SEHEMU YA 76.
Baada ya kupandishwa kwenye gari walichukua uelekeo wa kurudi Mbagala na ndani ya dakika chache tu walikunja kushoto na kuingia katika kambi ya jeshi.
Eneo hilo licha ya kuhifadhia maghala makubwa ya siraha za kijeshi lakini vilevile lilikuwa na gereza la siri ambalo hufungia wafungwa maalumu.
Ndio gereza ambalo mara nyingi lilitumiwa na kitengo cha MALIBU na TISA kwa ajili ya kuhoji na kutesa kupata taarifa.
Hamza mara baada ya kutolewa kwenye gari ndani ya eneo hilo alipelekwa mpaka kwenye nyumba ambayo ilikuwa imejengwa kwa mawe, jengo hilo lilionekana kama ngome ambayo haina madirisha.
Mara baada ya kupitishwa kwenye mlango mpana wa chuma hatimae aliingizwa kwenye chumba maalumu cha mahojiano ambacho kilikuwa kama sero.
Chumba hicho kilikuwa kimezungukwa na vioo vigumu ambavyo havipitishi risasi na hata kuhimili mlipuko wa bomu la kawaida, kulikuwa na kila aina ya ufundi uliotumika eneo hilo kuhakikisha usalama na ilimshangaza Hamza huku akijiuliza kama kuna mtu ambae ashawahi kufikishwa ndani ya eneo hilo.
Hamza alikarishwa kwenye benchi na kujikuta akigeuza macho na kugundua kulikuwa na kila tahadhari zilichochukuliwa , ilikuwa ni kama vile waliomleta hapo walikuwa wakimhofia na kujikuta kutamani kucheka.
Lakini kitendo cha kuona namna ambavyo chumba hiki kimejengwa aliamini pengine Tanzania sio nchi ya Amani kama ambavyo alitarajia,pengine kuna mambo mengi yanaendelea chini chini.
Ikumbukwe kwamba kutengeneza chumba kwa vioo ambavyo vina uwezo wa kuzuia risasi na bomu gharama yake ni kama kutumia dhahabu, sasa kama nchi imeamua kutumia kiasi chote hiko cha hela kujenga eneo hilo aliona haiwezi kuwa bure.
Haikuchukua dakika nyingi wanajeshi kadhaa waliovalia kombati za jeshi waliingia , wakiongozwa na Afande Mdudu, mmoja kati yao alikuwa amevalia kombati za jeshi la polisi zenye cheo cha Kamishina.
Afande Mdudu alikuwa na tabasamu kama lote , kitendo cha kumwingiza Hamza kwenye eneo hilo alijiona mshindi na hakuwa na wasiwasi tena.
“Hamza huyu ni Kamanda Wazo mkuu wa kitengo cha Special Crimes,huyu mwingine ni mtaalamu wa mahojiano alietumwa kutoka makao makuu ya polisi , anaitwa Afande Maningi, Hawa ndio walikuwa bize kudili na kesi yako hivyo unapaswa kutoa ushirikiano kwa kuwajibu kila watakacho kuuliza bila kupindisha”Aliongea Mdudu.
Baada ya kuwatambulisha Afande Mdudu alivuta viti viwili na kuwapa ishara wale ma’afande kukaa .
Wote walionekana kuwa na vyeo vikubwa kuliko hata Afande Mdudu, hata ambae alikuwa na sare za jeshi la polisi alionekana pia ni mwenye cheo kikubwa kutokana na vyeo vilivyokuwa kwenye sare yake.
Afande Wazo aliwapa ishara ya kuondoka wanajeshi wote waliokuwa wamefuatana nao.
“Mnaweza kuondoka , huyu mfungwa yupo kwenye selo yenye ulinzi mkali hata kama ana uwezo mkubwa hawezi kufanya chochote”Aliongea Kamanda Wazo.
“Anachomaanisha kamanda mahojiano haya yanapaswa kuwa siri hivyo mtupe nafasi ya kufanya kazi yetu”Aliogea Afande Maningi na kufanya wale makomandoo na baadhi ya wanajeshi wengine kutoka ndani ya eneo hilo na kuwaacha.
“Hili gereza lenu ni la kisasa mno mnaliitaje?”Aliuliza Hamza huku akichezesha miguu chini.
