Reader Settings


 FOR YOU 3

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA SITA

★★★★★★★★★★★


Hatimaye Lexi akawa amefika nje ya hoteli aliyokaa Nora. Usiku ulikuwa umekwishaingia sasa, na maghorofa ya hoteli hiyo yalionekana yakimeremeta kwa taa zake nyingi. Alikuwa amekwishamtumia Nora ujumbe kwamba angefika hapo, na kusema angemweleza pia alikokuwa na kwa nini hakupatikana kwa siku hizo chache. Akaizima tena simu yake na kushuka kutoka kwenye gari na kuelekea huko ndani mpaka alipofika nje ya mlango wa chumba cha Nora. Akashusha pumzi ya kujiweka sawa, kisha akaugonga mlango kistaarabu na kusubiri. Hazikupita sekunde nyingi, nao mlango ukafunguliwa.

Lexi alihisi mapigo yake ya moyo yakidunda kwa kasi zaidi baada ya kumwona Nora kwa mara nyingine tena. Alivutiwa zaidi na jinsi alivyosuka wakati huu, na kufanya ajiulize ikiwa aliamua kujipendezesha kwa ajili yake. Nora alikuwa amesimama ndani hapo huku ameushikilia mlango na kumwangalia Lexi kwa hisia sana, kwa sababu kihalisi alikuwa amemkumbuka mno "mwanamke" huyu. Ijapokuwa kuna mambo mengi yaliyokuwa yakipita akilini mwake, akaachia tabasamu la mbali kuonyesha amefurahi kumwona, naye Lexi akatabasamu pia.

Nora akamkaribisha ndani, na baada ya Lexi kuingia akaufunga mlango na kushusha pumzi ndefu huku akiwa amefumba macho yake, naye akamgeukia taratibu.

"Pole, nimekufanya usubiri sana?" Lexi akamuuliza.

"Hapana. Nami ndiyo nimefika tu," Nora akajibu.

"Okay... sawa. Umekula?" Lexi akauliza.

Nora akatikisa kichwa kukubali.

"Ona... kulikuwa na mambo fulani ya kifamilia hapa katikati na... nilihitajika huko. Yalikuwa mambo mengi ndiyo maana nilikuwa sipatikani. Nisamehe kwa kukufanya uni-miss sana," Lexi akasema.

"Usijali... haina shida. Kwa hiyo... familia yako... mambo yako vizuri sasa?" Nora akauliza.

"Yeah, tumejitahidi kuyajenga. Kila kitu kiko sawa," Lexi akasema.

"Umefanyaje mkononi?" Nora akauliza.

Lexi akajitazama sehemu ya mkono wake iliyofungwa kwa bendeji, ambapo aliumizwa na yule mnyama wake, Zelda.

"Aam... niliumia tu kidogo wakati niko huko. Siyo kitu serious sana," Lexi akasema.

Nora akabaki kumtazama kwa njia ambayo ilimwambia Lexi kwamba mwanamke huyo alikuwa anawaza jambo fulani kumhusu.

"Vipi wewe? Mambo yamekwendaje huku wakati sipo?" Lexi akamuuliza.

Nora akabaki kumtazama tu.

"Uko sawa mheshimiwa?" Lexi akauliza kwa njia ya kujali.

Nora akamsogelea karibu na kuuliza, "Wewe unaonaje? Niko sawa?"

Swali hilo likamfanya Lexi atambue kuwa kweli kuna jambo hapa halikuwa sawa. Wazo la kwamba huenda Nora alikuwa amegundua yeye ni nani likamwingia, lakini akajitahidi kutoonyesha itikio lolote la kubabaika.

"Naona kama vile hauko sawa. Una hasira na mimi kwa sababu sikukujibu hizi siku mbili, eti?" Lexi akauliza.

"Sina hasira nawe. Nimeumia tu," Nora akasema.

Lexi akabaki kimya.

"Ila sijaumia kwa sababu ya wewe kutonijibu... la. Nimeumia kwa sababu... nilifikiri nimepata kitu fulani ambacho nakijua, ila sasa nimetambua kuwa sikijui kabisa," Nora akasema.

