Reader Settings

FOR YOU 2

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA KUMI NA NNE

★★★★★★★★★★★★★★★★★


Nora alifikishwa hospitalini haraka sana kupatiwa huduma za kitiba. Alivaa suruali yake wakati wakiwa mwendoni, hivyo kufikia sasa hakuwa ameachwa mtupu kwa chini. Matabibu walimsaidia, na baada ya muda fulani daktari akamjulisha Luteni Michael kwamba Nora angekuwa sawa tu kwa kuwa walifanikiwa kuzuia damu isivujie ndani ya tumbo lake na kumpa dawa ambazo zingetuliza maumivu ya kichwa chake. Luteni Michael akaomba kumwona ili waongee, lakini daktari akamwambia kuwa kwa wakati huo Nora alikuwa amekwishalala, hivyo ingempasa asubiri mpaka kesho ili kuongea naye.

Baada ya daktari kuwaacha, Mario akamwambia Luteni Michael kwamba aliwasiliana na Bobby kutokea kule walipomwacha na Alex, naye alikuwa amesema miili ile ya wanaume waliouawa jengoni pale iliondolewa hatimaye. Luteni Michael akamwambia Mario amwambie Bobby ahakikishe kwamba watu wa vyombo vya habari hawahusishwi na tukio hilo kwa sababu hakutaka gumzo mapema sana wakati tu walikuwa wametoka kwenye msiba. Kama ni taarifa ambayo maaskari walipaswa kutangaza ilikuwa ni vifo vya wanaume hao, na lawama waielekeze kwa Mess Makers kama kawaida yao, lakini masuala ya ACP Nora kutekwa hakutaka yasambazwe kokote.

Luteni Michael alijua vizuri kivumbi ambacho kingetokea endapo Jenerali Jacob angesikia kuwa binti yake aliwekwa hatarini, kwa kuwa Michael aliahidi kumlinda akiwa chini ya uongozi wa Kanali Oswald pia. Lakini ukweli wa jambo hilo haungeweza kufichwa kwa Jenerali Jacob kama walivyolenga, kwa sababu alizipata taarifa hizo kutoka kwa Luteni Jenerali Weisiko, ambaye pia alikuwa amezipata kutoka kwa "silaha" wake yule aliyeona kila kitu kilichotokea akiwa juu ya mnara.

Luteni Michael akawaambia Mario na Hussein wabaki hapo hospitalini ili kumpa ulinzi Nora mpaka atakapoamka, naye angeondoka kwenda kufanya uchunguzi wa kina pamoja na Bobby. Wanaume hao wakatii na kubaki hapo, wakimsindikiza Luteni kwa macho alipoondoka hospitalini.


★★★


Asubuhi iliyofuata, tayari vyombo kadhaa vya habari vilikuwa vimeshatangaza kuhusu tukio la usiku uliopita kwenye habari muhimu za asubuhi. Kwa sababu hakukuwa na mashuhuda wengine wa tukio, suala hilo lilielezewa na mapolisi tu, waliosema kwamba wanaume hao saba walikuwa ni wajenzi wa jengo hilo wenye familia bila shaka, lakini Mess Makers wakawaua bila sababu yoyote kwa kutaka jambo fulani kutoka kwenye jengo hilo. Ukweli ukafichwa kuhusiana na ACP Nora kutekwa na kukaribia kuuawa.

Nora akaamka hatimaye asubuhi hii kwenye mida ya saa 3, naye akatambua kuwa bado alikuwa kwenye kitanda cha hospitali. Alikuwa kwenye chumba cha peke yake, naye akageuza shingo yake upande mwingine na kumwona Mario akiwa ameketi kwenye kiti huku ameinamisha kichwa chake, na mikono kuikunjia kifuani. Alipomtazama vizuri, akatambua alikuwa amesinzia, mara kwa mara kichwa chake kikikaribia kudondokea mbele. Akamwonea huruma kiasi kwa sababu alijua hakulala usiku mzima na hivyo bila shaka alikuwa amechoka. Alipojishika kichwani, alitambua kuna plasta kubwa iliyogundishwa pembezoni mwa paji la uso wake, naye akaanza kutafakari mambo yote yaliyotokea usiku wa jana.