“Ukisikia Dragon lair ndio hili gereza , hakuna mtu ambae ashawahi kuingizwa hapa akatoka kwa hiari yake hata kama ana uwezo namna gani , tunao uwezo wa kukufungia hapa mpaka ukafa”Aliongea Afande Mdudu huku akicheka.
“Kwa maelezo yako hata mimi naamini hili gereza ni la hatari”Aliongea Hamza huku akitabasamu.
“Hamza huna haja ya kuwa na wasiwasi , sababu kubwa ya kukuleta hapa ni kutaka majibu juu ya maswali yetu , kama huna kosa hatuwezi kukusingizia”Aliongea Kamishina.
“Oh , maswali gani hayo afande?”
“Kwa muda mrefu kidogo tulikuwa tukifanya uchunguzi juu ya maninja wanaojiita wawindaji kutoka Samar ambao walikutwa wameuwa wilaya ya Bagamoyo , baada ya uchunguzi wetu tulibaini wewe ndio muhusika, hawa watu wametokea nchi ya Ufilipino na sio rahisi kuja Tanzania na kuuwawa hivi hivi , siku ya jana tumeweza kukamata wengine wawili ambao walijaribu kuzamia hapa nchini kama watalii na baada ya kuwafanyia mahojiano ya kina wamesema kwamba
wanafuatilia siri uliokuwa nayo juu ya kitu kinachoitwa Ankh”Aliongea Kamishina Maningi na kauli yake ilimfanya Hamza kukunja sura.
Hamza alijiambia inamaana wale wapuuzi hawakukata tamaa tu au walikuja kufuatilia kwanini wenzao hawakurudi, lakini hata hivyo aliona haiwezekani, mara nyingi wawindaji hao wa binadamu wakitumwa katika misheni kuna mmoja kazi yake ni kufuatilia kisirisiri maendeleo ya misheni hio , hivyo Hamza aliamini kwa onyo alilotoa lingefika kupitia huyo mwenzao.
“Hamza hawa bounty hunters inaonekana bado hawajakata tamaa na wamerudi tena nchini na kutaka hiki kitu kinachotwa Ankh, kwa taarifa yako hivi unajua kwasababu yako nchi imeingia katika hatari huko mipakani kutokana na ongezeko kubwa la wahalifu kutaka kuingia nchini?”
“Hilo kundi ni daraja B na kwa taarifa nilzokuwa nazo kitengo chenu cha MALIBU kinahesabika kama Daraja A kwa kuwa na wataalamu wengi wenye mbinu mbalimbali za kupambana mpaka na nguvu za giza , kinachowaogopesha nini juu ya hawa Wasamar?”Aliongea Hamza.
“Hili sio swala la sisi kuogopa ama kutokuogopa , tunachotaka kujua ni mzizi wa haya yote , mpaka sasa ma Ajenti wetu wanaendelea kuwahoji hawa Wasamar lakini hatujapata majibu , tunachotaka kujua kutoka kwako hiki kitu kinachoitwa Ankh ni nini?, kwa maelezo yao wanachosema Ankh ni kama dawa ya uzima wa milele , wengine wanasema Ankh ni kitabu cha ufunuo, sasa wewe tunataka utupe majawabu ya kipi ni kweli, pili sisi kama serikali utupatie hio Ankh ili tukutunzie , vinginevyo uwepo wako hapa nchini unaweka usalama wa nchi rehani”
“Si useme tu na wewe unachotaka ni Ankh, kwa bahati mbaya hicho kitu wanachozungumzia ni uzushi tu wa kinadharia ila hakuna kitu cha namna hio”Aliongea Hamza.
“Ongea ukweli wewe”Aliongea Afande Maningi huku akipiga kofi meza.
“Hawa wazamiaji wamesema kitu ulichokuwa nacho kimetoka kwa mwanasayansi nguli wa kihistoria maarufu kama kichwa cha Tembo au Dokta Genesha na ndani ya maabara yake aliacha anuani ya uelekeo wako na ndio maana wamekupata kirahisi hapa Tanzania. Kama ni kweli unafahamiana na Dokta Genesha basi wewe sio mtu wa kawaida, taarifa tulizokuwa nazo mpaka sasa haijulikani kama kweli Dokta Genesha amekufa ama yupo hai na hata mara ya mwisho alipozushiwa kifo chake iliaminika yupo hai baada ya kuwasiliana kwa siri na wewe, kwa mantiki hio lazima utakuwa na taarifa ya siri ambayo hutaki kuongea”
“Ushasema taarifa ambayo sitaki kuongea , kwanini nikuambie sasa Afande?”Aliongea Hamza.
