Reader Settings

FOR YOU 3

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA TATU

★★★★★★★★★★★


Kutokana na maelezo kuhusu Khalid Juma ambayo Torres alikuwa amewapatia, Lexi, LaKeisha na Victor wakaunda mpango mdogo tu wa kuweza kumnasa mtu huyo. Kama ni kitu ambacho watu kama Khalid walipenda, basi ilikuwa ni starehe na wanawake. Torres alikuwa amemsoma na kujua kuwa alipenda sana kwenda sehemu za starehe pamoja na marafiki zake wa jeshini, na mara nyingi walichukua wanawake kwa ajili ya kujitumbuiza. Kwa siku za karibuni mwanaume huyo hakuwa akienda sehemu aliyozoeleka, lakini bado angetafuta wanawake wa kujifurahisha pamoja nao.

Lexi alitaka kujua kwa nini mtu wa namna hiyo aliyejiachia kipuuzi tu angepewa "mission" ya kumwongoza muuaji hatari sana kwa helicopter. Huenda labda ilikuwa ni yeye tu ndiye aliyejua kuongoza helicopter, au katika kundi la wanajeshi waliotumiwa kufanya maovu ya Jenerali Jacob na Weisiko na yeye alikuwemo, na hivyo alijiamini kupita kiasi. Kwa vyovyote vile, siku ya leo isingekwenda vizuri kwake kwa sababu hiyo hiyo ya kujiachia sana.

Ikiwa imeshafika usiku, Mess Makers walipata kujua kwamba sasa Khalid Juma alikuwa amekwenda kwenye kumbi moja kubwa ya starehe, ambapo wengi wa "marafiki" zake walikuwepo pia. Wangechezewa dansi na wanawake waliovaa nusu utupu kwenye zile sehemu za watu muhimu zaidi (VIP), kisha wangechagua mwanamke wa kutoka naye ili kwenda kula bata, yaani bata.

Mpango rahisi wa Mess Makers hapa ulikuwa ni LaKeisha. Dada aliingia kwenye kumbi hiyo, akiwa amevalia nywele za wigi jekundu, na akiwa na mwonekano wenye kuamsha hisia sana. Alikwenda mpaka sehemu iliyoelekea kwa ma-VIP, lakini akazuiliwa kupita. Ila baada ya mmoja wa wanaume waliokuwa huko kumwona jinsi alivyokuwa mrembo, akawaambia mabaunsa wamruhusu apite, naye akaenda hapo na kuanza madoido sasa.

Kulikuwa na wanawake kadhaa hapo wakicheza na wengine wakiwa wamewakalia wanaume hao, naye LaKeisha akaanza kucheza pia. Siyo kwamba wengine walikuwa hawachezi vizuri, lakini LaKeisha alikuwa mtaalamu sana. Alikuwa anatumia mitindo mingi iliyowavutia wanaume hao, mitindo ya Ghana huko, na wengi wakawa wanamwangalia kwa matamanio. Baada ya karibia wanaume wote hapo kuonyesha kumtaka, yeye LaKeisha akamchagua Khalid Juma, ambaye alifurahi kupita maelezo. Mwanamke alimchezea mwanaume huyo mpaka akawa anamwaga tu hela kama kichaa vile, lakini LaKeisha hakujali pesa.

Lakeisha akaonyesha wazi kwamba alitaka watoke, naye Khalid hakukwaza. Akanyanyuka na kutoka naye sehemu hiyo ili waelekee kwenye vyumba, lakini LaKeisha akamwambia alitaka waende sehemu tofauti na kumbi hiyo ili ampe burudani bila makelele ya watu wengine. Khalid hakupinga, naye akatoka pamoja na "bebe" wake mpya na kwenda mpaka kwenye gari lake, na safari kuelekea kwenye hoteli ikaanza. Njiani LaKeisha alikuwa anamwambia Khalid maneno mengi yenye kusisimua, huku sikioni mwake akiwa na kifaa kidogo cha sauti kilichounganishwa kwa Lexi na Victor, ambao walikuwa wanasikia kila kitu anachosema ili kujua walikuwa wamefika wapi.

Baada ya mwendo wa dakika chache, gari la Khalid lilifika sehemu ya barabara isiyokuwa na makazi kwa pande hizo na kukanyaga kitu kama msumari kilichosababisha pancha. Ikabidi wasimame kwanza, naye Khalid akamwambia Lakeisha angeenda kubadili tairi upesi. Lakeisha akamwambia angemsaidia, hivyo wote wakashuka na kurudi mpaka nyuma ya gari. Lakini wakati tu Khalid alipotoa tairi, akashtuka sana baada ya kugeuka na kukuta watu wengine wawili waliovalia nguo nyeusi mwili mzima, na vitu usoni vilivyoficha nyuso zao, huku mmoja akiwa amemwelekezea bastola. Ilikuwa ni Victor na Lexi, na Victor akiwa ndiyo ameishikilia bastola akamwamuru Khalid anyooshe mikono yake juu.

