CHANGE 2
A Story by Elton Tonny
Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KWANZA
★★★★★★★★★★★★★
EFRAIM DONALD
Tupate mwanga zaidi kuhusiana na maisha halisi ya mwanaume huyu. Efraim Donald alikuwa ndiyo mzaliwa wa kwanza katika familia yenye watoto watatu. Mama yake, Halima, alikuwa ameachwa na mwanaume ambaye hakumwoa kisheria abaki kulea watoto hao peke yake tangu Efraim alipokuwa na miaka 9 tu, na hiyo ikamwacha Halima apitie mambo mengi magumu kwa sababu ya kutoweza kupata kipato cha kutosha kuwahudumia watoto wake kwa mahitaji yao mengi muhimu. Angalau alijikongoja kwa kufanya biashara za kuuza shanga, rozali, na urembo wa shingoni uliomhitaji afanye kazi kwa muda mrefu kuvitengeneza vitu kama hivyo kwa kuwa alitumia mbegu za matunda na mimea, lakini bado kipato kilikuwa kidogo sana.
Maisha yao yalikuwa magumu. Wakati mwingine ilibidi Efraim Donald aache kwenda shule ili amsaidie mama yake kwa kazi kama kuuza barafu, mkaa mdogo mdogo aliookota-okota na hata kufanyia watu kazi zao ili wamlipe chochote walichoweza. Alikua kwa kusontewa sana vidole kama mtu ambaye amelaaniwa, yeye pamoja na familia yake, kwa sababu hata ndugu zao wengi hawakujihusisha nao. Wadogo zake wote walikufa Efraim alipokuwa na miaka 19 baada ya kupatwa na ajali ya kuangukiwa na jengo walipokuwa wamesimama usawa wake. Kufikia kipindi hicho, Efraim Donald alikuwa mitaani tu akifanya shughuli zozote zile ili kumsaidia mama yake, na alikuwa amejitahidi sana kuwa na moyo wenye ukarimu kwa wengi hata kuwadaidia kwa vitu vingi lakini yeye kwa upande wake hakuwa akifanikiwa.
Baada ya vifo vya wadogo zake, Efraim Donald aliamua tu kuhama mji waliokuwepo na ili kwenda kutafuta maisha jijini, akimwacha mama yake huko, na ndiko alikoanza kufanya biashara za hapa na pale. Aliuza karanga, alipiga debe, alifanya udalali mdogo mdogo wa kila aina, hadi kuna mara ambazo alijiingiza katika mambo mengi haramu; yote hiyo ili kupata maisha aliyotaka sana ili kujiondoa pale pabaya alipokuwa. Angeona namna ambavyo watu au watoto wa watu wenye pesa waliishi na kujiahidi kwamba ipo siku angekuwa na maisha ya namna hiyo. Ingawa alikuwa kwenye mstari mbaya kimaisha, hakufanya mambo ambayo yangemwathiri vibaya kiakili au kimwili, kama kuvuta bangi au kutumia madawa ya kulevya, kwa sababu pamoja na vidogo alivyofanikiwa kupata alikuwa na akili nzuri sana ya kuendesha maisha yake kwa mpangilio ili asije kukata tamaa.
Lakini ilifikia kipindi akahisi kuchoka, kwa sababu umri ulienda, na mambo mengi hayakwenda vizuri sana. Alikuwa akifanya kazi kama kinyozi kwenye saluni ndogo alipokuwa na miaka 35, na ndiyo iliyokuwa inamsaidia sana hata kutengeneza mitaji ya kufanya biashara za pembeni, huku akimhudumia na mama yake aliyekuwa kule kule mkoani kwao. Alikuwa amepita kwa wanawake kadhaa ambao mwisho wa siku wangeachana naye kutokana na yeye kuonekana hana uwezo wa kuwamudu, na ni moja kati ya mambo mengi yaliyomkosesha amani ya moyoni kwa sababu ya kujiona ni kama hafai.
Basi, siku fulani alikuwa amekwenda kuonana na mwanaume mmoja kijana aliyefanya kazi kwenye kituo cha kujaza mafuta, au sheli, ambaye alikuwa na pesa yake ya kukopeshwa ili amrudishie. Yaani, Efraim Donald alimdai mwanaume huyo pesa, na ilikuwa imepita miezi miwili akiwa anamzungusha tu kwa kusema angemlipa wakati aliomba akopwe kwa wiki moja tu, na sasa Efraim alikuwa na uhitaji wa hali ya juu uliomnyima budi ya kwenda kumfata ili akaichukue; kwa kuwa ilionekana wazi kwamba alikuwa anakwepwa.
Alifika sehemu hiyo ya shell na kumkuta huyo mwanaume, naye akamwambia kilichompeleka hapo ni uhitaji wake wa kupata hela siku hiyo hiyo, na hakuwa na njia nyingine ya haraka kwa sababu alichotaka kufanyia kazi kilikuwa cha lazima. Lakini mwanaume huyo akaanza kumwambia kwamba hakuwa na hela, kwamba hata yeye ana wakati mgumu sana kwa hiyo hangeweza kumsaidia, ila Efraim akamweleza kuwa kilichompeleka hapo haikuwa kuomba msaada bali kuchukua kilicho halali kwake. Jambo hili likazua ugomvi mkubwa kwa sababu mwanaume yule alionyesha dharau sana, na ilimtia Efraim Donald ghadhabu nyingi kiasi kwamba akaanza kupigana naye kwa hasira. Walipigana mpaka kuumizana haswa, na ndipo maaskari wa ulinzi wakawa wamefika hapo ili kuwaachanisha.