“Kuwa na adabu , endelea kuongea dharau uone kitakacho kupata, unajua wewe ni nani hapa ndani? , wewe ni mfungwa na ukiendelea kuongea uongo usije kulaumu tukichukua hatua nyingne kali zaidi?”
“Elezea hizo hatua kali zaidi?”Aliuliza Hamza huku mwonekano wake ukibadilika palepale.
“Tuta..”Kabla hajaongea alizuiwa na Afande Maningi.
“Hamza huna haja ya kuwa mkali juu ya hili, sisi jukumu letu kama wanajeshi ni kuhakikisha usalama wa nchi unaendelea kudumu na kwakuwa wewe ni raia wa nchi yetu tunapaswa kujua hiki kitu kinachoitwa Ankh ni nini ili tupate namna ya kukulinda bila kuathiri usalama wa nchi , ukituambia kila kitu hatutafanya mambo kuwa magumu kwako , isitoshe tunajua wewe sio mtu wa kufanya vitu ambavyo vinaweza kuumiza usalama wa nchi”Aliongea na kumfanya Hamza kuwaangalia kwa zamu.
“Kwahio ni wewe unaetaka kujua hii siri ama ni serikali inayotaka kujua?”Aliuliza.
“Sisi kujua maana yake serikali imejua , wewe weka wazi Ankh ndio nini?”Aliongea Afande Wazo.
“Kama serikali ndio inayotakiwa kujua basi itifaki ya vyeo inapaswa kuzingatiwa?”Aliongea na kauli ile ilimfanya hata Mdudu kushangaa. “Unataka kumaanisha nini Mr Hamza ?”
“Namaanisha kwamba taarifa unayotaka kujua ni nyeti mno na inaingia katika taarifa za juu za siri za nchi , hivyo kwa cheo chako hutoshi, itifaki hapa ifuatwe nataka kuonana na kiongozi wa juu wa jeshi Daraja S?”Aliongea na kauli ile iliwafanya wote kutoa macho.
Katika nchi yoyote licha ya Raisi kuwa na madaraka makubwa ya kujua siri nyingi za nchi haimaanishi kwamba anaweza kujua kila siri ambayo anataka kuifahamu
Itifaki ya clearence ya siri za nchi huanzia dajara E ambao hawa mara nyingi ni polisi au wanajeshi wa kawaida tu kama wa doria , siri ambazo hawa wanajua ni zile ambazo mara nyingi zinahusisha matukio ya eneo husika ambazo hazina athari kubwa za ki’usalama hata zikiwa wazi, mara
nyingi maelekezo ya siri hizi hutolewa kwa mdomo tu kama onyo la kutoongea chochote.
Daraja D hili ni daraja ambalo huhusisha polisi au wanajeshi pia lakini wale polisi wa vyeo vikubwa ambao wengi wao wanafanya kazi mpaka kwenye vitengo vya usalama wa taifa , hawa wanakuwa daraja D kwasababu watu wa daraja E wote huwasilisha hizi taarifa kwao na kuamua ni siri gani iweke daraja lipi.
Daraja C hili linahusisha siri zinazoendelea katika vikosi maalumu kama vile tukio la Hamza kuua Wawindaji kutoka Samar , hio operesheni inasimamiwa na vitengo maalumu vya uchunguzi na mara nyingi hapa unaweza wakuta polisi au wanajeshi mfano wa Afande Mdudu na kuendelea.
Daraja linalofuatia sasa linakuja B halafu linafuatia daraja A , Daraja A hapa anazungumziwa raisi wa nchi , Amiri jeshi mkuu na baadhi ya viongozi wenzake wa juu, mara nyingi ikitokea siri ambayo inahitaji operesheni ndani ya eneo la tukio hapa wanahusishwa watu wa Daraja B.
Daraja B anaweza kuwa mwanajeshi yoyote anaweza kuwa hata na cheo cha Ukapteni lakini akawa na Clearence ya kujua siri zote zinazoendelea katika daraja B kwa kibali maalumu kulingana na kile anachofanyia uchunguzi.
