Baada ya wote kumwangalia Afande Mdudu na Mshauri pia alimwangalia Mdudu akionekana anahitaji maelezo na kumfanya afande huyo sura yake kuzidi kuwa nyeusi.
“Afande naripoti kwako.. mimi ndio nimemkamata”
Afande Mdudu hakuona haja ya kujificha muda huo hivyo aliamua kuuvaa ujasiri na kusogea mbele.
Ukweli ni kwamba hata alipoomba ruhusa kwa mkuu wake wa misheni Afande Msuya alipewa maelekezo ikitokea ameshindwa kumkamata Hamza basi ajisalimishe kama alichukua maamuzi peke yake , ijapokuwa ilikuwa kweli Msuya alikuwa akitaka kumkamata Hamza lakini alipingana na wazo hilo kwa kuhofia kile ambacho anaweza kufanya lakini Mdudu alilazimisha.
“Afande nimemkata kwasababu mpaka sasa ameua watu wengi , tulikuwa na wasiwasi ataende…”
“Haina haja ya kuendelea kuongea”Aliongea Afande Himidu akimkatishia njiani .
"Mdudu kama niko sawa wewe ni mtoto wa pili wa
Mkuu wa Majeshi aliepita Afande Mbwana?”
“Ndio afande , babu yangu pia ni waziri mkuu mstaafu”Aliongea kwa kujiamini.
“Huna haja ya kuendelea kuelezea vyeo vya wanafamilia yako , japo ni kweli familia unayotokea ni ya watu maarufu lakini haitoshi katika hali kama hii”Aliongea na kumfanya Afande Mdudu kuonyesha hali ya kuchanganyikiwa.
Ukweli alikuwa akijiamini katika sehemu nyingi , sifa za jina la familia yake lilikuwa likimtangulia katika maeneo mengi , sasa alijiuliza inakuwaje jina lake hapo lisitoshe au Afande anajaribu kuongea kitu gani.
“Afande umeulizia kuhusu familia yangu , hili swala lina uhusiano?”Aliuliza.
“Unaweza kufikiria unachoweza , ila itakuwa vizuri kama ukiongea na baba yako kwanza umwelezee kilichotokea leo, pengine inaweza kukusaidia”Aliiongea lakini kauli yake ilizidi kumchanganya Mdudu kwani hakuwa akijua ni kitu gani amekosea..
Hata upande wa Afande Wazo na Maningi hawakuelewa Mshauri anachojaribu kumaanisha.
“Acha kuonyesha dalili za kuchanganyikiwa , ninachomaanisha hapa fanya kila namna kuokoa maisha ako”Aliiongea.
“Lakini Afande baso sielewi , sijui kama kuna kosa lolote nimefanya kiasi cha kutaka kunipa adhabu”
“Una uwezo mdogo wa kufikiria na sijui aliekupatia uongozi wa hii kesi alikuwa akilenga nini , ninachomaanisha yule mtu akitoka unaweza usiwe salama na akiamua kukuua sitoweza kumzuia”Aliongea na mara baada ya kusikia maelezo hayo alijikuta akitetemeka.
“Lakini Afande huyu si mfungwa , kwani tunamuachia atoke?”
“Afande anachoongea ni sahihi , sidhani kuna haja ya kumuachia huru , ana siri juu ya kitu kinachoitwa Ankh na inaonekana ni siri ya thamani kubwa mno inayofuatiliwa na watu wengi kiasi cha kuhatarisha usalama wa nchi”
“Ndio Afande Hamza yupo pale na hakuna namna anaweza kutoka kwa hiari yake labda tumuachie bila ya kujali uhalifu wake”Alikazia Afande Mdudu.
Lakini Afande Himidu hakuwa akiwasikiliza kwa maneno yao, macho yake yalikuwa yamemkazia Hamza ambae alikuwa ashasimama tayari na kusogelea kioo huku akijivuta.
Japo kwa ndani ya chumba hicho ilikuwa ngumu kuona anaengalia nyuma ya kioo lakini muda ule ni kama Hamza alikuwa akiangaliana na Afande Himidu kwani alitoa tabasamu la ishara ya salamu na kumfanya hata Afande Himidu kutabasamu pia, huku macho yake yakionyesha ishara ya heshima kwa Hamza.