Wakati hayo yalipokuwa yanaendelea, kuna gari la kifahari lilikuwa limefika sehemu hiyo ili kujazwa mafuta, na aliyekuwa mwendeshaji ni yule yule Godwin Shigela. Aliweza kuona ugomvi huo, hasa kwa sababu watu wengi walijaa sehemu hiyo, naye alikuwa ameanza kuliondoa gari lake hapo ili akatafute sehemu nyingine ya kuweka mafuta lakini baada ya kumwona askari mmoja akimwongoza Efraim kuelekea upande mwingine wa eneo hilo, akaghairi kuondoa gari lake hapo. Ni kwamba alikuwa amemtambua, na ilikuwa imepita muda mrefu sana bila ya wawili hawa kuonana. Walisoma wote sekondari mpaka kufikia kidato cha nne ndipo wakaachana, na walikuwa ni marafiki wale wa kawaida tu siyo kwamba walipatana kwa ukaribu sana, lakini baada ya kumwona Efraim ndani ya shida hiyo, Godwin akataka kumsaidia.
Efraim Donald pamoja na yule mwanaume waliyepigana walipelekwa kwenye ofisi ya kituo cha mapolisi na kukalishwa ili ijulikane nini kilikuwa chanzo cha wao kupigana namna ile na adhabu gani ichukuliwe dhidi yao, na Efraim alieleza mengi sana kwa hisia kali kwa sababu ni yeye ndiye aliyeona kwamba hakutendewa haki. Lakini maaskari wa hapo wakawa wanasema eti yeye ndiyo mbaya kwa kuwa alimfata mtu kazini na kuanzisha vurugu, kwamba kama ni hayo mambo ya kibinafsi angemsubiri huyo mwenzake aondoke kazini ili ndiyo akamdai kuliko kuanza kupigana naye pale.
Maaskari walikuwa wanataka wawili hao watoe faini kubwa sana kwa sababu ya vurugu zile la sivyo wangewaweka ndani, na bila kukawia, mwanaume yule aliyekuwa anadaiwa na Efraim Donald akatoa faini kwa upande wake. Maaskari walitaka kila mmoja wao atoe laki moja, lakini mwanaume huyo akasema yeye alikuwa na elfu sabini tu na akawaomba waikubali, hivyo wakamkubalia na kumwachia. Efraim Donald alimwangalia sana mwanaume huyo, kwa sababu yeye alikuwa anamdai elfu hamsini, lakini akaona asimlipe makusudi kabisa ila kwenye kutoa faini ili kujiokoa akatoa kiasi cha juu. Aliingiwa na hasira zaidi, lakini hapo hakuwa na njia ya kujitoa kwa sababu hakuwa na pesa hata kidogo, kwa hiyo angefungiwa ndani ya gereza dogo na kuambiwa angekaa humo kwa siku mbili zaidi.
Lakini Efraim hakuwa bado amepelekwa ndani na maaskari hao ili kufungiwa pale Godwin Shigela alipofika na kuwaambia maaskari kwamba amekuja kumtolea dhamana rafiki yake. Efraim Donald alipomwangalia Godwin kwa mara ya kwanza, alihisi ni kama anamjua ingawa hakumkumbuka vizuri sana, na mwanaume huyo akawapa maaskari laki tano baada ya wao kumwambia ni laki moja tu ndiyo iliyohitajika. Ingawa ilionekana kama ametoa pesa kwa njia fulani ya dharau, wakazipokea, kisha wakamwachia Efraim Donald na kumwonya asirudie tena kufanya jambo kama alilofanya leo.
Baada ya hapo, Godwin Shigela akaongozana na Efraim mpaka kwenye gari lake, huku mwanaume huyu akiwa bado na maumivu mwilini na majeraha usoni ya kuvimba, naye Godwin akamwambia aingie ndani ya gari lake ili waongee vizuri.
"Dah, kaka pole sana aisee. Nimekuona hapo sheli nimekukumbuka sana... Efraim bwana. Za siku?" Godwin akasema.
"Siwezi kusema ni nzuri maana na hali uliyonikuta nayo ndiyo kama hivyo. Mambo hayajawa mepesi kwangu kaka," Efraim akamwambia.
"Pole sana," Godwin akasema.
"Ila unajua... nahisi kama nakufahamu sijui... tulisoma wote au?" Efraim akauliza.
"Ndiyo, ni muda mrefu. Mimi ni Godwin. Tumemaliza form four pamoja."
"Ooh sawa... Godwin Shigela... walikuwaga wanakuita mmasai mfupi..."
"Ahahahah... ndiyo mimi."
"Aisee... ni muda mrefu. Sikumbuki watu wengi niliosoma nao yaani..."
"Hiyo ni kawaida. Lakini vipi wewe? Maisha... yaani, tulipomaliza tu mitihani ukapotea, sikukuona hata Grad. Uliendaga wapi?"
"Aah... mambo mengi mazito ndugu yangu, basi tu. Kipindi hicho mambo hayakuwa rahisi kwetu kama tu yalivyo magumu sasa hivi, nilimaliza form four kwa msoto pia, na bado nilifeli... nilifiwa na wadogo zangu wawili ndani ya siku moja tu... kwa hiyo, kidogo nikahama kuja kutafuta maisha jijini hapa... ni mambo mengi... mambo mengi sana siyo rahisi kuelezea yote kaka," Efraim akasema kwa hisia.
"Pole sana. Ngoja twende hapo hospital angalau wakufanyie..."