Siri zote ambazo zinatokea katika Daraja A yaani ngazi ya raisi ambazo ni nyeti hupewa hadhi ya Top Secret na hizi watu wanaopewa Clearence ya kuziona ni Daraja S.
Sasa daraja S katika itifaki hio ni daraja ambalo lijategemea kabisa na hili ndio huwa na uwezo wa kujua siri kubwa za nchi(Top Secret) siri ambazo hata kama raisi azihitaji hapewi au kama akizitaka anapaswa kuomba ruhusa kwanza kwa watu wa hili daraja.
Raisi anaweza kujua siri za daraja S lakini ni baadhi na mara nyingi siri hizo zote huwa zinatokea katika kipindi chake cha uongozi , lakini ikitokea anahitaji siri ambazo zimetokea katika uongozi uliopita ambazo zipo chini ya Daraja S ni mpaka apate kibali ambacho kinaambatana na sababu maalumu na ikitokea akikataliwa hana cha kufanya kisheria.
Bila shaka kuna baadhi ya taarifa nyeti sana ambazo baadhi ya wanajeshi wanajua siri hizo wakati wa uchunguzi lakini hata kama walihusika kwenye uchunguzi wakitaka taarifa hio hawawezi kupewa ruhusa.
Hayo madaraja ni mfano tu ila kila taifa lina itifaki zake namna ya kutoa hizo Clearence lakini zinakuwa katika mtiririko huo katika kuhakikisha usalama wa nchi unazingatiwa.
Lakini pia kuna itifaki ambayo inahusisha kujuana nani anaclearence ya daraja lipi , kwa mfano asilimia nyingi ya wanausalama ambao wana Clearence ya daraja C hawajui nani ana Clearence(Uwezo wa kufungua) ya daraja S.
Kwa mfano kuna matukio ambayo yakawa yametokea katika uongozi wa kwanza wa serikali , matukio kama haya licha ya kwamba kuna uwezekano wa kuyafuta lakini serikali kama serikali haipaswi kuyafuta kutokana na kwamba kuna siku yanaweza yakahitajika hivyo hutunzwa katika jalada la siri nyeti za nchi.
Sasa Hamza alikuwa akitaka kutoa siri yake kwa mwanausalama ambae yupo daraja la juu kabisa ambalo ni S kitu ambacho kiliwafanya Mdudu na wenzake kumuona kama ana kichaa
“Unakichaa , wewe ni nani mpaka mpaka tukutie mtu wa cheo hicho?”Aliongea Afande Mdudu huku akionyesha kutoridhishwa na Hamza kabisa.
“Hamza unapaswa kutuambia ukweli , haina haja ya kupotezena muda la sivo tutatumia njia za mateso”Aliongea Afande Wazo.
“Mimi nimekuona kama mtu ambae una akili , lakini hapa unaonekana kama mtoto mwenye kiburi uliejaa sifa kiasi cha kutaka kuonana na kiongozi wa daraja la juu”
“Mnaongea sana , ila je kuna hata mwenye fununu
kati yenu juu ya hicho kitu kinachoitwa Ankh?”Aliuliza Hamza
“Kimya , kama hutaki kuongea ukweli hatuwezi kuendelea kubembelea”
“Kwahio mpo tayari kutumia nguvu kwa ajili ya hili?, kama ni hivyo msije kwenda kinyume na maneno yenu”Aliongea Hamza kwa namna ya tahadhari
Mara baada ya kuona namna ambavyo Hamza alionekana kutokuwa na hofu , wote watatu walijikuta wakisaga meno yao kwa hasira.
Kwa yale matukio machache waliokwisha kuona walijua kabisa Hamza uwezo wake sio kichekesho , lakini bado walishangaa kama alikuwa kwenye Gereza lao la Pango kwanini bado auaonyesha ukiburi.
