WhatsApp: 0621567672
UTANGULIZI.....
EPISODE 1.
BANZOKA
Pembezoni mwa barabara ndogo ya vumbi ambayo ilikuwa inaingia kwenye kichaka kilichokuwa kimemezwa na miti ya kutosha, mwanaume mmoja alikuwa akijikokota huku akiwa anavuja damu kwa wingi. Alikuwa anauburuza mguu wake ambao haukuwa kwenye hali nzuri kabisa, mguu wake ulikuwa una alama za kukatwa na makovu kadhaa ambayo hayakumfanya bwana huyo kuwa kwenye hali nzuri kiafya.
Hatua zake hazikuwa za kuridhisha kabisa kwa sababu alionekana kuwa mtu ambaye alitembea kwa muda mrefu bila kuwa na msaada. Alionyesha hofu usoni ambayo iliufanya hata moyo wake kwenda mbio kiasi cha kupiga mpaka kwenye kifua chake hata mtu ambaye angekuwa umbali kadhaa kutoka mahali ambapo alikuwepo basi angetambua kwamba bwana huyo alikuwa amemezwa na taharuki ambayo ilimnyima raha na amani kiasi cha kumpatia mawazo ya namna hiyo.
Sura yake haikuwa ikionekana vizuri huenda kwa sababu ya kiza ambacho kilikuwa kimelimeza lile eneo ukijumlisha na miti ambayo ilizungukia eneo hilo ndiyo kabisa ilizalisha kiza na kulifanya kuwa tulivu isipokuwa hatua za bwana huyo ambazo hazikuwa na umakini kwa sababu ya kukosa utaratibu maalumu kwani alikuwa akiumia. Kwa mwonekano wake wa mbali hakuwa mtu mwepesi, alionekana kuwa shupavu na shababi ambaye mwili wake ulikuwa umeshiba vilivyo kama sio kwa mazoezi makali basi bwana huyo alikuwa amezoea maisha magumu ama yale maisha ambayo hayana utulivu kabisa ndani yake.
Tafsiri ya maisha yake ilikuwa inakuja kwa namna alivyokuwa na hali ambayo alikuwa nayo kwa wakati huo, alikokuwa ametoka kwa nyakati hizo hakukuonekana kuwa na usalama wa kutosha ndiyo maana hali haikuwa inavutia kwa upande wake. Alisikika akiwa anahema kwa nguvu, ile sauti yenye kitetemeshi ndani yake mithili ya mtu ambaye alikuwa anautua mzigo mzito ambao aliubeba kwa muda mrefu kwenye mwili wake na moyo wake kwa ujumla. Mbalamwezi ilichanua nyakati hizo na kusababisha mwanga kwa mbali ambao ulifanya hata lile jasho lake kuchuruzika na kumpa nafasi ya kuona umbali mdogo ambao hata yeye mwenyewe hakuonyesha kama umbali huo ulikuwa unaenda kuwa na msaada kwa upande wake yeye.
Aligeuka nyuma mithili ya mtu ambaye alikuwa anahakiki jambo ama kuna kitu alikisahau huko ambako alitoka, aligundua kwamba hakukuwa na usalama wa kutosha kwani mwili wake haukuwa na utulivu, alikuwa anapata misisimko ambayo ilizidi kumpatia tahadhari juu ya eneo ambalo alikuwepo, mpaka wakati huo alitambua kabisa kwamba lilikuwa ni suala la muda tu kuweza kufikiwa mahali ambapo yeye alikuwepo. Mwili wake ulikuwa kama unashindana na nguvu zake za kutembea kwani alijihisi kama ana kizunguzungu kikali kwa nyakati hizo, kilikuja katikati ya hiyo safari yake na kwenye kumbukumbu za maisha yake hakuwahi kufikiria kama aliwahi kuwa na tatizo la namna hiyo kabla.
Alitikisa kichwa ili aweze kuwa sawa ila alihisi kama anaona nyota mbilimbili mbele yake, alishika kichwa huku akiwa anaguna kwa maumivu ambayo yalitosha kumfanya jicho lake kutoa chozi bila kupenda. Bwana huyo alijigeuza akiwa anazunguka hiyo sehemu na maumivu yake, hapo ndipo mwili wake ulionekana vyema. Upande wa ubavu mmoja ulikuwa na kisu ambacho kiligota hapo, kwenye mgongo wake kulikuwa na nondo fupi ambayo ilisalia kwenye huo mwili wake lakini pia upande wa nyuma wa shingo yake ulikuwa umetobolewa kidogo eneo ambalo lilikuwa linatoa damu taratibu. Mwili wake ulionekana kuchakaa vya kutosha kwa kipigo ukiacha upande wa mbele ambao alionekana aliulinda ipasavyo ndiyo maana ulionekana kuwa ngangali bado.