"Hapana, hapana, niko sawa Godwin. Nashukuru sana kwa msaada wako. Sijui hata nitaweza vipi kukulipa kaka maana... uwezo wenyewe hata sina," Efraim akasema.
"Nilikuwaga nakuona hata shuleni kaka, hukuwa... ukijichangsnya na watu, we' ulikuwa wa kuja, kuandika, na kuondoka. Najua mlikuwaga na maisha magumu sana, na roho imeniuma kuona kwamba bado mambo siyo rahisi kwako... nataka nikusaidie rafiki yangu," Godwin akasema.
Efraim Donald akatabasamu na kusema, "Nitashukuru sana kaka. Nahitaji kupata angalau kazi itakayoni-boost haraka maana mama umri unaenda, na bado me mwenyewe nina mambo mengi ya kurekebisha... wakati mwingine najitahidi kuwa mwema lakini malipo ni ubaya tu... inachosha sana. Sa'hivi ningekuwa hata na watoto watatu kaka lakini mama zao wakatoa mimba... na nani wa kuwalaumu? Hata kama wangezaa, ningesaidia vipi kuwatunza? Mpaka nahisi aibu yaani..."
"Usihisi hivyo, lakini ninaelewa unachopitia. Hata mimi sikupita sehemu rahisi, ila sikukata tamaa. Nawe pia usikate tamaa, utatoka tu," Godwin akamwambia.
"Asante sana Godwin..."
"Huyo mwanaume uliyegombana naye, ni mtu wa karibu?"
"Ni mpumbavu sana huyo. Nilimkopesha pesa maana alikuwa na shida akaahidi kurudisha ndani ya wiki... sa'hivi imepita miezi kaka... namwomba ananipiga chenga, mama yangu anakosa hata hela kidogo ya kula kwa sababu mimi nimejifanya mwema kwa mtu halafu nikalipwa fadhila kwa kutemewa mate usoni. Afu' alivyo na dharau anasema 'kwani hamsini pesa gani' wakati anaiomba alikuwa anatoa hadi na machozi, sa'hivi kapata yeye hataki kurudisha wema... yaani najiona fala sana Godwin... samahani kwa maneno yangu lakini...'
"Hapana usijali, naelewa. Ngoja nikwambie kitu. Usije ukafikiri kwamba maisha kwa watu ambao tayari wana pesa ni rahisi, wengi wao huwa wanazipata kwa njia ya mkato. Wengine wezi, wengine mashoga, wengine wafisadi, wengine wanafanya umalaya tu, na wanaonekana kufurahia maisha yao kwa kuwa wanaishi wakijua kwamba hicho walichonacho kinaweza kupotea muda wowote, ndiyo maana hawaachi kuyaishi kwa njia hiyo. Usije hata siku moja kudhani kwamba wema unaoonyesha utalipwa kwa wema, kwamba labda ndiyo utatajirika sasa... hapana. Ukikaa kusaidia watu wakati wewe mwenyewe una shida, hautafika popote kaka, kwa hiyo inabidi uanze kuishi kwa njia ya kichoyo, lakini... lakini Efraim, ile ambayo itakufanya hata ukitoa pesa nje, kwako wewe ndiyo zinazidi kuongezeka mfukoni."
Godwin alisema maneno hayo kwa uzito sana, naye Efraim akawa ameangalia chini kwa umakini akiwa anajaribu kuyaelewa kiundani zaidi.
"Unamaanisha nini... kichoyo?" Efraim Donald akauliza.
"Unataka nikusaidie ili uache kuishi namna hii... na uanze kuishi maisha mazuri kwa muda wote uliobakiza hapa duniani Efraim?" Godwin akauliza.
Efraim Donald akamwangalia tu usoni kwa umakini, kisha akatikisa kichwa kukubali.
Godwin akatabasamu kwa mbali na kumshika begani, kisha akasema, "Furahia kukutana nami Efraim, kwa sababu ukihakikisha unafuata kwa umakini kile nitakachokwambia, utaishi maisha mazuri sana... na utapata chochote kile unachotaka kwa ajili yako mwenyewe."
Efraim Donald akatega sikio lake kwa umakini, na mwanaume huyo akaanza kumwelezea mambo mengi ambayo kiukweli yalimchanganya sana mwanzoni, na baada ya kueleweshwa vizuri hata zaidi, mwanaume huyu akawa kama mtu aliyeachwa katikati ya barabara iliyomtaka achukue uamuzi wa kutumia upande fulani ili aweze kufika alikotaka kwenda, kwa kuwa mambo mengi yalikuwa ni mazito sana. Godwin alimhakikishia kwamba hakukuwa na haja ya kuhofu lolote lile, kwa sababu hata yeye alifanikiwa kupitia njia kama alizomwambia, hivyo akampa muda wa kufikiria aliyomwambia kisha angemjulisha. Akamwachia mwanaume huyu kiasi cha shilingi laki tano, kama tu alivyowapa maaskari wale, jambo lililomwambia Efraim Donald kuwa Godwin alikuwa akipata pesa nyingi sana, naye akawa ameingiwa na tamaa ya kutaka kujichumia pesa kama hivyo ili aachane na maisha aliyoyaona kuwa batili mno.
Wawili hawa wakaachiana namba za mawasiliano, hususani namba za Godwin kwa Efraim ili akiwa tayari kuafikiana na ushauri wake basi amtafute ili amwelekeze mambo mengi vizuri hata zaidi. Mwanaume huyo akampeleka Efraim mpaka kule alikoishi, kisha akamuaga huku akisema angesubiri kwa hamu kusikia jibu lake kwa uchanya, naye akaondoka na kumwacha Efraim Donald anatafakari kila kitu alichotoka kuambiwa.
