Hamza alijikuta akishikwa na soni , ijapokuwa haikuwa makusudi aliona pia sio sawa , aliuliza ili kupata majibu na hakujua angemkasirisha Regina kiasi hicho, aliona pengine uelewa wake juu ya wanawake una kasoro na anatakiwa kuanza kujifunza upya.
“Toka kwenye ofisi yangu sitaki kukuona!”Aliongea Regina kwa kufoka.
Hamza aliishia kushusha pumzi akikubali kushindwa maana hakutaka kumwagia moto mafuta , hivyo kimya kimya alitoka ndani ya ofisi ya Regina.
Regina mara baada ya kuona ni kweli Hamza kaondoka aijikuta akipandwa na hasira mara mbili zaidi na kuanza kumlaani ndani kwa ndani huku macho yakiwa mekundu, aliangalia viboksi vya matunda alivyoleta Hamza na kwa hasira alivichukua na kwenda kutupia kwenye Dustbin kama kwamba ndio anamtupa Hamza.
Upande wa Hamza alikuwa na mawazo , baada ya kutoka ndani ya ofisi ya Regina alikuwa akiipiga namba ya simu ya Eliza mfululizo lakini ilionekana mwanamke huyo amezima simu.
Muda huo alichotamani ni kwenda nyumbani kwake kumuangalia lakini alikumbuka ahadi yake na Yonesi muda ule kwa ajili ya kumuelekeza baadhi ya mafunzo hivyo hakutaka kuivunja na kuona aanzie huko na kisha ndio akamtafute Eliza.
Muda ambao alifika ndano ya floor ya kufanyia mazoezi Yonesi alikuwa amekwisha kufika na alikuwa akipasha mwili, alikuwa amevalia mavazi ya mazoezi tayari na ilionekana alikuwa akitegemea kujifunza kitu kipya kutoka kwa Hamza kwa hamu zote.
“Kapteni wewe ni mwanamke , kwanini upo siriasi sana na swala la mapigano?Aliuliza Hamza mara baada ya kuona namna ambavyo Yonesi alionekana kuwa siriasi.
“Kwani ni vibaya, unadhani mwanamke hana haki ya kujifunza vitu ambavyo anaweza kujifunza mwanaume?”Aliuliza na Hamza alitingisha kichwa kukubaliana nae , isitoshe aliuliza kumtania tu.
“Ngoja tuanze haraka ili tumalize, kuna sehemu nataka kwenda”Aliongea Hamza. “Kama una haraka kwanini tusifanye siku nyingine , mimi sio jiniasi naweza nisikumbuke kila kitu kwa maelekezo ya muda mfupi”Aliongea Yonesi huku akiwa siriasi.
“Utakumbuka maana nakwenda kukufundisha kitu chepesi sana , ndani ya saa tu utakumbuka kila kitu”Aliongea Hamza na kisha alianza kuonyesha ufundi wake.
Yonesi mara baada ya kuona miondoko kadhaa kutoka kwa Hamza alijikuta akishangaa zaidi huku akikunja sura
“Hamza ijapokuwa uwezo wangu wa kimapigano ni mdogo lakini huwezi kunitania na ulichonionyesha , hayo sio mafunzo bali ni kama kucheza mziki”
“Kapteni acha uharaka, wewe fanya kama nilivyokuelekeza na uone kitakachotokea”Aliongea Hamza.
Yonesi aliishia kuonyesha kutoridhika lakini alisogea kati na kuanza kujikakamaza kuigilizia kile ambacho ameonyesha Hamza.
“Mguu wako wa kushoto unatakiwa kuukunja zaidi kwenda nyuma na viganja vya mikono yako vigeuzie kuelekea juu na mguu wa kushoto upindishe kwenda mbele…”
Hamza alianza kuelekeza huku Yonesi akifuatisha hayo maelekezo na kadri alivyokuwa amekaa katika mtindo huo wa maelekezo uzito wa mwili wake ulianza kuongezeka kila dakika na alianza kuvuta pumzi kwa haraka
“Bado kuna kitu hukipati , mguu wako wa kushoto haujaunyoosha na wa kulia haujaupindisha kwa angle sahihi, ndio maana unaanza kukosa balansi ya mwili”
“Naupandisha kwa angle ngapi sasa?”
“Angalau zifike sitini”
“Angle sitini!!”Aliongea Yonesi akishanga kwa uona ni nyingi.