Picha kamili ya mauaji ya wanaume wale ilimrudia. Kihalisi, aliwaza kwamba hata yeye angewaua watu hao kwa mambo waliyotaka kumfanyia, lakini hakuwaza kamwe kwamba kuna mtu ambaye angewaua kwa njia ile iliyomwogopesha sana. Lakini tena mtu huyo alikuwa ni mmoja wa Mess Makers. Swali kuu kichwani kwake lilikuwa ni nini kilichomfanya mtu huyo amsaidie wakati yeye Nora ni sehemu kubwa kwenye mipango ya kutaka kulikamata kundi lao na kuliangamiza. Alipatwa na hisia fulani isiyoeleweka kila mara alipokumbukia jinsi mtu huyo alivyomtolea kitambaa mdomoni na kumrushia suruali ili avae; alikuwa anataka kuthibitisha nini? Kwamba Mess Makers si watu wabaya? Haikuingia akilini hata kidogo.

Alipohisi haja ndogo, Nora akajinyanyua taratibu na kuketi. Alihisi maumivu ya kichwa kwa mbali, naye akatambua kwamba alifungwa kwa bendeji tumboni. Nguo aliyokuwa amevalishwa kwa sasa ilikuwa "gauni ya mgonjwa," naye akashuka kutoka kitandani na kujaribu kusimama chini, lakini kizunguzungu kikamwangushia kitandani tena. Akachekea kwa chini kidogo, kisha akajitahidi kukikaza kichwa ili kizunguzungu kisimvae tena, lakini ni hapa ndiyo Mario akashtuka kutoka kwenye usingizi wake wa kuonja.

"ACP... unafanya nini, hutakiwi...."

Mario akasema hivyo na kwenda kumshika alipokuwa anajitahidi kusimama.

"Hutakiwi kutoka kitandani ACP..."

"Mario, sijikojoleagi kitandani. Nisaidie nielekee toilet," Nora akasema.

Mario akatii na kumpa egamio ili waelekee kwa choo, akimuuliza kama anahisi maumivu mengi, lakini Nora akakanusha. Akafanikiwa kumpeleka kupata haja ndogo, kisha akamrudisha tena kwenye chumba chake na kumwacha ili akamwambie daktari kwamba mgonjwa wake kaamka.

Nora alipouliza wengine walikuwa wapi baada ya Mario kurudi, akamwambia walikuwa wakiendelea na kazi, na ni yeye pamoja na Hussein ndiyo walioachwa kumlinda, lakini Hussein alitoka kidogo kwenda kufata vyakula kwa ajili yake. Daktari akafika kumwangalia Nora, naye akasema angehitaji kuendelea kuwa hospitalini hapo kwa siku mbili zaidi, lakini Nora akakataa. Akasisitiza kwamba alitakiwa kurudi kufanya kazi kwa sababu hakujisikia kuwa mgonjwa kama daktari alivyosema alihitaji uangalizi.

Daktari akamwambia kwamba akiondoka kabla ya wakati huenda akaisababishia afya yake madhara, lakini Nora akasema kama ni hivyo wampe tu dawa za kwenda nazo hata kama atazitumia mwaka mzima, lakini hangekaa hospitali kwa siku mbili zaidi. Mario naye akajaribu kumsisitiza asikilize ushauri wa daktari, lakini Nora akagoma. Ni hapa ndipo Hussein akaingia humo, huku nyuma akifuatwa na Luteni Michael.

Daktari akawaeleza hali, naye Luteni Michael akamshukuru na kumwomba aende tu ili aongee na mgonjwa.

"Jamani, acha kuniita mgonjwa, naonekana kama naumwa?" Nora akamwambia Luteni Michael wakati daktari alipoanza kuondoka.

"ACP... unatakiwa kumsikiliza daktari. Kama afya yako hairuhusu kuondo...."

"Luteni niko sawa. Hayo ni maneno ya doctor tu lakini najua niko sawa. Kichwa kitapona, ni pain killer tu, na hakuna shida tena. Siwezi kukaa me hapa kwa siku mbili zaidi nimebung'aa tu," Nora akasema kwa uhakika.

"Kubung'aa ndiyo nini?" Mario akauliza.

"Kukodoa macho. Angalia kwenye dictionary utalikuta hilo neno," Hussein akamtania.

"ACP... nimeshapoteza watu muhimu kwenye suala hili, na wewe ni muhimu zaidi. Sitahatarisha uzima wako...."

"Hauhatarishi chochote Luteni. Huu ni mwili wangu. Please, please, niondoeni kwenye hii sehemu. Tafadhali," Nora akasema.

"Haupendi hospitali eh?" Hussein akamuuliza.

"Sitaki tu kukaa hapa," Nora akajibu.

"Okay. Basi tutaongea na madaktari wakuachie mapema, lakini tunahitaji kuhakikisha uko vizuri sana," Luteni Michael akasema.

"Niko vizuri Luteni, na nikitoka hapa nataka tuendelee na kazi," Nora akasema.