★★★
Ilipita kama wiki baada ya Efraim Donald kuachiwa laki tano na Godwin Shigela, na sasa mwanaume huyu alikuwa ameamua kwenda nyumbani, yaani mkoani kwa mama yake ili akamsalimie kwa sababu hawakuwa wameonana kwa muda mrefu. Halima alimpokea mwanaye kwa furaha, na kufikia kipindi hiki mwanamama huyo alikuwa akiishi kwenye nyumba ya kupanga pamoja na vijana wengine watatu wa kiukoo, ambao walimsaidia katika shughuli zake za hapa na pale. Hata baada ya Efraim kufika na kutazama jinsi ambavyo mama yake aliishi, aliingiwa na simanzi kwa kuwa alihisi ni kama alishindwa kubadili maisha ya mzazi wake kuwa bora hata baada ya miaka mingi kupita.
Akiwa huku, yeye Efraim Donald alikaa kwenye chumba cha kulipia kwenye nyumba ya wageni kwa kutoa elfu sabini ili akae hapo kwa wiki, na ndiyo angekuwa anakwenda kwa mama yake ili kumtembelea kisha baada ya hapo angerudi jijini kwao. Dhumuni la yeye kuja huku ilikuwa ni ili azungumze kwa kina na mama yake kuhusu badiliko alilotaka kufanya maishani, na aliamini mama yake angemwongoza vizuri ili aweze kufanya maamuzi sahihi. Baada ya kukaa hapo kwa siku mbili, siku ya tatu alimwita mama yake ili aende pale alipochukua chumba waweze kufanya maongezi kwa kina. Halima alikwenda huko mida ya jioni baada ya kumaliza shughuli zake ndogo ndogo, naye Efraim akampokea vizuri na kuagiza chakula kizuri kwa ajili yake.
"Kwa hiyo tokea alipotoa mimba yako, mpaka leo hamjaonana tena?" Halima akawa anamuuliza huku akiendelea kula taratibu.
"Hapana, hatujaonana. Rafiki yake tu aliniambia hayo, hata nilipomtafuta sikumpata. Ila mara ya mwisho tumeonana aliweka wazi kabisa kwamba hawezi kuendelea kuwa na mwanaume suruali kama mimi... na inawezekana tayari alikuwa ameshampata huyo mwanaume wake mwingine ndiyo maana akaitoa mimba..." Efraim akamwambia.
"Mpumbavu sana. Yaani mwanangu, wanawake wa siku hizi ni wapumbavu sana, wanachoangalia ni pesa tu na si kingine. Ningekuwa na mjukuu wa tatu sasa hivi mimi aagh..." Halima akaongea kwa kuudhika.
Efraim Donald akatabasamu kwa mbali.
"Vipi kazi lakini?" Halima akauliza.
"Hivyo hivyo tu," Efraim akajibu.
"Uliponiambia kuhusu yule mshenzi aliyekudhulumu hela yaani nilitamani nije huko nimnyonge kwa mikono yangu mwenyewe! Watu wanafikiri hela zinaokotwa sijui? Na wewe Efraim uwe unaanglia, watu wengine siyo wa kuwaamini, hiyo hela ungetuma huku tukatumia badala ya kumpa huyo mjinga," Halima akasema.
"Ahahahah... unapenda hela mama..."
"Siyo kupenda hela, kulikuwa na shida. Angalau we' ndiyo unaweza kunisaidia..."
"Najua. Samahani. Mambo ni mengi afu'... magumu."
"Yaani! Sijui mpaka lini jamani, ah-ah," Halima akaongea na kuendelea kula.
Efraim Donald akamwangalia kwa umakini sana, kisha akasema, "Nafikiri nimepata njia ya kubadili maisha yetu mama."
Halima akamtazama kwa umakini pia, kisha akasema, "Nakusikiliza."
"Kuna... rafiki yangu... anaweza kunionyesha njia fulani ya kupata mali... haraka," Efraim akasema.
"Ahah... Efraim... hebu achana na hayo mambo. Nimeshakuelewa vizuri, na ndiyo maana nakwambia achana nayo. Mengi tunayasikia sijui mzee nani anafanya nini, lakini hakuna lolote huko. Unafikiri kama wangekuwa na huo uwezo kungekuwa na umasikini hapa nchini? Na wenyewe wanatafuta hela kwa hao hao wanaowaahidi hela nyingi, ni akili hiyo?"
"Hapana mama, siyo hivyo. Hii ni tofauti."
"Kivipi?"
"Ikiwa nitakubali kufanya jambo hilo... kuna malipo fulani natakiwa kutoa... lakini siyo pesa," Efraim akasema.
"Malipo yasiyo ya pesa? Efraim... unaongelea masuala ya kafara?" Halima akauliza huku akikiweka chakula pembeni.
Efraim Donald akabaki kumtazama tu usoni.
"Jamani! Mwanangu imeshafika mpaka hatua hiyo?"
"Mama, hapa kuna nafasi ya mimi kufanikiwa kweli... nachotaka kukwambia siyo masihara..."
"Najua siyo masihara kwa sababu nakujua vizuri. Akili yako ikishataka kitu yaani ndiyo utakazia hicho hicho tu, hautasikiliza la mwadhini wala mnadi suala. Efraim hayo mambo siyo, na unaweza ukajiweka kwenye matatizo makubwa sana ukiamua kufuata hiyo njia..."
"Hapana mama, niamini. Huyu rafiki yangu nayekwambia... amefanikiwa sana. Na... sidhani kama mambo ni mazito kihivyo maana...."