“Hebu fanyeni haraka , mfungulieni atoke”Aliongea kwa sauti kubwa iliojaa ubabe.
Kundi hilo la wanajeshi waliishia kusita kupokea maagizo hayo , hawakujua wamuachie Hamza au wasimauchie , isitoshe kwao walimuona kama mhalifu na Mshauri anataka kuvunja sheria.
Lakini sasa kilichotokea baada ya hapo kiliwafanya kuganda kama vile wamegeuka mawe ya barafu.
Hamza alikuwa akipiga piga kuta za eneo hilo la ndani kana kwamba anajaribu kuona ni wapi kuna udhaifu na uimara, baada ya kuonyesha kuridhika na kugonga gonga alisogelea kioo na kuweka kiganja cha mkono huku akionekana kufumba macho.
“Anajaribu kufanya nini , au amepatwa na uchizi wa ghafla?”Mmoja aliongea kwasababu waliamini kioo alichoshika Hamza kilikuwa ni kioo kigumu mno ambacho ni kipana kiasi kwamba hakiwezi kupitisha risasi wala kupasuka kwasababbu ya mlipuko.
Afande Maningi palepale wasiwasi ulimwingia na alibonyeza kitufe ambacho kinasafirisha sauti.
“Mr Hamza tunakuomba utulie tutakuachia muda si mrefu”Aliongea , alijua kama kweli Hamza anafahamiana na Afande Himidu basi kuna uwezekano asiwe wa kawaida.
Isitoshe walikuwa ni wanajeshi wa kitengo cha kupambana na nguvu za ziada na kupitia uzoefu na stori nyingi walizosikia juu ya mafunzo mbalimbali ya maajabu walipatwa na hisia za hatari wakiamini Hamza anaweza kuwa na hayo mafunzo ya nishati za mbingu na ardhi.
Hamza aliendelea kushikilia kile kioo kwa nguvu na alioekana kama mtu ambae anasali kwani midomo ilikuwa ikicheza kwa kuongea na kabla hata wale wanajeshi hawajachukua hatua ya kumfungulia eneo hilo lilianza kutetemeka kama vile ni mtikisiko wa ardhi.
Kitu kile kiliwafanya watoe macho washindwe kujua nini kinakwenda kutokea.
Wakati wakishangaa ghafla ule mtikisiko ulipotea lakini Hamza bado alikuwa ameshikilia kile kioo huku akiwa amefumba macho na kuendelea kuongea maneno.
Ghafla tu macho yaliwatoka mara baada ya kile kioo walichoamini hakiwezi kupasuka hata kwa nyundo kikianza kutengeneza nyufa taratibu kana kwamba kinapata kiwango cha juu cha moto ,hazikupita sekunde kumi kioo chote kama vile ni glasi imedondoshwa chini kwani kilipasuka vipande vipande.
Bahati ni kwamba kioo hakikuwa kimoja pekee kulikuwa na layers angalau tatu za vioo vinavyofanana.
“Afande wazo si umesema hivi vioo haviwezi kupasuka hata kama vipigwe na bomu?”Aliuliza Afande Mdudu huku akitetemeka. “Inawezekana vipi kupasua kioo bila ya kutumia nguvu?”Afande Wazo aliekuwa kwenye bumbuwazi.
Ilikuwa ngumu kukubali maana walitumia kiasi
kingi cha pesa kwa ajili ya ujenzi wa hilo eneo , lakini namna ambavyo Hamza alikuwa akividondosha sio uwezo wa kawaida.
Hamza kabla hajafikia kioo cha mwisho Afande Wazo alishikwa na hasira , alitaka kujihakikishia kama ni kweli vioo hivyo vilikuwa vigumu au kuna tatizo , hivyo mara baada ya kushika bunduki alianza kuvimiminia risasi. Lakini hakuna risasi hata moja ilioacha hata ufa kwani zilidunda tu na kudondoka chini.
“Hakuna haja ya kufanya majairibio , hakuna tatizo kabisa na ujenzi wa hili eneo, Shida ni kwamba ana uwezo mkubwa mno na wa ajabu”Aliongea Afande Himidu huku macho yake ni kama amefurahi kuona tukio kama hilo.
