Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

Mwanamke yule ambaye alimbeba yule bwana, alielekea naye kwenye kile kijiji ambacho kilikuwa kilomita moja tu kutoka lile eneo ambalo alimpatia. Wanaume wale ambao walikuwa wakimfukuza mpaka eneo hilo, hawakuweza kuendelea mbele kwa sababu walikuwa wanazijua sifa za eneo hilo, ni eneo ambalo hakuna mtu aliwahi kuingia akatoka akiwa hai hivyo wakaiona kama sehemu tukufu kwa ajili ya mizimu ya zamani kuweza kuishi lakini eneo hilo lilikuwa ni makazi ya watu kadhaa ambao walijichimbia kwenye hiyo misitu ambayo mwanzoni ilizungukwa na nyika kadhaa na vichaka vya kutosha.

 

Mwanaume huyo ambaye aliokotwa kule nyikani, alikuwa amelazwa kwenye kitanda cha ngozi ambacho kilionekana kuwa cha zamani sana. Kitanda hicho kilikuwa kimefungwa kwa kamba ngumu na kukifanya kiwe kinaelea taratibu. Ulikuwa ni mwezi mmoja umepita tangu yule bwana apate lile tatizo, mwezi mzima alikuwa ametibiwa pale na hakuwa amerudi kwenye fahamu zake za kawaida, ilionekana kwamba kitu alichokuwa amewekewa kwenye mwili wake kilikuwa na sumu mbaya ambayo ilimletea hali tofauti na ile ambayo mwili wake uliizoea tangu mwanzo. Bwana huyo alianza kuweweseka akiwa kwenye usingizi, kuweweseka kwake kulimfanya kuanza kutamka mambo mazito ambayo yalianza kuwatisha hata wale ambao walikuwa wanamtibia hilo eneo.

 

“Historia ya maisha yangu sio nzuri, sio nzuri kwa sababu mimi ni mtu wa tofauti, utofauti wangu unakuja kwa sababu ya kazi yangu ambayo nilikuwa naifanya, kazi ambayo nilizaliwa nikihisi nilitumwa kuja kuifanya kama sio kupewa kibali kuweza kuifanya tena kwa usahihi. Nilikuwa na kazi ambayo ni wanadamu wa kuhesabu tu duniani hapa huwa wanabahatika kuwa nayo hivyo nami nilikuwa miongoni mwa hao watu wa kuhesabu” mwanaume huyo alitulia kuweweseka, alitulia kwa sekunde kadhaa kisha akaendelea tena kuongea, alikuwa anaongea mithili ya mtu ambaye yupo ndotoni lakini alikuwa analiwasilisha jambo hilo mithili ya mtu ambaye alikuwa anamsimulia mtu amjuaye na simulizi nzima ya maisha yake.

 

“Jina langu maarufu wananiita Bazoka, King Bazoka. Hilo ni jina ambalo nilipewa na watu lakini kiuhalisia ni kwamba sijui hata maana yake ya asili ni ipi, sina nilijualo kuhusu hili jina ila niliamua kulivaa kwa sababu sikuona ubaya wake wowote. Mimi nilikuwa mlinzi wa raisi, ndiyo mimi ndiye nilikuwa nahakikisha usalama wa mheshimiwa raisi unakuwa sawa kwa masaa ishirini na manne ya siku mpaka pale ambapo nahisi nilishindwa kuweza kutimiza hilo jukumu langu, nahisi nilishindwa kwa sababu ni wajibu wangu, jambo lolote ambalo linatokea kwa raisi basi mtu namba moja kuweza kuwajibika ni mimi hapa.

 

Nilifanya kosa kubwa la maisha, kosa ambalo sina imani kama nitaweza kujisamehe mwenyewe hata huko akhera kwa sababu nilileta majonzi kwa mamiliona ya wananchi. Mimi ndiye nilileta matatizo yote ya taifa hili, mimi ndiye sababu ya kufanya kuwepo kwa hali ya fujo na watu kupoteza imani kabisa na uongozi wa taifa hili. Linaweza lisiwe kosa langu moja kwa moja lakini mimi ndiye ambaye nilitakiwa kulizuia jambo hilo lisiweze kutokea lakini nilishindwa kufanya hivyo, kushindwa kwangu kufanya hivyo ndio ukawa mwanzo wa taifa hili kuweza kupoteza mwelekeo jumla, mwelekeo ambao inaweza ikatumika mikaa miamoja kuweza kuurejesha kutokana na hali ambayo ipo mpaka sasa.

