CHANGE 2
A Story by Elton Tonny
Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA PILI
★★★★★★★★★★★★
Ilikuwa hivi. Maono ambayo Efraim Donald alipewa na "wakala" yule, yalimwonyesha vitu alivyotakiwa kufanya ili aweze kupata mambo aliyohitaji, lakini kwa uchaguzi. Yeye angepata mali alizotaka, lakini pia alitakiwa kutoa malipo kwa njia ya DAMU. Ibada yake kwa wa Lucifer ilimaanisha alitakiwa kutoa sadaka za damu kwa mmoja wa viumbe wa roho aliyekuwa mzawa wake Lucifer, na kiumbe huyo alichukua malipo hayo kwa njia ya damu. Haikuwa kwamba alipewa jina hususa na Lucifer, lakini kiduniani kiumbe huyo wa roho alifahamika kama JINI SUBIANI, na ndivyo ilivyoachwa na kuendelea kutumiwa na wengi kama walivyomdhania ili kumtofautisha yeye na viumbe wengine wa roho kutoka upande huo.
Kwa hiyo uchaguzi ambao Efraim Donald alipewa kwenye yale maono ilikuwa ni kwa masharti; masharti magumu sana. Ikiwa alitaka kupata mali nyingi na kuendelea kuzidumisha, alitakiwa kufanya mambo mengi sana ya kisadaka na kwa mpangilio hususa mpaka kufikia wakati fulani, ndiyo angemaliza na kuacha kutoa sadaka hizo. Masharti hayo yalimhitaji aue mzazi wake, kisha achukue damu yake ya tumboni na kuiunganisha na damu yake kidogo (yaani damu ya Efraim), halafu ampatie roho huyo ili ainywe. Hilo ndiyo lingekuwa lipo la kwanza.
Wakala yule alipomnyooshea mkono na kumwonyesha yale maono alikuwa pia anamwingizia Efraim roho ya kiumbe yule ili iishi ndani yake, kwa hiyo kwa maneno mengine ni kwamba SEHEMU ya roho ya JINI SUBIANI ilikuwa ikiishi ndani ya Efraim Donald, ili wakati wa kutoa malipo, au sadaka, yeye Efraim angeiruhusu roho hiyo iuvae mwili wake na kuchukua malipo hayo ya damu kila mara yalipotakikana. Siyo mchezo!
Kwa hiyo ili lipo la kwanza litimie ilimbidi Efraim autoe uhai wa mzazi wake na kuunganisha damu yake kidogo na ya kwake ili ampatie Jini Subiani, na kwa hivyo mwanaume huyo akamtafuta baba yake mzazi ili amuue!
Efraim Donald alikuja kumpata baba yake mkoa mwingine, ambaye tayari alikuwa na familia yake nyingine baada ya kumtelekeza yeye na wadogo zake miaka mingi sana nyuma, kwa hiyo hasira ya Efraim kumwelekea ilimchochea kumkamata na kumpa kifo kibaya sana kwa kuuchoma-choma mwili wa baba yake kwa visu karibia kila sehemu ya mwili, na ndiyo akakusanya damu yake na kutokomea nayo. Alifanikiwa kufanya hivyo kwa msaada wa Godwin Shigela, ambaye alimuunga mkono kabisa katika jambo hilo kwa sababu isingeingia akilini mwa Efraim kumtoa mama yake kipenzi kama sadaka.
Baada ya kufanikisha hilo, alipelekwa tena kwa wale mawakala, nao walimwambia namna walivyofurahishwa sana na roho ya ukatili aliyoionyesha, kisha sasa wakamwelekeza jinsi ya kufanya kila mara alipohitaji kuitoa roho ya Jini Subiani iliyokuwa ndani yake ili aweze kuipatia damu hiyo. Alifata maagizo yao vizuri mpaka akafanikiwa kumtoa roho huyo mwovu kwa mara ya kwanza. Kutoka kwa roho huyo ndani yake kulifanya mwili wa Efraim ubadilike.