“Ngoja nikusaidie kukuweka sawa”Aliongea Hamza na licha ya Yonesi kuonyesha wasiwasi alimshika vizuri paja na mikono na taratibu akaanza kumnyoosha.
Licha ya kupokea malalamiko kutoka kwa Yonesi asiende mbali kwenye kumgusa maeneo nyeti lakini Hamza alijifanyisha kuwa siriasi zaidi na kutomzingatia lawama zake.
Baada ya dakika kadhaa za kuchukua mazoezi ya kubalansi mwili alijikuta akishangaa, maana mwanzoni alidharau lakini aligundua ni kuna kitu cha upekee katika mafunzo hayo alianza kukipata.
“Hii ni aina gani ya mafunzo?”
“Hii ni mbinu ambayo nimeitengeneza mwenyewe ili kurahisisha mazoezi ya balansi mwili , ukirudia kujikunja mara mia moja nitakufundisha hatua inayofuata”
“Mara mia!!”
Aliongea Yonesi kwa mshangao maana alikuwa amechoka kwa mzunguko huo mmoja tu na kuona mara mia itakuwa ni nyingi mno.
Kwasababu Hamza alikuwa na haraka alimwambia awe siriasi na alichomwelekea ili amfunidshe hatua nyingne , licha ya Yonesi kujihisi kuchoka aliishia kutingisha kichwa kukubali na Hamza aliondoka haraka haraka kwenda kumtafuta Eliza.
*****
Ni muda wa saa nane kama na nusu hivi alionekana Kanali Dastani akiingia ndani ya ofisi yake akitokea kwenye kikao ambacho kiliitishwa na Mkurugenzi mkuu wa kitengo.
Alionekana kuwa na uso uliosawijika, mtu ambae ni kama amepokea taarifa ya kitu ambacho hajaridhishwa nacho lakini hana jinsi.
Akiwa ana nyonga tai yake vizuri mlango wa ofisi yake uligongwa na aliruhusu anaegonga kuingia na mara baada ya kugeza macho kumwangalia alieingia alionyesha tabasamu hafifu.
“Vipi Afande Mdudu kuna tatizo?”Aliongea Kanali Dastani huku akimkazia macho.
“Afande nilidhani utahitaji mtu wa kuongea nae , kwenye kikao hukupata mtu wa kukuunga mkono mawazo yako , kitu ambacho sio kawaida”
“Kwahio umekuja kuniunga mkono baada ya kikao kuisha?”Aliuliza Afande Dastani huku akikunja sura.
Afande Mdudu aliishia kutoa tabasamu na kisha alisogea na kwenda kukaa kwenye sofa.
“Hoja uliotoa ilikuwa ina mashiko Kanali , lakini unajua fika sisi ni wanajeshi , ijapokuwa mawazo yetu yanahitajika kwenye vikao lakini ikitokea kitu kishaamuliwa kikao kinafanyika kutufahamisha kinachoendelea na sio kusikiliza hoja zetu”Aliongea.
“Kama unachoongea unamaanisha basi ulipaswa kuuvaa ujasiri na kuunga mkono hoja yangu”
“Hoja yako ilikuwa na mantiki lakini haimaanishi ilikuwa uhalisia , swala la kesi zote zinazohusiana na Hamza kufungwa halipo ndani ya kitengo chetu tu mpaka TISA pia”Aliongea na kumfanya Kanali macho yake kuchanua.
“Mpaka TISA!!”
“Nimesikia taarifa hizi tokea juzi,Hamza alikuwa kwenye rada za usalama wa taifa kwa muda mrefu sana, ukiangalia hii kesi kwa umakini haina vigezo vya kuwa chini ya kitengo chetu ndio maana nikasema imekosa uhalisia licha kwa jicho pana la kichunguzi ilikuwa na mantiki” “Kama uhalisia wa hii kesi umekosekana katika kitengo chetu pekee kwanini Mshauri mkuu aingilie mpaka kwenye idara nyeti ya intelijensia ya taifa, hata kama ni swala la uchaguzi haliwezi kufanywa na watu wote wa kitengo”
“Swala la uchaguzi kwasasa ni nyeti sana kwa usalama wa taifa kosa kidogo kunaweza kutokea machafuko , swala la Jongwe kufariki limefanya idara zote za usalama kuwa katika tahadhari”
“Hio haikuwa hoja yangu Mdudu , najua
Uchaguzi ni swala la juu kabisa kwa nchi lakini hili lipo chini ya kitengo cha TISA na idara nyingine za usalama, Malibu ni Kitengo cha jeshi kazi yetu sio kuangalia upande mmoja tu wa nguvu zizisokuwa za kawaida”
“Hoja yako nakubaliana nayo , lakini mpaka sasa zimebakia siku kumi na tano tu zoezi la kupiga kura lianze, Mshauri mkuu ni mtu ambae hawezi kufanya maamuzi juu ya kitu kinachohatarisha usalama wa nchi”Aliongea Afande Mdudu na Kanali alionekana kufikiria kwa dakika kadhaa na kutingisha kichwa kukubaliaa nae.
