Reader Settings

Akiwa amepigwa na butwaa mbele ya mwili wa mwanae wa kwanza ndipo alipo shtuka kutoka kwenye huo mfadhaiko baada ya kumkumbuka mkewe ambaye alikuwa ni mjamzito na siku sio nyingi angefanikiwa kumletea mtoto wa kiume hapo ndani kwake na ni kitu ambacho alikuwa anakisubiria kwa hamu kubwa sana, alikurupuka kama hana akili timamu na kuanza kukimbia kuelekea sehemu ambayo ilikuwa na ngazi za kupandishia juu na huko ndiko ambako alihisi mkewe atakuwepo kwenye chumba chao cha kulala.

Alisita sana baada ya kufika kwenye mlango huo wa kuingilia chumbani lakini hakuwa na namna ilibidi ajikaze kiume huku akiwa anafuta machozi na jasho jingi ambalo lilikuwa likimtoka kwenye mwili wake na kufanya kuwa kama maji hususani kwenye eneo lake la uso, mlango uliegeshwa tu hivyo akausukuma kidogo huku akiwa anahema kwa nguvu sana, alitulia kama dakika nzima akiwa hajafanya mjongeo wowote wala kutamka neno lolote zaidi ya kutetemeka tu baada ya kumuona mkewe, mkewe alikuwa akihema kwa nguvu sana akiwa amemnyooshea mkono mmewe kumhitaji pale alipokuwepo yeye, alianza kuogopa sana mheshimiwa jaji mkuu baada ya kuona kuna binadamu ambaye hakuwa na uhakika sana kama naye aliwahi kuzaliwa na mwanamke kwa kitendo ambacho alikuwa amemfanyia mkewe.

Kisu chenye ncha kali mno kilizamishwa kwenye tumbo la mwanamke huyo na binadamu ambaye yeye hakumuona mpaka wakati huo, na huyo mkewe alikuwa amembebea mtoto wa kiume humo tumboni ambaye walikuwa wakimsubiria kwa hamu kubwa sana, machozi yalikuwa yanamshuka mwanaume taratibu huku akianza kutembea kwa kujivuta kuelekea pale alipokuwepo mkewe, wakati anazidi kusogea kuna ishara mkewe alikuwa akimpatia kwa sababu hakuwa na uwezo wa kutoa sauti kutokana na damu iliyokuwa imemtoka kwa wingi na nyingine ilikuwa ikiendelea kutoka mdomoni, mwanaume hakuelewa chochote alienda pale chini ya kitanda na kumuweka mkewe kwenye mapaja yake.

“Nisamehe nisamehe mama, nisamehe sana mimi nimekuulia wanao wote wawili lakini nimekuletea matatizo hata wewe pia nisamehe sana” aliongea kwa uchungu sana aakiwa amemkumbatia mwanamke huyo, mkewe alitabasamu kwa mbali sana kwa sababu tabasamu lake lilikuwa na maumivu makali sana ndani yake, alijitahidi sana kutaka kumpa ishara mumewe huyo kipenzi ambaye alijijua wazi kwamba yeye ndiye alikuwa dawa pekee ya mwanaume huyo, lengo lake alikuwa anahitaji kumpatia taarifa kwamba nyuma ya huo mlango kulikuwa na mtu lakini jaji mkuu hata hakushtuka kuhusu hilo.

Aliitoa simu yake na kuingia upande wa live video, aliipiga simu Kwenda nje ya nchi akiwa anatokwa na machozi kwenye macho yake, simu ilipokelewa na kwa upande wa pili ilionekna sura ya kijana mmoja ambaye alikuwa na sura kama shombe shombe ila ilikomaa kiasi chake na kumfanya kuwa mwanaume kweli, huyo alikuwa ni mdogo wake wa damu kabisa walizaliwa tumbo moja na walikuwa wawilitu. Mdogo wake alishangaa sana kumuona kaka yake akiwa kwenye hiyo hali ya majonzi ni kitu ambacho hata yeye mwenyewe kilimtia shaka.