Angerefuka kufikia futi nane mpaka tisa, ngozi ya mwili wake ingekuwa kama imechanika-chanika na nyeusi sana, viungo vyake vingejipinda-pinda, na mikono na miguu yake ingerefusha makucha yake kwa kiwango kikubwa. Kichwa chake kingekuwa kikubwa sana kwa muundo kama wa kichwa cha anaconda mkubwa, na usoni alitisha balaa. Angekuwa na macho makubwa mekundu yenye lenzi zenye kufanana na zile za nyoka mwenye sumu, na mdomo wake ungekuwa mpana sana wenye meno mengi makali na ulimi mrefu sana mweusi uliojikata mara mbili! Kwa njia hiyo ndiyo angekuwa ameiachia roho ya SUBIANI imtoke, kisha ndiyo roho huyo angekunywa damu kama alivyofurahia.
Baada ya kukamilisha lipo la kwanza kwa kutoa sadaka ya mzazi wake, Efraim Donald aliambiwa kwamba kuanzia hapo mambo mengi yangeanza kumwendea vyema, yaani angefanisika sana. Lakini huo ungekuwa ni mwanzo tu. Hii ilimaanisha kwamba muda ungepita, angepata mali, angeendelea na shughuli zake nyingi, na baada ya muda huo kuisha angetakiwa kuanza kutoa malipo kwa mara nyingine tena kwa njia tofauti kabisa ambayo ingempelekea mpaka kupata utajiri wa kudumu; yaani kama angemaliza kila jambo aliloagizwa kwa usahihi kabisa, ingefikia hatua hangehitaji tena kutoa sadaka hizo za damu.
Malipo haya kwa ujumla yaliitwa "MZUNGUKO WA MWISHO." Kwa kuwa sasa alikamilisha malipo ya mwanzo ya damu kwa kumtoa baba yake, Efraim Donald angetakiwa kutulia kwa siku 730 ili mafanikio na mali nyingi zianze kuingia mikononi mwake, kisha baada ya hapo ndiyo angetakiwa kuanza kutoa malipo ya mzunguko wa mwisho ambayo yangemhalalishia utajiri wa kudumu.
Siku hizo alizopewa zilikuwa ni sawasawa na miaka miwili, kwa hiyo baada ya Efraim Donald kutoka hapo, kweli mambo mengi yalianza kumwendea vyema. Alipata mali na ufanisi wake ukazidi kuongezeka, lakini kama ambavyo ilikuwa kwa Godwin tu, wote walitakiwa kuishi kwa akili sana ili wasisahau kwamba walikuwa chini ya viapo ndani ya sakata halisi lililowasaidia kufanikisha mambo yao.
Kufikia kipindi hicho ambacho Godwin alikuwa anamsaidia Efraim, yeye tayari alikuwa ameshamaliza mengi ya masharti aliyokuwa amepewa, kwa hiyo alikuwa na uzoefu mzuri sana uliomwezesha kumsaidia mwenzake kwa usahihi kwenye njia nyingi alizopita mpaka akainua makampuni na kuendelea kukua tu kipesa; tena ndani ya miaka miwili tu! Wengi waliomfahamu Efraim Donald walishangaa sana baada ya kuona mafanikio yake, na mwanaume huyo hakusahau kuwatafuta wale wote waliomwonyesha dharau kipindi cha nyuma na kuwaua kwa vificho; ikiwemo yule jamaa aliyemdhulumu pesa, na wale wanawake watatu waliotoa mimba za watoto wake!
Roho ya kikatili kama ya Jini aliyekuwa ndani yake ilimvaa vizuri sana mwanaume huyo, lakini alionekana kuwa mtu ambaye ni mwema kwa wengi kwa sababu alificha makucha yake kwa ustadi wa hali ya juu. Halima, mama yake, alishangazwa pia na ufanisi wa mwanaye uliokuja upesi na kuuliza mambo yalikwenda vipi, naye Efraim alimwambia hakukuwa na haja ya kuwaza sana juu ya hayo, bali alitakiwa kuishi kwa furaha zaidi kwa sababu sasa maisha kwao yalikuwa ya kung'ara. Alimjengea mama yake nyumba mpya na nzuri sana, na hata ndugu zao wengi walianza kujipendekeza kwa wawili hawa baada ya kuona mambo kwao yamenyooka, ingawa hawakujua ni kwa njia nyingi zilizopinda.
Efraim Donald alikuwa amepewa maagizo ya kutotafuta mtoto kwa kipindi hicho ambacho alipata mali nyingi, lakini kufurahia tendo la mapenzi na mwanamke ilikuwa ruksa. Kwa hiyo mwanaume huyu alitoka na wanawake wengi sana na warembo mno, lakini sikuzote alikuwa makini sana kutojikuta anamtia mimba yeyote kati yao. Yaani hii yote ilimfanya aanze kuishi kwa njia ya mahesabu tu, na uzuri kama siyo ubaya ni kwamba alikuwa na akili nyingi iliyompa faida katika kila kitu alichofanya, na hatimaye, siku 730 zikawa zimekamilika.