Hatimae vioo vyote vilipasuka chini bila ya kupigwa ngumi zaidi ya kuwekewa kiganja cha mkono tu. “Kuna mwenye sigara kati yenu?”Aliuliza Hamza mara baada ya kutoka nje lakini kila mtu alikuwa amemkodolea macho kana kwamba wameona mnyama.
“Mnashangaa nini sasa , au hamhawahi kuona kioo kikipasuka?”Aliongea Hamza na Afande Himidu ndio aliekuwa wa kwanza kushituka.
‘”Inamaana hamjamsikia , hakuna mwenye sigara kati yenu?”Aiuliza na Afande Wazo kwa kutetemeka aliingiza mkono kwenye mfuko wake wa kombati na kuchomoka na sigara na kibiriti.
Upande wa Afande Himidu hakushangaa Hamza kuhitaji sigara , kwa mtu wa kawaida anaweza kuona Hamza hakutumia nguvu kupasua vioo hivyo lakini kwa uelewa wake alijua Hamza ametumia nguvu nyingi tu japo sio zote, kutengeneza resonance pacha kwenye kitu kigumu kama hicho haikuhitaji tu nguvu lakini matumizi makubwa ya ubongo ili kupatia hivyo hufanya akili kupata hali ambayo inaweza kuondolewa na sigara au kilevi.
“Kijana naona una mabadiliko makubwa mno , umepata mke nini?”Aliongea Hamza akimshika bega Afande Himidu huku wakiwa na tabasamu .
Kwa namna ambavyo Hamza alianzisha mazunguzo na afande wa heshima kama huyo iliwafanya Mdudu na wenzake kuzidi kushikwa na wasiwasi.
“Kama ningekuwa nimeshaoa wewe ungekuwa wa kwanza kujua , yaani nifunge ndoa bila ya kukualika mlevi kama wewe”Aliongea Afande Himidu huku akicheka,
“Haha……utaachaje kunialika na unavyopenda vitu vya mteremko , sidhani bila kutoa mchangao wangu utataka kuoa wewe”Aliongea na kumfanya Afande Himidu kujikuta akicheka mpaka mabega yanamtingishika.
Muda huo Hamza akipata muda wa kuangalia watu waliokuwa ndani ya eneo hilo na aliweza kuona kila mtu alikuwa akimwangalia kwa wasiwasi.
“Nyie watu haina haja ya kujenga upya hivyo vioo , ni kujitia hasara tu”Aliongea Hamza huku akiwa na tabasamu la kejeli lakini Afande Wazo na Afande Maningi walikuwa na wasiwasi mno.
“Ndio Afande tumekuelewa” Aliongea Afande
Maningi huku hana uhakika kama kumuita Hamza afande ni sawa , alijaribu kubahatisha kwa namna yoyote ile ili kumtuliza asichukue hatua.
Muda ule Hamza macho yake yalitua kwa Afande Mdudu ambae alikuwa akijificha ficha kana kwamba anatamani kuikimbia hilo eneo.
“Afande Mdudu unajua umefanya kosa gani leo?”Aliongea Hamza na Afande Mdudu alijikuta akitetemeka kwa hofu.
“Sikupaswa kukukamata .. naomba msamaha wako”Aliongea
“Kunikamata halikuwa kosa kwasababu ulikuwa ukifuata sheria na ulikuwa na ushahidi , mtu kushurutisha watu kutii sheria sio kosa hata kidogo”
“Basi kosa langu itakuwa ni
kutokukuheshimu?”Aliongea huku aking’ata meno kwa hasira , mpaka dakika hio ameshindwa kujua kabisa Hamza ni mtu wa aina gani mbona anatisha.
“Mimi sio mtu wa kukasirika kwa vitu vidogo vidogo kama hivyo , hata mimi nisingekuongelesha kwa upole, kosa lako kubwa ni ni kujaribu kunitengenezea udhaifu mbele ya mwanamke huku ukiwa na uhakika mimi ni mhalifu, umeshindwa kunikamata nikiwa Kijichi na kuniwekewa mtego njiani, mpango wako haukuwa kunikamata ila kujaribu kunidhalilisha”Aliongea Hamza huku akionyesha hali ya ukauzu na swala lile lilimfanya Afande Himidu kuingiwa na wasiwasi.
