Reader Settings

FOR YOU 2

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!

★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA KUMI

★★★★★★★★★★★★

Asubuhi ilipofika siku iliyofuata, ACP Nora aliamkia kule kwenye jengo lile ilipokuwepo timu ya Luteni Michael. Aliwakuta baadhi yao tu; Bobby, Mario, Hussein, na Omari, nao wakamwambia alipendeza sana kwa msuko wake mpya, kisha wakamjulisha kwamba Luteni Michael na wengine walielekea kule alikokuwa Kanali Oswald Deule kwa kuwa walihitaji kumpa taarifa za maendeleo yao katika msako huu, na ili awapatie mbinu na mwongozo mpya pia kusaidia. Nora akamjulisha Bobby kwamba jana alitingwa na mambo fulani, hivyo utafiti wake kule hospitalini ulikwama, lakini leo angerudi tena ili kuukamilisha, kisha angekuja na mambo mapya pia. Mario akatania kwa kusema siku ya leo ingekuwa kama siku ya mapumziko kwao kwa sababu wasingepiga hatua yoyote mpaka Luteni Michael arudi.

Baada ya hapo, ACP Nora akawasiliana tena na daktari Shani kumuuliza ikiwa angekuwa na muda wakati huo ili aonane naye, na daktari huyo akamwambia angepata muda wa kuwa huru kwenye saa 8 mchana, hivyo aende wakati huo. Nora akakubali, kisha akawaaga wengine kwa kusema anaenda kufatilia mambo mengine. Kihalisi alitaka kwenda kumwona Asteria tena, naye akamtafuta na kumwambia watoke kupata chakula sehemu fulani.

Walikutana muda mfupi baadaye, naye Asteria akamwambia dada yake kuwa alijisikia vizuri zaidi sasa, na kwamba mpenzi wake alimwomba samahani na kumpa zawadi nzuri sana. Nora akafurahia sana kwa ajili yake, huku Asteria akimwambia na yeye pia atafute mwanaume kwa sababu alipitwa na mambo mengi. Nora akasema wakati huo ungefika tu, ila kwa sasa alihitaji kupiga kazi kwanza, na mapenzi yangefuata baadaye.

★★

Walikuja kuagana kwenye saa 7 ya saa 8, naye ACP Nora akaenda hospitalini kuonana na daktari Shani. Alipokelewa vizuri na mwanamama huyo, ambaye alibobea kwenye masuala ya upasuaji, kisha wakaanza mazungumzo kuhusiana na historia yao ya urafiki. Shani pia alisomea Marekani kama Nora, na kwa kipindi fulani walipatana sana kule ijapokuwa walisomea masuala tofauti na kuonana mara chache. Baada ya kukumbushia, Nora sasa akaja kwenye pointi iliyompeleka. Akamweleza alichohitaji, lakini Shani akasita kumpatia. Alimwambia alipewa jukumu la kuzilinda taarifa zile na watu wa "juu," yaani watu wenye nguvu, naye hakupaswa kuzitoa ovyo kwa yeyote.

Nora alishindwa kuelewa sababu ni nini kwa kuwa hata Shani hakujua sababu ni nini, lakini alijua tu kwamba hakupaswa kuyatoa bila idhini ya watu hao. Nora akalainisha mambo kwa kumwambia amwamini tu, kwamba alihitaji taarifa fulani tu ndogo, na baada ya hapo angemrudishia bila yeyote kujua. Akamwomba sana, naye Shani akalegeza. Akampatia mafaili yenye taarifa za majeruhi wale na kumsihi azirudishe kufikia kesho muda kama huu. Akamwomba sana asimwonyeshe yeyote yule, naye Nora akakubali na kumhakikishia kila kitu kingekuwa sawa.

ACP Nora akamuaga daktari huyo na kuondoka hapo hospitalini. Alikuwa anatamani sana kumuuliza ni nini na ni nani waliomzuia mwanamke huyo kuzitoa taarifa hizi, lakini hakutaka kumshurutisha kufanya mambo ambayo huenda yangemsababishia mama wa watu matatizo asiyokuwa na uelewa wowote kuyahusu. Akaona ni vyema tu aende yeye mwenyewe kutafiti alichohitaji kisha amrudishie mafaili hayo kabla ya jambo lolote lisilotazamiwa kutokea.

Lakini Nora hakuweza kuyapitia mafaili hayo baada ya Inspekta Jenerali wa Polisi, IGP Donald Ngassa, kumtafuta na kumwomba akutane naye ili ampatie msaada kwa jambo fulani. Yaani Nora hakuwa mtu wa kupumzishwa kabisa. Kwa kuwa ni siku chache zilikuwa zimepita tokea mara ya mwisho walipoonana, akakubali tu kwenda upande wake kuona angeweza kusaidia vipi. Akaahirisha kuyasoma mafaili yale na kuyapeleka tu hotelini kwake, kisha akaelekea kwa IGP.