“Kama unataka kuonana na kiongozi ambae ana Clearence daraja S , tukuambie tu kwamba hata sisi hatuwajui hawa viongozi maana majina yao ni siri , pili hata kama tunamjua mmoja wapo ni watu ambao hatuwezi kuwaambia kiwepesi wepesi lazima hatua za maombi pamoja na sababu za kueleweka zitolewe , kwahio hili ombi ambalo unataka halina mantiki, hivyo hakuna namna tunaweza kulitimiza”Aliongea Afande Maningi. “Kwa ulichoongea ni sahihi kabisa, kwa vyeo vyenu hapa sioni kama kuna amabe atakuwa anawajua hawa watu wa usalama wenye madaraja hayo ya Clearence , mnaonaje tukifanya hivi, kwa uelewa wangu katika kila idara ya ulinzi na usalama hapa nchini wapo wawili au watatu”Aliongea Hamza na kauli yake ilimfanya Afande Mdudu na Afande Wazo kuonyesha hali ya wasiwasi maana hawakujua Hamza imekuwaje akawa na taarifa hio maana yenyewe ni siri ya daraja C.
“Kuhusu mtu ambae nataka aje hapa kama sikosei cheo chake kitakuwa ni maarufu kama Mshauri wa jeshi”Aliongea Hamza kana kwamba anajaribu kukumbuka jina lakini kauli yake iliwafanya wale wanajeshi kushituka.
“Unafaamiana na Mshauri mkuu!!?”Aliuliza Afande Mdudu maana alikuwa akifahamu mshauri mkuu ndio huyo huyo mshauri mkuu wa jeshi.
“Mdudu anazungumzia mshauri yupi?”Aliuliza
Afande Maningi , sio kama hakujua ni kwasababu kulikuwa na washauri wengi na wote walikuwa wanajeshi.
“Ni Generali, Afande Himidu Siwa , unaweza kumuita mkuu wa vitengo vyote, kwanzia kitengo cha TISA, Malibu na kuendelea, hana cheo maalumu ila anafahamika kwa jina la code kama Mshauri Mkuu, kwa muda mrefu watu wanajua mshauri mkuu wa jeshi ni mkuu wa majeshi lakini yeye ndio mshauri mkuu sasa , kwa mtu ambae upo nje ya jeshi huwezi kuelewa, Afande Himidu alipaswa kuwa mkuu wa Majeshi mara mbili mfululizo lakini alikosa kigezo cha umri na kuishia kutoa ushauri wa majina ya nani awe mkuu wa majeshi huku yeye akijipachika cheo cha ushauri mkuu”Aliongea Mdudu.
Viongozi wengi wakisiasa walikuwa wakimheshimu Afande Himidu kutokana na kwamba ndio ambae alikuwa na cheo kikubwa katika utunzaji wa siri za nchi , hivyo kwa lugha nyepesi alikuwa akijua siri nyingi mno.
Kwa namna ambavyo Hamza alikuwa akiongea ni kama Afande Himidu alikuwa akimjua na hatanii katika hilo na ndio maana iliwafanya Afande Mdudu na wenzake kuwa na wasiwasi wakijiuliza amemjuaje.
“Unatuthibitishia vipi kama Afande Himidu anakufahamu na kwanini akubali kuonana na wewe?”Aliuliza Afande Wazo.
“Akigoma kuja kwa jina la Hamza, mwambie Murphy anataka kuonana na wewe”Aliongea Hamza.
“Mafiii!?”
Afande Wazo , Afande Maningi na Mdudu hawakujua jina hilo lilikuwa linamaanga gani ila limekaa kwa kingereza.
“Fanyeni haraka maana najua yupo makao makuu ya nchi , mimi nitatumia huu muda kujipumzisha kidogo mpaka akija maana mmenichosha bure tu”Aliongea Hamza na palepale alipandisha miguu kwenye benchi na kujinyoosha akiwa amejiagamiza na kufumba macho.
Ilikuwa sawa kupumzika maana kama kweli
Mshauri mkuu atatoka Dodoma mpaka kufika Dar basi inaweza kuchukua angalau masaa mawili mpaka kupanda ndege na kuanza safari.
Walikuwa hawajaridhika na maelezo ya Hamza lakini Afande Wazo alikuwa makini sana na cheo chake , hakutaka kukurupuka mpaka awasilishe ripoti kwanza kwa mkuu wa kitengo chake na kisha mkuu wa kitengo chake atoe taarifa kwenda kwa Mshauri mkuu.
“Nitawasiliana na Afande Msuya na atajua namna ya kumfikishia taarifa Afande Himidu, weka watu hapa wawe wanamwangalia”Aliongea Afande Wazo huku akitoka.