“They have killed us, they have killed us” aliongea kwa uchungu akiwa anapangusa machozi akiigeuza simu kuelekea upande ambao alikuwa amemkumbatia mkewe, mwanaume upande wa pili hakuongea kitu baada ya kumuona kaka yake kwenye hiyo hali alimuangalia shemeji yake kwa uchungu sana baada ya kuona kitu ambacho alikuwa amefanyiwa, alitabasamu kama kumpa tumaini la maisha shemeji yake kwa sababu kupigiwa simu ina maana yeye ni mtu aliyekuwa amekusudiwa kuwafariji kwa huo wakati na haikutakiwa aonyeshe udhaifu. Alikuwa na mengi sana ya kuuliza kwa sababu kwanza hakujua kipi kinaendelea na nini kilikuwa kimetokea mpaka wakati huo aliamua kuupa muda nafasi huenda kaka yake angemwambia ukweli, akiwa anaendelea kumuangalia kwa uchungu shemeji yake ambaye macho yake yalikuwa yameanza kufifia sana alitamka neno moja tu.

“Mama nakupenda sana” Huyo mwanamke wote walikuwa wakimuita hivyo mama kwa sababu jinsi alivyokuwa akiishi nao alichukua moja kwa moja nafasi ya mama yao mzazi ndiyo maana walimheshimu na kumpenda kiuliko kitu chochote kile kwenye maisha yao, mwanamke huyo alitaka kama kutabasamu lakini alishindwa taratibu akawa anayefumba macho yake, hilo tukio halikukamilika moja kwa moja kwa sababu mwanaume alianza kuona chenga chenga ghafla sana baada ya kusikia kishindo kikubwa na sauti kali ya maumivu ikilia upande wa pili

“Hey brother, brother talk to me please” alibaki anaita bila mafanikio yoyote yale, baada ya sekunde kama thelathini alisikia kwa mbali sauti yenye maumivu na isiyokuwa na matumaini kabisa ikisema

“They have killed your brother, they have killed your brother” ilififia baada ya kusikia mlio wa risasi na simu hiyo ikakatwa, alijaribu sana kuipiga tena simu hiyo lakini haikupatikana tena, aliishiwa nguvu mwanaume hakujua nyumbani ni tatizo gani la ghafla lilikuwa limetokea mpaka wakati huo kwa sababu kwa mara ya mwisho aliona kuhusu ile kesi iliyokuwa inaendeshwa na aliona kama kaka yake kama jaji mkuu alikuwa amefanya maamuzi ya maana sana kuweza kumuua mtu ambaye alikuwa moja kwa moja amehusika na mauaji ya mheshimiwa raisi na haikujulikana ni kwa sababu zipi yeye hakuweza kabisa kupiga simu nyumbani mapema sana kiasi hicho.

Nyumbani kwa jaji mkuu wakati anaongea na ile simu mwanaume aliyekuwa nyuma ya mlango alikuwa akimwangalia kwa umakini sana na hakutaka kukurupuka ili kama mtu huyo alikuja na watu au ulinzi basi iwe ni rahisi kukabiliana nao ndio maana hakuhitaji kukurupuka kumfuata hapo chini, baada ya kujihakikishia kwamba hilo eneo lilikuwa salama kwa upande wake yeye basi alimsogelea mwanaume huyo wakati akiendelea kuongea na simu alipigwa buti moja kali sana la kichwa na ndio ule muda ambao simu ilimponyoka na kuanza kuonyesha chenga chenga.