★★

Muda ulisonga, naye ACP Nora akawa amemaliza kumpatia IGP Donald Ngassa msaada aliohitaji kwenye masuala ya kuwaongoza baadhi ya polisi wa kitengo fulani upande mwingine wa jiji. Alikuwa amemwomba msaada huu Nora kwa sababu alijua kipawa chake cha kuongoza mambo kilikuwa kikubwa, lakini pia ni kwa sababu tu ya uvivu akaona ampe dada wa watu kazi zaidi.

ACP Nora akaanza kurejea upande wake wa jiji hatimaye. Aliwasiliana na Luteni Michael, ambaye alimwambia kwamba walikuwa wamerejea huku baada ya mkutano wao mfupi na Kanali Oswald, hivyo wangeendelea na kazi. Lakini akamwambia Nora apumzike tu kwanza kwa leo, ili kesho ndiyo wakutane na kujipanga vizuri zaidi. Nora akaafikiana na hilo, akisema pia utafiti wake aliotaka kuufanya ungekuwa mezani kwao kufikia kesho, naye akamshukuru Luteni Michael kwa kumpa muda wa kupumzika.

Giza lilikuwa limeshaingia kufikia wakati huu, naye Nora akaamua kwenda kule Sea House kwanza ili ajipe muda wa kutuliza akili yake kama kawaida. Alikuwa na wazo pia la kuonana na Lexi, kwa sababu ni kama alianza kumzoea "mwanamke" huyo ambaye alikuwa ameanza kuwa njia nzuri ya kumsaidia kusafisha akili yake kutokana na misongo mingi. Hakuwa na ukawaida wa kupendezwa na watu mpaka kutamani kuwaona tena, lakini kwa Lexi sasa ilianza kuwa tofauti.

Alipofika pale, alikaribishwa na Elias na jamaa kumuuliza ikiwa angependa amwekee kinywaji kama kawaida yake. Nora akakubali na kuketi, kisha akaendelea kuwa hapo akinywa wine yake taratibu kama anasubiri mtu. Lakini wakati huu Lexi hakufika hapo, hivyo akamuuliza Elias ikiwa leo angefika, au kama ratiba yake haikueleweka. Elias akatania kwa kumuuliza ikiwa alitaka kumkamata labda, lakini Nora akasema alikuwa tu anataka kumwona, naye Elias akamjulisha kuwa Lexi alifika hapo kabla yake kisha akaondoka kuelekea sehemu fulani za beach, lakini hakujua ni wapi.

Moja kwa moja Nora akakumbuka sehemu ile ambayo Lexi alimpeleka usiku wa jana, naye akamalizia kinywaji chake na kuondoka ili aende kujaribu kuona ikiwa alikuwa huko. Ilikuja kwa kumshangaza kiasi kwa nini alitia jitihada za kutaka sana kumwona "mwanamke" huyo, kwa sababu hata hakumfahamu vizuri namna hiyo. Lakini bado tu ikawa ni kama kuna kitu kinamsukuma kuendelea kumtafuta, akitarajia kuwa na mazungumzo mazuri pamoja naye kama usiku uliotangulia.

Baada ya kufika sehemu ile, alivikuta viti vile pale, na chini kukiwa na moto uliowaka katikati ya kitu kilichochengenezwa kama mafiga madogo. Nora akatabasamu baada ya kumwona Lexi akiwa ameketi kwenye kiti kimojawapo kwa kumpa mgongo. Alikuwa amevalia nguo nyeupe yenye kubana mwili kwa juu, iliyokuwa yenye mikono mirefu na kufunika mpaka sehemu ya shingo yake. Suruali ya jeans nyeusi ilionekana pia miguuni mwake, na viatu vya raba vya rangi nyeupe pia. Kulikuwa na chupa mbili za wine chini pamoja na vikombe viwili pia. Akaanza kusogea taratibu kumwelekea.

Lexi akahisi kabisa kwamba kulikuwa na mtu anakuja nyuma yake, na kwa sababu hakujua ni nani, akaishika chupa ya wine na kuikaza kiganjani mwake bila kugeuka ili kama ni adui basi amshambulie kiaina.

"Nimekubamba..."

Sauti ya Nora ikasikika kwake ikisema hivyo, naye Lexi akatenda upesi na kujifanya kashtuka na kugeuka nyuma.

"Hey! Don't do that... umenishtua!" Lexi akasema.

"Ahahahah... pole. Mambo vipi?"

"Safi. Karibu."

"Asante. Kuna mtu unamsubiri?"

"Hapana."

"Mbona naona chupa na vikombe viwili?"

"Labda nilikuwa nakusubiri wewe..."