“Unaonekana kumchukia sana huyu Hamza, Norbert na ujanja wake alishindwa kumkamata ilikuwaje wewe mpaka Mshauri mkuu akaingilia?”Aliongea.
“Huwa likija swala linalomuhusu Yonesi nakuwa jasiri mno”
“Haha.. Afande Yonesi!, kwanini?”
“Dastani acha kunikejeli ilihali unajua kinachoendelea”Aliongea Mdudu huku akiongeza usiriasi na kumfanya Afande Dastani kutoa tabasamu lilojaa ukejeli.
“Wewe na Amosi mmeteswa sana na penzi la Yonesi , ulienda mbali mpaka kumtumia baba yako umuoe lakini ‘kiko wapi’ kitisho kidogo umeufyata”
“Usinilinganishe na Mzee, Amosi ni mtu mzima aliejaribu bahati yake kwa Yonesi , mimi ni kijana ambae sikuwa nikibahatisha ila nilipigania kile ninachokitaka, mwanajeshi mwenye busara ni yule asiemdharau adui yake , natafuta namna ya kumrudia”Aliongea na kumfanya Kanali kutoa cheko.
“Likija swala la Yonesi unakuwa siriasi sana , anyway niambie unachohitaji , nadhani hujaja kwenye ofisi yangu kupiga soga wakati ni muda wa kazi huu”Aliongea na kumfanya Afande Mdudu kukaa vizuri.
“Nataka kujiunga na ushirika Black
Trinity”Aliongea Mdudu kwa sauti ya chini na kumfanya Amnosi kushituka
“Unaongea nini Mdudu?”
“Acha hizo kanali najua wewe ni mwanachama na ili nijiunge lazima nipate mwaliko kutoka kwa mwanachama”Aliongea Mdudu na Ghafla tu ni kama Kanali Dastani amebadilika na kuwa kivuli kwani alipotea alipokuwa amesimama na kuja kusimama Mdudu alikuwa amekandamizwa kwa nguvu kwenye ukuta huku akiwa amekabwa shingo.
Kilikuwa ni kitendo cha maajabu mno na cha haraka sana alichokifanya Kanali Dastani lakini ajabu Mdudu licha ya kukabwa hakuonyesha hofu ya aina yoyote lakini upande wa Dastani hakuwa wa kawaida, ni kama amegeuka na kuwa kiumbe cha ajabu.
“Unajua unachokiongea!?”Alikoroma Dastani huku akimwangalia Mdudu wa macho ya kuogofya.
“Kanali huwezi kunifanya chochote , najua wewe na Tresha Noah mpo kwenye Uwili na kama nitapoteza maisha hapa picha zenu mkifanya mapenzi ya rafu zitasambaa mtandaoni , hebu fikiria kitakachotokea na kisha upunguze presha tuongee vizuri , siri yako ipo salama na mimi kama utanipatia mwaliko, ombi jepesi sana”Aliongea Mdudu huku akionyesha tabasamu la kejeli lililoambatana na macho kodo.
*****
Hamza aliweza kufika ndani ya Apartment anayoishi Eliza na baada ya kugonga kwa dakika kama moja hivi mlango ulifunguliwa na Eliza aliekuwa katika mavazi ya nyumbani.
“Hamza ni wewe , unafanya nini hapa?”
“Eliza nini kinaendelea , kwanini umezima simu na umeomba kwenda kufanya kazi nje ya nchi?”Aliongea Hamza akiruka hata salamu. Kwa jinsi ambavyo mwanamke huyo alivyoonekana , ilikuwa ni dhahiri kabisa kuna kilichokuwa kikiendelea, alionekana alikuwa na wasiwasi mno kiasi cha kumfanya uso wake kupauka.
