Reader Settings

Pamoja na kujiamini kwa Rafaeli sana hata kuongea na kusimama mbele za watu, lakini huwa hana ujasiri wa kuangaliana na msichana yoyote ambaye hajamzoea, tofauti na vijana wengi wa umri wake. Hii ni kutokana na kutowahi kuingia kwenye mahusiano na msichana yoyote tokea azaliwe. Si kama amekosa wa kutoka naye — ila wapo wengi waliokuwa wanataka kuanzisha mahusiano naye, ila hakuwa tayari.

Mmoja wao alikuwa msichana mmoja aliyechanganya rangi ya Kiarabu na Mwafrika. Kwa jina lingine tunawaita Warabu Koko. Msichana huyu alikuwa akisomea Ubungo Islamic na alipata kumjua Rafaeli kipindi wanaenda shuleni hapo kushiriki mashindano ya mdahalo. Ndipo walipata kufahamiana.
Tokea kipindi hicho yule msichana alimwonesha kumpenda Rafaeli, lakini Rafaeli wala hakujali.
Ndo maana hata mwalimu alivyokuwa anafundisha na kuchekesha wanafunzi, alijikuta akigeuka kwa furaha na kumwangalia jirani yake upande wa kushoto — ndo akajikuta akiduaa kwa uzuri aliokuwa nao yule msichana wakati wa kucheka.

"Huyu msichana ni mzuri, sio poa," alijiwazia Rafaeli huku akiendelea kumsikiliza mwalimu aliyekuwa akiuliza maswali.

Mara mwalimu akauliza swali, akimnyoshea kidole:
"Rafaeli, wewe mwenye sura ya kitoto, hebu eleza sifa za bacteria anayeeneza kichocho. Maana naona umekaa tu huongei — utapata ugonjwa wa TMJ (temporal mandible joint disorder). Ugonjwa unaomfanya mtu kushindwa kuongea!"

Wanafunzi wakajikuta wanacheka kwa jinsi Rafaeli alivyotaniwa na mwalimu, mpaka akajikuta anapoteza kujiamini. Pia ikichangiwa kwamba hakuwa amesoma ile topic, maana yeye alichelewa kufika chuoni na wenzake walimuacha. Ikabidi atingishe kichwa tu kumaanisha kwamba hajui.

Baada ya kipindi kuisha walitoka break kujiandaa na kipindi cha mchana, huku wenzake wakimpachika jina la TMJ.

"Haha! Oya TMJ, unakaa na mtoto mzuri pale hata huongei mpaka mwalimu anakuita TMJ. Baada ya kupiga hata vocal unajikuta kauzu. Ngoja utakula kwa macho yani," alitania Elisha.

"Elisha, mzee, dogo mwenyewe mimi ndo nimeenda kukaa pale leo. We unafikiri nitaongea naye saa ngapi? Ila mimi kauzu mzee. Mimi nipo hapa kusoma, sina habari na wanawake."

"Hahaha… poa mzee. We uzege ndo unakusumbua. Ila freshi mzee, yule dogo Juma anamfatilia kinoma. Ndo hivyo, dogo hata kujibu message hataki, yani dogo yupo kauzu vibaya."

"Freshi. Yeye akomae tu maana hata mimi mtoto nimemuona mkali. Na vile vishimo wakati ule anacheka nimemkubali."

"Poa mzee, baadaye usisahau tutaenda kwenye zoezi. Poa ngoja na mimi nikanywe chai mzee maana naona tumbo linanguruma ile ile."

*******

Tukija chumbani kwa kina Jasmine, ambapo wanaishi wasichana wanne: Neema, Catherine, Fetty na Jasmine.

"Jasmine, leo naona umepata mgeni," alisema Neema.

"Mh? Mgeni gani tena?"

"Si yule uliekkaa naye nyuma yangu leo? Hujamuuliza jina?"

"Aka sijamuuliza. Yupo kauzu. Mimi nilitaka tu akae ile sehemu maana kidogo ananizibia, maana pale ni njiani. Dokta Mbale akiingia anapenda kushika-shika watu."

"Poa. Ngoja niwahi canteen nikachukue chai niwahi kipindi," alisema Neema akiongea na Jasmine.