LaKeisha akaanza kujifanya kuogopa, akimng'ang'ania Khalid huku anatetemeka eti, naye akamuuliza wangefanya nini. Khalid akamwambia asiogope kwa sababu hao wahuni hawakujua yeye ni mwanajeshi, hivyo angejifanya kuwatii halafu angewazunguka haraka na kuwadhibiti. Victor akarudia kumwambia anyooshe mikono yake na kugeukia gari, naye Khalid akafanya hivyo. Victor akaigiza kumwambia LaKeisha kwa ukali kwamba akimbie haraka sana la sivyo angemfyatua kwa risasi, lakini Khalid akajifanya mkaidi na kugeuka nyuma huku akiwaambia wawili hao kwamba kama walitaka pesa basi angewapa, lakini wasimuumize mpenzi wake. LaKeisha akazungusha macho kikejeli, kisha akaendelea kujifanya anaogopa.

Lexi akaushusha mkono wa Victor ulioshika bastola, naye akaanza kumfata Khalid. Akakunja ngumi kuonyesha anataka wapigane, naye Khalid akakunja ngumi kwa kujiamini na kumwambia LaKeisha kwa sauti ya chini angewashughulikia wote kwa zamu kisha wangeondoka, hivyo asiwaze. Yaani walikuwa wanamfanya jamaa kuwa mpumbavu sana, kwa sababu pale tu alipomfata Lexi ili kumpiga, Lexi akamzunguka na kumpiga kwa mtindo mmoja tu uliofanya jamaa apoteze fahamu. LaKeisha na Victor wakaanza kucheka, kisha Victor akamsaidia Lexi kumfunga Khalid mikono na miguu kwa kamba ngumu, na mdomo na macho yake pia kwa kutumia kitambaa, halafu wote wakasaidizana kumweka kwenye buti la nyuma la gari walilokuwa wameegesha upande wa pembeni kwa kificho.


★★


Wakaondoka eneo hilo na kumpeleka sehemu ya mbali iliyokuwa na msitu wenye giza zito, nao wakamtoa na kumkalisha kwenye kiti cha chuma walichokuwa wamekiweka huko tayari. LaKeisha alikuwa ameshavua nguo zile zilizomfanya aonekane kama anajiuza. Kuigiza kwao kwamba LaKeisha hakujuana nao ilikuwa ni kwa sababu Khalid alikuwa ameiona sura yake. Hivyo ilitakiwa ionekane kwamba LaKeisha kweli alikuwa mtu wa kawaida tu, ili hata wakimwachia Khalid baadaye basi asifikiri LaKeisha alikuwa mmoja wao.

Baada ya sekunde chache, Khalid akarejesha fahamu na kujikuta akiwa amefungwa huku ameketi sehemu asiyokuwa na utambuzi kuihusu. Bado macho yake yalifunikwa kwa kitambaa, lakini kutokana na upepo mkali na baridi alilohisi aliweza kutambua kwamba wako nje. Akaanza kusikia hatua zikimkaribia, na hofu yake ikapanda kwa kiasi fulani. Akahisi mdomo wake ukitolewa kitambaa kilichomfunga, naye akawa anapumua kwa kasi.

"Nyie ni akina nani? Mnataka nini?"

Khalid akauliza hivyo kwa sauti ya chini. Hakupata jibu lolote, lakini akasikia sauti za vitu kama cheche karibu yake.

"Hey! Nimewauliza nyie ni nani? Mnataka nini? Yule mwanamke mmemweka wapi?" Khalid akauliza tena.

"Tumemuua," Victor akajibu.

"Nini? We' ni nani? Kwa nini mmemuua mwanamke asiye na hatia?"

Swali hilo la Khalid likamfanya Lakeisha acheke bila kutoa sauti huku akimwonyesha Lexi kwa ishara kwamba eti ameguswa sana.

"Alikuwa hana hatia? Au ndiyo ulikuwa unaenda kumfanya awe na hatia?" Victor akauliza.

"Nini? Wewe unataka nini? Niambie kama ni pesa nikupe," Khalid akasema.

"Sihitaji pesa. Ninachotaka ni kukuua wewe..."

"Nini?!" Khalid akauliza huku pumzi zake zikipanda.