“Ni mtoto wa pili wa mkuu wa majeshi Afande Mbwana, babu yake pia alishawahi kuwa Waziri mkuu”Aliongea.
“Nishayajua hayo yote tokea muda tu , lakini kuwa mtoto wa nani haimaanishi ndio tiketi ya kuachwa afanye atakavvo”
“Unapanga kumuua?” Aliuliza. Afande Himidu akiwa na wasiwasi na Afande Mdudu kwa woga alipiga magoti mbele ya Hamza.
“Hamza naomba unisamehe , nilikosea kweli”Aliongea lakini Hamza ni kama hakuwa hata na hio hasira ya kumuua kama alivyoulizwa , alitaka kumtishia kidogo tu.
“Nikikuua mtu kama wewe nitaonekana kama mtu ambae naonea dhaifu, onyo langu kwako usije kumsumbua Yonesi tena”Aliongea Hamza na mara baada ya Mdudu kusikia kauli hio alijikuta akipatwa na ahueni huku akijiambia kwa muda huo ataacha kumsumbua Yonesi lakinin sio kama atamwacha kabisa.
“Asante sana Hamza” Aliongea huku akijifuta , licha ya kwamba alikuwa mwanajeshi lakini ukweli ni kwamba alilelewa kimayai sana kutokana na utajiri wa familia yao hivyo kumfanya kuwa mjivuni sana.
Sababu ya Hamza pia kutomfanya kitu chochote
Afande Mdudu ni kwa ajili ya Afande Himidu, alikuwa ni rafiki yake hivyo hakutaka kumuingiza kwenye matatizo.
“Mnaweza kutoka nje sasa , nataka kuongea na Hamza, hakuna anaeruhusiwa kusogelea hapa”Aliongea Afande Himidu mara baada ya hali kutulia.
Wote baada ya kutoka nje Afande Himidu ghafla tu alipiga goti kwa mguu mmoja huku akiongea kwa unyenyekevu
“My Prince!!”
“Inatosha Bro , kwanini unafanya hivi kama watu wengine bwana , hatujaonana kwa zaidi ya miaka sita lakini naona bado hujasahau hizi itifaki, nakumbuka kipindi kile ukiwa kambini ulikuwa mjeuri mno lakini baada ya kuimarika ukawa humble”Aliongea Hamza.
“Hakuna mtu yoyote ndani ya Tanzania hii naweza kumpigia magoti , hata awe raisi , kwangu hii ni ishara ya kukuheshimu kama mwalimu wangu na bosi wangu”Aliongea Afande Himidu huku akiwa na tabasamu.
“Haha. Vizuri , lakini naona sasa hivi unaitwa Himidu Mshauri , jina lako la Murphy Stopphilius umelitelekeza , huwa na kukubali sana maana hubadiliki sio kama rafiki yako Mameni”Aliongea Hamza.
Kitu ambacho hawakukijua wakina Afande Wazo na wenzake ni kwamba Murphy halikuwa jina la Hamza bali ni la Afande Himidu.
“Ukweli miaka miwili iliopita niliposikia umestaafu mwanzoni sikuwaza ni wapi utaenda , lakini nikikumbuka kipindi kile ulivyokuwa ukinisumbua kufahamu kiswahili nilijua tu lazima utakuwa hapa nchini na hisia zangu zilikuwa kweli , nimefurahi kukuona sana bosi”Aliongea.
“Mwaka wa kwanza wakati nafika hapa nchini nilikuwa nikijiuliza nikutafute au nipotezee , isitoshe kati ya marafiki zangu wote wewe ndio ulikuwa mtanzania pekee, lakini mara baada ya kupata taarifa umejipenyeza kwenye jeshi la Tanzania niliona nisikusumbue , isitoshe mpango wangu ulikuwa ni kuishi maisha ya chini chini” “Bosi hata usiwe na wasiwasi naelewa..”Aliongea huku akimwangalia Hamza kwa namna ya kumchunguza..