“Eliza ni nani anagonga?”Sauti kutokea ndani ilisikika na Eliza aliishia kurudi nyuma akimpa nafasi Hamza ya kuingia ndani.
Muda huo sasa Hamza alipata kumuona mwanamke mtu mzima hivi ambae kwa haraka haraka ilionyesha umri umeenda.
“Mama shikamoo , naitwa Hamza mimi ni mpenzi wa Eliza”Aliongea Hamza bila aibu na kauli ile ilimfanya Eliza kukakamaa mwili na aibu juu kwani ilikuwa ni kama hakutegemea.
Haikuwa kwake tu hata kwa mama huyo alionyesha hali ya kushangaa maana ni kama hajawahi kukutana na tukio la mwanaume kujitambulisha kwa kujiamini na pili hakuwa akijua kama Eliza alikuwa na mpenzi.
“Mama Mkubwa hapana huyo sio ”
Hamza hakumpa hata muda wa kumaliza kuongea na alimsogelea yule mama.
“Mama Mkubwa kama nilivyojitambulisha, napaswa kujua nini kinaendelea ama mpenzi wake ili kumsaidia maana Eliza hataki kuniambia, nimemtafuta sana kwenye simu”
Kauli ile ilimfanya yule mama kumwangalia Eliza kwa sekunde kadhaa na ilionekana alikuwa na uzoefu wa kutosha kwani kuna kitu aliweza kukisoma tayari kutoka kwa Eliza.
Licha ya kwamba alikuwa na mshangao lakini kwa wakati mmoja pia alionyesha kuwa na tumaini.
“Baba!, wewe kweli ni mchumba wa Eliza?”Aliuliza yule mama.
“Ni kweli kabisa Mama Mkubwa , Eliza ni mpenzi wangu na nampenda sana, nipo tayari kwa lolote kwa ajili yake”Aliongea Hamza ilikuwa ni kama amepata hadhira ya watu kwa ajili ya kuelezea hisia zake.
“Eliza ni kweli?!”Aliuliza Mama Mkubwa kwa shauku huku akimkazia macho Eliza lakini mrembo huyo hakujibu zaidi ya kuinamisha kichwa chini , ukweli ni kwamba alikuwa na hisia ambazo haikuwa rahisi kuzielezea alikuwa akimpenda Hamza lakini tokea asikie Hamza ni mume wa bosi wake hakujua tena Hamza ni mpenzi wake au ni nani kwake.
Wahenga wanasema ukimya ni jibbu pia , hivyo kwa Mama Mkubwa yake Eliza aliweza kujua watakuwa kweli ni wapenzi ila kuna kinachoendelea kati yao.
“Baba nitakuelezea kilichotokea kama Eliza anagoma kukuambia unaweza kuwa na msaada”Aliongea yule Mama huku akimuona Hamza kama mtu ambae ni kweli anao uwezo wa kumsaidia kutokana na mwonekano wake wa kitajiri na kujiamini.
“Mama Mkubwa hapana..”Eliza alitaka kumzuia lakini Hamza alimkatisha.
“Mama Mkubwa naomba uniambie, nadhani unamjua Eliza ni mwanamke wa aina gani , asiponiambia nitashikwa na mawazo mengi na sitojua namna ya kusaidia”Aliongea Hamza na Mama Mkubwa alivuta pumzi na kisha alikaa chini huku akionyesha kuwa katika hali ya mawazo.
“Mama Mkubwa ngoja nimwambie”Aliongea Eliza na kuingilia mara moja , aliona sio vyema kama Mama Mkubwa akichukua nafasi yake.
Hamza maara baada ya kumsikia Eliza akiongea hivyo alijikuta akivuta pumzi ya ahueni sasa maana alijua kama hatoambiwa kinachoendelea ukichaa wa hasira ungemshika.
“Baba amekamatwa..”Aliongea kwa sauti hafifu. “Baba yako mzazi amekamatwa?”Aliuliza Hamza kana kwamba hajasikia vizuri na Eliza alitingisha kichwa kukubali.
“Imekuwaje baba yako akakamatwa na waliomkamata ni wakina nani?”
“Unakumbuka nilikuambia baba yangu ni mstaafu na yupo kijini?”
“Ndio nakumbuka?”
“Basi baba baada ya kurudi nyumbani sikuwa nikijua kinachoendelea , ubize niliokuwa nao juu ya kumuuguza mama umenifanya nisifuatiilie yanayoendelea kijijini , Baba alivyorudi alishawishiwa na kaka yangu kujiingiza katika biashara ya uchimbaji madini huko Mkoani
Njombe…”
Eliza aliendelea kumsimulia Hamza kilichotokea na ilionekana baba yake alitapeliwa.