"Nataka kuikatakata miguu yako kwanza, halafu mikono yako. Nikimaliza nakatakata milango yako yote ya fahamu, na nikisema yote namaanisha hadi ngozi naichuna, na hapo bado utakuwa haujafa. Nataka ufe huku unahisi kabisa kwamba unakufa," Victor akamalizia.

LaKeisha akawa anacheka huku ameziba mdomo.

"Wewe! Wewe ni nani? Mimi ni mwanajeshi, unajua utaumia sana ndugu yangu kwa huu upuuzi, ni bora uniachie sasa hivi!" Khalid akatoa kitisho.

"Aaa... kwa hiyo unafikiri nakutania eeh?" Victor akauliza.

Kisha akamfanyia ishara Lakeisha, ambaye akasogea karibu na hapo huku akiwa ameshika kifaa kimoja cha kukatia chuma, kisha akakiwasha. Sauti ya jinsi kilivyozunguka kwa kasi ikamfanya Khalid ahofie sana. Akaanza kujivuta-vuta kwa woga.

"Wewe... nyie... subiri... mnataka kuniua kwa nini? Nimewafanya nini?" Khalid akauliza huku anababaika.

"Nataka uniambie ni kwa nini ulimuua Salim," Victor akasema.

"Nini? Salim gani?"

"Huyo huyo gani..."

"Mimi sijui unachokiongelea. Haloo... nakuombeni..."

LaKeisha akasogeza mashine hiyo karibu zaidi na sikio la Khalid ili kumtisha, naye Khalid akaogopa sana na kujaribu kufurukuta, lakini Victor akakishikilia kiti alichokalia kwa nguvu.

"Kwa nini ulimuua Salim?" Victor akauliza kwa ukali.

"Sijamuua!" Khalid akasema kwa hofu.

"Kata hilo sikio!" Victor akaongea.

"Subiri, subiri, subiri, subiri... sijamuua Salim mimi. Sikumuua mimi..."

"Alimuua nani?"

"Ni... ni Luteni...."

"Ongea!"

"Ni Luteni Jenerali Weisiko. Weisiko," akasema Khalid.

"Acha kumsingizia Weisiko. Ni wewe ndiyo uliyeenda na kumnyonga Salim. Sasa tutakuonyesha kifo kibaya zaidi ya hicho," Victor akaongea kwa kitisho.

"Hapana, hapana, ni Weisiko... siyo Weisiko yaani... ni Weisiko ndiyo alitutuma, lakini mimi sikumnyonga. Ni yule anayemwita silaha yake... huyo ndiyo alimnyonga..." Khalid akasema.

"Silaha yake? Nani, Black Widow?" Victor akauliza kama vile hajui.

"Sijui... si..si... sijamwona sura. Mimi nilimpitia tu na kumpeleka pale kama nilivyoambiwa, basi," Khalid akasema.

Victor akamtazama Lexi, naye Lexi akamwonyesha kwa ishara ya kidole kuwa aendelee.

"Kwa hiyo... mkajiunga ili kumuua boss wetu, si ndiyo? Sasa tunaanza na wewe, halafu tunamfata na huyo mtu wako!" Victor akamwambia.

"Hapana, sikia... mimi ninafuata maagizo tu ndugu yangu. Ninafuata amri, siyo kwamba ninapenda..."

"Siyo kwamba unapenda? Mmewaua watu nyie halafu mnawasingizia wengine mkafikiri hatutajua? Yaani leo tunaondoka na viungo vyako vyote vikiwa vimeachana..."

"Hapana, msiniue! Tafadhali jamani, nina familia..."

"Sikuzote mkiwa kwenye matatizo ndiyo mnakumbuka familia, nyau nyie!"

"Nawaombeni jamani! Nitafanya chochote kile lakini msiniue... tafadhali...." Khalid akaendelea kuomba.

"Sawa. Kama ni kweli haikuwa wewe uliyemuua, basi tuambie aliyemuua yuko wapi, labda ndiyo tutakuacha," Victor akamwambia.

Khalid akaanza kuwaelezea tu jinsi siku hiyo alivyopewa maelekezo ya kuipeleka helicopter mpaka juu ya nyumba fulani ya kifahari iliyokuwa imejitenga kwenye eneo fulani, na baada tu ya kutua, mtu huyo asiyefahamika aliingia kwa nyuma, kisha ndiyo akaipeleka helicopter kwenye jengo lile alikomuua Salim Khan. Akasema alipewa maelekezo ya kuwa makini sana na baada ya kumaliza jambo hilo aipeleke helicopter sehemu ya mbali ili iweze kuharibiwa huko. 