Ulikuwa umefika wakati wa kwenda kukutana na "mawakala" wa Lucifer kwa mara nyingine ili ishu ya malipo ya "mzunguko wa mwisho" ianze kazi. Wakati huu tayari Efraim alikuwa mzoefu sana, hasa kwa kuwa hata roho ya yule kiumbe mwenye nguvu iliyokuwa ndani yake ilimsaidia kuona mambo mengi kwa njia pana na kuu, kwa hiyo zamu hii alikwenda mwenyewe kwenye mochwari ile ili kupangwa vizuri zaidi.
Baada ya kufika siku hiyo, Efraim Donald alikwenda mbele za viumbe hao kwa njia ile ile kama alivyokuwa ameshazoeshwa na Godwin Shigela, naye akapiga magoti na kusujudu.
"Efraiiimmm.... mwana wa Donald Tumpe..." sauti nzito ya "wakala" ikasema.
"Ndiyo... ni mimi mtumishi wako," Efraim akasema.
"Umekuja na zawadi Efraiiimmm...." sauti hiyo ikasema.
"Ndiyo bwana wangu. Nimekamilisha mambo mengi sana kwa siku zote 730... na kwa umakini... na ninawashukuru kwa msaada wote ambao nimeupata, na sasa mimi kama mtumishi wako ninakuja mbele yenu ili niweze kutoa shukrani kwa malipo ya mzunguko wa mwisho... ninaomba mnipatie nafasi hiyo ili niweze kudumisha ufanisi wote mlionipatia... bwana wangu..." Efraim Donald akasema.
Sauti hiyo ikaanza kucheka kwa njia ile iliyoumiza sana masikio, kama tu ambavyo mtu angechukua masufuria, mifuniko ya bati, na zile sahani za muziki wa ngoma na kuanza kuvipiga-piga vitu hivyo kwa nguvu sana karibu na sikio. Kalakalakalakala.....
"Efraiiimmm...." sauti hiyo nzito ikaita.
"Ndiyo bwana wangu...." Efraim akaitika, akiwa bado amesujudu.
"Unaelewa kazi ya mfanyakazi wa mochwari ni nini?" sauti hiyo ikauliza.
"Ndiyo bwana wangu... ni kupunguza uzito wa hofu inayosababishwa na kifo. Wanawachukua watu waliokufa na kuwapendezesha... halafu mwisho wa siku wanakuja kutupwa chini ya ardhi chafu. Ila siyo kwamba wanafanya hivyo kwa ajili ya wafu, ni kwa ajili ya wafiwa, wanawarahisishia kusema kwa heri, na kupata malipo pia. Hiyo yote ni kwa sababu ya hofu. Watu wanaogopa kufa, na mtu wao wa karibu anapokufa inawalazimu kukumbuka... na kukubali kwamba nao pia watakufa. Tunaishi maisha yetu yote tukielewa kwamba muda wowote ule... bila onyo... bila sababu... maisha yetu yatakata. Ndiyo sababu tuna mifumo kama hii ya mochwari... ili kutusaidia kupambana na hali hiyo ya hofu ipasavyo..."
Efraim Donald alijitahidi sana kutoa jibu lake kama tu ambavyo kiumbe huyo alilielezea mara ya kwanza kabisa yeye kuletwa huku, na jambo hilo likaonekana kumfurahisha sana kiumbe huyo kwa kuwa alianza tena kucheka.
"Vizuri. Umetambua ni kwa nini nilikuuliza swali hilo?" sauti hiyo ikauliza.
"Ndiyo bwana wangu. Nikiwa mtumishi wako... sipaswi kuishi kwa hofu hata kidogo... kwa sababu ninajua hata kifo chenyewe kinakuogopa. Sihitaji msaada wa mtu yeyote kama mtunzaji au msafishaji wa maiti kwenye mochwari... kwa kuwa tayari niko upande wako... ninajua utanipa na kunisafishia chochote kile nikiwa chini ya nguvu zako... nami nitafanya kila kitu unachoniagiza ili kukupa utukufu wewe pekee..."