“Uliambiwa ukajifanya mjanja kuendelea kuyafanya yale ambayo wewe hukupaswa kuyafanya sasa utawapa somo na wenzako ambao utawakuta mbele huko” ni sauti moja kavu sana kutoka kwa mwanaume ambaye yeye mwenyewe baada ya kumuangalia alikuwa akimfahamu mtu huyo ila hakupewa nafasi ya kuendelea kuishi alitamka tu kwa nguvu

“They have killed your brother” akiamini kwamba mtu wa upande wa pili wa hiyo simu alikuwa akimsikia vizuri wakati akiwa anaongea na ndio huo muda ambao ulisikika mlio wa risasi na simu hiyo ikakanywangwa na mwanaume huyo ukimya ukawa umepita. 

Hiyo ilikuwa ni siku mbaya sana kwa Jason pamoja na watanzania wote ambao walishtushwa sana na taarifa za kifo cha ghafla sana cha mheshimiwa jaji mkuu wa nchi ya Tanzania Markvelous Japhary ikiwa ni muda mchache tu tangu aweze kutoka kumsomea hukumu mwanaume ambaye alisadikika kuwa alikuwa amemuua mheshimiwa raisi wa nchi ya Tanzania. Hata mwili wa mheshimiwa raisi ulikuwa bado haujapumzishwa lakini naye jaji mkuu alikuwa tayari amekufa na kibaya yeye alikufa na familia yake yote mtoto wake wa kike pamoja na mkewe mjamzito, zilitolewa taarifa chache sana kwamba kwenye hiyo familia alikuwa amebakia mtu mmoja tu ambaye ni mdogo wake na mheshimiwa jaji mkuu ambapo serikali iliahidi sana kumpatia ushirikiano mkubwa kijana huyo ikiwa ni pamoja na kumsaidia pale ambapo angehitaji msaada wowote ule kutokana na heshima kubwa pamoja na mambo makubwa ambayo kaka yake alikuwa ameifanyia nchi hii kwa kipindi chake ambacho yeye alikuwa yupo hai.

Polisi wa kutosha walikuwa ndani ya eneo la tukio wakiwa wanaendelea na uchunguzi wao ili kujua ni nani ambaye alikuwa amehusika na hilo tukio la mauaji ya mheshimiwa jaji mkuu,walichukua kila kiambatanisho cha ushahidi wote ambao ulipatikana kwenye hilo eneo ikiwepo simu na risasi ambazo zilitumika kuwaua watu hao kisha wakaibeba miili na kuelekea nayo mochwari ambako walikusudia kwenye kuifanyia uchunguzi zaidi.

“Haya matukio naona moja kwa moja yana uhusiano mkubwa sana kwa sababu mheshimiwa raisi amekufa ndani ya muda mfupi tu halafu baada ya mheshimiwa jaji mkuu kutoa hukumu kwa yule mtu naye amekufa leo leo tena kwa muda mfupi sana baada tu ya kumaliza ile kesi, nina uhakika haya matukio yalipangwa kwa muda mrefu na hayatokei kwa bahati mbaya na huenda wahusika ni wale wale hivyo hili jambo kwa mtu ambaye nimeapa kulitumikia vyema vazi langu la jeshi la polisi nitahakikisha nakula sahani moja na hawa wote walio husika na watakamatwa tu hii kesi naenda kuisimamia mwenyewe” Aliongea kwa msisitizo sana Afisa wa polisi (Asp) Bakari Zalimo akiwa anatoa maelezo kwa wenzake baada ya muda mchache aliokuwa amekaa hapo kuweza kung’amua baadhi ya mambo.

“Ndugu yangu huo uhodari wako ambao huwa unautafuta kuna siku utakuja kukuponza sana, huwa unafanya vitu bila hata kujiwazia kwamba kuna maisha baada ya hivyo vitu, hivi wewe unadhani mtu mkubwa kama huyu anaweza kuuawa kiwepesi tu kama unavyo hisi wewe? ni mtu gani wa kawaida ambaye anaweza kumuua mheshimiwa kama huyu huenda hao wanao tutuma hizi kazi ndiyo wahusika wenyewe kwa sababu sioni wakuu wakitilia mkazo sana katika hilo kwahiyo nadhani sisi tujiweke kando tu” Afisa mwenzake ambaye alijulikana kama UTAPEWA aliongea kumtahadharisha mwenzake huyo ambaye alionekana kuhitaji kulivalia njuga hilo suala ambalo lilikuwa na uzito kwa upande wake yeye.