"Ah wapi! Polisi huwa hasubiriwi..."

"Ahahah... ila anakimbiwa tu..."

Nora akaketi kwenye kiti cha pembeni.

"Unapenda kuwa hapa peke yako tu kwa nini sasa?" Nora akauliza.

"Nafikiri nilikwambia sababu ile jana..."

"Eeh kweli... kwa sababu pametulia..."

"Angalau lakini umekuja. Za huko? Unaonekana kama vile umetoka kukimbizana na akina Mess Makers ahahahah..." Lexi akatania kimakusudi.

"Ahahah... ungejua..." Nora akasema.

Lexi akaanza kuwekea kikombe cha pili wine, naye Nora akawa anamwangalia kichwani, akipendezwa na jinsi nywele laini za Lexi zilivyopeperushwa na upepo wa bahari.

"Hao jamaa bado wanawasumbua sana mapolisi, eti?" Lexi akauliza.

"Agh... achana na habari zao. Tuongelee mambo mengine lakini siyo kazi, sawa?" Nora akamwomba.

"Okay," Lexi akasema na kumpatia kikombe chenye kinywaji.

"Nywele zako ni natural, eti?" Nora akauliza.

"Naam? Ndiyo. Ni zangu," Lexi akajibu.

"Ni nzuri. Nafikiri ungependeza zaidi kama ungeziacha zote zikue badala ya kupiga duku hilo," Nora akamtania.

"Ahahah... asante kwa ushauri."

"Asili yenu... asili yako ni ya wapi?"

"Kwa kina bin Laden kule..."

Nora akacheka.

"Naonekana kama mhindi eti?" Lexi akauliza.

"Tena wale weupe..."

"Nimeshaambiwa na wengi niwape ushauri kuhusu dawa nayotumia usoni ili wawe kama mimi. Wanafikiri najichubua."

"Ahahahah... hamna wamekosea. Ngozi yako ni nzuri sana lakini."

"Asante. Hata we' siyo mbaya sana," Lexi akatania.

Nora akacheka na kunywa wine kidogo.

"Kwa nini dada mzuri kama wewe ukaamua kuwa polisi? Si ungepiga hata modelling?" Lexi akauliza.

"Ahahahah... wewe ni mtu wa ngapi sijui kuniambia hivyo," Nora akasema.

"Wote waliokwambia hivyo ujue wanasema kweli. Hauonekani kama type za mapolisi wanawake..."

"Kwa nini? Kwani type zao zikoje?"

"Manene manene, meusi, pardon me lakini, wengi wanaonekanaga kama hawawezi kukaa dakika zaidi ya mbili bila kuomba hela madereva wa magari barabarani..."

Nora akacheka. "Siyo wote wako hivyo bwana. Na mimi siko kundi hilo," akasema hivyo, naye Lexi akacheka pia.

"Kiukweli ndiyo moja ya mambo yaliyonifanya nisiamini kwamba wewe ni askari mara ya kwanza tulipoonana. Yaani dada uko vizuri kisura na kimwili. Hata ukisema uombe kupiga u-video vixen, wasanii watapanga foleni ili kukuchukua," Lexi akatania.

Nora akacheka na kusema, "Flattery ni nzuri kwa mwanamke wa aina yako Lexi. Kiukweli mimi nilipenda sana kuja kuwa askari tokea nilipokuwa mdogo."

"Kwa nini?"

"Mmmm... naweza kusema tu kwamba nilipenda kusaidia watu. Mara ya kwanza nimeokoa uhai wa mtu nilijisikia vizuri sana, nikataka kufanya mengi zaidi kiutumishi ili kuweza kuwasaidia wengi zaidi," Nora akaeleza.

"Mara ya kwanza umeokoa mtu ilikuwa wapi?"

"Ilikuwa... kwenye hoteli fulani hivi wakati niko mdogo. Tena nilikuwa na miaka 14 tu. Kuna mtoto mdogo alikuwa kwenye swimming pool, akashindwa kuji-handle vizuri na kuzidiwa na maji. Ndiyo nikaingia kumwokoa. Ni siku ambayo sitasahau yaani. Ilinifanya nijihisi vizuri sana," Nora akasimulia.

Lexi akabaki kukunja uso kwa kutafakari. Kisa alichokisimulia Nora kilifanana na kisa alichojionea yeye mwenyewe wakati alipokuwa mdogo. Akakumbuka pia kwamba aliwahi kukiandika kisa hicho kwenye moja ya kazi za madam Valentina wakati yuko chuo. Nora alipomwangalia Lexi, akatambua alikuwa amezubaa.

"Hey vipi?" akamuuliza.

"Oh, oh nothing. Aam... nimependezwa tu na hadithi yako. Umeanza kuwa hero tokea udogoni kumbe..." Lexi akajibu.