Alipoulizwa aliahidiwa kulipwa pesa kiasi gani, akasema tayari alikuwa ameshalipwa, kwa sababu alikuwa amefanya kazi nyingi haramu kwa ajili ya Weisiko kwa muda mrefu na hivyo aliwekwa kuwa kama mtu wa muhimu kwa ajili ya mishe za namna hiyo. Kwa hiyo wakati wowote ambao angehitajika basi angewajibika. Akawaambia ikiwa Weisiko angejua amemchongea namna hii, angeuawa. Victor akamwambia tu ampe maelekezo ya ni wapi nyumba hiyo ilipokuwa kwa usahihi, naye akamwahidi wakishamkamata mtu yule aliyemuua Salim basi wasingemuua yeye, na hata Weisiko asingejua. 

Khalid akawapa maelekezo ya ni wapi nyumba hiyo ilipokuwa, na baada ya hapo Lexi akawapa ishara wenzake wamfunge Khalid kwa bomu dogo la bandia walilokuja nalo, halafu Victor akamdanganya Khalid kwamba endapo angejaribu kutoka kwenye kiti hicho, basi bomu lingelipuka, kwa hiyo alipaswa kukaa hapo hapo mpaka warudi kuja kumtolea. Khalid aliwaomba sana wasifanye hivyo, lakini hii ilikuwa ni njia ya Mess Makers kuhakikisha hawampotezi mwanaume huyo wakati ambao wangekwenda kumtafuta Azra.

Wakatoka hapo na kumwacha akiwa ameketi kwenye kiti usiku katikati ya msitu huo mdogo, nao wakawasiliana na Torres na kumpa taarifa mpya waliyopata, ambaye akaanza kuwaongoza vizuri kuelekea kule kwenye nyumba hiyo waliyotumaini kumkuta Azra.


★★★


Siku hii haikuwa na mambo mengi sana upande wa Azra. Kutokea asubuhi, alikuwa ndani ya nyumba yake tu akifanya mambo ya hapa na pale yenye kuburudisha kiasi ili kupoteza muda. Alikuwa akihisi upweke wa hali ya juu, na hii hasa ilitokana na yeye kutokuwa na mtu wa kuzungumza naye kuhusu hisia zake.

Tokea alipofanikiwa kuwatoroka Mess Makers usiku wa jana, tena kwa msaada wa mmoja wao, alikuwa hajaondoka kwenye nyumba hiyo kabisa. Mara chache ambazo Weisiko alifika hapo ili kumpa ushirika wake hazikuondoa hisia nzito za majuto alizokuwa nazo moyoni, zilizomfanya ahisi ni kama amebeba mzigo mzito sana. Alijiona kuwa kama adui wa dunia yote iliyomzunguka, kwa kuwa alishinikizwa kufanya mambo mabaya yasiyokuwa na faida yoyote kwake, na hivyo kuhisi labda anastahili kuwa mwenyewe tu.

Kama ni jambo ambalo liliendelea kuzunguka akilini mwake, basi ni kitendo ambacho "mwanamke" aliyepambana naye usiku ule alifanya. Kutokea mara ya kwanza kabisa walipopigana, Azra alikuwa akijiuliza ni mafunzo ya aina gani ambayo mwanamke yule aliyapata mpaka kuzidi ya kwake yenye ubora zaidi, lakini sasa kilichosumbua akili yake kuhusu mwanamke huyo ilikuwa ni kwa nini aliokoa maisha yake baada ya kujaribu kuyaondoa mwanzoni. Kuna hisia fulani zilijijenga kwake, hisia ambazo zilikuwa ngeni kabisa kwake, lakini hakujiruhusu zimpoteze, kwa kuwa alifunzwa kutoruhusu jambo lolote limfanye kuwa dhaifu. Akajihakikishia kwamba endapo angekutana naye tena, basi asingesita kummaliza kabisa kwa sababu alikuwa ameanza kuwa tatizo kwake.

Wakati huu alikuwa amekaa tu kwenye chumba chenye TV kubwa sana, akitazama katuni ya Tom and Jerry, ambayo ilikusudiwa kufurahisha sana mtazamaji, lakini yeye hata kutabasamu hakutabasamu. Alikuwa tu anakula chips zilizokaushwa taratibu akiwa ameboeka sana, na baada ya kuangalia muda, akakuta ni saa 7 usiku tayari. Akaamua tu kuzima na kwenda kuutafuta usingizi kitandani.