Hawakukaa sana wakarudi darasani kuendelea na vipindi.
Rafaeli baada ya kumaliza kunywa chai alikuwa anarudi darasani kwenye kipindi kinachofuata. Ile anaingia darasani mara akaona ile sehemu alikokaa kakaa msichana mwingine.

"Daah! Sijui nikamtoe… ila ngoja nikae zangu hapa tu," alijiwazia.

"Oya Kassimu, vipi?" alisalimia Rafaeli.

"Safi vipi? Mbona umekaa hapa? Si ukamtoe ukae sehemu yako, yule msichana?"

"Daah! Mzee, mimi hata siwezi. Ngoja aendelee kukaa tu bwana."

"Acha uoga. Kamtoe ukae bhana!"

"Poa, ngoja niende," alisema huku akisogelea ile sehemu yake.

"Vipi sista, samahani. Hii ni sehemu yangu naomba utoke nikae," alisema kwa adabu.

"Lakini unaweza ukakaa sehemu yoyote tu kaka yangu. Nafasi zipo nyingi," alijibu msichana.

"Wee Lizzy, nae si mpishe kaka watu akae. Hii ni sehemu yake," aliongea Jasmine.

"Okey, it’s fine. I’m leaving," alisema Lizzy huku akiondoka kama akiwa amekasirika.

"Ngoja nikae zangu. Kama amekasirika atajua mwenyewe," alijiwazia Rafaeli.

Baada ya muda lecturer alifundisha na kutoka huku akiacha assignment kila group wafanye na ku-present kesho yake.

*******

"Oya Elisha, we si ndio CR (Class Representative)?"

"Ndiyo, vipi?"

"Niingize kwenye group lenye nafasi."

"Anhaa poa, utaingia group namba nne. Kiongozi ni Abdi, yule jamaa mrefu pale anayeongea na Neema."

"Oya Abdi, mambo vipi?" Rafaeli akasalimia.

"Poa man, vipi?"

"Safi. CR kanambia we ndo kiongozi wa kikundi namba nne. Nimekuja kukufahamisha nimepangwa kwenye kikundi chenu, ili kama mtaifanya ile kazi mnishtue tufanye wote."

"Anhaa poa. Ngoja nikaongee na hawa mademu halafu baadaye nitakushtua. Nipe namba yako ya simu."

"Poa, hii hapa. Andika."

"Poa. Basi me naenda mazoezini. Utanishtua ukishaongea nao."

"Poa."

Baada ya mazoezi, Rafa akijiandaa kwenda canteen kula chakula, mara simu yake ikatoa mwanga kuonesha kuna ujumbe wa maandishi umeingia:

"Oya madogo wanasema saa tatu usiku tukutane Lecture Four kufanya kazi."

"Anhaa poa," Rafa akajibu huku akitoka. Wakati anakaribia ofisi za utawala mara akakutana na Lizzy na marafiki zake wakampita.

"Huyu mkaka leo kaniboa kama nini. Nilikuwa nimekaa pale kwa Jasmine mara akaja akasema hii sehemu yake na Jasmine akamtetea sijui kampenda," alisema Lizzy.

"Wee Lizzy, nae sasa. Si sehemu yake. Unalalamika nini? Sema tu umempenda mkaka wa watu, usitusumbue sisi."

"Naniii? Mimi!? Mimi sio saizi yake hahaha!"

"Eti mimi sio saizi yake? Haya bhana, tutakuona!"

*****

Saa tatu ilipotimia Rafaeli akaenda zake darasa alikoelekezwa kwa ajili ya discussion. Kama alivyoambiwa na Abdi, akamuona Abdi upande wa nyuma amekaa na wasichana wanne naye Abdi peke yake. Akawasogelea.

"Mambo zenu jamani," Rafaeli akasalimia.

Wakajibu wote kwa pamoja huku Abdi akimwelekeza achukue kiti ajiunge. Discussion iliendelea mpaka ikafikia sehemu ya kupanga watakaowakilisha kesho.

"Wavulana zamu yenu. Juzi kwenye communication sisi ndo tulienda. Kesho zamu yenu," alisema Irene.

"Hakuna shida. Mimi nitaanza maana hata somo lenyewe nalipenda, halafu Abdi atamalizia," alisema Rafaeli.