"Ukiambiwa unitoe mimi kafara je?" Halima akamkatisha.
"Mama..." Efraim akamwita kwa upole.
"Yaani Efraim kwa kweli sielewi. Mimi nitakupa support kwa mambo mengi sana kwa sababu... najua tulikotoka... ila sasa hivi nikiona unakoelekea siyo kuzuri lazima nikwambie kwamba sitaweza kukuunga mkono kabisa... yaani kwa jambo hilo siwezi," Halima akasema.
Efraim Donald akaishika mikono ya mama yake na kumwambia, "Mama, sikuombi uniunge mkono, ninakwambia tu kwamba ninataka kujaribu hii bahati ili nione itanifikisha wapi. Sitakubali kukuweka sehemu mbaya nikigundua kwamba kuna vitu haviwezekani kufanywa, na ninakuamini sana ndiyo maana nimeona nikwambie. Sipendi kabisa kukuona unaendelea kuteseka toka zamani wakati mimi nipo na ninaweza kufanya jambo la kukuinua mama yangu. Nakuahidi kila kitu kitakuwa sawa. Naomba tu uniamini."
"Efraim... Efraim... Efraim mwana wangu! Haya. We' fanya unayotaka kufanya, ila usisahau maneno yangu. Mimi nitaendelea tu kukaa namna hii hii maana sijabakiza muda mrefu wa...."
"Usiseme hivyo mama. Utaishi maisha marefu na mazuri. Nakuahidi. Nitafanikiwa," Efraim akasema kwa ushawishi.
Halima hakuwa na namna ila kumwacha mwana wake afuate kile ambacho akili yake ilikuwa imemtuma, na ingawa aliogopa kwa ajili yake, yeye pia alitaka kuona namna ambavyo mambo yangekwenda ikiwa mtoto wake angechukua hatua hiyo. Kwa maneno mengine ni kama akili zao zilifanana hasa kwa sababu walielewana kwa mengi sana kutokana na magumu waliyopitia maishani.
Baada ya hayo, Efraim Donald akamweleza sasa kwamba bado hakuwa ameongea na Godwin tena baada ya msaada aliompatia wiki iliyopita, na ndiyo alikuwa anafikiria kumtafuta ili waongee tena. Akamhakikishia mama yake kuwa ikiwa njia ambazo angeonyeshwa zingezidi matarajio yake basi angeahirisha kufuata suala hilo na kumwomba tu Godwin amsaidie kupata kazi nzuri, na kwa hilo mama yake akawa ameridhia.
★★★
Efraim Donald alirejea jijini alikoishi baada ya safari yake kwenda kumwona Halima, na sasa alikuwa ameiweka akili yake sawa zaidi baada ya kuongea na mama yake na kuamua kumtafuta Godwin Shigela. Mwanaume huyo alifurahi sana na kumwambia Efraim wakutane siku na saa fulani, naye Efraim Donald akaridhia na kuanza kujipanga kwenda kukutana naye. Alielewa kwamba bila shaka angekutana na mambo mengi ambayo yangemfanya awe kama mgeni, lakini akajiahidi kusimama kiume ili akutane nayo na kushughulika nayo kwa njia ambayo ingempa faida kweli.
Wawili hawa walikuja kukutana kwenye siku ambayo Godwin aliamua kumtembeza Efraim kwenye sehemu kadhaa kati ya nyingi ambazo alimiliki kutokana na utajiri mwingi aliojichumia, kisha akakaa naye na kuanza kumweleza namna ambavyo alifanikiwa kupata hayo yote kwa kipindi kifupi sana.
Alimwambia kwamba kupata vitu hivyo haraka haikumaanisha vilikuja kimuujiza tu, lakini yeye Efraim kama mtu mzima angepaswa kutambua kwamba kila kitu kilitakiwa kuonekana kuwa halali kwa nje hata kama njia za ndani zilikuwa za mkato, na akasema njia aliyokuwa ametumia haikuwa ya mchezo hata kidogo. Akamwambia kwamba kuna nguvu kuu zilikuwa zinahusika, na wengi waliotaka kujiingiza katika jambo kama hilo waliambulia patupu kwa sababu hawakuwa na mioyo mikuu ya kuchukua hatua nzito ambazo zilihitajika ili kuwafanya wafanikiwe kweli; na baadhi yao hata walikufa.
Efraim Donald alikuwa ametarajia kuambiwa vitu kama hivyo, lakini bado alihitaji kujua kwa undani ni mambo kama yapi yaliyohusika. Godwin akasema ndiyo hicho sasa. Hangejua ni mambo gani ambayo yangehusika mpaka aingie huko ili kufanya makubaliano na "watu" waliotoa msaada huo, kwa hiyo alitakiwa kujua kwamba akienda huko, chochote kinaweza kutokea.
Hakukuwa na mambo yanayofanana kwa watu waliojihusisha na jambo hilo, kwa hiyo hata yeye angekutana na jambo tofauti. Godwin akamwambia asiwe na hofu kubwa labda ingemlazimu kufanya jambo baya mno, lakini akamwambia hapo kikubwa ni kuwa tayari kwa ajili ya lolote. Ikiwa kwa sasa angehisi kwamba hangeweza, basi angetakiwa kuacha. Lakini kama alikuwa anaenda, angetakiwa kuhakikisha anaiweka akili yake tayari kutimiza chochote kile ambacho angeombwa kufanya.