Makao yake haya yalikuwa makubwa kweli, lakini ni yeye peke yake ndiye aliyekuwa ndani ya nyumba. Eneo la nje lililindwa na wanaume maalum wa jeshi waliowekwa na Weisiko, lakini hakuna hata mmoja kati yao aliyeruhusiwa kuingia kule ndani. Hivyo kumwona binti huyu ilikuwa ni mpaka wakati alioamua kutoka kwenda "misele" mara moja moja sana, lakini walinzi hao hawakuwahi hata kumsemesha "mtoto wa boss."

Baada ya Azra kupanda kitandani na kuanza kutafuta usingizi, haikumchukua dakika nyingi sana naye akawa ametambua kuwa kuna jambo halikuwa sawa. Ilikuwa ni kama machale yake tu ndiyo yalimwambia hivyo, kwa sababu kwa mtu wa kawaida asingefikiria kulikuwa na tatizo lolote hapo kutokana na utulivu wa hali ya juu uliokuwepo. Akajinyanyua na kuketi, akiwa amevalia tu T-shirt nyeusi na kikaptura chepesi kilichoishia mapajani, na udadisi wake ukamfanya anyanyuke na kuchungulia nje kutokea kwenye dirisha pana la chumba chake kilichokuwa kwenye ghorofa. Alitazama mazingira ya hapo nje, na kwa uhakika akawaona walinzi wakiwa wanazunguka kwa zamu kulinda eneo la nyumba.

Akaamua kurudi kitandani tena, lakini bado akawa haupati wepesi wa amani kwenye machale yake. Akajiuliza ni kwa nini, naye akatoka kitandani ili aelekee sehemu za chini ya ghorofa hilo kuangalia kama kuna jambo halikuwa sawa. Alishuka ngazi na kuzunguka huku na huku, kukiwa na giza lakini mambo mengi yakionekana vizuri kutokana na mwanga hafifu wa taa za nje, naye akakosa jambo lolote lenye kutia mashaka.

Akaamua kurudi juu tu ili alale, na ile alipofika usawa wa korido pana lililoelekea mpaka kwenye chumba chake, akahisi mtu akitokea upande huo wa ukuta na kutaka kumshambulia, na kwa kasi akajirusha sarakasi na kuangukia upande mwingine. Alipojinyanyua ili amwone adui, akahisi kitu fulani kikimchoma kwenye shingo yake kutokea kwa nyuma, na kwa kasi akageuka na kumtandika mtu aliyemchoma kwa mtindo wake wa kumaliza nguvu, kisha akajiviringisha upande mwingine na kuzikaribia ngazi. Akajaribu kunyanyuka lakini nguvu zikaanza kumwishia na kusababisha ashindwe kusimama vyema, naye akawaona watu wawili waliovaa nguo nyeusi wakiwa wamesimama mbele yake, huku mwingine akiwa amepiga goti chini pembeni.

Hao walikuwa ni Lexi, Lakeisha na Victor. Tayari walikuwa wamefika hapo na kufanikiwa kuingia kwenye nyumba bila kutambulika, na ni Victor ndiye aliyemchoma Azra kwa sindano yenye dawa ya kulewesha baada ya LaKeisha kumzubaisha Azra kwa kujaribu kumshambulia. Azra akadondoka chini akiwa amejishika shingo, na ilikuwa kidogo tu aanze kudondoka kuelekea chini ya zile ngazi, lakini akahisi mkono ukimshika na kumvuta ili kuzuia hilo. Akiwa anahisi kichwa chake ni kizito sana, akawa anaangalia juu na kumwona mtu aliyemshika mkono, naye akatambua ilikuwa ni yule mwanamke aliyepanga kummaliza endapo wangekutana tena, yaani Lexi. Giza zito likafunika macho yake, naye akapitiwa na usingizi bila kupenda.

Lexi alikuwa ameshaitoa 'mask' yake wakati alipomfata Azra kuzuia asianguke kwenye ngazi, naye akamshika usoni huku akimwangalia kwa huruma.

"Damn! How does she do this? (hivi huwa anafanyaje hivi?)"

Victor akaongea hivyo akiwa amekaa chini sasa. Alikuwa analalamika kwa sababu mkono wake ulikuwa umekufa ganzi kabisa baada ya Azra kumpiga muda mfupi nyuma, naye akawa anashindwa kuunyanyua mpaka kutumia mwingine.

"Shh! Punguza sauti, walinzi nje," LaKeisha akanong'oneza kwa tahadhari.

"We gotta go (tunahitaji kwenda)," Lexi akasema.

"Tunamtoaje sasa huyo akiwa amelala, unajua jinsi ilivyokuwa ngumu kuingia hapa," Victor akasema.

"Tunatoka kama tulivyoingia," akasema LaKeisha.

"Nimevunjika mkono, sitaweza kuning'inia," Victor akasema.