Luteni Michael akaangaliana na vijana wake tu, kwa kuwa ilionekana hakukuwa na cha kumzuia Nora kufanya alichotaka. Hussein akaanza kufungua vyakula mbalimbali na kuweka chai pia ili ampatie ale.

"Tunaweza kuongelea kuhusu ni nini kilitokea jana usiku?" Luteni Michael akamuuliza.

"Yah. Aam... nilikuacha pale muda ule...."

"Yeah nakumbuka..." Luteni Michael akamalizia kimkato.

"Nilipofika tu... nje ya geti... akaja mwanaume mmoja... mmoja wao hapo kabla sijajua ni nani, na... alikuwa anaomba nishushe kioo kama anataka msaada. Nilipomsikiliza akaniambia kwamba kuna mtoto wa rafiki yake anapigwa vibaya nyumbani siyo mbali na hapo... kwamba alijua mi ni askari halafu.... Nikashuka ili nianze kumfata, ndiyo hapo hapo gari likaja mbele yetu kwa kasi. Sikujua kilichoendelea tena ghafla yaani...."

"Nafikiri kulikuwa na mwingine aliyekuja nyuma yako akakupiga kichwani," Luteni Michael akasema.

"Ndiyo, inawezekana. Niliamkia jengoni kule. Walikuwa wanataka kunibaka, kisha waniue. Lakini..." Nora akaishia hapo tu na kuonekana anatafakari jambo fulani.

"Nini kikafuata?" Luteni Michael akauliza.

"Kuna mtu aliingia... akaanza kupigana nao," Nora akasema.

"Nani?" akauliza Hussein.

"Sifahamu. Sikuweza kuuona uso wake," Nora akajibu.

"Kwa hiyo... alifika tu paap... akapigana nao na kuwaua wale wote saba? Yeye mwenyewe?" akauliza Hussein.

"Alionekanaje? Alikuwa mwanaume au mwanamke? Alivaa vipi? Na alipigana nao vipi?" Luteni Michael akauliza.

"Kila kitu kilitokea haraka sana na... kulikuwa na giza kwa hiyo... sikuona mambo mengi vizuri," Nora akadanganya.

"Atakuwa nani sasa? Jamaa amewaua vibaya sana wale wachizi... tena yaani kama vile siyo mtu wa nchi hii. Au labda ni yule aliyemuua Oscar?" akauliza Mario.

"Labda ni Super Mario," akasema Hussein kiutani.

"Hivi we' hauwezi kuacha kuniandama? Unanionaga kama sijaenda shule eti?" Mario akamwambia Hussein.

Wawili hawa wakaanza kubishana kama kawaida yao. Luteni Michael akawa anamwangalia tu Nora kiudadisi, akihisi kwamba kuna jambo alificha.

"Hussein hiyo chai itapoa. Em' mpe dada basi," akasema Mario.

"Mario, Hussein, naombeni mtupishe mara moja," Luteni Michael akawaambia.

Wawili hao wakatoka ndani ya chumba hicho baada ya Hussein kumsogezea Nora kiamsha kinywa karibu.

"ACP... nini kilitokea? Niambie tafadhali. Nahisi ni kama hausemi kila kitu," Luteni Michael akamsemesha.

"Nimekwambia kila kitu... ingawa ni kifupi lakini, ndiyo mambo yalivyokuwa," Nora akasema.

"Kwa hiyo, ni kama hatuna jambo lingine la kutoa kutokana na haya yote? Umetekwa jana ACP.... hatuwezi kubung'aa kama unavyosema, ni lazima tujue kila kitu ili tuyamalize matatizo haya haraka. Ikiwa utaficha jambo fulani haitasaidia... na kiukweli ni kama tumepoteza mwelekeo ACP. Usifiche lolote. Sisi ni timu. Sema kila kitu tusaidiane," Luteni akamwomba.

"Unataka kusikia nini? Kwamba niliuona uso wake? Sikuuona Luteni... aaghh..." Nora akasema kimkazo na kufanya kichwa chake kiume.

"Okay, okay, basi inatosha, usi... usijiumize. Samahani," Luteni Michael akamwambia kwa kujali.

"Nahisi njaa Luteni. Wacha nile kwanza, then nikitoka tutajadili mambo kwa kina. Sawa?" Nora akaomba.

"Okay. Haina shida. Sisi tutakuwa hapo nje. Pata chai kwanza," Luteni akasema.