Efraim Donald alitoa jibu hilo kwa uhakika kabisa. Alijua, na alielewa vizuri sana ni nani aliyekuwa akimtumikia.
Sauti hiyo ikaanza kucheka tena kwa nguvu, kisha ikasema, "Inuka."
Efraim Donald akainuka na kuketi kwa kupiga magoti, huku akiwa ameviunganisha viganja vyake.
"Unakubali kufata kila kitu kama utakavyoamriwa?" sauti hiyo ikauliza.
"Nakubali... na niko tayari," Efraim akajibu kwa uhakika.
Mwakilishi huyo akanyoosha mkono wake tena kwa njia ile ile kama mara ya kwanza na kumfanya Efraim Donald aone mambo mengi sana aliyohiraji kuyafanya kwa umakini wa hali ya juu ili hatimaye aweze kukamilisha malipo yake kwa njia ambayo ingempa utajiri wa kudumu. Sasa alionyeshwa mambo kwa njia hii:
Roho iliyoishi ndani yake, aliyoifanyia utumishi kwa kutoa malipo ya damu, ilimtaka aanze kufanya utumishi huo tena lakini zamu hii ikiwa ni kila mwezi. Alitakiwa kumpa Jini Subiani damu changa ya msichana yeyote mwenye umri wa miaka 19 kila ilipofika tarehe 19, na damu hiyo ilitakiwa kuwa karibu na mfumo wa hedhi wa msichana yeyote ambaye angemuua. Zoezi hili lilitakiwa kufikisha wasichana 19, ikimaanisha lingepaswa kuendelea kwa miezi 19.
Halafu, baada tu ya kukamilisha sadaka za mwanzo za damu za wasichana wanne, Efraim Donald alitakiwa kuoa mwanamke ambaye alikuwa wa pekee sana. Kusema pekee ilimaanisha kwamba mwanamke huyo asingekuwa aina ya mwanamke ambaye angefikiria hata kutoka nje ya ndoa na mwanaume mwingine mpaka malipo ya mzunguko wa mwisho yafikie hatamu. Pia, kwa muda wote ambao angekuwa amemwoa mwanamke huyo, Efraim Donald hangetakiwa kushiriki naye tendo la ndoa hata mara moja mpaka akamilishe zoezi hilo alilopewa.
Ilikuwa ni jambo fulani tata sana kifikira, lakini Efraim Donald alikuwa ameshakubali kujitoa namna hiyo mpaka ahakikishe linatimia. Kwa hiyo, wakati akiwa ameanza sakata la kuua msichana mmoja mmoja kila mwezi, mwanaume huyu angetakiwa kufanya uchunguzi wa makini sana kutafuta mwanamke ambaye angefaa kabisa kwa ajili ya jambo hili, na kwa sababu haingekuwa jambo rahisi, angetakiwa kuiomba roho yake msaada wa kipekee ili aweze kumtambua mwanamke huyo kwa macho yasiyo ya kibinadamu.
Ndiyo tunaweza kusema kwamba "macho" hayo yakawa yamemwangukia Namouih. Mwanamke huyo mrembo ndiye aliyepatikana kufaa zaidi kwa Efraim Donald kwa ajili ya jambo hili, na ndiyo sababu mwanaume huyu akafanya kila jitihada ili kuweza kumpata. Hiyo ndiyo sababu iliyofanya hata kipindi ambacho Efraim hajaanza rasmi kumtongoza Namouih, mwanamke huyu aliona kama mtu fulani anamtazama sana gizani mara kwa mara kwa njia yenye kutisha. Yalikuwa ndiyo hayo "macho" yanamwangalia.
Kila kitu kilikuwa ni kwa mpango na mahesabu ya hali ya juu. Efraim Donald hakuingia kwenye maisha ya Namouih kinagaubaga, ilikuwa kwa njia ya mpango wa siri. Alifatilia maisha ya mwanamke huyo kwa kina na kuunda mpango ambao ungekwenda kupatana na malengo yake, na kwa njia fulani mambo yakawa yamerahisishwa zaidi kwake kutokana na ugonjwa uliompata mzee Masoud, yaani baba yake Namouih. Alitumia maneno mazuri kumnasa, akatoa pesa nyingi, na kuifanyia mambo mengi familia ya mwanamke huyo ili aweze kumwingiza ndani ya pango lake la siri, na kama ujuavyo, alifanikiwa. Ila kuna vitu vingine vilivyotokea na kuongezeka baada ya Efraim kumjua Namouih vizuri zaidi.