"Basi utabaki," LaKeisha akamwambia huku akienda kumsaidia Lexi kumnyanyua Azra.

"Victor get yourself together, we don't have much time (Victor, jisawazishe vizuri, hatuna muda mwingi)," Lexi akamwambia.

Victor akasimama na kuanza kuwaongoza wengine kuelekea juu kabisa ya ghorofa hilo, Lexi na Lakeisha wakiwa wamembeba Azra. Walikuwa wametumia nyaya nene za nguzo kuingia hapo, ambazo zilipita karibu kabisa na jengo hilo. Wakati walipokuja, walitumia mahesabu kwa umakini sana kujua muda uliofaa kupita juu ya nyaya hizo, yaani nyakati ambazo walinzi wangefanya mizunguko na kuipa mgongo sehemu hiyo, ndiyo wao wangepita. 

Lakini wakati huu walikuwa na mtu aliyepoteza fahamu, hivyo ingekuwa ngumu sana kumtoa hapo kwa njia waliyotumia kuingia. Kwa sababu walinzi wale walikuwa na silaha nzito, kutafuta njia chini kusingekuwa na faida, hivyo njia ingepaswa kuwa hiyo hiyo. Kwa hiyo baada ya kuwa wameongea na Torres, akawaelekeza cha kufanya, ingawa hakuwa na uhakika kwa asilimia zote kama wangefanikiwa.

Mpango ukawa kwamba, wawili wangepaswa kutoka hapo kama walivyoingia, lakini mmoja wao azikate nyaya zile na kuzifunga kwenye mwili wake pamoja na Azra, halafu waitumie kama kamba ya bembea kujitupia upande wa pili wa kuta za nyumba hiyo, ambako wenzao tayari wangekuwa wameshasogeza gari ili wakitua tu wawaingize na kuondoka upesi. Lilionekana kuwa moja kati ya njia ngumu sana ambazo wangetakiwa kuchukua, lakini Lexi akakubaliana nalo na kusema yeye ndiyo angejifunga pamoja na Azra, hivyo Victor na Lakeisha ndiyo watangulie.

LaKeisha pamoja na Victor waliliona kuwa wazo baya sana, kwa sababu kwa kukata nyaya huenda wangesababisha shoti ambayo ingewaua wawili hao wakijifunga kwa huo waya. Torres akasema wangepaswa kuifunga sehemu hiyo kwa nguo nyingi kabla ya kuizungushia kwenye miili yao, na walipaswa kuwa makini sana. Akawapa matumaini kuwa kwa kukata nyaya huenda hata umeme ungekata, hivyo ingepunguza nafasi ya walinzi kuwaona wakitumia nyaya kama bembea. Lexi akawaambia wenzake kuwa yote yangepaswa kufanywa kwa umakini, lakini matokeo wangepaswa kuyaacha mikononi mwa Mweza yote, kwa sababu asingeondoka hiyo sehemu bila Azra.

Kwa kuwa muda ulizidi kuyoyoma, LaKeisha akaharakisha kurudi ndani ya nyumba hiyo na kufata mashuka manne marefu kabisa, kisha akapanda tena mpaka kule juu. Bado alikuwa na kile kifaa chake cha kukata chuma, hivyo akampatia Lexi na kumsihi sana awe mwangalifu. Mkono wa Victor ulikuwa umeanza kurudisha nguvu, na baada ya kuona upande huo ukiwa umepitwa na mlinzi tayari kule chini, akarukia nyaya hizo na kuanza kuelekea upande wa nguzo, kwa njia ya kuning'inia na kuibana miguu yake kwa pamoja. Lexi na Lakeisha wakamwangalia mpaka alipofanikiwa kuifikia nguzo upande wa pili wa kuta zilizozunguka nyumba hiyo, naye akashuka huko chini bila kutambulika. Upesi akawahisha kwenda walipoliacha gari lao na kuingia kumsubiri LaKeisha.

Lexi na Lakeisha walibaki kule juu na kusubiri walinzi wamalize zamu ya pili ya kuzungukia upande huo, na baada ya kuondoka, LaKeisha akafuata kuzirukia nyaya na kuanza kuielekea nguzo mpaka na yeye alipofanikiwa kufika upande wa pili. Haingekuwa rahisi kuwaona kwa sababu palikuwa parefu na nguo zao nyeusi zilifanya wafichwe vyema kwa giza la huko juu, lakini kimbembe kingekuja kwa Lexi. Angehitaji kumbeba Azra, kujifunga kwa nyaya za umeme zilizokuwa hatari sana, na kubembea naye mpaka nje ya kuta za nyumba hiyo kama Tarzan.