Luteni Michael akamwangalia kwa sekunde kadhaa, kisha akatoka ndani ya chumba hicho pia. Nora akashusha pumzi na kufumba macho yake, naye akaegamia tu mto na kuanza kutafakari vitu tena. Lakini akaamua kutokazika sana kimawazo, na njia nzuri ya kurejesha nguvu ili awahi kuondoka ingekuwa ni kula, hivyo akavuta chakula alichowekewa na kuanza kula taratibu.


★★★


Lexi alikuwa ameshaondoka Dar es Salaam na kwenda mpaka kule kwenye nyumba yao ya maficho, kule walikopaita "chini." Alifika na kwenda mpaka kwa Kendrick Jabari, ambaye alikuwa ameketi tu kwenye kiti chake huku akivuta sigara, na pembeni alikuwepo LaKeisha, Mensah, Victor, na Kevin.

"Lexi!"

LaKeisha akaita kwa shauku baada ya kumwona, lakini Lexi akafika tu hapo na moja kwa moja kumfata Kendrick, kisha akaikwapua sigara yake na kuirusha pembeni kwa hasira. Wengine wakawa wanamwangalia kimaswali sana wasielewe nini kilikuwa kinaendelea mpaka Lexi amzingue "boss" wao kiaina, lakini Kendrick akawa anaangalia tu chini kiutilivu.

"Lexi... nini unafanya?" Mensah akauliza.

"Saba? Really uncle? Ni akili mbovu kiasi gani iliyokufanya ufikie uamuzi huo?" Lexi akamuuliza Kendrick kwa hasira.

Wengine wakawa hawaelewi alichomaanisha na kubaki kuangaliana tu.

"Lexi... nini sweety? Nini... kinaendelea?" LaKeisha akauliza.

Lexi akabaki tu kumtazama Kendrick. Mwanaume huyu akashusha pumzi na kumtazama usoni "binti yake," naye aliona hasira tupu tu machoni mwake.

"Ulijuaje?" Kendrick akauliza kiutulivu.

"Nina njia zangu," Lexi akasema.

Kendrick akatikisa kichwa na kusema, "Ni Torres."

"Uncle, what you did was wrong. Hivyo siyo tunavyo-roll," Lexi akasema.

"Ku-roll kivipi?" Kendrick akauliza.

"Unawezaje kuagiza wanaume saba wamkamate mwanamke defenseless, wam...."

"Na wewe unawezaje kuingilia mipango yangu? Nani amekuruhusu?" Kendrick akamuuliza kiukali.

Wengine wote wakabaki kushangaa.

"Sikuhitaji ruhusa ya mtu yeyote kufanya jambo lililo sahihi," Lexi akasema kiukali.

"Sahihi? Kuwaua wanaume saba ni sahihi?" Kendrick akauliza na kusimama.

"Boss, Lexi... what's going on?" Mensah akauliza

"Ni ndoto gani ya kitandani iliyokufanya ukaingilia mipango yangu, huh?" Kendrick akauliza kwa hasira.

"Kama kumbaka mwanamke asiye na hatia na kumuua...."

"Asiye na hatia? Asiye na hatia? Huyo mwanamke ndiyo sababu hatuna Oscar tena hapa. Umewaua watu ambao wangelimaliza tatizo hili ili iweje? Aje kufanya tusiwe na Keisha, au Mensah, au Victor hapa tena? Eeh? Una matatizo gani?"

"Siyo yeye aliyemuua Oscar..."

"I DON'T CARE!"

"I DO! Why? Kwa sababu sisi hatutakiwi kuwa kama wao. Fanya mambo namna hiyo unakuwa hauna utofauti na Jacob wala Weisiko!" Lexi akasema kwa hasira.

"Unasemaje?" Kendrick akauliza kiukali na kuanza kumfata Lexi.

"Boss, boss, boss, boss, boss...." Mensah na Victor wakamwahi ili asimfanyie jambo baya Lexi.

"Mwacheni," Lexi akasema.

Mensah na Victor walikuwa katikati yao kumzuia Kendrick kumfata Lexi.

"Nimesema mpisheni!" Lexi akawaamuru.

Mensah akapisha taratibu, naye Victor akasogea pembeni pia. LaKeisha alikuwa ameingiwa na hofu, huku Kevin akiwaangalia kwa umakini tu.

"Njoo," Lexi akamwita Kendrick.

Kendrick akabaki amesimama tu, akitambua kwamba alikuwa ameziruhusu hasira zake zimwongoze vibaya na kutishia kumpiga Lexi.