“Haina maana yoyote ya kuvaa hilo vazi lako ambalo lipo kwenye mwili wako na hauna hata uwezo wa kulilinda, unajua tafsiri sahihi ya hilo vazi? Unakumbuka siku unaapa mbele ya bendera ya nchi yako na kauli uliyo itoa kuhusiana na hilo vazi? Basi kama unakumbuka unatakiwa kuliweka hilo kichwani mwako hiyo kofia ina maana kubwa sana kwenye maisha ya jeshi la polisi, hiyo ni alama ya mtu ambaye anapaswa kuipigania hiyo kofia mpaka pumzi yake ya mwisho, wananchi wanapo iona hiyo kofia na hilo vazi basi huwa wanajaa matumaini na kujihakikishia kwamba wapo kwenye eneo salama kabisa na hiyo ndiyo sababu hata leo hii ukimuona mwananchi amepata tatizo ambalo litahatarisha usalama wa maisha yake yeye, kitu cha kwanza lazima atapiga simu polisi ambako ana uhakika kwamba kuna usalama wa maisha yake”

“Sasa kama wewe hapo unavaa vazi ili kujifurahisha na kulitumia kama kivuli cha kujilinda na kuyaficha mambo yako ya hovyo pamoja na kujichumia mali ambazo zinatokana na kodi za wananchi kwa jasho lao wenyewe una utofauti gani na mtoto wa kike ambaye anaikataa mimba huku akiwa anatamani kuitwa mama? Kama unahisi hauiwezi hii kazi ungesomea hata ualimu ili ukawadanganye watoto kuhusu uzalendo ambao hata wewe mwenyewe hauna. Unatakiwa kujionea aibu mwanaume kama wewe kutanguliza uoga wa namna hiyo mbele ya haki ya mtu mwingine, sina uhakika kama ungekuta mama yako, baba yako, kaka yako, dada yako au ndugu yako wa karibu kafanyiwa hivi halafu ukawa na nguvu za kutamka huo utumbo wako, kumbuka ana mdogo wake ambaye inadaiwa muda wowote ule anaingia nchini lazima atahitaji ripoti juu ya kifo cha familia yake utamjibu nini wewe hapo zaidi ya kuishia kuingiza mikono mfukoni kama mgane ambaye amekataliwa na kila mwanmke kutokana na majivuno yake, siku nyingine usije ukaongea utumbo kama huo mbele yangu maana nitakupiga risasi, kawaambie na hao wenzio kesho asubuhi sana naingia kuanza uchunguzi wangu na ole wake nikukute hata wewe umo kwenye hilo kundi” Afisa wa polisi alichukizwa sana na kauli ya mwenzake UTAPEWA alitegemea mtu huyo na wenzake wangejadili namna sahihi ya kuweza kulifanyia kazi hilo jambo cha ajabu yeye alikuwa anamshauri jinsi ya kujiweka mbali na hilo jambo alimuona kabisa hafai kuwa kwenye hilo vazi ambalo yeye alikuwa analiona kama lina thamani kubwa sana.

Aliondoka kwa hasira sana baada ya kumwambia mwenzake ukweli wa kila ambacho alikona kilikuwa sahihi kwa upande wake, aliahidi kwamba kutakapokucha tu angeamkia Kwenda kuianza hiyo kazi ambayo kwake ilikuwa ni ya lazima kuifanya na haukuwa msaada bali alikuwa ana uhakika kwamba huo ulikuwa ni wajibu wake ndio maana alikuwa akilipwa.

Bado ni mapema sana, ndio kwanza tunaanza, leo tuishie hapa.

Wasalaam 

Bux the storyteller.

Previoua Next