Ingehitaji umakini wa hali ya juu kwa sababu kama angekosea mahesabu basi angeangukia ndani ya kuta hizo na siyo kule nje. LaKeisha akiwa ameshafika kwenye gari pamoja na Victor, akamjulisha Lexi, naye Lexi akasema akiwaambia tu waanze kulisogeza gari upesi mpaka upande ambao alitazamia kuangukia, basi wafanye hivyo haraka. Uwezekano wa kuonwa ulikuwa mkubwa sana, hivyo wangetakiwa tu kudondoka, kunyanyuka, na kuondoka.

Baada ya kujiweka sawa, Lexi akazirukia nyaya hizo akiwa ameshayafunga-funga mashuka yale kwa pamoja, naye akaanza kuyafungia karibu na sehemu aliyokusudia kuzikata. Wenzake walikuwa wametulia tu wakisikilizia mambo kama vile waliona kilichokuwa kinaendelea, na kiukweli ilikuwa ngumu sana kwa Lexi kufanya hivyo. Kwa kukadiria muda ambao walinzi wangepita upande huo, akajiachia kutoka huko juu na kuangukia ghorofani tena ili kujificha kwanza, na baada ya mlinzi kupita, akapanda tena na kukiwasha kifaa kile cha kukata chuma. Kilitoa sauti kali kiasi, hivyo akapitisha tu mkono wake haraka na kujiachia huku akiwa ameshikilia sehemu ya shuka iliyofungwa hapo kama kamba, na kuangukia ghorofani tena.

Hii ilifanya nyaya zikatike, naye akiwa bado amelishika shuka akawa anaona cheche zikipiga kutoka kwenye waya uliodondokea karibu na alipoangukia. Kwa haraka alijua walinzi wangekuwa wamesikia na hata kuanza kuja juu kuangalia nini kilikuwa kimetokea, hivyo akanyanyuka ili aanze jitihada za kuifungia miili yake na Azra kwa nyaya hizo na hatimaye wabembee mpaka nje. Lakini baada ya kunyanyuka, akatambua kwamba umeme haukukatika kwenye nyumba hiyo baada ya yeye kuzikata hizo nyaya, na alipochungulia kule chini, akaona walinzi wakiendelea na biashara zao tu, kuonyesha hata hawakusikia kilichotokea.

Sauti za shoti zilizotoka kwenye nyaya hizo zilizibwa na fundo la shuka lililokuwa limezungushiwa kwa ukaribu, hivyo Lexi akaona azidishe fundo hilo hapo ili zisisikike hata zaidi. Ilimshangaza kiasi kwamba umeme haukukatika, lakini labda hiyo ilimaanisha umeme wa nyumba hii haukuhusiana na nyaya hizo, au kulikuwa na jenereta la dharura endapo umeme ukikata linawaka moja kwa moja. Kwa vyovyote vile hii ilikuwa na faida kwake, kwa sababu angekuwa na muda wa kutosha kumweka Azra mwilini mwake vyema ili hatimaye waondoke.

Kutokea kule nje, LaKeisha na Victor waliona nyaya hizo zikilegea kule juu, nao wakawa wanamuuliza Lexi kama kila kitu kilikuwa sawa. Akawajibu mambo yalikuwa safi, hivyo akiwaambia tu "now" waanze kuendesha. Lexi alikuwa anahangaika kuhakikisha sehemu ya nyaya iliyokatika haingewagusa moja kwa moja kwa kuyarundika mashuka hapo. Sasa akaona kwamba ingekuwa ngumu kuubananiza mwili wake na wa Azra kisha aifunge kwa pamoja, kwa hiyo ili kuokoa muda akaamua kwamba angemweka mgongoni.

Kila kitu alichowaza alijua kingekuwa na hatari fulani, lakini akaazimia kufanya yote awezayo kutoka sehemu hiyo na mdogo wake. Akaziunganisha vizuri nyaya hizo, kisha akamnyanyua Azra na kumweka mgongoni, naye akatumia sehemu ya shuka kumfunga kiunoni kwake na kuikaza mikono ya Azra shingoni kwake kwa mkono mmoja, halafu akaishikilia nyanya hiyo kwa mkono mwingine na kusimama, naye akasema kwa sauti ya chini, "Now!"

Papo hapo akashika nyaya hizo kwa mikono yote na kujirusha kwa nguvu sana. Nyaya ikaanza kuwapeleka kuelekea chini kwa kasi sana, na walipoukaribia ukuta, miili yao haikuwa juu vya kutosha kuweza kuuvuka, hivyo wakaishia kujigonga karibu kabisa na mwisho wa kuta hizo!