"Huwa sijioni kama hero, ila kama mtumishi tu wa kawaida..."

"Unaonekana kuwa na life ya juu pia."

"Mh... hapana. Kawaida tu."

"Kwani huwaga mnasema sasa..."

"Ahahahah... haijalishi. Mimi napenda kuishi maisha ya kawaida tu..."

"Mmm... ya kivyako pia eeh?"

"Yeah."

"Hauna ndugu wengine wanaong'ang'ania chenji ya mshahara?"

"Ahah... wapo. Nina wadogo zangu wa kike wawili. Mmoja yuko Marekani kimasomo, na mwingine yupo huku... yeye ni kula bata tu. Sina ukaribu sana na ndugu wengine wa kiukoo... tuko distant. Ni wadogo zangu tu ndiyo niko in touch nao mara kwa mara," Nora akasema.

Lexi alikuwa anataka kuuliza kuhusu baba yake Nora, lakini akaona akaushe tu kwanza. "Lakini life ya kujitenga unaonekana kuishikisha sana mizizi. Hawawezi kuona kama vile dada hatupendi?" akamuuliza.

"Ahahah... hapana. Nawapenda wadogo zangu. Ila, kwa mambo mengi wanayofanya... mara nyingi yanawaleteaga hasara, na mimi nakuwa sitaki kujiingiza huko, si unaelewa? Wanapenda kujiachia sana na kutupa pesa mpaka inakuwa too much. Me nakuwa tu bize kuwasaidia wasije kufanya mambo yatakayosababisha wafungwe au hata wafe," akasema Nora.

Lexi akashusha pumzi na kusema, "Yeah, hata mimi ilikuwa hivyo na baadhi ya rafiki zangu tulipokuwa tunafanya kazi kwenye gereji ya mjomba wangu. Me ndo' nikawa kama mama yao pale."

"Subiri, wewe unafanyaga nini kwenye gereji ya mjomba wako?" Nora akauliza.

"Nafanyaga kazi, mezani, ku-order part za magari na kuhudumia wateja; wakati mwingine nashughulikiaga magari pia kama panakuwa pamejaa wateja."

"Basi me nikafikiri labda wewe mtoto wa boss tu unakaa na kuletewa kila kitu... yaani hauhitaji kufanya kazi," akasema Nora.

"Ahahah... naonekana wa kishua sana eeh?"

"Sana..."

"Well... hivyo ndivyo vitu nilivyofanya; na kuhakikisha familia inakaa kwa amani na kusaidia biashara isife..." Lexi akasema, akimaanishia wenzake kwa njia ya fumbo.

"Kumbe... okay. Nafurahi umeniambia hayo kuhusu wewe. Napendezwa na wewe zaidi sasa kama rafiki..."

"Wow! Unaniona kama rafiki sasa hivi?" Lexi akauliza kichokozi.

"Naapa kabisa kwamba kuanzia sasa sisi ni marafiki, siyo kwamba pombe imenichanganya," Nora akatania.

Lexi akacheka kidogo. Baada ya kutazama baharini kwa ufupi, akamuuliza, "Hivi ni kitu gani kuhusu huku Sea House kinachokufanya uonekane kuwa mtu tofauti sana?"

"Tofauti kivipi?" Nora akauliza.

"Tofauti na mapolisi wengine ambao nimeshawahi kukutana nao yaani..."

"Mmm... kila mtu nayefahamiana naye hapo ni kama familia. Unajua, niliwahi kuzimia hapa karibu kabisa na bahari, lakini badala ya kujikuta naelea kwenye maji bila nguo, kuna watu walinichukua na kunipeleka ndani na kunifunika na blanket kabisa... akiwemo Emmanuela. Kwa hiyo... ahah... samahani, sijui hata kwa nini naongelea hilo, naonekana kilaza kweli..." Nora akasema kwa haya kiasi.

Lexi akatambua kuwa sasa mwanamke huyu angalau alikuwa kamzoea sana. "Hamna, wala hata. Nimeshakuchunguza mheshimiwa na, siyo kwamba tu unakuwa na furaha ukilewa, ila unapendeka kwa kukuangalia tu," akatania.

"What! Lini uliniona nimelewa?" Nora akauliza.

Lexi akacheka na kusema, "Ni siri yangu!"

Nora akatabasamu na kusema, "Haya bwana, asante. Point ni kwamba, watu kadhaa hapo House wananijua mimi kama Nora, na siyo kuniona kama Kamishna tu. Ni kama ndo' kwetu vile."

"Inaonekana kama unataka kuja kuishi sehemu ya namna hii siku moja..."

"Ndiyo, labda miaka michache baadaye. Nimejipangia ku-retire nikifikisha miaka 40, hata niiuze na nyumba yangu kabisa, ili baada ya hapo niishi maisha niliyotamani kutokea zamani..."

