Reader Settings

EPISODE YA TATU

Ukumbi mkubwa wa jumba la mviringo uligeuka kimya zaidi ya kaburi. Najim alisimama katikati, akihisi joto lisilo la kawaida kwenye mgongo wake, joto ambalo halikutoka na jua bali kutoka ndani ya mwili wake mwenyewe. Mwili wake ulianza kuitikia mazingira kama vile ulikuwa unakumbuka mahali palipojificha kwenye kumbukumbu ya damu.

Mikono yake ilielea kidogo, kana kwamba kitu kilikuwa kinavuta mishipa yake. Kaja hakusema kitu. Alikuwa amesimama pembeni yake, macho yake yakiwa makavu kama almasi ya barafu.

Kwenye ukuta wa mbele wa ukumbi, kioo kirefu kilianza kuangaza. Kilionesha sura ya mtu aliyevaa mavazi meusi ya kijeshi, kofia ikiwa imepindika upande wa kushoto na alama ya msalaba uliochomwa nusu ikiwa kwenye bega lake. Hakuwa mwingine bali ni General Wayota.

“Najim Kifu…” sauti ilisikika kama mvua inayoanguka kwenye dari la chuma, nzito, ya mbali lakini inayopenya. “Niliwahi kukuamini. Sasa naomba unielewe.”

Najim hakujibu. Alikumbuka siku alipokabidhiwa faili la mwisho kutoka kwa Wayota, miaka kumi na mbili iliyopita. Faili lililoitwa: Kilio Kisicho na Mwili. Ndani ya faili hilo kulikuwa na picha ya msichana mdogo aliyeokotwa kwenye moto wa kijiji kilichofutwa kabisa kwenye ramani — msichana aliyekuwa na jicho moja la kawaida na jingine la rangi ya fedha.

Msichana huyo alikuwa anaonekana kwenye kioo pia, nyuma ya Wayota. Alikuwa mkubwa sasa. Mrefu, mwembamba, na macho yake ya fedha yalikuwa yanang’aa kama taa za taa zisizo na umeme.

“Anaitwa Imeli,” Wayota alisema. “Na ndiye atakayefungua Kidonda cha Tano.”

Najim alihisi mgongo wake ukichoma. Siyo kwa woga, bali kwa hisia ya tukio kubwa linalokaribia. Alikuwa amezoea operesheni za kusisimua. Aliwahi kuingia kwenye maktaba ya siri ya anga ya pili, alifuta kumbukumbu za taifa bandia, na aliwahi kumuokoa mtoto wa Rais wa nchi ambayo haikuwepo tena. Lakini hiki... hiki kilihisi kama ndoto ambayo haikuweza kuamka nayo.

Kaja alisogea karibu, akamgusa Najim kwenye bega.

“Tutahitaji kumtoa Imeli. Lakini si kwa vita. Kwa neno.”

“Hawezi kusikiliza neno la binadamu. Amekulia ndani ya mfumo wa sauti bandia.”

“Kwa hiyo tutazungumza kwa historia.”

Najim alitazama nyuma, akatoka ndani ya jumba. Hakusema neno. Kila kitu kilikuwa kinaingia kichwani kama muziki wa taratibu lakini unaobeba huzuni ya milima iliyoanguka.

Walirudi kwenye sehemu ya nje ya Rauta. Dunia pale haikuwa na upepo, wala harufu. Ilikuwa kama kuchora anga kwa wino wa kimya. Kila upande ulikuwa hauna muda.

Kaja alimpa kifaa kidogo kama saa, kilichoonyesha namba tano tu zinazobadilika taratibu.

“Hiki si kipimo cha muda,” alisema. “Ni kipimo cha uwongo.”

Najim alikiangalia, namba zilikuwa zinaonyesha 00047. “Na zikifika sifuri?”

“Dunia inasahau.”

Aliweka kifaa hicho mfukoni. Walitembea hadi kwenye njia ya mviringo iliyokuwa inaelekea kwenye bonde lenye mwanga wa kijani kibichi. Njiani walimkuta mlinzi wa ajabu — mtu mrefu mwenye ngozi ya shaba na macho mekundu. Hakuzungumza. Alinyosha mkono na kuonesha pembe ya jiwe.

“Unachotafuta kimefichwa kwenye kiumbe aliyejificha kwenye jina la mto,” alisema kwa sauti ambayo haikutoka kwenye kinywa, bali kwenye mwili wote.

Najim alihisi baridi ya ajabu kwenye uti wa mgongo wake. Aligeuka kumtazama Kaja.

“Mto?”

“Unajua ni mto gani?”

“Hapana.”

“Unajua jina lako lina maana nyingi?”

Najim hakujibu. Kaja alitabasamu kwa huzuni.

“Kifu si jina la ukoo tu. Ni sehemu ya neno la kale: ‘Kifurushwa’ — aliyetumwa lakini hatorudi.”

Walishuka kwenye bonde. Njiani, Najim alianza kusikia sauti ndogo. Sauti ambayo ilikuwa ndani ya mwili wake. Ilikuwa ni sauti ya mwanamke — aliyemwambia miaka saba iliyopita:

> “Ukirudi Kigoma, usiseme jina langu. Ukiniita, nitarudi kwa njia ambayo hutaitaka.”

Sauti ya Layna. Mpenzi wake wa zamani — aliyejificha kwenye kivuli cha dunia ya ujasusi. Alikuwa amepotea kwenye operesheni ya Ethiopia, lakini mwili wake haukuwahi kupatikana.

Najim alisimama. Moyo wake ulikuwa unamwambia kitu kimoja:

Layna hajaenda. Layna ni sehemu ya Kidonda cha Tano.

Aliweka mkono kwenye kifua chake. Mkufu wa shaba uliyopigwa na mwanga wa kijani ulianza kuwa mzito. Mwanga wake ulianza kuvutia viumbe wadogo waliotokea ardhini — wakiwa na sura za nusu-binadamu, nusu-ndoto.

Kaja alichomoa bastola, lakini Najim alimshika mkono.

“Hawatatupiga. Wametumwa kutupeleka.”

Waliongozwa kuelekea kwenye mlima mfupi wenye mlango wa shimo, ulioandikwa maneno:

> “Hapa ndipo historia hupumzika kabla haijawindwa.”

Walipoingia, joto lilipanda ghafla. Ndani ya mlango, walikuta jumba la kale lenye vitabu vilivyoandikwa kwa lugha ambazo hazijawahi kusomwa duniani. Na katikati, kwenye kiti cha dhahabu, alikuwa ameketi Layna.

Macho yake yalikuwa yamejaa maumivu ya karne, lakini tabasamu lake lilikuwa kama la mwanamke aliyewahi kumpenda kwa kweli.

“Nilikwambia, usinitaje.”

Najim alitaka kusema kitu, lakini ulimi wake haukumsikiliza.

Layna alinyanyuka taratibu. “Imeli si mtoto wa kawaida. Imeli ni mlango. Niliyeamua asifunguliwe.”

Kaja alisogea hatua moja mbele. “Lakini Wayota ameshafungua.”

Layna alicheka kwa sauti ya kimya. “Basi hamna muda. Dunia inaanza kusahau. Na mimi... nitakumbuka hadi mwisho.”

Najim alihisi dunia ikizunguka. Mlango uliofunguka haukuwa wa kutoka — bali wa kurudi. Na hakujua kama kurudi huko ni kwake, au kwa dunia nzima.

Previoua Next