Kauli hiyo ilimtikisa sana Lexi moyoni. Nora alisema maneno hayo kwa hisia nzito sana, na Lexi tayari akawa ameshakisia mwanamke huyu alielekea wapi ingawa alitaka kuhakiki zaidi.

"Mheshimiwa... mbona unaongea hivyo? Sielewi, niambie unamaanisha nini..." Lexi akasema.

"Oh Lexi... kwa nini lakini? Kwa nini ilipaswa kuwa wewe? Why was it supposed to be like this?" Nora akauliza na kuanza kudondosha machozi.

Lexi tayari akawa ameelewa. Nora alijua. Alijua kila kitu. Lakini utata ni kwamba alijua jinsi gani, na kwa sababu hiyo Lexi akaona aendelee kulazimisha mambo.

"Mheshimiwa... sielewi... tafadhali niambie, unamaanisha nini? Unaniogopesha..." Lexi akamwambia.

"Ahah... nakuogopesha. Hivi wewe ni nani? Kwa nini umeingia kwenye maisha yangu kama mwangaza mpya wa furaha lakini kumbe ni kitovu kikuu cha maumivu Lexi? Unafurahia sana kuumiza watu, eti? Furaha yako ipo kwenye huzuni za wengine, si ndiyo? Tell me. Najua unajua nachomaanisha. Tusizungukane kama watoto, just... tell me. Hakuna mtu mwingine hapa. Niambie tu. Kwa nini unafanya mambo haya yote? Kwa nini unaumiza watu wengi sana? Pesa? Ni pesa tu? Au kuna kingine dada yangu?" Nora akaendelea kuuliza.

Lexi alikuwa anamwangalia sana asijue la kusema. Angeanzia wapi kumwelezea maana ya mambo yote yeye na wenzake waliyokuwa wamefanya? Kuona kwamba hakuwa amemwitia labda maaskari ili wamkamate kulionyesha kwamba mwanamke huyu aliumizwa sana na ukweli alioujua kiasi kwamba alitaka kusikia kutoka kwa Lexi pekee sababu yake ni nini, ili amhukumu yeye kama yeye. Hii ilionyesha bado kuna vitu aliviona ndani ya Lexi vilivyompa matumaini ya kwamba huenda alikuwa na sababu iliyompelekea kufanya mambo mabaya, ingawa hiyo haingehalalisha matendo hayo yaliyopingana na sheria.

Lexi akabaki kutazamana na Nora tu kwa hisia sana, akijiuliza aseme nini sasa. Ajaribu kumwelewesha vizuri sababu zake, au amdanganye tu?


★★


Wakati hayo yakiwa yanaendelea, Luteni Michael, akiwa pamoja na Alex, Mario, Hussein, Rachel, Tariq na Zachary, walikuwa wanarejea jijini Dar es Salaam kutokea mkoa mwingine walipokuwa wamekwenda kutafiti masuala ya Mess Makers. Ulikuwa ni uamuzi wa Kanali Oswald Deule, ambaye kwa kujifanya mtaalamu sana aliwaagiza kwenda huko lakini hawakupata matokeo yoyote chanya.

Sasa wakiwa njiani kuelekea kule ambako jengo lao la utafiti lilikuwepo, wakatumiwa taarifa na Bobby zilizowaacha wote midomo wazi. Alikuwa amewatumia vigezo kwa njia ya simu vilivyowaonyesha watu sita ambao walitambulishwa kuwa Mess Makers. Kulikuwa na picha zao, majina yao, na taarifa chache zilizothibitisha kwamba wao kweli ndiyo waliokuwa Mess Makers. Hawa walikuwa ni Lexi Sona, Oscar Amari, Victor Quawey, Mensah Dodzi, Kevin Dass, na Kendrick Jabari!

Ni wawili tu ndiyo ambao hawakuwepo kwenye orodha hiyo, yaani LaKeisha na Torres.