"Ya kujiachia..."

"Ahahah... unaweza ukasema hivyo..."

Lexi alipendezwa sana na mtazamo wa Nora. Alianza kuvutiwa naye hata zaidi, kiasi kwamba ikabidi aangalie pembeni kwa kukumbuka kuwa hakupaswa kujiachia sana kwa mwanamke huyu huku akijua kwenye upande wa maadui wao, yeye pia alikuwemo.

"Nimefurahi sana pia kujua hayo kuhusu wewe," akasema Lexi.

Nora akatabasamu.

Kisha Lexi akataka kuichukua chupa ya wine chini ili aongeze, lakini kwa tukio baya akaipiga kwa vidole nayo ikaanguka na kuanza kumwaga kinywaji. Akanyoosha mkono wake ili aiokote upesi, na hiyo ikafanya nguo yake ivutike sehemu iliyofunika mpaka mwanzo wa kiganja chake, na hapo Nora akaona jambo fulani. Lexi hakutambua na kuiokota tu chupa haraka, kisha akamwangalia Nora na kukuta anamwangalia kwa umakini.

"Vipi? Unawaza kuniponda na ndala kisa share yako ya wine imemwagika?" Lexi akauliza kiutani.

"Hizo ni tattoo?" Nora akauliza.

Tabasamu la Lexi likafifia, kisha kwa haraka akaivuta sehemu ile ya nguo ili kuficha.

"Aam... yeah. Nilichoraga zamani... kama kupaka tu yna... hahah..." akasema na kuanza kumimina wine kwenye kikombe.

"Zinaonekana vizuri sana. Ulizichorea wapi?"

"Ni rafiki ya... mjomba wangu ndiyo alinichora. Nikuongeze wine?"

"Hapana, asante. Naweza kuziangalia?"

"Oh, wala usijisumbue... siyo hata nzuri, wala muhimu. Okay. Mmm... you're missing out. Ijapokuwa wine imemwagika lakini ladha bado ni tamu... na mchanga tu kidogo," Lexi akajitahidi kubadili mada.

Nora akatabasamu na kuangalia chini.

"Lakini kama umefikiria kuja kuishi sehemu kama ya namna hii, vipi Mr. Right wa baadaye akikataa? Akitaka mjenge state kama Illinois hivi utafanyaje?" Lexi akauliza.

"Ikiwa haupendi niangalie tattoo zako haina shida Lexi. Kila mtu ana siri zake," Nora akamwambia kiustaarabu.

Lexi akamtazama tu kwa umakini, naye Nora akaangalia muda kwenye simu yake.

"Asante Lexi kwa company yako. Nimefurahi kukuona leo," Nora akamwambia.

"Mimi pia mheshimiwa," Lexi akajibu.

Nora akatabasamu na kusema, "Naomba namba yako tafadhali. Tutakuwa tuna..."

"Tunachekiana... fresh kabisa. Ni vizuri kuwa na rafiki polisi... sasa hivi wanaonionea watanitambua," Lexi akasema.

Nora akacheka huku akimpa simu, naye Lexi akampatia namba yake. Baada ya Nora kujaribu kuipigia, simu aliyokuwa nayo Lexi hapo ikaita, naye akamwambia angeitunza yake pia. Nora akanyanyuka.

"Nahitaji kukimbia sasa. Wewe bado upo?" Nora akauliza.

"Ndiyo, ila sina muda mrefu nitaondoka pia..."

"Okay..."

Nora akabaki kumtazama tu Lexi kama anataka kusema kitu kingine, huku Lexi akimwangalia pia kwa njia ya kawaida.

"Okay... usiku mwema," Nora akasema kiajabu-ajabu.

"Kwako pia mheshimiwa rafiki," Lexi akamwambia.

Nora akatabasamu na kuanza kuondoka tu. Mara kwa mara angegeuka nyuma kumwangalia Lexi na kukuta bado anamtazama pia huku anatabasamu, na Lexi akampungia mkono wa kwa heri.

Baada ya Nora kuondoka, Lexi akabaki kutafakari mambo yote yaliyotokea hapo. Alijilaumu kiasi kwa sababu ni kama alikuwa anapoteza muda wake kupiga story na Nora badala ya kutafuta njia ya kunyonya taarifa kutoka kwake zenye umuhimu kwa timu yao. Ilikuwa wazi sasa kwamba alipendezwa na utu wa Nora, kwa kuwa alijionea jinsi mwanamke huyu alivyokuwa mnyoofu kwa kadiri kubwa. Lakini Lexi akajiahidi kuwa imara zaidi wakati mwingine, hasa kwa kuwa Nora mwenyewe aliomba namba yake, hivyo njia zingekuwa nyingi za kupata taarifa za nyendo zao.

