Reader Settings

Saa tatu asubuhi, anga la Dar es Salaam lilikuwa limetanda na mawingu meupe ya uongo na kweli, yale mawingu ambayo huahidi mvua lakini huishia kuwa ukimya wa joto linalounguza. Zara Mwinyi alikuwa mezani kwake, akinywa chai ya tangawizi bila sukari. Kioo kidogo kilichokuwa pembeni ya dirisha kilimwonyesha uso wake: bila make-up, bila hisia. Tu alama ndogo ya kuchoka chini ya macho yake.

Simu yake ya mezani ililia kwa mpigo wa haraka, sauti ile ile ikiashiria kuna taarifa ya barua pepe kutoka kwa ofisi ya chuo. Alipuuza. Kompyuta yake haikuwa imewasha toka jana usiku. Alikuwa bize sana usiku kucha akisahihisha mitihani mpaka saa tisa alfajiri.

Akiwa anajiandaa kunyanyuka, televisheni ya ukutani ilibadilika ghafla kutoka taarifa za biashara hadi habari za kimataifa.

Habari za hivi punde kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Waandishi watatu wa habari, akiwemo mwandishi mashuhuri wa vita Imran Said, wanaripotiwa kupotea baada ya shambulizi la ghafla katika mji wa Goma, mashariki mwa taifa hilo.”

Kikombe alichokuwa ameshikilia Profesa Zara kiligonga sahani pembeni yake, lakini hakikuvunjika. Zara hakuonyesha dalili yeyote ya kushtuka. Alinyanyua rimoti polepole na kuongeza sauti ya TV.

Taarifa kutoka kwa shirika la habari la Reuters zinaeleza kuwa gari lililowabeba wanahabari hao lilipotea mawasiliano dakika chache baada ya kutoka kambini. Vikosi vya Umoja wa Mataifa vimeanzisha msako, lakini hadi sasa hakuna taarifa rasmi ya walipo.”

Zara alipumua kwa ndani. Sio kwa mshangao. Sio kwa huzuni. Bali kwa aina fulani ya uthibitisho. Kama mtu aliyekuwa akisubiri jambo litokee. Alinyanyuka, akarudi chumbani. Funguo za droo ya chini ya kabati la vitabu zilikuwa pale pale alipoziweka wiki iliyopita. Alizifungua. Bahasha ya kahawia iliyokuwa ndani yake ilikuwa imeandikwa kwa mwandiko wa Imran:

“Do not open until things have changed”

Ikimaanisha Usifungue hadi mambo yatakapobadilika.

Lakini bado, hakuiangalia kwa undani. Alirudisha bahasha ile, akafunga droo, na akavaa blauzi nyeupe. Blauzi lile lile aliyolivaa siku walipopigwa picha ya harusi yao miaka kumi na tano iliyopita.

********

Wakati huo huo, ofisi ya Mkuu wa Idara ya Linguistic, Profesa Mwinjuma, ilijaa msongo wa hofu.

“Imran? Yule mume wa Zara?” aliuliza kwa mshangao.
“Ndio, ndio! Alienda tena Congo wiki iliyopita, kama kawaida yake ya hatari,” msaidizi wa idara alijibu.

Wanafunzi waliokuwa wamesimama mlangoni walinyamaza walipomuona Prof. Zara akipita. Alitembea kama kawaida miguu ya upole, kisogo kimeinuka, macho mbele. Hakusema chochote. Hakuitika salamu yoyote. Hakukuwa na machozi. Hakukuwa na wasiwasi.

 

Jioni yake, nyumba yao ya Mikocheni ilikuwa kimya kuliko kawaida. Mapazia yalikuwa yamefungwa, taa za nje zimewashwa nusu. Ndani, dada yake Neema alikuja akiwa na kikapu cha matunda, uso wake umejaa simanzi.

“Zara, tafadhali... niambie unajisikiaje,” alisema kwa sauti ya pole.

Zara aliketi kwenye sofa la bluu, mikono yake ikiwa imefungwa kifuani. Aliangalia picha ya harusi iliyoning’inia ukutani, Imran akiwa amevaa koti jeupe, akimuangalia kwa macho ya upole na upendo ambao kwa muda huo aliona ni bandia.

“Hii sio mara ya kwanza anapotea kwenye habari,” alisema kwa sauti ya kawaida.
“Lakini mara hii wanasema ni serious. Wamesema anaweza kuwa amekufa.” Neema alikazia.
“Na bado hawajapata mwili wake,” Zara alijibu. “Kama hawajapata mwili, basi bado kuna nafasi ya kuamini bado yuko hai.”

Neema alishindwa kujizuia. Alimkumbatia dada yake, lakini Zara hakujibu kumbatio hilo. Alibaki tu, macho yakiwa mbali.

********

Usiku wa saa saba, baada ya nyumba kutulia, Zara alijifungia katika ofisi yake. Dawati lilikuwa limepangwa kwa mpangilio wa kijeshi — vitabu vya Linguistic (Isimu), faili za wanafunzi, picha za miaka ya nyuma zikiwa zimefichwa kwenye droo.

Alifungua journal yake nyeupe, akachukua kalamu ya wino wa bluu. Akaandika:

"Today, the world has received his news. They have begun to mourn. I have begun to preserve — to preserve every silence they passed through without ever hearing my scream."

Akimanisha: Leo dunia imepokea taarifa za mumewe. Wao wameanza kuomboleza. Mimi nimeanza kuhifadhi. Kuhifadhi kila kimya ambacho wamepita nacho bila kusikia kelele yangu.

“Today marks the beginning of my silence. But not because of sorrow, because of a plan."

“Leo ndio mwanzo wa ukimya wangu. Lakini si kwa sababu ya huzuni. Ni kwa sababu ya mpango wangu.”*

Aliweka kalamu chini, akatabasamu kwa unyonge, na akaifunga journal hio kwa uzito. Kisha akatizama saa ya ukutani.

“Saa ya mwisho imeanza,” alijisemea.

Next