Wakati huu ni kweli Efraim Donald alikuwa mkatili na mbinafsi, ila alipokutana na Namouih, alimpenda kutoka moyoni. Mwanamke huyo angekuwa ni sehemu ya mpango wake ndiyo lakini alitaka kuhakikisha kwamba anaendelea kuwa naye hata baada ya kukamilisha utumishi wake wa malipo ya damu kwa Jini Subiani. Alielewa mambo mengi kwa njia pana zaidi, na kujua kwamba hakutakiwa kufanya mapenzi na Namouih kungekuja kusababisha maswali mengi akishamwoa, ndiyo kitu kilichomfanya atake kufanya naye mapenzi KABLA ya kumwoa.
Hakungekuwa na shida endapo kama angeshiriki mapenzi na mwanamke huyo kabla ya ndoa, na lengo lake pia lilikuwa kumfanya Namouih abebe ujauzito wake kabla hata hawajaoana, ili wakishaoana mwanamke huyo asikazie fikira sana kuhusu haki yake ya ndoa akiwa tayari na ujauzito na hata akijifungua. Lakini kutokana na Namouih kumkatalia kumpa penzi wakati huo, ikambidi Efraim Donald afikirie njia mbadala ya kuivuruga akili ya mwanamke huyu; hasa ukifika usiku wa ndoa yao.
Mara ambazo Efraim Donald alikuwa amejaribu kuweka jitihada za kufanya mapenzi na Namouih kabla hajamuoa ziligonga mwamba kutokana na mwanamke huyo kuwa bado na hisia zilizovurugika, ila walipoanza kuielekea ndoa yao, Efraim Donald alitambua kuwa mwanamke huyo alianza kumzoea zaidi, na alitazamia kumpa tunda lake la kwanza usiku wa ndoa yao, kwa hiyo Efraim akafanya mpango ili usiku wenyewe kutokee jambo fulani ambalo lingemvuruga kihisia mwanamke huyo, yaani, kifo cha mzee Masoud!
Kifo cha baba yake Namouih hakikuwa kwa sababu ya mwili wake kushindwa kustahimili maumivu, bali ni kwa sababu Efraim alitumia uchochezi wake kwa pesa nyingi ili kumlipa mtu fulani kule aweze kumuua mzee Masoud na kutuma taarifa za kifo chake kwa muda hususa ambao Efraim na Namouih ndiyo walikuwa wameingia tu chumbani kwao baada ya kufunga ndoa rasmi. Hayo yalikuwa mahesabu ya hali ya juu na ukatili mbaya sana!
Kwa hiyo baada ya kufanikiwa kuichanganya akili ya mke wake kwa miezi michache kutokana na kifo cha baba yake, mwanaume huyu akawa anaendelea kuua wasichana wengine wenye miaka 19 kila mwezi na kuipa roho yake damu zao, na siyo kwamba ilikuwa tu kutimiza wajibu kwa ajili ya kuudumisha ufanisi wake; alifurahia kabisa ukatili huo. Kwa sababu Namouih hakuwa mwanamke mwenye papara aliweza kutulia kwa miezi mingi bila ya kugusia suala la haki yake ya ndoa, hata mara chache ambazo alitaka kupatiwa penzi na mume wake na Efraim kutoa visingizio vya hapa na pale, alimwacha tu.
Lakini kadiri siku zilivyokuwa zinaenda, Efraim Donald alielewa kwamba mke wake angeanza kuchoka na angekuwa na maswali mengi kichwani, kwa hiyo alihitaji kuendelea kuwa mbunifu zaidi ili kuhakikisha miezi 19 inakamilika na msichana wa mwisho anauawa, halafu mengine ndiyo yafuate. Lakini, mara tu Namouih alipomsimulia kwa mara ya kwanza kuhusu ndoto mbaya alizokuwa ameanza kuota, mwanaume huyo alitambua fika kwamba mambo yangeharibika muda usio mrefu.
