Reader Settings

Chanzo ni Yeye
Sehemu ya 16
Na. Machokulenga TZ
0623238283

Ayubu alikuwa amefika mahali pa mwisho kwenye ramani ya karatasi aliyokabidhiwa na Rhoda. Mbele yake palikuwa na mto mkubwa wa maji baridi unaopita katikati ya msitu wa Lulanzi, kilomita chache kutoka Dodoma mjini. Mto huo haukuonyeshwa kwenye ramani za kawaida. Na mbele yake kulikuwa na daraja la ajabu—si la mbao, si la chuma—bali daraja lililojengwa kwa mfumo wa nishati ya sumaku.

Aliweka mguu wake wa kwanza juu ya daraja, akahisi mwili wake kama unakokotwa na nguvu isiyoonekana. Hakukuwa na sauti. Hakukuwa na mtetemeko. Ni kana kwamba daraja hilo lilimtambua, na kumpa ruhusa ya kupita. Alipofika katikati ya daraja, mfumo wa taa ndogo ndogo ulianza kuangaza njia yake. Kila hatua aliyokuwa anapiga, taa zilijizima nyuma yake. Hapakuwa na njia ya kurudi nyuma.

Baada ya kuvuka, alijikuta mbele ya mlango wa glasi, uliokuwa ukiongozwa na alama ya kidole gumba. Bila kuelezwa chochote, aliweka kidole chake—mlango ukafunguka. Ndani, alikuta chumba chenye ukubwa wa uwanja wa mpira, kikiwa kimetulia kimya, na taa za buluu zikimulika kwa mpangilio wa mduara. Katikati ya chumba hicho, kulikuwa na mashine kubwa ya sura ya duara, ikiwa na viti vinane kuizunguka.

Mara taa zilitimia mwanga mkali. Mtu mmoja aliingia kutoka upande mwingine wa chumba—alikuwa Dkt. Rhoda. Hakuwa tena na uso wa upole, alikuwa na uso wa amri na mamlaka.

"Karibu kwenye Chanzo cha Chanzo," alisema.

"Kuna vingine tena?" Ayubu aliuliza.

"Ndiyo, hii ndiyo msingi wa kila kitu. Pale ulipokuwa, ilikuwa ni maabara ya mafunzo. Hapa ndipo fahamu zako zilizaliwa."

"Nataka majibu sasa. Nani mimi? Na kwanini maisha yangu yote nimeishi katika giza la kutokujua?"

Dkt. Rhoda alimsogelea, akaweka mkono wake juu ya kifaa kimojawapo. Skrini kubwa ilionyesha picha ya maabara ya zamani, watoto wakiwa wamelala kwenye chumba kilichojaa gesi hafifu, huku mashine zikiendelea kuchanganua miili yao.

"Ulizaliwa kama sehemu ya kundi la majaribio la kwanza: Ayubu-001 hadi Ayubu-010. Wewe ndiye pekee uliyebaki hai. Wengine walikufa au waligeuka na kuwa mawakala wa giza. Maisha yako yamepangwa tangu siku ulipozaliwa. Barua ile uliyokuta mtaani ukiwa na miaka saba—tuliiweka sisi. Mwalimu uliyemfundisha kutumia kompyuta—tulimtuma sisi. Kila hatu yako ilikuwa imeandikwa kwenye programu."

"Na Nashiri?" Ayubu aliuliza.

"Alikuwa mlinzi wako. Lakini alipojaribu kukugeuza kuwa kama yeye, aliondoa maadili ya msingi ya mradi. Tulimvua mamlaka, lakini alitoroka."

Ayubu alikaa kwenye moja ya viti vile vinane. Akasema kwa sauti ya kujiamini, "Na sasa nini?"

Dkt. Rhoda akatabasamu kwa mara ya kwanza, kisha akamkabidhi kifaa kidogo kama diski.

"Sasa ni zamu yako kuamua. Diski hii ina mpango wa mwisho wa mradi. Iwapo utaichomeka kwenye mfumo mkuu, basi dunia nzima itaweza kufunguliwa kutoka kifungo cha akili kinachowashikilia. Lakini ukiamua kuondoka nayo, utasababisha mfumo kuendelea kuwepo—na maelfu ya wengine kama wewe wataumbwa."

Ayubu alitazama diski ile. Fikra nyingi zilimkimbia. Alikumbuka uso wa yule mama aliyempa chakula akiwa mdogo mtaani, alikumbuka kicheko cha rafiki yake aliyepotea siku ya mvua, alikumbuka kila hatua aliyopitia bila kujua sababu. Alikuwa amechoka kuishi maisha ya majaribio.

Aliinuka. Akatembea hadi kwenye mfumo mkuu—kishindo la hatua zake likiambatana na kimya kizito cha mashine zinazotazama. Aliweka diski. Skrini ikaangaza:

"Je, unathibitisha kuanzisha Programu ya Uhuru? Ndiyo / Hapana"

Ayubu akabonyeza: Ndiyo.

Mara taa zote zikalipuka mwanga mweupe. Mifumo yote ya kielektroniki ikaanza kufanya kazi, mashine zikaanza kubadilika kuwa sehemu za kutunza kumbukumbu huru, na taarifa zikaanza kusambazwa kwa satelaiti za kimataifa.

Dkt. Rhoda alishindwa kuzuia machozi yake.

"Umechagua kile ambacho hata sisi hatukuwahi kufikiria. Umevunja mnyororo."

Ayubu aligeuka na kusema, "Chanzo kilikuwa ndani yangu. Sasa ni wakati wa wengine kuamka."

Mlango wa nyuma wa chumba ulifunguka. Mwanga wa asubuhi ukaingia, ukiangaza uso wa Ayubu kwa mara ya kwanza akiwa huru kabisa. Na safari mpya ya dunia ilianza...

Lakini je, wale waliokuwa upande wa giza, watakubali kushindwa hivyo tu?
Endelea sehemu inayofuata...

Previoua Next