FOR YOU 2
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI NA TANO
★★★★★★★★★★★★★★★★
SIKU ILIYOFUATA
Kama ni habari mpya ya jiji siku hii iliyokuwa na ulingano na Mess Makers, basi ilikuwa ni kile alichofanya Salim Khan. Milionea huyo alikuwa amejiondoa katika mambo YOTE aliyowekeza pesa zake kwenye miradi ya serikali, haijalishi zilikuwa ni sekta gani; zote. Kwa muda wote ambao Mess Makers walikuwa wakiwapa shida yeye na kundi lake, Salim Khan ndiye aliyekuwa akimsaidia sana Raisi Paul Mdeme kwa masuala hayo, lakini tokea walipokosana kwa sababu ya viburi vyao, sasa akawa ameamua kuwaonyesha wazi kwamba hakuwa akitania aliposema yeye na wao ni basi.
Watu wengi sana walikuwa na maswali kuhusu uamuzi wa tajiri huyo, na wale waliokuwa wanamfanyia kazi wakavijulisha vyombo vya habari kwamba Salim Khan angeeleza sababu zake kwenye mahojiano maalum siku ya kesho, hivyo wangepata majibu waliyohitaji.
Raisi Paul Mdeme alijitahidi sana kumtafuta ili waongee, lakini Salim alimkwepa tu. Alijua uamuzi wake huo ungemuumiza sana, hivyo kufikia hapa alishindwa kujua angefanya nini. Mess Makers walikuwa wamemwibia matrillioni ya pesa, wakaiba na dhahabu zake, bado watu waliowekwa kuwafatilia hawakuwa wamewakamata, na sasa tena Salim alikuwa ameanza kuleta zengwe. Akaona amtafute Jenerali Jacob kwa simu ili wazungumze kuhusu ni nini ambacho wangefanya sasa.
"General... Salim anataka kuharibu mambo. Itakuwaje kama kwenye hayo mahojiano akisema kila kitu ambacho tumefanya?" Mdeme akasema.
"Hawezi," Jenerali Jacob akajibu.
"Unajuaje?"
"Atakuwa na mambo mengi ya kupoteza ikiwa ataropoka chochote kuhusu sisi. Anachotaka tu ni umati wa kumfuata... ndiyo sikuzote anachoangalia..."
"Nimejaribu kumtafuta, hanijibu. Yaani ni kama amekuwa mwendawazimu..."
"Anafanya hivyo ili kutukomoa, na kwa sababu pia anajua hatuwezi tukamfanya lolote..."
"Kwa hiyo tunatakiwa tu kukaa na kumwacha atambe? Maswali yakija kugeuziwa kwangu itakuwaje?"
"Mheshimiwa Raisi... mimi ni mwanajeshi. Mambo ya siasa huwa...."
"Oh, come on Jacob! Acha kujifanya modest sana katika hili. Ninajua hauwezi kukaa tu ukasubiri Salim atende kama mwehu. Niambie. Unawaza nini?"
"Okay. Ninawaza.... kumuua," Jenerali Jacob akasema kwa uhakika.
"Come again?!" Mdeme akashangaa.
"Yeah," Jenerali Jacob akasema.
"General... unajua unachokisema? Hebu tuache masihara basi!" Mdeme akamwambia.
"No, wewe ndiyo uache masihara. Acha kunyong'onyea mbele ya mtu eti kisa amewahi kukupa mia mbili. Salim anakutusi vibaya sana Mdeme, kwamba pamoja na kwamba wewe ni Raisi lakini hauwezi kumfanya kitu. Nilikuwa nikisubiria unipe amri hii lakini inaonekana mambo yamekuwa mengi sana kwako mpaka unasahau tulipotoka. Kumbuka tulitumia njia zipi kuwaondoa wale wote waliokuwa vikwazo kwetu. Salim sasa ni kikwazo kwetu Mdeme. Ni lazima aondolewe!" Jenerali Jacob akasema kwa mkazo.
"Lakini General, Salim siyo kama wengine. Hatuwezi tu ku...."
"Hatuwezi? Umeweka wingi! Hiyo inamaanisha unaniunga mkono, siyo?"
"General... Salim akifa kwa wakati huu haitakuwa nzuri kwangu. Kwa jinsi mambo yalivyo watu wanaweza wakafikiri moja kwa moja kwamba mimi ndiyo nimemuua... haitakuwa nzuri Jacob," Mdeme akasema.
"Usijali kuhusu hilo. Kila kitu kitakwenda kulingana na mpango..."
"Unamaanisha... yaani umeshapanga jinsi ya... kumuua Salim?"
"Ndiyo."
"Halafu nini kitafuata baada ya hapo?"
"Ndiyo maana nimekwambia kwamba kila kitu kitakwenda kulingana na mpango niliouweka. Sikuzote nimejitahidi kukulegezea mambo kaka, lakini hauonyeshagi shukrani vya kutosha. Unawafurahia zaidi watu ambao wanakuja kukugeuka wakati sisi tulio waaminifu unatuweka tu pembeni kama akiba ya mchele..."
"Jacob... siyo hivyo. Ni kwamba tu...."
"Haina haja ya kujikwarua sana. Wewe kaa kwa kutulia. Kila kitu kikikamilika, utakuja kunishukuru. Just play along," Jenerali Jacob akasema.
Kisha akakata simu na kumwacha Mdeme akiwaza mengi sana. Hakuwahi kufikiria angekuja kulazimika kuchukua uamuzi huu; kuua mtu aliyemwona kama rafiki kwa muda mrefu sana, hata ijapokuwa wote walitenda mambo mabaya. Lakini akaamua kuyaacha mambo mikononi mwa Jenerali Jacob, akiamini mwanaume huyo alijua akichokuwa anakifanya.
★★★
ACP Nora alikuwa akijiandaa kuondoka hospitalini. Luteni Michael alikuwa ameongea na madaktari kwa niaba yake siku iliyopita na kuwaambia Nora alitaka sana kuondoka, nao wakamwambia kwa kuwa alisisitiza basi angeondoka wakati huu. Ikiwa ni mida ya saa 6 mchana tayari, akawa amemaliza kuvaa nguo zingine nadhifu ambazo Mario alisaidia kumletea hapo, na sasa akawa anajiandaa kuondoka ndani ya chumba hicho hatimaye, huku Mario na Hussein wakiwa nje wanasubiri.
Lakini kabla hajauendea mlango, ukagongwa, na sauti ya Luteni Michael akiuliza kama ilikuwa sawa kuingia ikasikika. Kulikuwa na muuguzi wa kike ndani hapo pia ambaye alikuwa anamsaidia Nora kwa mambo kadhaa, naye akasema kwa sauti kubwa kiasi kwamba Luteni Michael angeweza kuingia. Luteni Michael alipoingia, Nora aliachia tabasamu dogo, lakini likafifia baada ya wengine waliomfuata nyuma yake kuingia.
Ilikuwa ni Inspekta Jenerali wa Polisi, IGP Donald Ngassa, akiwa pamoja na yule msaidizi mkuu wa mambo ya ndani yaliyohusiana na Jeshi la Polisi, Principal Secretary Joachim Uwesu. Kwa kuangalia uso wa Luteni Michael, Nora angeweza kuhisi kwamba jambo waliloleta hapo halikuwa na uzuri kwake. Akapiga saluti ya heshima kuwaelekea, lakini IGP Donald akamwambia ajiweke tu sawa. Muuguzi yule akawapisha na kuondoka.
