EPISODE YA PILI
(Hakuna anayeishi mara mbili bila kuacha kivuli)
Siku ilipofika asubuhi, jua liliangaza kama vile halikutaka kuonekana sana. Mawingu mepesi yalikuwa kama mapambo juu ya anga la Kigoma, lakini hewa ilikuwa nzito. Najim aliamka akiwa hajalala usingizi, macho yake yakiwa na madoa ya mawazo yaliyolala juu ya paji la uso.
Aliinuka, akavaa shati la rangi ya khaki, na kuivaa ile bastola ya zamani kwa mkono wake wa kushoto — mkono aliouzoea kuutumia kwenye mapambano ya gizani.
Ramani ya “Rauta” aliibana ndani ya koti lake. Kila aliipoiangalia, alihisi kana kwamba imechorwa si kwa wino bali kwa siri nzito.
Alishuka kwenye hoteli na kuelekea kwenye mtaa wa Sengo — sehemu ya mji ambayo inaonekana haina maana yoyote, lakini kila mtaa wa mji wa zamani una tabaka lililojificha. Aliingia kwenye duka la vifaa vya kale linalomilikiwa na mzee mmoja mjusi aliyeitwa Kombe.
“Najim Kifu,” mzee huyo alisema kabla hata hajafungua mdomo.
“Unaijua ramani ya Rauta?” Najim aliuliza moja kwa moja.
Kombe hakumjibu. Badala yake aligeuka, akafungua droo ya chini ya meza yake ya mbao, akatoa mkufu wa shaba wenye jiwe la kijani katikati, na kumpatia.
“Jiwe hili litangaza mlango wa muda ukikaribia.”
Najim alilikubali kimya kimya. Mara ya mwisho alipewa kitu kama hicho, alianza operesheni iliyomalizika na vifo 39, pamoja na yeye kuingia mafichoni.
“Sasa utakwenda Mbamba Bay,” Kombe alisema, “lakini si kupitia njia ya kawaida. Utapitia chini ya Ziwa.”
Najim alihisi kama Kombe anatania, lakini alijua hakuna utani katika dunia ambayo sasa anaitembea tena.
Alipewa kifaa kidogo cha mstatili chenye rangi ya kijivu. Kombe alimwambia, “Ukishafika ziwani, rudisha mpigo wa moyo wako hadi 30 kwa dakika. Ndipo mlango wa chini ya maji utaonekana.”
Najim hakuwahi kusikia kitu kama hicho — lakini alikubaliana. Dunia aliyomo sasa haina sheria za kawaida.
---
Njia ya kwenda Mbamba Bay ilianza saa saba mchana kwa chombo cha siri cha chini ya ardhi kilichobeba abiria wawili tu: Najim, na mwanamke mmoja mrefu mwenye nywele ndefu za rangi ya udongo wa mto. Hakuwa amevaa sare yoyote, lakini macho yake yalikuwa na harufu ya kikosi.
“Hujawahi kuwa mvivu kwenye historia zako,” alisema bila kumtazama.
“Na wewe hujawahi kuniita kwa jina,” Najim alijibu.
“Mimi ni Kaja.”
“Na bado unanipima.”
“Kwa sababu najua wewe si mtu mmoja,” alisema. “Wewe ni vivuli vitatu vinavyotembea kwenye mwili mmoja.”
Najim hakujibu. Watu wachache sana walimwelewa. Wachache zaidi waliwahi kumwona akikata tamaa.
Wakiwa chini ya ziwa, kifaa alichopewa na Kombe kilianza kung’aa. Jiwe la kijani kwenye mkufu wake pia likaanza kupiga kwa mwanga wa mdundo — kama moyo.
Kaja alimsogelea, akamshika mkono, na ghafla, sehemu ya ukuta wa chombo ilifunguka kama mlango wa ajabu. Maji yaliingia, lakini hayakuwagusa. Badala yake, walivutwa kwenye mwanga wa kijivu — kama kuingia kwenye tumbo la historia yenyewe.
---
Waliamka kwenye ardhi tofauti. Ilikuwa kavu, ya dhahabu, yenye mawe yanayofanana na meno ya tembo wa zamani. Jua lilikuwa linasimama angani bila kuzunguka.
“Ndio Rauta hii,” Kaja alisema.
“Hakuna watu?”
“Wapo, lakini si kama tunavyowajua.”
Walitembea kwenye njia ya matofali ya rangi ya bluu, hadi walipofika kwenye jumba la mviringo — lile lile kwenye ramani. Juu ya mlango wake palikuwa na alama ya ajabu: mduara uliofungwa na mistari mitano, kila mstari ukiwa na rangi tofauti.
Najim alipogusa lango, milango ilijifungua kwa sauti ya mpigo wa moyo. Ndani kulikuwa na ukumbi mkubwa wa miale ya mwanga wa kale. Mbele, kulikuwa na viti vitano, kila kimoja kikiwa na picha ya mtu.
“Mmoja kati yao alikusaliti miaka 12 iliyopita,” Kaja alisema, sauti yake ikiwa ya chini kama siri.
Najim alimuangalia, lakini kabla hajazungumza, picha moja ikabadilika — sura ya mtu aliyejulikana kama General Wayota, mkuu wa zamani wa ujasusi wa Bara la Nooma.
“Wayota alikufa,” Najim alisema.
“Hakufa,” Kaja alijibu. “Alihamishiwa kwenye mfumo wa majira.”
Najim alipumua kwa nguvu. “Hii dunia inazidi kuwa ndoto ya usingizi mbaya.”
“Karibu kwenye vita ya mwisho, Najim,” Kaja alisema. “Mwisho wa dunia hauanzi kwa mabomu. Unaweza usikie kelele yake kabisa.”
Comments