Efraim Donald alionyesha kuwa na uhakika baada ya kumwambia Godwin kwamba yuko tayari, hivyo aonyeshwe mambo hayo yalikuwa ni nini. Godwin akampongeza kwa hilo, kisha akamwambia kwamba angemkutanisha na "mawakala" wa mtu fulani muhimu sana ambaye ndiyo alikuwa chanzo kikuu cha kuwawezesha wapate utajiri, na ni mawakala hao ndiyo ambao walimwakilisha, na ikiwa angejitoa kwao kwa asilimia zote basi angepata faida kubwa sana. Akamwonya pia, akisema alitakiwa kuwa mwangalifu mno ili chochote kile ambacho YEYE Efraim Donald angechaguliwa kufanyia kazi, ahakikishe anakitimiza kwa nguvu zake zote kwa sababu ikiwa asingefanikiwa basi kungekuwa na madhara.
Baada ya kuwa amemwelewesha waziwazi lakini kwa njia yenye mafumbo mengi, Godwin akampeleka Efraim sehemu yenye kumbi ya starehe ili wajifurahishe pamoja, naye akamfanyia mpango ili apate vitumbuizo kutoka kwa wanawake kadhaa na ajichagulie yeyote aliyetaka ili kufanya naye mapenzi. Ilikuwa moja kati ya njia nyingi ambazo Godwin alitumia kumwonyesha kwamba angefurahia vitu vingi vizuri kama angefanikiwa kufata maagizo yake, na mambo hayo yalikuwa yameanza kumwingia vyema Efraim Donald ndani ya moyo wake baada ya kuonyeshwa raha ambazo angezipata kwa sehemu tu, hivyo akawa anataka kuzipata hata zaidi.
★★★
Baada ya siku chache, Godwin Shigela akamtafuta Efraim Donald na kumwambia kwamba sasa ulikuwa umewadia wakati wa kwenda kukutana na "mawakala" wale ili mpango uanze kazi. Efraim alielewa kwamba vitu hivi huenda hata vingehusisha masuala ya kuzimu huko, lakini tayari alikuwa ameshaazimia moyoni mwake kuwa angefanya yote yaliyo ndani ya uwezo wake kuhakikisha anafanikiwa. Ni maisha magumu yenye kumchosha sana aliyokuwa amepitia, kwa hiyo kama hii ndiyo ilikuwa nafasi aliyoshushiwa ili ayaonje na kuyaishi yale maisha mazuri zaidi, yeye alikuwa nani kuikataa?
Alijiandaa vyema na kukutana na rafiki yake, kisha Godwin Shigela akampeleka mpaka sehemu ya mbali ya jiji hilo iliyokuwa na hospitali ndogo iliyojengwa zamani sana. Walikuwa wamekwenda usiku, usiku wa saa nane, kwa hiyo walifika huko yapata saa tisa usiku. Eneo hilo halikuwa na makazi mengi sana karibu ingawa kuna watu waliishi kwenye mitaa yake, naye Godwin akamwambia kwamba hapo ndiyo mahali ambapo kulikuwa na "mlango" muhimu wa kuwakutanisha na hao mawakala. Efraim Donald hangehitaji kuuliza maswali kama hao mawakala ni nani, na walimfanyia kazi nani; tayari alielewa kabisa kwamba huu mchezo wote ulikuwa na jina moja tu la aliyekuwa kama mhusika mkuu: Lucifer.
Godwin akamwambia Efraim kwamba "mlango" huo wa kuwapeleka kwa mawakala wale ulikuwa ndani ya chumba kimoja cha mochwari, ambako hakuna mtu yeyote aliyetakiwa kuingia kwa wakati huu isipokuwa yeye, kwa sababu tayari alikuwa na makubaliano na mtunzaji wa hifadhi za maiti; kumaanisha alikuwa na funguo kwa ajili ya kuingia ndani huko. Hata mtunzaji huyo hakujua kuhusiana na habari hizi lakini Godwin alikuwa ameshamnunua, yaani alikuwa anamlipa pesa ili asiseme kwamba kuna mtu ambaye huenda pale mara kwa mara kwa ajili ya kufanya biashara zisizoeleweka.
Wawili hawa wakaelekea mpaka upande wa vyumba vya mochwari, naye Godwin akampigia simu mhifadhi huyo na kumwambia yuko nje na aje kumruhusu apite kwa kufungua geti. Kulikuwa na kamera za ulinzi za CCTV pia kwa ndani na nje kwa hiyo mhifadhi yule alitakiwa kuhakikisha zinazimwa kwa wakati huu mpaka Godwin amalize biashara zake. Baada ya mhifadhi huyo kuwafungulia, marafiki hawa wakaelekea mpaka kwenye chumba kile ambacho Godwin alidhamiria kumpeleka Efraim, kisha akatangulia kwenda ndani huku Efraim akifata nyuma taratibu. Mwanaume huyu hakuwa na woga wa kuona maiti wala nini baada ya kuingia, ila bado alijiuliza maswali mengi sana kuhusu "mlango" huo, na hivyo angetakiwa kusubiri kuona matokeo ya mambo haya yote.
Mlango wa kuingilia ndani ya chumba hicho ulifungwa kwa nje na yule mhifadhi, wawili hawa wakiachwa ndani humo ambapo palikuwa na meza kadhaa zilizofunika miili michache pamoja na masanduku makubwa yenye majokofu ya kuhifadhi miili ya maiti, na kiukweli harufu ya ndani hapo haikuwa nzuri hata kidogo. Kulikuwa na giza kiasi katika chumba hiki lakini mambo yalionekana vyema kama kwa mwanga wa mbali wa tochi. Godwin akafika usawa wa ukuta na kusimama, akimwambia Efraim asimame pembeni yake, naye akatii. Akamuuliza ikiwa yuko tayari, na baada ya Efraim kutikisa kichwa kukubali, Godwin akamwambia aunganishe viganja vyake na kufumba macho, kisha akae kwa kutulia. Alikuwa ameshamwambia kwamba asishangae endapo angekutana na hali iliyobadilika, kwa hiyo Efraim akawa ameiandaa akili yake kwa chochote kile ambacho angeona.