Luteni Michael akamuuliza Bobby taarifa hizo alizipata vipi, naye akasema zilikuwa zimerushwa tu kutoka kwenye chanzo kisichojulikana, na alipojaribu kukifatilia akashindwa kukipata. Taarifa zilizothibitisha kwamba watu hao walikuwa ni kutoka kundi la Mess Makers ni pamoja na rekodi za sauti za maongezi yao wakati ule walipoiba dhahabu kwenye treni, wakati ambao Kendrick Jabari alifanya mpango wa kumteka ACP Nora ili kumuua kupitia kwa wanaume wale saba, na wakati ambao Salim Khan alikufa.

Ingawa hakukuwa na taarifa nyingi sana, mambo hayo tu yalitosha kabisa kuthibitisha kwamba ilikuwa ni kweli hasa kwa kuona uwepo wa Oscar na Kevin kati ya watu hao. Bobby alimwambia Luteni Michael kuwa mambo hayo yalikuwa yamesambazwa mpaka kwenye vyombo vya habari, na bila shaka yangekuwa yameshafika mpaka kwa wakuu wao. Wanajeshi waliopata taarifa hizo walishangaa sana kujua kwamba Kendrick Jabari alikuwa hai, kwa sababu walimfahamu kuwa na cheo cha Kapteni miaka kadhaa nyuma kabla ya tukio lililosababisha "kifo" chake.

Ikabidi Luteni Michael amtafute Kanali Oswald, ambaye naye tayari alikuwa amezipata na kumwambia waanze kutafuta ni wapi ambapo watu hao wangekuwa kupitia kwa Manengo na Bobby. Walikuwa wakimlenga zaidi Kendrick Jabari, hasa kwa sababu ya utata wa yeye kuhusika na Mess Makers wakati ilidhaniwa alikuwa amekufa kitambo. Manengo akawa amefanikiwa kujua kwamba Kendrick Jabari alikuwa nchini humo kwa zaidi ya mwaka sasa kutokea Ghana, na alikuwa akimiliki kampuni zilizohusiana na madini. Hakuwahi kuonwa hadharani lakini aliziendesha kampuni hizo kwa muda mrefu, na ikashangaza kwamba hakuwa ametambulika kwa muda wote huo.

Baada ya kufatilia taarifa za mawasiliano ya kawaida za Kendrick na wengine, kama walivyofanya tu mara ya kwanza kwa Kevin Dass, Manengo akabaini kuwa kwa sasa mwanaume huyo alikuwa kwenye moja ya kampuni zake pamoja na wenzake wawili, na eneo hilo lilikuwa hapo hapo jijini. Upesi, taarifa hizo zikatumwa kwa Luteni Michael ili yeye na wenzake wapitilizie huko huko. Kanali Oswald akawaambia kwamba angetuma taarifa kwa vyombo vya usalama vya maeneo ya huko kwenye kampuni ya Kendrick ili waagize vijana mahiri kwenda kuwakamata watu hao wakati Luteni Michael na wengine wakiwa njiani kuelekea huko.

Safari ya timu ya Luteni Michael ikageuza mkondo haraka sana. Luteni Michael alijawa na hamu kubwa mno ya kuja kumwonyesha Nora ukweli huo kumhusu Lexi ambao tokea mwanzo aliuhisi, lakini Nora na kila mtu akamwona mjinga. Alikuwa na hasira sana pia iliyomfanya atake kuwa wa kwanza kumshika Lexi ili amwonyeshe nini maana ya dharau kama aliyomwonyesha siku ile kwenye chumba cha Nora.


★★


Kufichuliwa kwa timu ya Mess Makers kulianza kusambaa kutoka kwenye vyombo vya habari, na pia mitandao ya kijamii haikuwa nyuma kuifanya hiyo kuwa mada iliyoongoza zaidi a.k.a "number one trending." Zilifika kwa wakuu wa jeshi, yaani Jenerali Jacob na Luteni Jenerali Weisiko, na hata Raisi Paul Mdeme pia, na wote walikuwa wameachwa midomo wazi kwa kutoamini kabisa ukweli huo. Waliwasiliana na kuanza kuulizana iliwezekana vipi kwa Kendrick Jabari kuwa hai muda wote huo na wenyewe wasijue, na kilichoshangaza hata zaidi ni kumwona mtoto wa Meja Casmir akiwa hai pia.