Kesi hio ya Hamza ilikuwa chini ya Mkuu wa kitengo msaidizi Afande Msuya na kwa kufuata itifaki hata kama Afande Wazo alikuwa na namba ya mshauri mkuu basi asingempigia simu moja kwa moja.
“Fanya hivyo afande , huyu haina haja hata ya kumuwekewa watu wa kuangalia , hii sehemu hawezi kutoka hata kama a na uwezo kiasi gani”Aliongea Afande Maningi na wote walikubaliana nae.
*****
Mji kuu wa kiserikali licha ya kuwa na vumbi la kuchafua pamoja na jua la saa tisa mchana kwenda saa kumi kuwa kali kwa watu wenye vyeo na matajiri hawakusumbuliwa na hali hio ya karaha ya mji.
Haikuwa nyumba kubwa sana wala ndogo sana , ilikuwa ya wastani lakini yenye mazingira ya kuvutia ambayo yaliwakilisha hadhi ya mtu anaeishi ndani ya hilo eneo katika mtaa maarufu wa Mji mpya.
Upande wa eneo la bustani ndani ya nyumba hio walionekana watu wawili mwanamke na mwanaume wakiwa wamekaa katika eneo la bustani la kupumzikia pembeni ya Swimming pool.
Mwanaume alikuwa amevalia tshirt ya rangi ya ugoro , jeans na American boot , alikuwa na kipara na muonekano wake ulikuwa wa kawaida lakini macho yake yalijaa umakini ulioonyesha utulivu wa akili..
Upande wa mwanamke aliekuwa nae alikuwa mrembo haswa alievaa akapendeza , nywele zake ambazo haikufahamika ni za bandia au asili zilikuwa ndefu na nyeusi zilizomfikia mgongoni , alikuwa amevalia kana kwamba ni mgeni ambae yupo ndani ya hilo eneo kwa ajili ya kumpagawisha mwanaume aliekuwa pembeni yake.
“Ni watu wachache sana ambao wanaweza kucheza mchezo wa Chess hapa nchiin na mmoja wapo ni wewe Sophia . ijapokuwa nakwenda kushinda hii mechi lakini niseme umezidi kuimarika tokea mara ya mwisho tulivyocheza pamoja , sio mbaya licha huwezi kunishinda pengine siku zijazo utafanikiwa ukiendelea na mwendo huu huu”Aliongea yule mwanaume kwa sauti nzito na kisha alichukua chupa ya maji na kunywa kidogo huku akimsubiria yule mwanamke mrembo kucheza.
Wawili hao walikuwa makini katika kucheza mchezo maarufu wa Chess.
Mwanamke yule mrembo alionekana kukodolea ubao ule wa kuchezea kwa macho yenye hali ya kutafakari kwa kina, upande wa mwanaume simu yake ya batani iliokuwa na mkonga mkubwa ilianza kuita na aliichukua na kuipokea.
“Ongea!”Alitikia akiwa sirasi , mara nyingi akipokea simu kupitia simu hio basi ni ya kikazi ndio maana anakuwa siriasi.
“Mshauri mkuu , jina langu ni Afande Msuya..”
“Hebu acha kuzunguka nishakufahamu , nenda moja kwa moje kwenye pointi”Aliongea kwa sauti ya amri kama mtu ambae hakupendezwa kupigiwa simu hio.
“Sawa afande , ipo hivi kuna operesheni maalumu ya ki uchunguzi ambayo inaendelea hapa kitengoni chini yangu , katika operesheni hii tumeweza kumkamata mtuhumiwa anaefahamika kwa jina la Hamza Mzee , nimepokea simu kutoka kwa wanausalama wakiwa wanamfanyia mahojiano na amekataa kutupa taarifa na anataka kuonana na wewe Afande”Aliongea .
“Hamza Mzee!!”Aliongea yule bwana huku akionekana kama vile anawaza wapi amesikia hilo hina lakini hakukumbuka.
“Simfahamu mtu wa jina hilo mimi , hili swala mnaweza kudili nalo wenyewe sidhani linahitaji ushauri wangu , sitaki ripoti za namna hii kuripotiwa kwangu”Aliongea na muda ule wakati akitaka kukata simu upande wa pili uliropoka.