"Unajisikiaje binti yangu?" IGP Donald akamuuliza.
"Niko sawa mkuu. Tayari kurudi kazini," akasema Nora.
"Habari za muda ACP?" Secretary Joachim akamsalimu.
"Ni nzuri tu Joe. Unaendeleaje?" Nora akarudisha salamu pia.
"Vizuri zaidi yako," akajibu Joachim, naye Nora akatabasamu.
"Unajua ulikuwa unatakiwa kuendelea kukaa hospitalini ACP... kwa nini unang'ang'ania kuondoka?" IGP Donald akamuuliza.
"Kukaa hapa hakuna utofauti na kukaa gerezani. Na tafadhali naomba mwache kunitendea kama vile ndiyo nimetoka kutotolewa... mnaweza kunichangia sasa hivi na wote nikawakunja," Nora akatania.
Wawili hao wakacheka kidogo.
"Mmekuja kunitembelea tu, au kuna mapya?" akauliza Nora.
"Vyote. Kwanza... pole kwa yote yaliyokupata dada. Ni mambo yenye kusikitisha sana, na tunaelewa ni jinsi gani ilivyo ngumu kwako," akasema Secretary Joachim.
"Ahah... Joe ukishagaanza kuzunguka sana wote tunajua tu kwamba bomu linakuja," Nora akasema.
"Ah... Nora ameshaanza. Sikuzote ananifikiria kama vile mtu aliyeficha kisu nyuma ya mgongo wake," Joachim akasema.
IGP Donald akatabasamu.
"Kwa hiyo, mapya ni yapi?" akauliza Nora.
"Siwezi kusema ni mapya, ila... unajua kiukweli kama ingekuwa ni mimi ndiyo nimepatwa na mambo hayo yote yaliyokupata, ningeahirisha uchunguzi huu kwa sababu tayari najua kuna watu wameniwekea target kwa nyuma," akasema Secretary Joachim.
"Hata me ningefanya hivyo, kama ningekuwa wewe," akajibu Nora.
"Ahahahah... usijifanye Alexander the Great," Secretary Joachim akasema.
"Kwa hiyo unasema kwamba... nimeondolewa kwenye hii mission?" Nora akauliza.
"Oh Nora, hatutafanya hivyo. Najua unavyopenda kazi yako, na... kiukweli tunakuhitaji sana. Wewe ni wa muhimu katika hili hakuna asiyejua. Na ndiyo sababu hatuwezi kuruhusu chochote kibaya kikupate. Lakini pia najua huwa haupendi walinzi," akasema Secretary Joachim.
"Yeah... kabisa..." akasema Nora.
"Kwa hiyo ni muhimu tutumie njia fulani kukulinda...."
"Joe... tafadhali acha kuzunguka sana, just... tell me," Nora akamkatisha.
"Okay. Kuanzia sasa utapaswa kufanya uchunguzi wako wote... mbali na timu ya Lieutenant Michael," Secretary Joachim akasema.
Nora akamtazama Luteni Michael kimshangao, lakini yeye alikuwa anamwangalia kwa njia ya kawaida.
"Unamaanisha nini... mbali?" Nora akauliza.
"Tunakupa ofisi yako maalum huku, utakuwa unafanya kazi zako za utafiti huko, kisha zinatumwa kwa Luteni ili wazishughulikie," akasema IGP Donald.
Nora akakunja uso kimaswali. "I don't... yaani... nifanye kazi na watu ndani ya jiji moja bila kuonana nao, ndiyo unachosema?" akauliza.
"Yeah," akajibu IGP Donald.
"Kwa nini?" Nora akauliza.
"Kama nilivyosema... ni ili kukulinda," akasema Secretary Joachim.
"Luteni Michael amekuwa akinilinda vizuri tu mbona? Na... sihitaji ulinzi mimi. Sihitaji kupewa ofisi, sihitaji chochote... nitakuwa sawa. Huwezi kunitenganisha na timu hii. Nachotaka hata zaidi sasa ni kurudia kazi hii nikiwa nao kwa kuwa tumetoka mbali... nimewazoea... sitaweza kufanya kazi bila kuonana nao," Nora akawa anaongea kwa hisia.
"Basi ACP, tafadhali jitulize. Unapaswa kujitahidi tu kuyaona mambo kwa njia pana zaidi. Hii itakuwa nzuri kwako. Unaweza ukawa subject wa tukio lingine kama lililokupata kwa sababu hauna uangalizi maalum," IGP Donald akamwambia.
"Hivi kweli... Luteni... does this make sense?" Nora akamuuliza Michael.
Lakini Luteni Michael akabaki kimya tu.
"Nora... tafadhali kubali hili. We are just looking out for you. Tafadhali nakuomba just... please... nakuomba kama rafiki. Ni muhimu sana kwako," Secretary Joachim akamwomba.
"Na kama nikikataa?" Nora akauliza.
"Basi... ni kwamba hautapaswa kujihusisha na kesi hii... utapaswa kurudi kwenye post yako Dodoma," IGP Donald akasema.
"Unbelievable!" Nora akasema kimshangao.
"Nora please... tunakuhitaji, just do this, hakuna ugumu wowote... ni kwa ajili yako," Joachim akamsihi.
"Luteni..." Nora akamwita kama anamhitaji amuunge mkono.
"Wako sahihi ACP. Ni bora iwe hivi... ili uwe salama zaidi," Luteni Michael akamwambia.
Nora akarudi sehemu ya kitanda na kuketi, huku akitikisa kichwa taratibu kwa kutoamini.
"Ni General wenu ndiyo amefanya haya yote, siyo?" Nora akauliza bila kuwatazama.
IGP Donald na Secretary Joachim wakaangaliana, kisha Joachim akasogea usawa wa Nora.
"Hapana, ni mheshimiwa Raisi. Alijisikia vibaya sana kwa kilichokupata ndiyo maana akatoa agizo hili," Joachim akasema.
"Angekuwa amenipigia simu kuniambia," Nora akasema.
"Ana mambo mengi kama unavyojua, ndiyo maana tuko hapa," IGP Donald akamwambia.
Secretary Joachim akatoa karatasi fulani jeupe na kumpatia Nora.
"Sign tu hapo kuthibitisha kwamba umekubali," Secretary Joachim akasema.
"Nina uhakika gani hiyo siyo bogus treaty?" Nora akauliza.
"Ahahah... unaweza kuisoma ukihitaji. Lakini hata wewe unajua blah, blah, blah, ni nyingi hapo," Secretary Joachim akamwambia.
Nora akamtazama Luteni Michael kiufupi. Luteni aliona kwenye macho ya mwanamke huyu kwamba kweli hakutaka kufanya hivyo, lakini kwa sababu alikuwa chini ya hali iliyomlazimu kutenda kupatana nayo, hakukuwa na jinsi. Nora akaichukua karatasi hiyo, naye Secretary Joachim akampatia kalamu ili atie sahihi.