Jenerali Jacob alimkumbusha Weisiko sasa kwamba kwa sababu ya kutokufuatilia kwake mambo vizuri usiku ule, mwanaume huyu alikuwa amesababisha madhara makubwa yaliyoletwa na wawili wale na kundi lao wakati huu. Ikawa wazi sasa kwamba hii ishu yote ya "Mess Makers" ilitokana na Kendrick Jabari na mtoto wa Casmir kama njia yao ya kuwalipizia kisasi. Ingawa bado hawakuweza kuelewa wawili wale walitaka kuwalipizia kisasi kwa njia gani kikamili, bado kuwa kwao hai ilikuwa ni tatizo kwa Majenerali na Raisi kwa sababu ni watu waliojua ukweli wote kuhusiana na Demba Group miaka nane iliyopita.

Raisi Paul Mdeme alikuwa amewasiliana na Jenerali Jacob na kumwambia kuwa haya yote yalikuwa makosa yao yeye na Weisiko kwa kukosa kuwamaliza wawili wale miaka mingi iliyopita, na sasa mambo mengi hata zaidi yangevurugika. Jenerali Jacob alipandwa na hasira sana. Hivi siyo jinsi alivyotaka mambo yaende hata kidogo, kwa sababu vyombo vya habari kujua kuhusu watu hao mapema namna hiyo kungeweza kufichua siri zao nyingi sana.

Akamwamuru Weisiko afanye juu chini ili kuwakamata watu hao upesi, kwa njia zozote zile ambazo tayari zilikuwa zimewekwa, afanye lolote lile ili kuwapeleka watu hao upande wao waweze kuwashughulikia wenyewe. Weisiko akamwambia tayari hilo lilikuwa likifanyiwa kazi, na bila shaka wangehakikisha wanafanikiwa; iwe isiwe.


★★


Lexi bado alikuwa kwenye chumba cha hoteli pamoja na Nora, akiwa bado anatafuta namna ya kujieleza kwake, lakini akashindwa. Nora alikuwa anaongea maneno yenye kuonyesha hisia nyingi za kuvunjika moyo, akimwambia kwamba kwa sababu ya mambo hayo, angetakiwa kumfunga pingu na kumpeleka jela yeye mwenyewe ikiwa hangempa sababu nzuri ni kwa nini alifanya mambo mabaya kuielekea serikali hii.

Lexi aliwaza; ikiwa kweli Nora angetaka kumtia mikononi mwa sheria, basi angekuwa amemwekea mtego mapema wakati alipofika hapo. Aliona ukweli wa kwamba mwanamke huyu hakuwa na hasira wala chuki kumwelekea, bali aliumia sana kwa sababu alidhani yeye ni tofauti. Sasa akawa anapambana na hisia zake mwenyewe hata zaidi, kwa sababu ilionekana ni kama alitakiwa kujigawa mara mbili kutoka kwenye yale aliyofanya, na kile alichohisi moyoni. Hata kama angesema nini, alijua mwanamke huyu asingemwamini kirahisi.

Wakati Nora alipokuwa akiendelea kusubiri jibu kutoka kwa Lexi, simu yake ikaita. Akaitoa kutoka mfukoni mwa suruali yake na kupokea bila kuangalia ni nani, huku bado akiwa anamtazama Lexi machoni. Lakini baada ya kutambua kwamba ilikuwa ni Bobby ndiye aliyempigia, akaweka umakini wake hata zaidi. Mwanaume huyo akamjulisha mambo yote yaliyokuwa yakiendelea, akisema Mess Makers walikuwa wamefichuliwa na mtu fulani asiyejulikana.

