiwa mtoto”
“Dean mimi sikuwa na mashavu”Aliongea Prisila huku akionyesha kushangaa japo alikuwa na furaha lakini pia alikuwa na wasiwasi.
“Hamza kasema kitu kilichomkumbusha ni mashavu yako , ni maneno yake sio yangu”Aliongea huku akicheka.
“Mzee Hizza nadhani imepangwa tukutane tukiwa ukubwani , mimi na Prisila tunafanya kazi kampuni moja ila kumbe tulijuana tukiwa watoto?”Aliongea Hamza.
“Kila jambo lina sababu yake , kama ambavyo sikutegemea ungerudi kwenye kituo chetu kunisalimia ni kama hivi wewe na Prisila”Aliongea na kumfanya Hamza kukumbuka siku ambayo alifika Tanzania na kukutana na Mzee Hizza kama mtu wa kwanza kumjua.
Mzee Hizza alikuwa ni kama mmiliki wa hicho kituo na karibia ujana wake wote ameumalizia kukiendesha , hata kipindi ambacho wafadhili waliondoka ni yeye aliepambana kuendelea kukisimamia mpaka kuja kupata wafadhili wengine.
Kwa muda huo mzee huyo hakujua chochote juu ya Hamza kuandishika ndoa na maswala mengine, hivyo alijua pengine kukutana kwa Prisila na Hamza kutafungua milango mingine.
Stori ziliendelea ndani ya eneo hilo na kutokana na uchangamfu wa Mzee Hizza hata Prisila ambae alikuwa na wasiwasi alichangamka.
Baada ya maongezi machache Prisila yeye alienda kusalimiana na watoto na Hamza na mkuu wa kituo walibakia kuongea.
Moja ya vitu muhimu ambavyo Hamza alimuuliza ni kama kuna kitu chochote amekumbuka juu ya aliemleta kituoni hapo wakati akiwa mtoto, lakini kauli ya Mzee Hizza haikubadilika.
Kauili yake ilikuwa ni ileile ya siku zote kwamba Hamza aliachwa kituoni na mtu aliejitambulisha kwa jina la Mzee huku akitoa maelezo Hamza angekuja kuchukuliwa na mzazi wake.
Hamza alikuwa akijua kauli hio ilikuwa ikimaanisha nini, lakini alitamani kumjua mtu ambae alimuacha hapo kituoni , kuna kila hisia mtu huyo alikuwa ni Mzee anaemjua maisha yake yote lakini hakuwa na uhakika kwasababu Mzee Hizza hakumuona vizuri na mtu ambae inasadikika alimuona kwa macho kasema keshafariki muda mrefu.
Kwahio Hamza katika kipindi chote alichofika Tanzania alikuwa akitembelea kituo hicho mara kwa mara
Prisila alionekana kutokuwa na muda mrefu wa kukaa hapo hivyo aliaga na Hamza hakutaka kumuachia aondoke , isitoshe walikuwa na mengi ya kuongea hivyo aliomba lift na Prisila.
Hata Mzee Hizza licha ya kutaka Hamza abaki kwa chakula cha mchana lakini alitaka waondoke pamoja na Prisila ili wapate muda wa kuondoka.
Hamza kabla ya kuondoka alitoa cheki ya kiasi cha pesa ambacho alikipata kwa bosi Laizer na kumpatia Mzee Hizza.
Ilikuwa cheki ya hela nyingi mno hivyo ilimfanya mkuu huyo kusita kupokea, isitoshe alimuona Hamza bado hakuwa ameyapatia maisha kama Prisila , hivyo alishangaa kupewa cheki ya hela nyingi kiasi hicho.
Lakini Hamza alimwambia sio kwa ajili yake bali ni ya watoto na Mzee Hizza alipokea kwa unyenyekevu huku akimshukuru sana Hamza kwa kutatua changamoto ambayo ilikuwa ikiwasumbua, alimuona Hamza kama malaika.
Upande wa Prisila aliona tukio hilo la Hamza kutoa kiasi kikubwa cha pesa , kilikuwa kiasi kingi mno na hajawahi kutoa kiasi hicho , sio kama hakuwa na roho ya kutoa hiko kiasi ila ukweli ni kwamba uwezo wa kutoa kiasi hicho mara moja hana.
Kutokana na kitendo kile kidogo alionyesha hali ya wasiwasi kwenye macho yake kupungua.
“Prisila kuna kitu kimetokea , najua hatukufahamiana sana utotoni kiasi cha kuwa na furaha baada ya kujuana ukubwani lakini kuna hali ya wasiwasi kwenye macho yako tokea unafika hapa” Aliongea Hamza wakati wakiwa kwenye gari Hamza akiwa ameomba kuendesha.
“Ukiachana na kazi yako kama msaidizi wa Regina ni kazi gani nyingine unafanya?”Aliuliza Prisila akiwa siriasi na swali lile lilimshangaza Hamza.
Comments