Eliza anasema kuna wataalamu wa utafiti wa maswala ya madini walifika mkoani Njombe na kufanya utafiti wa uwepo wa Dhahabu ndani ya maeneo ya msituni ya mkoa huo , moja ya watu wa ndani ya mkoa walioshiriki katika utafiti huo ni kaka yake Eliza anaefahamika kwa jina la Hebert Mlowe, baada ya watalaamu wale kumaliza utafiti walitoa majibu yao kwa vijana wa mkoa huo ambao waliambatana nao ikiwemo Hebert na walisema eneo x katika shamba la Mzee Mlowe kuna kiasi kikubwa cha madini ya dhahabu ambacho kipo ardhini, majibu hayo ya kitaalamu yalimfanya kijana Hebert kupatwa na tamaa kubwa sana huku tamaa yake ikimpoza na kuamini kila kitu ambacho wataalamu walisema.
Baada ya watalamu wale kuondoka wakiahidi kurudi kwa ajili ya utaratibu wa kuanza uchimbaji , Hebert hakutaka fursa ya kuwa tajiri impite hivi hivi hivyo aliwajumuisha na wale vijana wenzake walioshiriki na wataalamu hao kisha walimpelekea taarifa mzee Mlowe juu ya uwepo wa madini ndani ya shamba lao la miti ya biashara , Hebert bila ya kuwa na uhakika alimhakikishia baba yake eneo hilo la shamba lao limebeba mali nzito itakayobadilisha maisha yao kabisa na Mzee Mlowe alijikuta akishawishika na kutumia kiinua mgongo chake chote kuwekeza katika uchimbaji wa Dhahabu, kiasi cha hela ambacho kilikuwa ni kidogo kutokana na kumaliza karibia ya robo tatu ya hela yote..
Baada ya kuchimba kwa muda wa mwezi mmoja hawakuambulia chochote na kiasi cha pesa walichowekeza kiliishia kwenye mchakato na kununua vifaa, yalikuwa matokeo mabaya kwao lakini Mzee Mlowe hakukata tamaa baada ya Hebert kumhakikishia wataalamu walisema madini yapo chini sana hivyo wasikate tamaa na kuendelea kuchimba..
“Nini kilitokea baada ya hapo?”Aliuliza Hamza huku akijua nini ambacho kinaenda kutokea.
“Walichukua mkopo kwa ajili ya kuendelea na aliewakopesha aliwapa kiasi mara kumi ya kile walichoomba”
“Na ndio kiasi gani?”Aliuliza Hamza na kauli ile ilimfanya hata Mama Mkubwa kujiinamia kichwa chini kuna namna Hamza aliona pia huyo mama alihusika.
“Milioni mia tatu, baada ya kupewa kiasi kikubwa hivyo cha pesa ukichaa wa hela uliwavaa, mwanzoni wakati baba amewekeza kaka na marafiki zake walihusika kwa kuchimba lakini mara baada ya kupewa mkopo hawakuchimba tena na waliweka vibarua , lakini hela yote hawakuitumia kama ilivyohitajika kwani walianza kufanya starehe na kucheza kamari”Alingea Eliza huku akiona hata aibu ya kumwangalia Hamza machoni.
“Kwanza inaoneana kilichotokea ulikuwa mpango wa hao watalaamu na pengine hawana utalaamu wowote na ndugu zako walikuwa wakiingizwa kwenye mtego , pia kitendo cha wakopeshaji kuwakopesha zaidi ya mara kumi ya kiasi cha hela walichotaka inaleta mushikeli ya matukio yote kuwa na muunganiko”Aliongea
Hamza na Eliza alitingisha kichwa kukubali.
“Sikujua kinachoendelea, mbaya zaidi baba ndio aliehusika katika taratibu zote za kuomba mkopo”
“Waliahidi nini kama dhamana ya mkopo?” “Asilimia hamsini ya faida itakayopatikana kwenye kuuza madini watakayopata”Aliongea Eliza na kauli ile ilimfanya Hamza kukunja ndita huku akipatwa na msisimko wa kujua kwa undani ni mpango gani unaendelea.
“Kwahio waliomkopesha baba yako baada ya kushindwa kulipa mkopo ndio hao waliokuja
kumkamata?”