Simu hii ambayo alimpatia namba Nora, aliitumia kwa mawasiliano ya kawaida katika "maisha ya kawaida" ambayo yeye na kundi lake waliishi ili kutojulikana. Hangewasiliana na wenzake kupitia simu hii, bali wote walikuwa na vifaa vingine maalumu walivyotumia kuwasiliana ambavyo viliunganishwa moja kwa moja na Torres kwa ajili ya kupeana taarifa muhimu. Lakini kama ni namba za simu za kawaida walizotumia, kila mtu alikuwa nazo, ila wangechekiana tu kwa jumbe fupi ambazo hazingekuwa na nuksi yoyote ile ili kuzuia kutambulika.

Walikuwa makini sana hawa watu, lakini sikuzote huwa hakuna uhakika wa kujua ni wakati gani mambo yangekuja kuharibika, na kwa Mess Makers, hilo halingechukua muda mrefu.

★★

Nora aliporudi kwenye chumba cha hoteli alikokaa, alianza tena kupitia mafaili ya wafanyakazi waliojeruhiwa wa makao ya benki kuu. Alijua kwamba wafanyakazi wengi wa pale walishikiliwa kwa muda fulani baada ya tukio lile la wizi kwa ajili ya mahojiano, na matokeo yalikuja kwamba hakuna hata mmoja aliyejua kilichotokea kwa sababu baada ya mabomu yale kulipuka, wengi walikimbia kuokoa uhai wao, isipokuwa labda wale waliojeruhiwa ndani huko.

Nora akaanza kupitia taarifa za wale waliojeruhiwa, nao walikuwa ni watu 11 tu; wanaume saba, wanawake wanne. Tokea mwanzo ilisemwa tu kwamba waliojeruhiwa walikuwa wengi sana, lakini namba hii ilikuwa ndogo kulinganisha na "wengi sana." Hakukuwa na mambo mengi kwenye mafaili hayo kama alivyotarajia, hivyo akatafuta rekodi za watu hao waliojeruhiwa kwenye laptop yake, lakini kwa sababu fulani zikawa zimefungiwa.

Hii ilimshangaza kiasi. Ni kwa nini taarifa za watu hao zilifungiwa? Alitaka sana kujua ili kuipa nguvu kauli yake ya mara ya kwanza kwamba wezi wale walitoka kwa kujifanya wamejeruhiwa, kwa sababu ambulance zilizofika kuwachukua walioumia zilirudi hospitalini pungufu ya moja. Alitaka kujua kwenye ambulance iliyotokomea ni wafanyakazi gani WALIOTAKIWA kuwa mule, kwa sababu isingepatana na akili kwamba hawakufika hospitalini halafu waje kudai kuwa siku hiyo walikuwepo kazini. Aliwaza huenda kati ya wafanyakazi waliojeruhiwa, wale waliotoroka kwa kujifanya wamejeruhiwa ndiyo walikuwa wezi waliofanya jambo fulani kuwaziba mdomo wafanyakazi halisi wa hapo ili kufanikisha mipango yao.

Wazo la kwamba huenda hata ni baadhi ya watu wa hapo hapo ndiyo walifanya mpango wa kuiba pesa hizo kijanja halikuwa mbali na akili yake, na labda ndiyo sababu zilipita siku mbili kabisa baada ya wizi huo pakiwa kimya, na waandishi wa habari kuzuiwa kufika huko ili kuficha yaliyoendelea pale, ambayo ndiyo yaliyozusha utata mkubwa wa suala hili lote. Yeye alitakiwa tu kusaidia kuwakamata wezi, sawa, lakini alitaka kujua anamkamata nani hasa. Mambo yote yalionekana kuzama kwenye suala zito mno zaidi hata ya ugaidi.

Kwa hiyo akaamua kwamba angemjulisha Luteni Michael kesho ili amsaidie kupata taarifa hizo bila kuhusisha mtu mwingine zaidi ya timu yake, wapate taarifa alizohitaji, kisha wachimbe zaidi ili kupata ukweli. Akaingia kujipumzisha tu baada ya hapo.

★★★

Asubuhi na mapema ACP Nora akawa amefika kwenye jengo lile na kuikuta timu yote ya Luteni Michael ikiwepo. Wakamsalimu na kumkaribisha vizuri, nao wakamwambia kuhusu njia kadhaa ambazo wamejaribu kufanya ili kupata chochote kutokana na uchunguzi wao wa mara nyingine tena wa kampuni zile za madini bila mafanikio yoyote, kwa sababu hawakupata kiashiria chochote chenye kuwaongoza kwa Mess Makers.