"Fanya chochote unachotaka juu yangu, lakini kamwe usiumize watu wasio na hatia. Yote tunayofanya, tunayafanya tukiwa na lengo moja... la pamoja, lakini hili ulilofanya lilikuwa ni tendo lenye ubinafsi... wala siyo kwa ajili ya Oscar. Ninajua ulifanya hivyo ili kumkomoa Jacob kwa sababu Nora ni mwanaye. Naomba ujue hili uncle. Ukitenda kwa unyama kwa mtu asiye na hatia kwa sababu tu ya kibinafsi, basi mimi siwezi kukufuata tena..." Lexi akasema kwa hisia.

"Lexi!" akawa amefika Torres hapo na kuita hivyo.

"Torres, what the fuck is going on?" akauliza Mensah.

"Boss, Lexi, tafadhali... tukae chini tusuluhishe mambo kama familia. Tusiwe na conflict over jambo hili kwa sababu... look... najua in perspective, boss tunaweza ku-differ... na...."

Torres akaendelea kuongea kwa njia ya kutafuta suluhu, naye Kendrick akawa tu anamwangalia Lexi kwa hisia akitafakari maneno yake. Lexi pia alikuwa anamtazama kwa hisia, kisha kabla hata ya Torres kumaliza kuongea, Lexi akaondoka sehemu hiyo haraka sana. LaKeisha akamfata upesi ili kujua tatizo lilikuwa ni nini, naye Kendrick akawaambia wengine wampishe kwa sababu alitaka kuwa mwenyewe.

Baada ya wote kuondoka sehemu hiyo, Kendrick akaketi na kubaki anamfikiria sana Lexi. Hakupenda hata kidogo kumwona akiudhika hasa kwa sababu alimpenda kama mwanaye wa kumzaa, lakini kwa upande mwingine alikuwa amekasirishwa sana na uamuzi wake wa kuingilia mpango wake wa kuwatuma watu wale ili wamfedheheshe mtoto wa adui yake. Kitendo alichofanya Lexi kilikuwa kimeikorofisha sana nafsi yake, na hii ikaanza kujijenga kuwa sababu kubwa ya mgogoro kati ya wawili hawa.

Ijapokuwa LaKeisha alijaribu kumzuia Lexi asiondoke na amwambie kila kitu kilichotokea, Lexi alikuwa amefadhaika sana na kutoweza kuongea lolote lile. Akamwambia tu LaKeisha alihitaji kuondoka na kurudi Dar, lakini akamhakikishia kuwa bado alikuwa pamoja naye. Baada ya Lexi kutembea, ikabidi LaKeisha na wengine wakae na Torres ili awaelezee yaliyokuwa yametoka kutendeka.

Torres aliwaweka wazi sasa kuwa alijua kuhusu mpango wa kisiri wa Kendrick wa kuagiza watu wale saba wamteke ACP Nora ili wamtendee vibaya kimwili, kisha waache ujumbe kwenye mwili wake ulioelekezwa kwa Jenerali Jacob ili kumuumiza kihisia; kama kumkomoa. Aliwaambia kwamba Kendrick alimtumia yeye (Torres) kuwalipa wanaume hao kwa njia isiyo ya moja kwa moja (yaani bila kujua wanalipwa na nani) ili wafanye kazi hiyo, kisha wangeongezewa pesa zaidi kazi hiyo ikikamilika. Wanaume wale saba walikuwa watu wabaya ambao walijikusanyia pesa kwa kutenda mambo maovu, hivyo kwa msaada wa Torres, Kendrick ndiyo alifanikiwa kuwapata na kuwaongoza kisiri kufanya jambo hilo.

Lakini baadaye Torres aliongea na Lexi kumjulisha alichofanya Kendrick, na ndiyo Lexi akaamua kwenda kumsaidia Nora. Torres akaweka wazi kuwa alimwambia Lexi kama kumfahamisha tu, siyo kwamba alitegemea angefanya jambo alilofanya. Sasa Torres akawa hana uhakika kama "boss" wao huyo angeendelea kumtumaini kwa sababu ilionekana alifanya usaliti kwake, lakini kihalisi ni dhamiri yake tu ndiyo iliyomsumbua kutokana na kitendo hicho cha boss wao kuwa kibaya sana.

Kevin, Victor na Mensah wakamwambia Torres angetulia tu na kutomwambia Lexi kwa sababu hawakuona faida yoyote ya kumsaidia mwanamke yule, lakini LaKeisha akawarekebisha kwa kusema jambo aliloagiza boss wao halikuwa jambo zuri kiukweli. Vipi kama ingekuwa ni dada zao, au mtoto wa kike wa Victor? Akashauri tu kuyaweka hayo pembeni kwanza ili wajaribu kusaidia kuweka mambo sawa baina ya Lexi na boss mkubwa. Wawili hao ndiyo waliokuwa nguvu kuu ya timu hii, hivyo kama wangetofautiana namna hii kwa muda mrefu basi mambo mengi yangeharibika.