Mwonekano wa sura ya kushangaa kiasi usoni kwa Nora ukamwambia Lexi kuwa kuna jambo lilikuwa likiendelea; jambo baya. Nora hakuongea chochote kile zaidi ya kuitikia na kuendelea tu kumsikiliza Bobby, ambaye akamwambia kwamba alikuwa amemtumia taarifa hizo zenye kushangaza kwenye mfumo wake wa siri wa kutunza mambo. Huo ulikuwa umeunganishwa kwenye "tablet" yake Nora, hivyo upesi akampita Lexi na kuifata ilipokuwa kwenye mkoba wake. Akamgeukia Lexi na kumtazama kidogo, kisha akaiwasha na kuanza kutafuta habari hizo. Alikuwa anataka kuona uthibitisho zaidi ikiwa Lexi angekuwapo pia kwenye taarifa hizo, na baada ya kumwona, akachoka sana. Akafumba macho yake na kutikisa kichwa chake kidogo, akiwa amehisi kuvunjika moyo hata zaidi.

Alipogeuka nyuma tena ili amwonyeshe vizuri zaidi sasa Lexi ukweli yeye mwenyewe, akashangaa kukuta kwamba Lexi tayari alikuwa ameondoka. Yaani ilikuwa ghafla na kwa njia ya haraka, naye hakuwa ametambua hilo. Kwa haraka akafikiria kwamba ni lazima tu Lexi angekuwa amekimbia ili labda kwenda kuwaonya wenzake, na kwa sababu Bobby alikuwa amemtumia taarifa za walikokuwa wenzake na Lexi, Nora akaamua kwamba angekwenda huko huko pia. Akarudi sehemu yenye droo upesi na kutoa bastola yake, kisha akazifunga nywele zake vizuri kwa nyuma na kutoka hapo haraka sana.

Moto sasa ungeanza kuwa mkali zaidi!


★★★


Kendrick alikuwa bado pamoja na vijana wake kule kwenye kampuni yake, na sasa walikuwa wamemaliza kufanya yale ambayo Torres alihitaji kufanya. Hii ilikuwa ni hatua ya kwanza, na hatua ya pili ndiyo ingekamilisha mpango wao maalum waliokuwa wameuweka. Azra alipata kujionea mambo mengi hapo yaliyothibitisha kwamba watu hawa waliofahamika kama "Mess Makers" hawakuwa wabaya kama alivyodhani, na hisia mpya ya kujiona kuwa "sahihi" ikamwingia kwa sababu ya kuwa upande wao. Kendrick akamwambia kwamba kuna mambo mengi wangetimiza pamoja, mambo ambayo yangekuwa faida kwa watu wengi sana kutokana na yale waliyoyafanya.

LaKeisha pamoja na wengine walikuwa pembeni, na mwanamke huyu alikuwa ameboeka, hivyo akaamua tu kuzama kwenye mitandao ya kijamii; akitafuta udaku wa hapa na pale. Si ndiyo akazibamba sasa zile taarifa! Mwanzoni alihisi ni kama masihara, lakini alipofuatilia vizuri, akatambua kwamba kundi lao lilikuwa limevurugwa.

Upesi akawaonyesha wenzake mambo yalikuwa vipi, na wao pia wakapigwa na butwaa zito baada ya kuona mambo hayo. Wakaanza kujiuliza iliwezekana vipi wao kuweza kutambulika kirahisi namna hiyo mpaka kwenye mitandao ya kijamii, na fikira ya kwanza ilikuwa ni ACP Nora. Walidhani labda mwanamke huyo ndiye aliyefanya jambo fulani kuwafichua baadhi yao. Walianza kuzivunja laini na simu zao zote za kawaida, nao wakaanza kujiandaa kutoka jengoni hapo haraka iwezekanavyo.

Walitumia lifti ile ya kibinafsi kushuka mpaka kule chini ili waelekee kwenye magari yao, pale waliposhtushwa na magari matatu yaliyokuwa yamefika upande huo na kusimama umbali fulani kutoka kwao. Waliweza kuyatambua kwa haraka kuwa magari ya wanajeshi maalum, au majasusi, nao wakajiuliza walifikaje hapo haraka hivyo na hata walijuaje wangekuwa hapo.