"Kuna air condition nzuri kwenye hiyo ofisi?" Nora akauliza kiutani.
"Ahahahah... chochote kwa ajili yako Malkia," Joachim akamwambia.
Nora akatia sahihi yake, kisha Secretary Joachim pamoja na IGP Donald Ngassa wakamuaga na kumwambia kwamba walikuwa wamefanya mipango ya kumbadilishia hoteli ya kukaa ili awe sehemu mpya na salama, hivyo angepaswa kwenda kupumzika leo, halafu kesho ndiyo angepelekwa kwenye ofisi yake mpya ili aendelee na kazi. Nora bado alipingana sana na mambo hayo yote, lakini kama ingemhitaji kuyafuata tu ili kuendelea na kazi aliyopewa, basi angefanya hivyo. Alikuwa amekwishazoea kufanya kazi bega kwa bega na timu ya Luteni Michael, lakini kuanzia sasa ingekuwa ni kurushiana mawe mbali kwa mbali.
"Eti 'wako sahihi ACP'... Kweli na wewe unakubaliana na huu upuuzi?" Nora akamwongelesha Luteni Michael.
"ACP..."
"Well, hakuna jinsi now. Tutapaswa kufanya kazi kama vile hatujuani, na... kama vile hatujapitia mambo mengi pamoja," akasema Nora, akionekana kuudhika.
Akanyanyuka ili aanze kuuelekea mlango, lakini Luteni Michael akamshika mkononi kumzuia.
"Nora..." Luteni Michael akamwita kwa sauti yenye hisia.
Nora alipomwangalia, akatambua kuwa Luteni Michael alikuwa akimwonyesha hisia fulani hivi mpya, na hili likavuta umakini wake.
"Leo ndiyo kwa mara ya kwanza umeniita kwa jina langu. Hii yote kuni-please kwamba jambo hili lote ni sahihi?" Nora akauliza.
Luteni Michael akamsogelea karibu zaidi.
Nora akabaki kumtazama kama ameduwaa.
"Siyo rahisi kwangu pia Nora. Nilikuwa napenda sana ukiwa karibu yangu. Bado natamani hilo. Lakini siwezi ku... kujua nitafanya nini kama na wewe ukipotea kwa sababu ya kuwa nasi muda mwingi... siwezi kujisamehe kama utapatwa na lolote baya Nora..." Luteni Michael akaongea kwa hisia.
Nora akawa anajiuliza sababu ya Luteni Michael kumwambia haya yote ni nini, lakini lile wazo lile, halikuwa mbali sana akili yake.
"Luteni...."
"No... niite Michael," Luteni Michael akamwambia.
"Unataka kusema nini?" Nora akauliza.
Luteni Michael akaona amjibu kwa vitendo. Akaanza kuusogelea mdomo wa Nora taratibu, naye Nora akatambua kuwa jamaa alitaka kumbusu. Michael alipokuwa ameukaribia zaidi mdomo wa Nora, mwanamke huyu akainamisha uso wake na kupiga hatua chache nyuma. Hii ikamuumiza sana Luteni Michael.
"Luteni.. hhh... Michael... samahani ila...."
Nora akakatishwa baada ya mlango wa chumba hicho kufunguliwa. Wakaingia Mario na Hussein.
"Tulikuwa tumewasindikiza hao wawili mpaka kwenye gari... ahah... Secretary Joachim ni mcheshi," akasema Mario.
"Lakini ACP... ni kweli eti sasa hivi hautaambatana nasi?" akauliza Hussein.
"Ndiyo. Ndiyo inavyoonekana," Nora akajibu huku akijaribu kupotezea kilichokaribia kutokea baina yake na Luteni Michael.
"Dah! Itakuwa ngumu kutokukuona tena," Mario akasema.
"Lakini hata kukutembelea si itakuwa poa?" Hussein akauliza.
"Ndiyo. Mnaweza kunitembelea... ila sijui sana," akasema Nora.
"Tutaku-miss. Hasa Luteni," akasema Mario.
Nora akamtazama Luteni Michael, ambaye alikuwa anamwangalia kwa hisia pia.
"Na sisi tumeongezewa jamaa wengine kwenye timu yetu. Ila hawataweza kuwa-replace wenzetu waliopotea... never," akasema Hussein.
"Wamekuja wangapi?" Nora akauliza.
"Watano. Special unit toka JKT," akasema Hussein.
"Okay. Nadhani sote tu tukiendelea na kazi... hata kama tutakuwa tumetenganishwa... tutafanikiwa tu," akasema Nora huku akimtazama Luteni Michael.
"Yeah... ACP yuko sahihi," Luteni Michael akasema.
Kwa kuwa hali kati ya hawa wawili ilikuwa imejivuruga kwa njia ambayo haikutazamiwa, Nora akaona tu aanzishe mwendo ili kuondoka hospitalini hapo. Wanajeshi hao watatu wakamsindikiza, huku Mario akimwambia alilileta na gari lake Nora pia. Luteni Michael akapendekeza amwendeshe mpaka kwenye hoteli mpya ambayo angekaa ikiwa hakuwa na nguvu za kutosha, lakini Nora akasema angekuwa sawa tu kuendesha ili kujipa nguvu zaidi. Ingawa hivyo, Mario na Hussein wangetakiwa kumsindikiza ili kuhakikisha anafika salama, naye Luteni Michael angeelekea kule jengoni kwa timu yake.
Wakaachana muda mfupi baada ya hapo, naye Luteni Michael akabaki tu akitafakari sana kuhusu itikio la Nora ndani ya chumba kile. Mwanzoni alipofikiria kumwambia hisia zake, alikuwa tayari kwa lolote lile ambalo lingetokea, lakini leo baada ya Nora kukwepa hisia zake, bado alikuwa akitaka sana kurekebisha hali hiyo ili ampate mwanamke huyo. Akaingia tu kwenye gari lake akiwa anafikiria ni nini kifuate kuhusiana na jambo hilo.
★★
Baada ya Nora kufika hotelini na kusindikizwa na Mario pamoja na Hussein mpaka nje ya mlango wa chumba chake kipya, wawili hao wakamuaga na kusema ahakikishe anafunga mlango kwa ndani. Walikuwa wameongea naye kuhusu mambo mengi, kutia ndani suala la Salim Khan kuitimulia vumbi serikali na kusema kama kweli jamaa alikuwa ameamua kufanya aliyoyafanya basi na wao wangeacha kazi yao na kwenda kucheza tu mpira na timu ya Yanga. Hii ilikuwa ni njia yao ya kumtania, naye Nora alifurahia sindikizo lao na kuagana nao vizuri. Alipoingia kwenye chumba chake, alipendezwa na mandhari safi na mpangilio mzuri wa vitu, na vingi vilikuwa vya gharama. Akaelekea kitandani na kuketi ili kutafakari mambo kwa ufupi.
Kumbukumbu za mambo yote yaliyotokea usiku ule aliotekwa, zilimfanya ahisi ni kama yale yote aliyoona yalikuwa kwenye ndoto ya kutisha, lakini alijua wazi ilikuwa ni mambo halisi. Bado mtu yule aliyetokea ghafla kumwokoa alizunguka sana kichwani kwake, fikira ya kwamba ni adui aliyeokoa uhai wake ilimtatiza sana. Lakini tena, akaituliza tu akili yake na kuamua kwamba asitafakari mambo yenye kuvunja sana moyo kwa muda huo, bali ajaribu kujipa wakati wa kutosha kuijaza nguvu akili yake ili kufikia kesho kazi zianze.