 

Najua kwamba kuna watu watanicheka na kuna wengine wananishangaa vile vile, mlinzi wa raisi wa nchi nafikiaje mpaka kuwa hatua kama hii ambayo nipo nayo leo? Kiukweli hata mimi siwashangai hao watu kwa sababu hata ningekuwa mimi kwenye nafasi zao pia ningeshangaa, lakini jambo hilo haliwezi kuondoa ukweli kwamba mimi nilikuwa mlinzi wa raisi kwa miaka isiyo pungua minne. Miaka yangu bora ambayo niliitoa kwa ajili ya kumpambania yule mwanamapinduzi imekuja kuishia sehemu mbaya na kuacha historia mbaya zaidi kwenye maisha yangu na siku zangu ambazo nimepata kuishi juu ya uso wa dunia hii isiyo na shukrani.

 

Dunia imepata kushudia mengi miaka na miaka lakini jambo ambalo huwa linasisitizwa mno na watu wenye maarifa makubwa ni kwamba duniani watu ambao huwa wanachukiwa kupita kiasi ni wawili tu! Mtu wa kwanza ni ambaye ni mzuri zaidi kwenye anacho kifanya. Kwenye hili kundi la kwanza ni la wale watu ambao mara nyingi huwa wanafanikiwa zaidi kuliko watu ama makundi mengine, hawa ni watu ambao wanajua zaidi kwenye mambo ambayo wanayafanya hivyo hupelekea kufanikiwa kupita kile kiwango ambacho wanadamu wamewapangia na hilo kwao ni tatizo kubwa. Kundi la pili ni la wale watu ambao wanausema ukweli ama kusimama kwenye ukweli hata kama ukweli unaumiza, sasa mimi nimehukumiwa na ulimwengu kwa hizo sababu mbili.

 

Naweza kusema nilikuwa makini na bora kwenye kazi yangu, niliifanya kazi yangu kwa ufanisi mkubwa huenda kuliko mtu yeyote ambaye amepata kupita kwenye ile nafasi, niliifanya kazi kwa weledi na moyo wote lakini kwa bahati mbaya jambo la kutisha kwenye historia ya taifa hili lilitokea kwenye kipindi changu hivyo likapelekea kuniharibia sifa yangu na kunifanya mimi kuonekana kama mtu ambaye ndiye nilishindwa kutekeleza majukumu yangu. Mwanaume ambaye alikuwa kama mfano wa maisha kwangu kwa namna alivyokuwa anaufanya kwa usahihi uongozi wake mimi nahisi nilimuangusha lakini yote yametokea kwa sababu yake yeye.

 

Alipenda mno haki, alikuwa na mipango ya muda mrefu kuhusu taifa hili, aliamua kuyatoa hata maisha yake sadaka kwa ajili ya kuwapigania watu. Hata pale ambapo aligundua kwamba maisha yake yasingekuwa marefu bado aliendelea kuipiga kazi yake kwa usahihi kwa sababu aliamini kwamba kama asipotokea mtu wa kujitoa mhanga basi hakuna namna taifa linaweza kufika mbali wala kusogea mahali popote pale. Kiongozi huyo alikuwa ni muumini mkubwa wa falsafa za miongoni mwa waanzilishi wa falsafa duniani, Socrates. Bwana huyo ambaye alipata kuishi maelfu ya miaka iliyopita huko nyuma aliamini kwamba wanadamu wanatakiwa kuwa na uwezo wa kuhoji na kuuliza kila jambo ambalo lilikuwa linaendelea ama kufanyika. Watu walitakiwa kujua wanatoka wapi, wanaenda wapi na kwanini mambo yanafanyika? Hawakuwa mazombi wa kupelekeshwa hovyo kama watu wasiokuwa na mwelekeo wowote ule hivyo akaamua kuwa mfano.

 