Bwana huyo ile hali ilionekana kabisa kumuelemea pale alipokuwepo, hakuweza kusimama tena kama mwanzo, aliyumba yumba na kujisogeza mpaka pembezoni eneo ambalo lilikuwa na mti mfupi na mnene. Alidondokea upande wa pili na kuegamia mti huo huku akiwa bado anahangaika na maumivu ya mwili, kichwa ambayo kwa pamoja yalikuwa yanashindana na mawazo yake.
“Zyra” alitamka jina ambalo lilionekana kuwa la kike kwa sauti yenye kitete lakini ambayo ilishiba vya kutosha, alilitamka neno hilo kwa sauti ndogo na nyepesi ila ule uzito wake ndio ambao uliifanya isikike kwa mbali. Haikueleweka sababu ya mtu huyo kuweza kulitaja jina hilo tena akiwa sehemu kama hiyo ambayo ilionekana kutokuwa salama kabisa kwa upande wake. Huenda lilikuwa ni jina ambalo ndiyo ilikuwa sababu ya yeye kuishia sehemu ama eneo hilo ama lilikuwa ni jina ambalo lilikuwa na maana kubwa kwenye maisha yake, kwa nyakati hizo ni yeye pekee ambaye alikuwa ana majibu ya sababu za kulitaja jina hilo eneo kama hiyo na wakati kama huo.
Aliketi kwa kuuegamia huo mti lakini akiwa anahangaika na maumivu makali ambayo yalimvaa huku akijua kabisa maisha yake yalikuwa kwenye hatari kubwa, akili yake ilimrudisha nyuma dakika kadhaa ambazo zilikuwa zimepita. Bwana huyo alikuwa anakimbia kwa spidi ambazo kama mtu ambaye alikuwa anamfukuza asingekuwa na kasi ya kutosha basi abadani asingempata kwenye maisha yake yote. Alionekana kukimbia ili kuiponya nafsi yake ambayo haikuwa na usalama wa kutosha kwa nyakati hizo, alitamani kama angekuwa anafukuzwa na mtu mmoja ama wawili lakini haikuwa hivyo, walikuwa ni wanaume wapatao sita ambao walikuwa wapo nyuma yake kula naye sahani moja.
Ile miondoko yake ambayo ilikuwa inakatisha tamaa kwa wakimbizaji, haikufua dafu kuweza kuwafanya wanaume hao kughairi safari ya kumpata bwana huyo. Akiwa anaendelea kukimbia ni kama mwili wake ulianza kuchoka mpaka akahisi ile hali haikuwa ya kawaida kwake, hakuwa mbovu namna ile kiasi kwamba kwa muda mfupi tu aweze kuwa na ule uchovu. Akiwa anaendelea kujiwazia huku akiwa anaendelea kuikata nyika ndipo alihisi hali isiyo ya kawaida, ni ile hali ya mvumo wa upepo, ni kama ilizidi kwa upande wake, alihisi kuja jambo zito nyuma yake hivyo alijivutia pembeni ambapo kulikuwa na mti. Kujivuta kwake kulimsaidia kuikwepa nondo moja ndefu kiasi na yenye makali ya kutosha ikaenda kukita kwenye mti mdogo ambao ulikuwa mbele yake kiasi kwamba nondo hiyo ilizama na kutokezea upande wa pili.
Kama ingefanikiwa kuingia kwenye mwili wake basi mpaka muda huo asingekuwa hai kwa namna yoyote ile. Alihema na kuendelea na safari yake kwani alikuwa ameshaanza kuvisikia vishindo vizito vikiwa vinakuja karibu na alipo tena wahusika wakionekana kuwa na usongo mkali na huyo bwana kama wangempata. Kila ambavyo alikuwa anajaribu kukimbia ndivyo ambavyo mwili wake ulizidi kuwa wa utofauti mpaka yeye mwenyewe akaanza kujitilia shaka na hizo harakati zake za kujiokoa. Kujiuliza uliza mara mbili mbili wakati ambao alitakiwa kuyapambania maisha yake kwanza likawa kosa lake la maisha ambalo kila dakika ilivyozidi kwenda mbele alianza kulijutia kwa maumivu makali.