Njia nzuri iliyokuja haraka kuliko zote akilini mwake, ilikuwa ni Lexi. Akafikiria ampigie simu ili kuongea naye, na labda hata aonane naye. Zilikuwa zimepita siku kama tatu bila kuonana naye, na akikumbukia mambo yalipoishia baina yao, akajawa na hamu kubwa zaidi ya kutaka kumtafuta. Akachukua simu yake na kumpigia, naye akapokea.
"Hey..." Nora akasema.
"Hey..." Lexi akasikika.
"Mbona kimya?" Nora akauliza.
"Mimi, wewe?" Lexi akauliza pia.
Nora akatabasamu na kusema, "Wewe."
"Hakuna. Ni wewe ndiyo umeona unichunie," Lexi akasema.
"Sijakuchunia wala. Nili..patwa na matatizo," Nora akasema.
"Matatizo gani?"
"Nilitekwa..."
"Wewee.... lini?"
"Juzi..."
"Eh! Uko sawa lakini mheshimiwa?"
"Ndiyo, niko sawa..."
"Pole sana jamani. Kwa hiyo... eh... yaani hata nimekosa la kusema..."
"Usijali... nitakuwa sawa."
"Nimeona kwenye habari, mlimkamata mmoja wao... anaitwa Oscar eh? Ndiyo maana wakakuteka eti?" Lexi akauliza kama vile haujui ukweli.
"Hapana Lexi... sijui sana. Tafadhali... tusiongelee hayo..." Nora akamwomba.
"Okay, sawa mheshimiwa. Uko wapi sasa hivi?" Lexi akauliza.
"Niko hotelini... napokaa..."
"Oh, okay. Unahitaji kupumzika..."
"Nahitaji kukuona..." Nora akasema kwa hisia.
Lexi akiwa upande wa pili, alifumba macho baada ya Nora kusema hivyo. Bado alikuwa na wakati mgumu pia baada ya kilichotokea baina yake na Kendrick kuhusiana na suala zima la kumteka mwanamke huyo. Ijapokuwa alihisi hatia sana kwa kilichompata Nora, alijua bado angetakiwa kuwa makini kwa sababu yeye bado alikuwa adui yake.
"Aam... unahitaji kuniona?" Lexi akauliza.
"Ndiyo..." Nora akasema.
"Lakini..."
"Please..." Nora akamwomba.
"Okay. Uko hoteli gani?" Lexi akauliza.
"Hyatt Regency," Nora akasema.
"Wow! Halafu ulikuwa unaniita mimi mtoto wa kishua!" Lexi akasema.
Nora akacheka kwa sauti ya chini.
Lexi akamwambia angefika hapo muda si mrefu sana, nao wakaagana baada ya hapo.
Nora sasa akajihisi kama vile alikuwa ameanza kuutua mzigo mzito wa mawazo baada ya kuongea na Lexi. Akaona ampigie na mdogo wake, Asteria, ili kumjulia hali, lakini kwa sababu fulani hakupokea simu yake mara nne kabisa. Hivyo Nora akaweka tu simu yake pembeni na kubaki hapo kwenye chumba chake akimsubiri kwa hamu Lexi, akitarajia mambo mengi sana.
★★
Ilipita kama nusu saa hivi, naye Lexi akampigia Nora kumjulisha kwamba tayari alikuwa nje ya jengo hilo la hoteli. Nora akamwelekeza namba ya chumba chake, kilichokuwa kwenye ghorofa ya 7 kabisa, naye Lexi akaanza kupanda huko juu. Hoteli hii ilikuwa ya kifahari sana, ikiwa na vitu vingi vya gharama na vyenye ubora wa hali ya juu. Chumba kwa kulala usiku ilikuwa ni laki nne, sasa fikiria Nora alikuwa analipa kiasi gani kukaa hapo kwa muda wote ambao angeendelea kuwapo!
Baada ya Lexi kufika nje ya mlango wa chumba cha Nora akaugonga, naye Nora akafungua. Walipeana tabasamu lenye hisia huku wakiangaliana sana. Lexi alikuwa amevaa nguo fulani nyekundu kwa juu yenye mikono mirefu kufunika mpaka viganja ikiacha vidole vichache wazi, suruali nyeupe ya jeans laini, na sneaker nyekundu kwa chini. Kichwani kwake alivaa kofia nyeusi yenye maandishi "TMT," akionekana kama muhuni wa genge fulani hivi.
Nora akamkaribisha ndani, naye akapita na kuelekea sehemu yenye sofa. Vitu vingi hapo vilikuwa vizuri sana kutazama, na baada ya Lexi kugeuka akakuta Nora amesimama karibu naye huku anatabasamu. Yeye pia akatabasamu, kisha Nora akaichukua kofia yake (Lexi) na kuivaa yeye. Lexi akatabasamu kwa furaha, kisha akamkumbatia Nora. Nora alijihisi vizuri sana baada ya Lexi kufanya hivi, naye akazungusha mikono yake mgongoni kwake kurudisha kumbatio hilo pia.
"Mbona hauongei sana leo?" Nora akauliza.
"Nimefurahi tu kuona unaendelea vizuri mheshimiwa," Lexi akasema.
Wakaachiana taratibu, lakini Nora akaendelea kuvishikilia viganja vya Lexi kwa chini.
"Kirefu cha TMT?" Nora akauliza huku anaipiga kofia kwa kidole.
"The Money Team," Lexi akajibu.
"Ahahahah... unapenda sana hela eeh?" Nora akauliza.
"Kupita msosi," Lexi akasema.
Nora akaendelea kumwangalia kwa hisia. "Nime... nimeku-miss," akamwambia.
Lexi akachekea kwa chini.
"Nini?" Nora akauliza.
"Hii yote... siyo ajabu kwako?" Lexi akauliza pia.
"Kwa nini iwe ajabu?"
"Ahahah... ulishawahi kuiona movie ya Deadpool 2?" Lexi akamuuliza.
"Deadpool... Marvel?"
"Yeah..."
"Ndiyo... nimeziangalia zote..."
"Well, kulikuwa na hali tete wakati Wade anamwomba Cable wakumbatiane..."
"Ahahahah... pelvis to pelvis?" Nora akamkatisha.
"Hahah... kumbe unajua..."
"Acha zako Lexi... Deadpool ni chizi," akasema Nora huku akiendelea kucheka.
"Na sisi je?" Lexi akauliza.
Nora akaweka umakini kiasi. "Sisi...." akaishia tu hapo.
"Waliokuteka walikuumiza sehemu gani?" Lexi akabadili mada ghafla.
"Lexi... nilikwambia tusiongelee hayo leo..." Nora akasema.
"Sorry. Unataka tuongelee nini?" Lexi akauliza.
"Mimi... na wewe..." Nora akasema na kumsogelea karibu zaidi.
"Pelvis... to pelvis," Lexi akatania.
Nora akatabasamu kwa hisia.