Majasusi hao maalum wakashuka wakiwa wamevalia nguo nyeusi na kushikilia bunduki huku wakiwaelekea wakina Kendrick, nao walikuwa wakiwaambia wajisalimishe haraka sana. Kendrick na vijana wake wakaanza kukimbilia pande ambazo kulikuwa na nguzo nene zilizoshikilia ghorofa ili wajifiche, wakati huo Victor akawa ametoa bastola yake ndogo na kuwafyatulia risasi ili kuwachengua, na majasusi hao wakajikinga kwenye baadhi ya magari na nguzo za pembeni. Victor akawahi na kujirusha kwenye nguzo moja, kitu kilichofanya adondoshe begi lake, huku majasusi wale wakianza kusogea taratibu na kufyatulia risasi nyingi sana upande wa Mess Makers, zilizotoboa kuta, magari, na kupasua sehemu za nguzo zile walizojifichia.

LaKeisha alikuwa anatukana kwa hasira kwa sababu ya kutoelewa haya yote yaliwezekana vipi, lakini wakati huo huo tayari Torres akawa amemwelekeza Mensah cha kufanya, kwa kuwa walikuwa wamejifichia sehemu moja. Kwenye moja ya mabegi waliyokuwa nayo, kulikuwa na zile nguo zao za mapambano, naye akamwambia Mensah avae moja haraka sana ili awashughulikie majasusi wale. Alijua mwanaume huyu alikuwa na shabaha nzuri sana, na kwa hapa aliyekuwa na bastola ni Victor pekee, hivyo akamwambia Victor amrushie bastola Mensah, na baada ya Victor kufanya hivyo, Torres akamwambia Mensah awalenge majasusi wale sehemu za miguu au mikono ili kuwaangusha chini, lakini ahakikishe haui yeyote kati yao. Mensah alikuwa anataka kuwaua wote kwa sababu alihisi hasira, lakini Torres akasisitiza afuate alichomwelekeza.

Baada ya Mensah kumaliza kuvaa nguo yote, majasusi wale walikuwa karibu zaidi na nguzo waliyojifichia Kendrick na Azra, ambao walijitahidi kujibana hapo kwa uangalifu, nao wakatoa onyo la mwisho kwamba ikiwa wasingetoka basi wangewaua wote. Lakini papo hapo Mensah akatokea mbele yao, akiwa amejiviringisha kutoka alipokuwa amejibanza na Torres, naye akaanza kufyatua risasi kwa ustadi sana. Majasusi walikuwa wameanza kumfyatulia na yeye pia, lakini zikawa zinadunda, huku za kwake Mensah zikiwapata mmoja baada ya mwingine na kuwaangusha chini.

Walibaki majasusi 7 kati ya 15 waliofanikiwa kujikinga kwenye magari, huku wenzao wakiwa chini wanajivuta-vuta huku wakisikilizia maumivu ya risasi zilizowapata miguuni na sehemu za mikono. Mensah akajiviringisha mpaka kwenye gari moja na kujibanza, akihisi kama kuna vitu vingi vya moto vikiuchoma mwili wake kutokana na kumiminiwa risasi nyingi, lakini hakuwa ameumizwa sana kutokana na nguo yake kumlinda.

Kutokea kwenye nguzo nyingine, LaKeisha akamuuliza Torres kwa kikabila cha Hausa ikiwa na wao wangepaswa kuvaa nguo zao za mapambano, lakini Torres akasema muda usingetosha, na majasusi hao bila shaka walikuwa wanapanga kufanya jambo fulani kwa ukimya huo waliouweka. Mensah akasema risasi za kwenye bastola yake zingeisha haraka, hivyo labda kuvaa nguo zao kungesaidia. Lakini vipi kuhusu Kendrick na Azra, ambao hawakuwa na nguo za aina hiyo hapo? Victor pia alikuwa amedondosha begi lake mbali na alipokuwa, hivyo na yeye asingeweza kuweka kitu mwilini cha kumlinda.

Majasusi wale walikuwa wanafanya mpango wa kuwazunguka taratibu, naye Kendrick akasema kama Mensah angeweza, basi asogee mpaka pale ambapo majasusi wale walioumia walidondoshea bunduki zao na kuzichukua ili kuwapa wenzake. Mensah akachungulia kidogo, na hapo hapo risasi zikafyatuliwa upande wake na kufanya ajikinge tena, na hivyo akamwambia Kendrick haingekuwa rahisi sana kwa sababu nguo yake isingeweza kustahimili nguvu kubwa ya risasi za majasusi hao kwa muda mrefu.