Vijana hawa wakatawanyika baada ya mazungumzo yao mazito kuelekea suala hilo. Lakini hawakujua kuwa ni Kevin ndiye aliyempa Kendrick wazo lile la kuwaajiri wanaume wale saba ili wamfanyie Nora ukatili ule. Jamaa alikuwa ameongea na Kendrick na kumpa ushauri huo tokea wakati ule alipoona ni kama Lexi hajui jinsi ya kufanya mambo vizuri, naye Kendrick aliona kweli ingekuwa sahihi kufanya hivyo bila Lexi kujua ili amwondoe Nora, aliyemwona kama kisababishi cha kifo cha Oscar. Kwa hiyo hapa Kevin alikuwa akiigiza kama vile mambo haya yote ni mapya kwake, kumbe ni yeye ndiye aliyesababisha sasa Lexi na Kendrick wakatofautiana.

Kevin akajaribu kumfata Kendrick ili waongee kifaragha, lakini bado mwanaume huyo hakutaka kuzungumza na yeyote. Akamwacha tu, na ijapokuwa mpango ule wa kumwondoa Nora haukufanikiwa kwa sababu ya Lexi, ikamridhisha kuwaza kwamba utofauti wa wawili hawa ungefanya Lexi awekwe pembeni kuanzia sasa ili yeye aweze kuendelea kumshawishi Kendrick kijanja kufanya mambo kwa njia aliyotaka.


★★★


IKULU


Kundi la kufanya maovu la Raisi Paul Mdeme lilikutana tena kwa pamoja Ikulu. Walikuwa wanataka kuzungumzia mambo yote yaliyofanyika tokea mara ya mwisho walipokutana hapo, na kwa sababu hayakuwa mambo mazuri, hali iliyokuwepo kati yao pia haikuwa nzuri. Salim Khan, yule milionea, kama kawaida alikuwa akilalamika kwamba mambo yote aliyotabiri kutokea yangetokea, hasa kwa sababu Mdeme aliwahakikishia mzigo wake wa dhahabu ungefika na kuutumia kwa njia fulani, lakini Mess Makers walifanikiwa kuuiba pia.

Ingawa Mdeme alisema walipiga hatua katika msako wao wa wezi wale, bado haikuwa na faida yoyote kwa wenzake kwa sababu mambo yao mengi yaliharibika kwa kuwa hawakupata "support" nzuri kama ilivyokuwa mwanzoni. Salim Khan aliongea na kuongea, naye akamkumbusha Luteni Jenerali Weisiko kwamba alimwambia kama mpango ule ungeharibika basi angemkata kichwa kwa sababu alimwonyesha jeuri, na hilo likamkasirisha sana Weisiko.

Katika maongezi yao wote, Jenerali Jacob alikuwa kimya tu wakati wote, na wengine wakataka kujua aliwaza nini.

"Mnataka niseme nini? Na mimi nianze kulalama kama mtoto anayedai pipi? Itasaidia kufanya mambo yawe shwari?" Jenerali Jacob akaongea.

"Unataka kusema nini?" Gavana Laurent Gimbi akamuuliza.

"Salim aache utoto!" Jenerali Jacob akasema.

"Unasemaje?" Salim akauliza kiukali.

"Unajua ukifunga ndoa, shangwe na furaha, au tabu na mateso ni vitu vya lazima. Wewe umefurahia raha kwa miaka mingi, sasa tabu zimeanza unataka kujifanya kama vile sikuzote tulikuwa kile ambacho kimekupa raha kwa muda huu wote. Grow up. Kuwa kama mwanaume, acha kuongea sana, fanya vitendo. Ikiwa wewe ndiyo mwenye pesa zaidi nchini, onyesha nguvu yako na siyo kukaa tu nyuma ya mgongo wa mtu!" Jenerali Jacob akasema.

Luteni Jenerali Weisiko akatabasamu kwa kiburi baada ya kuona Jenerali amempausha mwanaume huyo.

"Mgongo wa mtu? Unamaanisha mimi nabebwa na Mdeme tu, si ndiyo?" Salim akauliza.

"Unajua mwenyewe!" Jenerali Jacob akasema kwa kukerwa.

Wengine wakamshangaa. Hata Mdeme alikuwa akijiuliza ni kwa nini Jenerali Jacob alikuwa mwenye hasira sana.

"Jamani... naona sisi sote tuko high sana. Tutaongea wakati mwi...."

"Wakati gani Eliya?" Waziri Mkuu Yustus Kagame akamkatisha Makamu wa Raisi.