“Lakini bosi kwanini naona kama umebadilika sana , mbinu uliotumia kupasua vioo haifanani kabisa na ile niliokuzoea nayo?”Aliongea na kauli ile ilimfanya Hamza kucheka.
“Ndio sijatumia kabisa mbinu ya nishati za mbingu na ardhi maana nishaachana nazo?”
“Kama ni hivyo umetumia mbinu gani sasa?”Aliuliza huku akiwa anashangaa , ukweli ni kwamba hakujua kabisa ni kitu gani kinaendelea kuhusu Hamza.
“Usiwaze sana nimeachana na mbinu zote zilizozoeleka sasa hivi nipo kwenye kitu kingine kabisa”
“Boss kila siku unaonyesha wewe sio mtu wa kawaida , yaani umepata mbinu mpya na umeweza kujifunza ndani ya muda mfupi tu na sasa unaonekana kama mtu mwingine , yaani
unatufanya sisi binadamu wa kawaida tukose kabisa hata tumaini”
“Hehe.. unawaza nini sasa, kama tungefanana unadhani ningekuwa bosi wenu wewe mshenzi, huna haja ya kuwaza sana labda kama unataka kunipindua”
“Hamna bosi bado najichukulia nipo chini ya himaya yako mpaka sasa. halafu sio kama nina cheo kikubwa tokea nirudi kuliko kule”
“Huko nako ndio kujihusha , ndani ya miaka saba uliorudi nchini umeweza kuingia ndani ya kitengo cha Malibu na baadae kuwa mshauri wa vitengo vyote vya usalama na ulinzi na kupanda cheo mpaka kuwa jenerali , sio kazi ndogo kulingana na umri wako”
“Mafanikio yangu ni kama kichekesho nikijaribu kulinganisha na yako , isitoshe kwa kujilinganisha na wenzangu niliowaacha sidhani napaswa kusema nina mafanikio ya juu”
Hamza aliona alichoongea kinaleta maana , isitoshe kwa kipindi kirefu walichokuwa chini yake, alikuwa kama kikwazo kwa mafanikio yao , lakini wengi baada ya kuwaachia na kurudi kwenye mataifa yao waliweza kupata mafanikio makubwa ndani ya muda mfupi.
Walijikuta wakiongea kwa muda mrefu kidogo mpaka muda ambao Afande Himidu alikumbuka swala la Ankh.
“Bosi vipi kuhusu hili swala la Ankh , kwannini watu wanakufualitia nalo sana au ulikuwa mtego wa Genesha?”
“Genesha aliiniingia kwenye majaribu ni kama ananiambia hata kama nimekufa huwezi kuishi kwa amani , unadhani ni nani kajua kuhusu hii siri kama sio yeye alieisambaza , mtu ananipa kitu halafu anawapa watu taarifa ili waanze kuniwinda , huyu alichotaka ni kuona sipati amani.
Hivi unajua ndio alinirudisha hapa Tanzania , baada ya kunitumia ujumbe wa kila aina kwamba anakaribia kufa na yupo hapa hivyo nionane nae kwa mara ya mwisho , lakini sikujua kama aliacha anuani kwenye maabara yake ili ijulikane nipo Tanzania.
“Nini! , kwahio unamaanisha Dokta Genesha alifia hapa nchini, maiti yake..”
“Nilimtupia baharini , aliniambia mwenyewe niifunge maiti yake na jiwe zito na kisha nimtupe”Aliongea Hamza huku akiwasha kwa mara nyingine sigara na kuvuta moshi kidogo.
“Kama ni hivyo bosi , vipi kuhusu hii Ankh , ni siri gani , maana kwa ninavojua kama nipo sahihi Ankh maana yake ni alama ya msalaba ambayo ilikuwa ikiwakilisha uhai ndani ya Misri ya kale , si ndio?”