Sharti la kuhakikisha kwamba mke wake hatoki ndani ya ndoa na kulala na mwanaume mwingine lilikuwa pana sana. Ikiwa Namouih angemsaliti Efraim kwa kuvutiwa au kutoka kimapenzi na mwanaume mwingine, mwanamke huyo angeanza kuona mambo mengi yaliyokuwa yanamzunguka bila yeye kutambua. Hii ilimaanisha kwamba angeweza hata kumwona Efraim Donald akifanya mambo ya kikatili kwa wasichana wengi kupitia ndoto zake, na hilo lingekuwa jambo zito sana kwa mpangilio wa mambo mengi yaliyotakiwa kukamilishwa na Efraim Donald. Kwa hiyo aliposimuliwa na mke wake yale mambo ya vivuli vyenye kutisha, Efraim Donald alitambua kwamba huenda mke wake alikuwa ameanza kutoka nje ya ndoa au kumpenda mwanaume mwingine; kitu kilichomfanya aanze kumfatilia kisiri.
Siku ile ambayo Namouih alikutana na Felix Haule kujadili kuhusiana na utata wa vifo vya wasichana, hususani kifo cha Agnes, na shuku zake kumwelekea mwanasheria Draxton, ni Efraim Donald ndiye aliyekuwa akiwaangalia kwa umbali mfupi ndani ya gari lake kutokea sehemu ile wawili wale walipokutana. Alifanya hadi makusudi ya kumpigia mke wake simu na kumuuliza yuko wapi, na kwa kufikiri alimdanganya baada ya kusema ametoka ofisini na kwenda kukutana na mtu kikazi ili tu awe na Felix, Efraim akadhani kwamba huyo Felix ndiye aliyekuwa shida.
Kwa hiyo, siku hiyo akawa amepanga kuhakikisha kwamba anamwondoa mwanaume huyo kuwa kikwazo haraka sana, na ndicho kitu alichokwenda kufanya usiku huo baada yeye na Namouih kwenda kwenye harusi ya rafiki na kumuaga mke wake akisema anakwenda kukutana na mtu fulani kushughulika na masuala ya kikazi; tena "mkuu wa Cargo." Hii inakumbukwa, siyo?
Ndiyo. Mwanaume huyo alikwenda mpaka eneo alilojua angemkuta Felix, na ilikuwa ni sehemu ile ile yenye kumbi ya starehe ambapo Blandina na Draxton walikutana na Felix na kuzungumza naye kwa ufupi. Efraim Donald, akiwa pamoja na Suleiman, walimsubiri mwanaume huyo atoke sehemu hiyo, kisha wakamfatilia mpaka alipokwenda sehemu nyingine tena kupata kinywaji; kwa sababu kule alikotoka alikuwa anavunga tu kwamba alienda kupata vinywaji ili amchunguze Draxton kwa ufupi.
Felix akiwa sehemu hiyo nyingine sasa, Suleiman alikwenda huko na kutengeneza kisa kidogo cha kupamiana naye, kisha akaweka dawa fulani ndani ya kinywaji chake ambayo ilikuwa na kusudi la kufanya mtu aharishe sana. Felix alimfahamu Suleiman kuwa dereva wa mume wake Namouih, nao wakasalimiana vizuri huku Suleiman akiomba samahani kumpamia, kisha mwanaume huyu akarudi mpaka kwenye gari la Efraim Donald. Suleiman hakuwa dereva-mlinzi tu, alikuwa mkono muhimu wa Efraim kwenye mambo yake haramu pia.
Felix alihisi vibaya sana tumboni mwake baada ya kumaliza kinywaji alichochukua, naye akatoka upesi kwenda kutoa haja kubwa. Choo cha sehemu hiyo kilikuwa kimejaa watu, kwa hiyo akatoka hapo na kwenda upande mwingine uliokuwa na choo cha kulipia, naye akaingia huko na kuanza kushusha haja zake zilizokuja ghafla sana. Alipomaliza mpigo wa kwanza, mwanaume huyu akaanza kuvaa suruali yake na kujiandaa atoke ili aondoke kwenda kutafuta dawa ya kutibu tumbo, na ndipo alipofungua tu mlango akakutana uso kwa uso na Efraim Donald.
Felix alishtuka kwa sababu ya ujio usio rasmi wa mwanaume huyo, lakini pia ni jinsi alivyoonekana. Efraim alikuwa amevalia nguo nyeusi mwili mzima wakati huu pamoja na viziba viganja vyeusi (hand gloves), na nguo hiyo ilikuwa yenye sehemu ya kufunika kichwa chake mpaka kuziba uso kufikia usawa wa macho, na kabla hata Felix hajanena lolote Efraim akamchoma kwa kisu tumboni huku akiuziba mdomo wake kwa nguvu sana. Alimkandamiza sehemu ya nyuma kabisa ya ukuta wa choo hicho, naye akaendelea kumchoma na kumchoma mara nyingi sana tumboni, kisha akafanya kama kulikata kutokea ubavu mmoja kwenda mwingine!