Godwin akaanza kuongea maneno fulani ambayo hayakueleweka hata kidogo masikioni mwa Efraim, na mwanaume huyu akaendelea kusimama kwa utulivu zaidi akisubiri maagizo mengine. Ndipo akaanza kuhisi kama upepo mkubwa ukipuliza sehemu aliyokuwepo, lakini tena ni kama alikuwa kwenye sehemu isiyotoa sauti yoyote hata kidogo. Aliingiwa na msisimko zaidi baada ya kuanza kusikia sauti kama hatua za mtu anayetembea kumwelekea, lakini akajitahidi kutofumbua macho yake hata mara moja. Sauti hizo zikageuka kuwa kama sauti za matone ya maji yakidondoka kidogo kidogo ndani ya tenki lenye maji, na ndipo sauti nzito ikasikika ikifanya kama mguno wa mtu aliyeridhika.
"Hmmmm... Efraiiimmm..."
Jina lake lilitajwa kwa njia nzito sana, na wasiwasi mwingi ukamwingia mwanaume huyu kwa kutotambua nani aliyetamka jina lake.
"Piga magoti..."
Mnong'onezo huo kutoka kwa Godwin ulipenya vyema masikioni mwa Efraim, naye akatii na kupiga magoti chini kabisa.
"Godwinnn... mwana wa Isaya Shigelaaah..."
Sauti hiyo nzito ikasema maneno hayo.
"Ni mimi... mtumishi wako," Godwin akatamka maneno hayo.
Efraim Donald alikuwa ameingiwa na wasiwasi mwingi sana kufikia hapa, akijiuliza ikiwa bado alitakiwa kuendelea kufumba macho au la.
"Umeniletea zawadi Godwinnn..." sauti hiyo ikasema.
"Nimeleta zawadi bwana wangu. Ni zawadi ambayo itakupa kilicho bora kwa njia yoyote unayotaka..." Godwin akasema.
"Hmmmm... Efraiiimmm..." sauti hiyo ikaita.
Efraim Donald, akiwa bado amefumba macho yake, akajiongeza na kusema, "Ndiyo, bwana wangu..."
Sauti hiyo ikaanza kucheka sana kwa njia iliyomuumiza Efraim masikio, lakini akajitahidi kujikaza na kuendelea kushikanisha viganja vyake huku akiwa amefumba macho.
"Fungua macho yako Efraiimmm..."
Baada ya sauti hiyo kusema hivyo, Efraim Donald akafumbua macho yake na kushangazwa sana na mazingira aliyojikuta katikati yake. Ilionekana ni kama yuko msituni, pakiwa na uoto mwingi wa asili, na mbele yake vilisimama viumbe vitatu virefu sana vilivyofunikwa kwa nguo nyeusi juu mpaka chini. Hakuelewa walifikaje hapo, lakini akajitahidi kujikaza zaidi na kuonyesha ujasiri na uhakika. Akaangalia pembeni na kumwona Godwin akiwa amepiga magoti kando yake, na rafiki yake huyo akamtikisia kichwa kumwonyesha kwamba wako pamoja.
"Unajua uko mbele ya nini Efraiimmm...?" sauti hiyo ikauliza.
Efraim aliweza kutambua sasa kwamba huyo kiumbe aliyesimama katikati ya wale wawili ndiye aliyeongea, akiwa kama mwakililishi na wakala mkuu wa mzee mwenyewe, naye Efraim akasema, "Ndiyo bwana wangu. Niko mbele ya sehemu takatifu."
Sauti hiyo ikacheka kwa njia iliyojaa hila nyingi sana, naye Efraim akamwangalia Godwin kiufupi, ambaye alimwonyesha kwa ishara ya macho kuwa anajitahidi.
"Utanipa nini Efraiiimmm...?" sauti hiyo ikauliza.
"Chochote kile utakacho bwana wangu..." Efraim akajibu huku mapigo yake ya moyo yakidunda kwa nguvu sana.
"Na wewe unataka nini, mwanangu?" sauti hiyo ikauliza.
"Ninahitaji... kupata pesa na... mali nyingi sana... bwana wangu..." Efraim akasema.
"Hmmmm... ni mambo ambayo wengi hutaka... lakini nahitaji kujua kwa nini unayataka..." sauti hiyo ikasema.
"Ninataka kuboresha maisha yangu... ninataka nisiendelee kuonekana kuwa kitu cha kudharaulika bwana wangu... nipate heshima... si heshima kama unayostahili wewe... yaani heshima isiyoweza kukaribiana na yako... bali heshima ile itakayozidi kukupa utukufu wewe pekee bwana wangu..." Efraim Donald akasema.
"Hmmmm... maneno mazuri sana. Nimekuangalia Efraim... kwa muda mrefu. Wewe ni kiumbe wa pekee... na upekee wako utakufikisha mbali ikiwa tu utafanya kile ulicholetwa duniani kufanya.... NIABUDU MIMI EFRAIIMMM!"
Sauti hiyo ilinena hayo kwa uzito sana, naye Godwin akainama zaidi kama anasujudu, kitu kilichomfanya Efraim Donald atende namna hiyo hiyo pia.