“Upo sahihi Ankh ni ishara ambayo alitengeneza Nekhbet mungu wa Misri ya kale kama ishara ya zawadi ya uhai kwenda kwa Farao, sababu ya dokta Genesha kuipa siri hii Ankh ni kwasababu ni siri ambayo inahusianisha na uhai wa binadamu, ushawahi kusikia mtu yoyote anasema simulizi ya njiwa juu ya mti wa Uzima?”Aliongea Hamza. “Nakumbuka nilishawahi kusoma hiki kitu kwenye Deep web , nilichukulia kama uzushi lakini walisema kuna Dokta kagundua siri juu ya kwanini binadamu anakufa mapema?”
“Unadhani nimeanza kukuelezea juu ya Nekhbet
ili ulichukulie hili swala kama hadithi za kale?”Aliuliza Hamza.
“Kwahio Bro unasema Ankh ni kitu cha enzi ya Farao au unamaanisha nini?”
“Kama nilivyokwisha kusema Ankh kama Ankh ni ishara tu ambayo imetumika kuficha siri juu ya hatua za uhai wa binadamu ulivyo , chukulia ni kama maandiko ya enzi hizo yameonekana sasa hivi kwa ligha ngumu isioweza kutafsirika”
“Kwahio bosi kama ulichoshikilia ni kanuni , si inamaanisha umeshika siri ya dunia , sidhani ni makundi ya kihalifu tu ambayo yanaweza kupigania, hata nchi zitajiingiza katika vita za kupata hiki kitu”
“Enzi ya kale watu walikuwa tayari kusafiri kwa kuvuka bahari kwa ajili ya kutafuta namna ya kurefusha maisha lakini sasa hivi sio kutafuta bali sayansi imeendelea na wanasayansi wanakaa tu maabara kufanya tafiti za kutengeneza madawa , lakini mtu yoyote ukimwambia kama kuna uwezekano maisha yakarefushwa na dawa atakuona kichaa tu”Aliongea Hamza na kumfanya Himidu kutingisha kichwa kukubaliana nae.
“Kwahio bosi kama ulichoshikiria ni kanuni juu ya siri ya uhai wa binadamu , je imewezwa kufanyiwa utafiti?”
“Hapana , Genesha alijaribu kufanyia utafiti ili kuweza kuitafsiri lakini alishindwa , kulingana na maelezo yake ana uhakika kabisa ni kitu ambacho kinaweza kubadilisha mtazamo wa binadamu juu ya uhai , lakini kutokana na msongo wa mawazo juu ya mke wake yalimshida hivyo aliniachia kila kitu na kisha akajiua , nadhani unajua nisingeweza kumzuia kama alitaka kujiua mwenyewe”
Afande Himidu alijikuta akivuta pumzi ya ahueni ,ukweli kulingana na mtazamo wake anaomba isiwe kweli , aliona kama kweli binadamu atajua namna ya kurefusha maisha , basi atakuwa kiumbe hatari zaidi kuliko hata siraha za nyuklia.
“Mimi kwangu naona hizi ni kama stori tu na uwezekano huo haupo?”Aliongea Himidu.
Hamza licha ya kuamua kumwambia ila hakutaka kumpa ukweli wote , isitoshe kuna misheni ilikuwa ikiendelea kuhusu yeye chini chini
“Ukweli ni kwamba Ankh ni ni nadharia ambayo wanasayansi wanayo tayari”Aliongea Hamza.
“Kivipi?”
“Kwanza unajua namna mwili unavyofanya kazi , mfano tu chukulia seli ambazo zinazunguka utumbo zinajigawa kila baada ya siku tatu mpaka tano na kuweka nyingine , sio hivyo tu kila baada ya miezi miwili seli za kibofu cha mkojo zinajiondoa na kuwa zingine , seli za damu zenyewe zinabadilika kila baada ya miezi minne , maana yake ni kwamba asilimia tisini na nane ya seli zote zilizopo ndani ya mwili wetu zinaondolewa na hewa na chakula kwa mwaka , kwa ligha nyepesi ni kwamba kila mwaka mmoja ukipita mwili wako umebadilika vitu vingi sana, sasa kadri mwili unavyoendelea kwa kasi kuzalisha seli mpya na kuhamisha zile zilizokufa huo mchakato unazuia mwili kuzeeka , , hivyo kama mchakato huu ni endelevu bila kupungua nyakati zote basi binadamu asingekufa mapema, ukichana na swala la kuugua na kupata ajali”
“Kama ni hivyo sasa kwanini sisi binadamu bado tunaendelea kuzeeka?”Aliuliza Afande.