Baada ya Felix kuwa ameishiwa nguvu kabisa na kukata roho, Efraim akaingiza kisu hicho ndani ya mdomo wa mwanaume huyo na kuukata ulimi wake, halafu akautupa ndani ya tundu la choo huku damu nyingi ikitapakaa chini. Kisha akaanza kuvua nguo hiyo aliyokuwa amevaa upesi sana pamoja na hizo glovu mikononi, kitu kilichomfanya abaki na nguo zake za kawaida, halafu akaziweka ndani ya mfuko mgumu aliokuwa nao na kuufunga kwa nguvu.
Hakukuwa na mtu yeyote ambaye aliweza kuhisi tukio hili kwa sababu sikuzote Efraim Donald alipofanya jambo kama hilo, roho yake ya ndani ilikuwa ikimpa "ulinzi" ili iwe kama vile hakuonekana. Hii haikumaanisha kwamba hakuna mtu ambaye angeweza kuona mambo hayo kama angeingia humo, ni kwamba roho yake ingesaidia kufanya hata WAZO tu la kuingia ndani hapo lisifikirike kwa yeyote mpaka Efraim aondoke. Hiyo ndiyo sababu hata Draxton alipojaribu kufatilia harufu ya mtu au watu waliofanya mauaji ya Agnes na Felix alishindwa kuipata kwa sababu ilikuwa ni kama "imepotea tu."
Kwa hiyo baada ya Efraim Donald kumaliza kufanya mauaji ya Felix, alirejea kwa mke wake usiku huo na kumkuta akiwa na yule rafiki yake mpya, mwanamama daktari Salome, naye akaendelea kufanya maigizo yake ya kuwa mume mwema mpaka waliporudi nyumbani na Namouih. Walipokorofishana kidogo kuhusu kwa nini Efraim hampi mke wake haki yake ya ndoa, Namouih ndiyo alipigiwa simu na Blandina kupewa taarifa kwamba Felix alikuwa ameuawa.
Kwa hiyo haingefikirika kwa mtu yeyote kuwa Efraim ndiye aliyehusika na mauaji yake kwa kuwa muda huo alikuwa pamoja na Namouih na hata akaanza kumbembeleza mpaka kuja kwenda naye msibani. Alijua sana kuficha makucha yake mwanaume huyo, na kufikia wakati huo alidhani kwamba kwa kumuua Felix ndiyo alikuwa amemaliza tatizo la Namouih la kupatwa na ndoto mbaya zenye kumwonyesha mambo yaliyoendana na maovu ya mume wake, akifikiri huyo ndiye aliyekuwa kitovu cha usaliti kutoka kwa mke wake.
Lakini siku ambayo Namouih alikuja kuota tena ndoto mbaya iliyomhofisha mpaka akatukana kwa hasira, ndiyo siku Efraim Donald aliyotambua kwamba kitendo cha kumuua Felix hakikuwa na faida yoyote. Alifanya hadi kumuuliza jinsi ndoto hiyo ilivyokuwa, na Namouih ndiyo akamwelezea kwamba alijiona akiwa mochwari, mara msituni akiwa bila nguo, na aliona kiumbe mwenye kutisha aliyekunywa damu ya mtu baada ya kumuua kikatili sana. Efraim Donald alielewa wazi kabisa kwamba ndoto hiyo ilihusiana moja kwa moja na jinsi mambo yake ya gizani yalivyokuwa, naye akashindwa kuelewa kwa nini bado zilikuwa zikimpata.
Alikuwa ameshamfatilia Namouih vya kutosha kuelewa kwamba mke wake hakuwa akienda nje ya ndoa yao wala kumsaliti kwa kutoka na mwanaume au mwanamke mwingine, kwa hiyo ikawa wazi kwake kwamba Namouih alikuwa ameanza kuvutiwa na mtu fulani bila yeye mwenyewe kutambua hilo. Hiyo ndiyo sababu bado ndoto hizo hazikumwonyesha mambo mengi waziwazi lakini kama angetoka ndani ya ndoa yake na kufanya mapenzi na MTU mwingine, yote aliyofanya Efraim yangefunuliwa kwake.....