“Bado sijajua , waliomkamata baba walijitambulisha kama polisi, lakini baada ya ndugu kwenda kituo cha polisi hakukuwa na taarifa zao jambo ambalo lilishangaza , baada ya kusumbua sana polisi wamesema Baba amesafirishwa kuja huku Dar es salaam , lakini mpaka sasa tumeshindwa kupata kujua baba ameshikiliwa gereza lipi na polisi hawataki kutoa ushirikiano..”Eliza alikuwa akitia huruma kweli.
Hata Hamza alimuonea huruma , isitoshe ilikuwa ni kama kila matatizo ya familia Eliza ndio aliekuwa akihusishwa kwa kiasi kikubwa kuyabeba, kwanzia swala la mama yake mpaka swala hilo la familia yake.
“Kaka yako yeye yupo wapi?”
“Herbert ametoroka na milionni therathini zilizobakia na mpaka sasa hajulikani alipo”. “Poleni sana, hili swala nitalifanyia kazi ndani ya muda mrefu nitapata majibu , niambie ni watu gani ambao wametoa mkopo”
“Hamza unataka kufanya nini?”Aliuliza Eliza kwa wasiwasi.
“Hili swala mkiliendea kisheria hamtopata majibu kwa uharaka , hapa sio swala la mkopo kuna kitu kingine kinachotafutwa”
“Hamza sitaki kukuingiza kwenye matatizo yangu ya kifamilia, nimeenda benki kwa ajili ya kuomba mkopo kwa ajili ya kulipa mkopo huo na baada ya hapo nimeomba nafasi ya kwenda kufanyia kazi nje ya nchi, kule malipo ni maradufu zaidi ya hapa ,ndani ya miaka mitatu nitaweza kurudisha kiasi chote”Aliongea Eliza huku akionyesha hali ya usiriasi kwenye macho yake.
Licha ya kwamba Hamza alikuwa na hasira ya Eliza kutomhusisha katika matatizo yake lakini vilevie alizidi kumpenda , alikuwani mwanamke ambae hakosi njjia ya kutokea , lakini alijua kama akiruhusu swala hilo litokee basi mrembo huyo ataishia kupoteza ujana wake tu kwenye ulipaji wa madeni.
“Eliza unajua kabisa huu ni mtego umewekewa kwanini unataka kulipa kirahisi , ni kweli ndugu zako waliingizwa kwenye mtego lakini hujiulizi ni
kwanini iwe ni kwa familia yako tu?”Aliongea Hamza
“Najua lakini bado nashindwa kuelewa kwanini haya yanatokea?”
“Hatua ya kwanza ya kutatua tatizo ni kujua kiini chake ni nini , unaweza ukaenda nje ya nchi , unadhani kila kitu kitaishia hapo?”Aliongea Hamza huku akipandisha sauti na Eliza aliishia kuinamisha kichwa chini.
Ukweli Hamza alikuwa kuna kitu ambacho Eliza hamwambii na alijua kuna uwezekano wa hicho kitu ndio kilichoifikisha familia yake katika hatua hio ya kutengenezewa mtego.
“Eliza niambie kila kitu ili nipate kukusaidia , kukubali matatizo bila ya kujua chanzo sio njia sahihi ya kuyatatua”Aliongea Hamza huku akimwangalia Eliza.
Kitendo cha kuangaliana kwa sekunde kadhaa na Hamza machozi yalianza kumtoka mfululizo na haikuchukua hata sekunde alianza kulia kilio cha kwikwi jambo ambalo si tu kumshangaza Hamza lakini pia lilimshangaza na Mama Mkubwa wake.
Hamza alijikuta akihisi hisia mchanganyiko kwenye moyo wake , ilionyesha Eliza alikuwa akipitia wakati mgumu mno na kujitahidi sana kuficha kile ambacho anapitia na hali hio ilimfanya Hamza kuona licha ya kwamba walikuwa na muda mchache tokea wajuane ila hakuwajibika vya kutosha.
Aliishia kumkumbatia pekee na kumfuta machozi tukio ambalo lilionyesha kumgusa sana Mama Mkubwa.
“Eliza nyamaza na niambie nini kimekutokea”Aliongea Hamza kwa kumbembeleza lakini ilikuwa ni kama anaongezea mafuta kwenye moto.
Dakika chache baadae Eliza aliweza kutulia sasa na kuanza maongezi.
