Reader Settings

Mvua ya saa nne asubuhi haikuwa nzito, lakini ilikuwa ya kutosha kulowesha nyasi za bustani ya mbele ya nyumba ya Zara. Njia ya mawe iling’aa kwa unyevunyevu, na sauti ya matone ikipiga bati ilikuwa kama muziki wa taratibu wa muda mrefu.

Zara alikuwa jikoni, akikata kipande cha limau kwa mkono wa kushoto. Kikombe cha chai kilikuwa tayari na maji ya moto, lakini bado hakuwa amemimina. Alitazama kioo cha dirishani, matone yakitiririka kama machozi yanayokataa kudondoka.

Kengele ya mlango ililia.

Alitulia kwa sekunde chache, kisha akatembea pole pole na kufungua mlango bila kuuliza nani.

Mbele yake alisimama mwanaume wa umri wa karibia miaka hamsini. Urefu wa wastani, ngozi ya kahawia iliyoiva na ndevu zilizochanganyika na weupe. Alikuwa amevalia koti jeupe la mvua na glovu nyeusi mkononi.

“Profesa Zara Mwinyi?” aliuliza kwa sauti ya heshima.
“Ndiyo,” alijibu kwa utulivu.
“Mimi ni Mpelelezi Karim Obuya, kutoka kitengo cha upelelezi wa kimataifa. Ningependa kuzungumza nawe kidogo kuhusu mume wako, Imran Said.”

Zara alifungua mlango zaidi. “Ingia.”

Karim aliketi kwenye kiti cha mkono kilicho mbele ya meza ya kahawa. Zara aliweka kikombe cha chai mbele yake, bila sukari, bila maelezo.

“Samahani kwa usumbufu. Hatujaweza kuthibitisha taarifa zozote mpya bado, lakini kuna vipande vya mawasiliano kutoka Goma vinavyoonyesha kuwa Imran alionekana mara ya mwisho siku moja baada ya taarifa rasmi kuripotiwa,” alisema Karim huku akiangalia notes zake.

Zara hakutikisika. Alikunywa chai yake taratibu.

“Niliambiwa amepotea,” alisema kwa sauti ya kawaida.
“Ni kweli. Lakini kazi yangu ni kuchambua upya muktadha, kuangalia ikiwa kuna mtu alizungumza naye kabla ya safari, au alionyesha hofu yoyote isiyo ya kawaida.”

Kimya kilijaa chumba kizima.

“Imran ni mwandishi wa habari za vita,” Zara alisema. “Hofu au hatari kwake ni kama chai ya kila siku.”

Karim alitabasamu kwa upole, lakini macho yake yalibaki makini.

“Alikutumia ujumbe wowote wa mwisho? Barua pepe? Voice note? Kitu chochote?”

“Ameacha ujumbe kwenye bahasha moja humu ndani kwetu.

Imeandikwa ‘do not open until things have changed.’ Sijafungua bado,” Zara alijibu, akimtwisha jibu hilo kana kwamba halikuwa na uzito.

“Unaweza kuionyesha tafadhali?”
“Samahani. Hiyo ni la faragha.”
“Hata ikiwa linaweza kusaidia katika uchunguzi?”
“Hata hivyo siwezi,” alikata kauli kwa sauti tulivu lakini ya mwisho.

Karim akaweka notebook yake chini.

“Sawa. Natambua ni kipindi kigumu. Lakini ukibadilisha mawazo, wasiliana nami. Tuko hapa pamoja kwalengo la kusaidia.”

Alisimama kuanza kuondoka. Kabla hajafika mlangoni, aligeuka:

“Zara… unajua ni kwa nini watu wengi wanalia kupita kiasi wakifiwa?”
Zara akamtazama.
“Kwa sababu hofu yao kubwa si msiba. Ni ukweli mpya usioweza kufutwa.”

Zara hakujibu.

Alifunga mlango nyuma ya Karim. Akabaki amesimama pale pale kwa dakika kadhaa.

*******

Usiku katika chumba chake cha kazi, Zara alifungua journal yake na kuandika:

"They’ve sent someone to investigate me. But Karim cannot read the language of silence. And that is what I’m speaking now."

“Wametuma mtu wa kunichunguza. Lakini Karim hawezi kusoma lugha ya ukimya. Na ndicho ninachokizungumza sasa.”

Kisha, kwa mstari wa chini zaidi, akaandika:

"Some people come with questions. I create a world that needs no answers."

“Kuna watu huja na maswali. Mimi natengeneza dunia isiyohitaji majibu.”

Previoua Next