Mlinzi mmoja aliona jambo hilo, na kutokea alipokuwa akawapa tahadhari wengine kwamba kuna jambo lilikuwa linatokea upande wa Lexi, nao wakaanza kukimbilia huko. Lexi alikuwa amejitahidi kuendelea kuzishika nyaya hizo, huku akihisi kabisa jinsi Azra alivyoanza kuteleza kutoka mgongoni kwake, lakini akajivuta kwa nguvu kuelekea juu na kufanikiwa kuishika chuma iliyochongoka juu ya kuta hizo. Kulikuwa na nyanya za chuma zenye mtindo wa miiba zilizozungushiwa pia kwa juu, hivyo kwa kiasi fulani zikawa zinachoma vidole vyake vilivyokuwa ndani ya 'gloves' ngumu.

Ukuta huo ulikuwa mrefu sana, na baada ya walinzi kufika usawa huo, wakamwamuru aliyembeba Azra ajisalimishe la sivyo wangempiga kwa risasi. Lexi hakutaka kukata tamaa. Kutokea juu hapo aliweza kusikia sauti ya gari kwa kule nje, naye akatambua ilikuwa ni Victor na Lakeisha, hivyo akaongeza bidii ya kujivuta na kufanikiwa kupigisha goti lake juu ya kuta hizo. 

Mlinzi mmoja kati ya sita waliokuwa hapo alimlenga Lexi kwa umakini sana na bunduki yake ili amfyatue yeye na siyo Azra, huku walinzi wawili wakikimbia kuelekea geti ili wafike kwa nje. Mlinzi huyo akafyatua risasi iliyofanikiwa kumpiga Lexi sehemu ya juu ya mbavu yake, lakini haikuweza kumdhuru kutokana na nguo yake kuzuia risasi hiyo ingawa ilikuwa na nguvu kali sana. Msukumo wa risasi hiyo nzito ukasababisha Lexi asukumwe kwa nguvu sana na hivyo yeye pamoja na Azra wakaangukia upande wa pili wa kuta hizo, yaani kwa kule nje!

Ilikuwa ni shukrani kwa Mungu tu kwa sababu tayari Victor na Lakeisha walikuwa wamesimama sehemu waliyoangukia kwa huko nje, na hivyo Victor akajiweka vizuri na kufanikiwa kumdaka Azra, nao wakadondokea pembeni bila ya Azra kuumia vibaya sana, ingawa alikuwa na mikwaruzo kwenye miguu kutokana na nyaya zile za miiba kumkwarua. LaKeisha hakuwa na uwezo wa kumdaka Lexi vizuri, lakini kwa ujasiri alijiweka sehemu ambayo Lexi angeangukia na hivyo akamdondokea na wote kuanguka kwa pamoja. LaKeisha aliumia kiasi kwenye mkono wake, naye Lexi alihisi maumivu kichwani na msuguo mkubwa kwenye nyonga, lakini wote wakajitahidi kunyanyuka na kuambiana walikuwa sawa.

Lexi akaonya kwamba walinzi wale walikuwa wanakuja, hivyo upesi wakamwingiza Azra kwenye gari, naye Victor akawaondoa hapo haraka isivyo kawaida. Aliendesha kwa kasi sana na kufanikiwa kufika mbali bila kuwaona walinzi wale wakija, na baada ya kufika sehemu walikoacha gari lingine, wakalifata na kuliacha hili walilotumia, kisha Victor akafanya kama kulilipua kwa kupiga risasi sehemu ya tenki la mafuta kwa bastola yake ndogo.

Wakawa wamefanikiwa kuondoka na Azra, ambaye bado alikuwa mbali kiusingizi. LaKeisha akamuuliza Lexi ikiwa aliumia sehemu yoyote kwa sababu walisikia mlio wa risasi kule ndani, naye akasema hakuumia. Victor akaweka wazi kwamba mchezo waliokuwa wametoka kufanya ulikuwa hatari sana, hivyo walistahili mambo mazuri kutoka kwa mdogo wake Lexi na siyo wamfikishe huko halafu awazingue. Torres kupitia kifaa cha mawasiliano, akawapongeza sana kwa kazi nzuri na kusema angemjulisha "boss" wao kuhusu mafanikio waliyopata.

Lexi alikuwa amekaa siti ya nyuma ya gari hilo, huku Azra akiwa amelaza kichwa kwenye mapaja yake, naye akatabasamu kwa hisia huku akipitisha kiganja chake kwenye nywele laini za mdogo wake. Hatimaye akawa pamoja na mdogo wake tena.

★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★

Previoua Next