Nora bila kuchelewa akaweka wazo lake jipya mezani. Baada ya kuwajulisha kuhusu uchunguzi wake, wote waliona kweli hapo katikati kulikuwa na nuksi, lakini baadhi wakasema inaonekana taarifa hizo zimefichwa kwa sababu fulani ambazo hazikuwahusu wao, kwamba wenyewe walitakiwa tu kukamilisha "mission" waliyopewa.

Ijapokuwa hata Luteni Michael kipindi cha nyuma alikuwa na mtazamo huo, sasa akasema kwamba wazo alilotoa Nora kweli lingetakiwa kufanyiwa kazi, kwa kuwa muda ulikuwa unasonga na walihitaji kutafuta kila njia ya kupata matokeo mazuri. Akawakumbusha kuhusu jinsi mara ya kwanza Nora alivyotumia hekima kutambua Kevin Dass alijifanya kichaa mpaka wakamkamata, hivyo hata kwa hili akaunga mkono kwa sababu aliheshimu kipawa chake katika kuona mambo kwa njia pana. Nora akafurahi baada ya kuona Luteni Michael alibadili mtazamo wake, naye akamshukuru kwa hilo.

Basi baada ya kukubaliana, upesi Bobby akaingia kwenye kompyuta na kuanza yake ili kuzipata taarifa zilizofichwa. Baada ya dakika mbili za kubofya hapa na pale kwenye "keyboard" huku screen ikileta taarifa za mambo kadhaa, akasitisha zoezi hilo na kubaki ameitazama tu kompyuta.

"Vipi mzee?" akauliza Omari.

"Luteni... hizo taarifa zimefichwa kwenye database za Ikulu," Bobby akasema.

"Nini?" Luteni Michael akashangaa.

"Kwa nini?" Mario akauliza.

"Me nitajuaje sasa? Nenda ka-date na mmoja wa ma-IT wa huko atakwambia," Bobby akamwambia Mario.

Nora akatazamana na Luteni Michael kimaswali.

"Ina maana... yaani watu kujeruhiwa tu ndiyo taarifa zinafi... hapana... hii harufu mbaya siyo ya panya aliyekufa, ni mzoga mkubwa sana umefichwa," Alex akasema kitamathali.

"Ingia sasa uziangalie," Mishashi akamwambia Bobby.

"Acha bangi kaka. Wakigundua nimeingia na kuiba hizo info, sisi wote hatuna kazi hapa. Ni kama unaniambia ni-hack Ikulu mzee," akasema Bobby.

"Dead end kwa hiyo? Tunafanya nini sasa Luteni?" akauliza Alex.

Luteni Michael bado akawa anaangaliana na Nora, akiona jinsi mwanamke huyu alivyotaka sana afanye uamuzi ambao huenda ungewaletea shida. Lakini kiukweli hata yeye alitaka sana kujua ni nini kiliendelea mpaka taarifa hizo kufichwa Ikulu, hivyo akaamua kuuchukua huo huo uamuzi.

"Bobby... ingia," Luteni Michael akasema.

"Nini?!" Bobby akashangaa.

"Umenisikia," Luteni Michael akasema.

"Luteni, nina watoto watano, mmoja ni mlemavu, na...."

"Do it!" Luteni Michael akamkatisha Bobby.

Bobby hakuwa na jinsi ila kutii tu japo kishingo upande, naye akaingia kwa njia ya marufuku ili kupata taarifa hizo. Alifanya mambo chap chap na kufanikiwa kuipata orodha ya wafanyakazi wale waliopelekwa hospitali siku hiyo, kisha akatambua kwamba ma-IT wa ikulu walimgundua na kuanza kumzibia njia.

"Shit!"

Bobby akatamka hivyo na kufungia kila kitu haraka ili wasifanikiwe kumpata, ingawa alielewa kwamba hicho ni kitu ambacho hakingewashinda. Uzuri ni kuwa tayari alikuwa ame-copy orodha hiyo, naye akairusha moja kwa moja kwenye tablet (kama simu) nyingine.

"Luteni, kazi yangu..." Bobby akasema.

"Usijali Bobby kuhusu hilo, nita-handle mimi. Mpe ACP aangalie," Luteni Michael akamwambia.

Bobby akampatia Nora taarifa zile, naye akaanza kuzipitia.

"Okay, so genius wetu, unaona nini hapo?" akauliza Hussein.

"Walitakiwa kuwa 11, lakini ni 9 tu ndiyo waliofika hospitalini," Nora akasema.

"Nini? Kwa hiyo inamaanisha nini?" akauliza Vedastus.

"Inamaanisha kati ya hao, wawili ndiyo wezi wetu!" Mishashi akamwambia.

"Siyo uhakika Misha. Nafikiri kuna kitu hawa Mess Makers walifanya ili wenyewe ndiyo waingie kazini sehemu ya hawa wawili siku hiyo... ila sijajua ni jinsi gani," Nora akasema.