Azra alipochungulia kidogo, akaona kweli majasusi hao waliobaki walikuwa wanazunguka kwa mtindo wenye ustadi, na sasa walikuwa wakikaribia sehemu aliyojikalisha Victor. Akataka sana kumwonya, lakini hiyo ingemhatarisha zaidi yeye na Kendrick kwa sababu majasusi wangeona walipokuwa wamejibanza, naye akashindwa kujua afanye nini ili kumsaidia mwanaume huyo.

Jasusi mmoja alikuwa akisema kwamba hakukuwa na haja ya kujificha tena, kwa kuwa walikuwa na mabomu, hivyo wajitokeze kabla ya wao kuwarushia. Torres alijua hiyo kuwa njia yao ya kuwalaghai tu, kwa sababu kama wangekuwa na mabomu hapo wangekuwa wameyarusha, ila wasingeweza kwa sababu na wao yangewaua.

Wakati mchezo huu mdogo wa "nasaka mke wangu" ulipokuwa ukiendelea, Kendrick na wengine wakashtushwa baada ya kusikia sauti za vishindo na mayowe ya kadiri kutoka kwa baadhi ya majasusi wale. Wakaanza kusikia na sauti za risasi, lakini hazikupigwa kuelekea upande wao, bali ule walikotokea majasusi wale. Mensah alipochungulia, akamwona mtu akiwa anawachanganya majasusi hao, na kwa haraka akatambua ilikuwa ni Lexi baada ya kuona nguo alizovaa kuwa kama zao za mapambano. Torres akauliza ni nini kinaendelea, naye Mensah akawafahamisha wote kwamba ilikuwa ni Lexi.

Kusikia hivyo, Azra akanyanyuka na upesi kujibinua sarakasi nyingi mpaka karibu kabisa na Victor, naye akamvuta na kuangukia naye pambeni, kwa sababu ni wakati huo huo tayari jasusi yule alikuwa amefika usawa wake na kuanza kufyatua risasi, hivyo akawa amesaidia Victor asipigwe. Mensah akamwona jasusi huyo na kumpiga risasi kifuani, naye akaanguka chini.

"Shit!"

Neno hilo lilimtoka Mensah baada ya kutambua kwamba alitenda kwa uharaka lakini akawa amesababisha kifo. Kendrick, LaKeisha na Torres walichungulia pia na kumwona Lexi akijitahidi kuwashughulikia majasusi wengine waliobaki, naye Mensah akajisogeza sehemu nzuri ili kuwalenga miguuni wanaume hao. Walikuwa wanammiminia Lexi risasi mwilini kila alipotoka kwa mmoja na kumfata mwingine, na nguo yake pia ikawa inapungukiwa na uwezo wa kuzizuia risasi zile.

Mensah aliwalenga vizuri majasusi hao walipokuwa wamekengeushwa na Lexi, naye akawatandika risasi miguuni na kuwafanya waanguke chini huku wakiugulia maumivu. Upesi Mess Makers wakawafata wote na kuwanyang'anya bunduki zao, maana bado kuna wengine walikuwa wakijitahidi kuonyesha uimara kwa kufyatua risasi ingawa nao walikuwa wamejeruhiwa kwa risasi. Mensah alikuwa amewatandika risasi kwa ufundi ambao ungewafanya wasinyanyuke, lakini wasingekufa.

Walipokaribiana, Torres akamuuliza Lexi ilikuwa vipi mpaka watu hawa wakajua utambulisho wao, naye Lexi akawaonya wote kuwa wangepaswa kuondoka haraka sana kwa sababu wengine walikuwa wanakuja kuwakamata. Kabla hawajafikiria kufata magari, hapo hapo tena yakaingia magari mawili ya maaskari wengine wakija upande wao kwa kasi. Lexi akawaambia wenzake waondoke haraka sana, na yeye angejaribu kuwazubaisha maaskari hao ili wenzake waponyoke. Kendrick akawa anakataa, akisema walipaswa kuondoka kwa pamoja, lakini Lexi akalazimisha na kumwambia angetoka akiwa salama, hivyo watangulie na yeye angefata. Akafanya kama kuwaamuru kabisa, nao wakaanza kuelekea kwenye gari ambalo halikuwa lao, kwa sababu ya kwao yalikuwa yameharibiwa kwa kupigwa risasi.