“Anasema Murphy anakuita”Aliongea na jina lile lilimfanya yule bwana mwenye sura ya maji ya kunde kukunja sura kiasi cha kumfanya mwanamke mrembo aliekuwa pembeni yake kumwangalia kwa wasiwasi.
“Wewe.. umesemaje hebu rudia vizuri?”
“Amesema kama humtambui kwa jina la Hamza, nikuambie Mafi…. Murphy anakuita”Sauti upande wa pili ilirudia na kumfanya yule bwana kuvuta pumzi nyingi na kuzishusha.
“Waambie wanisubiri wasifanye chochote , narudia huyo mtu ambae umesema anaitwa Hamza asichokozwe , nitafika hapo ndani ya lisaa limoja au mawili yajayo kwa kutumia chopa ya jeshi”Aliongea kwa msisitizo.
“Mshauri ni kweli unafahamiana na huyu Hamza?”Upande wa pili uliuliza kwa namna ya mshangao.
“Hata mimi simjui ni nani mpaka nimuone mwenyewe”Aliongea na kisha palepale alikata simu.
“Sophia nataka kwenda Dar es salaam mara moja , nina haraka , vipi tuongozane wote?”
Mwanamke huyo mrembo alievalia nguo za rangi nyekundu aliishia kutingisha kichwa kukataa bila ya kusema neno.
“Naona kwa leo mechi yetu inaishia hapa ,
isitoshe sikuwezi na nakufanya usifurahie mchezo, nakuombea apatikane mtu wa kuendana na uwezo wako”Aliongea kwa namna ya kuvutia kana kwamba anamtega.
“Nadhani kuna kitu kingine tunaweza kupimana uwezo”Aliongea na kauli yake ilimfanya yule mrembo ukauzu kumvaa palepale na ghafla tu aliinua mkono wake wa kulia na kuanza kuchezesha vidole katika muundo wa ajabu na hazichukua sekunde vitu kama moshi moshi ulitawala vidole vyake.
“Upo sahihi , siku nyingine nitakuonyesha ufunuo niliopata kwenye kuvuna nishati za mbingu na ardhi”Aliongea .
“Naisubiri hio siku kwa hamu kubwa”Aliongea Afande Himidu na yule mwanamke alitingisha kichwa na kisha akasimama na kitendo cha kuinama kama mchawi alipotea palepale.
********
Masaa kama mawili mbele katika eneo la kambi ya jeshi walionekana Afande Mdudu na wenzake wakipiga saluti mbele ya Kamanda Himidu anaeshuka kwenye chopa huku wakijitahidi kupotezea wasiwasi wao na tabasamu la kulazimisha.
“Afande umetokea ghafla sana , tulikuwa tukipanga kuja kukupokea na escort”Aliongea Afande Wazo lakini upande wa Afande Himidu hakuwa na muda wa kuongea nao kwani baada ya kutoka kwenye chopa aliwapita. “Huyo Hamza yupo wapi?”Aliuliza
“Yupo ndani ya Dragon Lair Afande”
“Nini!, yaani mmefungia ndani ya hilo gereza, vipi hakuwaletea ukinzani wowote?”Aliongea huku akionyesha mshangao kidogo.
“Afande hakuleta ukinzani pengine ameogopa wingi wetu , anaweza kutushindwa mmoja mmoja
lakini kwa wingi wetu hawezi kufanya chochote”Aliongea Afande Wazo kwa majigambo.
“Una akili kweli wewe , unajua hata ninachomaanisha , nakuuliza je mpo salama?”Aliuliza lakini swali lake liliwachanganya.
“Afande unauliza nini kuhusu usalama?”Aliuliza lakini Afande Himidu hakutaka hata kuwaelezea kile anachoataka kumaanisha.
Afande huyo mara baada ya kuingia ndani na kumwangalia Hamza kupitia kioo kizito kilichokuwa mbele yake mshangao ulivaa palepale huku pumzi yake ikiwa nzito ni kama vile ameona mtu ambae hakutarajia kumuona.
“Mshauri yule ndio Hamza”Aliongea Afande Maningi.
“Nani alietoa wazo la kumfungia pale?”Aliuliza akiwa siriasi na kuwafanya Afande Wazo na Afande Maningi kuangaliana , wao sio ambao walikuwa wamemkamata Hamza Afande Mdudu ndio alifanikisha hilo na wao walipewa jukumu la kumhoji pekee.
Comments