Reader Settings

Mwisho wa Dunia Kimya Kimya – Episode ya Kumi na Mbili

Mhusika Mkuu: Najim Kifu

---

Najim hakutembea; alianguka taratibu ndani ya mwanga huo kama tone la maji kwenye kisima kisicho na mwisho. Kulikuwa na ukimya, lakini ndani ya ukimya huo, kulisikika sauti moja tu ikijirudia taratibu:

"Usisahau... lakini usiwe mateka wa kilichopita..."

Alipofumbua macho, hakuona dunia aliyokuwa akiijua. Kulikuwa na anga la manjano linalong'aa kama jua la mchana, lakini bila chanzo. Ardhi ilikuwa laini, kama mawazo mazito ya mtu aliyechoka kuamini. Huko ndiko kulikuwa Mwisho wa Nafsi.

Akasimama. Hakukuwa na njia. Hakukuwa na mtu. Lakini akili yake ilijaa majina. Layna. Shafii. Zuhura. Fatma. Na jina moja lililomtisha — Yusuph.

Yusuph alikuwa jina lililojitokeza kwenye faili za zamani alipokuwa mjasusi. Faili ambazo hazikupaswa kuwepo. Alikuwa wakala wa kivuli, aliyeitwa Mchongaji wa Hatima. Aliwahi kuwa rafiki. Kisha akawa adui. Kisha… akatoweka, pamoja na kumbukumbu zake.

Sasa jina hilo lilikuwa kwenye mwangwi wa nafsi ya Najim.

Akiwa bado anatafakari, kivuli kikubwa kilitua mbele yake. Kilikuwa na sura ya mtu, lakini miguu yake haikugusa ardhi. Akamkaribia taratibu.

“Najim Kifu,” sauti hiyo ikasema. “Umeingia eneo ambalo haiandikwi historia. Hapa hujulikani kama shujaa, msaliti, au mpenzi. Wewe ni nafsi tupu. Uko tayari?”

Najim akasema bila kusita, “Ndiyo.”

Kivuli kikageuka kuwa mtu kamili — kijana aliyekuwa na macho yenye huzuni nzito. Alivaa vazi jeusi lililoning’inia kama kivuli. Alikuwa Yusuph.

“Unanikumbuka sasa?” aliuliza.

Najim akapumua kwa uzito. “Nakumbuka ulivyonisaidia kuokoa familia ya Elika Nairobi. Nakumbuka vile ulivyopotea kwenye operesheni ya Bogotá. Lakini pia nakumbuka ule msaliti aliyeharibu mawasiliano yetu Zanzibar.”

Yusuph akasogea, “Ulikuwa sahihi na umekosea. Mimi sikusaliti. Nilitoweka kwa sababu nilipewa agizo. Nilikuwa mlinzi wa Layna. Sio kwa hiari, bali kwa kiapo kilichovunjika.”

Najim akamtazama kwa macho ya mtu anayetamani kuelewa. “Layna yuko hai?”

Yusuph akasema, “Yuko hai. Lakini hajakamilika. Kumbukumbu zake zimesambaratika, zimegawanyika vipande vipande. Kila pande iko kwa mtu tofauti.”

Najim akauliza, “Na nilipata kipande gani?”

Yusuph akatabasamu kwa huzuni. “Ulipata pande la ahadi. Ambalo wewe mwenyewe ulilisahau. Na sasa, ili kumrudisha Layna, lazima utembee njia ya kumbukumbu zako ulizosahau kwa makusudi.”

Kutoka ardhini, kipande cha mti uliochomwa kikajitokeza. Kilikua haraka, na kuwa mlango wa kale wa mbao. Juu yake, kulikuwa na maandishi:

"Mlango wa Majuto Saba."

Najim akasema, “Niingie?”

Yusuph akatikisa kichwa. “Huwezi kuingia peke yako. Unahitaji nafsi inayolingana — nafsi ambayo haiogopi kuumia tena. Kuna mtu amefuata mwanga wako. Ameshawasili.”

Kwa mbali, sauti ya miguu ikasikika. Najim alipogeuka, alishangaa kumwona msichana aliyevalia joho la kahawia, sura yake ikiwa na mchanganyiko wa maumivu na ujasiri. Alikuwa Khadija, mtaalamu wa tiba za kale kutoka Lindi aliyekuwa sehemu ya zamani ya kundi la Najim lakini aliachana nao baada ya Layna kupotea.

“Najua hukunitarajia,” Khadija alisema kwa sauti tulivu. “Lakini moyo wa mtu aliyekupenda hauwezi kuamini kuwa uliamua kumsahau Layna bila sababu.”

Najim alijibu kwa sauti ya chini, “Sikusahau kwa hiari. Nililazimishwa.”

Khadija akasema, “Basi acha nikusaidie kukumbuka — kwa herufi, sauti, na hisia.”

Wakakumbatiana. Dunia ilitetemeka. Mlango ukafunguka wenyewe. Ndani kulikuwa na ukuta ulioandikwa maneno saba:

> 1. Nilikimbia

2. Nilimwacha

3. Nilijificha

4. Nilililia kimya

5. Nilimtamani zaidi ya dunia

6. Nilimtafuta bila kumuona

7. Nilimkataa nilipomwona

Najim alisikiliza kila neno kwa maumivu. Akaketi mbele ya ukuta huo. Kisha akasema taratibu:

“Lakini sasa nimekuja.”

Mwangaza mkali ulilipuka, ukitengeneza barabara mpya. Kichwani mwake, sauti ya Layna ilisikika:

"Najim... Najim... najua haukusahau. Najua hukukimbia kwa sababu ya woga... ulikuwa unanilinda. Lakini sasa, nipo tayari kukumbuka. Njoo.”

Khadija akachukua mkono wa Najim. “Tunaenda. Lakini usisahau: Kile tutakachokikuta mbele, hakiwezi kurudishwa nyuma.”

---

Previoua Next