Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

 

Ilikuwa ni ngumi iliyoshiba ya mwanaume mmoja ambaye alitokea pembezoni mwa mti mmoja mwembamba lakini kutokana na kwamba alikuwa kwenye mwendo, ndiyo sababu hakufanikiwa kabisa kuweza kumuona bwana huyo. Alikuwa ameinamia ardhini huku akitapika damu kwa uzito wa ile ngumi, hapo alipata majibu kuhusu wale wanaume wengine watatu ambao hakuwaona kwa mara ya kwanza, watu hao walikuwa wamegawana maeneo na nyakati hizo alikuwa amekutana nao wote sita. Nyuma yake walikuwa wamefika wale ambao alikuwa amewakimbia mwanzo na mbele yake walikuwepo wale wengine watatu hivyo hakuwa na sehemu nyingine ya kuweza kukimbilia ama kuyaponya maisha yake. Mwanaume huyo kitu pekee ambacho alikuwa anakitegemea kuweza kumtoa mahali hapo akiwa hai ilikuwa ni miujiza pekee ila kwa nguvu za mwanadamu ilihitaji bahati kubwa mno ambayo ni wanadamu wa kuhesabika huwa wanahatika kuipata kwenye maisha yote ya kuishi.

 

Mwili wake ulikuwa umeanza kulegea kwa kiasi baada ya kupata hayo majeraha yake mwilini na kipigo cha kushtukiza. Alisogea hatua moja mbele ili awe anawaona wote vyema maana kiza kilikuwa kimetanda kwa ukubwa na macho yake yalikuwa yanapoteza nuru ya kuweza kuona mbele vizuri hivyo alihitaji kuweza kujipa msaada mwenyewe kuendana na hali halisi ambayo ilikuwa mbele yake kwa nyakati hizo. Mikono yake ilishiba, haikuwa na udhaifu mkubwa huku kichwa kikiwa na nywele za kutosha ambazo zilisambaratika bila mpangilio lakini kabla ya hapo, zilionekana kutunzwa kwa usahihi na ustadi wa hali ya juu.

 

Aliona vivuli vinamsogelea karibu yake, alihema taratibu huku misuli yake ikiwa inatuna, vivuli vulikuwa viwili, aligeuka kwa kuinama kidogo ambapo alipishana na ngumi moja huku akiusikilizia upepo wake, ngumi nyingine ilikuwa inakuja kwenye usawa wake wa uso ambapo aliinamia pembeni ikamkwaruza kidogo shingoni yeye akaitua yake kwenye uso wa mwanaume huyo ambaye alisikika akipiga yowe. Ilizama kwenye pua na kuipasua hiyo pua kiasi kwamba damu ikasambaa mpaka kwenye nguo zake yeye. Wakati mwanaume yule akiendelea kuishikilia pua yake, alirusha ngumi nyingine ambayo ilitua kwenye kifua na kupelekea bwana yule kuinama kwa maumivu ambayo yalimsababishia kupokea mguu ulioshiba kwenye uso wake.

 

Alidondokea mbali kidogo kutoka lilipokuwa lile eneo huku akiwa anajisikilizia taratibu na kelele kadhaa, mwanaume yule aligeuka lakini aligundua kwamba muda ulienda, alikutanishwa na teke moja la mbavu lakini wakati anaendelea kujishauri kwa maumivu, ngumi moja ilitua kwenye shingo yake upande wa nyuma na hapo aligundua kwamba mhusika ambaye alikuwa ametua mkono huo alikuwa na silaha ndogo mithili ya sindano mkononi kwani ilimpatia tobo. Aliuma meno yake na kuruka sarakasi mbili za mbele, zilimfanya kusimama kando ya mti ambapo alidunda kwenye huo mti na kugeuka akiwa amejilaza kama mtu ambaye alikuwa anahitaji kulala.