“Kwasababu inafikia hatua ule mchakato wa seli kugawanyika ndani ya mwili na kutengeneza mpya hupungua kabisa , huu mchakato wote unadhibitiwa na DNA, Chukulia urefu wa uhai wako ni kama kamba ya kiatu, kadri unayotoka mwanzo wa kamba kueleleka mwisho wa kamba ndio namna unavyopunguza siku za uhai wako kutokana na seli za mwili kutojigawa na kutengeneza mpya , ukifika mwishoni mwa kamba unakutana na kile kichopoo ambacho kimeifunga kamba kuonyesha ndio mwisho, sasa pale ndio mwisho wa seli za mwili kujitengeneza upya , ukizungumzia kisayansi sasa DNA ina muundo kama wa kamba kwani mwishoni mwa urefu wake kumefungwa kitu kama kichopoo ambacho kisayansi kinaitwa Telomere.
Sasa chukulia kitendo cha kutaka kuongeza urefu wa kamba ndio kuongeza urefu wa maisha ya binadamu , utakachofanya ni kuondoa kile Kichopoo na kutafuta kamba inayofanana kwa asilimia mia moja na ulokuwa nayo kisha kutafuta namna ya kuunganisha ile kamba bila kubadili muundo wake na mwisho wa siku utafanikiwa kuiongezea urefu, ukichukulia huo mfano katika muundo wa DNA utakuwa umeongeza urefu wa maisha yako, hiki ndio kitu ambacho Genesha anaamini kipo katika siri ya Ankh”Aliongea Hamza.
Ijapokuwa hakuwa mwanabailojia lakini kwa kiasi kidogo alihisi kuelewa alichokuwa akitaka kumaanisha juu ya itu kinachoitwa Ankh.
“Inaonekana nadharia yake inaleta maana kwa kiasi flani , lakini kwasababu haikukamilika na kanunni imeshindikana kutafsirika kutokana na lugha yake si inamaanisha ni kitu ambacho hakitowezekana, kwanini akaamua kukupatia wewe hii siri ya Ankh?”
“Kwasababu anaamini kazi kubwa amekwisha ifanya , kwa maelezo yake anaamini kuna elementi moja ambayo haijagundulika bado na inaweza isigundulike kama tu kutakosekana tafsiri ya Kanuni ya Ankh , elementi hii ameitaja kama Elementi ya Nuru na kama ikipatikana basi kila kitu kitabadilika”
“Kwahio bosi Dokta Genesha anaamini fumbo la
hii elementi litapatikana katika tafsiri ya kanuni hio ya Ankh?”
“Uwezekano huo upo ila sina uhakika , kuna uwezekano hii elementi isiwepo kabisa hapa duniani au hata angani katika sayari nyingine”
Ilikuwa ni siri nzito sana juu ya Ankh aliopata kuisikia Afande Himidu ,ijapokuwa aliona Hamza hakuwa ameielezea vizuri kueleweka lakini aliona pengine kuna sababu ya Dokta Genesha kumpatia Hamza, hata hivyo alijiuliza kwanini maana Hamza sio mwanasayansi.
“Bosi hiki kitu ni kama kiazi cha moto ni kheri ubakie nacho tu , sitouliza tena kuhusu hili , kuna kila sabababu ya Dokta Ganesha kutotaka tafiti zake zipotee , lakini hata hivyo swala hili likijulikana kwa watu wachache ni bora zaidi”
“Ndio maana nilitaka kuongea na wewe , ili uweze kutuliza shauku wanayoanza kuipata wanajeshi wenzio , siku zote watu wakinifuata niliishia kuwaambia simulizi ya njiwa juu ya mti wa uzima ni uzushi tu, nafanya hayo kwasababu nataka watu wasahau, vyovyote vile hata kama ikitokea kanuni yote nimeijua nitaenda nayo kaburini , sioni kama kuna faida ya binadamu kuishi muda mrefu, hivyo hakikisha uchunguzi wowote unaendelea kuhusu mimi uachwe mara moja , sio salama watu wengi kuanza kuulizia kuhusu Ankh , wakikusumbua wewe waonyeshee dole”Aliongea Hamza na kufanya Afande Himidu kucheka.