"Majina?" Luteni Michael akauliza.

"Nathan Masunga... na Eunice Shirima," Nora akasema.

"Bobby, tafuta waliko hawa," Luteni akasema.

Bobby akaanza kuwasaka upesi, naye akafanikiwa kupata anwani zao.

"Luteni nimewapata. Lakini, huyu Shirima amekufa," Bobby akasema.

"Tokea lini?" akauliza Luteni Michael.

"Ana kama wiki sasa. Tena siku nne baada ya wizi," Bobby akasema.

"Harufu ya huo mzoga bado inaingia vizuri puani mwako?" Hussein akamuuliza Alex kiutani.

Alex akamwonyeshea dole la kati.

"Kwa hiyo ni kusema kwamba hawa Mess Makers ndiyo wamemuua au?" akauliza Vedastus.

"Amekufa vipi?" akauliza Nora.

"Aliumwa. Kifua. Ndiyo ilivyoandikwa," Bobby akasema.

"Huo msiba basi ulifanywa kimya kimya sana aisee, maana haujasikika popote," Mario akasema.

"Kama kweli angekuwa mmoja wa majeruhi wa bomu, basi mpaka muda huo angekuwa hospitali labda. Na lazima tu kifo chake kingetangazwa. Lakini prrrrr... Ikulu," Omari akasema.

"Vipi kuhusu Nathan?" akauliza Mishashi.

"Yupo. Yupo maeneo siyo mbali na Kivukoni. Bado anasomeka kama mfanyakazi mwaminifu, lakini kwa sasa haendi kazini maana alivunjika mguu kwenye bomu," Bobby akasema.

"Kwa hiyo, unasema kwamba hatoki nyumbani?" akauliza Luteni Michael.

"Ndiyo inavyoonekana," Bobby akajibu.

"Nipe address yake haraka. Veda, Omari, Hussein, mko nami. Tunamfata huyo pimbi. Mario, Omari, nendeni na ACP pande za huyo Shirima mwangalie kama kuna nuksi zingine huko. Bobby, usiache kutupa touch zozote mpya," Luteni Michael akanena.

"Luteni, usisahau kuhusu ka-hacking nilikotoka kufanya hapa..."

Bobby akawa anamkumbusha kuhusu hilo huku tayari Luteni Michael akiwa ameanza kuondoka na wengine. Nora akamshukuru Bobby kwa kazi nzuri, kisha naye akaelekea nje kwa wengine ili kwenda walipoambiwa.

★★

Iliwachukua kama nusu saa kwa ACP Nora na wenzake kufika maeneo alikoishi Eunice Shirima kutokana na msongamano wa magari barabarani. Walipata kuwaona baadhi ya watu wa familia yake, ikiwemo mkane aliyemwacha na watoto watatu. Waliongea na mwanaume huyu ambaye aliwaeleza kwamba mke wake alikufa siku chache baada ya kujeruhiwa vibaya kwenye bomu lile, naye alizikwa kule kwao Arusha. Walimuuliza ikiwa alikwenda hospitali kumwona, na kama alimwona, lakini akasema ijapokuwa alijaribu, hakuweza kabisa kumwona mpaka alipopewa taarifa kwamba alipoteza maisha kutokana na mapafu yake kuingiwa na moshi mwingi.

Nora aliweza kugundua kwamba mwanaume huyo aliongea mambo ambayo ALIDHANI ni kweli kabisa, kwa hiyo akaamua tu kuwaambia wenzake wamwache kwa sababu kwa hapo hawangepata jambo lolote lenye nuksi, hasa kwa kuwa mkane huyu alionekana kuwa mwenye huzuni bado.

Upande wa Luteni Michael, akiwa amesindikizwa na Vedastus, Omari na Hussein, alifanikiwa kufika mpaka kwenye nyumba waliyoitambua kuwa ya Nathan Masunga. Ilikuwa kubwa kiasi yenye uzio wa kuta kuizunguka, nao wakafika getini na kugonga mlango mdogo wa geti hilo. Wakaendelea kuligonga bila kujibiwa kwa dakika mbili zaidi, ndipo likafunguliwa.

Wote wakashangaa baada ya kumwona mwanaume huyo ambaye walijua wazi ni Nathan Masunga mwenyewe. Alikuwa nzima kabisa, akisimama vizuri, bila kuonekana na kitu chochote kilichoashiria kwamba mguu wake ulikuwa umevunjika. Cha ajabu hata zaidi baada tu ya kuwaona wanajeshi hawa, mwanaume huyo akafunga mlango wa geti upesi, lakini Vedastus akawahi na kuanza kubishana naye kuusukuma ili asiufunge kwa ndani, ila Nathan akafanikiwa kuufunga.

Sasa nuksi wakawa wameipata huku.

★★★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★★★

Previoua Next