Hali hii mpya ilikuwa ikimfurahisha sana Nora, lakini Lexi alikuwa akijitahidi kuzizuia hisia zake kumwelekea mwanamke huyu, na ukweli ni kwamba alikuwa ameanza kuvutiwa na Nora. Kwa hiyo alijihisi vibaya kwa kadiri kubwa kwa sababu haikutakiwa kuwa hivi; mpango kutokea mwanzo ulikuwa ni kumpeleleza Nora ili kupata taarifa muhimu kutoka kwake, lakini sasa kuingiza hisia ingesababisha ajihisi mwenye hatia kwa sababu alijiona mnafiki. Ila ukitegemea na jinsi yeye na Kendrick walivyotofautiana kutokana na mwanaume huyo kumfanyia ubaya Nora, ni kama ndiyo nguvu ya kumkaribia zaidi mwanamke huyu iliongezeka.
Nora akaigeuzia kofia upande wa nyuma ili isizuie uso wa Lexi alipokuwa akimkaribia zaidi, na moja kwa moja Lexi alijua Nora alitaka ambusu kama wakati ule wako ufukweni. Nora akaizungushia mikono yake kiunoni kwa Lexi, miili yao ikiwa karibu zaidi sasa, kibofu kwa kibofu, na walipotaka tu kupiga busu mlango ukagongwa.
"Aagh... hivi ni kwa nini hiyo huwa lazima itokee?" Nora akauliza kwa kukerwa.
"Ahahah... nenda kaangalie ni nani," Lexi akamwambia.
"Usikimbie," Nora akasema kiutani.
Kisha akamwachia na kuuelekea mlango. Alishangazwa kiasi baada ya kukuta ni Luteni Michael ndiye aliyefika hapo.
"Luteni..." Nora akaita.
Lexi alikuwa ametazama pembeni aliposikia Nora akisema hivyo, na macho yake yakakaza kwa kuhisi hasira. Sababu ilikuwa ni kwamba usiku ule Oscar alipokufa, Luteni Michael alikuwa pale, hivyo kwa njia fulani ilikuwa ni kama Lexi alimchukia kwa kuhisi ni kama yeye ndiye aliyesababisha mwenzake asiweze kujilinda vizuri kwa kuwa aliamuru afungwe pingu. Akakunja ngumi akizizuia hisia zake, bila kugeukia upande wao.
"Nora... tunaweza kuongea?" Luteni Michael akamwomba.
"Luteni...."
"Nilikwambia niite Michael..."
"Okay. Michael. Kuna jambo lolote jipya? Ungenipigia tu simu, si ulikuwa umeenda kule..."
"Nakupenda..."
Nora akabaki kumtazama tu kwa njia ya kawaida, kama vile katafunwa na butwaa zito. Lexi aliyasikia maneno hayo, naye akapandisha nyusi zake huku akiachia tabasamu kwa mbali.
"Nakupenda Nora. Ndiyo jambo jipya nililokuja kukwambia," Luteni Michael akanena kwa hisia.
"Michael... aam..."
"Siyo lazima unijibu leo. Najua nimekushtukiza kule hospitalini, na... nilikuwa nataka sana kukwambia hivi kwa muda mrefu nyuma, ila... Nora nimekupenda. Ninaomba unipe nafasi kwenye moyo wako," Luteni Michael akamwambia.
Lexi akachekea kwa chini akiwaza ni jinsi gani jamaa alivyokuwa anajitafutia kuvunjika moyo mapema sana.
"Michael... ona... mimi... sijui nisemeje... kiukweli siko tayari kuwa kwenye mahusiano na mwanaume yeyote kwa sasa. I'm so sorry," Nora akamwambia ukweli.
"Kwa nini?"
"Nina sababu zangu..."
"Sababu gani?"
"Michael!"
"Kama haujanipenda niambie tu dada yangu, sitaki kukaa nikisubiri kwa sababu nitaendelea kuumia..."
"Michael sisi siyo watoto... najua unaelewa ninachomaanisha..."
"Hapana, labda unieleweshe vizuri..."
Lexi akawaza; huyu jamaa vipi? Mbona kama analazimisha vile?
"Seriously? Luteni... tumetoka tu kutenganishwa kwa sababu apparently wewe ni hatari kwangu, si ndiyo? Hivyo nahitaji kuwa salama. Na wewe ukatia tiki kwamba ni sahihi..."
"Ni kitu ambacho kiko nje ya uwezo wangu, lakini kuwa nawe ninaweza. Kuwa pamoja nawe haitakuwa kama kazi Nora..."
"Luteni tafadhali... ni kama nilivyokwambia. Samahani sana..."
"Ona... samahani pia kwa kuwa nimepitiliza sana kihisia na... Nora... hii ndiyo mara yangu ya kwanza kufunguka namna hii kwa...."
Wakati Luteni Michael akiendelea kumwaga maneno yake ya moyoni, Lexi akaona achokoze.
"Mheshimiwa, ni nani, mbona umekawia?" Lexi akauliza.
"Aa... nakuja..." Nora akasema.
"Nani huyo?" Luteni Michael akauliza.
"Ni rafiki yangu..."
"Rafiki? Yaani umetoka hospitalini, sasa hivi unaniambia unahitaji kupumzika kumbe kuna mtu ndani?" Luteni Michael akauliza.
"Ish! Luteni una haki gani ya kuniuliza mimi maswali hayo? Umenioa?" Nora akauliza akiwa ameudhika.
"Kuna tatizo?" Lexi akasikika akiuliza.
Luteni Michael akampita Nora na kuingia mpaka ndani. Nora alishangazwa sana na jambo hilo.
"Lieutenant Michael! What do you think you're doing?" Nora akamuuliza kiukali.
Luteni Michael sasa akawa anamtazama Lexi uso kwa uso. Lexi hakuonyesha woga wa aina yoyote kumwelekea kwa jinsi alivyokuwa akimtazama.
"Kwa hiyo... kumbe huyu ndiyo 'rafiki' yako? Ninge-guess kumbe mara ya kwanza nilipomwona," Luteni Michael akamwambia.
"Michael, nakuomba uondoke..." Nora akasema.
"Bro, kuna shida gani?" Lexi akamuuliza Luteni.
"Usiniite bro, nitakuwasha sasa hivi!" Luteni Michael akamwambia kiukali.
"Michael!" Nora akamwita kwa hasira.
"Nakuomba ujaribu," Lexi akamwambia Luteni Michael bila kuogopa.
Luteni Michael na Nora wote wakamwangalia Lexi kimshangao kidogo.
"Unasemaje?" Luteni Michael akamuuliza.
"Nataka ujaribu kuniwasha!" Lexi akamwambia kiutulivu kabisa.
Luteni Michael akakunja uso kwa hasira, naye Nora akaingia katikati ya wawili hao.
"Luteni... naomba uondoke sasa hivi..." akamwambia.
"Nora... unanifukuza namna hiyo ukiwa na huyu mtu usiyemjua kabisa?" Luteni Michael akauliza.
"Unajuaje simjui? Na kwani mimi nilikuita hapa?"
"Unapaswa kuwa makini na watu unaowaingiza kwenye maisha yako Nora..."
"Get out..."