“Bosi usiwe na wasiwasi , hii ni siri yagu na wewe kwanzia sasa , hata taarifa azitake Mfalme Nyoka” “Haha.. halafu huyu Mfalme Nyoka sijamuona kwa muda mrefu , unadhani atakuwa amenipita ki uwezo kwasasa?”
“Kama ni kipindi cha mwanzo ningeweza kusema unamuweza , lakini sasa hivi naona umeua nguvu zako zote za nishati , hivyo ni ngumu kutabiri chochote”
******
Waliongea mambo mengi mno mpaka juu ya Hamza kuoa, na Afande Himidu alitaka kujua imekuwaje kuwaje Hamza akaoa lakini Hamza alimwambia ni stori ndefu.
Alimwambia kama ni stori ndefu basi amtambulishe kwa shemeji, Hamza aliona sio mbaya kumtambulisha kwa Regina , hivyo alimwambia wakitoka hapo watafute sehemu kwa ajili ya chakula cha usiku na ampigie simu Regina kufika.
Afande Himidu alitoa maagizo kwa makamanda waachane na uchunguzi wote unaohusiana na Hamza kwanzia dakika hio na wiki inayofuatia atafika makao makuu kutoa maelekezo zaidi.
Kwasababu maneno yake ni sheria wote walikubali na kisha waliondoka huku bado wakiwa na maswali mengi , kati yao ambae hakuwa ameridhika kwa kiasi kikubwa alikuwa ni Afande Mdudu.
Baada ya Hamza kuingia kwenye V8 ya Afande Himidu ili kutafuta sehemu kwa ajili ya kupata chakua cha usiku , Hamza alitumia nafasi hio kumtafuta Regina na kumuuliza kama yupo free wakapate Dinner lakini Regina alisema yuko bize na kazi hivyo Hamza hakujishughulisha nae zaidi.
Japo Himidu alitaka kujua Hamza kashikika kwa nani lakini mara baada ya Hamza kumwambia haiwezekani kwa siku hio kukutana na shemaji yake aliamua kuridhika . Hamza hakumwambia kama ni Regina mmiliki wa makampuni ya Dosam , alitaka kuweka cheo chake pembeni na kutambulisha Regina kama Regina.
Hamza kwasababu alikataliwa na Regina kutoka wote Dinner aliona haina haja ya kwenda mjini kwa ajili ya chakula bali walichukua barabara ya kuelekea Kijichi kwa Dina.
Himidu alishangaa kuona Hamza alikuwa na mahusiano na Dina , alikuwa akimjua sana Dina kutokana na faili nyeti la mtandao wa Chatu alikuwa amekwisha kulisoma.
Kwa Hamza ilikuwa kama sherehe ya kukutana na rafiki yake na kwasababu ilikuwa wikiend walijiachia mgahawani kwa Dina na baadae wakabadilisha kijiwe na kwenda mjini zaidi.
Himidu aliamua kutumia pesa zake kuhakikisha Hamza anayafurahia maisha na Hamza hakuona shida.
Hamza upande wake hakusahau kumpigia simu
Prisila na kumpa taarufa alishatoka , taarifa ambayo ilikuwa nuri kwa Prisila.
Hamza hakufanikiwa kurudi nyumbani kabisa siku hio na kuishia kulala nyumbani kwa Dina mpaka asubuhi na kulivyokucha aliendelea kukaa mpaka muda wa jioni ndio alivyoanza safari ya kurudi nyumbani.
Ilikuwa muda wa saa kumi na moja kama na nusu hivi ya jumapili ndio aliingia nyumbani na kitendo cha kuingia getini aliweza kuona gari ambayo sio ya Regina ikiwa katika maegesho ya muda mfupi.
Hamza palepale kwa kuichunguza tu hio gari aliikumbuka vizuri.
“Hii gari si ni ya Yulia hii, anafanya nini hapa nyumbani”Aliwaza Hamza huku hisia zikimwambia huyo mwanamke kamfuata mpaka hapo zikimvaa.
Comments