Alipo mkaribia mwanaume mmoja alijigeuza na kutua ardhini ambapo alishikilia kwa mkono mmoja kisha akajifyatua, alikuja kutua kwenye shingo ya bwana yule aliyekuwa karibu naye, aligeuka naye kwa miguu yake akiwa anainyonga shingo hiyo tatatibu na kwenda kumkita bwana huyo kwenye mti ambapo baada ya kudondoka alikuwa amevunjika kiuno. Aliruka juu na kutua kwenye shingo ya huyo bwana akaivunja na mtu huyo akapoteza maisha hapo hapo. Muda ambao aliutumia kuinuka ni muda ambao aligundua kwamba alikuwa amezamishiwa kisu kwenye mwili wake, kisu kilicho mpatia maumivu makali.

 

Aligeuka kwa ghadhabu na kumkosa bwana huyo shingo ambapo wakati anafanya hayo yote alijisahau kwamba kwa nyuma yake kulikuwa na watu wengine, aliirusha mfulizo mikono yake mpaka alipofanikiwa kuidaka shingo ya huyo bwana, ile shingo ilivunjwa lakini wakati huo alizamishiwa nondo kubwa kiasi, nondo hiyo ilivutwa kidogo kwa nyuma na mguu mwingine ukafuatia kwenye mguu wake kiasi kwamba uliteguka pale pale. Alisikika akitoa sauti ya maumivu makali lakini wakati huo alikuwa anamrukia yule bwana ambaye alimshambulia na nondo kwenye mwili wake. Akiwa juu ya bwana huyo alipishana na mguu mzito ambao ulimkosa na kuzipuliza nywele zake, aliinuka kwa sarakasi ya mbele ambapo alitua sehemu ambayo ilikuwa na majani mengi makavu akiwa anavuja damu kila sehemu kwenye mwili wake.

 

Wakati anatua alifika hapo na kuyazoa majani hayo kwa nguvu kubwa akayarushia nyuma ambako alijua watu hao wanamjia kwa kasi, ni kweli wale mabwana walikuwa wanamjia alipo na kama bahati kwake yale majani yalikuwa kwenye mavumbi hivyo wakati anayarusha yaliruka na mavumbi na kuwapata wale wanaume kwenye macho yao isipokuwa mmoja ambaye aliinama na kuziba uso wake ili asikumbwe na hiyo dhahama. Watu hao walitulia baada ya sekunde kama kumi na baada ya eneo hilo kutulia, mtu wao hakuwepo, yaani alikuwa amekimbia na haonekani kama aliingia sehemu ipi kwa nyakati hizo. Walionekana kulaani mno jambo lile kuweza kutokea, huyo mtu wao hakutakiwa kuendelea kuwa hai mpaka nyakati kama hizo, alitakiwa kufa kwenye mikono yao kwa namna yoyote ile na ndipo wakaamua kuufuata ule uelekeo ambao walikuwa na uhakika kwamba alikuwa ameelekea huko baada ya pale kwani waliamini hawezi kufika mbali kwa sababu alijeruhiwa, ilikuwa ni lazima wampate tu.

 

Ile ndiyo ilikuwa hali iliyomfanya bwana yule aweze kuwakimbia watu wale na kuishia kuwa kwenye hali kama ile kwa nyakati ambazo alikuwa anayapigania maisha yake lakini jambo hilo lilionekana kuwa gumu zaidi kwake baada ya hali kubadilika kabisa na kuishia kwenye ule mti hali yake ikiwa imebadilika ghafla kiasi kwamba akaishia kulitamka jina ambalo ni yeye pekee ndiye alijua kwamba lilikuwa jina la nani. Alikuwa amefikia hatua amekata tamaa kabisa, alikuwa tayari kuwasubiri watu hao kuja lile eneo na kuyabeba maisha yake kwani hakuwa na jambo la ziada ambalo angeweza kulifanya kwa nyakati zile likamsaidia. Bwana huyo akiwa anahangaika na maumivu makali nyakati kama hizo huku macho yake yakiwa yamepoteza uwezo wa kuona vizuri fahamu zilianza kumtoka taratibu akiwa amekata tamaa hatimaye alijilaza mahali hapo hapo akiamini safari yake ilifika mwisho.