"Huyu mwanamke ulimleta mpaka kwenye condo letu, na sasa hivi anani-challenge ki...."
"Get out!" Nora akafoka.
Luteni Michael akamwangalia tu kwa ufupi, kisha akamtazama na Lexi kwa umakini, naye akaondoka hapo akiwa amevunjika sana moyo.
Nora akamgeukia Lexi na kukuta ametazama pembeni. "Lexi... samahani..."
"No... usiombe samahani. Niko sawa," Lexi akamwambia.
"Yaani... nashindwa kuamini Luteni Michael kati ya watu wote amefanya kitu kama hicho... sijui tu amekuwaje..."
"Usha'sikia kitu kinaitwa wivu wa mapenzi?" Lexi akatania.
Nora akatabasamu na kutikisa kichwa kwa kusikitika.
Lexi akamwangalia kwa sekunde kadhaa, kisha akaanza kusema, "Sikia... kuna kitu nataka nikwambie. Kiukweli..."
"Lexi... tafadhali usiongelee jambo lolote lenye kuvunja moyo. Watu wananisumbua, Michael tayari ameanza kuwa kikwazo kwangu... please just... tuigize kwa leo kwamba hakuna matatizo. Nahitaji sana kuituliza akili yangu. Utanisaidia?" Nora akamwambia kwa upole.
Lexi akashusha pumzi, kisha akatikisa kichwa kukubali.
"Okay, kwa hiyo... ungependa tufanye nini?" Lexi akauliza.
"Anything you want," Nora akajibu.
"Okay. Unaonaje tukienda kutembea? Say... labda shopping?" Lexi akasema.
"Ahahahah... nawe unafanyaga shopping?"
"Yeah. Huwa nafanya shopping kubwa asikwambie mtu... au, bado hauko fit ku..."
"Nipe dakika tatu nibadili nguo," Nora akasema huku akielekea sehemu yenye begi lake la nguo.
Lexi akawa anamwangalia kwa huzuni sana. Ilikuwa kidogo tu amwambie ukweli kuhusu yeye, ijapokuwa hakujua hiyo ingemwacha wapi. Lakini tena, fikira ya kwamba angewaponza wenzake kwa sababu tu ya hisia zake ikamfanya aliondoe wazo la kutaka kumwambia jambo hilo, na badala yake afurahie muda huu pamoja naye, haijalishi ungekuwa mfupi kadiri gani.
★★★
Luteni Michael alirudi kwa timu yake akiwa ameudhika sana. Akafika na kukaa karibu na Bobby, ambaye kwa haraka aligundua kwamba kuna kitu kilimtatiza Luteni wake. Wanajeshi wale watano waliokuwa wameongezwa na Kanali Oswald kwenye timu hii waliitwa Rachel (36), Tariq (42), Manengo (40), Aliyah (30), na Zachary (39). Wanne walikuwa watanzania asilia, isipokuwa Tariq, ambaye alikuwa na asili ya uarabu, lakini alikuwa mswahili sana. Wote walikuwa na mafunzo mazuri ya kijeshi, na toka walipofika walikuwa wakisaidiana na "wenyeji" kama Alex, Mario na Hussein, katika kufatilia mambo kadha wa kadha.
Tokea usiku ule ACP Nora alipotekwa, wanajeshi hawa kwa pamoja walikuwa wanatafuta uwezekano wa kupata "server" zozote ambazo zilikuwa zimefichika nchini (aina fulani za kompyuta au programu za kompyuta zenye uwezo wa kupata taarifa na kuingia sehemu yoyote hususa kwenye mtandao). Walikuwa wakitafuta hizi kwa sababu waliona kwamba Mess Makers walikuwa wanapata taarifa nyingi na kufanya mambo mengi kitaalamu, hivyo bila shaka kungekuwa na pazia linalowaficha kitaalamu pia; teknolojia. Manengo pia alikuwa mtaalamu kwenye masuala ya teknolojia kama Bobby, na ni yeye ndiyo alitoa wazo hilo walilokuwa wakilifanyia kazi. Walitaka kujua ziko wapi hizo server ambazo Mess Makers walitumia na kama wangezipata, basi wangewapata wao.
Lakini kiukweli ilikuwa ngumu sana kufanikiwa katika hili kwa sababu ni kama Torres aliweka ukuta wenye nguvu sana kwenye mitambo yake ili usiweze kuvunjwa kirahisi. Mara zote ambazo timu ya Luteni ilikuwa ikikaribia kupata sehemu (location) yao, Torres angegeuza upande waliokuwa kwa kuwachanganya sana. Wangeona mara server hizo ziko Sweden, wakati huo huo ziko Sumbawanga, mara Cairo, yaani walishindwa kujua ipi ni halisi na ipi ni ya uwongo. Chanzo kikuu cha mitambo yake Torres alikificha kwa ustadi sana, ustadi ambao ulikuwa mtata sana kwa wataalamu hawa wa kijeshi kuufikia.
"Mmepata lolote lingine?" akauliza Luteni Michael.
"Hapana. Hizi zingine zinazojitokeza sehemu nyingi zinachanganya bado. Siyo rahisi kugundua ipi ni original au fake maana...." Manengo akaishia tu hapo.
"Kwa hiyo jamaa na wenyewe wamekuwa kama Cypher?" akasema Mario kiutani.
"Cypher ndiyo nini?" akauliza Luteni Michael.
"Ni kwenye... Fast and Furious..."
"Fast and Furious ndiyo nini?" Luteni Michael akauliza kiukali.
Wanajeshi wengine wakabaki kumtazama tu. Mario akabaki kimya.
"Luteni, alikuwa anatania tu," Bobby akamwambia.
"Sihitaji masihara kwenye kazi. Inaeleweka?" Luteni Michael akasema.
"Ndiyo mkuu," akajibu Mario.
"Labda mtu anayekuwa anawapa info hayuko nchini. Maana tungekuwa tumeshaikamata engine yao mapema sana," Aliyah akasema.
"Labda hata Marekani?" akauliza Mario.
"Labda hata Ujerumani," akasema Alex.
"Au labda ni mtu fulani tu anatuzunguka hapa hapa. Bobby... unamkumbuka yule dada aliyekuja humu siku ile?" Luteni Michael akamuuliza.
"Dada?" Bobby akauliza pia.
"Yule rafiki yake na ACP?" akauliza Alex.
"Ndiyo. Yule mwanamke siyo. Kuna jambo fulani kuhusu yeye ambalo haliko sawa. Kama vile anajua kitu, au anaficha kitu," akasema Luteni Michael.
"Ndiyo nani?" Rachel akauliza.
"Ni rafiki yake ACP Nora Lois. Lakini Luteni, anahusianaje na mambo haya sasa?" Bobby akamuuliza.
"Huyo mwanamke mara ya mwisho kuonana naye ameni-challenge kabisa. Ananiambia nijaribu kumpiga kama naweza!" Luteni Michael akasema.
Wengine wakaanza kuangaliana kimaswali, isipokuwa Hussein, ambaye muda wote alikuwa anatazama sehemu moja.
"Kisa?" akauliza Alex.
"Mwanamke kukupa challenge inamaanisha ni mmoja wa Mess Makers?" akauliza Zachary.
