Reader Settings

Mwisho wa Dunia Kimya Kimya – Episode ya Kumi na Tatu

Mhusika Mkuu: Najim Kifu

---

Walikanyaga ardhi ya barafu, lakini mioyo yao ilikuwa moto. Walikuwa kwenye ukingo wa Nyanja ya Sita — mahali ambapo kila mtu aliyetaka kusahau aliwahi kupita, lakini hakuna aliyerudi na uso ule ule. Kulikuwa na giza laini, si la kutisha, bali la ukimya ambao unaleta ukweli kuliko mwanga.

Najim na Khadija walitembea kimya. Walisikia sauti ya upepo, lakini pia sauti ya ndani — sauti ya Layna ikimuita Najim kwa jina lake la ndani:

“Najimu...”

Khadija alimtazama. “Aliwahi kukuita hivyo tu mara moja. Wakati mlipokuwa mkifukuzwa Mogadishu. Ulimwambia asilitumie tena kwa sababu lilikuwa jina ambalo mama yako alikuitaga kabla hajauawa.”

Najim akageuka polepole. “Unakumbuka hayo?”

Khadija akasema, “Sikuwahi kusahau. Nilikuwa pembeni yenu siku hiyo.”

Wakiwa bado wanazungumza, kwa mbali waliona kitu kikielea angani. Ilikuwa chombo — kama ndege ndogo, lakini hakikuwa na injini. Kiliendeshwa kwa mawimbi ya akili. Kilikuwa na nembo ya kale: NDOTO ZA AFRIKA – TAWI LA ZAMANI.

Kilipotua, mlango wake ulijifungua taratibu. Ndani, walikuta mtu mmoja: mwanaume wa makamo, mwenye ndevu ndefu zilizojaa vumbi la historia. Alikuwa amevaa koti la buluu ya damu baridi, na mkononi mwake alibeba kifaa cha kale kilichoitwa Mwambatano wa Kumbukumbu.

“Najim,” alisema kwa sauti yenye shikamoo ndani yake. “Kama unatafuta Layna, unahitaji kupita kwenye sehemu ya mwisho ya kumbukumbu za dunia — ile iliyozimwa rasmi mwaka 1947. Mahali ambapo historia na hadithi zilianza kuingiliana. Mahali panapoitwa Itale-Ya-Mwisho.”

Najim akasogea, “Wewe ni nani?”

“Mimi ni Azori,” akajibu. “Niliwahi kuwa msaidizi wa Mwandishi wa Kwanza wa Dunia. Lakini nilisaliti maandiko, nikachagua moyo.”

Khadija akamuangalia Azori. “Mbona sura yako… kama mtu niliyemwona kwenye ndoto?”

Azori akatabasamu kwa huzuni. “Ndoto zako hazikusema uongo. Niliwahi kukupenda kabla hujazaliwa.”

Kimya.

Najim akasimama kati ya Azori na Khadija. “Itale-Ya-Mwisho iko wapi?”

Azori akaonyesha kifaa chake, kisha akakipiga pale ardhini. Sehemu kubwa ya nchi ikayumba, ikafunguka kama kurasa za kitabu, na ndani yake kukatokea njia ya ngazi zilizotengenezwa kwa mawe yanayong’aa — kila jiwe likiwa limeandikwa jina moja la waliowahi kupotea.

Akitazama chini, Najim aliona majina aliyoyajua. Max. Imeli. Shafii. Janina. Zuhura. Kisha, kwenye jiwe la mwisho, jina lilikuwa Layna — likiwa limeandikwa kwa damu.

Azori akasema, “Njia hii inaweza kuwakumbusha kila kitu, lakini pia inaweza kuwasahaulisha kila kitu.”

Khadija akauliza, “Na kama tukisahau kila kitu?”

Azori akajibu kwa sauti ya uzito, “Basi mtarudi kuwa wageni kwa kila mmoja — kwa dunia na kwa nafsi zenu.”

Najim alisimama juu ya jiwe lililoandikwa Layna. Akapiga magoti. Akasema, “Nitakumbuka. Nitamlinda. Nitampenda tena hata kama sitamkumbuka.”

Kisha akageuka kwa Khadija. “Ukisahau mimi, usijilaumu. Kama moyo wako utaweza kunitambua bila akili yako, nitajua kuwa mapenzi hayakupotea.”

Wakakubaliana.

Wakaingia.

Ngazi zikiwa na mwanga wa ndoto, giza la kumbukumbu, na harufu ya mvua ya miaka iliyopita. Walianguka kwenye mwanga mwingine — dunia nyingine.

Walipofumbua macho yao, walikuwa… Kigoma.

Lakini Kigoma ambayo haijawahi kutokea. Kigoma yenye mnara mkubwa wa saa ambao hukimbia nyuma badala ya mbele. Kigoma yenye watoto wanaimba wimbo usio na lugha, lakini kila mtu huuelewa.

Ndipo, kutoka nyuma ya mti mkubwa wa miembe, msichana mmoja akatokea.

Macho yake yalikuwa kama usiku wenye nyota, nywele zake zikiwa kama miale ya asubuhi, na sauti yake… ilikuwa sauti ya mwisho aliyosikia Najim alipokuwa akilia kwa kimya miaka mingi iliyopita.

Layna.

Aliinua mkono wake, akasema:

“Najimu... umechelewa. Lakini moyo wangu bado uko hapa.”

---

Previoua Next