“Unakumbuka siku ambayo ulinikuta kwa mara ya kwanza nikidhalilishwa na watu ambao niliwakopa??”Aliuliza na Hamza alitingisha kichwa kukumbuka.
“Wale uliowakuta hawakuwa wahusika wakuu?”
“Unamaanisha kuna muhusika mwingine?”Aliuliza Hamza akiwa na utulivu na Eliza alitingisha kichwa kukubali.
“Kuna mwanaume nilikuja kukutana nae kipindi mama amelazwa hospitali ya taifa , hii ilikuwa ni siku kadhaa baada ya kupata mkopo kwa ajili ya kulipia matibabu ya mama , nakumbuka kwa mara ya kwanza nilikutan nae hoteli ya Serena akiwa pamoja na aliewahi kuwa Dokta wa hospitali ya taifa ambae alijaribu kunitaka kingono ndio mama afanyiwe matibabu , bahati nzuri nilikutana na Dokta mmoja ambae sasa hivi ni mkufunzi wa chuo cha Uchumi , ndio alienisaidia kufichua ushenzi ambao alikuwa akifanya yule Mkurugenzi kwani kesi zake zilikuwa nyingi kiasi cha serikali kumuwekea mtego”
“Ilikuwaje ukakutana nae Serena?”Aliuliza Hamza.
“Wakati mama anapatiwa matibabu huyu dokta aliniita ofisini kwake na kuanza porojo zake za kunitaka kimapenzi, nilikuwa nimechanganyikiwa kipindi kile na sikumpa jibu , siku kadhaa mbele aliniita hotelini na ndio nilikutana nae”
“Hili ni tukio la pili anaombwa rushwa ya ngono na daktari?”Aliongea Hamza ndani kwa ndani huku akikumbuka tukio lile la Kigamboni.
“Kwahio unaamini huyo mwanaume ambae ulikutana nae huko hotelini ndio chanzo?” “Ndio chanzo cha kile ambacho kilikuwa kikiendelea kwa Amosi na genge lake , Amosi ndio alienikopesha hela kwa ajili ya matibabu , kipindi kile nilikuwa desparate kumtibia mama na sikuwa na kazi ya kueleweka mpaka nilipokutana na Regina, baada ya kupata mkopo baadae ndio nilikuja kukutana na huyo mwanaume ambae alichokuwa akitaka kwangu ni kilekile , nilale nae kwa siku tano kisha afute mkopo wangu , nilimkatalia na matokeo yake yalikuwa ule udhalilishaji ulionikuta nao na nilishangaa hawakuja tena kunidai na kuomba msamaha kabisa”Aliongea Eliza.
“Wale niliwapa onyo mimi ndio maana hawakukusumbua tena , kama ulivyosema ni kweli basi huyu mtu bado hakuwahi kukata tamaa juu yako , lakini inafikirisha sana , kama yeye kweli ndio mhusika na ameenda mbali mpaka kumwingiza baba yako kwenye mtego basi kuna cha ziada”Aliongea Hamza.
“Wewe ndio uliewazuia kipindi kile? , kama ni hivyo kwanini unaamini kuna kitu cha ziada?”Aliongea Eliza huku akionyesha mshangao na macho ya shukrani kwa Hamza , hakuwahi kujua kama Amosi kutokumsumbua Hamza ndio alihusika lakini alipatwa na woga baada ya kuona pengine mzee yule sio ngono pekee anayotaka kutoka kwake.
Hamza kuna kitu ambacho alikuwa akifikiria lakini hakuwa na uhakika kama ni kweli na alipaswa kulitafutia hilo swala ufumbuzi, aliwaza hilo kutokana na uzoefu wake.
Hamza muda huo alikuwa ameweka umakini kwa Eliza na alisahau hata kuna mama aliekuwa pembeni na baada ya kugeuka aligundua Mama Mkubwa alikuwa ameloa machozi , ilionekana alikuwa ameguswa sana na maswaibu ambayo Eliza alikuwa akipitia.
“Bado sijajua ila naamini nitalifanyia ufumbuzi hili swala na lazima nitapata kitu”Aliongea Hamza lakini kwa Eliza licha ya kuwa na shukrani lakini bado alikuwa na wasiwasi na kile ambacho Hamza anakwenda kufanya , maana kwa alichokuwa akijua mtu huyo hakuwa mdogo , alikuwa tajiri ambae vigogo wengi wa kiserikali walikuwa wakimkingia kifua.