"Siyo hivyo. Fikiria mara ya kwanza alikuja tu humu na kuingia... bila kuogopa chochote akaingia ndani humu. Ndiyo hiyo siku tulikuwa tumempata Oscar Amari, halafu ghafla kuna watu huko wakatokea kumsaidia. Unadhani walijuaje kwamba tungemfata?" Luteni Michael akasema.
"Kwa sababu wana njia zao nyingi hawa jamaa... kama ilivyokuwa Mwanza," akasema Alex.
"No, Alex. Mwanza Kevin Dass aliwasha tracker baada ya kutuona, na hata wenzake wakaja baadaye sana. Huyu Oscar hakuwa na njia ya kujua tumeanza kumfata isipokuwa kuwe na mtu alimwambia mpaka kufanya wenzake wafike kabla hatujamshika. Think," akasema Luteni Michael.
"Kwa hiyo... huyo mwanamke... alipofika hapa aliona picha ya Oscar, akaenda kumwambia... labda kwa njia fulani lakini siyo simu, si ndiyo? Kwa hiyo yuko na Nora ili kupata taarifa muhimu kutoka kwetu, ndiyo unachosema Luteni?" Bobby akamwambia.
"Ndiyo ninachofikiri. Nyie mnaonaje?" Luteni Michael akawauliza.
"Inawezekana ikawa kweli. Kwa nini kwanza mliruhusu mtu aingie humu?" Tariq akaongea.
"Kaliingia tu utafikiri ni kwake humu. Nani anakakumbuka sura vizuri? Eeh? Alex?" Mario akauliza.
Alex akatikisa kichwa kukataa.
"Bobby?"
Akakataa pia.
"Hussein?"
Kimya.
"Oya, vipi?" Mario akamuuliza.
"Eeh? Yah... yeah namkumbuka... lakini mkiniambia tumchore siwezi," Hussein akajibu huku akiendelea kutazama sehemu ile akiwa anachezea ndevu zake laini taratibu.
Mario alipomtathmini vizuri, akatambua Hussein alikuwa analitazama kalio kubwa kiasi la Aliyah lililokuwa ndani ya suruali ngumu ya kardet, naye Aliyah alikuwa ameshatambua hilo ila akawa anapuuzia tu. Mario akatikisa kichwa kwa kukerwa.
"Hatuna muda wa kuanza kuita mchoraji. Manengo, search simu ya ACP utafute namba yenye jina 'Lexi,' kisha check usajili wa mtu huyo uangalie background zake zote. Naenda nje mara moja," Luteni Michael akasema huku akinyanyuka.
"Lakini Luteni... ACP... sidhani atafurahi kujua ikiwa..." Bobby akasema.
"Kwani ni lazima ajue?" Luteni Michael akauliza.
Wote wakakataa.
"Fanya hivyo. Mario, Hussein, mko nami," akasema Luteni Michael huku akiondoka.
Manengo akaanza upesi kazi aliyopewa. Mario akaanza kumfata Luteni Michael, naye Hussein akawa anarudi kinyume-nyume huku anamwangalia Aliyah. Aliyah alikuwa anamtazama pia kwa njia ya kutopendezwa, naye Hussein akamrushia busu kwa ishara ya mdomo huku akiwa amelegeza macho. Hii ikafanya baadhi ya waliobaki hapo kucheka kidogo, huku Aliyah akitabasamu kwa mbali na kutikisa kichwa.
"Hivi huyo jamaa anakuwaga makini kweli?" Zachary akauliza.
"Achana naye huyo, masihara huwa ndiyo fani yake," Bobby akasema.
"Hussein anaonekana kupenda sana masihara. Angalieni isije ikawa-cost," akasema Rachel.
"Yeah, toka tumefika amekuwa akifanya vitu kama teenager. Ana miaka mingapi?" akauliza Zachary.
"Acha kujaji sana Zach," Tariq akaongea.
"Ndiyo fani yake," Manengo akasema kiutani.
"Ana miaka 32. Na hapana.
Mambo anayofanya ni sehemu tu ya utu, ila kikazi yuko vizuri mno. Hussein naweza kusema labda ndiyo kijana makini zaidi kuliko wote humu ndani," Alex akamwambia Zachary.
"Kweli?" Rachel akauliza.
"Yeah. Baada ya kujuana naye vizuri mtaona hilo," akasema Alex.
"Siyo fair kwa Mario kutania ila ni fair kwa Hussein kutania, ndiyo unachosema?" Aliyah akauliza.
"Hamna. Luteni kuna kitu tu kinamsumbua. Huwa hayuko hivyo sikuzote. Amekuwa namna hiyo tokea...." Alex akaishia tu hapo.
"Tokea vifo vya wenzenu... inaeleweka. Naomba tusizungumzie hayo tena. Ila Aliyah sasa hivi una kupe mkiani kwa hiyo kuwa macho," Tariq akaongea kwa utani.
Wengine wakacheka kidogo, wakijua alimaanisha Hussein.
"Anyway, tunaweza kuendelea na mambo mengine...." akasema Bobby.
Wanajeshi hawa wakaungana na Manengo katika utafiti wake mpya.
★★★
Lexi pamoja na Nora walielekea katikati ya jiji kutafuta viburudisho mbalimbali. Nora alifurahia kwelikweli uwepo wa Lexi karibu yake. Walikwenda kupata msosi wa nguvu pamoja, wakaangalia mechi ya alasiri pamoja, kisha wakaamua kwenda 'supermarket' ili kununua vitu vingi kwa ajili yao wote. Kwa wale ambao wangewaangalia, waliwaona kama dada wenye undugu tu wakiwa kwenye matembezi, lakini ndiyo walikuwa kwenye mwanzo wa pendo lao jipya.
Wakati wawili hawa walipokuwa wakielekea sehemu ya malipo kwenye supermarket hiyo, walikuwa wakiongelea mambo mengi yenye kufurahisha sana, na Nora alishindwa kujizuia kucheka mno kwa jinsi Lexi alivyokuwa na story nyingi za kuchekesha. Wakawa wamefika kwenye meza ya mahesabu, na mhudumu akawa anatoa bidhaa kupima bei (wanajua wenyewe wanavyofanyaga), huku Lexi akimsimulia Nora vichekesho fulani.
"Ahahahah... kwa hiyo hakurudi tena?" akauliza Nora.
"Hakuonekana kabisa!" Lexi akasema.
"Okay. Nyingine..."
"Mh... mheshimiwa haujachoka kucheka?" Lexi akauliza.
"Aahh... bado..."
"Ahahah... okay. Aam... kulikuwa na mwalimu mpya wa dini aliyehamia kwenye shule nyingine katikati ya muhula. Alipewa darasa la 6... nafikiri, ili afundishe hilo somo. Kwa hiyo kwenye kipindi chake cha kwanza akataka kujua wanafunzi walikuwa wanajua mambo mengi kadiri gani kuhusu mada walizojifunza kabla ya yeye kufika. Akaamua kuanza na mada ya mwisho ambayo mwalimu aliyepita aliishia kuwafundisha...."
"Mm-hmm..." Nora akamuasa kuendelea.
"Akawasalimu. Halafu akawauliza, 'Ni nani aliyeangusha kuta za Yeriko?'"
