Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

Sasa kwenye zile harakati zake aliingia sehemu moja ambayo naweza kusema kwamba ni mbaya, huenda raisi wa kila taifa ana mamlaka makubwa kwenye taifa lake hapa duniani lakini ukweli ni kwamba ile ni dhamani tu ya uongozi na mamlaka ya kuamuru ila nguvu ya kweli ipo kwenye pesa. Aliwagusa wenye pesa kwa sababu walikuwa wanawanyonya watu maskini, watu wale walikuwa hawalipi kodi lakini hawakuwa wakiheshimu sheria na mamlaka kwa ujumla kwa sababu walijua kwamba wangeweza kumnunua yeyote, walikuwa wana uwezo wa kumpata wamtakaye kwa muda ambao wangeutaka wao lakini kuingia kwake kulibadilisha yote hayo.

 

Wale mabwana walihenya na kuteseka, jina lile liliogopeka kuliko hata ukoma, watu walikuwa wakilisikia jina lake wanatamani hata kuvunja kuta za nyuma wasikutane naye ana kwa ana. Alikuwa na lengo jema na taifa lakini nyakati hazikuwa bora kwake, nyakati zilimkana kabisa na kumkataa na alipofikisha miaka minne na nusu kwenye uongozi wake ndio ukawa mwanzo wa hadithi mbaya ambayo haikuwa na ndoto bali ilikuwa ni hadithi ya maisha ya kweli. Mimi kama mlinzi wake ndiye ambaye nilishindwa kabisa kuinusa ile hatari japo kwa mambo yalivyokuwa nilielewa kwamba kuna siku inaweza kuja jambo lile likatokea ila sikutegemea kama ingekuwa kwa namna kama ile.

 

Lile jambo liliwahi kipindi tukiwa hatujajiandaa bado japo ni mara kadhaa niliwahi kumsikia akidai kwamba hana imani kabisa hata na watu wake wa karibu, alinusa usaliti lakini angefanya nini? Aliwabadilisha watu wengi mpaka baadhi ya ndugu zake lakini bado alihisi kuna hatari na watu wananunulika kwa pesa. Yeye ndiye alikuwa kiongozi wa juu zaidi kwenye taifa, hakuwa na mahali pa kwenda kulalamika kuhusu jambo lile zaidi ya kupambana na hali ambayo ilikuwepo ya kufa na jambo lile moyoni huku akijaribu kuwa makini na hatua zake lakini nadhani ni wakati ulifika kwamba asingeweza kuishi tena, hakukuwa na namna ya yeye kuwa salama kwa ajili ya kulijenga taifa, nyakati za giza zilikuwa zinatanda kwa mfululizo wa wingu zito ambalo halikuwa likionekana kwa uso wa kawaida. Kwa wale ambao tulimfahamu kiundani tuliona mapema hatari ya taifa kwenda kumpoteza shujaa ambaye aliletwa kwa ajili ya ukombozi lakini kwa watu wengine ambao walikuwa nje na mbali ya pale, hawakuwa na wazo lolote kuhusu kesho ya taifa lao, walikuwa wakishangilia kwenye kumbi za starehe wasijue ni wapi taifa lilikuwa linaenda.

 

Raisi wangu alikufa, alikufa nikiwa pembezoni mwa kitanda ambacho sikuwahi kufikiria kwamba kingeibeba maiti yake namna ile. Raisi alikufa nikiwa namuona, lakini raisi hakufa kwa sababu ya kuumwa. Ingekuwa kweli mimi ningejua, mimi nilikuwa mtu wake wa karibu huenda kuliko watu wengi kwa sababu kila wakati ilinilazimu kuwa naye, ilikuwa ni kwa ajili ya majukumu ya kazi lakini mimi naweza kuwa miongoni mwa watu wa kuhesabu ambao yeye alikuwa anawaamini kwa maisha yake yote. Kwa maana hiyo naweza kusema kwamba raisi aliuawa” mwanaume yule alitamka kwa sauti kubwa neno hilo tena kwa hisia kiasi kwamba wale ambao walikuwa karibu yake walirudi nyuma kidogo lakini wakati anatamka yale maneno ya mwisho, alishtuka na kuyafumbua macho yake.

 

 

 

TUNDUMA.

TAZARA.

Kwenye reli ambayo inayaunganisha mataifa mawili ya Tanzania na Zambia, karibu kabisa na eneo hilo alionekana mwanaume mmoja akiwa anaikata mitaa kuelekea kwenye hiyo reli. Alikuwa maeneo ya majengo nyakati ambazo kwa saa za Tanzania zilikuwa zinasoma kama saa nane na dakika zake usiku. Bwana huyo alionekana kuwa mzoefu wa mitaa hiyo kwani hakuwa na wasiwasi kabisa, sio kama hakuwa na taarifa juu ya mambo ambayo yalikuwa yanaendelea kwenye mji huo mdogo ambao unakua kwa kasi kubwa mno kwenye suala zima la biashara, lahasha! Bali alikuwa anajua jambo ambalo analifanya hata imani juu ya nafsi yake mwenyewe ilikuwa ni kubwa.