"Kwa hiyo Jenerali... umeamua kunitukana leo, si ndiyo?" Salim Khan akamwambia.

"Aagh... halafu nilikuwa nakuona wa maana kweli, lakini mambo yako ya kitoto sana mwanangu," Weisiko akamwambia Salim.

Salim Khan akasimama na kumfata Weisiko, naye Weisiko akasimama pia.

"Ah-aaah... mambo gani haya tena?" akauliza Yustus.

Salim Khan alikuwa na mwili mnene na mrefu pia, hivyo alikuwa mwenye nguvu na alitaka kumwonyesha Weisiko kuwa hakuogopa mwanajeshi.

"Kwa hiyo mkipigana tatizo ndiyo litaondoka?" akauliza Raisi Paul Mdeme.

"Huyu mbwa mchanga tuliyemfuga na kumfundisha jinsi ya kutafuna nyama leo anajifanya kutubwekea sisi... unacheza na moto Weisiko!" Salim akamwambia akiwa karibu na uso wake.

"Sijali una nguvu kiasi gani kaka. Hili tatizo siyo lako peke yako, limetuathiri sisi wote. Ungekuwa na busara kweli ungetafuta njia za kusuluhisha badala ya kujibweteka tu ukisubiri mheshimiwa Raisi ndiyo afanye kila kitu kama vile unamlipa," Weisiko akamwambia.

"Unajuaje kwamba simlipi?" Salim akauliza.

"Analipwa na serikali," Weisiko akajibu.

"Ahahahah... serikali gani? Hii hii ya trilioni 20?" Salim akasema kikejeli.

"Inatosha! Nionyesheni heshima mkiwa hapa!" Mdeme akaamuru.

Salim akaifata meza ya Mdeme na kuweka mikono yake juu ya meza, huku akimwangalia usoni kwa hasira.

"Mambo yote ambayo yametokea ni makosa yako. Hakuna yeyote anayepaswa kulipa ila wewe. Kuanzia sasa, sitaki tena kufanya lolote na nyie. Kivyangu, kivyenu," Salim akasema.

Wengine wakashangaa, isipokuwa Jenerali Jacob na Luteni Jenerali Weisiko. Wakaanza kumwambia asiongee namna hiyo kwa sababu ya hasira tu, lakini Salim akaonekana hatanii. Akamsogelea tena Weisiko usoni.

"Tutaonana," Salim akamwambia.

Weisiko alikuwa anamtazama kwa hasira kuu moyoni. Salim akaondoka hapo, akiwa amejitoa kwenye kundi hili kwa sababu ya tofauti zao kutokana na mambo yote haya. Mdeme akawa anamwangalia sana Weisiko, kama vile anamlaumu kwa kilichotokea.

"Mheshimiwa..."

"Shut your mouth!" Mdeme akamkatisha Weisiko.

Weisiko akatulia. Wengine walimwangalia Mdeme kwa wasiwasi kiasi, lakini Jenerali Jacob alikuwa ameangalia pembeni tu.

"Eliya, Yustus, Gimbi..." Mdeme akaita.

Watatu hao wakaitika.

"Mnaweza kwenda. Nahitaji kuongea na hawa wawili," akasema Mdeme.

Makamu wa Raisi, Waziri Mkuu, na Gavana wa Benki Kuu wakanyanyuka na kuondoka kama walivyoamriwa. Wakabaki wazee wa kazi hapo. Mdeme alikuwa akimtazama sana Jacob, naye aliona bado alikuwa kwenye hasira.

"Una shida gani wewe? Kwa nini umeongea vitu vikali namna ile?" Mdeme akamuuliza Jenerali Jacob.

"Nilikuwa najaribu kutetea upande wako, halafu me ndo' mbaya?" Jenerali Jacob akamuuliza.

"Unajua Salim ni nani... kashifa kwake hazitasaidia kwa sababu bado tunamhitaji..."

"No. Unamhitaji wewe. Mimi sijawahi kumhitaji. Nimekuwa nikifuata mambo yote uliyoniagiza kufanya tokea tulipoanza hii ishu, lakini mimi siyo mbwa wa mtu. Sisi sote hapa tuna dignity kaka... siwezi kukaa kuangalia tu mtu anatufokea kama vile sisi watumwa wake," Jacob akasema.

"Jacob, kumbuka ni kwa msaada wake ndiyo...."

"Huo msaada wake ungefanikiwa bila sisi kuhusika? Tusingetumia vijana wetu kwenye kila kitu tulichofanya, mngekuwa mlipo?" Jenerali Jacob akamwambia.