Nora akaanza kucheka kwa sauti ya chini kabla hata Lexi hajaendelea.
"Ahahah... ikapita dakika moja darasa zima likiwa kimyaaa. Wanafunzi wote walikuwa wanamwangalia tu. Kwa hiyo akachagua wale waliokaa madawati ya mbele waanze kujibu. Akaanza Amosi: 'Mwalimu mimi ni mgeni hapa, nilianza tu shule wiki iliyopita.' John: 'Mwalimu mi siku hizo kuta zilipovunjika sikuja shule, haki ya Mungu...'"
Nora akaendelea kucheka, na mhudumu yule wa mahesabu akawa anacheka pia.
Lexi akaendelea, "Mary akasema, 'Sir, mimi niliupita tu nikakuta umeshavunjwa, hata sikuugusa...'"
"Jamani..." Nora akasema huku akitabasamu.
Lexi akaendelea, "Mwingine akasema, 'Mwalimu yaani tena mimi ndo' kabisaaa hata sikujua kama umevunjika! Ndo najua sahivi.' Mwalimu akashangaa sana na kukasirika mno. Akaenda kwenye ofisi ya mkuu kumweleza kilichotokea. Mkuu akamwambiaje, 'Pole sana kuhusiana na hilo. Unajua watoto walivyo watukutu saa nyingine wanakuwa wanaharibu tu vitu vya watu afu wanakataa. Lakini usihofu, tutalitatua suala hili. Andika tu gharama yote inayohitajika ili kuutengeneza huo ukuta, halafu kwenye kikao kinachofuata tutalizungumzia hilo suala na wengine.'"
Nora pamoja na mhudumu yule wakawa wanacheka.
"Mwalimu mkuu na yeye walewale tu," akasema Nora.
"Acha kabisa," Lexi akasema.
"Kwa hiyo ikawaje?" Nora akauliza.
"Teacher wa dini akaacha kazi siku hiyo hiyo!" Lexi akamwambia.
Nora akacheka tena.
"Hiyo ni nzuri sana. Niliisomaga zamani sijui wapi..." yule mhudumu akawaambia.
"Eeh.. mimi pia. Kwenye mavitabu ya jokes... ya kiingereza," akasema Lexi.
"Eee ndiyo, ya kiingereza," mhudumu akahakikisha.
"Ahahah... basi mimi sikuwahi kufuatilia sana jokes yaani... sikujua ni nzuri sana mpaka...."
Nora alipokuwa anaendelea kuongea hivyo, Lexi akahisi nguo yake inavutwa kwa nyuma, naye akageuka upesi akifikiri kuna mtu anataka kumwibia. Lakini hakukuwa na mtu mzima hapo, bali msichana mdogo aliyekuwa anamwangalia kwa makini. Lexi akatabasamu na kuchuchumaa, akimtazama kirafiki. Nora alipomwangalia Lexi na msichana huyo, akakunja uso wake kimaswali.
Msichana huyu alikuwa amevalia gauni la mtindo wa jeans ya samawati, ambalo liliishia magotini, na viatu vya rangi ya pink vyenye manyoya. Alikuwa mweupe, na nywele zake zilisukwa kwa mtindo wa mabutu makubwa kuzunguka kichwa chake. Kwa kumwangalia, kadirio la umri wake ingekuwa ni kati ya miaka mitano mpaka saba. Kilichomshangaza Nora ni kwamba macho ya msichana huyo yalifanana kabisa na macho ya Lexi, lakini Lexi hakuwa ametambua hilo.
"Hi, mambo?" Lexi akamsalimu.
"Poa," akajibu msichana huyo.
"Nambie mrembo. Umekuja kununua nini?" Lexi akamuuliza.
"Soseji, sneakers, diapers, na mavitu mengi," akajibu.
"Ahahahah... hizo diapers ni kwa ajili yako?" Lexi akauliza.
"No. Ni za mama," kakajibu na kuwafanya watatu wale wacheke.
"Mama yuko wapi?" Nora akauliza.
"Yupo huko... najificha asinione," akajibu.
"Kwa hiyo unamsumbua mama yako makusudi ili akutafute?" Nora akauliza.
"Ndiyo. Mpaka aninunulie ice cream," kakajibu.
"Aaaa... hapo umefanya la maana," Lexi akamwambia.
"Dada, unafanana na huyo mtoto, ni ndugu yako?" mhudumu wa mahesabu akamuuliza Lexi.
"Nini?" Lexi akauliza.
"Nilifikiri ni mimi tu labda, kumbe na wewe umeona?" Nora akaongeza.
"Ndiyo, mnafanana," mhudumu akamwambia tena Lexi.
Lexi akatabasamu tu na kumwangalia huyo mtoto. "Eti ni kweli tunafanana?" akamuuliza kirafiki.
"Ndiyo. Mama aliniambia umekufa lakini leo nimekuona," mtoto huyo akajibu.
Lexi na Nora wakakunja sura zao kimaswali. Wakaangaliana kama kuulizana mtoto alikuwa anaongea nini huyu, kisha Lexi akamtazama tena msichana huyo.
"Unaitwa nani?" akamuuliza.
"Alexa," mtoto akajibu.
Lexi akashangaa.
"Alexa? Jina lako linataka kuendana kidogo na la huyu. Anaitwa Lexi. Alexa na Lexi," Nora akamwambia kwa shauku.
Lexi akawa bado anamwangalia mtoto huyo kimaswali.
Simu ya Nora ikaanza kuita, naye akasogea pembeni kidogo kupokea. Mhudumu wa mahesabu akamwambia Lexi gharama ya vitu walivyonunua, naye akanyanyuka ili alipie. Lakini, kutokea nyuma yake, alianza kusikia sauti ya mwanamke ikiita jina la 'Alexa,' naye Alexa akacheka kidogo na kujificha karibu na miguu ya Lexi; akiing'ang'ania. Lexi alikuwa ameangalia mbele tu, kwa sababu ya mapigo yake ya moyo kukimbia kwa kasi sana baada ya msisimko mkubwa kuuvaa mwili wake. Aliifahamu sauti hiyo vizuri sana.
"Hivi wewe, nimeshakwambia nini kuhusu... mmm?"
Mwanamke huyu akasikika akiongea hivyo nyuma ya Lexi, naye Alexa akawa anacheka huku akimpiga chenga kwa kwenda huku na huku usawa wa miguu ya Lexi.
"Dada samahani sana... watoto kama ujuavyo..."
Mwanamke huyo akamwambia Lexi hivyo akihofia labda hakupenda mchezo aliokuwa anafanya Alexa. Lakini Lexi alipogeuka tu kumtazama, mkoba aliokuwa ameushika mwanamke huyu ukamponyoka kutoka mkononi mwake na kudondoka chini, akiwa anamwangalia Lexi kwa mshangao. Lexi alikuwa anamtazama kwa umakini sana, huku machoni chozi likijaa haswa, na mwanamke huyo akaonekana akianza kutetemeka midomo.
"Ss... Xander?!" mwanamke huyo akaita kwa sauti yenye kutetemeka.
Lexi akadondosha chozi huku akihisi mkono wake umeishiwa nguvu.
"Valentina," Lexi akasema kwa hisia.
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Comments