 

Wakati anakata hiyo tamaa yake, kuna mwanamke mmoja ambaye alifika eneo hilo akiwa ameufunika uso wake, alionekana kabisa kwamba hakuhitaji kutambulika na mtu yeyote yule ambaye alikuwepo kwenye hilo eneo. Alimbeba bwana huyo na kwenda kumzamisha kwenye kichaka kimoja kisha yeye akapanda juu ya mti kwa kasi ya ajabu na kujibanza kwenye matawi baada ya kusikia hatua za watu zikiwa zinakuja eneo hilo. Akiwa pale aliwaona wanaume wanne ambao waliishia ile sehemu ambapo alikuwa amepotezea fahamu yule bwana, walionekana kuongea jambo fulani huku wakiwa wanasonya kwa hasira na baada ya dakika kama moja baada ya kukubaliana jambo walionekana kuanza kuondoka ile sehemu mpaka walipo ishia.

Mwanamke yule baada ya kuhakikisha wale mabwana wameweza kupotea kutoka kwenye ile sehemu, alishuka taratibu na kusogea mpaka pale ambapo alimhifadhi yule mwanauma, alimbeba na kutokomea naye kuingia sehemu ya ndani zaidi ambako kulianza kuonekana kama kuwa na msitu mzito kiasi.

 

 

 

KIJIJI CHA BANZOKA

Ni kijiji cha zamani mno ambacho kilikuwa kimepotea kwenye masikio ya wengi ama kwenye dunia ya watu wengi. Kijiji hicho kilikuwa umbali kadhaa kutoka eneo ambalo lilikuwa linafikika na wengi, huenda ndiyo sababu ambayo ilikifanya kuweza kuukosa umaarufu kwa watu wengi na kuwafanya waweze kukifahamu ama kukisikia kama ambavyo ilikuwa inasikika miji mingine na vijiji vingine maarufu ambavyo vilikuwa vinatoa watu mashuhuri. 

 

Ni kijiji kilichokuwa na idadi ya watu wa kuhesabu tu, hawakuwa wengi kabisa ndani ya eneo hilo na watu ambao walikuwa wakipatikana huko hawakuwa wakiyaishi yale maisha ya kawaida. Kilikuwa kinapatikana ndani ya msitu mmoja wa zamani ambao ulitengwa, ulitengwa kwa sababu ya mambo ambayo yalikuwa yanasimuliwa kutokea ndani ya eneo hilo. Lilikuwa ni eneo ambalo lilidaiwa kuwa na maajabu tangu enzi, eneo ambalo lilikuwa na watu wa kale wakiishi kama mizimu, ilidaiwa kwamba hakuna binadamu alikuwa anaruhusiwa kuweza kuingia huko na kama angeingia basi hakuna mtu ambaye aliwahi kurudi hata mmoja hivyo lazima angekufa. Jambo hilo ndilo lilifanya watu waanze kuogopa kwa ukubwa kuwepo kwenye hivyo viwanja huku kukiwa hakuna mtu hata mmoja ambaye alikuwa ana ushahidi juu ya jambo hilo.

 

Ndani ya kijiji hicho ndipo alipokuwepo yule mwanaume ambaye mara ya mwisho alipoteza fahamu baada ya kupokea kipigo kutoka kwa wanaume sita ambao walikuwa wamemvamia, hakikuwa kipigo ambacho kilimpotezea fahamu, ilionekana kwamba kuna kitu cha ziada ambacho kiliunyong’onyesha mwili wake na kuufanya kukosa kabisa nguvu kiasi kwamba akaishia kwenye ile hali yake mbaya. Bwana huyo akiwa amekata tamaa ya maisha kabisa na hajui ni jambo gani liliendelea kwa wakati ule ndipo alipo tokea mwanamke mmoja ambaye alijifunika huku kwenye mwili wake akiwa na nguo za asili mithili ya mtu ambaye aliishi mwituni kwa muda mrefu, alimbeba na kupotea naye kuelekea sehemu ambayo haikuwa inajulikana.

 

Episode ya pili inaishia hapa, ni muda wa kwenda kujua yaliyomo ndani ya hilo eneo lisilo julikana.

 

FEBIANI BABUYA.

Previoua Next