Kwenye kuhoji kwake kulileta matatizo kwa sababu kuna watu ambao walikuwa nyuma ya hiyo mipango, hawakutaka kabisa mambo hayo yaweze kujulikana kwani watu wakiwa na maarifa mengi ni ngumu kuwaongoza ila ukiwa na wajinga wengi ni rahisi zaidi kuweza kuwaongoza. Sasa kuanza kuhoji hoji kungekuja kuwaharibia hapo baadae kwani watu wangejitoa kwenye utumwa wa fikra hivyo mwaafalsafa huyo kwao akawa kama adui mkubwa ambaye alikuwa anakuja kuwaharibia biashara yao wakaamua kumuua. Mwanafalsafa huyo hakuogopa kufa kwa sababu aliamini hata kama akifa basi ipo siku moja kuna watu watakuja kuguswa na hadithi ya maisha yake, wale watu watatamani kujua alikuwa anafanya nini hasa na kwanini alikuja kupotezwa baadae? Maana yake wangekuja kutambua kwamba alikufa kwa sababu ya kusambaza maarifa kwa watu na maarifa hayo lazima yangekuwa nuru kwa wengi ndiyo maana wakahitaji kuweza kumpoteza ili yasiwafikie. Kuanzia hapo aliamini kwamba hata kama yeye atakufa basi lazima watakuja kutokea wana mapinduzi wengine kabisa ambao wataanzia alipo ishia yeye na kuendelea mbele jambo ambalo hakuwa na uhakika kama lingetokea karibuni ila alikuwa ana uhakika kwamba ipo siku lingekuja kutokea kwa namna yoyote ile.

 

Hilo ndilo ambalo lilimpatia yeye imani ya kuweza kuendelea kupambana na kusimamia kile alicho kiona kwamba ni sahihi na kina manufaa kwa taifa. Kuna jambo moja kubwa ambalo wananchi wengi hawalijui na hawatalijua abadani, nazungumzia namna nchi inavyo endeshwa, siasa ilivyo kwa watu. Kwenye mitandao ya kijamii ni tofauti na siasa halisi ilivyo. Siasa yenyewe inatisha, ni maisha ambayo unayatamani ukiwa nje ila ukiingia ndani yake yanatisha, wanaweza kuyaishi watu wachache ndiyo maana wengi huwa wanakuwa watumwa, wengine wanakufa mapema na wale ambao wanaamua kuukana ubinadamu na kuwa watu wabaya ndiyo wana nafasi kubwa zaidi ya kuweza kuishi kwa muda mrefu kwenye siasa za namna yoyote ile. Hawa hawawazi kuyebeba maisha ya watu ili kutimiza malengo yao, hawa huwa wanawapa maneno matamu raia kwa sababu wanaambiwa yale ambayo wao wanataka kuyasikia na sio uhalisia ambao upo.

 

Sasa yule raisi hakuwa hivyo, hakuwa mtu mnafiki kukupa taarifa ya uongo eti kwa sababu tu wewe umetaka kuisikia hapana, alikuwa mtu muwazi ambaye aliamini zaidi kwenye ukweli na uhalisia. Aliamini hakuna jambo lililokuwa linakuja kirahisi kwenye haya maisha. Alielewa kwamba ni lazima kuna watu wafe, ni lazima kuna watu hususani matajiri waweze kulia, alielewa kwamba kuna watu wanatakiwa kuumia haswa ili taifa lifike kule ambako linahitaji kuwepo. Huwezi kufanikiwa kwa raha, ni lazima uvuje jasho kwanza ndipo ufike kule ambako wewe unakuhitaji na maisha siku zote yapo hivyo ila watu huwa hawataki kwa sababu hiyo njia ni ngumu.

 

Hivyo ile miaka ambayo nilikaa naye karibu, nilijifunza mengi kupitia yeye. Haina maana kwamba kila wakati alikuwa sahihi, hapana bali alikuwa ni muwazi, mkweli na mtu ambaye alipenda kulipigania taifa lake hata pale ambapo angehisi kwamba watu wengi hawapo upande wake. Ni kweli aliua watu wa kutosha, aliwapoteza baadhi ya watu kwenye utawala wake lakini wale watu wengine hawakuwa na hatia ila walikuwa ni hatari kwa mapinduzi ya taifa. Watu wengi ambao aliwapoteza ni wale ambao walikuja kuanza kuharibu ile mipango ambayo alikuwa nayo ya muda mrefu, mipango ambayo ilikuwa inalipeleka taifa kwenye anga za ulimwengu wa mapinduzi ya nne ya viwanja. Kiukweli hao aliwaua tena kikatili, hao aliwaona kuwa maadui wa taifa kwani aliamini hata viongozi shupavu wa zamani ambao walipata kuishi, kuna muda walilazimika kuwaua hata watu wao wa karibu kama ikiwalazimu ili kuhakikisha hawapati vikwazo kuelekea kwenye nchi ya ahadi.

 

Huyu bwana anajaribu kutaka kutupa taarifa gani? Episode ya tatu nabwaga kalamu hapa, panapo majaaliwa tukutane tena wakati ujao.

 

FEBIANI BABUYA.

Previoua Next