Lexi akawageukia maaskari wale, wakiwa 8, waliokuwa wameshafika hapo na kushukia umbali mfupi wakiwa na mabunduki yao, na wakiwa wamewaona majasusi wale waliopigwa risasi, naye akaanza kuelekea upande wao huku akiwa amenyoosha mikono yake juu. Mmoja wao alikuwa anafoka kwa sauti akisema Lexi apige magoti na wengine walioingia kwenye gari watoke, lakini Lexi akaendelea tu kuwafata bila woga.

Mmoja wa maaskari hao akafyatua risasi mguuni kwa Lexi, lakini Lexi akaanza kukimbia kuwaelekea kwa kasi sana, huku akipindisha mwili wake huku na huko. Maaskari hao wakawa wanafyatua risasi zao ambazo hazikuwa na nguvu kali sana kama za bunduki walizotumia majasusi, naye Lexi akawafikia na kuanza kuwapiga kwa mitindo ya sarakasi nyingi.

Torres akawa amefanikiwa kuliwasha gari waliloingia, naye akaligeuza na kuanza kuelekea upande wa kutokea. Alipokaribia usawa ambao Lexi alikuwa akipambana na wale maaskari, alitaka kusimama hasa kwa sababu wengine walikuwa wanamwambia afanye hivyo ili wamsaidie Lexi na yeye aingie kwenye gari, lakini Lexi akatoa ishara kwamba wasisimame na waondoke haraka sana. Torres alihuzunika mno, lakini alikuwa anajua kile ambacho Lexi anafanya, yaani kuwatanguliza wao badala yake yeye.

Akapitiliza tu na kuwafanya LaKeisha na Mensah wabaki wakilalamika kwa nini alimsikiliza Lexi wakati alikuwa kwenye shida. Torres aliliondoa gari hapo kwa kasi sana, huku akisema Lexi alifanya hivyo kwa sababu alijua wakitoroka wao, hata kama yeye angekamatwa basi wangeweza kutafuta njia ya kumsaidia. Lakini Kendrick alijua ingekuwa ngumu kufanya hivyo sasa hivi kwa sababu tayari wengi wao walijulikana, hivyo ikaonekana ni kama wamemwacha Lexi peke yake kwenye shimo lenye simba wakali. Akafumba macho yake akihisi huzuni kuu moyoni, na gari lao likafanikiwa kutoka eneo hilo.

Lexi alijitahidi kupambana na maaskari hao waliokuwa watata sana, naye akafanikiwa kuwafanya wote wapoteze fahamu. Alihisi kuchoka na maumivu kiasi kwa sababu ijapokuwa nguo yake ilisaidia kuzuia risasi, zilikuwa zimedunda kwa njia iliyofanya ahisi kama mtu aliyepondwa na kokoto ndogo ndogo mwilini. Akawa anapumua kiuchovu, naye akaamua kuivuta "mask" yake na kuitupa pembeni, halafu angeelekea kwenye gari mojawapo kati ya yale waliyokuja nayo maaskari ili aondoke hapo.

Akaanza kulielekea moja, na ile tu alipoufikia mlango wa gari hilo, sauti aliyoifahamu vizuri sana ikamsemesha kwa nguvu.

"Tulia!"

Lexi akanyanyua macho yake na kukuta ni Nora, akiwa amesimama kutokea umbali mfupi mwanzoni kabisa kwenye mwingilio wa eneo hilo la maegesho. Alikuwa ameshika bastola huku ameilekeza kwa Lexi, naye akaanza kutembea polepole kumwelekea huku akiwa amekunja sura yake kuonyesha hasira. Akasimama baada ya mwendo huo mfupi, naye Lexi akaachia mlango wa gari na kubaki anamtazama kwa umakini.


★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★

Previoua Next