★★★★
Efraim Donald akiwa nchini Kenya jijini Nairobi kwa ajili ya kufanya mikutano yake ya kikazi, alikuwa amekutana na rafiki yake wa karibu sana Godwin Shigela, ambaye ndiye aliyempa "msaada" wa kumwinua kutoka kwenye ufukara wa kadiri mpaka kuwa tajiri. Wakiwa wamekutana usiku mmoja kwenye kumbi ya kifahari ya starehe, Efraim akawa amemwelezea rafiki yake namna ambavyo hali ya Namouih ilimkosesha amani, kwa kuwa alikuwa amebakiza msichana mmoja tu wa kuua ili kukamilisha malipo yake ya mzunguko wa mwisho. Yaani kutokea alipomuoa Namouih mpaka wakati huu, alikuwa ameshaua wasichana 18, yule Agnes akiwa ndiyo wa mwisho, na sasa alikuwa akisubiri tarehe 19 ya mwezi uliofuata ili aue msichana wa mwisho kukamilisha jambo hilo.
Haingekuwa ngumu kwake kupata msichana wa miaka hiyo, kwa sababu mara nyingi alitumia wasichana ambao waliishi maisha yao kwa kutojali sana, kama malaya vile. Angechukua mmoja na kwenda naye mbali kujiridhisha, kisha angemuua na kuchukua damu yake ili kwenda kuitoa sadaka kwa roho ya JINI SUBIANI iliyokuwa ndani yake. Siyo kwamba kufanya mambo hayo ilikuwa rahisi, ni kwamba tu alifurahia sana kuifanya ionekane kuwa rahisi kiasi kwamba mpaka kufikia wakati huu hakuna mtu aliyeweza kutambua hila zake. Lakini sasa hivi, hakuwa na lengo la kuchukua msichana yeyote tu, alikuwa anataka kumaliza mchezo huu kwa njia ambayo ingemburudisha sana, na ndiyo sababu alimwambia Godwin kwamba ana mpango wa kupata raha fulani hivi ambayo Subiani angeipenda sana, maana ilionekana kuwa tamu mno. Mpango wake huo ulikuwa umeanza kazi.
Baada ya kujitumbuiza vya kutosha na rafiki yake sehemu hiyo ya starehe, Godwin akamtafutia Efraim mwanamke mweupe mwenye umbo nono haswa ili amtumie kwa ajili ya kumridhisha kimapenzi usiku huo. Efraim Donald kutompa Namouih haki ya ndoa haikumaanisha asingeweza kufanya mapenzi na wanawake wengine, na alipenda sana kufanya mapenzi na wanawake weupe. Hii bila shaka ilikuwa ni kwa sababu ya mke wake. Alikuwa anampenda Namouih, na alitamani sana kwa kipindi kirefu mno kumshika na kumwonyesha namna anavyotaka kumpa penzi murua, lakini alikuwa makini sana kutosahau aina ya maisha aliyotakiwa kuishi. Alikuwa anatazamia kwa hamu kubwa kumaliza haya mambo mengine yote ili hatimaye aje kumuonja mke wake, kama tu alivyosema, na kwa sababu sadaka alizotoa zilikuwa zinaelekea mwishoni alihisi hamu kubwa sana iliyofanya awe kama mtu anayekosa subira.
Lakini yote kwa yote, bado suala la Namouih kuwa na hisia kwa mtu mwingine bila yeye mwenyewe kutambua ni jambo ambalo Efraim Donald alitakiwa kulifatilia kwa kina ili ahakikishe analitatua, kwa sababu kama asingeangalia, lingeweza kumsababishia hitilafu kwenye mipango yake. Akamchukua mwanamke huyo na kumpeleka mpaka kwenye hoteli aliyochukua chumba jijini hapo, naye akapatiwa huduma nzuri sana kwa kupewa penzi, lakini bila shaka la malipo. Sikuzote alipofanya mapenzi na mwanamke mwingine angevuta taswira kwamba yuko na mke wake, kwa kuwa alitazamia kwa hamu sana siku ambayo angemvua nguo yeye mwenyewe na kufanya alichotamani kumfanya kwa muda mrefu sana.
Huyo ndiyo alikuwa EFRAIM DONALD!
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Comments