"Unajua kazi ya wafanyakazi wa mochwari ni nini?" sauti hiyo ikauliza.
Efraim Donald akatulia tu akiwa bado amesujudu bila kutoa jibu.
"Kazi yao ni kupunguza uzito wa hofu inayosababishwa na kifo, na wakati huo huo wakipata faida kutokana na msiba unaowapata wengine. Wanawachukua watu waliokufa na kuwapendezesha; wanazitengeneza nywele zao, wanawavalisha nguo safi, halafu mwishowe wanakuja kutupwa chini ya ardhi chafu. Ila unafikiri hao wafu huwa wanajali hilo? Hapana... hawajali. Lakini watu wa mochwari hawafanyi hayo kwa ajili yao. Wanafanya hayo kwa ajili ya wale wanaowaombolezea. Wanawarahisishia kusema kwa heri, kama njia ya kutoa kitulizo cha kihisia. Wanawasaidia kukubaliana na ukweli wa kwamba mpendwa wao amewatoka daima, na wakati huo huo wakiingiza malipo mifukoni mwao. Sababu bila shaka ni hofu. Watu huogopa kifo, na pale mtu wa karibu anapokufa inawalazimu kukumbuka na kukubali kwamba nao pia watakufa. Wanyama hawana hili tatizo. Muda mchache wa maumivu makali sana yenye kupelekea kifo ndiyo utakaomfanya mnyama atambue uzito wa jambo hilo... lakini wanadamu... mnaishi maisha yenu yote mkielewa kwamba muda wowote ule, bila onyo, bila sababu, maisha yenu yanaweza kukata. Hiyo ndiyo sababu mna mifumo kama hii ya mochwari... ili kusaidia kupambana na hali hiyo ya hofu ipasavyo..."
Efraim Donald hangeweza kuelewa ni kwa nini kiumbe huyo aliongea maneno hayo, lakini alijua lazima kulikuwa na ujumbe muhimu aliotakiwa kuelewa hapo.
"Nitakupa unachotaka Efraiimmm... ikiwa utanitumikia kwa njia nayotaka," sauti ya mwakilishi ikasema.
"Ndiyo bwana wangu... nitakutumikia wewe tu," Efraim akasema akiwa bado amesujudu.
"Hmmmm... ninakupa utumishi Efraiimmm... utumishi kwa mmoja wa wanangu... mtumikie... mpe anachotaka kwa wakati anaotaka... mfurahishe... na kila kitu unachokitaka utapewa..." sauti hiyo ikasema.
"Ndiyo bwana wangu... niko tayari..." Efraim Donald akasema kwa uhakika.
"Vizuri. Ninakupa mmoja wa wanangu... msababishaji wa ajali... mzuiaji wa hedhi kwa mwanamke... mpenzi wa damu changa ya mwanamke... mtumikieee... mfurahishe... apate nguvu zaidi... aniongezee nguvu maradufu... nami nitakupa kila kitu unachotaka..." sauti hiyo ikamwambia.
"Ninakubali utumishi huo bwana wangu... nitafanya unavyoniagiza," Efraim Donald akasema.
Sauti hiyo ikacheka kwa kishindo sana, kisha ikasema, "Inuka."
Efraim Donald akajinyanyua taratibu na kurudia kupiga magoti, vile vile na Godwin pia, kisha kiumbe huyo akaonekana kunyoosha mkono wake, sijui mkono, sijui nini; akiuelekeza kwa Efraim Donald, na hapo hapo mwanaume huyu akaanza kuhisi kizunguzungu cha hali ya juu, kama vile kuna vitu vilikuwa vikiingia ndani ya kichwa chake kwa kasi sana, na kwa muda huo aliweza kupatwa na vitu kama maono mengi sana yaliyomwelezea vitu vingi mno, kisha hisia hiyo ikakoma ghafla, naye akabaki kupumua kwa njia ya kichovu.
Aliponyanyua macho yake kumtazama yule kiumbe, akajikuta akiwa ndani ya chumba kile cha mochwari, na hapo hapo bega lake likashikwa. Akageuka kwa kasi na kukuta ni Godwin ndiye aliyemshika, naye Efraim akatulia na kukaa chini kwanza.
"Uko sawa?" Godwin akamuuliza.
Efraim Donald akatikisa kichwa kukubali.
"Umeonyeshwa vitu... vitu vingi sana unavyohitaji kufanyia kazi, siyo?" Godwin akauliza.
"Ndiyo. Nafikiri najua nachopaswa kufanya sasa," Efraim akajibu.
"Na?" Godwin akauliza.
Efraim Donald akaachia tabasamu lililoonyesha hila, kisha akasema, "Nafikiri nita-enjoy."
Godwin akatikisa kichwa chake huku akitabasamu kwa furaha sana, kwa kuwa sasa alitambua kwamba aliweza kumbadili rafiki yake awe aina ya mtu ambaye yeye pia alikuwa amegeuzwa kuwa. Akamsaidia kunyanyuka na kumwambia waondoke hapo upesi, na angemwelezea mambo yote aliyoona na aliyotakiwa kuanza kufanyia kazi ili zoezi lake la kupata mali nyingi lifanikiwe haraka sana. Mambo yote haya yalikuwa yenye kutisha sana, lakini kwa sasa Efraim alikuwa ameshabadilishwa moyo kwa njia kubwa mno, na angehakikisha anafanya kila kitu ili kukamilisha mambo yote aliyotakiwa kufanya kwa umakini wa hali ya juu.
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Comments