“Eliza pole sana mwanangu , hakuna aliekuwa akijua unapitia wakati mgumu kiasi hicho?”Aliongea Mama Mkubwa yake Eliza na kumfanya Eliza kutingisha kichwa.
Ukweli ni kwamba katika familia nzima ya Eliza Mama Mkubwa wake Merieta ndio ambae alikuwa akimjali mno na ndio yeye aliefunga safari kutoka kijijini kuja mpaka Dar kwa ajili ya Eliza , shida tu ni kwamba katika ukoo wote yeye ndio aliekuwa na hali ya chini ya kiuchumi , utajiri wake ulikuwa ni ukarimu na busara pekee lakini mbele ya ndugu zake hakuonekana wa maana.
Hata baba yake Eliza hakujali kabisa kuhusu mke wake wa kwanza kuumwa kwake , baada ya kupata kiinua mgongo alihamia mkoani kwa mke mdogo ambae ndio mama yake Hebert hivyo kumfanya Eliza kuhangaika mwenyewe kumtibia mama yake, uzuri wake tu ilikuwa ni kwamba licha ya kumtelekeza Eliza hawakujihusisha nae kwenye mambo yoyote na hata hela hawakumuomba baada ya kuajiriwa.
Licha ya yote Eliza alikuwa akiijali familia yake sana na alikuwa ndio kama kichwa cha familia na asingemuacha baba yake kuchukuliwa na watu bila kufanya chochote.
“Mama Mkubwa nadhani mpaka hapa nimepata pakuanzia , Eliza umesema ni watu gani wamemkopesha baba yako, kama ni shirika nitajie jina lake?”Aliongea Hamza na muda ule Eliza alimwangalia Mama Mkubwa akionekana ndio mwenye kujua jina hilo .
“Kwa ninavyojua sio kampuni wala benki , ni shirika la kukopesha watu kwa riba nafuu , wanajiita Utatu?”
“Utatu!!”Aliongea Hamza kwa kushangaa.
“Unawajua?”
“Sina uhakika lakini kuna umoja wa siri wa giza wenye washirika waliosambaa dunia nzima , unafahamika kwa jina la Black Trinity, huwezi kuelewa ila nadhani nishaanza kupata picha ya kile kinachoendelea”Aliongea Hamza.
“Nini kinaendelea Hamza mbona
unanitisha?”Aliuliza Eliza huku wasiwasi ukizidi kumvaa.
“Huna haja ya kuogopa kwanzia sasa , ili mradi nishaanza kupata picha ya kile kinachoendelea , hili ni swala ambalo napaswa kulishughulikia”Aliongea Hamza huku akipatwa na hisia mchanganyiko, alijua kama kweli ni Black Trinity ndio wanaojiita Utatu basi Eliza alikuwa kwenye hatari kubwa mno.
Hamza aliwahakikishia hakuna kitakachowapata na atamtafuta baba yake na kumrudisha salama na kisha aliaga na kuondoka.
Hamza mara baada ya kuingia kwenye gari alitoa simu yake haraka na kupiga simu kwenda kwa Dina na baada ya salamu alienda moja wa moja kwenye lengo la simu hio.
“Dina kuna kitu nataka unisaidie , Eliza yupo kwenye matatizo, unakumbuka ile siku uliniambia Eliza alikuwa shabaha inayolengwa kwa ajili ya kuingizwa ndani ya kampuni ya Dosam?”Aliuliza Hamza.
“Ndio, nini kimemtokea Eliza?”Aliuliza Dina na Hamza alimwelezea kwa ufupi kinachoendelea.
“Nataka uniambie nani alikuwa nyuma ya mkopo wa Eliza , sitaki kusikia ni yule Amosi najua kuna wa nyuma yake”Aliongea Hamza.
“Ni kweli kuna waliopo nyuma ya Amosi”
“Waliopo!?”
“Ndio ni swala nyeti sana ambao kwa kipindi kirefu nimejitahidi kukaa nje na kutokufukunyua , ila uzuri ni kwamba najua mmoja wapo na nadhani ndio huyo”Aliongea Dina na Hamza tabasamu lilimvaa palepale.
“Ni nani?”
“Acha haraka , ulivyoanza kuzungumzia hili swala umenifanya mwili wangu kusisimka , njia rahisi ya kumjua ni kupitia tukio la leo”Aliongea Dina.
“Tukio la leo!! , unamaanisha ninI?”
Comments