 

Alitembea kwa muda wa dakika kadhaa za kuhesabu huku akiwa anaikata mitaa kwa hatua zake kubwa ambazo zilikuwa na ukakamavu wa kutosha ndani yake. Alionekana kuwa na uhakika wa sehemu ambayo alikuwa anaelekea ndiyo maana hakusita hata eneo moja. Baada ya kufika ilipo reli hiyo, alitazama kila upande kisha akaanza kujongea taratibu kuelekea eneo ambalo lilikuwa na behewa kadhaa za treni ambazo hazikuonekana kuwa pale kwa makusudi bali zilikuwa ni mbovu ama zilikuwa kwenye matengenezo. Aliingia ndani bila hata kujiuliza mara mbili, alilivuka lile behawa la kwanza na kuingia la pili lake ambalo kwenye siti moja alimuona mwanaume mmoja ambaye alikuwa amempa mgongo huku kwenye mwili wake akiwa na koti zito ambalo hakuelewa kama bwana huyo alilivaa kwa sababu ya baridi kali ambalo linapatikana ndani ya mkoa huo wa Songwe ama kulikuwa na sababu zingine nyuma yake ambazo yeye binafsi hakuwa na uelewa nazo. Alihema mara moja na kuanza kuzitupa hatua zake kwenda kwa yule bwana ambaye bila shaka alionekana kwamba alikuwa pale kwa ajili ya kumsubiri yeye tu na si vinginevyo.

 

“Umechelewa sana na unajua kabisa kwamba huwa sipendi kumsubiri mtu mmoja kwa muda mrefu. Kuna sababu zipi unapuuzia amri yangu nikikuita mahali namna hii?” aliongea kwa sauti nzito bwana yule ambaye ni wazi alikerwa na mwanaume yule kuweza kuchelewa kufika eneo lile.

 

“Nilikuwa nahakikisha usalama na kuwa na uhakika kwamba hakuna mtu hata mmoja anajua kwamba mimi nipo au nataka kufanya jambo gani”

“Mhhhh! Naanza kuwa na mashaka na uwezo wako kwa sasa, unatakiwa upunguze kufanya mapenzi yanakupelekea pabaya. Wewe ni mwenyeji wa hili eneo, huwezi kunipa sababu ya kitoto namna hiyo kwa kuamini kwamba nitakuelewa kwa sababu unaijua kila kona na kila mtaa wa mji huu”

 

“Nisamehe kiongozi, hili halitajirudia kwa mara nyingine tena”

“Ni bora iwe hivyo kwa sababu utanilazimisha nije kukuua mwenyewe kwa mkono wangu jambo ambalo sitaki kulifanya”

“Nimekuelewa mkuu”

 

“Mtu wako atakuwa hapa ndani ya nusu saa ijayo, atakuwa Mwaka pale akisubiri saa tisa kamili usiku aweze kuvuka kwenda Zambia na baada ya hapo asubuhi asafiri kwenda Afrika ya kusini”

“Natakiwa kumuua au kuondoka naye akiwa hai?”

“Tangu lini umeanza kuondoka na watu ambao wapo hai?”

“Namanaanisha kwamba kuna taarifa ambayo natakiwa kuondoka nayo kutoka kwake?”

 

“Sio taarifa bali kuna begi dogo ambalo analo kwenye mkono wake ndilo ambalo linahitajika. Hilo begi ukilipata hautakiwi hata kulifungua kwa namna yoyote, lifike kwangu likiwa vile vile na baada ya hapo nadhani unajua ni kitu gani unatakiwa kukifanya”

“Ndiyo mkuu”

“Natarajia kwamba hilo begi litafika Dar es salaam kesho mapema juu ya meza yangu ofisini”

“Nimekuelewa bosi, na vipi kuhusu Bazoka?”

 

“Kuna watu wameenda kumalizana naye muda sio mrefu hivyo muda wowote kuanzia sasa nasubiri simu kutoka huko ili nijue kazi yote imeenda sawa kwa pamoja”

“Una imani kwamba watu ambao umewapa kazi wanaweza kumuua yule mtu?”

“Umekuwa na wasiwasi na ufanyaji wangu wa maamuzi?”

“Hapana ila najaribu kuangalia aina ya mtu ambaye wanamtafuta”

 

“Go and do your fucking j….” mwanaume huyo mtu mzima aliongea sentensi nusu kwa kufoka akiwa anajiandaa kutoka eneo hilo baada ya simu yake mfukoni kumshtua kwa mtetemo mkali ambao huenda ulisikika vyema kwa sababu ulikuwa ni usiku mzito na maeneo hayo yalikuwa na utulivu mkubwa.

“Nipe ripoti”

“Whaaaat?” alionekana kuongea yeye tu kwa sababu mtu wa upande wa pili hakuwa anasikika. Hakujibu kitu tena, aliyainua macho na kumwangalia bwana yule kwa umakini mkubwa usoni kwake akionekana kabisa kwamba hakuwa sawa.

 

“Maliza kazi yako sasa hivi na asubuhi ya mapema kabisa uwe Songwe pale uwanja wa ndege kwa sababu kuna dharura, unatakiwa kuwepo Dar haraka iwezekanavyo”

“Sawa bosi” aliondoka eneo hilo akiwa kama hayupo sawa, baada ya kutoka pale, alitembea hatua kama kumi na tano wakajitokeza wanaume wanne ambao waliungana naye mpaka kwenye gari ambayo ilikuwa imepakiwa mahali ambapo hakuna mtu angeweza kufikiria kwamba ilikuwa kwa ajili ya bwana huyo. Alipanda kwenye gari na kutulia kwa muda huku akiwataka wale vijana wake wakae nje kwanza kwani alikuwa anahitaji kufikiria jambo kwa muda tena akiwa mwenyewe tu.

 

Episode ya nne ya JUMBE JEUSI natundika daruka hapa, tukutane ndani ya episode inayo fuatia.

 

FEBIANI BABUYA.

Previoua Next