"Jacob! Unathubutu vipi kunisemesha namna hiyo? Umesahau sehemu yako?" Mdeme akasema kiukali.

"Naijua vizuri sehemu yangu, na ndiyo maana ninaongea. Nilikwambia kuwaendekeza hao Mess Makers ni hatari, lakini kwa sababu ya woga wako ukakifanya kichwa chako kiwe kigumu. Mimi sitakaa kupelekeshwa na Salim kama vile ananimiliki. Wewe si umeshaagiza mambo yafanywe namna unayotaka, basi tuyaache namna hiyo hiyo," Jenerali Jacob akaongea.

Raisi Paul Mdeme akawa anamtazama kimaswali sana.

"Ikiwa tumemaliza hapa, niruhusu niondoke.... mheshimiwa," Jenerali Jacob akasema.

Kisha akanyanyuka na kuanza kuondoka, akifuatwa na Weisiko.

"Una hasira na mimi kwa sababu ya kilichompata Nora, sivyo Jacob?" Mdeme akauliza hivyo.

Majenerali wakasimama na kumgeukia.

"Unanilaumu kwa kilichompata mtoto wako... kwa sababu mimi ndiyo nilimwingiza kwenye mission hiyo... ndiyo maana leo umeamua kunionyesha wazi hasira yako," Mdeme akamwambia.

"Ninaweza kuwa na uhusiano usioeleweka na mwanangu, lakini nampenda sana. Tokea mwanzo nimekuwa nikifuata kila kitu unachosema Mdeme, lakini inapokuja kwenye suala la damu yangu... sitakuwa mzuri," akasema Jenerali Jacob.

Mdeme akasimama na kumfuata mpaka karibu.

"Najua nimekosea ndugu yangu. Ni makosa yangu kwamba nimemwingiza Nora matatizoni... na kwa hilo naomba unisamehe. Nakutegemea sana Jacob. Wewe ndiyo nguvu yangu. Siko radhi hata kidogo kukupoteza," Mdeme akamwambia.

Jenerali Jacob na Weisiko wakatazamana.

"Ikiwa unataka... nitamwondoa Nora katika msako huu. Akae tu pembeni ili awe salama kwa sababu... hata mimi kiukweli sijajisikia vizuri baada ya kujua kilichompata. Namwona kama binti yangu pia," Mdeme akasema.

"Nora hatakubali kuacha hii ishu, tena hasa baada ya kilichotokea. Unajua jinsi alivyo na king'ang'anizi," Weisiko akamwambia Jenerali Jacob.

"Basi nitaagiza arudishwe kabisa Dodoma... yaani asihusike hata kidogo na...."

"Hapana," Jenerali Jacob akamkatisha Mdeme.

Mdeme akamtazama tu kwa umakini.

"Najua Nora ni wa muhimu katika hili. Atapaswa kuendelea na kazi yake, lakini nitataka awekwe mbali na action zozote za kuwafuata watu hawa," akasema Jenerali Jacob.

"Usijali Jacob. Nitafanya mpango. Natumaini mambo kati yetu yataendelea kubaki sawa kijana wangu," Mdeme akamwambia.

"Na huu uzee unamwita kijana? Acha kumdekeza sana mheshimiwa," Weisiko akatania.

Mdeme akatabasamu na kusema, "Salim mniachie mimi, nitadili naye. Endeleeni tu na kazi. Ninajua wakati huu matokeo yatakuwa mazuri."

Viongozi hawa wa jeshi wakatikisa vichwa vyao kukubali, naye Luteni Jenerali Weisiko akapiga saluti ya heshima, kisha wakatoka kwenye ofisi yake.


★★


Wakiwa bado wanaelekea nje, Weisiko akamuuliza Jenerali Jacob, "Tuna uhakika Mdeme atafanya mambo yawe sawa, au tuendelee na mambo yetu kisiri?"

"We' unaonaje?" Jenerali Jacob akamuuliza.

"Mimi ninafata chochote unachochagua General," Weisiko akamwambia.

"Tunaendelea Weisiko. Hatutaruhusu siri zetu zivuje. Hawa jamaa wanatuchezea mchezo wa kuzungusha sana, wakifikiri sikuzote faida itakuwa kwao, ila tutahakikisha wanakwisha wote," akasema Jenerali.

"Na Salim?" Weisiko akauliza.

"Kwa hizo dharau? Unajua cha kufanya," akajibu Jenerali Jacob.

Weisiko akaachia tabasamu la kuridhika baada ya kusikia kauli hiyo. Wawili hao wakaondoka jengoni hapo hatimaye ili kwenda kufanikisha mipango yao.


★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★

Previoua Next