"Poa, tumekubaliana hapo," Irene akamalizia.

****

Kesho asubuhi, Rafaeli akajiandaa na kuelekea darasani. Alimkuta Jasmine, akampa hi na akakaa huku akipitia wanavyoenda ku-present. Baada ya kama nusu saa mwalimu wa somo la entrepreneur akaingia.

"Hamjambo?" Madam akasalimia.

"Hatujambo," wakajibu wanafunzi.

"Kikundi cha kwanza mpaka cha tano leo mta-present. Kikundi cha kwanza watoke waanze. CR rekebisha projekta vizuri, huku nyuma waone vizuri."

Walimaliza ku-present vikundi vyote. Vilivyobaki ni la Rafaeli na group namba tano. Kikundi namba nne akatoka Rafaeli akiwa amechomekea na kapendeza kweli kweli.

"Morning," alisalimia.

"Morning," wakajibu.

"I am in front of you to represent what we have discussed in our group. Our question was: what are the responsibilities of a good entrepreneur and qualities of a good entrepreneur. For me, I will discuss the first question."

Moja ya jukumu la mjasiriamali ni pamoja na kuajiri wafanyakazi, kutoa mtaji kwa ajili ya biashara, kujua jinsi ya kuwa na muunganiko kati ya wazalishaji, kuvumilia hasara, na kuhakikisha masuala yote ya biashara yanaenda vizuri.

Huyo ni Rafaeli akiwa anatoa somo kwa ufasaha kabisa tena kwa lugha ya Kiingereza.

"Kuna mwenye swali?"

Hakuna aliyeonyesha kuwa na swali.

"Ahsanteni kwa kunisikiliza. Namkaribisha mwenzangu kwa ajili ya kumalizia."

Akaenda mbele Abdi akamalizia, kikaja kikundi kingine nacho kikamaliza ku-present. Watu wakatoka lunch.

******

Siku hiyo, ikiwa mida ya saa kumi, Neema na wana-kikundi wake walikuwa discussion mara wakamwona Rafaeli anapita barabarani akiwa kwenye bodaboda ikionekana anaenda mjini.

"Rafa yule," akasema Neema.
"Yaani yule mkaka ana macho mazuri halafu handsome. Lazima nimwambie nampenda, hahaa!"

"Neema, ni wewe kweli? Yaani kesho usipomwambia sisi lazima tumwambie," akasema Catherine.

"Yaani tena tunakubeba," akaongezea Sadiki.

"Jamani, mimi nilikuwa natania tu."

"Hakuna cha kutania. Tutamwambia wewe ukishindwa."

*******

Siku hiyo, Rafaeli akiwa anaingia darasani kujisomea mara akakutana macho kwa macho na Jasmine aliyekuwa anajisomea.

"Ngoja nikamsalimie tu niondoke nikakae kule nyuma," alijiwazia.

"Mambo Jasmine."

"Poa. Mzima wewe?" alijibu huku akitabasamu.

"Kumbe unalijua jina langu?"

"Yeah. Nililijua jana kwenye ndoto nilisikia mtu anakuita. Hahaha! Haya bhana, wewe waitwa nani?" huku akimpokonya daftari na kusoma jina.

"Niite Rafa tu, inatosha."

"Anhaa, poa. Nina shida ya past paper yoyote unitumie kwa WhatsApp."

"Anha, nipe namba yako." Akamtajia.

"Karibu. Basi poa, asante. Mimi naenda kukaa kule nyuma."

"Poa."

Jasmine alivyorudi hosteli mara akawakuta wenzake wanapiga stori ile anaingia tu.

"Enhee Jasmine, bora hata umekuja. Yaani Neema kasema anampenda yule Rafa. Kwa hiyo tunapanga kesho akamwambie. Eti kweli Neema, Jasmine?" akamuuliza.

"Hamna, mimi nikitaka nitamwambia mwenyewe."

"Mh, haya bhana," Jasmine aliitikia kinyonge hivi huku akipanda kwenye kitanda chake.

"Kesho inabidi nikae karibu na yule mkaka, Neema asipate nafasi maana nimempenda. Anaonekana hana tamaa," huku naye Neema akiwaza kumfuata Rafaeli kesho kabla hawajamwambia.

Previoua Next