Nairobi
Ijumaa, Februari 21 - Saa 2:00 Asubuhi
Brenda Nyaki alitoka kwenye jengo la kifahari la apartments alikokuwa akiishi Westlands, na kujikuta kwenye mvua ya manyunyu ya baridi iliyokuwa inanyesha juu ya kila kitu bila ya upendeleo. Barabara zilijaa magari ya kifahari mno yakiendeshwa na madereva waliovalia sare (chauffeurs), wakielekea Kenyatta Avenue, na vilevile juu ya mitaa ya mabanda ya Mathare, ambapo nyumba zilizotelekezwa na kufungwa kwa mbao zilikusanyana kwa huzuni kupokea mashambulizi ya mzito nzito iliyokuwa inapiga jiji zima.
Mvua hiyo iliosha vumbi kwenye magari ya kifahari na kwa upande mwingine, ilifanya taka zilizorundikana mbele ya nyumba zile za mitaani kuwa tope la kusikitisha.
Brenda alikuwa njiani kuelekea kazini. Alitembea kwa mwendo wa haraka barabarani, akiwa na headset zake za Skullcandy akielekea mashariki mwa Biashara Street, alipokuwa akifanya kazi benki. Ilimbidi ajizuie kuimba kwa sauti, juu ya furaha iliyokuwa imemvaa… ilikuwa ya ajabu sana.
Alivaa koti la mvua la njano ang'avu, buti za mvua, na kofia ya mvua ambayo kwa shida iliweza kuficha nywele zake nyingi za kahawia zilizong'aa. Alikuwa katika miaka yake ya kati ya ishirini, akiwa na uso ulijaa uhai na akili, mdomo wenye lipsi pana zenye mvuto, macho yenye kung’aa ambayo yangeweza kubadilika kutoka kijani kibichi laini hadi rangi ya zumaridi kwa sekunde chache tu, na mwili wenye umbo zuri la kibantu lililokaa kimazoezi.
Ngozi yake ilibadilika kutoka nyeupe yenye mwangaza hadi waridi wa kina, kulingana na hali aliyokuwa nayo wendani hasira, uchovu au msisimko. Mama yake alikuwa amemwambia siku moja,
"Kwa kweli mwanangu, wakati mwingine nashindwa kukutambua. Una rangi zote za upepo ndani yako."
Sasa, alipokuwa akitembea mitaani, watu walimgeukia na kumtazama kwa tabasamu, wakimuonea wivu kwa furaha iliyoandikwa usoni mwake. Naye aliwapa tabasamu la kurudisha.
“Ni dhambi mtu kuwa na furaha kubwa namna hii,” Brenda alijiambia moyoni.
“Ninaolewa na mwanaume ninayempenda, na tayari nina ujauzito wake.”
“Kuna nini tena?” alijikuta akimuigizia mchekeshaji maarufu Joti kuongea na kucheka mwenyewe kama chizi
Akiwa karibu na benki, alitazama saa yake. Saa mbili na dakika ishirini. Milango ya Benki ya Uaminifu na Maendeleo ya Afrika Mashariki (East African Trust & Development Bank) haikuwa imefunguliwa kwa wafanyakazi mpaka dakika kumi baadaye, lakini Bwana Clarence Desmond, Makamu wa Rais Mwandamizi wa Idara ya Kimataifa, tayari alikuwa anaizima alarm ya usalama na kufungua milango.
Brenda alipenda kushuhudia mchakato huo wa kila asubuhi. Alisimama kwenye mvua, akisubiri, huku akimtazama Desmond akiingia benki na kufunga mlango nyuma yake.
Benki zote ulimwenguni huwa na taratibu zao za kiusalama za ndani ambazo ni ngumu kueleweka kwa watu wa kawaida, na Benki ya Uaminifu na Maendeleo ya Afrika Mashariki haikuwa tofauti. Mpangilio wa kila siku haukuwa ukibadilika kamwe, isipokuwa (security signal) ishara ya kiusalama, ndio iliyokuwa ikibadilishwa kila wiki.
Wiki hiyo, ishara ilikuwa ni Half-Lowered Venetian Blind ikimaanisha pazia lilishushwa nusu - kuashiria kwa wafanyakazi waliokuwa wakisubiri nje kwamba ukaguzi wa usalama ulikuwa unaendelea ndani ili kuhakikisha hakuna mtu yeyote mgeni aliyejificha ndani ya benki kwa nia ya kusubiri watu waingie na kuwashikilia wote mateka.
Bwana Clarence Desmond alikuwa akikagua maeneo ya vyoo, stoo ya kuhifadhi vifaa, chumba cha hazina, na sehemu ya masanduku ya amana. Na baada tu ya kujiridhisha kwamba alikuwa peke yake ndani ya benk yote, ndipo angeinua pazia juu kama ishara kuwa hali ilikuwa salama.
Mhasibu mkuu alikuwa ndiye wa kwanza kuingia kila siku. Kazi yake ya kwanza ilikuwa kusimama karibu na kitufe cha dharura cha kengele ya usalama hadi wafanyakazi wote waingie ndani, kisha afunge mlango kwa ndani.