Ule wakati ambao aliutumia kuwaza ni wakati ambao alikuwa amefikiwa, alichotwa kwa nguvu kubwa na kwa sababu hakuwa na balansi ya kutosha, bwana yule alibaki anaelea hewani huku akitoa sauti ile ya mshtuko wa kutoamini bado kama jambo hilo lilikuwa linamfika hizo nyakati eneo ambalo yeye mwenyewe alitambua kwamba hakuwa na msaada kutoka kwa mtu yeyote yule zaidi ya mikono yake na mbio zake tu pekee. Alitua kwa sarakasi nne ambazo zilimfanya kuyumba kwani hakutarajia, muda ambao alikuwa anaendelea kujipanga alihisi kama kuna kitu kimezama kwenye mwili wake hapo akaundua kwamba ni nondo fupi ilipita nyuma ya tumbo. Alipiga hesabu za kujivuta mbele zaidi ila huko ndiko kulioonekana kuwa na hatari kubwa zaidi ya nyuma.
Alikutana na mguu ambao ulitua kwenye shingo yake, ule mguu ulikuwa mithili ya mtu ambaye alikuwa anapiga mpira aina ya volley. Damu ilimtoka mdomoni bila kupenda huku akiwa anatokwa na jasho jingi na nondo ikiwa kwenye mwili wake. Alisogea pembeni akiwa anahema kama kuku ambaye aliwekwa kati kwa ajili ya kuliwa na wali, hapo ndipo akawaona hao mabwana ambao walikuwa wanayahitaji maisha yake kwa nyakati hizo. Walikuwa watatu, wawili mbele na mmoja nyuma, moyo wake ulipiga kite baada ya kugundua kwamba aliingizwa kwenye mtego mwingine uliohitaji muda wa kutosha kuweza kuutegua lakini kwa habati mbaya hata huo muda hakuwa nao. Aligundua kwamba wanaume hao walikuwa sita tangu mwanzo, sasa hao watatu walikuwa wapi? Haukuwa muda sahihi kwa yeye kuweza kulijibu hilo swali lake zaidi ya kuweza kuyapigania maisha yake.
“Ulitakiwa kulihama hili taifa wakati ambao ulikuwa na nafasi, unajua kabisa ambacho kimewatokea watangulizi wako ambao wamewahi kuwa kwenye hiyo nafasi yako lakini bado ukaleta jeuri. Maisha hayaendi hivyo ndugu yangu, ona sasa muda huu unaenda kufa tena kama mbwa bila msaada ndani ya kichaka kidogo kama hiki kisicho na sifa hata ya kuitwa msitu” alitamka bwana mmoja ambaye alikuwa amevaa nguo zilizokuwa nzito lakini kwa upande wake hata huo uzito haukuwepo kabisa, alikuwa anaongea na mtu aliyekuwa katikati yao akiwa hana mahali pakwenda. Walionekana kutambuana kwenye maisha mengine ambayo yalipita ila kwa wakati huo ni huyo mwanaume mmoja ambaye alitakiwa kuyapigania maisha yake kutoka kwa hao mabwana.
Hakuwapa nafasi ya kuwajibu maneno yake ya thamani kwani alijua kabisa kwamba hayakuwa na msaada wowote kwa upande wake. Alizikunja ngumi zake kwa ustadi na kuwanyooshea wanaume hao ambao walimfuata kwa pamoja pale kati. Alikimbilia mbele na kuinama akipiga goti ambapo alijilaza kabisa na kughala ghala huku akiwa makini ile nondo isizidi kuingia ndani kiasi kwamba wale mabwana wakapishana naye akaibukia upande wa pili, hakusimama, bali zilikuwa ni mbio ambazo zilitakiwa kumponya. Kwenye kukimbia kwake ndiko ambako kulimponza kwa sababu baada ya sekunde thalathini tu alirudi nyuma kwa hatua kama kumi baada ya kukutanishwa na kitu ambacho yeye alihisi ni kama nyundo nzito imetua kwenye kifua chake.
Ndiyo kwanza kabisa naifunua episode ya kwanza ya simulizi hii bora mno ya JUMBA JEUSI. Ni simulizi ambayo ina mengi ya kutupatia ndani yake, utaisoma siasa kwa undani zaidi na namna inavyofanya kazi hususani kwenye mataifa ya Afrika hivyo nakusihi ungana nami kuanzia mwanzo mpaka siku ambayo nitatua nukta ya mwisho na kusema nimeimaliza rasmi.
Nyuma ya kalamu ni mwandishi wako pendwa wa siku zote, FEBIANI BABUYA wao wanapenda kuniita Bux the storyteller.
Wasalaam.
Comments