Saa 2:30 asubuhi kamili, Brenda Nyaki aliingia kwenye jengo lenye mapambo mazuri la benki hiyo, akiwa na wafanyakazi wenzake. Alivua koti lake la mvua, kofia, na buti zake, huku akisikiliza kwa furaha ya ndani manung’uniko ya wenzake kuhusu hali mbaya ya hewa.
"Huu upepo wa kisulisuli umepeperusha na mwavuli wangu," mlalamikaji mmoja - mtunza fedha - alisema.
"Nimeloana maji mwili mzima."
"Mimi nimeona bata wawili wakielea kwenye barabara ya Moi Avenue," Mweka hazina mkuu akatania.
"Yule jamaa wa hali ya hewa amesema wiki nzima itakuwa hivi. NatBrenda ningekuwa vacation Zanzibar au Cape Town."
Brenda alitabasamu na kuelekea ofisini kwake.
Alikuwa msimamizi wa kitengo cha uhamishaji wa fedha kwa njia ya mitandao ya kimataifa (Cable Transfer Department). Hadi hivi karibuni, kuhamisha fedha kutoka benki moja hadi nyingine - iwe ndani ya nchi au nje ya mipaka - ilikuwa kazi ngumu, ya kusumbua na yenye mlolongo mrefu wa taratibu. Ilihitaji kujaza fomu nyingi kwa mkono, kupitia kwa maafisa wa benki, na kutegemea huduma za posta za kitaifa au kimataifa, ambazo zilihitaji siku kadhaa kufikisha maagizo ya malipo.
Lakini ujio wa kompyuta na maendeleo ya mitandao ya fedha ya kidijitali, kama vile SWIFT (Society for Worldwide Interbank Financial Telecommunication), CHIPS (Clearing House Interbank Payments System), na RTGS (Real-Time Gross Settlement), ulibadilisha taswira nzima ya huduma za kifedha. Mfumo wa SWIFT, kwa mfano, uliwezesha taasisi za kifedha zaidi ya 11,000 duniani kuwasiliana kwa haraka na kwa usalama kwa kutumia ujumbe wa kielektroniki unaoelekeza uhamisho wa fedha.
Kwa sasa, fedha nyingi sana zinaweza kuhamishwa kutoka akaunti moja hadi nyingine kwa sekunde chache, bila ya karatasi wala foleni. Mifumo ya blockchain na fintech platforms zimeongeza kasi zaidi ya mageuzi haya, huku zikitoa uwazi na usalama wa hali ya juu katika miamala. Katika mazingira haya mapya, jukumu la msimamizi halikuwa tu kufanikisha uhamisho, bali pia kuhakikisha miamala inaendeshwa kwa usahihi, kwa kufuata viwango vya kimataifa vya usalama na uwiano wa kifedha, ikiwa ni pamoja na udhibiti dhidi ya utakatishaji wa fedha na ufadhili wa ugaidi.
Kwa kifupi, kile kilichokuwa kazi ya siku kadhaa sasa ni suala la sekunde - dunia ya kifedha ilikuwa imeingia kwenye zama mpya za kasi, usahihi, na ufanisi wa kidijitali.
Ilikuwa ni kazi ya Brenda kutoa taarifa za uhamishaji wa usiku kucha kutoka kwenye mfumo wa kompyuta na pia kutuma uhamishaji mpya kwa benki zingine. Shughuli zote zilikuwa kwa njia ya misimbo ya siri, ambayo ilibadilishwa mara kwa mara ili kuzuia upatikanaji usioidhinishwa.
Kila siku, mamilioni ya fedha za kielektroniki zilipitia mikononi mwa Brenda. Ilikuwa kazi ya kuvutia sana - kama mishipa ya damu ya biashara ya dunia nzima. Na mpaka Brian Okello alipoingia kwenye maisha yake, benki hiyo ilikuwa ndio kitu cha kusisimua zaidi maishani mwake.
Benki yao ilikuwa na kitengo kikubwa cha kimataifa, na wakati wa chakula cha mchana, Brenda na wenzake wangeketi pamoja wakijadili matukio ya kifedha ya asubuhi hiyo. Mazungumzo yao yalikuwa ya kushangaza kweli kweli. Kwa mtu mlala hoi asingeamini hizo idadi ya fedha wanazokuwa wakizungumzia kwenye stori zao.
Deborah, mhasibu mkuu, alitangaza kwa fahari, "Tumefunga mkopo wa pamoja wa dola milioni mia moja kwa ajili ya serikali ya Ghana leo..."
Mae Trenton, katibu wa Makamu wa Rais wa benki hiyo, aliongea kwa sauti ya siri:
"Katika kikao cha bodi asubuhi hii, wamekubali kujiunga na mpango mpya wa ufadhili kwa Peru. Malipo ya awali ni zaidi ya dola milioni tano..."
Jon Creighton, mfanyakazi mwenye ubaguzi wa wazi, aliongeza kwa dharau, "Nasikia tunashiriki kwenye mpango wa kuiokoa Mexico kwa dola milioni hamsini. Hao watu hawastahili hata senti yetu moja..."
"Inafurahisha," Brenda alisema kwa tafakari, "kwamba mataifa ambayo huyakosoa Marekani kwa kupenda pesa mno, ndio huwa wa kwanza kuja kuomba mikopo."
Na hilo ndilo lililokuwa chanzo cha mabishano yao ya kwanza yeye na Brian.
Comments